Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wasoma Kasida za Ahlul Bait AS Chapa
30/03/2016
Leader meets with PanegyristsAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatano) ameonana na majimui ya wasoma kasida za Ahlul Bait AS kwa mnasaba wa maulidi ya Bibi Fatimatuz Zahra Salamullahi Alayha binti mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW na kusema kuwa, kazi ya kubainisha masuala muhimu katika maisha ya Ahlul Bait Alayhimus Salaam inapelekea watu wazidi kuzingatia na kupiga mbizi zaidi katika sira na maisha ya watukufu hao na huku akiashiria namna maadui wanavyotumia kwa sura ya kuendelea mbinu na nyenzo zote walizo nazo kwa ajili ya kukabiliana na taifa la Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Katika kipindi hiki tata sana cha sasa hivi na kijacho, hakuna budi kutumiwa nyenzo zote za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiulinzi kwa ajili ya kutia nguvu nafasi ya Iran ulimwenguni.
Ametumia fursa hiyo kutoa mkono wa kheri na fanaka kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Swiddiqatul Kubra, Bibi Fatimatuz Zahra Salamullahi Alayha na kusema kwamba, kuwa na kipaji cha kusoma kasida za kuwasifu Ahlul Bait AS ni fakhari kubwa.
Ameongeza kuwa, miongoni mwa sifa za kipekee za jamii ya Kishia ni suala hili la kusoma kasida za Ahlul Bait kwa sauti nzuri za kuvutia na kwa tungo zenye maana pana za kina na kujikita vizuri jambo hilo kati ya watu wote na kusema kwamba, kuna haja kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na watafiti walifanyie kazi suala la kuimarishwa kielimu na kuenezwa zaidi kiutaalamu suala hilo.
Ayatullah Khamenei amesema, suala la kuelewa na kubainisha vile inavyotakiwa hasa nafasi adhimu iliyojaa nuru ya Bibi Fatimatuz Zahra Salamullahi Alayha ni jambo lisilowezekana kabisa na kuongeza kuwa: Pamoja na hali kuwa hivyo, lakini sira na maisha ya mtukufu huyo yamejaa nukta nzuri za kuweza kuzibainisha na kupata mafunzo na somo la maana ndani yake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba, kuwa kwake binti wa Bwana Mtume Muhammad SAW na mke wa walii wa Mwenyezi Mungu ni katika mambo yanayoonesha utukufu, nafasi aali na adhama ya Swidiqatul Kubra Salamullahi Alayha na kuongeza kuwa: Hatua ya bibi huyo mtukufu ya kulea mabwana wawili wa vijana wa peponi, usafi na utoharifu wake wa kiroho na batini ya maisha yake, uchaji Mungu na usafi wake wa moyo ni miongoni mwa sifa za kipekee za mtukufu huyo ambazo watu binafsi na jamii nzima ya wanadamu inaweza kujifunza na kufaidika nazo katika maisha kupitia taqwa na kujichunga daima na katika hatua zote za maisha ya kila siku.
Vile vile amewausia washairi na wasoma kasida za Ahlul Bait AS kushikamana vilivyo na nukta na mafundisho hayo matukufu na kuyaingiza kwenye tungo na kasida zao na kusisitiza kuwa: Kutaja cheo kitukufu cha kimaanawi huleta mapenzi na mwanga moyoni lakini hilo halitoshi bali inabidi mimbari zitumiwe vizuri kwa ajili ya kutoa darsa za maana zenye faida za kivitendo kutoka katika maisha ya Maimamu watoharifu Alayhimus Salaam na kuandaa uwanja wa kuimarika imani kwa watukufu hao na kutekelezwa kivitendo mafundisho ya Ahlul Bait AS katika jamii.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema ni jambo la dharura kuzingatia masuala ya kila leo katika tungo na kasida za Ahlul Bait AS na kusisitiza kuwa: Mfumo wa kibeberu uliosimama juu ya msingi wa kutumia mabavu ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijeshi, haudharau hata fursa moja unayoipata kwa ajili ya kuliletea madhara taifa la Iran, na inapasa kuwa macho wakati wote kuhusu uhakika huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia namna maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu wanavyotumia mbinu zote za zamani na za kisasa kwa ajili ya kuifanyia uadui Iran na kusisitiza kuwa: Maadui wanatumia mbinu zote, wanatumia mazungumzo, mabadilishano ya kibiashara, vikwazo, vitisho vya kijeshi na kila wenzo wanaoupata ili kufanikisha malengo yao, hivyo taifa la Iran nalo linapaswa kujiimarisha vizuri katika nyuga zote ili liweze kujihami na kukabiliana vilivyo na njama hizo za maadui.
Vile vile amesema, uwezo wa kijeshi ndio nguzo kuu inayotumia na waistikbari kwa ajili ya kulifanyia ubeberu taifa la Iran na kuulizwa swali moja la kimsingi akisema: Je, iwapo katika mazingira haya ya sheria za msituni zinazotawala duniani leo; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatosheka tu na kufanya mazungumzo na kuwa na mabadilishano ya kibiashara na hata ya kielimu na kiteknolojia na kusahau kujiimarisha kijeshi, hata nchi ndogo kabisa duniani hazitapata uthubutu wa kutoa vitisho kwa taifa la Iran?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewalaumu vikali watu ambao wanaona kuwa mustakbali wa taifa la Iran unaishia tu kwenye mazungumzo na si kwa kuwa na nguvu za makombora na kusema kuwa, kama wanaotoa matamshi hayo wanayatoa kwa kutojua, hilo si neno, lakini kama wanayatoa kwa kujua, basi watambue kuwa huo ni usaliti. Amesema, mustakbali wa taifa la Iran unategemea mambo yote, vinginevyo, haki ya taifa la Iran italiwa na kupotea kirahisi sana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, majaribio ya makomboa yaliyofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH hivi karibuni kwa umahiri na utaalamu wa hali ya juu sana yameyafurahisha mataifa ambayo yanateswa na kunyanyaswa na Marekani na utawala wa Kizayuni na hayawezi kufanya lolote kukabiliana na mbeberu hao.
Amesema, maadui muda wote wanafanya juhudi za kuimarisha uwezo wao wa kijeshi na wa makombora, sasa vipi sisi tunafikia hadi ya kusema kuwa mustakbali wa makombora umepitwa na wakati?
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, matamshi hayo yanafanana na matamshi ya baadhi ya watu waliokuwemo kwenye serikali ya mpito ya mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu ambao walikuwa wakisema ndege za kivita za F-14 zilizonunuliwa kutoka Marekani tuzirejeshe kwani hazina faida yoyote kwetu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Wakati huo tulisimama imara na tukafichua njama zilizokuwa nyuma ya pazia na muda mrefu haukupita ila Saddam aliivamia Iran na hapo tukaona ni kiasi gani zana hizo za kijeshi zilikuwa muhimu na zenye manufaa kwetu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena amesema kuwa anaunga mkono kutumika njia za kidiplomasia na mazungumzo ya kisiasa isipokuwa katika baadhi ya mambo tu na kuongeza kuwa: Watu wasifanye propaganda za kuonesha kuwa tunapinga mazungumzo, bali tunachosema sisi ni kuwa tuingie kwenye mazungumzo tukiwa macho na tukiwa na nguvu ili tusije tukalaghaiwa.
Amma kuhusiana na uchumi wa kimuqawama na usiotetereka amesema: Kukariri mara kwa mara matamshi na nara na kaulimbiu hizo kwa hizo kila siku kunachosha hivyo hivi sasa ni wakati wa kuchukuliwa hatua na vitendo kwa ajili ya kuimarisha hali ya kiuchumi na hali ya maisha ya watu nchini.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametumia fursa hiyo kutoa nasaha kwa wasoma kasida za Ahlul Bait AS na wanaotaja sifa za watukufu hao akiwahimiza wakabiliane na njama za maadui wanaojaribu kudhoofisha imani za vijana na kusisitiza kuwa jambo hilo ni muhimu sana kwao. Amesema, kuna njama zinafanyika za kudhoofisha imani za vijana kwa Uislamu na kujaribu kuonesha kuwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hauna faida na kufikia hadi njama hizo kujaribu kuonesha kuwa kuendelea kuwepo Jamhuri ya Kiislamu ni jambo lisiloyumkinika kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema: Tab'an miaka 37 sasa imepita na siku zote maadui wanaendelea kufanya njama mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kupiga domo la kudai kuwa ni jambo lisiloyumkinika kuendelea kuwepo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini mfumo huu wa utawala uliochaguliwa na wananchi wenyewe wa Iran hivi sasa umestawi na umetoka katika hali ya mche mchanga wa awali ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuwa mti imara ulionawiri vizuri sana na uhakika huo unathibitisha kuwa vipaji vya watu wetu vimeongezeka, vimeimarika na kuwa na nguvu ndani ya dhati ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na vinazidi kuimarika na kustawi kadiri siku zinavyosonga mbele.
Kiongozi Muadhamu Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, upeo wa mustakbali wa Iran unang'ara na uko wazi kabisa na ametoa nasaha kwa wasomaji wa kasida za Ahlul Bait AS akiwataka watumie vizuri vipaji vyao kutunga tungo zenye maana pana na kuendesha sanaa zao kwa umahiri wa hali ya juu ili waweze kuwageuza wasikilizaji wao kuwa watu wenye matumaini, wachapakazi na watu wa maana katika jamii. Aidha amewaambia wasomaji kasida za Ahlul Bait AS kwamba jukumu lao kuu ni kuwaongoza watu njia sahihi na kuleta mwamko, busuri na muono wa mbali katika jamii.
 
< Nyuma   Mbele >

^