Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Rais wa Iraq Chapa
24/11/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumanne) ameonana na Rais Fuad Masum wa Iraq na ujumbe alioandamana nao na kusisitiza kuwa, kina cha uhusiano wa nchi mbili na mataifa mawili ya Iran na Iraq ni kirefu, ni cha muda mrefu na ni cha kihistoria na kinapindukia uhusiano wa nchi mbili jirani zilizoko kwenye eneo moja. Aidha amesisitizia ulazima wa kulindwa umoja na mshikamano wa kitaifa wa Iraq na kusema: Taifa la Iraq ni taifa kubwa lenye historia kongwe na lenye fursa nyingi sana likiwa na vijana imara, wenye nguvu na walio macho na inabidi fursa hiyo itumiwe vizuri ili kuipandisha Iraq kwenye daraja na hadhi yake inayostahiki kuwa nayo.
Vile vile amegusia uhusiano wa kidini, wa kimapenzi na wa kushibana uliopo baina ya mataifa mawili ya Iran na Iraq licha ya nchi hizi mbili kupigana vita vya miaka minane vilivyonzishwa na Saddam dhidi ya Iran kwa uchochezi wa madola ya kibeberu na kusema kuwa, hilo lilikuwa ni jambo la kustaajabisha sana. Ameongeza kuwa: Maandamano ya kuadhimisha 40 ya Imam Husain AS ni moja ya mifano ya kuweko uhusiano huo mkubwa wa kidugu kiasi kwamba hatuoni kitu kingine kutoka kwa wananchi wa Iraq kwa ajili ya kuwahudumia wafanya ziara kutoka Iran zaidi ya kuwaonesha mapenzi, kuwaonesha ukarimu mkubwa na kuwapokea kwa heshima kubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Viongozi wa nchi mbili za Iran na Iraq wanapaswa kutumia anga na fursa hiyo kwa njia bora kabisa kwa ajili ya kulinda manufaa ya nchi mbili.
Ayatullah Udhma Khamenei ameelezea kufurahishwa kwake na mafanikio yaliyopatikana hivi karibuni nchini Iraq na kuweza kuishinda fitna ya kundi la Daesh kwa namna takriban nzuri, na huku akisisitizia wajibu wa kuwa macho na kulindwa vilivyo umoja na mshikamano uliopo hivi sasa nchini Iraq na kuongeza kuwa: Katika muundo wa mamlaka ya serikali nchini Iraq, rais wa nchi hiyo ana nafasi muhimu na anaweza kutoa mchango mkubwa katika kupunguza hitilafu na kuongeza kiwango cha mshikamano na umoja nchini humo.
Aidha ameashiria namna pande za kigeni zinavyofanya njama za kuzusha mizozo na mifarakano nchini Iraq na kuongeza kuwa: Wananchi wote wa Iraq, Mashia kwa Masuni; Wakurdi kwa Waarabu, wamekuwa wakiishi pamoja kwa amani kwa karne nyingi bila ya matatizo yoyote, lakini inasikitisha kuona kuna baadhi ya nchi katika eneo hili na vile vile madola ya kibeberu duniani yanafanya njama za kuchochea na kukuza hitilafu na mifarakano, na inabidi kusimama imara kukabiliana na njama hizo na kujiepusha kutoa mwanya wowote wa kuzuka mizozo na hitilafu nchini humo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuzusha hitilafu na halafu kuziingiza hitilafu na mizozo hiyo katika safu za wananchi huko Iraq, kuwa ni jambo linaloandaa mazingira ya kujiingiza mabeberu katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na kuongeza kuwa: Haipaswi kuruhusiwa anga ya Iraq kuwa kwa namna ambayo Wamarekani watapata uthubutu wa kuigawanya vipande vipande na kwa uwazi kabisa ardhi ya Iraq.
Ayatullah Udhma Khamenei amehoji kwa kusisitiza akisema: Kwa nini nchi kama Iraq ambayo ni nchi kubwa, tajiri na yenye historia kongwe ya maelfu ya miaka igawanywe vipande vipande na kugeuzwa vieneo vidogo vidogo kwa shabaha ya kuliweka taifa hilo katika hatari ya mizozo isiyoisha?
Ameongeza kuwa: Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba, viogozi wa Iraq wanapangilia uhusiano wao wa nje kati yao na nchi nyingine ikiwemo Marekani kwa kuzingatia maslahi na manufaa ya wananchi wao, lakini pamoja na hayo, inabidi kuwa macho zaidi na wasiruhusu Wamarekani wadhani kuwa Iraq ni kama milki yao binafsi na kusema wanalotaka na kutenda wanalopenda nchini humo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Iraq leo hii ni nchi tofauti na inatofautiana kabisa na ilivyokuwa huko nyuma kutokana na kuwa kwake taifa kubwa lenye vijana wenye nguvu na walio macho na kuongeza kuwa: Vijana wa Iraq hivi sasa wameamka na wanazijua vyema nguvu na uwezo na bila ya shaka yoyote vijana wa namna hiyo kamwe hawatakuwa tayari kuwa chini ya ubeberu wa Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei amewataja watu waliojitolea katika vita dhidi ya Daesh ni ushahidi wa wazi wa kuwa macho na kuwa na nguvu vijana wa Iraq na kusisitiza kuwa: Inabidi kutumiwa vizuri na kwa kadiri inavyowezekana fursa ya vijana na uwezo wao kwa ajili ya kuifikisha Iraq kwenye daraja ya juu inayostahiki kuwa nayo.
Vile vile amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kikamilifu kwa ajili ya kuipatia Iraq uzoefu wake na uwezo wake wa kielimu, kiteknolojia, kiulinzi na kiutumishi na kuongeza kuwa: Inabidi kufanyike juhudi za kuhakikisha kuwa kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi wa nchi mbili hizi kinapanda kwa daraja kubwa zaidi.
Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Bw. Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Fuad Masum wa Iraq ameelezea furaha yake kubwa kwa kupata fursa ya kuonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na ameashiria pia nafasi, taathira na nguvu za matamshi ya Ayatullah Udhma Khamenei kati ya wananchi na viongozi wa Iraq akiwa ni mwanachuoni mujtahid na marjaa takilidi mkubwa na kumwambia: Nasaha zako kuhusiana na wajibu wa kulindwa mshikamano na kujiepusha na mifarakano nchini Iraq, bila ya shaka yoyote zitakuwa na taathira nzuri.
Rais wa Iraq pia ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na misaada yake kwa nchi yake hususan katika kipindi kigumu cha kuvamiwa Iraq na kundi la kigaidi la Daesh na huku akiashiria mambo mengi ya pamoja ya kihistoria, kidini na kiutamaduni baina ya mataifa mawili ya Iran na Iraq amesema: Sisi tunapenda kuona uhusiano wa nchi hizi mbili unastawishwa kwa kadiri inavyowezekana ili kwa njia hiyo tuweze kustafidi vizuri zaidi na usoefu na uwezo wa Iran katika nyuga mbali mbali.
Bw. Fuad Masum pia amesema kuwa, hali jumla ya Iraq na mshikamano wa ndani ya taifa hilo umekuwa bora hivi sasa ikilinganishwa na huko nyuma na kuongeza kuwa: Kumepatikana mafanikio makubwa pia nchini Iraq katika vita dhidi ya Daesh na kwamba ushirikiano mzuri uliopo baina ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya kujitolea pamoja na vile vya Peshmerga vya Kikurdi, umeandaa uwanja wa kupata kipigo kikali genge la kigaidi la Daesh.
 
< Nyuma   Mbele >

^