Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Katibu na Maafisa wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa Chapa
03/02/2016
Secretary and officials of Supreme National Security Council met with LeaderAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi ameonana na Admeli Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa pamoja na manaibu na wataalamu wa sekretarieti ya baraza hilo na huku akiashiria namna istilahi na neno "usalama" lilivyo tata na lilivyo na vipengee vingi tofauti katika dunia ya leo, amelitaja jukumu la Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kuwa ni kufanya maamuzi kwa kuangalia upana na vipengee vyote vya neno usalama na kwamba jukumu kuu la sekretarieti ya baraza hilo ni kuandaa maamuzi ya kuonesha njia sahihi ya uchukuaji maamuzi ndani ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa. Amesisitiza kuwa: Ili sekretarieti hiyo iweze kutekeleza vizuri na kwa njia sahihi nafasi muhimu sana ya kuandaa maamuzi, inabidi anga iliyopo katika sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na mikakati yake ikubaliane kikamilifu na "fikra sahihi, halisi na safi ya kimapinduzi na ya kihizbullah (ya mtu aliyeko kwenye chama cha Mwenyezi Mungu yaani aliyeshikamana vilivyo namafundisho ya dini)."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, usalama ni moja ya mambo ya kimsingi zaidi na ya lazima zaidi katika jamii na ni kwa sababu hiyo ndio maana Qur'ani Tukufu imelizungumzia mara nyingi suala hilo. Ameongeza kuwa: Leo hii suala la usalama limetoka katika sura yake ya kuishia tu kwenye masuala ya kijeshi na kiusalama na lina upeo pia wa masuala ya kiuchumi, kimaisha, kiutamaduni, kisiasa, kijamii, kisaikolojia na kimaadili.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja jukumu kuu la Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kwamba ni kuwa na mtazamo mpana kuhusu kadhia ya usalama na kuzingatia vipengee vyake vyote. Ameongeza kuwa: Sekretarieti ya baraza hilo inapaswa kutekeleza vizuri mno wajibu wake mkuu wa kuandaa maamuzi kwa namna ambavyo misimamo inayochukuliwa na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa iwe inachukuliwa kutokana na kuwa na mtazamo sahihi unaozingatia pande zote za neno usalama.
Vile vile amegusia kazi tofauti za sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na kusema kuwa: Suala la sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa ya kuweza kutekeleza kwa njia sahihi majukumu yake, linategemea kutawala kikamilifu anga ya asilimia mia moja ya kimapinduzi katika chombo hicho kwani kama misimamo inayokinzana na misimamo ya Mapinduzi ya Kiislamu itajipenyeza kwenye suala la uandaaji wa maamuzi katika sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, basi matunda yanayotakiwa hayataweza kupatikana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, misimamo ya kimapinduzi si fikra chapwa zisizo na lolote ndani yake na kuongeza kuwa: Misimamo ya kimapinduzi ni jambo la kweli lililo wazi na wadhiha kikamilifu na ni lenye msingi wake katika matamshi ya Imam (Khomeini) Rahimahullah.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia jinsi baadhi ya watu wanavyojaribu kubadilisha njia na mipaka ya asili na ya wazi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Imam - Mwenyezi Mungu amrehemu - ndiye dhihirisho la Mapinduzi ya Kiislamu na kwa msingi huo, matamshi yake yaliyokusanywa kwenye jalada kadhaa za kitabu cha "Misingi ya Mapinduzi" ndiyo marejeo mipaka hiyo.
Amesema, mambo yaliyokaririwa na Imam Khomeini (quddisa sirruh) katika matamshi yake hayo ni mipaka na mistari mikuu na ndiyo misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Kwa mujibu wa matamshi ya Imam - Rahimahullah -suala la "wananchi," "uhuru wa nchi," "kushikamana na dini na misingi ya Uislamu," "kupambana na uistikbari na ubeberu," "kadhia ya Palestina," "suala la maisha ya wananchi," "kuwazingatia wanyonge na kutokomeza umaskini" ndiyo misingi mikuu ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yanapokusanyika pamoja yanajenga muundo mkuu na halisi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, maamuzi ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa yanapaswa kuwa ndani ya fremu ya misingi mikuu ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Inabidi fikra sahihi na halisi ya kimapinduzi na "kihizbullah" itawale kikamilifu ndani ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na sekretarieti ya baraza hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Tangu mwanzoni kabisa mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kuna baadhi ya watu walikuwa hawakubaliani na fikra ya kimapinduzi, na kwamba baadhi yao, licha ya kwamba walikuwemo ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, lakini walikuwa hawaitakidi kuwa kuna haja ya kupambana na ubeberu na uistikbari; sasa inabidi kusimama imara kukabiliana na watu wenye misimamo kama hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, mapambano yamekuwepo katika kipindi chote cha miaka 37 iliyopita, hata hivyo lakini amesema: Tab'an, leo hii mapambano hayo yamekuwa nyeti mno na magumu zaidi kutokana na mbinu mpya na tata mno zinazotumiwa na adui kama vile kutumia mitandao ya kijamii na kujipenyeza katika masuala ya kiutamaduni, kiitikadi, kijamii na mambo mengine yaliyo dhidi ya amani na usalama wa taifa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia jinsi mbinu mpya zinazotumiwa na maadui zinavyoathiri pole pole na kimya kimya misingi ya ndani kabisa ya usalama katika jamii na kuongeza kuwa: Baraza Kuu la Usalama wa Taifa lina wajibu wa kufuatilia masuala yote hayo katika sekta tofauti na hatimaye kuyachukulia maamuzi na ndio maana sekretarieti ya baraza hilo inapaswa kuwa na tafakuri sahihi na kufanya juhudi zisizochoka na za kiutaalamu zilizosimama juu ya msingi wa fikra ya kimapinduzi na baadaye kuandaa maamuzi sahihi ya kuweza kukabiliana vilivyo na mbinu tata na mpya za adui wa usalama na amani ya taifa.
Mwishoni mwa hotuba yake, amemtaja Admeli Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kuwa ni miongoni mwa kumbukumbu nzuri sana za kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu (Vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) na ameishukuru sekretarieti ya baraza hilo kutokana na jitihada na kazi zake nzuri za kuandaa ripoti muhimu na za wakati mwafaka kuhusiana na maudhui tofauti.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Bw. Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa ametoa ripoti fupi kuhusu kazi za sekretarieti ya baraza hilo na kusema kuwa, kupanga sera, kuratibu na kusimamia ndiyo majukumu makuu ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa nchini. Ameongeza kuwa, sekretarieti ya baraza hiyo ina jukumu la kuunga mkono na kusaidia kiutaalamu maamuzi wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na kwamba nafasi hiyo daima inapaswa ioane na iwe katika mkondo wa siasa kuu za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

 

 
< Nyuma   Mbele >

^