Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Amirijeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi Atembelea Maonyesho ya Zana na Ulinzi Chapa
31/08/2016
Leader visits exhibition of Ministry of Defense's achievementsHusainia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) mjini Tehran leo (Jumatano) ilikuwa mwenyeji wa maonyesho ya mafanikio ya sekta ya ulinzi ya Wizara ya Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei ambaye ni Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran ametembelea maonyesho hayo kwa muda wa zaidi ya masaa mawili na kuona kwa karibu teknolojia za kisasa na za ndani ya Iran za taasisi za elimu za kimsingi ambayo ni matunda ya jitihada, ubunifu, maarifa na utafiti wa wataalamu wa ndani ya nchi na ambayo yana athari za moja kwa moja katika kuongezeka uwezo wa kijeshi wa vikosi vya ulinzi vya Iran.
Katika maonyesho hayo kumeoneshwa maendeleo mbali mbali yaliyopatikana katika utengenezaji wa mifumo mbali mbali ya kiulinzi na zana za kisasa katika nyuga za makombora, rada, vifaa vya baharini n.k.
Baada ya kutembelea maonyesho hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa hotuba mbele ya Waziri, maafisa, watafiti na wataalamu wa Wizara ya Ulinzi na kusema kuwa ni haki iliyo wazi ya Iran kuwa na nguvu za kiulinzi na za kimashambulizi. Aidha amesisitizia ulazima wa kuendelea na njia ya kuongeza uwezo wa kiulinzi taifa na kusema: Katika dunia hii ambapo madola ya kiistikbari, kibeberu na yasiyo na chembe ya maadili, utu na ubinadamu, madola ambayo hayasiti hata chembe kuzivamia nchi nyingine na kuua watu wasio na hatia, ni jambo la kawaida kabisa kwa nchi kuimarisha viwanda vyake vya utengenezaji wa zana za kiulinzi na kimashambulizi, kwani usalama wa nchi hauwezi kupatikana kama madola hayo ya kibeberu hayataona kuwa nchi yetu ina nguvu kubwa za kijeshi.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesema ni jambo linalomfurahisha na kumvutia sana kutembelea maonyesho ya maendeleo ya viwanda vya ulinzi na kuongeza kuwa: Jambo linalonifurahisha zaidi ni kuona kuwa, mbali na kuwa na uwezo huo wa kila namna wa kiulinzi, ambao una nafasi kubwa sana katika kukuza na kuimarisha nguvu na uwezo wa kiulinzi wa nchi, ninaona kuna nguvu kazi ya wasomi, watafiti, wataalamu na watu wenye fikra nzuri wanazoziakisi kivitendo na ambao wana imani thabiti. Hilo ndilo linalonifurahisha zaidi.
Vile vile amesema: Kuwepo nguvu kazi hiyo katika sekta za ulinzi nchini, ni mfano wa kuwa na kito chenye thamani kubwa ambacho haiwezekani kukikadiria thamani yake.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha sababu zinazomfanya asisitizie mno suala la kuongeza na kuimarisha uwezo wa kiulinzi nchini kwa kusema: Wakati tunapoona kuwa madola ya kibeberu yamefungua "mwavuli" wa nguvu zao na hayana huruma hata chembe, bali yanashambulia bila kisisi sherehe za harusi na mahospitali kwa madai ya eti kupambana na ugaidi na kuua kikatili mamia ya watu wasio na hatia na hakuna taasisi wala chombo chochote kinachoyazuia na kuyaambia chochote, lazima na sisi tuongeze uwezo na nguvu zetu za kijeshi kadiri tunavyoweza ili kuyafanya madola ya kiistikbari yaingie woga na yasithubutu kutushambulia.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kusema: Ni jambo lililo wazi kuwa sisi tunajiwekea mipaka katika kuimarisha sekta zetu za kiulinzi na kwa mujibu wa itikadi zetu za kidini, haifai kutengeneza silaha za mauaji ya umati kama vile silaha za kemikali na silaha za nyuklia.
Amesisitiza kuwa: Marufuku ya kutengeneza silaha za kemikali tumejiwekea kwa ajili ya silaha za kushambulia tu kwani kuwa na zana za kiulinzi za kujilinda na kujihami mbele ya mashambulizi ya kemikali, hilo halina tatizo lolote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema: Ukitoa mipaka hiyo, hatuna mipaka mingine yoyote tunayojiwekea katika kuimarisha nguvu zetu za kijeshi, bali ni jukumu letu kujiletea maendeleo katika nyuga zote hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia nafasi ya kiistratijia iliyo nayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na pia umuhimu mkubwa wa eneo la magharibi mwa Asia na namna madola ya kibeberu yanavyoliangalia kwa tamaa eneo hili muda wote na kuongeza kuwa: Kuna wajibu wa kuongeza na kuimarisha uwezo wa mashambulizi sambamba na uwezo wa kujilinda na kujihami kama njia ya kudhamini usalama wa taifa, wa nchi na mustakbali bora.
Vile vile amegusia hamaki zinazooneshwa na madola ya kibeberu kuhusiana na suala la Iran kununua zana za kijeshi kutoka kwa baadhi ya nchi na kusema: Madola hayo yanayodai kuwa yana akili na insafu na ambayo yanajifanya yamepevuka kimaadili kiasi kwamba yanajipa haki ya kuziamulia nchi nyingine duniani kuhusu ipi inastahiki kuwa na silaha fulani na ipi haistahiki, yenyewe madola hayo, hayana chembe ya maadili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema: Serikali ya Marekani haina ustahiki wowote wa kimaadili wa kuifanya iwe na haki ya kusema lolote kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema: Hakuna chama chochote kinachoingia madarakani huko Marekani kati ya vyama viwili (vya Republican na Democrat) chenye ustahiki wa kufanya hivyo, iwe ni chama cha serikali iliyoko madarakani hivi sasa au chama cha upinzani kwani vyama vyote hivyo viwili vimetenda jinai na kusababisha maafa ya kila namna duniani.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, dhambi kubwa iliyofanywa na chama kilichoko madarakani hivi sasa nchini Marekani, ni kuanzisha kanali za hatari mno za kigaidi na kusisitiza kwamba, chama cha serikali ya hivi sasa ya Marekani kimeanzisha kundi la kigaidi ambalo hivi sasa serikali hiyo hiyo ya Marekani inajifanya kulishambulizia na mahala pake kuweka kundi jingine la kigaidi jambo ambalo ni ushahidi wa wazi wa namna siasa zinavyotawala maadili.
Ameongeza kuwa: Serikali iliyopita ya Marekani ndiyo iliyofanya jinai na kusababisha maafa makubwa katika nchi za Iraq na Afghanistan kiasi kwamba mamilioni ya watu wasio na hatia wameuawa na hata maelfu ya wasomi na wanasayansi wa Iraq walisakwa na genge la mauaji la Black Water na kuuliwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kwa kuzingatia hayo tutaona kuwa hakuna chama chochote kati ya vyama hivyo viwili huko Marekani ambacho kina ustahiki wa kimaadili.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Sisi tunakabiliana na tawala za namna hii huko Marekani, hivyo ni kosa kudhani kuwa tunaweza kufikia maelewano na Marekani kupitia mazungumzo.
Aidha amesema kwa kusisitiza kwamba: Hilo ndilo linalonifanya asisitizie mara kwa mara wajibu wa kutofanya mazungumzo yoyote na Marekani kwani uzoefu umethibitisha kuwa badala ya kutafuta maafikiano, siku zote Wamarekani wanataka kuwatwisha wengine misimamo na maamuzi yao na mfano wa wazi ni matukio yaliyotokea hivi karibuni.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Brigedia Jenerali Dehqan. Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti fupi kuhusu kazi zilizofanyika katika viwanda vya ulinzi, kuanzisha kanali ya wafanyakazi wa wizara ya ulinzi na kuanzisha mawasiliano mazuri na ya kuendelea baina ya viwanda vya ulinzi na vyuo vikuu pamoja na mashirika ya elimu za kimsingi. Amesema, Leo hii sekta ya ulinzi nchini Iran kutokana na kustafidi vizuri na miundombinu ya kiufundi na elimu za kimsingi, ina uwezo wa kudhamini mahitaji yote yanayotakiwa na vikosi vya ulinzi nchini.
 
< Nyuma   Mbele >

^