Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kuteuliwa Hujjatul Islam Raisi kuwa Mfawidhi wa Haram ya Imam Ridha AS Chapa
07/03/2016
Ayatullah Udhma Sayyid Aki Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemteua Hujjatul Islam Sayyid Ibrahim Raisi kuwa mfawidhi wa Haram tukufu ya Imam Ridha Alayhis Salaam.
Matini kamili ya hukumu ya uteuzi huo ni kama ifuatavyo:

Bismillahir Rahmanir Rahim
Janabi Hujjatul Islam Alhaj Sayyid Ibrahim Raisi (damat barakatuh)
Hivi sasa ambapo janabi Hujjatul Islam Walmuslimin Bw Tabasi (Mwenyezi Mungu amrehemu) ametangulia mbele ya Haki baada ya kupitisha miaka mingi ya kufanya juhudi za kiikhlasi na za ufanisi katika kumtumikia Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenye Haram tukufu na iliyojaa nuru ya Imam Ali bni Musa ar Ridha (ziwe juu yake maelfu na rehema na baraka za Mwenyezi Mungu), na kuzikwa pembeni mwa mtukufu huyo, ninatumia fursa hii kukuteua kuwa mfawidhi wa Haram iliyojaa nuru na tukufu ya Imam Ridha AS kwa kuzingatia kuwa wewe pia chimbuko lako ni katika eneo hilo lililojaa baraka na una sifa za utendaji bora na uaminifu kama ambavyo pia una utambuzi na weledi wa kutosha katika kusimamia mambo makubwa kama haya. Sambamba na uteuzi huu ninapenda kuitumia fursa hii kukumbusha mambo yafuatayo:
1 - Kupata fursa ya kutumikia Haram tukufu ya Imam Ridha AS ni fakhari kubwa ya kimaanawi na ni fursa ya kuweza kustafidi vizuri mno na hali ya kimaanawi ya eneo hilo tukufu na kuzidi kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kupitia utukufu wa Wilaya na nuru hiyo iliyotanda kila sehemu. Basi itumie vizuri sana fursa hii ya kipekee na hakikisha unaelekeza juhudi na nguvu zako zote kwenye jambo hilo na rasilimali ya kimaanawi ambayo Alhamdulillah unayo ya kutosha, iongeze zaidi kupitia fursa hiyo.
2 - Kuwahudumia vizuri wafanya ziara katika Haram hiyo tukufu hususan wanyonge na wahitaji ifanye kuwa ajenda kuu ya kazi zako.
3 - Kuwatumikia majirani wa Haram hiyo tukufu hususan watu maskini na wanyonge ni jukumu jingine ambalo linastahiki kulitilia hima na kulipa umuhimu mkubwa.
4 - Haram ya Imam Ridha AS ina uwezo mkubwa na adhimu wa kiutamaduni ambao unaweza kutoa athari katika anga ya nchi nzima na duniani kote kiujumla; hivyo ni jambo la busara kusaidiana na weledi wa masuala ya kiutamaduni katika kuutumia vizuri sana uwezo huo wa kipekee kwa ajili ya kueneza mafundisho ya Qur'ani Tukufu na mafundisho ya Ahlul Bayt Alayhimus Salaam.
5 - Eneo la Haram tukufu ya Imam Ridha AS na majengo yake ni hazina ya kipekee ya usanifu majengo wa Kiislamu na ni eneo lenye mvuto na ubora wa kielimu na kisanii wenye maana pana wa taifa la Iran; hivyo unapaswa kulihifadhi na kulilinda vizuri eneo hilo la kumbukumbu adhimu ambalo katika kipindi cha marhum Sheikh Tabasi ubora wake umeongezeka karibu mara kumi zaidi ya huko nyuma, na hilo ni katika majukumu makubwa yanayostahiki kuzingatiwa.
6 - Kulindwa vizuri vitu vinavyowekwa wakfu na kuvitumia kwa njia bora kabisa tena kwenye mambo yake yenyewe - suala ambalo marhum alikuwa akilipa umuhimu mkubwa sana - hususan katika kuwasaidia maskini katika maeneo vilipo vitu hivyo vilivyowekwa wakfu, nalo pia ni katika majukumu makubwa ambayo inabidi yatekelezwe kwa mujibu wa unavyosema muongozo wa kusimama na kuendesha vitu hivyo vilivyowekwa wakfu.
7 - Kuunda taasisi za kiuchumi na za kutoa huduma katika Haram tukufu ya Imam Ridha AS na kuzitabikisha na sheria ni jambo jingine muhimu ambalo linapaswa litiliwe hima muda wote na kutolidharau hata kidogo.
Kwa mara nyingine ninatumia fursa hii kukupa nasaha kwamba tumia vizuri sana fursa hii na stafidi vilivyo na nuru tukufu ya eneo hilo la kimaanawi suala ambalo bila ya shaka yoyote litakusaidia sana katika kufanikisha majukumu yako na hasa zizingatie nasaha za pili na za tatu katika hili. Ninamuomba Mwenyezi Mungu ammiminie rehema, maghufira na radhi Zake mfawidhi wa Haram hiyo tukufu aliyetangulia mbele ya haki ambaye amefanya kazi kubwa kwa ikhlasi katika kuendesha taasisi hiyo kubwa sana na kuiletea maendeleo makubwa. Ninamuomba pia Mwenyezi Mungu Mtukufu akupe taufiki wewe na watumishi wote wa Haram hiyo takatifu, nikikushukuruni nyote kwa jitihada zenu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullah
Sayyid Ali Khamenei
17 Isfand 1394
(7 Machi, 2016).

 
< Nyuma   Mbele >

^