Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina Chapa
14/12/2016
Imam Khamenei meets with the head of the Palestinian Islamic Jihad movementAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo mchana (Jumatano) ameonana na Bw. Ramadhan Abdullah, Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina na ujumbe alioandamana nao na kusisitiza kuwa: Pamoja na kuweko njama nyingi na za mfululizo za waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni wa Israel za kuzusha migogoro ya kila namna ili kulisahaulisha suala la Palestina, lakini ardhi hiyo takatifu itakombolewa kwa baraka za muqawama na jihadi ya wananchi na makundi ya Kipalestina.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewapongeza Wapalestina kwa moyo wao wa kiimani na wa kusimama kidete wa kupigania malengo yao matakatifu na kuongeza kuwa, njia pekee ya kuikomboa Quds Tukufu ni mapambano na muqawama kwani njia nyingine zote ni tasa na hazina mwisho mwema.
Vile vile ameelezea kufurahishwa kwake na pendekezo la mada 10 la harakati ya Jihadul Islami ya Palestina kwa ajili ya kuleta umoja na kuimarisha muqawama wa kupambana na Wazayuni na kuongeza kuwa, kutilia mkazo mapambano, kupinga kikamilifu mikataba yote ya mapatano na Wazayuni na kusisitizia umoja na mshikamano baina ya mkundi ya Palestina sambamba na kulaani njama za baadhi ya nchi zenye fikra butu za kutaka mapatano na adui, ni miongoni mwa nukta muhimu za mpango huo uliopendekezwa na harakati ya Jihadul Islami ya Palestina.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kwamba, kuna wajibu wa kuhakikisha kuwa, mpango huo unatekelezwa na kukumbusha kwamba, bila ya shaka yoyote kuna baadhi ya watu wamepewa kazi ya kuzuia kutekelezwa mada na vipengee hivyo kumi vya pendekezo hilo la Jihadul Islami, hivyo inabidi kuwa macho ili mpango huo usiishie tu kwenye karatasi na kusahauliwa pole pole hata kabla ya kuanza kutekelezwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, msababishaji mkuu wa matatizo ya eneo la Mashariki ya Kati ni beberu na shetani mkubwa yaani Marekani na huku akigusia namna vishetani vidogo vidogo navyo vinavyojiingiza kwenye migogoro hiyo amesema, lengo kuu la shetani mkubwa na vishetani hivyo vidogo ni kuhakikisha kuwa kadhia ya Palestina inasahauliwa kabisa; au umuhimu wake unafifia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, licha ya kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inashughulikia baadhi ya matukio ya eneo hili, lakini daima imekuwa ikitangaza wazi kwamba, Palestina ndiyo kadhia kuu ya ulimwengu wa Kiislamu na inatekeleza vilivyo jukumu lake katika uwanja huo.
Aidha ameashiria majukumu ya makundi ya Palestina, maulamaa, wasomi, wanafikra na waandishi wa nchi za Kiarabu katika kulibakisha hai suala la Palestina kwenye fikra za walio wengi duniani amesema: Kuna wajibu wa kuanzishwa anga ya kifikra na mijadala ya umma katika ulimwengu wa Kiislamu kuhusiana na kipaumbele cha kadhia ya Palestina na kufanyike juhudi za ziada kwa namna ambayo wale viongozi wa baadhi ya nchi wanaopigania mapatano na adui waingie woga mbele ya radiamali ya wananchi wao.
Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia pia njama za Marekani na waitifaki wake wa kieneo za kuzusha mizozo ya kila namna na kutumia hitilafu za kimadhehebu kuwagombanisha Waislamu kwa shabaha ya kuisahaulisha au kuififiliza kadhia ya Palestina na kuongeza kuwa: Kinyume kabisa na propaganda hizo za maadui, Waislamu wa Kisuni wa Halab (Syria), Mosul (Iraq) na miji mingine iliyovamiwa na magenge ya wakufurishaji watenda jinai, wameuliwa kwa umati na magenge hayo hivyo, migogoro iliyozushwa kwenye eneo hili haina uhusiano wowote na Usuni na Ushia.
Amesema, jukumu kubwa lililopo hivi sasa ni watu wote kusimama kidete kupambana na makundi ya kitakfiri kama vile Daesh, Jabhatun Nusra na magenge mengine ya kigaidi kwani kama hilo halitatendeka, basi makundi hayo yataendelea kuzusha migogoro wakati wote na hatimaye kadhia ya Palestina itatupwa pembeni.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia njama za mfululizo na zisizosita za mabeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kwamba: Sisi tuna yakini ya nyoyoni kuwa Mwenyezi Mungu Yuko pamoja nasi na tunaendelea kutekeleza vizuri majukumu yetu katika nyuga zote na hatuogopeshwi na upinzani wa dola lolote la kibeberu.
Vile vile ameyataka makundi ya Palestina yawe macho na yatambue kuwa maadui wanafanya njama muda wote za kuzusha mizozo na migogoro kati ya makundi ya Palestina. Amesema, umuhimu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina hivi sasa ni mkubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote uliopita.
Katika mkutano huo, Bw. Ramadhan Abdullah, Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amemshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kutokana na misimamo yake ya kishujaa, kihekima na busara na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na ndugu wa Kiislamu wa Hizbullah ya Lebanon kwa malengo matakatifu ya taifa madhlumu la Palestina na kuashiria hali mbaya iliyopo hivi sasa kwenye eneo la Mashariki ya Kati na kusema: Inasikitisha kuona kuwa, baadhi ya tawala za nchi za Kiarabu zimeitelekeza kadhia ya Palestina na zinashindana na kupigana vikumbo katika kujipendekeza na kujenga uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.
 
< Nyuma   Mbele >

^