Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wananchi wa Qum Chapa
09/01/2016
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi ameonana na maelfu ya wananchi wenye shauku wa Qum na huku akiwapongeza wananchi wa mji huo kwa mapambano yao ya tarehe 19 Dei 1356 (Januari 9, 1978) na kubainisha sababu na mambo yanayopelekea Mapinduzi ya Kiislamu yazidi kuimarika amesisitiza kuwa: Mwamko wa watu wote nchini Iran umeyafanya Mapinduzi ya Kiislamu yadumu na yazidi kuwa imara na kufanikiwa kuleta utulivu na uraufu katika taifa na kuzishinda njama za maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kuyaenzi mapambano hayo ya Dei 19 (Januari 9, 1978) ya wananchi wa Qum dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah na ambayo yalifanyika kwa ajili ya kuunga mkono "umarjaia" na wanavyuoni, amesema kuwa wananchi wa Qum ni watu waliko mstari wa mbele katika kufanikisha Mapinduzi na kuyaimarisha na kuongeza kuwa: Katika miaka ya mapambano, hotuba za Imam Khomeini (quddisa sirruh) na nafasi tukufu ya "umarjaia" na maulamaa wa kidini ni mambo ambayo yaliandaa mazingira ya kujitokeza wananchi kwa ajili ya kupambana na utawala wa kidikteta wa Shah, na kwamba mapambano ya Dei 19 ya wananchi wa Qum ndiyo yaliyofungua mapambano hayo muhimu mno.
Amesema, ushujaa na muono wa mbali wa wananchi na kuhisi wajibu wa kuingia kwenye medani ya mapambano kwa wakati unaofaa, ni katika sifa kuu za mapambano ya Dei 19 na kuongeza kuwa: Mapambano hayo ya wananchi wa Qum yaliyofanyika kwa ajili ya kumuhami Imam (Khomeini -quddisa sirruh) na matukio yaliyotukia baada yake, ndiyo yaliyopelekea kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulipatikana licha ya kwamba, utawala uliokuweko madarakani wakati huo nchini Iran ulikuwa ni utawala wa kibaraka na wa kidikteta ambao ulikuwa ukiungwa mkono kwa kila hali na madola ya kiistikbari, na kwa mahesabu ya kimaada na kijuu juu, ilionekana ni jambo lisiloyumkinika kabisa kuupindua utawala kama huo.
Ameongeza kuwa: Ushindi huo wa Mapinduzi ya Kiislamu ulionesha kuweko sunna ya Mwenyezi Mungu, yaani nguvu za nyuma ya dunia ya kawaida ambayo mtu anayezingatia masuala ya kidunia tu hawezi kuielewa.
Amesisitiza kuwa: Hivi sasa pia, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unakabiliana na kambi pana na kubwa ya maadui, iwe ni Marekani na utawala wa Kizayuni au vibaraka na vitimbakwiri vya mabeberu au makundi yao ya kitakfiri kama vile Daesh ambapo kama tutatumia zana za sunna ya Mwenyezi Mungu yaani kusimama kidete, kuwa na muono wa mbali na kuchukua hatua katika lahadha na sekunde inayotakiwa, basi bila ya shaka yoyote Mapinduzi ya Kiislamu yatapata ushindi dhidi ya kambi hiyo, kama yalivyopata ushindi dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia sababu zinazopelekea kudumu na kuzidi kuwa imara Mapinduzi ya Kiislamu ikilinganishwa na baadhi ya matukio muhimu katika historia ya hivi karibuni ya Iran na duniani kiujumla.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia matukio mawili ambayo ni mapambano ya kuyafanya mafuta kuwa mali ya taifa nchini Iran pamoja na mapambano ya kupigania utawala wa sheria nchini na kusema: Katika mapambano ya kuyafanya mafuta kuwa mali ya taifa, matakwa ya wananchi, yalikuwa ni matakwa ya chini kabisa na yaliishia tu katika kukatwa mkono wa Uingereza kwenye maliasili ya mafuta ya taifa la Iran na katika mapambano ya kipindi cha kupigania utawala wa sheria na bunge pia, matakwa ya wananchi yalikuwa ya chini kabisa yaani kubana nguvu na uwezo mutlaki aliokuwa nao Shah.
Ameongeza kuwa, matukio hayo mawili ijapokuwa yalikuwa na malengo ya chini kabisa, na wananchi waliingia kwenye medani kwa ajili ya kuyafanikisha, lakini yalishindwa. Hata hivyo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ijapokuwa yalikuwa na malengo ya juu kabisa, yaani kuleta uhuru wa pande zote na kuipindua kabisa serikali ya kifalme na ya kiimla ya Shah, lakini yalifanikiwa na yamedumu na kubakia imara hadi leo hii.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Kama vijana watapata uchambuzi sahihi kuhusiana na jambo hilo, basi njama za baadhi ya watu za kupandikiza mbegu ya woga, hofu na kukata tamaa katika nyoyo za wananchi wa Iran hazitafua dafu, na njia sahihi ya mustakbali bora wa nchi itakuwa bayana.
Vile vile ameashiria namna mapinduzi mengine duniani kama yale ya Ufaransa na ya Umoja wa Kisovieti yalivyoachana na njia na malengo yake ya awali na baadaye kutoweka kabisa na kuongeza kuwa: Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ndiyo mapinduzi pekee ambayo yameweza kubakia juu ya msingi na malengo yake yale yale ya awali.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, lengo kuu kabisa la vituo vya kifikra na kinadharia ya ulimwengu wa kiistikbari ni kuangamiza vielelezo na misingi inayoyafanya Mapinduzi ya Kiislamu yadumu na yazidi kuwa imara.
Ameongeza kuwa: Juhudi zote za maadui katika kipindi chote cha miaka ya hivi karibuni, iwe ni wakati wa vita vya kulazimishwa (vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran), mashinikizo ya kiuchumi na vikwazo vingine vingi vya kila aina vya hivi karibuni, zote zimelenga kuangamiza misingi hiyo inayoyafanya Mapinduzi ya Kiislamu yadumu na tab'an kila muda wanavumbua mbinu na njama mpya za kufanikisha malengo yao maovu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa, katika mwaka 2009, Wamarekani walikusudia kutekeleza mbinu yao waliyoitumia na kufanikiwa katika nchi kadhaa, ya kutumia kisingizio cha uchaguzi kufanya machafuko nchini Iran. Walitumia mbinu ya kuwakuza watu wachache ambao walishindwa katika uchaguzi, na kuwasaidia kifedha na kisiasa ili kuvuruga matokeo ya uchaguzi nchini Iran lakini Mapinduzi ya Kiislamu yalifelisha mbapinduzi hayo ya "rangi" ya maadui kwa msaada kamili wa wananchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia uungaji mkono wa Rais wa Marekani kwa wapinzani wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika matukio ya mwaka 2009 na kuongeza kuwa: Serikali ya Marekani ilisaidia matukio hayo kwa kadiri ilivyoweza, lakini kutokana na kujitokeza wananchi wa Iran katika medani kwa wakati mwafaka kabisa, njama hizo za maadui hazikufanikiwa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Wamarekani hivi sasa wanasema kuwa, kipindi cha baada ya mazungumzo ya nyuklia kitakuwa kipindi cha kuibana Iran, utadhani huko nyuma wamewahi kukaa bila ya kuibana na kuilegezea kamba Iran. Hata hivyo vijana, wananchi na viongozi walio macho, wenye matumaini na walio na mwamko wa Iran wamesimama imara katika muqawama na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kwa kutegemea nguvu zake katika kukabialiana na maadui, na hilo ni jambo muhimu sana.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, tabia ya uchaguzi ni kutoa nafasi mpya kwa taifa na kuongeza kwamba: Hisia za wananchi za kuhisi ni wajibu wao kutekeleza vizuri majukumu yao na ambazo zinaakisiwa kupitia kushiriki kwenye uchaguzi na kufelisha njama za maadui, ni katika mambo makuu yanayoyafanya Mapinduzi ya Kiislamu kuzidi kudumu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema pia kwamba, kuna mambo mawili yana umuhimu mkubwa katika uchaguzi, nayo mosi ni kushiriki kwenyewe kwenye uchaguzi na pili ni kuchagua watu wazuri na kuwapigia kura wagombea wanaofaa zaidi.
Kwa mara nyingine tena amesisitizia udharura wa kushiriki watu wote waliotimiza masharti ya kupiga kura katika uchaguzi na kuongeza kuwa: Kama tulivyofanya huko nyuma, hivi sasa pia tunawasisitizia watu wote, hata wale ambao hawamkubali Kiongozi Muadhamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, washiriki kwenye uchaguzi, kwani uchaguzi ni mali ya taifa zima, ni mali ya Iran na ni mali ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la watu wote kushiriki katika uchaguzi kuwa linapelekea kuzidi kuimarika na kupata nguvu mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na vile vile kuendelea kudhaminiwa usalama kamili nchini na kuongezeka itibari na heshima ya taifa mbele ya walimwengu na pia kuongezeka haiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha pia umuhimu mkubwa wa kuwapigia kura wagombea bora zaidi na kuongeza kwamba: Kuwa na misimamo na maoni tofauti hakuna tatizo, lililo muhimu tufanye juhudi na tuwe makini na kuhakikisha kuwa chaguo letu ni sahihi.
Ameongeza kuwa: Iwapo umakini huo utazingatiwa na kupewa nafasi, na baadaye ikatokezea baadhi ya watu waliochaguliwa wakawa si wale waliostahiki kuchaguliwa, lakini juhudi na umakini wa mpiga kura katika kuchagua wagombea bora zaidi zitamridhisha Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia nafasi muhimu na ya juu ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) katika masuala ya ndani ya nchi na ya kimataifa na kuongeza kuwa: Majlisi (ya Ushauri ya Kiislamu) ina umuhimu wa kipekee katika masuala mengi hususan katika suala la kupasisha sheria, kuziwekea njia za kupita serikali zinazoingia madarakani na kudhihirisha uimara, kusimama kidete na kutotetereka taifa.
Ameitaja misimamo ya bunge la sasa hivi katika masuala ya kimataifa kuwa ni misimamo mizuri na kuongeza kuwa: Bunge ambalo litasimama imara kukabiliana vilivyo na maadui katika suala kama la nyuklia na masuala mengineyo na kubainisha misimamo ya taifa, kishujaa, kwa uhuru na istiklali kamili, lina tofauti kubwa mno na bunge ambalo litakuwa linakariri na kurudia matamshi yale yale ya adui katika masuala tofauti.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kila mbunge ana mchango na anahusika katika kuundika harakati na misimamo ya bunge la taifa na kuongeza kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndio maana wananchi wa mikoa na miji yote nchini wanapaswa wawe makini kikamilifu katika kuchagua wabunge wao na wawe na yakini kuwa mtu wanayemchagua ndiye anayefaa zaidi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Tab'an ni jambo zito kumjua kwa undani na kiukamilifu kila mgombea, lakini inawezekana kuwajua watu kwa kuangalia historia na misimamo yao na kupitia orodha ya wagombea na mirengo yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kama waliotoa orodha ya wagombea ni watu waumini na wanamapinduzi na ambao kwa yakini wanaikubali njia ya Imam (Khomeini - quddisa sirruh), basi mtu anaweza kuiamini orodha hiyo na kuwachagua wagombea waliopendekezwa na watu hao kwa ajili ya kuwapeleka bungeni na katika Baraza la Wanavyuoni Wataalamu, lakini kama waliopendekeza wagombea si wanamapinduzi, wala hawashughulishwi sana na dini wala uhuru wa nchi, na wanachozingatia wao ni kukubaliana na maneno ya Marekani na mabeberu wengine, orodha ya watu hao si ya kuaminika na haifai.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu (linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu) ni muhimu mno na kuongeza kuwa: Tofauti na wanavyodhani baadhi ya watu, kazi ya Baraza la Wanavyuoni Wataalamu si kukutana mara moja au mbili kwa mwaka, bali miongoni mwa kazi muhimu mno za baraza hilo ni kumchagua Kiongozi Muadhamu, pale Kiongozi aliyepo hivi sasa atatangulia mbele ya haki; na Kiongozi maana yake ni mtu mwenye ufunguo wa harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu, na suala hilo kwa hakika ni muhimu mno.
Aidha amesisitizia udharua wa kuwa macho kikamilifu katika kuchagua wagombea wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu na kuongeza kuwa: Kulingana na muundo wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu, wajumbe wa baraza hilo wana kazi ya kumchagua mtu wa kuwa Kiongozi Muadhamu kila inapobidi ambaye ataweza kusimama imara kiushujaa katika kukabiliana na maadui kwa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kuendeleza njia ya Imam, lakini pia kuna uwezekano wajumbe hao wakamchagua Kiongozi ambaye ana sifa tofauti na hizo, hivyo kuwapigia kura watu makini mno ambao ustahiki wao unaweza kujulikana kwa kupitia utafiti, umakini wa hali ya juu, kuwajua na kuwa na imani nao ni jambo muhimu na la dharura kabisa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, kushiriki katika uchaguzi na hususan kuwa makini katika kuchagua wagombe wazuri na wanaostahiki zaidi, kutafanikisha malengo mawili makuu; mosi ni kuzidi kudumu na kuwa imara Mapinduzi ya Kiislamu na pili ni taifa kupata utuvu na utulivu.
Vile vile ametoa ufafanuzi kuhusu athari za kuchagua watu sahihi katika kuyafanya Mapinduzi ya Kiislamu yadumu na kuongeza kuwa: Tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu, tumekuwa tukishuhudia mitikisiko, mititigo na pia madmbo mazuri mengi. Kuna baadhi ya watu walikuwa wanamapinduzi, lakini kutokana na labda kudhulumiwa na mtu fulani, walilaumu asili ya Mapinduzi yenyewe na kuachana nayo. Wako pia baadhi ya watu ambao kutokana na masuala yao binafsi na familia zao wamebadilisha misimamo yao, lakini lililo muhimu ni kuwa, mambo mazuri ya Mapinduzi ya Kiislamu katika nyuga tofuati zikiwemo za kuweko nguvukazi za watu waumini, wanamapinduzi, wataalamu, wasomi, watu wenye manufaa na weledi wa mambo ni mingi zaidi ikilinganishwa na masuala hasi yaliyoyabakili Mapinduzi ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Katika kipindi cha hivi sasa pia, kama wananchi watatekeleza vizuri majukumu yao katika kuchagua wagombea wanaofaa zaidi kwa ajili ya Baraza la Wanavyuoni Wataalamu, basi mimea iliyonawiri vizuri ya Mapinduzi ya Kiislamu itakuwa mingi zaidi na jambo hilo litazidi kuyadumisha Mapinduzi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja sifa nyingine maalumu ya kutekeleza vizuri majukumu katika kuyaimarisha Mapinduzi ya Kiislamu na kuyafanya yadumu kuwa ni kuleta utulivu katika nyoyo za wananchi na ametoa ushahidi wa aya za Qur'ani Tukufu kuhusu kushushiwa utuvu na utulivu wa nyoyo masahaba waliombai na kutangaza utiifu wao kwa Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Waalihi Wasallam na kuongeza kuwa: Mtu yeyote leo hii atakayeyabai na kutangaza utiifu wake kwa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa Imam Khomeini (quddisa sirruh) na kwa njia ya Imam, huwa ni sawa na mtu aliyembai na kutangaza utiifu kwa Bwana Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Waalihi Wasallam na Inshaallah Mwenyezi Mungu atamlipa malipo mema kwa kutangaza bay'a na utiifu wake huo na ataondoa daghadagha, wasiwasi na kukosekana matumaini ndani ya taifa na kuweka mahala pake yakini na utulivu wa nyoyo.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Kuendelea kudumu na kuwa imara Mapinduzi ya Kiislamu na kusimama kidete kunakoleta matumaini na kulikojaa utulivu kwa watu, kwa yakini kutapelekea taifa la Iran liishinde Marekani na njama zote za maadui.
 
< Nyuma   Mbele >

^