Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Sherhe ya Hadithi Chapa
20/02/2008

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Kinachokuja hapa ni sehemu ya hadithi za Bwana Mtume Muhammad SAW na Ahlul Bayt Watoharifu AS zilizojaa johari za balagha na ufasaha ambazo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezichagua kutoka katika vitabu vyenye itibari (vyenye kutegemewa) kwa ajili ya kufungulia darsa zake za khariji za fikihi na kuzifafanua na kuzichambua kwa muhtasari.

Kwa vile lengo letu ni kutoa faida zaidi, tumeona ni bora kwanza tuzilete baadhi ya darsa hizo katika ukurasa huu wa Sherhe ya Hadithi na baadaye kila wiki mara moja au kila siku katika ukurasa wa mbele  katika siku za usoni.

Sehemu ya kwanza ya darsa hizo ambayo ni hadithi zenye nasaha za Bwana Mtume SAW, zimechaguliwa kutoka katika kitabu cha Tuhafu 'l-Uqul kwa ajili ya wapenzi wa Mtume Muhammad na Ahlul Bayt wake (rehema na baraka za Allah ziwe juu yao).

• Nasaha na mawaidha ya Mtume Muhammad SAW
• Mawaidha na maneno ya hekima ya Amiru 'l-Muuminin Imam Ali AS
• Mawaidha na miongozo ya Imam Zainul Abidin AS

Nasaha na Mawaidha ya Mtume Muhammad SAW

Mtume Mtukufu SAW amesema:

{من اكل ما يشتهي ولبس ما يشتهي وركب مايشتهي لم ينظر اللّه اليه حتى ينزع او يترك}

 

"Alaye anachopenda na kuvaa anachopenda na kupanda anachopenda, Mwenyezi Mungu hatomwangalia mpaka ajivue na aache."
(Tuhafu 'l-Uqul, uk. 38)

Katika kirai kinachosema, rakiba maa yashtahi, kuna uwezekano kwamba maana yake hasa ni neno "kutamani" kwa maana ya kupanda kila kipando apendacho na achaguacho mtu. Kuna uwezekano ibara hii ikawa na maana nyingine ya rakiba 'l- amr, yaani mtu kufanya jambo lolote apendalo. Alaakullihali, fadhili za Mwenyezi ndiyo asili ya kheri zote na ni chimbuko la ukamilifu wote wa binadamu katika ulimwengu wa uwepo. Kwa kuyafanya mambo hayo mtu hukosa (fadhila hizo), na kama ni kuyaacha hayo basi kuwe ni kujinyima na kujitenga nayo kwa hiari - yaani mtu kuwa anatamani kufanya mambo fulani na anao uwezo wa kuyatenda, lakini hujiweka mbali nayo. Wale watu ambao hawana uwezo wa kuyapata matamanio yao yote wanapaswa wathamini na washukuru neema hiyo, kwani ni neema kubwa mtu kukosa fursa na uwanja mpana licha ya kuwa na hawaa na matamanio ya nafsi - tabaan akiweza kukabiliana na matamanio hayo atapata thawabu nyingi.

Darsa ya 19 - 3/10/1999 (11/7/1378)

Mtume Mtukufu SAW amewaidhi:

{الدنيا دُوَل، فما كان لك أتاك على ضعفك وما كان منها عليك لم تدفعه بقوّتك ومن انقطع رجاءه مما فات، استراح بدنه ومن رضي بما قَسَمه اللّه قرّت عينه.}

 

"Dunia ni mzunguko (duwal), kilicho chako hukujia licha ya udhaifu wako, na kilicho na madhara kwako huwezi kukiondoa licha ya nguvu zako. Mwenye kukata matumainio yake kwa kilichopita hutuliza mwili wake, na mwenye kuridhika na alichoruzukiwa na Mwenyezi Mungu hufurahisha macho yake."
(Tuhafu 'l-Uqul, uk.40)

Duwal ni wingi wa dawlah, na maana yake ni kitu kitokacho mkono huu hadi mkono ule. Maumbile ya dhahiri ya dunia yamo katika hali ya kubadilikabadilika. Tusidhani kuwa mali, cheo, suhula, afya na uzima tulio nao (hivi sasa) tutakuwa nao hadi mwisho wa umri wetu. Si hivyo! Mara nyingi tumeshuhudia vitu vingi vikitutoka. Makusudio ya (neno) dunia hapa ni kwamba kila anayekata matumaini yake ya dunia huwa amejiondolea wasiwasi. Dunia ni chukizo na shutumivu (madhmum). Yaani ni kitu ambacho binadamu hujikumbizia mwenyewe kwa hawaa yake. Muradi hapa si yale mambo matukufu, neema za Akhera wala si yale mambo ambayo mtu inabidi ayapate kwa ajili ya kufanikishia jukumu fulani. Vilevile makusudio hapa si yale mambo ya ujenzi na utengenezaji wa dunia.
Darsa ya 20 - 7/11/1999 (16/8/1378)

Mtume Mtukufu SAW amesema:

{ثلاثٌ من كنّ فيه استكمل خصال الإيمان:الذي إذا رضي، لم يُدْخِله رضاه في باطلٍ وإذا غَضِبَ لم يخرجه الغضب من لحقّ وإذا قدر لم يتعاط ما ليس له.}

 

"Mambo matatu anapokuwa nayo mtu hukamilika imani yake: Anaporidhia ridhaa yake haimtumbukizi katika batili, anapoghadhibika ghadhabu zake hazimtoi katika haki, na anapokuwa na uwezo hachukui kisicho chake."

(Tuhafu 'l-Uqul, uk. 43)

Maana ya riwaya hiyo si kwamba imani inapatikana katika mambo hayo matatu tu, bali maana yake ni kwamba mtu yeyote aliye na sifa hizo tatu katika nafsi yake, basi sifa zote za imani huwa zimekusanyika ndani yake. Kwani kila moja ya mambo hayo matatu linakusanya sifa nyingi njema ndani yake. Furaha na mapenzi ya mtu yasimsukume kwenye batili na yasiwe sababu ya kumtetea na kumlinda kinyume cha haki. Vilevile ghadhabu zake zisimfanye atende maovu na kutoka katika haki. Aidha wakati anapokuwa na uwezo na nguvu, zisimlenge kufanya mambo ambayo si ya haki kwake kuyatenda.
Darsa ya 21 - 8/11/1999 (17/8/1378)


Mtume Mtukufu SAW amesema:

{الحياءُ حياءان، حياءُ عقلٍ وحياء حُمْقٍ، وحياء العقل العلم وحياءُ الحُمقِ الجهل.}

"Haya ni haya mbili: haya ya kiakili na haya ya kipumbavu; na haya ya kiakili ni elimu na haya ya kipumbavu ni ujinga."
(Tuhafu 'l-Uqul, uk. 45)

Haya za akili ni zile ambazo mtu huona haya kwa kutumia akili, kama vile kutahayari wakati wa kutenda dhambi, au kuwa na uso wa haya mbele ya watu ambao ni wajibu kwake kuwaheshimu. Haya ya aina hiyo huwa ni haya ya elimu, yaani ni mwendo wa kielimu. Amma haya ya ujinga ni ile ya mtu kuona haya kuuliza, kujifunza, au kufanya ibada na mifano kama hiyo. (Kwa mfano, wapo watu ambao huona haya kusali [mbele ya watu] katika baadhi ya mahali). Haya za aina hiyo ni mwendo wa kijinga.
Darsa ya 22 - 9/11/1999 (18/8/1378)


Mtume Mtukufu SAW amesema:


{خياركم أحسنكم أخلاقاً، الذين يَألفون ويُؤلفون.}

"Wale walio bora wenu ni wenye tabia nzuri kuliko wote ambao wanaamiliana vyema na kuamiliwa vizuri na watu."
(Tuhafu 'l-Uqul, uk. 45)

Wabora wenu ni wale watu ambao miamala yao na watu ni bora kuliko wengine. Wana nyuso za bashasha zinazowavutia watu na kuwafanya wawapende, wawazoee na kufanya urafiki nao. Maana ya hadithi hapo si kwamba mtu asiyeshikamana na (mafundisho ya) dini lakini akawa mchangamfu ni bora kuliko mtu anayetekeleza majukumu yake kidini lakini asiwe mchangamfu. Hapana bali muradi wa hadithi ni kwamba muumini ambaye anatekeleza majukumu yake ya kidini na akawa na tabia njema, ni bora kuliko muumini anayetekeleza majukumu yake ya kidini lakini asiwe na tabia nzuri.
Darsa ya 23 - 14/11/1999 (23/8/78)

 

 

^