Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Waziri Mkuu wa Hungary Chapa
01/12/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumanne) ameonana na Waziri Mkuu wa Hungary, Bw. Viktor Orbán na huku akiashiria kuweko nyuga nyingi za kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi mbili, ameitaja mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni kushirikiana na mataifa yote duniani na kusisitiza kwamba: Siasa zilizotangazwa na serikali ya Hungary kuhusiana na kuzizingatia nchi za bara la Asia ni siasa nzuri na zinaweza kuwa chimbuko la kuongezeka kiwango cha ushirikiano wa kila aina kwenye eneo hili.
Katika mazungumzo hayo, Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kiwango cha uhusiano wa kiuchumi na usio wa kiuchumi baina ya Iran na Hungary kiko chini na si kizuri na amemwambia Waziri Mkuu huyo wa Hungary kwamba: Taifa la Iran halina kumbukumbu yoyote mbaya kuhusiana na Hungary na kwamba tunapouangalia ujumbe ulioandamana nao ambao ni ujumbe wa ngazi nzuri wa viongozi, tunapata matumaini kwamba safari yako hii itakuwa ni utangulizi mzuri wa kupanua wigo wa ushirikiano wa pande mbili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu kwamba ni kuwa na ushirikiano na watu na mataifa yote na kuongeza kuwa: Tab'an kuna baadhi ya mambo yanatoka katika mkondo huo kutokana na sababu maalumu lakini ukitoa mambo hayo maalumu, sisi huwa tunajibu hisia na siasa za kuheshimiana kwa hisia nzuri na za kweli.
Aidha ameunga mkono matamshi ya Waziri Mkuu wa Hungary kuhusiana na udharura wa kuweko welewa sahihi kuhusu serikali na mataifa ya dunia ukiwa ndio msingi wa ushirikiano baina ya mataifa hayo na kuongeza kuwa: Kuna haja ya kuandaliwa muundo madhubuti wa kuzingatia mambo ya kimsingi kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano na mabadilishano ya kiuchumi, kielimu, kiutamaduni na kimasomo kati ya mataifa mbali mbali duniani.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, chanzo cha uadui na chuki baina ya mataifa ya dunia ni kukosekana welewa sahihi kuhusiana na pande husika na kuongeza kuwa: Katika anga ya propaganda nyingi sana inayotawala duniani leo hii, matukio yanayojiri kwenye maeneo tofauti duniani yanaoneshwa kinyumenyume na jambo hilo la kubereuza mambo lina madhara makubwa kwa utu na ubinadamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia namna Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inavyoendesha mazungumzo mazuri na ya kujenga mapenzi baina ya ulimwengu wa Kiislamu na wa Kikristo na kuongeza kuwa: Kutumiwa vizuri fursa hizo kwa ajili ya kuongeza idadi ya nukta za pamoja na kuzidi kuweka wazi uhakika mbali mbali wa mambo ni moja ya hatua za kuleta welewa sahihi kuhusu masuala tofauti ikiwa ni pamoja na amri na mafundisho ya Uislamu.
Amesema, propaganda nyingi mbaya dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ambazo zimekuwepo katika kipindi chote hiki cha miongo minne iliyopita, ni mfano mwengine wa miamala ya kindumakuwili ya vyombo vya kipropaganda duniani kuhusiana na matukio mbali mbali na kuongeza kuwa: Kuweko mazungumzo na kutembeleana wasomi na wanafikra ni kwa manufaa ya juhudi za kubainishwa uhakika kwa sura inayotakiwa na ni kwa sababu hiyo ndio maana sisi tunaafikiana na mabadilishano ya namna hiyo.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Ayatullah Khamenei ameitaja tathmini ya Waziri Mkuu wa Hungary kuhusiana na kutokuwa nzuri hali ya nchi za Magharibi katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kiulinzi na kuhusiana na kuwepo migogoro ya kila aina ya kimaanawi na matatizo mengi ya kiutamaduni barani humo kuwa ni tathmini ya kielimu na kiutaalamu na ni iliyo karibu na uhakika wa mambo na kuongeza kuwa: Baadhi ya wanafikra wenye uchungu wa Magharibi kwa miaka mingi waligundua kuweko hatari hiyo na wamekuwa wakionya kuhusiana na hatari hiyo kwa muda mrefu sasa.
Amesisitiza kuwa: Hivi sasa kuna mmea wa kimaanawi unaoendelea kumea pole pole na bila kuhisika katika nchi za Ulaya na Marekani hususan ndani ya jamii ya vijana na kuna uwezekano katika siku za usoni Ulaya ikaweza kushuhudia kiwango sawa cha maendeleo kati ya maendeleo kimaanawi kwa upande mmoja na maendeleo ya kimaada, kielimu na kiteknolojia kwa upande wa pili.
Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Bw. Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Bw. Viktor Orbán, Waziri Mkuu wa Hungary ameelezea kufurahishwa kwake na ziara yake ya nchini Iran na kusema: Mimi nimekuja na ujumbe wa ngazi za juu wa kibiashara na kiuchumi kwa lengo la kustawisha uhusiano wetu na Iran na ninaamini kwamba kuna maeneo mengi ya kuweza kuimarishwa ushirikiano wa pande mbili.
Waziri Mkuu wa Hungary amekumbushia udharura wa kuimarishwa muundo wa ushirikiano baina ya nchi mbili hizi na kumwambia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba: Kuweko welewa sahihi kuhusiana na masuala ya pande mbili ndio usuli na msingi wa ushirikiano mzuri na kwa kuzingatia nafasi kubwa na ya kuheshimika ya Iran katika milingano wa kimataifa, tunatumai - kwa uungaji mkono wako - tutaweza kuandaa fursa nyingi za ushirikiano wa pande mbili katika viwango tofauti.
Waziri Mkuu wa Hungary amegusia pia matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na namna vyombo vya kipropaganda vinavyobereuza na kuonyesha kwa sura isiyo sahihi matukio yanayotokea kwenye maeneo tofauti duniani na kusema kuwa, yeye binafsi na Baraza lake la Mawaziri ni wanachama wa Mapinduzi dhidi ya ukaliaji kwa mabavu.
Ameongeza kuwa: Sisi hatukuwa na matatizo yoyote wakati wote ambapo tumekuwa katika mapambano ya kimapinduzi, lakini mara baada ya hawa watu kuelewa kuwa tunafanya juhudi za kuunda mfumo mpya wa kuijenga nchi yetu, wameanza kuendesha propaganda mbaya dhidi yetu.
Bw. Viktor Orbán ameashiria pia suala la kuendelea kubadilika mahusiano ya kimataifa na kuongeza kuwa: Mabadiliko hayo ya haraka yametoa pigo kwa taswira iliyoundwa na Magharibi na madola makubwa ulimwenguni ni hivi sasa madola hayo ya kibeberu yamo katika hali mbaya ya kiroho na kisaikolojia.
Amesema: Kulifanya suala la ustawi wa kimaada kuwa msingi mkuu na kusahau masuala mengine ya kiroho na kimaanawi kumevitumbukiza katika hatari ya kusambaratika vielelezo vya huko nyuma vya Magharibi katika upande wa maadili, siasa na dini na kuviingiza vielelezo hivyo katika kipindi kigumu na tete sana.
Waziri Mkuu wa Hungary ameyataja matatizo kama vile kupungua idadi ya watu katika jamii, kupotea thamani za familia na kupata nguvu fikra ya kuundwa familia zisizo salama, migogoro ya mtawalia ya kiuchumi, kudhoofika uwezo wa kiusalama na kiulinzi na kupata nguvu magaidi kuwa ni miongoni mwa migogoro iliyozikumba nchi za Ulaya hivi sasa.
Ameongeza kuwa: Migogoro hiyo imeilazimisha Magharibi kubadilisha misimamo yake na kuelekeza macho yake katika udharura wa kuwa karibu na nchi za Mashariki ili kwa kupata matukufu ya kimaanawi ya nchi hizo, ziweze nchi za Magharibi kupata njia za kujikwamua kutoka katika migogoro yao mizito.
 
< Nyuma   Mbele >

^