Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wananchi wa Najafabad Chapa
24/02/2016
People of Najaf Abad meeting with the LeaderAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumatano) ameonana na maelfu ya wananchi wenye shauku kubwa wa mji wa Najafabad (wa mkoani Isfahan, katikati mwa Iran) na huku akitoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na maneno "misimamo ya wastani na misimamo mikali" na kuwataka wananchi wote hususan viongozi na wanasiasa kuwa macho mbele ya njama na hila za adui mwenye nia ya kuzusha kambi mbili bandia na kuharibu anga ya uchaguzi nchini amesema kuwa, uchaguzi ni fursa ya kujiimarisha kitaifa na kudhihirisha uaminifu na kusimama kidete kitaifa na uungaji mkono wa heshima na uhuru wa nchi na kusisitiza kuwa: Watu wote wanaopenda kuiona Iran ya Kiislamu inazidi kuwa na heshima wanapaswa kushiriki katika uchaguzi wa siku ya Ijumaa na kwamba tarehe 26 Februari, dunia itaona namna wananchi wa Iran wanavyoshiriki kwa hamasa na shauku kubwa kwenye masanduku ya kupigia kura.
Ayatullah Udhma Khamenei amezitukuza siku hizi za kukumbuka kufa shahidi Bibi Fatimatuz Zahra Salamullahi Alayha na kuashiria chaguzi mbili muhimu za Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na Baraza la Wanavyuoni Wataalamu zinazotarajiwa kufanyika keshokutwa Ijumaa na kuongeza kuwa: Umuhimu wa uchaguzi wenyewe nchini hauishii tu kwenye kupiga kura, bali uchaguzi nchini Iran una maana ya kuweka kifua mbele na kutanua misuli taifa la Iran mbele ya adui baada ya mashinikizo na vikwazo vya kila aina vya kidhalimu na propaganda za kikhabithi na kiafiriti za adui.
Amelitaja suala la kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi kutayaongezea tena haiba na heshima Mapinduzi ya Kiislamu duniani na kuongeza kuwa: Mbali na kuonesha nguvu, nia ya kweli na kutoyumba kitaifa, uchaguzi unaonesha pia uaminifu na ushujaa wa taifa kubwa katika medani ya kupambana na malengo machafu ya maadui.
Baada ya kubainisha umuhimu wa kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi watu wa matabaka mbali mbali waliotimiza masharti ya kupiga kura, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hila na njama za adui katika kipindi cha miaka 37 iliyopita katika vipindi tofauti vya uchaguzi dhidi ya taifa la Iran na kusema: "Kuukana na kudai uchaguzi wa Iran ni wa uogo," "kuendesha njama za kuwafanya wananchi wa Iran wasijitokeze kwa wingi kwenye uchaguzi" na "kueneza propaganda za kuonesha kuwa hakuna faida kwa wananchi kujitokeza kwenye uchaguzi kwa madai ya eti matokeo ya uchaguzi yameshajulikana tangu zamani" ni miongoni mwa propaganda chafu za watu wanaolitakia mabaya taifa hili, ili kupunguza hamu ya wananchi ya kushiriki kwenye uchaguzi na njama ambazo zimekuwepo katika miaka yote iliyopita, bali katika baadhi ya wakati viongozi wa Marekani wamewahi kutamka waziwazi kuwa wananchi wa Iran wasishiriki katika uchaguzi.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa Wamarekani hivi sasa na kutokana na uzoefu waliopata wameelewa vyema kuwa, kila wanapochukua misimamo ya wazi hupata majibu yaliyo kinyume kabisa na matarajio yao na kuongeza kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndio maana Wamarekani hivi sasa wamenyamaza kimya kuhusu uchaguzi wa mara hii lakini vibaraka na vitimbakwiri vyao wanatumia mbinu tofauti kuendesha njama zao.
Ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu njama hizi mpya za Wamarekani kwa kusema: Watu wasiolitakia kheri taifa la Iran wanafanya njama za kuzusha kambi mbili bandia kuhusu uchaguzi wa mara hii ili kujaribu kuonesha kuwa wananchi wa Iran wamegawanyika na hawako kitu kimoja.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia kuwa, tabia ya uchaguzi ni mithili ya shindano ambalo linaambatana na hamasa na shauku yenye mshindi na mshindwa na kusisitiza kuwa: Kushinda na kushindwa katika uchaguzi, hakuna maana ya taifa kuwa na kambi mbili na wala kuwa na mirengo mwili na wala kuwepo uadui na chuki baina ya wananchi, na kwamba kupandikiza madai kuwa wananchi wa Iran wamegawanyika katika kambi mbili ni uongo ulio wazi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, kambi mbili za kweli zilizopo nchini Iran ni kambi mbili baina ya wafuasi na wapenzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na misingi ya Imam (Khomeini - quddisa sirruh) kwa upande mmoja na kambi ya kiistikbari na watu wenye fikra kama zao kwa upande wa pili. Amesisitiza kuwa: Tab'an katika kambi hizo mbili, kambi ya taifa la Iran ni kambi ya kimapinduzi, ni ya watu wanaoyapenda Mapinduzi ya Kiislamu na walio watiifu kwa Imam (quddisa sirruh) na walioshikamana na fikra na misingi yake.
Amesema: Kituo kikuu cha kuzusha kambi hizo mbili bandia, kiko nje ya Iran lakini inasikitisha kuona kuwa baadhi ya wakati ndani ya Iran pia kunasikika sauti za baadhi ya watu zikiunga mkono njama hizo za maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mfano wa kambi hizo mbili za uongo ambazo adui anajaribu kuzihusisha na uchaguzi wa mara hii wa nchini Iran ni kudai kuweko "Bunge la Serikali" na "Bunge lililo dhidi ya Serikali" na kuongeza kuwa: Waliopanga kambi hizo bandia wanajaribu kuonesha kuwa, baadhi ya wananchi wa Iran wanaunga mkono Bunge la Serikali na wengine wanapinga bunge la Serikali wakati ambapo uhakika wa mambo ni kuwa taifa la Iran halina haja na Bunge la Serikali na wala Bunge lisilo la Serikali.
Ayatullah Udhma Khamenei amefafanua zaidi kwa kusema: Taifa la Iran linataka bunge la watu wenye dini, watu wema, watu mashujaa na watu wasioyumba na wanaosimama imara katika kukabiliana na madola yaliyojaa tamaa ya kibeberu ambayo yanapenda kujikumbizia kila kitu upande wao. Wanataka bunge la watu watakaolinda heshima na uhuru wa taifa lao, wenye mapenzi ya kweli kwa maendeleo ya nchi, wanaoamini harakati ya kielimu na vipaji vya vijana na wenye imani na uchumi unaojiimarisha kwa kutumia nguvu za ndani, wanaojua vizuri vilio vya wananchi na wenye nia ya kweli ya kutatua matatizo ya wananchi. Watu ambao wanatekeleza vizuri majukumu yao ya kisheria bila ya kuogopeshwa na Marekani.
Ameongeza kuwa: Wananchi wa matabaka yote wa Iran wanataka bunge lenye watu wa aina hiyo na si bunge linalomuunga mkono mtu fulani au watu fulani tu.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia njama za Marekani baada ya makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 maarufu kwa jina la makubaliano ya JCPOA na kusisitiza kuwa: Baada ya JCPOA Wamarekani wameanzisha njama nyingine mpya dhidi ya Iran na eneo hili (la Mashariki ya Kati) na hadi hivi sasa wanaendelea kutekeleza njama zao hizo kwani wanajua vyema ni nchi gani imesimama imara kukabiliana na malengo yao maovu katika eneo hili.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, moja ya mbinu zinazotumiwa na Wamarekani kutekeleza njama zao hizo ni kujipenyeza na kujaribu kuwa na ushawishi ndani ya Iran na kuongeza kuwa: Tangu suala la ushawishi na ulazima wa kuwa macho katika kukabiliana na ushawishi huo lilipoanza kuzungumzwa, kuna baadhi ya watu humu ndani wamehamaki na wanasema, kwa nini muda wote linazungumziwa suala la ushawishi na kujipenyeza adui; lakini kwa kweli kuhamaki watu hao si jambo lililozuka vivi hivi bila ya sababu yoyote.
Amesisitiza kuwa: Suala la ushawishi na kujipenyeza ni jambo lililopo na halina shaka, lakini baadhi ya wakati mtu aliyeathiriwa na jambo hilo huwa hajijui yuko katika njia gani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria matamshi ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) ambaye daima alikuwa macho na mwenye uzoefu aliyesema kuwa baadhi ya wakati matamshi ya adui yanafikishwa kwa wananchi kupitia wasita na watu kadhaa wa pembeni na kuongeza kuwa: Huyu mtu aliyelengwa, huwa hakupewa pesa na wala hakujifunga kwenye ahadi yoyote, lakini utamuona anakariri maneno ya adui bila ya yeye mwenyewe kujua lakini kwa hakika kufanya kwake hivyo huwa kunaandaa mazingira ya kujipenyeza maadui bila ya yeye mwenye kutambua anachokifanya.
Ayatullah Khamenei ametoa mifano kadhaa ya ushawishi wa aina hiyo ambao baadhi ya wakati watu waliathiriwa nao huwa huwa wanafanya mambo bila ya wao wenyewe kujua kwa kusema: Katika miaka ya huko nyuma, kwenye vikao vya wazi vya Bunge, mbunge mmoja alithubutu kuutuhumu mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuwa eti unasema uongo, alisema hayo bila ya kujua kuwa anaakisi maneno ya adui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mfano mwengine akisema: Katika kipindi ambacho timu ya nchi yetu ya mazungumzo ya nyuklia ilipokuwa imo katika mazungumzo magumu na kwa hakika katika mapambano na upande wa pili, ambapo wakati huo mheshimiwa Rais wa hivi sasa (wa Iran) ndiye aliyekuwa mkuu wa timu hiyo ya mazungumzo ya nyuklia, kuna baadhi ya watu walipeleka muswada wa dharura bungeni ambao uliunga mkono upande wa pili uliokuwa unazungumza nasi na mheshimiwa Rais wetu wa hivi sasa akalilalamikia suala hilo na kusema kuwa, muswada huo ulikuwa ni kwa manufaa ya adui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka wananchi wote na hususan viongozi na wanasiasa kuwa macho kikweli kweli mbele ya ushawishi na wasiruhusu kujipenyeza adui na kusisitiza kuwa: Jambo la lazima katika kuchukua tahadhari huko ni kwamba, kama adui atajitokeza na kumuunga mkono au kumsifia mtu yeyote humu nchini kwa lengo la kuzusha mizozo na mifarakano baina ya wananchi, bila ya kuchelewa mtu huyo aliyesifiwa na adui amkanushe haraka adui na achukue msimamo wa wazi dhidi yake.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia pia maneno ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) aliposema kuwa "Ukiona adui anakusifu basi tilia shaka vitendo na mambo unayofanya" na kuongeza kuwa: Matamshi hayo ndiyo nguzo na kioo cha utekelezaji wa mambo katika Mapinduzi ya Kiislamu, hivyo kuna wajibu wa kila mtu kuchukua msimamo wa haraka wa kuwakana mabeberu mara wanapomsifu na asikumbwe na mghafala katika jambo hilo.
Amesisitiza kuwa, jambo la lazina la kuweza kuiendesha nchi yenye upana na ukubwa wote huu na kutekeleza matakwa ya wananchi waungwa na wenye adhama kama hawa, ni kuwa makini, kukaa macho wazi na kuwa na nia na azma ya kweli ya kupambana na adui.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka viongozi na wanasiasa nchini kujiepusha kutumia misamiati ya kisiasa ya maadui hususan kutumia maneno kama misimamo mikali na misimamo ya wastani na kuongeza kuwa: Tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, watu wanaolitakia mabaya taifa hili wamekuwa wakitumia maneno hayo na lengo lao kuhusu watu wenye misimamo mikali ni wale watu ambao wanashikamana na Mapinduzi ya Kiislamu na fikra na misingi ya Imam (Khomeini - quddisa sirruh) na ambao kila kukicha wanashikamana zaidi na misingi hiyo. Na lengo la maadui hao kuhusu watu wenye misimamo ya wastani ni wale watu ambao wamesalimu amri mbele ya waistikbari na ambao wako tayari kuburuzwa kwenye mapatano.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesema: Watu wanaotumia istilahi hizo ndani ya Iran wanapaswa watalii na wasome kwa kina mafundisho ya Uislamu kwani katika Uislamu hakuna mgawanyo wa aina hiyo na kwamba maana ya misimamo ya kati na ya wastani katika Uislamu ni njia iliyonyooka, si njia nyingine. Hivyo katika mkabala wa njia ya wastani yaani njia iliyonyooka hakuna njia ya misimamo mikali bali kuna njia ya wapotofu wanaokwenda kinyume na njia hiyo.
Ameongeza kuwa: Kuna uwezekano katika njia hiyo iliyonyooka baadhi ya watu wakawa wanakwenda kwa kasi zaidi na wengine wakawa wanakwenda kwa kasi ndogo, na hilo ni jambo ambalo halina tatizo lolote kwani wote wamo kwenye njia hiyo hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Katika msamiati wa kisiasa wa mabeberu, kundi la Daesh nalo ni katika watu wenye misimamo mikali wakati kundi hilo linakwenda kinyume kabisa na mafundisho ya Uislamu na ya Qur'ani na halimo kabisa katika njia iliyonyooka.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa muhtasari wa matamshi yake hadi kufikia hapo kwa kusema: Watu walioko nje ya mipaka ya nchi yetu wanapotumia neno misimamo mikali, wanakusudia mirengo ya watu walioshikamana na dini walio waaminifu na walio watiifu kikamilifu mbele ya Mapinduzi ya Kiislamu, hivyo humu ndani ya nchi inabidi watu wawe makini wasikariri na kurudia neno hilo kwani kufanya hivyo ni kutumikia lengo la adui.
Amegusia pia namna Wamarekani wanavyokiri kuwa, ndani ya Iran hakuna watu wenye misimamo ya wastani katika kukabiliana na ubeberu wao na kuongeza kuwa: Taifa lote la Iran linayapenda Mapinduzi ya Kiislamu na limesimama imara kuyalinda mapinduzi yake hayo, tab'an kuna uwezekano baadhi ya wakati wakatokezea watu wakakosea au wakatetereka, lakini hakuna mwananchi yeyote wa Iran aliyeko tayari kuburuzwa na kugeuzwa nchi yao kuwa kibaraka wa mabeberu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa miongozo pia kuhusu namna ya kuchagua watu wanaofaa zaidi kuingia Bungeni na katika Baraza la Wanavyuoni Wataalamu kwa kuwaambia wananchi kwamba: Matokeo ya chaguo lenu lolote lile katika uchaguzi huu, iwe ni chaguo zuri au baya, yatarejea kwenu nyinyi wenyewe, hivyo jitahidini kuchagua watu bora zaidi katika uchaguzi huu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, kupata radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu au kutopata radhi Zake, ni matokeo mengine ya kuzingatiwa katika kuchagua wagombea na kuongeza kuwa: Inabidi ihakikishwe kuwa kunachaguliwa wagombea kwa uangalifu mkubwa, kwa kuangalia mbali na kwa kumjua vyema mtu anayepigiwa kura.
Aidha amewasisitizia wananchi akiwaambia: Katika kuwapigia kura wagombea wa ubunge katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu inabidi mzingatie kushikamana na dini, utekelezaji wa ahadi, uaminifu kwa Mapinduzi ya Kiislamu, kusimama imara katika njia ya Mapinduzi ya Kiislamu, kutokuwa na woga katika kupambana na adui, kuwa na nia na azma ya kweli na ushujaa wa kila mgombea mnayempigia kura.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kama kutakuwa na mgombea humjui, usiseme simpi kura yangu kwa sababu tu simjui, bali fanya uchunguzi wa kugundua na kupata yakini kuhusu kushikamana kwake na dini, uaminifu wake katika kutekeleza ahadi na namna alivyo na busuri na mtazamo wa mbali.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, njia ya malengo, majukumu na masuuliya iko wazi katika suala hili na kuongeza kuwa: Kama kazi hii kubwa itatekelezwa vizuri, bila ya shaka yoyote Mwenyezi Mungu ataleta msaada Wake na matokeo yoyote yale ya uchaguzi huo yatakuwa ni kwa faida ya nchi.
Vile vile amesema: Mimi nina yakini kwamba pamoja na kuwepo njama zote hizi za watu wanaolitakia mabaya taifa letu, lakini Mwenyezi Mungu ataufanya ushindi wa mwisho kuwa wa taifa la Iran na kwa uwezo, tawfiki na baraka za Mwenyezi Mungu, adui hatoweza kutoa pigo kwa Mapinduzi na mfumo huu wa Jamhuri ya Kiislamu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewashukuru wananchi wa Najafbad kutokana na imani, uaminifu, ukweli na kusimama kwao imara katika njia ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusema kuwa: Katika kipindi cha mwamko wa Kiislamu wananchi wa Najafbad walionesha kivitendo hamasa, hisia na welewa wao wa hali ya juu katika kuunga mkono mapambano ya wakati huo, na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia, katika vipindi tofauti na hususan wakati wa vita vya kujihami kutakatifu (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran), wananchi hao kwa mara nyingine walionesha kivitendo uungwana, ghera, umakini na kusimama kwao kidete katika kuyalinda Mapinduzi hayo matukufu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Hasanati, Imam wa Sala ya Ijumaa ya mji wa Najafabad amegusia uungwana na hamasa kubwa ya watu wa mji huo ambao wametoa mashahidi wengi katika njia ya haki katika kipindi cha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na wakati wa vita vya kujihami kutakatifu na kutoa zaidi ya mashahidi 2500 katika njia hiyo tukufu na kusema kuwa: Wananchi waaminifu wa Najafabad, wameshikamana na ahadi na agano lao kwa Uislamu, Qur'ani, Imam (quddisa sirruh) na kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na watalinda ahadi na agano lao hilo hadi tone lao la mwisho la damu.
 
< Nyuma   Mbele >

^