Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Makamanda wa Brigedi za Jeshi la Basiji Chapa
25/11/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatano) ameonana na makamanda elfu mbili na mia tano wa jeshi la Basiji na kusema kuwa jeshi hilo ni mwakilishi mwenye baraka nyingi wa taasisi za taifa la Iran na huku akibainisha mbinu za kiadui za mabeberu dhidi ya taifa la Iran amesisitiza kuwa: Taifa la Iran litaendelea kutekeleza majukumu yake katika vita vya kweli baina yaya kambi ya kiistikbari na kambi ya kupigania utambulisho na ukombozi. Taifa la Iran litatekeleza vilivyo majukumu yake katika kuwahami wanyonge na watu wanaodhulumiwa hususan taifa shujaa la Palestina na Intifadha ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya Azar 5 (Novewmba 26) siku ya kukumbuka ilipotolewa amri ya kuundwa jeshi la Basiji na Imam Khomeini (quddisa sirruh) ubunifu ambao umejaa neema na baraka na kuongeza kuwa: Suala la kuundwa makundi ya muqawama katika baadhi ya nchi wakati wa mapambano na wakati wa kukabiliana na ukandamizaji lilikuwepo wakati mrefu nyuma, lakini kuweza makundi ya muqawama kuendelea kubakia baada ya kupatikana ushindi wa harakati hizo za ukombozi, na si kubakia tu, bali kupata nguvu na kustawi zaidi katika upande wa wingi na ubora, sifa hiyo inahusiana tu na jeshi la Basiji.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa maana ya kina ya neno Basiji akisema: Basiji imetoka ndani ya wananchi na ni mwakilishi wa taifa zima na mabasiji ni matabaka mbali mbali ya wananchi ambao wanapatikana katika kila medani ambayo ni lazima kupatikana wakiwa na lengo kuu la kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kufanya kazi kwa moyo usiojua kuchoka ambao wanadhihirisha vipaji vyao kwenye medani hizo na hawaogopeshwi hata kidogo na hatari zilizomo kwenye njia hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kudhihiri na kustawi vipaji vya wananchi ndani ya Basiji kuwa ni moja ya uhakika wa kustaajabisha wa Basiji na kuongeza kuwa: Ukiachilia mbali makamanda wakubwa na waliopata umashuhuri mkubwa katika vita vya kujihami kutakatifu (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran), kuna watu wakubwa wengine ambao nao walikuwa mabasiji na wamepata umashuhuri mkubwa katika medani ya elimu na teknolojia kama vile mashahidi wa nyuklia. Mabasiji hao wa upande wa elimu na teknolojia nao wamefanya kazi kubwa katika nyuga hizo.
Amesema, miongoni mwa sifa muhimu za kipekee za Basiji ni kushiriki kwake vilivyo kwenye nyuga tofauti za kijeshi, kielimu kiteknolojia, kisanaa, kiutamaduni na katika uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete.
Ameongeza kuwa: Tumewaagiza viongozi serikalini kwamba waitumie Basiji katika kufanikisha uchumi wa kimuqawama, lakini makamanda wa Basiji nao wanapaswa kuwa macho kikamilifu kwani masuala ya fedha na ya uchumi ni mambo yanayoteteresha mno imani za watu na ni katika mitego ya maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, lengo la Basiji la kuweko kwenye medani na nyuga tofauti ni kulinda malengo makuu matakatifu, tunu, thamani na utambulisho wa kimapinduzi na kitaifa wa Iran mbele ya adui msaliti, laghai, mdanganyifu na mwenye sifa za kishetani na kuongeza kuwa, serikali ya Marekani leo hii ndiyo dhihirisho la uadui wa kibeberu dhidi ya taifa la Iran.
Amesisitiza kuwa, leo hii mapambano makuu duniani yapo baina ya kambi ya harakati ya kiistikbari inayoongozwa na Marekani na kambi ya harakati ya matukufu na ukombozi wa kitaifa na kupigania utambulisho ambayo mhimili wake ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: Uistikbari mbali na kuwa na taasisi na vyombo vya kisiasa, umejizatiti pia kifedha na misaada ya makampuni na mashirika makubwa ya Kizayuni. Kwa hakika kambi ya kibeberu inatumia mambo matatu makuu, fedha, mabavu na mauaji kuendeshea njama zake zisizoisha.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha pia kuwa, udanganyifu katika vitendo vya vyombo vya kisiasa na kidiplomasia vya mabeberu unathibitisha wazi kwamba, mabeberu hao hawaaminiki hata kidogo kwani pale pale wanapocheka na wewe na kukukumbatia, ndipo hapo hapo wanapokuchoma jambia la moyoni.
Vile vile amegusia udharura wa kuwa macho daima mbele ya njama na mbinu tofauti za uadui mkali na uadui laini wa mabeberu na kusisitiza kuwa: Moja ya masuala muhimu sana katika uadui laini ni kutumiwa mpango wa kujipenyeza kwa siri na bila ya kujulikana; ndani ya mataifa mengine.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kuna baadhi ya watu utawaona wanaguswa sana kila linapozungumziwa suala la kujipenyeza adui na wanasema kuwa suala hilo linatumika ili kufanikisha malengo ya mrengo fulani. Tab'an kama kuna watu wanatumia suala hilo kimrengo hilo ni kosa, lakini suala hilo halipaswi kuwafanya watu wasahau na kughafilika na maudhui kuu na suala la kimsingi, nalo ni hilo la kujipenyeza adui.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Lililo muhimu hapa ni kuwa, tuelewe na tuamini kwamba adui anafanya njama na mipango ya kufanikisha malengo yake katika uwanja huo bila ya kusita hata sekunde moja.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amessema, kuna mbinu za aina mbili kuu zinazotumiwa na adui katika kufanikisha suala hilo nazo ni kujipenyeza kwa suala moja moja na kujipenyeza kwa sura ya kimrengo na kikanali.
Baada ya hapo ametolea ufafanuzi mbinu hizo mbili kwa kusema kuhusu kujipenyeza kwa suala moja moja kuwa, kuna mifano mingi ya huko nyuma na ya hivi sasa inayothibitisha jambo hilo. Ameongeza kuwa: Mbinu hiyo ina historia ndefu katika taasisi za kisiasa, kiserikali na hata za kidini. Watu wanaomtumikia adui huficha sura zao kwa maneno na kivitendo na wanajidhihirisha kwa sura ya marafiki na wanaingia hadi katika nyumba za watu waliowakusudia au katika taasisi na jumuiya za mtu waliyemkusudia.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, miongoni mwa malengo ya watu hao ni kukusanya taarifa na kufanya ujasusi na wakati huo huo lakini amesisitiza kuwa, lengo muhimu zaidi la kujipenyeza huko kwa masuala mamoja mamoja ni kuwasahilishia njia wanaochukua maamuzi na wapangaji wa njama za maadui.
Ameongeza kuwa: Katika mbinu ya kuathiri katika maamuzi ya taifa fulani, mtu aliyejipenyeza kwenye taasisi hizo na katika jamii hiyo, hufanya juhudi za kuhakikisha kuwa anabadilisha misimamo na mitazamo ya viongozi au watu wenye ushawishi kwenye harakati za jamii na za nchi husika katika masuala tofauti na kuwafanya watu hao wachukue maamuzi na wafanye harakati zao kwa mujibu wa njia ile ile inayotakiwa na adui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kujipenyeza kwa kutumia kanali na mirengo maalumu ndiyo mbinu hatari zaidi ikilinganishwa na mbinu nyenginezo za adui. Ameongeza kuwa: Katika mbinu hii, adui kimsingi hutumia njia mbili kuu, fedha na uvutiaji wa kijinsia kwa kufungua kanali zake za kuendeshea mambo hayo ndani ya taifa na nchi fulani ili kwa njia hiyo aweze kuwapoka watu wa taifa na nchi hiyo malengo yao matukufu, imani na itikadi zao na hatimaye aweze kubadilisha mtindo wa maisha yao.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Katika mbinu hii hatari sana ya kimrengo, huwa kuna makundi ya watu yanakutanishwa na kufanywa kuwa na mawasiliano ya pamoja kwa malengo ya uongo na kwa mbinu tofauti kwa shabaha ya kubadilisha pole pole mitazamo yao kuhusiana na masuala tofauti na kuifanya mitazamo yao ifanane na ile ya adui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja mbinu hiyo ya kubadilisha mitazamo ya watu kuwa huandaa uwanja wa kubadilika malengo matukufu, itikadi, thamani na imani za watu na kwa njia hiyo mabeberu wanaweza kujipenyeza kwenye taifa na nchi husika na kufanikisha malengo yao bila ya kujulikana.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, viongozi, wakuu wa sekta mbali mbali, watu wenye vipawa na wenye taathira katika maamuzi makuu ya nchi ndio walengwa wakuu wa mipango ya kujipenyeza adui katika taifa na nchi fulani na kwa mara nyingine amesisitiza kuwa: Haiwapasii watu kudharau asili ya suala la kujipenyeza maadui na umuhimu wake kwa madai ya uwezekano wa baadhi ya watu kutumia vibaya suala hilo kwa ajili ya kufanikisha malengo ya mirengo yao.
Amesema, kuyapa umuhimu mambo ya pembeni na kusahau masuala ya asili, ni mkamilishaji wa mpango wa kujipenyeza maadui na kuongeza kuwa: Katika suala hilo utaona kuwa, wale watu ambao wako imara katika kulinda matukufu na mambo yao ya asili wanapachikwa majina ya watu wenye misimamo mikali na misimamo ya kuchupa mipaka kwa shabaha ya kuwanyamazisha ili kwa njia hiyo iwezekane kudhoofisha polepole thamani na malengo matukufu ya taifa na ya nchi fulani na hatimaye kuandaa uwanja wa kufanikisha malengo ya mpango maalumu wa kujipenyeza adui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametumia fursa hiyo kuwakosoa vikali watu na mirengo ambayo inathubutu kuituhumu Basiji kuwa ina misimamo ya kufurutu ada na kuongeza kwamba: Sitaki kusema kuwa watu na mirengo hiyo wanatoa tuhuma hizo kwa kujua, lakini ijulikane kuwa, tuhuma hizo zinadhoofisha msingi madhubuti wa Basiji na ni katika kukamilisha malengo hatari ya kujipenyeza adui; ni sawa tu wanaofanya hayo wanajua wanachokifanya au hawajui.
Aidha ametoa nasaha kwa watu ambao wanatumia mimbari na minasaba tofauti kujaribu kuwadhoofisha na kuwakosoa watu wanaopigania mambo ya asili na misingi mikuu ya Mapinduzi ya Kiislamu akiwaambia: Si sahihi kumtuhumu kila mtu anayetetea matukufu na misingi mikuu ya Mapinduzi ya Kiislamu na Imam (quddisa sirruh) kuwa anafanya hivyo kwa malengo ya kufanikisha shabaha za mrengo fulani au kudai kuwa ana misimamo mikali.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria kustawi na kuimarika taathira na baraka za mtawalia za Basiji na kuongeza kuwa: Mustakbali wa Basiji unang'ara lakini inabidi kuchukuliwe tahadhari ili kusije kukatokea ugonjwa hususan ugonjwa wa ndani kwa ndani utakaohatarisha usalama wa mti huo imara na madhubuti wa Basiji.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja maradhi kama ghururi, kukumbwa na mghafala utokanao na kujiona na kutumbukia kwenye ushindani wa kupigania mambo ya kidunia kuwa ni miongoni mwa magonjwa ya ndani kwa ndani ambayo Basiji na watu wa Basiji wanapaswa kuwa macho nayo na kujiweka mbali nayo kikamilifu.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amebainisha vipaumbele vya Basiji kuwa ni taqwa, busuri na kuwa na muono wa mbali na kusisitiza kuwa: Inabidi Basiji iielewe vizuri medani ya ndani ya nchi, alama za maadui na nukta za kujiimarisha ndani kwa ndani na kuitambua vyema nafasi aali na yenye heshima kubwa ya taifa la Iran kieneo na kimataifa.
Aidha amewalaumu vikali wale watu ambao wanazikana nguvu na uwezo adhimu wa taifa la Iran kutokana na wao wenyewe kujiona duni mbele ya Magharibi na kuongeza kuwa: Ni jambo lisilo na shaka kwamba kuna mapungufu ya hapa na pale humu nchini, lakini si sahihi hata kidogo kujiona duni mbele ya mabeberu na kulidharau taifa na hivyo kuitoa thamani nafasi muhimu ya Iran kieneo na kimataifa na kutoona thamani za mafanikio na uwezo mkubwa wa wananchi wa taifa hili kubwa, azizi na lenye heshima.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, kipaumbele kingine kikuu cha Basiji ni kujiimarisha na kujiweka tayari wakati wote na kusisitiza kuwa: Hatuwezi kukaa kimya mbele ya mapambano baina ya kambi ya kibeberu na kambi ya matukufu na ya kupigania ukombozi na ni kwa sababu hiyo ndio maana misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala tofauti ya eneo hili hususan kadhia ya Palestina na masuala ya Bahrain, Yemen na Syria na Iraq, ukawa ni msimamo wa wazi kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, lengo kuu la kambi ya kiistikbari ni kufifilizisha na kusahaulisha malengo matukufu ya Palestina na kusisitiza kwamba: Pamoja na kuwepo njama zote hizo za kambi ya kibeberu na hata baadhi ya nchi za Kiarabu zinazoifuata kibubusa kambi hiyo, lakini tunaona kuwa Intifadha ya wananchi wa Palestina mara hii imeanzia katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia dhulma zinazofanywa na vyombo vya habari vya madola ya kibeberu hususan kuhusu kadhia ya Palestina akisema: Vyombo hivyo vinatangaza kuwa eti ni magaidi watu ambao hawana silaha ghairi ya kurusha mawe wanaolalamikia kukaliwa kwa mabaru ardhi zao na kuvunjwa nyumba na makazi yao! Wakati huo huo lakini vyombo hivyo vinaliunga mkono kundi ambalo limeangamiza heshima na haki za Wapalestina na vinadai kuwa eti kundi hilo lina haki ya kujilinda.
Ameongeza kuwa: Je, kuangaliwa kwa namna hii kadhia ya Palestina, ni kosa na dhulma ndogo ambayo mtu anaweza kuipita vivi hivi? Je, kitendo hicho cha kidhulma mtu anaweza kukiangalia kwa macho tu bila ya kufanya chochote?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Sisi tutaendelea kuiunga mkono harakati ya wananchi wa Palestina kwa nguvu zetu zote na kwa njia zote na kwa muda wote tutakaoweza kufanya hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia suala la Bahrain na kusema: Kosa la wananchi wa Bahrain ni lipi? Je, wananchi hao wanataka kitu kingine chochote ghairi ya kila mmoja wao kuwa na haki ya kupiga kura? Je, hiyo si demokrasia? Hivi kwani Wamagharibi hawajigambi kuwa wanapigania demokrasia duniani?
Vile vile ameashiria namna wananchi wa Bahrain wanavyowekewa mashinikizo na kudhalilishwa na madhalimu wachache wanaong'ang'ania madaraka na kuongeza kuwa: Ubaya wa madhalimu hao wachache ni mkubwa na umefikia hadi kwamba wanadharau na kuvunjia heshima hata matukufu ya Waislamu na maombolezo ya Muharram ya wananchi wa Bahrain.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia mashambulizi ya miezi mingi sasa ya mfululizo wanayofanyiwa wananchi madhulumu wa Yemen na kusema: Yale mashirika na taasisi zinazodai kupigania demokrasia na haki za binadamu duniani, ndizo hizo hizo ambazo leo hii zinawaunga mkono watu ambao wanawashambulia kinyama kwa kila aina ya mashambulizi, wananchi madhulumu wa Yemen.
Amma kuhusiana na kadhia ya Syria na Iraq, Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Kambi ya kiistikbari inawaunga mkono magaidi khabithi na maafiriti zaidi katika nchi hizo na amma kuhusiana na huko nchini Syria, kambi hiyo inang'ang'ania kuwapangia wananchi wa nchi hiyo serikali inayotakiwa na kambi hiyo.
Amehoji kwa kuwaambia mabeberu lwamba: Nyinyi ni nani na mna haki gani ya kutoka huko mlikotoka na kwenda kuwapangia wananchi wa Syria nini cha kufanya? Kila taifa lina haki ya kujiamulia lenyewe ni utawala gani linautaka uwatawale bila ya kuingiliwa na mtu yeyote yule.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Basiji inaweza kubainisha kwa ufasaha kabisa kwamba misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na Palestina, Syria, Iraq, Yemen na Bahrain ni misimamo ya kimantiki kabisa ambayo inaweza kuchukuliwa na mtu yeyote mwenye insafu na mwenye akili.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, Basiji ni hazina na dafina isiyo na kikomo na kusisitiza kuwa: Kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, taifa la Iran litailinda dafina hiyo na litazidi kufukua vito vya thamani kutoka katika hazina hiyo na litaweza kufikia kwenye taraja za juu za ubora kupitia hima, irada, utashi, busuri na muono huo mkubwa wa mbali wa Basiji na kwamba maadui hawatoweza kufanya chochote.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Meja Jenerali Muhammad Ali Jaafari, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa, Basiji ni mwana na mzaliwa wa umaanawi wa mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Imam Khomeini - quddisa sirruh) na kuongeza kuwa: Basiji hivi sasa inajiweka tayari kwa ajili ya kutoa michango mbali mbali kimataifa katika njia ya kuyafikia malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu na kubadilisha milingano kwa manufaa ya wanyonge na Waislamu wote duniani.
Naye Brigedia Jenerali Muhammad Reza Naqdi, Mkuu wa Taasisi ya Basiji ya Wanyonge ametoa hotuba fupi na huku akiashiria namna matakwa ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) yalivyoweza kufanikishwa kuhusiana na kustawishwa na kupewa nguvu Basiji katika matabaka yote amesema kuwa: Mabasiji wamesimama imara hadi tone la mwisho la damu zao kulinda ahadi walizowekeana na mashahidi na kamwe hawatotulia hadi pale dhulma yote itakapoangamizwa.
 
< Nyuma   Mbele >

^