Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana naBaraza Kuu la "Kituo cha Kigezo cha Kiislamu Kiirani cha Maendeleo" Chapa
25/04/2016
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo (Jumatatu) ameonana na wajumbe wa Baraza Kuu la Kituo cha Kigezo cha Kiislamu - Kiirani cha Maendeleo na kusema kuwa lengo la Mapinduzi ya Kiislamu ni kuleta na kufanikisha ustaarabu wa Kiislamu. Vile vile ameashiria misingi ghalati na mibovu ya vigezo vya ustawi vya kimataifa na udharura wa kutolewa kigezo kipya cha Kiislamu - Kiirani na kuongeza kuwa, "kazi ya kijihadi na kimapinduzi," "kustafidi vizuri na uwezo tajiri na makini wa vyanzo vya Kiislamu na vyuo vikuu vya kidini," "kuwa na nguvu za kielimu" na "kuyafanya mambo hayo yaenee na kuwa mjadala mkuu katika jamii" ni katika mambo ya lazima ya kuandaa na kutunga "Kigezo cha Kiislamu - Kiirani cha Maendeleo."
Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha pia hatua tano za kufanikisha malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na uhusiano wa hatua hizo na kigezo hicho cha maendeleo na kusema kuwa: Hatua ya kwanza katika mchakato huo ni kufikia ushindi Mapinduzi ya Kiislamu, na baada ya hapo kuundwa mfumo wa Kiislamu tena bila ya kuchelewa, ambapo suala hili la kuunda mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa hakika lilionesha kipaji kikubwa alichokuwa nacho Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja hatua ya tatu katika mchakato huo kuwa ni hii iliyopo na inayoendelea hivi sasa yaani kuunda serikali ya Kiislamu kwa maana ya kuunda serikali ambayo imetimiza kikamilifu vigezo na vielelezo vyote vya Kiislamu na kuongeza kuwa: Hatua ya nne ya kuunda jamii ya Kiislamu haitaweza kushuhudiwa hadi pale hatua hii ya kuwa na serikali kamili ya Kiislamu itakapofanikishwa kikamilifu, na kama hilo halitafikiwa, basi suala la mtindo wa maisha ya Kiislamu nalo litabakia kuwa maneno na gumzo tu katika jamii.
Amesema, hatua ya tano na ya mwisho ya mchakato huu wa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu ni kufanikishwa ustaarabu wa Kiislamu na kusisitiza kuwa: Ustaarabu wa Kiislamu hauna maana ya kwenda kuvamia na kuziteka kijeshi nchi nyingine, bali ni kuyafanya mataifa mengine yaathiriwe na na yavutiwe na fikra ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, kigezo cha maendeleo cha Kiislamu - Kiirani ni jambo la lazima kwa ajili ya kufanikisha kuzaliwa ustaarabu wa Kiislamu na huku akijibu swali kwamba, kwa nini vigezo vilivyopo na ambavyo vimeshafanyiwa majaribio duniani haviwezi kuwa vigezo vizuri kwetu amesema: Vigezo vya ustawi wilivyoenea leo duniani vimesimama juu ya msingi ghalati na mbovu wa Humanism (elimu ya ubinaadamu inayomtanguliza mbele binadamu na mahitaji yake kuliko misingi ya dini na kwa mujibu wa fikra hiyo, mwanadamu yuko huru kufanya analopenda bila ya kujali mipaka iliyowekwa na dini) pamoja na misingi isiyojali mafundisho ya Mwenyezi Mungu na kwa upande wa taathira na matokeo yake ni kuwa vigezo hivyo vimeshindwa kufanikisha ahadi zake kuhusu mambo ya thamani katika maisha ya mwandamu kama vile uhuru na uadilifu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja hali isiyo nzuri ya baadhi ya nchi zinazofuata kibubusa vigezo hivyo katika mambo ya kimsingi kama vile madeni makubwa ya kifedha yaliyozisakama tawala za nchi hizo, ukosefu wa kazi, umaskini, ufa mkubwa baina ya watu wa matabaka mbali mbali katika jamii za nchi hizo kuwa ni uthibitisho wa wazi kwamba vigezo vya ustawi vilivyopo duniani leo havifai kabisa na kuongeza kuwa: Ijapokuwa jamii za nchi hizo zimepata maendeleo ya aina fulani, lakini maendeleo hayo yameshindwa kupenya hadi ndani kabisa ya jamii hizo na yameshindwa kuleta maadili bora, uadilifu, umaanawi na usalama. Hivyo tunapaswa tuarifishe na tuonyesha kigezo chetu wenyewe cha maendeleo kilichosimama juu ya msingi wa Kiislamu na utamaduni wa Kiirani.
Amesema, jambo la msingi kabisa kwa kigezo hicho cha maendeleo ni kuhakikisha kuwa kinakuwa cha Kiislamu na kusisitiza kwamba: Jambo la lazima la kufanikisha suala hilo ni kufanywa utafiti wa kina kuhusiana na Uislamu na kuwa na mawasiliano ya karibu, ya mfululizo na ya kina na Hawza (vyuo vikuu vya kidini) na wanachuoni wa kidini wenye fikra pana, wenye mwamko na waliotabahari vilivyo katika misingi ya kifalsafa, akida na fikihi.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kupewa umuhimu sura ya Iran katika jina hilo la "Kigezo cha Kiislamu - Kiirani cha Maendeleo" kuwa ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwani Iran ndiyo medani ya kufanikishia kigezo hicho hivyo kama kigezo hicho hakitazingatia utamaduni, historia, jiografia, eneo, mila, desturi na hazina na maliasili muhimu ya kibinadamu na kimaumbile ya nchi hii, basi kigezo hicho cha maendeleo kitakuwa ni hati chapwa isiyoweza kufanikishwa na isiyo na faida.
Baada ya kubainisha umuhimu na udharura wa Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kuelezea mambo ya lazima ya kufanikisha jambo hilo.
Ameyataja masuala kama kuweko mpangilio na utaratibu mzuri wa kielimu, kuandaa mazingira ya kufanyika uchunguzi na misuguano ya hoja kuhusu kigezo hicho, kuainishwa mipaka na vielelezo maalumu kwa kutumia matoleo mbali mbali ya utafiti na fikra tofauti duniani, kuzingatia kwa wakati mmoja malengo matukufu na uhakika wa mambo, kuzingatia faida za jambo hilo na kuwa na nguvu na muqawama wa kielimu mbele ya mitazamo inayokinzana na inayoipinga fikra hiyo, kuwa ni miongoni mwa mambo ya lazima katika kazi ya kutunga na kuratibu Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kutoa nasaha kadhaa kwa wajumbe wa Baraza Kuu la Kituo cha Kigezo cha Kiislamu - Kiirani cha Maendeleo.
Miongoni mwa nasaha zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa wajumbe wa Baraza Kuu la Kituo cha Kigezo cha Kiislamu - Kiirani cha Maendeleo ni kutofanya pupa katika kuandaa na kutunga kigezo hicho, kuchunguza mapungufu ya juhudi na kazi za miaka mitano za kituo hicho, kuwa na hoja za nguvu na za kweli za kukosoa vigezo vya ustawi vilivyoenea leo duniani, kulipa uzito wa hali ya juu suala la kufanya kazi kijihadi na kimapinduzi na kuwatumia vizuri watafiti vijana, wenye fikra pana, wanamapinduzi na walioshikamana vilivyo na dini, kuwa na uhusiano wa karibu na taasisi na mfumo mzima wa utendaji nchini na kuhakikisha kuwa suala hilo linazoeleka na kuwa miongoni mwa mijadala mikuu nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia zaidi umuhimu wa kufanywa suala hilo kuwa mjadala mkuu nchini kwa kusema: Inabidi suala hilo lienezwe vizuri nchini kwa kutumia vyombo na suhula mbali mbali kwa namna ambayo Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani kiwe mjadala mkuu unaotawala katika akili na nyoyo za vijana yaani kizazi cha viongozi wa baadaye nchini.
Vile vile amesema kuwa, sharti la lazima kwa ajili ya mafanikio ya hatua yoyote ile ni kuwa na imani na itikadi madhubuti na amemshukuru mkuu na wajumbe wa Baraza Kuu la Kituo cha Kigezo cha Kiislamu - Kiirani cha Maendeleo kutokana na juhudi zao kubwa katika kufanikisha suala hilo.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Dk Vaez-Zadeh, Mkuu wa Baraza Kuu la Kituo cha Kigezo cha Kiislamu - Kiirani cha Maendeleo ametoa ripoti fupi kuhusiana na kazi na mipango ya kituo hicho na hatua zilizofikiwa hadi hivi sasa katika kuandaa na kuratibu kigezo cha kimsingi cha maendeleo cha Kiislamu - Kiirani.
 
< Nyuma   Mbele >

^