Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Waziri Mkuu wa Algeria Chapa
24/11/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumanne) ameonana na Waziri Mkuu wa Algeria, Bw Abdul Malik Salal na ujumbe alioandamana nao na huku akiashiria namna mitazamo ya kisiasa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inavyokaribiana sana na ile ya Algeria katika masuala mengi ya kieneo na kimataifa amesema: Mbali na kuweko misimamo ya karibu ya kisiasa, daima taifa la Iran limekuwa likiiangalia kwa jicho zuri nchi na wananchi wa Algeria na suala hilo nalo limetokana na jihadi kubwa ya wananchi wa Algeria katika kupambana na ukoloni wakati wa kipindi cha mapinduzi ya Algeria.
Vile vile ameutaja mfungamano wa kimaanawi na wa moyoni uliopo baina ya mataifa ya dunia kuwa ni uwanja mzuri mno wa kuweza kustawisha ushirikiano baina ya mataifa hayo hususan katika upande wa kiuchumi na amemwambia Waziri Mkuu wa Algeria kuwa: Kiwango cha mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na Algeria kiko chini sana hivi sasa na ni matumaini yetu kuwa kwa safari yako hii ya kuitembelea Iran na kwa kuundwa kamati ya pamoja ya nchi mbili, na kwa kuzingatia safari ya karibuni hivi itakayofanywa na Bw. Jahangiri (Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) nchini Algeria, uhusiano wa kiuchumi wa nchi hizi mbili utaweza kuimarishwa na kustawishwa kwa kiwango cha juu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia matamshi ya Waziri Mkuu wa Algeria kuhusiana na genge la Daesh na wajibu wa nchi za eneo hili kukabiliana vilivyo na magaidi ambao wanaharibu sura ya Uislamu na kusema kuwa: Suala la Daesh na magaidi walioenea kila mahala katika eneo hili kwa jina la Uislamu si suala jepesi na wala si la kawaida, bali magaidi wamezushwa kwa makusudi na wanaendelea kuungwa mkono na madola mbali mbali.
Ayatullah Udhma Khamenei ameelezea kusikitishwa kwake na namna baadhi ya nchi za Kiislamu za eneo hili zinavyowaunga mkono magaidi wa Daesh na vile vile amegusia uungaji mkono wa Marekani na maadui wa Uislamu kwa magaidi hao na kusisitiza kuwa: Nchi za Kiislamu ambazo zina uchungu (na dini na mataifa yao) na ambazo zina maelewano mazuri zaidi baina yao, zinaweza kupata njia nzuri ya kivitendo ya kupambana na magaidi kupitia ushirikiano na mazungumzo baina ya nchi hizo.
Aidha amekumbushia kambi ya muqawama iliyoundwa na Algeria, Iran, Syria na nchi kadhaa nyingine mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya na kuongeza kuwa: Baadhi ya nchi ambazo zinaifuata kibubusa Marekani zimekuwa kikwazo cha kuendelea harakati za kambi hiyo ya nchi za muqawama lakini hivi sasa inaonekana kumeshaandaliwa uwanja mzuri wa kuundwa kambi ya nchi za Kiislamu zenye misimamo ya pamoja (kwa ajili ya kuwa na taathira katika masuala yote muhimu duniani).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kama kutaundwa kambi kama hiyo, nchi hizo za Kiislamu zitaweza kuwa na taathira nzuri katika masuala muhimu duniani na zitaweza kuchukua hatua za maana kwa ajili ya kutatua matatizo ya eneo hili na kupambana vilivyo na magaidi.
Mwishoni mwa matamshi yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameomba dua kwa kusema: Ninamuomba Mwenyezi Mungu ampe afya njema ya haraka Rais wa Algeria, Bw. Bouteflika.
Kwa upande wake, Bw. Abdul Malik Salal, Waziri Mkuu wa Algeria amesema katika mazungumzo hayo kuwa, kikao cha Tehran cha wakuu wa nchi zinazosafirisha gesi kwa wingi duniani kilikuwa cha mafanikio na huku akiashiria mazungumzo aliyofanya na viongozi mbali mbali wa Iran amesema: Mitazamo ya Iran na Algeria katika masuala ya kisiasa hususan kadhia ya kupambana na Daesh na magaidi wengine kwenye eneo hili, ni ya karibu mno na ni matumaini yetu kwa kuzingatia mazungumzo tuliyofanya Tehran, kiwango cha uhusiano wetu wa kiuchumi nacho kitatoka katika hali yake ya hivi sasa na kufikia daraja inayokubalika.
 
< Nyuma   Mbele >

^