Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Rais wa Russia Chapa
23/11/2015
 Ayatullah Udhma Sayid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo jioni (Jumatatu) ameonana na Rais Vladimir Putin wa Russia na huku akikaribisha juhudi za kustawisha zaidi ushirikiano wa pande mbili, wa kieneo na kimataifa, ameipongeza Moscow kwa kushiriki vilivyo katika juhudi za kutatua migogoro ya Mashariki ya Kati hususan kadhia ya Syria.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Mipango ya muda mrefu ya Marekani katika eneo hili ina madhara kwa mataifa yote na kwa nchi zote hususan nchi za Iran na Russia na inabidi kuwa macho na kuamiliana kwa karibu zaidi na suala hilo ili kuvunja njama hizo za Marekani.
Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa karibu masaa mawili, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemtaja Bw. Putin kuwa ni shakhsia mkubwa na muhimu katika dunia ya leo na huku akiishukuru Russia kwa jitihada zake nzuri katika kutatua kadhia ya nyuklia ya Iran na kuongeza kuwa: Kadhia hii ya nyuklia imepiga hatua fulani, lakini sisi hatuwaamini hata kidogo Wamarekani na tunaiangalia kwa jicho la wazi na kwa uangalifu mkubwa miamala na vitendo vya serikali ya Marekani kuhusiana na suala hilo.
Vile vile ameashiria namna Bw. Putin na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu wanavyolipa uzito wa hali ya juu sana suala la kupanua na kustawisha uhusiano wa nchi mbili na kusisitiza kuwa: Kiwango cha ushirikiano baina ya pande mbili kinaweza kustawishwa zaidi na zaidi kuliko hivi sasa hususan katika masuala ya kiuchumi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria ushirikiano mzuri uliopo baina ya Tehran na Moscow katika nyuga za kisiasa na kiusalama na ameitaja misimamo ya rais wa Russia hususan katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita kuhusiana na masuala tofauti kuwa ni misimamo mizuri sana na ya kiubunifu na kuongeza kuwa: Wamarekani daima wanafanya njama za kuwafanya wapinzani wao wachukue hatua za pupa, lakini wewe umeweza kuzibatilisha siasa hizo za Marekani.
Aidha ameyataja maamuzi na hatua mbali mbali zinazochukuliwa na Moscow kuhusiana na Syria kuwa zimepelekea kuongezeka itibari ya kieneo na kimataifa na Russia na pia heshima ya Rais Putin mwenyewe nayo imeongezeka na kuongeza kuwa: Katika njama zao za muda mrefu, Wamarekani walikuwa wamekusudia kuidhibiti Syria na baadaye kulidhibiti eneo zima la Mashariki ya Kati ili kufidia kushindwa Magharibi kulidhibiti eneo la magharibi mwa Asia na kwamba njama hizo ni hatari kwa mataifa yote na kwa nchi zote duniani hususan Russia na Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Wamarekani na vitimbakwiri wao katika kadhia ya Syria wamekusudia kufanikisha malengo yao waliyoshindwa kuyafanikisha kwa njia za kijeshi; kupitia njia za kisiasa na kwenye meza ya mazungumzo, hivyo inabidi tuwe macho na tuwe na misimamo imara ya kuzuia kufanyika jambo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei amekitaja kitendo cha Wamarekani cha kung'ang'ania kuondoka madarakani Bashar al Assad, yaani Rais halali aliyechaguliwa na wananchi wenyewe wa Syria, kuwa ni katika nukta dhaifu kwenye siasa zinazotangazwa na Washington na kuongeza kuwa: Rais wa Bashar al Assad amechaguliwa kwa kura nyingi za wananchi wa Syria ambao wana mitazamo tofauti ya kisiasa, kidini na kikaumu, hivyo Marekani haina haki ya kudharau chaguo hilo la wananchi wa Syria.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema kwa kusisisitiza kwamba: Kuhusiana na kadhia ya Syria ni kuwa, njia yoyote ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo lazima wananchi wa Syria waijue, na ipate ridhaa kamili ya wananchi na viongozi wa nchi hiyo.
Ameitaja misaada ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja ya Wamarekani kwa makundi ya kigaidi kama vile Daesh kuwa ni nukta nyingine inayoonesha udhaifu wa wazi wa saisa za Marekani na kuongeza kuwa: Kushirikiana na nchi ambazo kutokana na kuunga mkono magaidi zimepoteza kabisa heshima na itibari katika fikra za walio wengi kwenye eneo hili na duniani kiujumla kunaonesha kuwa Wamarekani hawana udiplomasia wenye heshima.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndio maana ukitoa kadhia ya nyuklia (ambayo nayo ina sababu zake maalumu) Iran haifanyi na haitofanya mazungumzo yoyote ya pande mbili na Wamarekani kuhusiana na kadhia ya Syria na suala jengine lolote lile.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kututaliwa kwa njia sahihi suala la Syria ni jambo muhimu mno na lina taathira ya moja kwa moja katika mustakbali wa eneo hili na kuongeza kuwa: Iwapo magaidi wanaofanya jinai zote hizo huko Syria hawataangamizwa, wigo wa vitendo vyao viharibifu utaenea hadi Asia ya Kati na katika maeneo mengine ulimwenguni.
Kwa upande wake, Rais wa Russia amesema kwenye mazungumzo hayo kuwa anauthamini uzoefu wenye thamani kubwa wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na ameelezea kufurahishwa kwake na kupata fursa ya kuonana naye. Vile vile amesema: Suala la kustawishwa uhusiano wa nchi mbili ikiwa ni pamoja na katika nyuga za teknolojia, anga za mbali na teknolojia za kisasa limeingia kasi zaidi na sisi tumepata furaha kubwa kuona kuwa tunashirikiana vilivyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika suala la usalama na kutatua migogoro ya kieneo na kimataifa.
Rais Putin amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ni nchi huru, iliyosimama imara na yenye mustakbali mzuri sana na amemwambia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba: Nyinyi ni waitifaki wa kuaminika mnaoweza kutegemewa kieneo na kimataifa.
Rais wa Russia ameongeza kuwa: Tunaamini kwamba, tofauti na wanavyofanya wengine, sisi hatujawahi kuwaendea kinyume washirika wetu na kamwe hatujawahi kufanya mambo nyuma ya pazia dhidi ya marafiki zetu na kama kutatokezea tofauti baina yetu, tunatatua tofauti hizo kwa njia ya mazungumzo.
Rais Putin ameitaja misimamo ya nchi mbili za Iran na Russia kuhusiana na kadhia ya Syria kuwa ni ya karibu mno na huku akiashiria umuhimu mkubwa wa kuweko ushirikiano zaidi katika medani hiyo amesema: Sisi pia tunasisitiza kuwa, utatuzi wa mgogoro wa Syria utapatikana tu kwa njia ya mazungumzo na kuheshimiwa maamuzi ya wananchi wa nchi hiyo na matakwa ya kaumu na makundi yote ya Syria na kwamba mtu yeyote hana haki ya kuwatwisha wananchi wa nchi hiyo matakwa yake na kuwaundia yeye serikali yao na kuainisha yeye hatima ya Rais wa Syria.
Rais wa Russia aidha amemwamia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba: Kama ulivyosema, Wamarekani wanataka kufanikisha malengo yao kwa njia ya mazungumzo baada ya kushindwa kuyafanikisha kwenye medani za mapigano; na sisi tuko macho sana kuhusu suala hilo.
Vladimir Putin amesisitizia pia wajibu wa kuendelezwa mashambulizi ya nchi nchi yake dhidi ya magenge ya kigaidi nchini Syria na kusema kuwa ni jambo la dharura mno kuendelea kuwepo ushirikiano na misimamo ya pamoja baina ya Tehran na Moscow kuhusu mchakato wa kuutatua kisiasa mgogoro wa Syria. Amesema: Wale watu ambao wanadai kupigania demokrasia duniani, hawezi kupinga kufanyika uchaguzi nchini Syria.
Mwishoni mwa mazungumzo hayo, Rais wa Russia amempa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu zawadi ya Qur'ani Tukufu ikiwa ni zawadi yenye thamani kubwa. Kiongozi Muadhamu amemshukuru Bw. Putin kwa zawadi hiyo muhimu sana.
 
< Nyuma   Mbele >

^