Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Sala ya Idul Fitr Iliyosalishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu (1437 Hijria) Chapa
06/07/2016
Photos of Eid al-FitrWananchi Waislamu na wacha Mungu wa Iran, leo (Jumatano) wamesali Sala ya Idul Fitr kwa hamasa na shauku kubwa katika kona zote za Iran ikiwa ni katika kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa taufiki ya kutekeleza ibada za mwezi mzima wa Ramadhani. Hamasa kubwa zaidi ya kuonyesha shukrani kwa Mwenyezi Mungu imeonekana kwenye msikiti mkubwa wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) jijini Tehran, wakati maelfu ya Waislamu waliposhiriki katika sala ya Idul Fitr iliyosalishwa na Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Katika khutba ya kwanza ya Sala hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa umma mkubwa wa Kiislamu na kwa taifa la Iran kwa mnasaba wa kuwadia sikukukuu ya Idul Fitr na kusema kuwa, mwezi wa Ramadhani nchini Iran mwaka huu ulikuwa ni mwezi uliojaa umaanawi, kumzingatia Mwenyezi Mungu, tawassul, unyenyekevu na kujikurubisha mno kwa Allah. Ameongeza kuwa: Sisi viongozi tunapaswa tuone fakhari kwamba ni viongozi wa watu waumini wa kweli wenye nyoyo zilizojaa nuru, na tab'an tuna wajibu pia wa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia tunapaswa kujua kuwa, majukumu yetu ni makubwa mno mbele ya wananchi hawa waumini wa nchi yetu.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kufunga saumu wananchi wa Iran hususan vijana na mabarobaro katika wakati huu wa msimu wa joto ambapo mchana unakuwa mrefu zaidi na hali ya hewa inakuwa ya joto kubwa zaidi kuliko siku nyingine zote za mwaka, kuwa ni katika madhihirisho ya kuvutia sana yaliyojidhihirisha katika mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka huu na kuongeza kuwa: Tab'an kuna mikono ya kikhabithi na kiafiriti iliyojaribu kuwashawishi vijana wetu wale mchana na wadharau saumu katika mwezi wa Ramadhani lakini kwa uwezo na taufiki ya Mwenyezi Mungu njama zao zimeshindwa na katika siku za usoni pia wataendelea kushindwa.
Vile vile amesisitiza kuwa: Viongozi nchini Iran wanapaswa muda wote wazingatie kuwa, maadui maafiriti wa Iran ya Kiislamu wamepanga njama nyingi za kujaribu kuwaweka mbali vijana wa nchi yetu na dini ya Kiislamu lakini njama za mwaka huu pia za maadui hao wanaolitakia mabaya taifa hili, zimeshindwa kutokana na kuwa macho wananchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kufanyika maandamano makubwa ya Siku ya Kimataifa ya Quds tena katika hali ya hewa ya joto kali hususan katika mikoa ya kusini mwa Iran, ni dhihirisho jengine lenye mvuto wa aina yake na ni moja ya kazi kubwa na jitihada za kupigiwa mfano zilizofanywa na wananchi wa Iran katika mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka huu. Ameongeza kuwa: Kutokana na wananchi kujitokeza kwa wingi mno katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kupiga nara kwa sauti kubwa za kuunga mkono kadhia muhimu ya Palestina, maana ya hatua hiyo ya wananchi wa Iran kwa hakika ni kutangaza kwamba, hata kama baadhi ya tawala za nchi za Waislamu zimeyasaliti malengo matukkufu ya Palestina au kudharau kutekeleza wajibu wao mbele ya malengo hayo na hata kama wako baadhi ya watu hawaijali kabisa kadhia ya Palestina, lakini taifa la Iran lipo na limesimama imara kukabiliana na maadui na kulibakisha hai daima suala la Palestina.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka huu yalikuwa ni maonyesho ya mambo matukufu ya kimaanawi ya wananchi na huku akiashiria namna wananchi wa Iran walivyofanya jalsa na vikao vikubwa, vingi na vilivyojaa umaanawi vya Qur'ani katika haram mbali mbali tukufu na maeneo tofauti nchini Iran na kuakisiwa kwa njia bora kabisa na Shirika la Sauti na Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) amesema kuwa, maonyesho mengine matukufu ya kimaanawi katika mwezi huo wa Ramadhani ni namna wananchi walivyojotolea kugawa futari katika miji tofauti ya Iran na hususan katika maeneo mengi ya mji wa Tehran na kwamba umaanawi na moyo huo wa kutumikia watu kwa hakika unamuathiri na kumvutia mtu yeyote yule.
Amesema, sunna nzuri ya kugawa futari kwa watu inasimama upande wa pili wa zile futari za kufanya israfu na za kifakhari na kusema: Inasikitisha kuona kuwa baadhi ya taasisi zilitoa futari za gharama kubwa mahotelini tena kwa watu wasiostahiki na kwa kweli hilo ni jambo baya sana na inabidi tuseme kuwa futari za gharama ndogo na za kuwapa watu wanaostahiki na za kugawa mitaani kwa ajili ya wapita njia ndizo futari bora katika mkabala wa futari hizo za kifakhari na za israfu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kugawa chakula katika nyumba za maskini na wahitaji kulikofanywa na vijana ambao walijipa jina la "maashiki wanaozunguka mitaani," kufanyika jalsa na vikao vilivyofana vya dua na kunong'ona na Mwenyezi Mungu misikiti, kwenye Husainia mbali mbali na katika maziara ya mashahidi hususan katika mikesha ya Laylatul Qadr, kuendeleza sunna inayozidi kustawi na kupata nguvu ya itikafu katika kumi la mwisho la Ramadhani na hatua ya baadhi ya madaktari ya kuamua kuwatibu bure wagonjwa mahospitalini kwenye mwezi wa ramadhani ni katika madhihirisho ya kuvutia sana yaliyoongeza mvuto katika mwezi mtukufu wa Ramadhani wa mwaka huu. Amesisitiza kuwa: Bila ya shaka yoyote, Ramadhani ya namna hii hutakabaliwa na Mwenyezi Mungu na kupelekea kupatikana rehema Zake.
Katika khutba yake ya pili ya Sala ya Idul Fitr kwa mwaka huu wa 1437 Hijria, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia miripuko ya kigaidi iliyotokea katika siku za hivi karibuni kwenye nchi za Iraq, Uturuki, Bangladesh na katika baadhi ya nchi nyingine duniani na kusema: Inasikitisha kuona kuwa, mwaka huu, sikukuu ya Idul Fitr imekuwa chungu kwa Waislamu wa baadhi ya nchi kutokana na vitendo vya kigaidi vya watu ambao wanataka kufuta Uislamu wa kweli na kuweka mahala pake Uislamu bandia kwa amri ya mabwana zao na kwamba jinai hizo ni matunda ya hatua za mashirika ya usalama ya Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni wa Israel ya kulea magaidi na kuwasambaza katika kona mbali mbali za dunia.
Vile vile amesisitiza kuwa, jukumu na lawama za uhalifu wa kuuliwa watu wasio na hatia zinawaendea waungaji mkono wa magenge ya kigaidi na kitakfiri ambao tab'an ni hao hao ndio waliyoyaanzisha na kuyalea magenge hayo na hivi sasa pole pole madhara yake yanawafikia hao hao waungaji mkono na waanzishaji wa makundi hayo, lakini jambo moja liko wazi nalo ni kwamba madhambi na uhalifu wao huo hauwezi kusahauliwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuwasha moto wa vita na kuvuruga amani na usalama katika nchi za eneo hili zikiwemo nchi za Syria, Libya na Yemen, ni jambo linalosikitisha sana na kuongeza kuwa: Hivi sasa mwaka mmoja na miezi mitatu imepita tangu wananchi wa Yemen waanze kumiminiwa mabomu katika mashambulizi ya mfululizo ya wavamizi wa nchi yao. Amesema: Inabidi kuwapongeza viongozi wenye busara wa wananchi wa Yemen ambao pamoja na nchi yao kushambuliwa mtawalia katika kipindi chote hicho na licha ya nchi yao kuwa katika kipindi cha joto kali, lakini wamewakinaisha wananchi wao kushiriki kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kuiadhimisha siku hiyo kwa hamasa na shauku kubwa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, lengo na shabaha kuu ya madola ya kibeberu na kiistikbari ya kuanzisha vita na kuvuruga usalama na kueneza vitendo vya kigaidi katika eneo la Mashariki ya Kati ni kujaribu kusahaulisha kadhia ya Palestina. Amesema: Mapambano ya ukombozi wa Palestina ni mapambano ya Kiislamu na yanawahusu watu wote na kwamba kuendelea na harakati hiyo ya ukombozi wa Palestina ni jukumu la Kila Muislamu. Hivyo ni ghalati na ni makosa makubwa kulitoa suala la Palestina katika hali yake hiyo ya asili na kulifanya kuwa ni suala la ndani au la nchi za Kiarabu tu.
Katika sehemu ya mwisho ya khutba yake ya Sala ya Idul Fitr kwa mwaka huu wa 1437 Hijria, Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia suala la mishahara na utwaaji wa fedha wa kidhalimu na usio wa kiadilifu nchini na kusisitiza kuwa utwaaji huo ulio kinyume cha sheria katika fedha za hazina na Baytul Maal ni madhambi na ni usaliti kwa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa: Bila ya shaka yoyote huko nyuma kuna makosa na mghafala ulifanyika na inabidi makosa yote hayo yafidiwe. Vile vile amesema: Viongozi wa sekta mbali mbali nao wana wajibu wa kulifuatilia kwa nguvu kubwa suala la mishahara iliyo kinyume cha sheria na isiwe ni kupiga makelele tu na baadaye suala hilo kusahauliwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemsifu Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wakuu wa mihimili mingine mikuu ya dola ya Kiislamu yaani Bunge na Mahakama kutokana na misimamo yao thabiti ya kukabiliana na jambo hilo na kulifuatilia suala hilo la aibu bila ya kutetereka na kusisitiza kuwa: Kuhusu suala hilo ni kwamba lazima fedha zote zilizotwaliwa kinyume cha sheria zirejeshwe na lazima sheria ichukue mkondo wake kuwaadhibu watu wote waliotumia vibaya sheria kufanya jambo hilo lisilokubalika na inabidi wavuliwe vyeo vyao kwani hawana ustahiki wa kupewa majukumu ya kusimamia sehemu kama hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesisitiza kuwa, maadui wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanafanya njama za kulitumia suala hilo dhidi ya mfumo huo wa Kiislamu na kusema kuwa: Watu waliochukua mishahara iliyo kinyume cha sheria ni wachache mno ikilinganishwa na viongozi walio wasafi wa Jamhuri ya Kiislamu lakini hata hiyo idadi ndogo, ina madhara na ni aibu kwa mfumo wa Kiislamu na inabidi jambo hilo likabiliwe vilivyo.
Amesema, moja ya sababu za kutokezea tukio la aibu la mishahara iliyo kinyume cha sheria ni kulewa anasa na kusisitiza kuwa: Wakati jamii inapokuwa na masuala ya anasa, israfu na kupenda makubwa, matokeo yake ni kuzuka ndani ya jamii hiyo mambo maovu na ya aibu kama kutwaa fedha kinyume cha sheria.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwa mara nyingine tena umuhimu wa kuchukuliwa hatua kali za kukabiliana na tatizo hilo na kusema kuwa: Suala la kufutwa kazi, kupokonywa vyeo na kurejeshwa fedha kwenye hazina ya nchi inabidi liwe ajenda kuu ya viongozi nchini kwani wananchi wana hisia kali kuhusiana na jambo hilo na kama hatua za lazima hazitachukuliwa, imani ya wananchi kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu itapungua.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, kupungua imani ya wananchi kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni maafa na kusisitiza kuwa: Viongozi nchini wana wajibu wa kulifuatilia vilivyo suala hilo na kuchukua hatua kali dhidi yake ili kulinda imani ya wananchi.
 
< Nyuma   Mbele >

^