Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Wakuu wa Vyuo Vikuu, Vituo vya Utafiti, Vituo vya Vijiji vya Sayansi Chapa
11/11/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatano) ameonana na wakuu wa vyuo vikuu, vituo na taasisi za elimu ya juu, vijiji vya sayansi na teknolojia na vituo vingine vya utafiti nchini Iran na huku akibainisha historia ndefu, turathi na uzeofu mkubwa wa kielimu wa Iran katika kipindi cha kabla na baada ya Uislamu na nafasi na mchango wa vyuo vikuu katika historia ya zama hizi hususan katika mwamko wa Kiislamu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, ametilia mkazo ulazima wa kuweko mipangilio mizuri katika vyuo vikuu na vituo vya elimu nchini kwa ajili ya kustafidi kwa njia bora na turathi na uzoefu huo mkubwa wa kielimu, kwa shabaha ya kutoa mchango bora na unaotakiwa katika juhudi za kuleta ustaarabu mpya wa Kiislamu.
Vile vile amelitaja suala la kufanyia utafiti na tathmini sahihi mambo ya kielimu yanayohitajika hivi sasa na katika siku za usoni nchini Iran, kuzuia kupungua kasi ya maendeleo ya kielimu, kutekeleza kwa njia bora na kwa kina ramani kuu ya kielimu nchini, kulipa uzito suala la ubora katika elimu ya juu, kulifuatilia kwa uzito wa hali ya juu suala la ushirikiano baina ya vyuo vikuu na viwanda, nafasi ya vyuo vikuu katika uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete, kupanua anga ya utamaduni wa kiimani na Kiislamu, kustawisha na kulifanya kuwa na kina kikubwa suala la kuwa na busuri na muono wa mbali wa kidini na kisiasa na kutoa fursa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na wahadhiri wao wanaojali thamani za taifa, wanamapinduzi na wenye misimamo thabiti ya kidini; kuwa ni katika mambo ya lazima ya kuviwezesha vyuo vikuu nchini Iran kutoa mchango unaotakiwa katika juhudi za kuunda ustaarabu mpya wa Kiislamu.
Katika mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amevitaja vikao vyake na watu wa vyuo vikuu kuwa ni moja ya vikao bora na vinavyompa raha kubwa na huku akiashiria nafasi ya elimu ikiwa ni wenzo wa kuwa na nguvu na kupiga hatua za kimaendeleo taifa, amesema: Chuo Kikuu ni kituo muhimu sana cha kulea viongozi wa baadaye wa nchi kiasi kwamba kazi sahihi au zisizo sahihi cha vyuo vikuu kwenye suala hilo, zinauathiri moja kwa moja mustakbali wa nchi.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia historia ndefu ya malezi na mafundisho ya watu wakubwa na watu wenye vipaji vya kielimu nchini Iran kama vile Ibnu Sina, Farabi, Zakariya Razi, Kharazmi na magwiji wengine wakubwa wa kielimu wa Kiirani katika nyuga tofauti na kusema kuwa: Katika kipindi chote cha historia, Iran ilikuwa ni jabali la kuzalisha fikra na elimu na hali hiyo iliendelea hadi kabla ya kipindi cha utawala wa wafalme wa Qajar na Pahlavi nchini Iran.
Ameongeza kuwa: Inasikitisha kuona kuwa, katika kipindi cha wafalme wa Qajar na Pahlavi, harakati ya kielimu nchini Iran ilisimama kwa sababu maalumu na kwa bahati mbaya, katika kipindi cha ustawi wa kielimu barani Ulaya, sisi hatukuweza kutumia vizuri vipaji vyetu katika masuala kielimu na maadili ya kielimu, na ndio maana tulibakia nyuma katika harakati ya kielimu duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia mipango ya Wamagharibi kwa ajili ya nchi zinazodaiwa ni za ulimwengu wa tatu ambapo nchi hizo za Magharibi zinataka kuhakikisha kuwa malezi ya wasomi na wataalamu wa nchi hizo unakwenda kwa mujibu wa fikra na mtindo wa kimaisha wa Wamagharibi kupitia vyuo vikuu na kuongeza kuwa: Hata hivyo Wamagharibi wamekwama na wamekumbwa na matatizo makubwa katika njama zao za kufanikisha malengo yao hayo nchini Iran kutokana na utambulisho wa Wairani na vile vile kuwa na nguvu sana fikra za Kiislamu na kidini kati ya wanachuo na watu wa vyuo vikuu nchini, na baada ya mwamko wa Kiislamu wa mwaka 1341 (Hijria Shamsia sawa na mwaka 1962 Milaadia), kulianza harakati adhimu ya elimu ya dini katika vyuo vikuu vya Iran iliyostawi na kupata nguvu kadiri siku zilivyosonga mbele.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambao ulikuwa mithili ya zilizala katika ulimwengu wa Magharibi na Mashariki wakati huo, umetoa athari kubwa katika vyuo vikuu kiasi kwamba wafuasi waaminifu zaidi na waliojitolea muhanga zaidi katika kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu wametoka katika vyuo vikuu.
Vile vile amegusia hali ya vyuo vikuu vya Iran katika kipindi cha miaka 37 iliyopita pamoja na kuweko panda shuka na mitazamo tofauti ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na vile vile kuweko mirengo tofauti ya kifikra kwenye vyuo vikuu na kusisitiza kuwa: Suala muhimu zaidi hapa ni kwamba, vipi vyuo vikuu vitaweza kustafidi na turathi hii ya kihistoria na kielimu na uzoefu huu wenye thamani kubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika kuunda ustaarabu mpya wa Kiislamu ambao ndiyo hiyo jamii bora na kamilifu inayokusudiwa kuundwa na dini tukufu ya Kiislamu?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka maafisa wa elimu ya juu na wakuu wa vyuo vikuu na vituo vya kielimu nchini kulitafakari na kulifikiria kwa kina suala hilo na kuongeza kuwa: Inabidi mipangilio yote na njia zote za harakati ya vyuo vikuu zielekee upande wa kutoa mchango vyuo hivyo katika juhudi za kuunda ustaarabu mpya wa Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, jambo la lazima katika harakati hiyo ni viongozi na maafisa wa Wizara ya Sayansi na Tiba kuwa na taarifa za kina na za wakati unaofaa kuhusiana na hali halisi ilivyo kwenye vyuo vikuu na kusisitiza kuwa: Si sahihi kutosheka tu na ripoti zinazotolewa, bali inabidi mambo yanayoandikwa kwenye ripoti hizo yachunguzwe kivitendo kwenye medani ili kupata uhakika ni kwa kiwango gani malengo yaliyokusudiwa yameweza kufanikishwa.
Pia amesema, ni jambo muhimu kuwa na nguvu kazi inayofaa na iliyojizatiti inavyotakiwa kwa ajili ya kuendeshea harakati ya kielimu na kusisitiza kuwa: Jambo lililo muhimu zaidi ya kuwa na nguvu kazi iliyojizatiti vyema ni muelekeo mzuri wa kielimu kwani kama muelekeo wa kielimu hautakuwa sahihi na hautazingatia maadili na umaanawi, basi madhara ya kukosa muelekeo huo sahihi yatakuwa makubwa sana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja masuala mawili ya "ukoloni" na "bomu la atomiki" kuwa ni mifano miwili katika historia ya mwanadamu inayoonesha madhara ya kutumbukia elimu katika njia ghalati na isiyo sahihi na kuongeza kuwa: Inabidi kuwa macho na kuhakikisha kuwa wakati wote elimu inakwenda sambamba na maadili mema na umaanawi.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kufanyia utafiti na tathmini ya kina mahitaji ya kielimu kwa ajili ya kipindi cha hivi sasa na kipindi cha siku za usoni cha nchi kuwa ni jambo la dharura mno na kuongeza kwamba: Inabidi yazingatiwe mahitaji ya hivi sasa na mahitaji ya siku za usoni ya nchi katika harakati ya kielimu; na uwekezaji ufanyike kwenye maeneo ambayo yatakidhi mahitaji ya nchi.
Vile vile amesema, suala la kuelekezwa makala za kielimu na tasnifu za shahada za udaktari upande wa kukidhi mahitaji ya hivi sasa na ya siku za usoni ya nchi ni jambo muhimu na kuongeza kwamba: Teknolojia ya nyuklia ni miongoni mwa mambo yanayohitajiwa na nchi yetu ambapo imewekeza kwenye suala hilo tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na sababu ni kwamba kama itafika wakati itakuwa haiwezekani tena kutumia mafuta, au kama akiba ya mafuta itamalizika, basi bila ya shaka yoyote tutahitajia kuwa na nishati nyengine ya kuziba pengo la nishati hiyo (na nishati hiyo ni nishati ya nyuklia).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyengine amegusia suala la kuzalishwa urani iliyorutubishwa kwa asilimia 20 na wataalamu vijana wa Iran na kuongeza kuwa: Kuna wakati fueli nyuklia ya kinu cha Tehran kinachotumika kuzalisha dawa za mionzi ilikuwa inakaribia kumalizika, na Wamagharibi walituwekea masharti mazito sana kuhusiana na kutupa fueli hiyo, lakini vijana wetu wenye vipaji na waumini wa kweli, walifanya kazi za usiku na mchana na wakafanikiwa kuzalisha urani iliyorutubishwa kwa asilmia 20 na kukidhi mahitaji ya nchi yetu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, kazi ngumu zaidi katika hatua za urutubishaji urani, ni kurutubisha kwa kiwango cha hadi asilimia 20 na ukiweza kurutubisha kwa asilimia 20 huwa rahisi tena kurutubisha kwa kiwango cha juu zaidi hadi kufikia asilimia 99 ya urutubishaji urani.
Ameongeza kuwa: Hilo ndilo lililowafanya Wamagharibi wachanganyikiwe katika kadhia ya nyuklia ya Iran na wasijue cha kufanya. Tab'an lau kama Wamagharibi wangelitupa fueli tunayoihitaji pale pale tulipowataka wafanye hivyo, sisi tusingelijishughulisha na suala la kurutubisha urani kwa asilimia 20.
Baada ya hapo ametoa muhtasari wa hotuba yake hadi kufikia hapo kwa kuandika: Kufanya tathmini ya kielimu na kuwekeza kwenye elimu inayohitajiwa na nchi ni jambo muhimu sana na inabidi lizingatiwe na lipewe umuhimu wakati wote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuwa na kasi ya maendeleo ya kielimu kwa ajili ya kufidia pengo la kubakishwa nyuma kimaendeleo na vile vile kuendelea kwa namna inayotakiwa na harakati ya kielimu nchini, kuwa ni jambo la dharura na la kimsingi na kuongeza kuwa: Inasikitisha kuona kwamba kuna baadhi ya watu hata wa Vyuo Vikuu unatawaona wanawambia wanafunzi katika vyuo vikuu kuwa ni uongo kusema kuwa kuna maendeleo ya kielimu nchini! Cha kujiuliza lakini ni kwamba, kama ni kweli hakuna maendeleo hayo ya kielimu, kwa nini vituo vya utafiti vya utawala wa Kizayuni vinaelezea wasiwasi wao kuhusiana na maendeleo ya kielimu ya Iran.
Amegusia pia kubakishwa nyuma kielimu taifa la Iran katika historia yake na kusisitiza kuwa: Kama kasi ya maendeleo ya kielimu nchini itapungua, mwanya wa maendeleo ya kielimu baina yetu na dunia utakuwa mkubwa, hivyo inabidi tuhakikishe kuwa kasi yetu ya maendeleo ya kielimu haipungui kwa namna yoyote ile.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia wajibu wa kufanywa vyuo vikuu kuwa vituo vikuu vya utafiti, kutekelezwa ipasavyo na kwa umakini ramani kuu ya kielimu nchini, kuzingatia ubora wa elimu ya juu na kuainisha vielelezo kwa kina, kwa kutumia mantiki na kwa kuzingatia uhalisia wa mambo na kuweko mawasiliano na uhusiano wa karibu baina ya Vyuo Vikuu na kuongeza kuwa: Moja ya njia za kuandaa fursa za kazi kwa ajili ya wanachuo wanaomaliza masomo na kuweko uhusiano na ushirikiano wa karibu baina ya vyuo vikuu na viwanda na kwamba jambo la lazima la kuweza kufanikisha suala hilo ni kuweko mipangilio mizuri ya wizara husika na kuleta ushirikiano mpana baina ya vyuo vikuu na sekta ya viwanda katika sekta za serikali na zisizo za serikali.
Ayatullah Udhma Khamenei ametilia mkazo ulazima wa kuweko mchango mkubwa wa vyuo vikuu katika kufanikisha uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete kupitia mashirika ya elimu za kimsingi na kuhusu utekelezaji wa siasa za uchumi wa kimuqawama amesema: Kuhusiana na utekelezaji wa uchumi wa kimuqawama, jambo ambalo linapaswa kutokea hadi sasa bado halijatokea na viongozi serikalini ndio kwanza wamewasilisha kwangu ripoti kuhusiana na mipango iliyokusudiwa kutumiwa kwa ajili ya utekelezaji wa siasa za uchumi huo wa kimuqawama.
Ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia masuala ya utamaduni katika vyuo vikuu na huku akikosoa baadhi ya hatua zilizochukuliwa kwenye vyuo vikuu amesema: Kuna baadhi ya watu wanafanya makos; wanahusisha kazi za utamaduni na matamasha ya muziki na kuweka kambi zenye michanganyiko ya watu wa jinsia zote na wanajaribu kuhalalisha jambo lao hilo lisilo sahihi kwa kusema kuwa, wanachuo wanatakiwa wafurahi na wachangamke.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Suala la kuwa na furaha ni zuri katika mazingira yoyote yale, lakini cha kujiuliza, furaha hiyo ipatikane kwa gharama gani? Kwa gharama ya kufanya sherehe na kuweka kambi zenye mchangayiko wa wanawake na wanaume? Hivi Wamagharibi wamefaidika na nini katika utamaduni wao wa kuchanganyika wanaume na wanawake? Je, kuna kitu walichofaidika nacho zaidi ya jinai za kijinsia tunazoziona leo? Sasa vipi kuna watu wanataka kufuata njia na mbinu hiyo ghalati ya Wamagharibi?
Vile vile amelitaja suala la vijana kuwa na busuri na mtazamo wa mbali wa kidini na kisiasa na kuwazuia kutumbukia kwenye mitego na kuyumba kwenye itikadi zao kuwa ni suala muhimu sana na kusisitiza kuwa: Sababu iliyopelekea watu wengi kuyumba katika fitna ya mwaka 2009, na watu hao wala hawakuwa watu wabaya, ni kukosa kwao kuwa na muono wa mbali. Wakati mtu unapoona upande wa pili unakwambia kuwa uchaguzi ni kisingizio tu bali kinacholengwa hasa ni mfumo wenyewe wa Jamhuri ya Kiislamu, mtu mwenye imani na mfumo huo anapaswa kufanya nini? Kama hatokuwa na muono wa mbali, basi atashindwa kutekeleza jukumu lake inavyopasa na katika wakati unaotakiwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amelitaja suala la kuleta nguvu za kujiamini na matumaini ya mustakbali bora kati ya vijana kuwa ni kazi nyengine za kiutamaduni zilizo lazima kufanywa kwenye vyuo vikuu na kuongeza kuwa: Nchini Iran kuna mambo mengi sana ya kutia matumaini kama vile uwezo mkubwa wa taifa, nafasi na nguvu za hivi sasa za nchi.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kujiona duni kuwa ni jambo la hatari sana na kuongeza kwamba: Suala lenyewe la kujiona duni hupelekea kudharauliwa na kupuuzwa uwezo na nguvu za taifa na nchi. Wakati ambapo kila mmoja anaziona na anazikiri nguvu na ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo hili, inashangaza kuona anatokea mtu ndani ya Iran na kusema, sisi si lolote si chochote, tumetengwa!
Vile vile amelitaja suala la kulea vijana walioimarika kiimani na wenye itikadi thabiti na wenye uhuru wa kifikra, kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi kuwa ni miongoni mwa kazi za kiutamaduni zilizo lazima kutendwa kwenye vyuo vikuu. Amesema: Kuna habari zinanifikia kutoka katika baadhi ya vyuo vikuu na ni matumaini yangu habari hizo si za kweli. Zinanifikia habari kuwa katika vyuo vikuu kuna mashinizo yanawekwa dhidi ya jumuiya za watu waumini, wanamapinduzi na wenye fikra nzuri. Ni matumaini yangu kwamba, hali ni tofauti na hivyo.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewaambia maafisa wa Wizara ya Sayansi na Tiba na wakuu wa vyuo vikuu nchini kwamba: Mnapaswa kuwafungulia njia vijana wanamapinduzi, waliojengeka kiimani, wenye moyo na fikra nzuri, walioshikamana na dini na wenye heshima katika nafsi zao kwa kadiri ya kuhakikisha kwamba anga yote inamilikiwa na vijana wa namna hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa muhtasari wa hotuba yake kwa kugusia uhusiano mkubwa na wa muda mrefu baina ya Chuo Kikuu na jamii ya watu wa vyuo vikuu na kusisitiza kuwa: Leo hii vyuo vikuu na wanachuo wanakumbwa na mawimbi ya njama kubwa zaidi na kwamba maadui wa Iran wana woga mkubwa wa kuweko wasomi wa vyuo vikuu wenye moyo wa kimapinduzi na wenye moyo wa kuingia vilivyo kwenye medani mbali mbali na kuharibu mistari myekundu ya maadui hao sambamba na kupeperusha juu bendera ya elimu na kunawirisha kaulimbiu za Mapinduzi ya Kiislamu. Maadui wanatumia fedha nyingi kupanga na kuendesha mipango ya kukabiliana na harakati hiyo kubwa ya kielimu ya Iran.
Vile vile amegusia namna wakoloni walivyobadilisha mbinu zao hivi sasa na kuongeza kuwa: Wanachofanya mabeberu hivi sasa ni kuhakikisha wanabadilisha fikra za wanaharakati, watu werevu na wenye vipaji wa nchi fulani na kuwafanya watu hao wawatumikie mabeberu badala ya kutumikia nchi zao.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesisitizia udharura wa kuenezwa thamani za taifa na za nchi katika maeneo ya vyuo vikuu na kusema kuwa: Inabidi kuzizingatia na kuzipa umuhimu daghadagha za wanachuo wanaothamini matukufu na masuala ya Mapinduzi ya Kiislamu na vile vile maelfu ya wahadhiri wa vyuo vikuu ambao ni waumini wa kweli na ni wanamapinduzi na inabidi kuwaenzi vilivyo wahadhiri hao na kujua thamani yao.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Dk Mohammad Farhadi, Waziri wa Sayansi, Utafiti na Teknolojia wa Iran ametoa hotuba fupi na kulitaja suala la kuupa umuhimu uchumi unaotegema elimu za kimsingi na kuzalisha utajiri kupitia elimu na teknolojia kuwa ni katika ajenda kuu za wizara yake katika upande wa ufanikishaji wa siasa za uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete. Amesema: Kuandaa na kupasisha hati ya uchumi wa kimuqawama, kuangalia upya na kufanyia marekebisho mipango na ratiba za masomo, kushirikiana na sekta mbali mbali za viwanda na za kutoa huduma nchini, kulitilia hima suala la utekelezaji wa hati ya Chuo Kikuu cha Kiislamu, kuanzisha kozi na masomo ya kuwajenga wanachuo na kuwafanya wawe na uhuru wa kufikiri na kutilia nguvu anga ya kidini na kimapinduzi katika vyuo vikuu, ni miongoni mwa hatua na mikakati muhimu sana ya wizara yake.
Naye Dk Ghazizadeh Hashemi, Waziri wa Afya, Matibabu na Elimu ya Tiba amesema kuwa daraja ya Iran hivi sasa ni ya kwanza katika eneo la Mashariki ya Kati katika upande wa uandikaji makala na ni ya 24 duniani katika suala hilo na kuongeza kuwa: Kupata daraja ya juu ya kuwa marejeo ya kielimu katika eneo hili, kuwa amilifu na mwenye taathira katika nyuga za kimataifa, kuyabp umuhimu matibabu ya jadi, ya kitaifa na maadili ya udaktari, kuanzisha chuo cha tiba na dini, kuchunga haki za wagonjwa na kuanzisha hospitali maalumu kwa ajili ya wanawake, ni miongoni mwa ajenda za wizara yake ya Afya, Matibabu na Elimu ya Tiba
 
< Nyuma   Mbele >

^