Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Ashiriki Sherehe za Kuhitimu Mafunzo Wanachuo wa Chuo Kikuu cha Imam Husain AS Chapa
23/05/2016
Ayatollah Khamenei Attends a Graduation Ceremony at Imam Hussain (a.s.) Military AcademySambamba na maadhimisho ya tarehe 3 Khordad (Mei 23), siku ya kukombolewa mji wa Khorramshahd wa Iran kutoka mikononi mwa utawala wa wakati huo wa Iraq, katika operesheni ya kujivunia ya Baytul Muqaddas, leo asubuhi (Jumatatu) kumefanyika sherehe za kuhitimu mafunzo wanafunzi wa chuo kikuu cha maafisa wa kijeshi na cha malezi ya maafisa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Imam Husain (Alayhis Salaam) na kuhudhuriwa na Ayatullah Khamenei, Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran.
Wakati wa kuingia kwenye uwanja wa sherehe hizo, awali Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekwenda kwenye maziara ya mashahidi waliotoweka bila kupatikana athari zao na kuwasomea faatiha na kuwaenzi mashahidi wa kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu akimuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwapandisha daraja za juu ya utukufu.
Baada ya hapo Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran amekagua vikosi mbali mbali vya wanajeshi waliokuwa amepiga paredi katika uwanja huo.
Vile vile Ayatullah Udhma Khamenei amewakagua kwa karibu majeruhi wenye fakhari kubwa za kujivunia wa vita wakiwemo majeruhi waliojitoa muhanga kulinda Haram pamoja na watu kadhaa wa familia azizi za mashahidi.
Katika sherehe hizo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa hotuba muhimu na huku akibainisha mantiki ya Qur'ani na Uislamu kuhusu istilahi ya "Jihadi Kubwa" yenye maana ya kusimama imara na kutoifuata kambi ya kiistikbari, pamoja na vipengee na mambo yake ya lazima katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu; amegusia njama na mipango mikubwa ya kambi ya kibeberu ya kujaribu kujipenyeza kwa nia ya kubadilisha muundo wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na amesema kuwa: Jukumu kubwa zaidi la hivi sasa la Vyuo Vikuu na Hawza (vyuo vikuu vya kidini), watu na vijana waumini na wanamapinduzi na vile vile taasisi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, ni kuchukua hatua zenye umakini mkubwa na za hekima nyingi kwa ajaili ya kubainisha na kuwaamsha watu kuhusiana na maana pana na zenye kina kirefu za kaulimbiu za Mapinduzi ya Kiislamu, na kujiepusha kuchukua hatua nyepesi na za upeo wa juu juu usio wa kina, kulea vijana madhubuti kwa ajili ya mustakbali, kuandaa na kuhifadhi kielimu uzoefu mkubwa na wa kustaajabisha wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kipindi chote hiki cha miaka 38 ya uhai wa Mapinduzi hayo matukufu.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa pia mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imam Mahdi AS na pia maadhimisho ya tarehe 3 Khordad ya siku ya kukombolewa mji wa Khorramshahr na kusema kuwa, siku hiyo haiwezi kusahaulika katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu kwani ni nembo ya nguvu za Mwenyezi Mungu kwa watu wanaoinusuru dini Yake.
Ameongeza kuwa: Kuhusu operesheni ya kuukomboa mji wa Khorramshahr na operesheni nyinginezo za kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu, kuna vipengee vingi vya ndani ambavyo wananchi wengi hususan vijana hawavijui na ni kwa sababu hiyo ndio maana tunahimiza watu wahakikishe kuwa wanasoma sana vitabu vinavyozungumzia operesheni hizo.
Amebainisha moja ya nukta muhimu zilizokuweko kwenye operesheni ya ukombozi wa mji wa Khorramshahr na namna Mwenyezi Mungu alivyoonesha nguvu Zake katika operesheni hiyo kwa kusema: Imam (Khomeini - quddisa sirruh) mja huyo wa Mwenyezi Mungu mwenye hekima alizopewa na Mola wake Mungu na mcha Mungu wa kweli alisema, Mwenyezi Mungu ndiye aliyeikomboa Khorramshahr.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, mantiki ya maneno hayo ya Imam ni kuwa, wakati watu wanapofanya jitihada zao zote na kufanya jihadi kubwa kwa kuingiza nguvu zao zote katika medani ya mapambano, na hapo tena wakatawakali kwa Mwenyezi Mungu, bila ya shaka yoyote watapata msaada wa nguvu za Mwenyezi Mungu na matunda ya msaada huo ni kama huko kukombolewa mji wa Khorramshahr kutoka mikononi mwa adui ambaye alikuwa amejizaititi kwa kila aina ya suhula na silaha.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kwa mantiki hiyo, upo uwezekano wa kukombolewa dunia nzima inayodhibitiwa na mabeberu; upo uwezekano wa kukombolewa Palestina kama ambavyo pia upo uwezekano wa kutokuwepo taifa lolote dhaifu linalokandamizwa ulimwenguni.
Amesisitiza kuwa: Taifa lolote lile linalotumia mantiki hiyo na ambalo linafanya jitihada zake zote katika njia ya Mwenyezi Mungu na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu, bila ya shaka yoyote haliwezi kutishwa na nguvu za kijeshi, kifedha, kipropaganda na kisiasa za madola ya kibeberu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia namna kambi ya kiistikbari ilivyofeli katika njama zake zote za kujaribu kuyashinda nguvu Mapinduzi ya Kiislamu katika kipindi chote hiki cha miaka 38 iliyopita licha ya kambi hiyo kutumia njia na mbinu za kila namna na kwamba huo ni mfano wa wazi wa kushinda mantiki ya jihadi na kusimama imara kwa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu. Amesisitiza kuwa: Taifa la Iran bado liko imara katikati ya medani; na vijana wake wako tayari mno kujitolea roho zao katika njia ya Mapinduzi ya Kiislamu na ni katika jambo kama hilo ndimo Mwenyezi Mungu anamodhihirisha nguvu na uwezo Wake mkubwa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, mapambano ya namna hiyo mbele ya kambi ya kiistikbari ni vita visivyo na mlingano. Amesema: Katika vita hivi visivyo na mlingano, pande zote mbili zina uwezo wake na hata vyanzo vya nguvu zao navyo ni tofauti, kila upande una suhula za uwezo na vyanzo vya nguvu vinavyotofautiana na vya upande wa pili. Kwa hakika chanzo cha nguvu za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kumtegemea na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu. Ni kutegemea nguvu za Mwenyezi Mungu, kuwa na yakini na ushindi na kutengemea nguvu za irada ya watu waumini wenye imani ya kweli ya Mwenyezi Mungu.
Amesisitiza kuwa, vita visivyo na mlingano ni vita vya irada, maamuzi na nia za kweli na kuongeza kuwa: Katika medani ya vita hivyo, nia ya kweli ya upande wowote kati ya pande hizo mbili inapolegalega, bila ya shaka yoyote upande huo utashindwa na upande wa pili, hivyo inabidi kuwa macho ili zisije propaganda na wasiwasi unaoenezwa na adui ukatia doa katika nia na irada hiyo madhubuti.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mipaka ya vita hivyo inapindukia mipaka ya vita vya kijeshi, bali ni aina fulani ya jihadi na kuongeza kuwa: Leo hii uwezekano wa kutokea vita vya kijeshi dhidi ya Iran kwa sura ya jadi ni mdogo sana lakini suala la jihadi litaendelea kuwepo na jihadi hii ambayo kwa mantiki ya Qur'ani na Uislamu inaitwa "Jihadi Kubwa" ikiwa na maana ya kusimama kidete, kuwa imara katika muqawama na kutowafuata makafiri na washirikina nayo itaendelea kuwepo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, "Jihadi Kubwa" inaonekana kwa upana na uwazi pia katika nyuga za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kisanii na kuongeza kwamba: Badala ya kuifuata kambi ya makafiri na washirikina, inabidi kufuata miongozo ya Uislamu na Qur'ani Tukufu katika medani zote hizo.
Amesema, kadhia ya leo hii ya Jamhuri ya Kiislamu na kambi ya kiistikbari ni suala la ufuataji mambo na kuongeza kuwa: Upande wa kambi ya kibeberu unatumia mbinu, mashinikizo na njama zake zote za kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na kipropaganda pamoja na vibaraka wake wasaliti ili kujaribu kuupigisha magoti mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuufanya uifuate kambi hiyo ya kiistikbari, lakini kitu kinachoihamakisha vibaya kambi hiyo ya kibeberu kuhusiana na taifa la Iran ni kwamba wananchi wa Iran kutokana na kuwa ni Waislamu, hawako tayari kabisa kuwafuata mabeberu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kitendo cha mabeberu cha kuzusha mambo kama vile miradi ya nyuklia, nguvu za makombora na haki za binadamu, ni kisingizio tu cha kufanikishia malengo yake ya kiadui na kusisitiza kuwa, sababu kuu ya kuweko uadui wote huo na kutafuta visingizio vya kila namna ili kulikwamisha taifa la Iran ni kuwa taifa hili limekataa kuwafuata mabeberu. Amesema, lau kama taifa la Iran lingelikuwa tayari kuwafuata waistikbari, basi bila ya shaka yoyote mabeberu wangeliyaweka pembeni masuala kama nguvu za makombora na miradi ya nyuklia ya taifa hili na kamwe wasingelisema chochote kuhusiana na haki za binadamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia pia makelele yanayopigwa na mabeberu kuhusiana na suala la uwezo wa makombora wa Iran kwa kukumbushia nukta moja muhimu na kusisitiza kuwa: Hivi karibuni wameanzisha makelele mengi kuhusiana na uwezo wa makombora wa Iran, lakini wanapaswa kutambua kuwa, makelele yao hayo hayataathiri chochote, na hawawezi kutufanyia ghalati wala upuuzi wowote ule.
Ameendelea kubainisha sababu kuu za uadui wa mabeberu kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema kuwa: Wamarekani wanafanya njama kubwa za kujaribu kukwepa kutamka hadharani sababu ya uadui wao huo, lakini baadhi ya wakati huwa wanafichua sababu hiyo kwa matamshi yao wenyewe, na mfano wa wazi kabisa ni matamshi ya siku chache zilizopita ya kiongozi mmoja wa Marekani ambaye baada ya kukariri tuhuma za kila siku dhidi ya Iran, bila ya kujielewa aliashiria suala la aidiolojia yaani fikra ya Kiislamu na kusema kuwa, fikra ya Kiislamu ndiyo inayolifanya taifa la Iran lisikubali kuburuzwa na kambi ya ukafiri na ya kibeberu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kusimama imara, kutomfuata adui na kulinda utambulisho wa kimapinduzi na Kiislamu ndizo nguzo kuu zinazoupa nguvu mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran na kusisitiza kuwa: Marekani na madola mengine ya kibeberu yanachukizwa mno na jambo hilo lakini pia hayana la kufanya na ni kwa sababu hiyo ndio maana yanafanya njama za kila aina kwa tamaa kuwa yataweza kuzitoa katika njia yake taasisi za kuchukua maamuzi na kutunga sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini wameshindwa na kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu wataendelea kushindwa katika mustakbali.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Jukumu kuu la SEPAH (Jeshi la walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu) ni kuhakikisha kuwa linafanya kazi zake zote kulingana na jihadi hiyo kubwa.
Amegusia pia tuhuma nyingi zinazotolewa dhidi ya jeshi la SEPAH na kusema: Sababu kuu ya kushuhdiwa hamaki zote hizo za maadui, ni kusimama imara Sepah katika njia ya Mapinduzi ya Kiislamu na kulinda misimamo na moyo wa Mapinduzi ya Kiislamu na moyo wa Uislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakhutubu vijana wa Iran na wanachuo waliokuwepo kwenye sherehe hizo akiwaambia: Mustakbali wa Mapinduzi ya Kiislamu uko mikononi mwenu na ni jukumu lenu kuilinda historia hii kwa heshima kubwa na jueni kuwa katika mustakbali, kuna Khorramshahr nyingi, lakini tab'ani si katika medani za vita vya kijeshi, bali katika medani ambazo hazina uharibifu wa vita vya kijeshi, bali ni kinyume kabisa na vita hivyo vya kijeshi kwani vita hivyo vipya vina hata ustawi ndani yake, lakini ni vita vigumu zaidi kuliko vita vya kijeshi.
Ayatullah Udhma Khamenei ametumia fursa hiyo kubainisha pia vipengee tofauti vinavyohusiana na "Jihadi Kubwa" katika nyuga za kiuchumi, kiutamaduni na kijamii na kuongeza kuwa: Sisitizo kuhusu utekelezaji wa uchumi wa kimuqawama, ni sehemu ya kiuchumi ya jihadi hiyo; sisitizo kuhusiana na maudhui kwamba vijana waumini, walioshikamana ipasavyo na dini na wanamapinduzi wanaojihusisha vilivyo na kazi za kiutamaduni kwa kujitolea wanapaswa kuendelea kwa nguvu zote na kazi hizo na taasisi za kiutamaduni nazo zinapaswa kwenda katika muelekeo huo huo, hiyo nayo ni sehemu ya kiutamaduni ya jihadi hiyo. Aidha sisitizo juu ya kutumia vizuri uwezo wote uliopo na vipaji vyote nchini katika kuleta maendeleo yanayotakiwa, ni sehemu ya harakati za kijamii ya jihadi hiyo kubwa.
Amezungumzia pia tuhuma zisizo sahihi zinazotolewa na wapinzani wa harakati hiyo na madai kuwa kutumia uwezo wa ndani ya nchi kuna maana ya kukata uhusiano na dunia na kuongeza kuwa: Sisi kamwe hatujawahi kuunga mkono suala la kukata uhusiano na dunia na kujifungia peke yetu kwenye mipaka ya nchi yetu, bali tunachosema sisi ni kuwa mnapaswa kuwa na mahusiano ya kisiasa na mabadilishano ya kiuchumi na dunia, lakini wakati huo huo mhakikishe mnachunga na kulinda utambulisho na shakhsia yenu ya asili na wakati mnapoamua kusema kitu au kutia saini mkataba fulani, mzungumze kama wawakilishi wa Iran ya Kiislamu na wawakilishi wa Kiislamu na wakati mnapokaa kwenye meza ya mikataba mkae mkiwa na muono mpana na mwamko unaotakiwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, "Jihadi Kubwa" inahitaji watu kuwa macho na kuwa na ikhlasi na amegusia njama na tamaa za adui za kujaribu kujipenyeza ndani ya Iran na kusisitiza kwamba: Leo hii adui amekata tamaa na suala la kutoa pigo kubwa kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu lakini kwa kutumia zana tofauti na tata, ana nia ya kujipenyeza ili kuharibu utambulisho wa vijana na kuufanya ukubaliane na siasa zake na za mabeberu wengine, kwani kama atafanikiwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kwake kufanikisha malengo yake ya kibeberu pamoja na njama zake nyingine bila ya gharama yoyote.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, kutokana na Marekani na kambi ya kibeberu kuwa na utambuzi pungufu kuhusiana na taifa la Iran ndicho chanzo kikuu cha mahesabu yao ghalati na mabovu na kuongeza kuwa: Tab'an maadui hawajakata tamaa kuhusiana na suala la kujipenyeza ndani ya Iran, na katika hali kama hii, kuna jukumu kubwa juu ya mabega ya watu wote wenye uchungu na taifa la Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu likiwemo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, SEPAH.
Vile vile amesisitiza kuwa, Sepah inapaswa kuwa tayari kijeshi wakati wote na kuwa katika hali bora kabisa na ubunifu wa hali juu muda wote na kuongeza kwa kusema: Hata hivyo jukumu la Sepah haliishii tu katika medani ya kijeshi bali katika kipindi cha hivi sasa, moja ya majukumu muhimu ya watu wote wenye uchungu, wenye mapenzi na waaminifu kwa Mapinduzi ya Kiislamu ikiwemo Sepah, ni kubainisha uhakika wa mambo na kuamsha watu pamoja na kuzielimisha akili za watu kuhusu kina kirefu na kipana cha uhakika na kaulimbiu za Mapinduzi ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mwito kwa watu wote kulitilia hima suala la kubainisha uhakika wa mambo na kuwaelimisha watu na kufanya kazi zenye umakini na athari kubwa na kusema: Kutoa ufafanuzi wa kina na kuzitangaza kaulimbiu za Mapinduzi ya Kiislamu na kuwaelimisha watu kuhusu kina kirefu cha kaulimbiu hizo, ni miongoni mwa mambo asili ya lazima katika ufanikishaji wa "Jihadi Kubwa" kwani kaulimbiu za Mapinduzi ya Kiislamu, ni mithili ya vielelezo na muongozo wa kumulika njia sahihi ya Mapinduzi ya Kiislamu na njia iliyonyooka.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la hisia na huruma kuwa ni jambo la lazima katika kufuatilia uhakika na kaulimbiu za Mapinduzi ya Kiislamu lakini amesema halitoshi na kusisitiza kuwa: Kama suala hilo litabainishwa kwa kina na kwa ufasaha wa hali ya juu, bila ya shaka yoyote imani na itikadi za watu kuhusiana na kaulimbiu hizo itaongezeka na watabakia nayo daima.
Amesema, sababu kuu inayowafanya baadhi ya watu kubadilisha misimamo kwa daraja 180 katika nyakati tofauti za Mapinduzi ya Kiislamu, ni kutokuwa na welewa wa kina na kuangalia kwao mambo kijuu juu na kusisitiza kuwa: Inabidi kuwa ni fikra na welewa wa kina kuhusu masuala makuu, na kaulimbiu za Mapinduzi ya Kiislamu na kustafidi vizuri na miongozo ya wahadhiri wema wa vyuo vikuu katika jambo hilo.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kutayarisha na kuleta watu makini wa baadaye na kuandaa kielimu vipengee vingi muhimu vya historia ya miaka 38 ya Mapinduzi ya Kiislamu katika panda shuka za kila namna za kustaajabisha kuwa ni jambo jingine la lazima katika "Jihadi Kubwa" na kuongeza kuwa: Vituo na taasisi zote za vyuo vikuu na hawza (vyuo vikuu vya kidini) na hasa Chuo Kikuu cha Imam Husain (Alayhis Salaam) vina mas'ulia na jukumu zito katika jambo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha udharura wa kuchukuliwa hatua za kina na wakati huo huo amekosoa baadhi ya hatua zisizo za kimantiki zinazochukuliwa na baadhi ya watu kusisitiza kuwa: Baadhi ya wakati wanatokezea watu na vijana ambao pengine ni wazuri na wenye imani, lakini kwa sababu ya kumpinga mtu fulani au hotuba ya mtu fulani, wanapiga makelele na mayowe na kuharibu kikao au mkutano anaohutubia mtu huyo, wakati ambapo mimi tangu zamani siviungi mkono vitu kama hivyo na hivi sasa pia siviungi mkono kwani havina maana yoyote na ninaamini kuwa faida inapatikana kupitia kubainisha mambo kwa njia sahihi na kufanya mambo inavyotakiwa, si kupiga makelele na kuvuruga mikutano.
Aidha ametoa mwito kwa vijana waumini na wanamapinduzi kuwa macho na kuongeza kuwa: Tab'an baadhi ya wakati wanatokezea watu na kufanya mambo hayo yasiyo sahihi kwa malengo yao maalumu na baadaye kujaribu kuwaonesha watu wengine kuwa, mambo hayo yamefanywa na watu waumini walioshikamana vilivyo na dini. Hivyo inabidi watu wawe macho kikamilifu katika jambo hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kazi ya kuwaelimisha watu kwa kina na kuchukua hatua sahihi na za hekima na busara ni katika majukumu makuu ya watu hao wema na kusisitiza kwamba: Hatua zote hizo zitaweza kuwa na taathira iwapo tu zitafanywa kwa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwa kutawasali Kwake.
Mwishoni mwa hotuba yake hiyo, Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, kama watu wanataka kuwa imara, basi hawana budi kuimarisha vilivyo uhusiano wao wa nyoyoni na Mwenyezi Mungu, wawe na mapenzi makubwa na ya karibu na Qur'ani Tukufu na wazizingatie kwa kina aya za Mwenyezi Mungu, waizingatie Sala na kuitekeleza kwa kuuhudhurisha vilivyo moyo na kutumia ipasavyo fursa za miezi mitukufu ya Shaaban na Ramadhani.
Katika maadhimisho hayo, Meja Jenerali Mohammad Ali Jaafari, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa, sababu kuu ya kuwa na nguvu mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni istiqama na kusimama kwake imara mbele ya Marekani inayopenda kujikumbizia kila kitu upande wake. Amesema: Katika jitihada zake za kuvunja njama za maadui, Sepah imejikita katika mikakati kama kujizalishia nguvu za kulihudumia jeshi la Sepah na Mapinduzi ya Kiislamu, kuyabakisha hai Mapinduzi ya Kiislamu kwa sura na kwa sira, na kuyatekeleza kivitendo maelekezo na miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amegusia pia vita mbali mbali vinavyoendeshwa kwa niba ya Marekani kupitia tawala zenye fikra mgando za eneo la Mashariki ya Kati na kusema kuwa, mwamko na muqawama wa Kiislamu bado unaendelea na kwamba njama za kambi ya kibeberu haziwezi kuzuia kuendelea kuwepo Mapinduzi ya Kiislamu na mwamko wa Kiislamu.
Meja Jenerali Jaafari ameongeza kuwa: Maafisa vijana wa leo hii wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH wako tayari na imara katika medani nzito, ngumu na tata za siku za usoni kwa ajili ya kuulinda kwa nguvu zao zote Uislamu, Mapinduzi ya Kiislamu na heshima ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Kwa upande wake, Admeli Morteza Safari, kamanda wa Chuo Kikuu cha Imam Husain (Alayhis Salaam) ametoa ripoti fupi kuhusu hatua na ratiba za kielimu, kiutamaduni na kimafunzo pamoja na kuongeza uwezo wa kijeshi zinazofanyika katika chuo kikuu hicho.
Katika sherehe hizo, makamanda kadhaa, wakurugenzi, watafiti, wabunifu na mwakilishi wa maafisa waliohitimu mafunzo yao ya kijeshi pamoja wanachuo bora wa Chuo Kikuu cha Imam Husain (Alayhis Salaam) wamepokea zawadi kutoka kwa Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama ambavyo pia mwakilishi wa wanachuo wa Chuo Kikuu cha Imam Husain (Alayhis Salaam) amepata fakhari ya kupandishwa cheo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwenye sherehe hizo.
Kutekeleza mpango wa "Ibadis Swalihin" ni miongoni mwa ratiba zilizokuwepo kwenye sherehe hizo za leo za kula kiapo maafisa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na wanachuo wa Chuo Kikuu cha maafisa wa kijeshi cha Imam Husain (Alayhis Salaam).
Vile vile katika sherehe hizo, vikosi mbali mbali vya kijeshi vilivyokuwepo kwenye uwanja wa sherehe hizo wamepita kwa gwaride mbele ya jukwaa alilokuwepo Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
 
< Nyuma   Mbele >

^