Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
ROHO YA TAWHIDI Chapa
20/02/2008

Kifuatacho ni kitabu cha ROHO YA TAWHIDI Kutomwabudu Asiyekuwa Allah kilichotungwa na Ayatullah Udhma Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Unaweza kupata maelezo kamili kuhusu mtungaji kwa kusoma wasifu wake katika tovuti hii hii.

 

********

Huenda unaelewa kwamba utamaduni wa Kiislamu na fasihi yake umetajirika kwa maneno mahsusi na ya asili kwa sababu chemchemi yake — ambayo ni Qur'ani, Kitabu cha Mwenyezi Mungu — hububujisha maneno hayo na kuufurisha. Kwa hivyo, huwa ni vigumu kuyazuia mafuriko hayo katika maziwa ya lugha nyinginezo. Inatubidi tuchimbe mifereji kadhaa ili kupunguza uzito na kuhifadhi mito. Na hilo ndilo tulilolifanya. Wakati wowote tulipoona kwamba haiwezekani kutumia neno fulani na wakati huohuo likatoa maana hasa iliyokusudiwa katika lugha ya asili ya Kiarabu na katika istilahi ya Qur'ani, hapo tukmetumia neno lake laasili na kulifafanua katika ukurasa wa msamiati na istilahi. Kwa njia hii, utaelewa vizuri maudhui na ujumbe uliokusudiwa katika kitabu hicho, na kwa wakati huohuo utatajirisha msamiati wako wa Kiislamu. 

************ 

MSAMIATI 

adilisha: tendea haki, wema na uadilifu.
daawa:utangazaji wa mafundisho ya dini ya Kiislamu; tablighi,   uhubiri.  Mwanadaawa:   mtu   anayetangaza   mafundisho   ya   dini   ya   Kiislamu; mubalighi; mhubiri.
dhahania: —a mawazo.
hasi:—a kukana; —a kinyume kabisa.
irfani:mafundisho au imani inayohusiana na maarifa ya hakika ya Mwenyezi Mungu yapatikanayo kwa njia ya mtu kujisahau nafsi yake na kumwabudu Mwenyezi Mungu tu; usufii; uwalii.
maada: asili au dhati ya kila kitu; meta.
maadili: (elimu inayohusiana na) tabia njema au mwenendo sahihi wa mtu; akhlak.
mantiki:hekima; kauli; fani ya utumiaji wa akili.
maono:fikra, ufahamu au uonaji wa kimoyomoyo (wa dini moja au mfumo mmoja wa kiitikadi) juuya ulimwengu mzima, viumbe na vitu; nadharia.
metafizikia:elimu   ihusikanayo   na  asili   ya  mwanzo  wa uhai, Uungu, n.k.
nara:matamko mafupi au mwito maalum wa kikundi cha  watu, chama  au  dini  ambao unatolewa aghlab katika medani   za   vita,   mikutano, misafar, n.k. kwa lengo la kutia shime, kuhamasisha au kutangaza shabaha yake, n.k, Pia shaari, kaulimbiu. 
radiamali:jambo au kitendo kinachofanywa kurudia kitendo fulani kilichotendwa; majibu ya kitendo kilichotendwa.
shaari:Taz. nara.
shirki:hali ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kiumbe au kitu chochote katika ibada, uumbaji na tadbiri Yake ya ulimwengu; ushirikina.
stadhaafika:kuwa katika hali ya kukandamizwa kiuchumi, kisiasa, kiitikadi au kiutamaduni. Ustadhaafu: hali ya kustadhaafika. Mstadhaafu: (wastadhaafu/mustadhaafina): mtu mwenye kukandamizwa kiuchumi, kisiasa, kiitikadi au kiutamaduni; mnyonge; mwenye kudhoofishwa au kustadhaafishwa.
takabari:(stakabari): fanya jeuri au kiburi na kuona wengine si kitu; kandamiza watu kiuchumi, kisiasa, kiitikadi au kiutamaduni. Utakabari (ustakabari): hali ya kutakabiri au kustadhaafisha. Mtakabari/mstakabari (watakabari/wastakabari): mtu mwenye kukandamiza watu kiuchumi, ksiasa, kiitikadi au kiutamaduni.
taghuti:(ma-) kitu au kiumbe ambacho ni sababu ya uasi au uvunjaji wa sheria za Mwenyezi Mungu, k.v. miungu, utawala wa haramu, n.k.; mtu yeyote anayefuatwa bila ya idhini ya Mwenyezi Mungu; mtu anayependelea mambo yenye kukiuka mipaka (sheria za Mwenyezi Mungu). 
tasnifu:ithibati; maandiko ya kitaaluma yanayochanganua mada maalumu, agh. kwa ajili ya kupata shahada ya juu (thesis).
Tawhidi:Umoja na Upweke wa Mwenyezi Mungu katika dhati, sifa, vitendo na ibada Zake.

  

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu 

Siku ambayo Mtume wa Uislamu, Muhammad SAW, alipotangaza mwito (nara) wa : (لا اله الا الله) ("Hakuna mungu ila Allah") ili kuwaokoa wanadamu, watu wa kwanza waliosimama kumpinga walikuwa viongozi, wakuu na watu watukufu wa makabila. Mwanzoni, maadui hao walitumia silaha ndogo sana, yaani kumfanyia mzaha na kumtukana, lakini baadaye kila harakati ya Kitawhidi ilipozidi kuimarika na kuratibika, silaha zao pia zikawa kali zaidi. Watu wengine pia walishawishiwa na wapinzani hao, na wakasimama kumpinga na kumfanyia uhasama Mtume Mtukufu na wafuasi wake; na kwa mara nyingine tena mandhari ya kifedheha katika historia iliyokuwepo katika miaka ya kumi na mitatu kabla ya Hijria ikakaririwa.

Uhakika huu wa kihistoria unahitaji kuchunguzwa kwa makini sana kwa ajili ya kuufahamu Uislamu kwa jumla, na hasa Tawhidi ambayo ni kiini cha mafundisho ya Kiislamu.

Katika zama zetu, mojawapo kati ya mambo yenye kusikitisha sana ambalo ni msiba mkubwa kwa zama zetu, ni kupotoshwa maana halisi ya ujumbe wa Mitume wa Mwenyezi Mungu ambayo ni Tawhidi. Kupotoshwa maana ya Tawhidi ni kupotosha msingi halisi wa mafundisho ya dini, kwa sababu hakuna itikadi yoyote nyingine katika historia nzima ambayo inaweza kwa kadiri hii kuwaokoa watu na kuwakomboa waliokandamizwa.

Kwa kadiri tunavyojua, ujumbe wote wa Mitume ulikusudiwa kuleta mabadiliko ya kimapinduzi kwa faida ya watu, kuwakomboa wanyonge na wanaokandamizwa, na kupinga udhalimu, ubaguzi na uonevu. Kiini cha maadili ya dini zote kuu, kama alivyosema Erich Fromm, ni kuthibitika malengo ya elimu, mapenzi ya kindugu, kupungua shida za watu, uhuru na hisia za majukumu. (Hapana shaka kwamba malengo yaliyo bora zaidi hayawezi kutambuliwa kwa macho ya mchunguzi wa kimaada.)

Malengo yote hayo yanategemea msingi wa Tawhidi. Kwa kupiga nara ya Tawhidi, Mitume walikuwa wakitangaza makusudio na malengo yao yote, na kwa wakati huohuo, kwa kupiga nara hiyo walikuwa wakiandaa mapambano kwa ajili ya kutekeleza malengo hayo katika dunia au kuyakaribia.

Kwa hakika ni jambo la kusikitisha sana, si tu kwa wenye kuitakidi Tawhidi, bali hata kwa wale wote wenye kuyapigania malengo hayo, kuona kwamba katika zama hizi wakati ambapo malengo hayo huhitajika kwa haraka na kwa dharura zaidi — kuna ujinga na upotoshi wa msingi na maana ya Tawhidi, na kwamba watu hutosheka na tafsiri yake ya juujuu na ya kimawazo tu.

 

*************

 

Tumesema kwamba mkabala na upinzani uliokuwepo mwanzoni mwa Uislamu unaweza kufafanua uhakika muhimu wa maana halisi ya Tawhidi.

Uhakika wenyewe ni huu, kwamba shaari (nara) ya Laa ilaaha illallaah — ("Hakuna mungu ila Allah"), kwa hatua ya kwanza, ni pigo zito kwa walewale watu ambao walisimama kuipinga, yaani tabaka la wenye mamlaka na utawala katika jamii. Vitendo vya uhasama dhidi ya fikra moja na harakati moja, vinabainisha misimamo yake ya kijamii, kiwango na kina cha taathira zake katika misimamo hiyo. Kwa njia hii, tunaweza  kujua misimamo ya kitabaka na ya kijamii ya harakati hizo kwa kusoma nyuso za maadui wa harakati hizo. Vilevile tunaweza kupima kina na taathira za harakati hizo kwa kuangalia ushadidi na ukali wa upinzani wao.

Kwa sababu hii, njia mojawapo inayoaminika kutumiwa kwa ajili ya kutambua barabara daawa za Mitume, ni kuzichunguza safu za waungao mkono na safu za wapingao harakati hizi.

Tunapoona kwamba tabaka la wenye nguvu na mamlaka katika jamii ni watu wa kwanza waliosimama kupinga dini bila ya kusita hata kidogo katika upinzani wao, hapo ndipo tunapotambua waziwazi kwamba kwa kawaida dini na harakati za kidini zinapinga tabaka hilo. Kimsingi, Mitume walikuwa wakipinga ujeuri na ubepari wao, na nafsi ya tabaka lenyewe ambalo lilikuwa likijitenga mbali na wengine.

Ili tuweze kuzingatia suala la Tawhidi katika kipengee hiki cha kuupinga utawala wa kitabaka katika jamii, ni lazima kwanza tujue kwamba kinyume na vile inavyodhaniwa na watu wa kawaida, Tawhidi si nadharia ya kifalfasa na kidhahania peke yake, bali ni nadharia ya kimsingi kuhusu binadamu na ulimwengu, na ni itikadi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa pia.

Miongoni mwa istilahi za kidini na zisizo za kidini, ni taabu sana kupata istilahi kama hii iliyojaa maana ya kimapinduzi na kiurekibishaji yenye kuzingatia vipengee mbalimbali vya kimaisha, kijamii na kihistoira vya binadamu. Haikuwa sadfa kwamba miito yote ya Mitume wa Mwenyezi Mungu katika historia nzima ilianzia kwa kutangazwa Upweke na Umoja wa Mwenyezi Mungu na umilikaji Wake Peke Yake.

Ufuatao ni muhtasari wa vipengee mbalimbali vya maudhui ya Tawhidi:

1) Tawhidi katika Kipengee cha Nadharia juu ya Ulimwengu na Maisha

a) Tawhidi maana yake ni umoja na ufungamano wa ulimwengu mzima na vitu vyote vilivyomo humo.

Ilivyokuwa mfumo wa uumbaji ni mmoja, na kila kltu kimeanza na kutokana na chanzo na asili moja bila ya kuwepo miungu na waumba wengi tofauti; hivyo, vitu vyote hivyo vinaingia katika mkusanyiko na mfumo mmoja,na ulimwengu mzima ni mmoja, na wote una mwelekeo mmoja.

مَّا تَرَى فِي خَلْقِ الرَّحْمَنِ مِن تَفَاوُتٍ فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَى مِن فُطُورٍ (الملك 3

"Huoni hitilafu yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa rehema." (alMulk, 67:3)

أَوَلَمْ يَتَفَكَّرُوا فِي أَنفُسِهِمْ مَا خَلَقَ اللَّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَأَجَلٍ مُّسَمًّى...(الروم 8

"Je, hawatafakari juu ya nafsi zao? Allah hakuumba mbingu na ardhi, na vilivyomo baina yao ila kwa [mfumo wa] haki na kwa muda maalum. "(ar-Rum, 30:8)

Kufuatana na mtazamo huu, ulimwengu huonekana kama msafara mmoja ambao wasafiri wake wote hufanya kazi kwa pamoja kuelekea kwenye mahali na lengo moja kama mnyororo ulioshikamanishwa pamoja kwa vikuku na kama vipande vldogo na vikubwa vya mashine. Kila kitu katika mfumo huo hufanya kazi kufuatana na hali na nafasi yake, maana na sababu iliyowekewa. Hivyo, katika mwendo huu wa ukamilifu, kila kitu hukisaidia na kukikamilisha kitu kingine, na vyote ni vitu vya lazima katika mjumuiko huo. Kusimama, kuharibika, kupanguka au kwenda kombo kimojawapo katika vitu hivyo husababisha kuharibika, kuparaganyika na kwenda kombo mfumo mzima. Kwa  hivyo, ufungamano halisi na wa  kiroho wa mfumo mmoja ndio unaounganisha vitu vyote hivyo.

b) Tawhidi maana yake ni kuwepo shabaha katika uumbaji. Ulimwengu umeumbwa kwa mpango, hesabu na utaratibu maalum; na kila kitu chake kina maana na roho (dhati) pia. Kwa vile ulimwengu umeumbwa na Muumba Mwenye hekima, hivyo, ni lazima kuwepo hekima, lengo na shabaha katika asili ya kuumbwa kwake kama inavyoonekana katika vitu vingi vya hapa ulimwenguni.

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا لَاعِبِينَ (الانبياء 16)

"Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yao kwa mchezo na bila shabaha]." (al-Am-biyaa, 21:16)

Kwa mtazamo huu, hakuna kitu chochote katika ulimwengu kilichoumbwa bila ya kuwa na shabaha au maana yoyote, bali mfano wake ni kama mashine iliyotengenezwa kwa ajili ya kufanya kazi maalum. Tunaweza kuuliza kuhusu shabaha yake, lakini hatuwezi kuuliza kuhusu asili ya shabaha hiyo. Mfano wake ni kama shairi moja la maana ambalo unaweza kulifahamu kwa kuzingatia maana yake, lakini huwezi kulifahamu kwa kutegemea sauti au mizani yake tu.

c)Tawhidi maana yake kubwa zaidi ni kunyenyekea vitu na viumbe vyote vya ulimwengu mbele ya Mwenyezi Mungu.Hakuna kitu chochote katika mkusanyiko huo chenye hiari yake yenyewe. Kanuni zote za ulimwengu (maumbile) na kila kitu kinachofuata kanuni hizo ni lazima kitii, kijitolee na kisalimu amri kwa Mwenyezi Mungu tu. Kwa hivyo, kuwepo kanuni za kimaumbile katika ulimwengu mzima hakumaanishi kwamba hakuna Mwenyezl Mungu na Muumba wa ulimwengu.

إِن كُلُّ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ إِلَّا آتِي الرَّحْمَنِ عَبْدًا.( مريم 93)

"Hakuna yeyote aliyemo mbinguni na ardhini ila atafika kwa Mwingi wa rehema hali ni mtumwa." (Maryam, 19:93)

بَل لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ كُلٌّ لَّهُ قَانِتُونَ. (البقرة 116)   

"Bali ni Vyake vyote vilivyomo mbinguni na ardhini. Vyote vinamnyenyekea Yeye." (al-Baqarah, 2:116)

وَمَا قَدَرُوا اللَّهَ حَقَّ قَدْرِهِ. وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّماوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَى عَمَّا يُشْرِكُون. (الزمره 67)

"Na hawakumheshimu Allah heshima anayostahiki, na (katika) Siku ya Kiyama ataidhibiti ardhi yote, na mbingu zitakunjwa kwa uwezo Wake. Ameepukana na upungufu na Yu mbali na yale wanayomshirikishiya." (az-Zumar, 39:67)

2) Tawhidi katika Kipengee cha Uchunguzi na Uamuzi kuhusu Binadamu

a) Tawhidi maana yake ni kwamba wanadamu wote ni wamoja na ni sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Yeye ni Mola wa wanadamu wote. Hakuna mtu aliye na uhusiano mahsusi na Mwenyezi Mungu kwa sababu ya umbile lake la kibinadamu tu, wala hakuna mwenye ujamaa Naye. Yeye si Mungu wa taifa, umma au kabila fulani. Hakuumba wala hakufadhilisha jamii moja kuliko nyingine. Wote ni sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Hakuna mtu mwenye utukufu mahsusi mbele ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kutokana na jitahada zake. Kila mtu anaweza kupata utukufu na fadhila za Mwenyezi Mungu akijitahidi zaidi kutoa huduma njema kwa wanadamu na kwa kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu ambayo ni dhamana ya pekee ya kumtukuza binadamu.

وَقَالُواْ اتَّخَذَ اللّهُ وَلَدًا سُبْحَانَهُ بَل لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ كُلٌّ لَّهُ قَانِتُون. (البقرة 116

"Wanasema!   'Allah   amejipangia mwana.' Ameepukana na hilo; bali ni Vyake vyote vilivyomo mbinguni na ardhini.  Vyote vinamnyenyekea Yeye." (al-Baqa-rah, 2:116)

فَمَن يَعْمَلْ مِنَ الصَّالِحَاتِ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَا كُفْرَانَ لِسَعْيِهِ وَإِنَّا لَه كَاتِبُونَ. (الانبياء 94

"Na atakayefanya vitendo vizuri na hali ni muumini, basi haitokata/iwa juhudi yake; na kwa hakika Sisi tutamwandikia." (al-Ambiyaa, 21:94)

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَى وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ. (الحجرات 13

"Enyi watu! Kwa hakika tumekuumbeni nyote kutokana na mwanamume na mwanamke, na tumekufanyeni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika anayeheshimiwa sana miongoni mwenu mbele ya Allah ni yule anayemcha [Mungu] zaidi katika nyinyi." (al-Hujaraat, 49:13)

b)         Tawhidi maana yake ni kwamba wanadamu wote ni wamoja na ni sawa katika kuumbwa kwao na katika asili yao ya ubinadamu. Ubinadamu ni asili moja inayopatikana katika wanadamu wote bila ya kutofautiana. Wanadamu waliogawika katika matabaka mbalimbali ya kijamii si waja wala
viumbe wa waungu mbalimbali hata asili na maumbile yao yakatofautiana pia, na matokeo yake ukakuwepo mpaka usiovukika baina yao. Wala hakuna mungu wa tabaka aali (tukufu) aliye na nguvu zaidi kuliko mungu wa tabaka la chini. Wote ni viumbe wa Mwenyezi Mungu Mmoja, na
wote wameumbwa sawa katika maumbile yao ya asili.

(1 يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُواْ رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ (النساء 

"Enyi watu! Mcheni Rabi wenu Ambaye amekuumbeni katika nafsi moja." (an-Nisaa, 4:1)

c)         Tawhidi maana yake ni kwamba wanadamu wote ni sawa na wamoja katika kuweza kujiendeleza na kujikamilisha. Wanadamu wote ni sawa katika asili na maumbile yao ya kibinadamu. liivyokuwa Mwenyezi Mungu Mwenye hekima amempa kila mtu umbile la kibinadamu, hivyo, hakuna mtu yeyote asiyekuwa na uwezo katika dhati na umbile lake wa kufuata njia iliyonyooka na njia ya kujikamilisha. Kwa sababu hii ndiyo maana mwito wa Mwenyezi Mungu ukawa ni kwa watu wote bila ya kuwa ni mahsusi kwa watu, taifa au tabaka fulani. Ingawa mazingira tofauti yanaleta athari tofauti kwa binadamu, lakini athari hasi za mazingira haziwezi kabisa kumfanya binadamu awe shetani au malaika daima, au kumfungia njia ya kujiamulia yeye mwenyewe. Qur'ani inamhutubu hivi Mtume Mtukufu:

 

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ. (سبإ 28

"Na hatukukutuma [kwa jamii mahsusi tu] ila kwa watu wote." (Sabaa, 34:28)

وَأَرْسَلْنَاكَ لِلنَّاسِ رَسُولاً. (النساء 79

"Na tumekutuma kwa watu wote kuwa Mtume." (an-Nisaa, 4:79)

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءكُم بُرْهَانٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَأَنزَلْنَا إِلَيْكُمْ نُورًا مُّبِينًا.  فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُواْ بِاللّهِ وَاعْتَصَمُواْ بِهِ فَسَيُدْخِلُهُمْ فِي رَحْمَةٍ مِّنْهُ وَفَضْلٍ وَيَهْدِيهِمْ إِلَيْهِ صِرَاطًا مُّسْتَقِيمًا. (النساء 175/174)

"Enyi watul Imekufikieni hoja kutoka kwa Rabi wenu, na tumekuteremshieni nuru dhahiri; ama wale waliomwamini Allah na kumshika barabara, basi atawaingiza katika rehema Zake na fadhila, na kuwaongoza Kwake kwenye njia iliyonyooka." (an-Nisaa, 174, 175)

d) Tawhidi maana yake ni kuwakomboa wanadamu wote kutoka katika utumwa na unyenyekevu wa yeyote asiyekuwa Mwenyezi  Mungu,  na  kwa   maana nyingine  ni ulazima (wajibu) wa kumwabudu Mwenyezi Mungu tu. Tawhidi inapinga mwanadamu kuingia katika utumwa na utiifu usiokuwa wa Mwenyezi Mungu. Kwa kuzingatia maana pana ya ibada, utumwa huo unaweza kuwa ni wa kifikra, kitamaduni, kiuchumi au kisiasa. Tawhidi inakataza kuishi maisha kama haya ya kujichukulia mtu mwingine kuwa ni mshirika na sawa katika ibada ya Mwenyezi Mungu. Tawhidi humchukulia binadamu kuwa ni mja wa Mwenyezi Mungu tu, na humkomboa kutoka katika utumwa na utiifu wa kila mtu, mfumo au nguvu yoyote ambayo humfanya amshirikishe katika ibada ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, Tawhidi maana yake ni kukubali utawala wa Mwenyezi Mungu tu na kukana na kupinga utawala wowote mwingine usiokuwa wa Mwenyezi Mungu, uwe na sura au umbo la aina yoyote.

 

إِنِ الْحُكْمُ إِلاَّ لِلّهِ أَمَرَ أَلاَّ تَعْبُدُواْ إِلاَّ إِيَّاهُ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ. (يوسف 40

"Hukumu (utawala) ni ya Allah tu, ameamrisha msimwabudu yeyote ila Yeye tu. Hiyo ndiyo dini iliyonyooka." (Yusuf, 12:40).

وَقَضَى رَبُّكَ أَلاَّ تَعْبُدُواْ إِلاَّ إِيَّاهُ. (الإسراء 23

"Na Rabi wako [Mwenye amri na utawala] amehukumu kwamba msimwabudu yeyote ila Yeye tu." (al-lsraa, 17:23)

e) Tawhidi maana yake ni kumheshimu na kumthamini binadamu. Umbile tukufu na la fahari la binadamu lina thamani zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu na wala halina haja ya kufanywa nyonge, dhalili au mtumwa mbele ya yeyote ghairi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu tu Mwenye ukamilifu na jamala mutlaki Ndiye Ambaye anastahiki kuabudiwa na binadamu, kusifiwa na kupendwa. Kutukuza huko ni daraja moja ya mja kupata utukufu.Ghairi ya Dhati Takatifu hakuna kitu wala kiumbe chochote chenye utukufu na hadhi ambayo kwayo inamstahikisha amfanye binadamu kuwa mtumwa wake. Masanamu yote yenye uhai na yasiyo na uhai ambayo yamejipachika katika fikra, moyo na kiwiliwili cha binadamu na yamechukua kwa nguvu utawala wa Mwenyezi Mungu katika maisha ya binadamu, ni najisi na uchafu unaochafua usafi wa umbile la binadamu. Masanamu hayo humletea binadamu madhila na uduni, hivyo, inambidi ayaangamize na ayasafishe katika ibada yake ili apate kurejesha hadhi yake tukufu. Hakuna mawazo yoyote ya kimaada ya binadamu yaliyoweza kujadili kwa undani na ufasaha utukufu na thamani ya binadamu, kama Tawhidi inavyojadili.

فَاجْتَنِبُوا الرِّجْسَ مِنَ الْأَوْثَانِ وَاجْتَنِبُوا قَوْلَ الزُّورِ. حُنَفَاء لِلَّهِ غَيْرَ مُشْرِكِينَ بِهِ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّهِ فَكَأَنَّمَا خَرَّ مِنَ السَّمَاء فَتَخْطَفُهُ الطَّيْرُ أَوْ تَهْوِي بِهِ الرِّيحُ فِي مَكَانٍ سَحِيقٍ. (الحج 31/30)

"Basi jiepusheni na uchafu wa masanamu na maneno ya uwongo; mhalisike kwa Allah bila kumshirikisha. Na anayemshirikisha Allah basi ni kana kwamba ameanguka kutoka mbinguni kisha ndege [tai] wakamnyakua au upepo ukamtupa mahali pa mbali." (al-Hajj, 22:30, 31)

لاَّ تَجْعَل مَعَ اللّهِ إِلَهًا آخَرَ فَتَقْعُدَ مَذْمُومًا مَّخْذُولاً. (الإسراء 22  

"Usimfanye mungu mwingine pamoja na Allah, usije ukawa mwenye kushutumiwa (na) kutupwa." (al-lsraa, 17:22).

وَلاَ تَجْعَلْ مَعَ اللّهِ إِلَهًا آخَرَ فَتُلْقَى فِي جَهَنَّمَ مَلُومًا مَّدْحُورًا. (الإسراء 39

"Wala usimfanye mungu mwingine pamoja na Allah, usije kutupwa katika Jahannam hali ya kuwa mwenye kulaumiwa (na) mwenye kufukuzwa." (al-lsraa, 17:39)

f) Tawhidi maana yake ni ulinganifu na umoja baina ya maisha ya binadamu na kuwepo kwake. Maisha ya binadamu yamefanyika kwa dhamiri na uhakika, fikra na amali (matendo).  Ikiwa kimojawapo kati ya vitu viwili hivo, au sehemu   moja  yake  itaathiriwa   na nguvu  zilizo   kinyume

cha  Uungu    kama vile dhamiri  ya  kumwamini  Mungu kuambatana na uhakika usiokuwa wa Kiungu, au uhakika wa kumpenda Mungu kuambatana na moyo wa kutomjua Mungu — basi matokeo yake yatakuwa ni kupatikana hali mbili zinazopingana katika maisha ya binadamu na kufanyika shirki   (ushirikina)   katika   kumwabudu   Mwenyezi  Mungu. Katika hali kama hiyo, binadamu huwa kama akrabu ya dira ambayo huelekea sehemu nyingine kwa sababu ya kuvutwa na mvutano usio wa kawaida, hivyo, kama haitoelekea kwenye ncha ya kawaida itaharibika. Kwa hivyo, ikiwa binadamu

atapotoka kwenye njia iliyonyooka na mwelekeo ulio sawa ambao ni umbile aliloumbiwa, basi atapotoka kwenye njia ya Mwenyezi Mungu.

أَفَتُؤْمِنُونَ بِبَعْضِ الْكِتَابِ وَتَكْفُرُونَ بِبَعْضٍ فَمَا جَزَاء مَن يَفْعَلُ ذَلِكَ مِنكُمْ إِلاَّ خِزْيٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يُرَدُّونَ إِلَى أَشَدِّ الْعَذَابِ. (البقرة 85

"Je, mnaamini baadhi ya Kitabu [maarifa na maamrisho ya dini] na kuyakataa mengine? Basi hakuna malipo kwa mwenye kufanya hivyo katika nyinyi ila fedheha katika maisha ya dunia, na Siku ya Kiyama watarudishwa kwenye adhabu kali kabisa." (al-Baqa-rah, 2:85)

g) Tawhidi maana yake ni kwenda sambamba binadamu na mazingira yake ya ulimwengu. Upana usio na kikomo wa ulimwengu ni uwanja wa amali na radiamali zisizohesabika za kanuni za ulimwengu. Hakuna tukio au jambo lolote, liwe dogo vipi, ambalo linaweza kuepukana na kanuni hizo. Kutokana na ulingano, utaratibu na umoja wa kanuni za ulimwengu ndipo unapopatikana mfumo wenye utaratibu na umoja katika ulimwengu. Binadamu ni sehemu moja ya mfumo huo, hivyo, yeye pia hutawaliwa na kanuni hizo za kawaida  pamoja   na   kanuni  maalum  ambazo zinakwenda sambamba na kanuni nyinginezo. Lakini binadamu, kinyume cha viumbe vinginevyo ambavyo vinalazimika kufuata maumbile bila ya kuwa na hiari yoyote, ana uwezo wa kuchagua na kujiamulia mambo yake mwenyewe. Inambidi binadamu achague njia ya asili na ya umbile lake ambayo ndiyo njia inayomnyanyua, kumwendeleza na kumkamilisha. Hii pia ina maana kwamba ana uwezo wa kwenda kinyume na njia hiyo ya umbile (fikra).

فَمَن شَاء فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاء فَلْيَكْفُرْ (الكهف 29)

"Basi anayetaka aamini, na anayetaka akufuru." (al-Kahf, 18:29)

Tawhidi humtaka binadamu afuate njia ya kiasili na ya kimaumbile ambayo pia inafuatwa na ulimwengu mzima. Binadamu akiwa ni kiungo muhimu katika ulimwengu, hujitahidi kujiunganisha na kujiambatanisha na viungo vingine vya ulimwengu ili upatikane umoja na ufungamano kamili kati ya binadamu na ulimwengu.

أَفَغَيْرَ دِينِ اللّهِ يَبْغُونَ وَلَهُ أَسْلَمَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَإِلَيْهِ يُرْجَعُونَ. (آل عمران 83

"Je, wanataka dini ghairi ya Allah na hali kila kilichomo mbinguni na ardhini kinamtii Yeye kwa upendo au karaha, na Kwake watarejeshwa?" (Aali 'lmraan, 3:83)

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ يَسْجُدُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ وَالنُّجُومُ وَالْجِبَالُ وَالشَّجَرُ وَالدَّوَابُّ وَكَثِيرٌ مِّنَ النَّاسِ. (الحج 18

"Je, huoni kwamba kinamsujudia Allah kila kilichomo mbinguni na kilichomo ardhini, na jua na mwezi na nyota na milima na miti na wanyama na miongoni mwa watu walio wengi?" (al-Hajj, 22:18)

3 ) Tawhidi katika Kipengee cha Sera ya

Kijamii, Kiuchumi na Kisiasa

a) Tawhidi maana yake ni kwamba hakuna mtu yeyote ghairi ya Mwenyezi Mungu anayefaa peke yake kupanga na kuamua mambo ya ulimwengu na ya binadamu. Hii ni haki ya Mwenyezi Mungu tu Ambaye Ndiye Muumba wa binadamu na ulimwengu na Mratibu wa vitu vyake vyote. Yeye tu anajua uwezo na mahitaji yao yote. Kwa hakika, Yeye tu hujua kwa ukamilifu nguvu, uwezo na nishati zilizomo katika kiwiliwili na roho ya binadamu, na vilevile hazina zisizohesabika katika ulimwengu, kadiri na matumizi yake na vipi kuvisawazisha.

Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu Peke Yake tu Ndiye anayeweza kuratibu ratiba ya maisha ya binadamu na sera ya uhusiano wake katika mfumo wa ulimwengu. Yeye tu Ndiye anayeweza kupanga mifumo ya kisheria na kijamii katika maisha ya binadamu.

Haki hii ya pekee ya Mwenyenzi Mungu inatokana na uhakika huu wa kiasili na kimantiki kwamba Yeye ni Muumba. Kwa hivyo, uingiliaji wa aina yoyote katika kuamua sera ya kimatendo ya wanadamu utakaotokana na wengine, utakuwa ni sawa na kuingilia utawala wa Mwenyezi Mungu na kudai Uungu, na buko kutachukuliwa kuwa ni shirki.

فَلاَ وَرَبِّكَ لاَ يُؤْمِنُونَ حَتَّىَ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لاَ يَجِدُواْ فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُواْ تَسْلِيمًا. (النساء 65)

"Siyo, kwa haki ya Rabi wako! Hawatoamini mpaka wakufanye hakimu katika yale [mambo ya shabaha ya maisha] wanayohitalifiana kati yao, kisha wasione adha nyoyoni mwao juu ya uliyohukumu, na wanyenyekee kabisa." (an-Nisaa, 4:65)

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا  (الأحزاب 36)

"Si haki kwa mwanamume muumini wala mwanamke muumini kuwa na hiari katika mambo yao wakati Aliah na Mtume Wake wanapokata shauri; na mwenye kumwasi Allah na Mtume Wake, basi bila shaka amepotea upotofu ulio dhahiri." (al-Ahzaab, 33:36)

b) Tawhidi maana yake ni kwamba hakuna mtu yeyote aliye na haki ya kutawala na kusimamia jamii na maisha ya binadamu isipokuwa Mwenyezi Mungu tu. Utawala na usimamizi wa mtu mmoja juu ya mwingine kama utachukuliwa kuwa ni haki ya pekee isiyokuwa na jukumu lolote, hapana budi huleta udhalimu na uonevu. Jamii inawezekana kuepukana na udhalimu na upotofu ikiwa Nguvu Kuu, itaweka utawala na uongozi wa mambo ya jamii katika mikono ya mtu mmoja au kikundi cha watawala ambao watakuwa na majukumu yatakayoambatana na uwezo. Hiyo Nguvu Kuu, katika lugha ya kidini, ni Allah Mwenye ezi (Mwenyezi Mungu) Ambaye uwezo Wake na upana wa elimu Yake hauwezi kushindwa na uwezo au elimu yoyote.

لَا يَعْزُبُ عَنْهُ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ. (سبإ 3

"Hakifichikani Kwake kitu chochote (hata) kilicho na uzito wa chembe katika mbingu wala katika ardhi." (Sabaa, 34:3)

Sifa Zake za kuwa Mkali wa kuadhibu na Mlipizaji hazitoi fursa yoyote kwa wale aliowateua kupotoka kwenye njia Yake.

 

وَلَوْ تَقَوَّلَ عَلَيْنَا بَعْضَ الْأَقَاوِيلِ. } لَأَخَذْنَا مِنْهُ بِالْيَمِينِ. ثُمَّ لَقَطَعْنَا مِنْهُ الْوَتِينَ. (الحاقة 46-44)

"Na lau [Mtume] angelizua juu Yetu baadhi ya maneno, bila shaka tungelimshika kwa mkono wa kulia, kisha kwa hakika tungelimkata aorta. . . " (al-Haaq&h, 69:44-46)

Huyo Allah Mwenye ezi si kama umma au taifa ambalo linaweza kudanganywa au kumilikiwa; wala si kama chama kinachoweza kugeuzwa kuwa ni chombo cha kudhulumu na kukandamiza; na wala si kama viongozi na wakuu ambao wanaweza kununuliwa au kushirikishwa katika hiana.

Kwa kuzingatia kwa undani zaidi, ikiwa kupatikana umakini na utaratibu katika maisha ya binadamu kutalazimika vyombo vyote vinavyohusika na maisha vikutanike katika kitovu kimoja, na mambo yote yadhibitiwe na nguvu moja, basi nguvu hiyo haiwezi kuwa kitu kingine isipokuwa nguvu ya Muumba wa ulimwengu na binadamu.

Kwa hivyo, utawala na uongozi wa jamii ya binadamu ni haki mahsusi ya Mwenyezi Mungu. Utawala huo humilikiwa kupitia kwa wateule wa Mwenyezi Mungu ambao ni watu waliochaguliwa kufuatana na sifa na kipimo maalum kilichowekwa na dini ya Mwenyezi Mungu. Wale ambao sifa zao huafikiana na kipimo hicho, hushika hatamu ya utawala na hapo ndipo mfumo wa kidini wa kusimamia sheria za Mwenyezi Mungu unapothibitika na kutekelezeka.

قُلْ أَغَيْرَ اللّهِ أَتَّخِذُ وَلِيًّا فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَهُوَ يُطْعِمُ وَلاَ يُطْعَمُ قُلْ إِنِّيَ أُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ أَوَّلَ مَنْ أَسْلَمَ وَلاَ تَكُونَنَّ مِنَ الْمُشْرِكَينَ. (الأنعام 14

"Sema: 'Je, nifanye mtawala [msimamizi] ghairi ya Allah, Mwumba wa mbingu na ardhi, Naye hulisha wala halishwi?' Sema: 'Hakika mimi nimeamrishwa niwe wa kwanza katika wenye kutii [amri ya Mola],' na [nikaambiwa:] 'Usiwe miongoni mwa washirikina.'" (al-An'aam, 6:14)

إِنَّمَا وَلِيُّكُمُ اللّهُ وَرَسُولُهُ وَالَّذِينَ آمَنُواْ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلاَةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُمْ رَاكِعُونَ. (المائدة 55

"Hakika mwenye amri (utawala) juu yenu [Umma wa Kiislamuj ni Allah na Mtume Wake na wale walioamini ambao husimamisha sala na hutoa zaka, na hali ya kuwa wanarukuu. " (al-Maaidah, 5:55)

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ. مَلِكِ النَّاسِ. إِلَهِ النَّاسِ. (الناس 1-3)

"Sema: 'Najikinga kwa Rabi wa watu. Mmiliki (Mtawala) wa watu. Mwabudiwa wa watu.' " (an-Naas, 114:1-3)

c) Tawhidi maana yake ni kwamba umilikaji mutlaki na wa asili wa neema, maliasili na hazina zote za ulimwengu ni wa Mwenyezi Mungu Peke Yake. Mtu yeyote hana haki ya kumiliki peke yake kitu chochote. Kila kitu kimewekwa amana kwa binadamu ili akitumie kwa ajili ya kumsaidia katika mwendo wake wa kujikamilisha na kujiadilisha. Hairuhusiwi kwa mtu aliyeneemeka kuharibu, kuangamiza au kutotumia neema za dunia ambazo ni matokeo na matunda ya jitahada za maelfu ya viumbe na matukio. Neema hizo zisitumiwe katika njia yoyote isipokuwa kujiadilisha binadamu. Mali anayomiliki binadamu — ingawa ni kwa ajili yake — lakini kwa hakika amepewa na Mwenyezi Mungu, hivyo, ni lazima aitumie katika njia ambayo ameonyeshwa na Mwenyezi Mungu; nako ni kuitumia katika njia yake ya asili na ya kimaumbile, katika njia ambayo imeumbiwa. Kuitumia na kunufaika nayo katika njia yoyote nyingine ni kukwepa njia yake ya kimaumbile, nako huleta ufisadi.

Jukumu la binadamu katika utumizi wa anuwai za neema za Mwenyezi Mungu ni kutumia katika njia iliyo sahihi kwa lengo la kuzihuisha na kuzikamilisha.

} قُل لِّمَنِ الْأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُون. سَيَقُولُونَ لِلَّهِ قُلْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ.  ( المؤمنون 85-84)

"Sema: 'Ni ya nani ardhi na vilivyomo ndani yake, ikiwa nyinyi mnajua?' Watasema: 'Ni ya Allah!' Sema: 'Basi je, hamkumbuki?' " (al-Mu'minuun, 23:84, 85)

هُوَ الَّذِي خَلَقَ لَكُم مَّا فِي الأَرْضِ جَمِيعاً (البقرة 29

"Yeye Ndiye aliyeumba kwa ajili yenu [binadamu] vyote vilivyomo katika ardhi." (al-Baqarah, 2:29)

اعْبُدُواْ اللّهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَهٍ غَيْرُهُ هُوَ أَنشَأَكُم مِّنَ الأَرْضِ وَاسْتَعْمَرَكُمْ فِيهَا... (هود 61)

"Mwabuduni Allah; nyinyi hamna Mungu ghairi Yake. Yeye Ndiye aliyekuumbeni kutokana na ardhi, na akakukalisheni humo." (Huud, 11:61)

وَالَّذِينَ يَنقُضُونَ عَهْدَ اللّهِ مِن بَعْدِ مِيثَاقِهِ وَيَقْطَعُونَ مَآ أَمَرَ اللّهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الأَرْضِ أُوْلَئِكَ لَهُمُ اللَّعْنَةُ... (الرعد 25

"Na wale   wanaovunja  ahadi ya Allah   baada  ya kuifunga, na wanakataa aliyoyaamuru Allah yaunganishwe, na wanafisidi katika ardhi; hao ndio watakaopata laana na makao mabaya." (ar-Ra'd, 73:25)

d) Tawhidi  maana yake ni kwamba watu wote wana

haki sawasawa katika kutumia neema za ulimwengu. Uwezekano na fursa zote ni sawasawa kwa wanadamu wote ili kwamba   kila   mtu  aweze  kunufaika  na   neema  hizo  kwa kadiri ya haja yake na jitahada zake. Katika ulimwengu huu wa neema, hakuna eneo lolote lililowekwa kuhodhiwa na

kikundi fulani tu. Watu wote wanaweza kutumia hima na uwezo wao kunufaika na neema mbalimbali za ulimwengu huu. Katika kutumia fursa hii, hakuna ubaguzi wowote kwa sababu ya ukabila, rangi, jiografia, historia au hata itikadi (dini).

وَالأَنْعَامَ خَلَقَهَا لَكُمْ فِيهَا دِفْءٌ وَمَنَافِعُ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ. وَلَكُمْ فِيهَا جَمَالٌ حِينَ تُرِيحُونَ وَحِينَ تَسْرَحُونَ. وَتَحْمِلُ أَثْقَالَكُمْ... (النحل 7-5

"Na amewaumba wanyama [ngamia, ng'ombe na kondoo]', katika hao mnapata joto na manufaa na wengine mnawala. Na katika hao ni uzuri kwenu mnapowarudisha jioni na mnapowapeleka malishoni asubuhi, Na hubeba mizigo yenu..." (an-Nahl, 16:5-7)

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ مِنَ السَّمَاء مَاء لَّكُم... (النحل 10

"Yeye Ndiye anayekuteremshieni maji kutoka mbinguni...  (an-Nahl, 16:10)

يُنبِتُ لَكُم بِهِ الزَّرْع... (النحل11)

". . . Kwayo  hukuotesheeni mimea..." (an-Nahl,16:11)

وَمَا ذَرَأَ لَكُمْ فِي الأَرْضِ... (النحل 13

". . . Na alivyokuumbieni katika ardhi. . ." (an-Nahl, 16:13)

 اللَّهُ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَنْعَامَ لِتَرْكَبُوا مِنْهَا وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ. (غافر 79

"Allah Ndiye aliyekuumbieni wanyama ili muwapande baadhi yao na wengine wao muwale. " (Gha-afir, 40:79)

Katika aya hizo zinazofuatana mwanzoni mwa Sura an-Nahl, wanaozungumziwa ni wanadamu wote kwa jumla, bila ya kufadhilishwa kabila au taifa fulani, kama aya hizi zinavyoashiria pia:

... وَلَوْ شَاء لَهَدَاكُمْ أَجْمَعِينَ (النحل 9)

 

"Na   lau   angelitaka   bila  shaka   angelikuongozeni nyinyi [wanadamu] nyote. " (an-Nahl, 16:9)

إِلَهُكُمْ إِلَهٌ وَاحِدٌ... (النحم 22

"Mungu wenu [enyi wanadamu] ni Mungu Mmoja." (an-Nahl, 16:22)

*************

Hayo tuliyoyataja ni sehemu moja tu ya maana kubwa na pana ya vipengee tofauti vya Tawhidi. Muhtasari huu unaweza kufafanua waziwazi kwamba Tawhidi si nadharia tupu ya kifalsafa na kidhahania (kimawazo) isiyoweza kuwa ya kimatendo; au kusema kwamba haihusu maisha ya kila siku ya binadamu; au kwamba haiingilii kati katika kuamua malengo, jitahada na vitendo vya binadamu. Tawhidi haitoshi kuwa ni imani tupu inayoaminiwa na watu badala ya itikadi nyinginezo.

Kwa upande moja, Tawhidi ni mtazamo mzima juu ya ulimwengu, binadamu, msimamo wa binadamu juu ya matukio ya dunia, historia pamoja na uwezo, vipaji na mahitaji yake. Tawhidi inatazama malengo na mwongozo wa binadamu katika kujikamilisha na kujiadilisha.

Kwa upande mwingine, Tawhidi ni imani ya kijamii ambayo hupanga na huratibu mfumo ufaao wa mazingira ya binadamu, mazingira ambayo yatamwezesha kwa urahisi na haraka kujiendeleza kufikia utukufu na ukamilifu maalum. Ni pendekezo na kielelezo mahsusi kwa ajili ya jamii na huonyesha sera yake ya kiasili na kimsingi.

Kwa hivyo, wakati wowote sauti ya Tawhidi inapopaazwa katika jamii za kijahili au kishirikina (zilizosimama juu ya msingi wa kutojua uhakika wa binadamu), na jamii za kitaghuti (zilizosimama juu ya msingi wa kudhulumu thamaniza haki za binadamu), huleta mabadiliko ya kimapinduzi katika jamii, huhuisha na kuzindua nyoyo dhaifu na roho zilizokufa, hufanya mawimbi katika bahari iliyotulia ya jamii, na huisawazisha jamii iliyochafuka. Huleta mapinduzi na mabadiliko katika vyombo vya kinafsi, kiuchumi, kijamii, kimaadili na kibinadamu. Kwa ufupi, Tawhidi hushambulia hali iliyopo ya kijahili na nguvu zinazoilinda hali hiyo, na huondoa kabisa mazingira yanayostawisha hali hiyo.

Kwa hivyo, Tawhidi si ufumbuzi mpya peke yake katika masuala ya kinadharia na kiitikadi yenye matendo machache tu, bali ni njia mpya kwa binadamu ambayo licha ya kuchungua masuala ya kidhahania na kinadharia, hudhamiria kuratibu sera mpya kwa ajili ya matendo na maisha.

Kwa kufahamu jambo hili ndipo tunapoitakidi kwamba Tawhidi ni kiini na msingi wa dini ambao kwao jengo zima la dini husimama juu yake.

Kusema kwamba Tawhidi ni nadharia inayohusu metafizikia au ni tasnifu ya hali ya juu ya kimaadili na kiirfani peke yake, maana hii haiwezi kupewa itikadi kuu kama ya Kiislamu ambayo inatawala maisha nzima ya kijamii.

Hapana shaka kwamba katika kila zama walikuwepo watu ambao ingawa walimwamini Mwenyezi Mungu na waliitakidi Tawhidi, lakini walighafilika au walipuuza umuhimu wa itikadi hiyo katika matendo, na hasa jamii. Katika kila zama watu hao walio wepesi kuamini waliishi maisha yaliyokuwa sawa na maisha ya wasioamini Tawhidi; na kwa sababu hii ndiyo maana kwamba itikadi yao haikuleta mwamko wowote nyoyoni mwao kuhisi kwamba haiwezekani kwa mwenye kuamini Tawhidi kuafikiana na kujilinganisha na maisha yasiyokuwa na Kitawhidi; au kwamba haiwezekani kupata utulivu katika mazingira mazito na ya kubana ya ushirikina. Katika mwanzoni mwa kudhihiri Uislamu wakati mji wa Makka ulipokuwa ni kitovu na mji mkuu wa ushirikina na masanamu maarufu ya Waarabu, walikuwepo wafuasi wa dini halisi ya Ibrahim. Lakini kwa kuwa katika fikra zao Tawhidi haikuwa zaidi ya itikadi ya kidhahania na kiroho katika maumbile na matendo yao ya kibinafsi, hivyo, kuwepo kwao hakukuleta taathira yoyote ya kifikra na kijamii katika mazingira ya kijahilia (kishirikina). Kuwepo kwao hakukuhisika hata kidogo, na maisha ya kishirikina yaliendelea kwa salama na amani. Hao waumini wa Umoja wa Mwenyezi Mungu walikuwa wakiishi pamoja na washirikina bila ya kusumbuliwa na mila na desturi mbaya za maisha ya kishirikina. Aina hii ya mtazamo wa kidhahania wa Tawhidi ndiyo iliyowafanya wakose uwezo na satua muhimu katika maisha, na hasa maisha ya kijamii.

Katika mazingira kama hayo ndipo Uislamu ulipotangaza maana ya Tawhidi kuwa ni itikadi inayoahidi kutoa muundo mpya na mpana kwa ajili ya maisha ya kijamii. Katika hatua zake za kwanza, Uislamu ulionyesha sura yake kama ni ujumbe wa kimapinduzi kwa watu wote — waumini na makafiri. Wote walielewa kwamba ujumbe huo ulikuwa ni mfumo mpya wa kijamii, kiuchumi na kisiasa ambao haukubaliani na mifumo mingine iliyopo duniani. Uislamu uliyapinga mazingira yaliyokuwepo na badala yake ulisimamisha mfumo mpya.

Kwa sababu ya upambanuzi wake, waumini waliukubali ujumbe wake kwa hamu na shauku na wakajitolea kwa ajili yake; na kwa sababu hiyohiyo wapinzani na makafiri wa ujumbe wa Tawhidi waliupinga vikali na kila siku upinzani wao ulizidi.

Uhakika huu wa kihistoria unaweza kuwa ni kipimo kwa ajili ya kupima na kutathmini usahihi au utovu wa usahihi wa madai ya Tawhidi katika awamu zote za historia. Wakati wowote utakapoonekana kwamba madai ya Tawhidi yanayotolewa na watu yanafanana na madai ya wale waumini wa Umoja wa Mungu wa mjini Makka kabla ya kudhihiri Uislamu, hapo tutaweza kushuku ukweli wa madai yao ya kuitakidi Tawhidi. Tawhidi inayokubaliana na ibada ya masanamu na miungu ghairi ya Mwenyezi Mungu si Tawhidi tena, bali ni dhana iliyo kinyume cha Tawhidi iliyofundishwa na Manabii.

Kwa hivyo, kufuatana na maana halisi ya Tawhidi iliyofundishwa na Mitume, tunaweza kuelewa vizuri sababu ya Uislamu kusambaa na kuwa na nguvu katika siku za mwanzoni, na sababu ya kuzorota kwake katika zama za baadaye.

Mtume Muhammad SAW aliwaonyesha watu Tawhidi kama njia na mwongozo kwa ajili yao; lakini katika zama za baadaye, Tawhidi ikajadiliwa katika mahafali na mabaraza kama mawazo au dhanio. Katika zama za Mtume Mtukufu, Tawhidi ilikuwa ikiangaliwa kama mtazamo au ono jipya kwa ajili ya dunia na harakati kwa ajili ya maisha; lakini baadaye ikageuzwa kuwa maudhui ya kiitikadi tu kwa ajili ya kuchunguzwa na kujadiliwa na wanavyuoni wakati wa masomo na faragha. Katika zama za Mtume Mtukufu, Tawhidi ilikuwa ni msingi wa mfumo mzima na kitovu cha uhusiano wote wa kijamii, kiuchumi na kisiasa; lakini baadaye ikafanywa kuwa kama taswira nzuri iliyochorwa kwa usanifu kisha ikatundikwa kwenye ukuta wa maonyesho kama pambo. Jambo gani linaweza kupatikana kutoka katika pambo lisilokuwa na uhai?

**********************

Hayo tuliyokwishasema yanathibitisha wazi kwamba kwa mtazamo wa kimatendo, Tawhidi ni kama kalibu (kielelezo) ambayo kwayo jamii hupata umbo au sera ya kuishi. Ni jina la mfumo uliowekwa na dini ya Kiislamu na kufaa kabisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo makubwa ya binadamu. Kwa upande wa kinadharia, ni itikadi ambayo ni msingi wa kifalsafa wa mfumo huo.

Baada ya utangulizi huu, tunaweza kurejea yale tuliyoyasema mwanzoni na tukalichunguza suala hili katika kipengee maalum.

Tumesema kwamba wapinzani wa kwanza wa nara ya Tawhidi walikuwa ni viongozi na watu wenye fedha, nguvu na utukufu katika jamii; na hii inaonyesha kwamba upinzani mkubwa kuliko wote unatoka katika tabaka linalotawala na linalomiliki katika jamii ambalo linaitwa 'tabaka la wastakabari' katika Qur'ani. Tumesema kwamba mara tu miito ya Kitawhidi inapotolewa katika jamii katika zama yoyote na kutangazwa msimamo wake kwa tabaka la wenye utawala na wastakabari, basi hukabiliwa na radiamali mbili zinazotofautiana kutoka matabaka mawili yanayopingana katika jamii — hupingwa na hufanyiwa uadui na wastakabari, na hukubaliwa na huungwa mkono wa wastadhaafu (wanyonge).

Kwa hakika hali hii ya kuwepo radiamali mbili tofauti inaonyesha sura ya asili na ya kweli ya Tawhidi, na inamaanisha kwamba katika kila zama za zamani na baadaye, wakati Tawhidi inapotangazwa katika sura yake sahihi na maana yake halisi, basi hapana budi itakabiliwa na hali hiyo.

Sasa tuangalie ni kipengee kipi kati ya vipengee mbalimbali vya Tawhidi, kinapinga moja kwa moja maslahi na hata kuwepo kwa tabaka la wastakabari (madhalimu)? Kwa maana nyingine, kipengee kipi cha Tawhidi au pendekezo lipi la Kitawhidi kwa ajili ya jamii ambalo linapingwa kwa vikali sana na tabaka la wastakabari ?

Kujua sura za wastakabari katika Qur'ani kutasaidia sana kuelewa vizuri zaidi suala hili.

Katika zaidi ya mahali arobaini, Qur'ani inaonyesha sifa za kinafsi za wastakabari, hali zao za kijamii, ubarakala wao, na shabaha zao.

Kwa jumla, Qur'ani hubainisha sifa hizi za wastakabari:

a) Ingawa mstakabari (mustakbir) humwamini Mwenyezi Mungu kama ni uhakika wa kidhahania au wa kimila, au mwenye utawala wa kiasi fulani, lakini, kwa hakika, humkataa Mwenyezi Mungu kwa maana inayofahamika katika nara (shaari) ya Laa ilaaha illallaah — kwamba utawala na mamlaka yote inahodhiwa na Mwenyezi Mungu tu.

إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ يَسْتَكْبِرُونَ. (الصافات 35

"Hakika wao walipokuwa wakiambiwa: 'Hakuna mungu ila A llah,' walikuwa wakitakabari (wakikataa). " (as-Saafaat, 37:35)

b)         Mstakabari hapimi utukufu wa binadamu kwa mujibu wa kipimo sahihi cha ubora, bali hujichukulia mwenyewe kuwa ni bora na mtukufu kuliko watu wote kwa kutegemea kipimo cha kijahili (kishirikina) cha utajiri na nguvu.

... فَاسْتَكْبَرُوا فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَقَالُوا مَنْ أَشَدُّ مِنَّا قُوَّةً... (فصلت 15

"Basi walitakabari katika ardhi bila haki, na wakasema: 'Ni nani mwenye nguvu zaidi kuliko sisi?' " (Fussilat, 41:15)

c)         Kutokana na mawazo hayo batilifu, mstakabari hupinga aya za Mwenyezi Mungu ambazo ni ujumbe (ufunuo) kwa ajili ya kuunda mfumo mpya na vipimo vya thamani za kweli.

وَإِذَا تُتْلَى عَلَيْهِ آيَاتُنَا وَلَّى مُسْتَكْبِرًا كَأَن لَّمْ يَسْمَعْهَا كَأَنَّ فِي أُذُنَيْهِ وَقْرًا فَبَشِّرْهُ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. (لقمان 7

"Na' anaposomewa aya Zetu, huzipa mgongo kwa kutakabari, kama hakuzisikia, kana kwamba masikioni mwake mna uzito; basi mpe habari ya adhabu inayoumiza." (Luqmaan, 31:7)

d)         Mstakabari hupinga mwito wa Mtume wa kuleta mabadiliko na ukombozi kwa kutoa visingizio na kusema kwamba: "Lau (Mtume) angekuwa mkweli, tungemtambua mapema zaidi kuliko wengine," au kwamba: "Ni lazima Mwenyezi Mungu azungumze nasi moja kwa moja." Na kwa kutoa visingizio hivyo, husimama kupigana vita dhidi ya Mtume.

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا لَوْ كَانَ خَيْرًا مَّا سَبَقُونَا إِلَيْهِ... (الأحقاف 11

"Na waliokufuru waliwaambia walioamini: 'Lau [dini yao] ingelikuwa bora (kheri), wasingetutangulia kwayo [kuifuata].'" (al-Ahqaaf, 46:11)

 وَإِذَا جَاءتْهُمْ آيَةٌ قَالُواْ لَن نُّؤْمِنَ حَتَّى نُؤْتَى مِثْلَ مَا أُوتِيَ رُسُلُ اللّهِ... (الأنعام 124

"Na inapowafikia aya, husema: 'Hatuamini mpaka tuteremshiwe kama yate waliyoteremshiwa Mitume wa Allah.'" (al-An'aam, 6:124)

e)         Wastakabari humtuhumu mtangazaji (mwanadaawa) wa ujumbe wa Tawhidi kama mtu mwenye kutafuta cheo na maslahi, na kwa njia hii hutetea desturi zao za zamani zenye kuunga mkono tabaka lao ili apate kudhoofisha nguvu za mwito wa Tawhidi kati ya watu.

قَالُواْ أَجِئْتَنَا لِتَلْفِتَنَا عَمَّا وَجَدْنَا عَلَيْهِ آبَاءنَا وَتَكُونَ لَكُمَا الْكِبْرِيَاء فِي الأَرْضِ وَمَا نَحْنُ لَكُمَا بِمُؤْمِنِينَ. (يونس 78)

"Wakasema [kumwambia Musa]: 'Je, umetujia ili utuondoe katika [nyendo na mila] zile tulizowakuta nazo mababu zetu, ili ukubwa (na utawala) uwe wenu wawili katika nchi? Na sisi hatuwezi kukuaminini.' " (Yuunus, 10:78)

f)          Wastakabari hutumia nguvu, mabavu na ujanja kujaribu kuwaweka watu katika hali ya kunyonywa, utumwa na kutii bila ya sharti yoyote, na huwachochea wakatae na wapinge jitahada zozote za kuwakomboa ili wapate kuwaweka watu katika hali wanayoitaka wao. [Hivyo, katika Siku ya Kiyama, wanyonge ambao walikubali kudhulumiwa na wastakabari hao watasema haya:]

وَقَالُوا رَبَّنَا إِنَّا أَطَعْنَا سَادَتَنَا وَكُبَرَاءنَا فَأَضَلُّونَا السَّبِيلَا. (الأحزاب 67

"Watasema: 'Rabi wetu! Hakika tumewafuata mabwana zetu na wakubwa wetu, basi wao wametupoteza njia.' " (al-Ahzaab, 33:67)

...فَيَقُولُ الضُّعَفَاء لِلَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا إِنَّا كُنَّا لَكُمْ تَبَعًا فَهَلْ أَنتُم مُّغْنُونَ عَنَّا نَصِيبًا مِّنَ النَّارِ. (غافر 47)

"Na wanyonge watakapowaambia wale waliotakabari: 'Hakika sisi tulikuwa wafuasi wenu [duniani], basi Je, mnaweza [leo] kutuondolea sehemu ya [adhabu ya] Moto?' "[Ghaafir, 40:47)

قَالَ الْمَلأُ مِن قَوْمِ فِرْعَوْنَ إِنَّ هَذَا لَسَاحِرٌ عَلِيمٌ. يُرِيدُ أَن يُخْرِجَكُم مِّنْ أَرْضِكُمْ فَمَاذَا تَأْمُرُونَ. (الأعراف 110-109

"Wakasema kikundi cha wakuu katika kaumu ya Firauni [kuwaambia watu wanyonge]: 'Hakika huyu [Musa] ni mchawi stadi. Anataka kukutoeni katika ardhi yenu; basi mnatoa shauri gani?' " [al-A'raaf, 7:109,110)

g) Mwishowe, wakati Mtume na wafuasi wake wanaposimama dhidi ya mfumo unaotawala wa wastakabari ili kuupindua, hukabiliwa na mashambulio, udhia na uhasama mkubwa kutoka kwa wastakabari:

قُتِلَ أَصْحَابُ الْأُخْدُودِ. النَّارِ ذَاتِ الْوَقُودِ. إِذْ هُمْ عَلَيْهَا قُعُودٌ. وَهُمْ عَلَى مَا يَفْعَلُونَ بِالْمُؤْمِنِينَ شُهُودٌ. (البروج 7-4

"Wameangamizwa Watu wa Mahandaki (As'haabul Ukhduud), [waliouwasha] moto wenye kuni nyingi, walipokuwa wamekaa hapo, wakishuhudia yale [mateso] waliyokuwa wakiwafanyia waumini." (al-Buruuj, 85:4-7)

وَقَالَ فِرْعَوْنُ ذَرُونِي أَقْتُلْ مُوسَى وَلْيَدْعُ رَبَّهُ إِنِّي أَخَافُ أَن يُبَدِّلَ دِينَكُمْ أَوْ أَن يُظْهِرَ فِي الْأَرْضِ الْفَسَادَ. (غافر 26

"Na akasema Firauni [kuwaambia washauri wake]: 'Niachieni nimwue Musa, naye amwite Rabi wake [kadiri anavyoweza]j Hakika mimi ninaogopa asije kuibadili dini yenu au kuleta ufisadi katika ardhi [hata watu wakatuasi].' " (Ghaafir, 40:26)

Hii ni sehemu ndogo tu ya aya za Qur'ani zenye kuelezea sifa za wastakabari. Katika aya nyinginezo, licha ya kuchora taswira, Qur'ani inafafanua zaidi kwa kuonyesha kwamba ustakabari ni kama tabaka moja maalum, au kwamba kila mmoja wao ni kama nembo au alama inayowakilisha tabaka hilo.

ثُمَّ بَعَثْنَا مِن بَعْدِهِم مُّوسَى وَهَارُونَ إِلَى فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ بِآيَاتِنَا فَاسْتَكْبَرُواْ... (يونس 75

"Kisha baada ya [Mitume] hao tukawatuma Musa na Harun kwa Firauni na viongozi [wa utawala wake] wakiwa na miujiza Yetu, lakini [Firauni na mafirauni] wakatakabari. ..." (Yuunus, 10:75)

وَقَارُونَ وَفِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَلَقَدْ جَاءهُم مُّوسَى بِالْبَيِّنَاتِ فَاسْتَكْبَرُوا فِي الْأَرْضِ... (العنكبوت 39

"Na Qarun na Firauni na Hamana; na hakika Musa aliwafikia kwa ujumbe bayana, lakini walitakabari katika ardhi [ya Mungu na mbele ya waja na ujumbe wa Mola]." (al-'Ankabuut, 29:39)

Sote tunamjua Firauni. Hamana alikuwa mshauri muhtasi wa Firauni na waziri mkuu katika utawala wa Misri. Malau Fir'awn ni viongozi na wakuu katika utawala wa Firauni ambao walikuwa washauri na wasaidizi katika mfumo huo wa Kifirauni. (Tazama Sura al-A'raaf, 7:126 na aya nyinginezo.) Qarun alikuwa bepari mkubwa ambaye alihodhi hazina kubwa kwa kadiri kwamba "Kulihitajika watu kadhaa wenye nguvu kuweza kubeba funguo za hazina hizo!"

Baada ya kuangalia aya kadhaa za Qur'ani, tunaweza kuwatambua wastakabari kama ni tabaka linalotawala katika jamii ya kishirikina bila ya kustahiki kushika hatamu za kisiasa na kiuchumi. Ili kuendeleza unyonyaji na utawala wao wa kidhuluma, wastakabari hudhibiti utamaduni na itikadi za watu, na hutumia mbinu mbalimbali, ili wapige msasa bongo za watu, kuwafanya wawanyenyekee na wakubali hali hiyo. Ili kuhifadhi maslahi yao, wastakabari huwa tayari kupigana kufa kupona dhidi ya mwito wowote wenye kuleta mwamko, seuze tena harakati za kimapinduzi.

#     *     *     *     #

Sasa turejee tena kwenye maudhui ya asili.

Vipi Mitume na Manabii walikuwa wakitangaza Tawhidi? Namna shaari (kaulimbiu) hiyo ya Tawhidi ilivyokuwa ikitangazwa na Mitume — ambayo ni msingi wa asili wa mafundisho yao — inaonyesha kwa urahisi kipengee kipi cha Tawhidi hakiwezi kuvumiliwa na wastakabari, na sababu ya kuikataa kwao. Kwa nini tabaka hilo haliwezi kuikubali Tawhidi inapoelezwa kwa maana hiyo?

Tunajua kwamba shaari (nara) ya Tawhidi — ambayo ni msemo wa Laa ilaaha illallaah — ni utangulizi wa mwanzo wa miito yote ya Mitume.

Maneno haya ya Mtume Mtukufu kwamba: "Semeni: 'Hakuna mungu ila Allah' mfaulu," ni maneno yaliyo maarufu sana.

Vilevile tangazo hili linalosema: "Enyi watu! Mwabuduni Allah, [kwani] hamna mungu ghairi Yake" (7:59) limetolewa na Manabii wakubwa kama Nuh, Hud, Salih, Shu'ayb, n.k. ambalo lilikuwa muhimu sana katika kuhubiri kwao; na limekaririwa mara kadhaa katika Qur'ani.

Kama tunavyoona katika matamko hayo, jambo linalosisitizwa ni "kukana ibada kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu"; na Tawhidi inaangalia kwa mtazamo huu kwamba asiabudiwe yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu. Kwa kutumia matamko hayo, Mitume walikuwa wakiwaonya watu wajinga na waghafilifu ambao walizama katika matope ya mifumo ya kijahili (klshirikina) na kitaghuti, na walikuwa wakiwatahadharisha wasimwabudu mtu yeyote isipokuwa Allah Mwenye ezi. Daawa za Mitume zilianza kwa kutangaza vita dhidi ya wanaodai uungu.

Na nani katika jamii wanaodai uungu? Kupambana na wajigambao uungu kunamaanisha nini? Malengo gani ya kijamii (yaliyoahidiwa na Manabii) yanatazamiwa kutimizwa katika uandalizi huu?

Kwa kawaida, ibara 'kudai uungu' inachukuliwa kwa maana kwamba mtu hujidai mwenyewe kuwa ni 'mungu' mwenye uwezo ule mkubwa ambao watu walikuwa wakiitakidi katika historia nzima. Kwa hakika, hii ni maana ya kijuujuu tu.

Hapana shaka kwamba walikuwepo wahalifu wapumbavu ambao kwa kutumia nguvu zao za kisiasa na kijamii, waliwafanya watu walio wapumbavu zaidi kuliko wao waamini kwamba waungu walikuwa na sehemu ya roho ya Mwenyezi Mungu. Lakini tunapochungua maana pana ya maneno 'ibada' na 'uungu' katika Qur'ani, tunapata natija hii kwamba ibara 'wanaodai uungu' ina maana kubwa zaidi.

Qur'ani inatumia neno 'ibada' kwa maana ya kujitolea na kumtii mtu au kiumbe chochote bila ya sharti lolote. Wakati wowote tunapojitolea kabisa kwa mtu fulani, tunapotenda kufuatana na amri yake, na tunapojitolea na kutii amri yake tu, hapo huwa 'tunamwabudu' yeye. Vivyo hivyo, ikiwa nguvu yoyote — kutoka ndani ya nafsi yetu au nje yake — itaweza kutufanya tuwe wanyenyekevu na watiifu kwake kwa kuvidhibiti viwiliwili na roho zetu, na kwa kuzielekeza nishati zetu zote kwenye matakwa yake, basi sisi tutakuwa ni 'waabudu' wake, naye atakuwa 'mwabudiwa' wetu.

Aya zifuatazo zinafafanua jambo hili. Mwanzoni mwa daawa yake, Musa alimlaumu Firauni kwa kumwambia:

وَتِلْكَ نِعْمَةٌ تَمُنُّهَا عَلَيَّ أَنْ عَبَّدتَّ بَنِي إِسْرَائِيلَ. (الشعراء 22

"Na hiyo ndiyo neema uliyonifadhilia ya kuwatia katika ibada yako Wana wa Israili?" (ash-Shu'araa, 26:22)

Firauni pamoja na wakuu na washauri wa utawala wake walikuwa wakisema:

...أَنُؤْمِنُ لِبَشَرَيْنِ مِثْلِنَا وَقَوْمُهُمَا لَنَا عَابِدُونَ (المؤمنون 47

"Je, tuwaamini wanadamu wawili walio mfano wetu na kabila lao ni wenye kutuabudu sisi?" (al-Mu'mi-nuun, 23:47) Ibrahim alimwambia baba yake (mdogo):

يَا أَبَتِ لَا تَعْبُدِ الشَّيْطَانَ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلرَّحْمَنِ عَصِيًّا. (مريم 44

"Ewe baba yangu! Usimwabudu Shetani, hakika Shetani ni mwasi kwa [Mola] Mwingi wa rehema." (Maryam, 19:44)

Mwenyezi Mungu anawauliza wanadamu wote kwa jumla:

أَلَمْ أَعْهَدْ إِلَيْكُمْ يَا بَنِي آدَمَ أَن لَّا تَعْبُدُوا الشَّيْطَانَ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ (يس 60

"Je, sikukuagizeni, enyi wanadamu, kwamba msimwabudu Shetani? Hakika yeye ni adui dhahiri kwenu." (Yaasiin, 36:60)

Mwenyezi Mungu anawaahidi wale wenye kutumia akili:

وَالَّذِينَ اجْتَنَبُوا الطَّاغُوتَ أَن يَعْبُدُوهَا وَأَنَابُوا إِلَى اللَّهِ لَهُمُ الْبُشْرَى فَبَشِّرْ عِبَادِ  (الزمر 17

"Na wale wanaojiepusha kufanya ibada ya mataghuti [tawala za kidhalimu] na wakaelekea kwa Allah [kwa uwezo wao wote], bishara [habari njema] ni zao." (az-Zumar, 39:17)

Mwenyezi Mungu anawaambia haya wale wanaowakejeli wale waliomwamini Mwenyezi Mungu na Utume:

... مَن لَّعَنَهُ اللّهُ وَغَضِبَ عَلَيْهِ وَجَعَلَ مِنْهُمُ الْقِرَدَةَ وَالْخَنَازِيرَ وَعَبَدَ الطَّاغُوتَ أُوْلَئِكَ شَرٌّ مَّكَاناً وَأَضَلُّ عَن سَوَاء السَّبِيلِ (المائدة 60

"[Yule] ambaye Allah amemlaani na kumghadhibikia na amemfanya miongoni mwa waliogeuzwa kuwa kima na nguruwe, na akamwabudu  taghuti.  Hao ndio wenye mahali paovu kabisa na   waliopotea kabisa katika njia iliyo sawa," (al-Maaidah, 5:60)

Katika aya hizi, kumtumikia na kumtii Firauni na wakuu wa utawala wake, na kuwatii na kuwatumikia mataghuti (madhalimu) na mashetani kunafasiriwa kama ni 'ibada' na 'kuabudu'.  Kwa jumla, aya hizi pamoja na aya nyingine kadhaa za Qur'ani, zinaonyesha kwamba maana ya 'ibada' katika Qur'ani ni kufuata, kusalimu amri na kuitii kabisa kudura. (nguvu)  moja ya kihakika au ya kimawazo (kidhahania),  kwa  njia ya hiari na raghba au kwa nguvu na lazima, kutakoambatana au ambako hakutoambatana na hisia ya kiroho ya kuheshimu, kunyenyekea na kutukuza.

Kwa vyovyote vile, kudura hiyo ni mwabudiwa na mungu, na mtiifu huyo ni mwabudu na abdi.

Kwa maelezo hayo, inafahamika kwamba neno 'Uungu', 'Mungu' au 'Allah' lina maana sawa na 'uabuduji' na 'Mwabudiwa'.

Katika mfumo mpotofu wa kishirikina ambapo watu hugawanywa katika matabaka mawili ya wastakabari (mustakbiruun) na wastadhaafu (mustadh'afuun) — yaani tabaka linalotawala la mabepari na wanyonyaji, na tabaka la wanyonge na maskini — tunaona mfano dhahiri kabisa wa uhusiano baina ya 'mwabudiwa' na 'waabudu' ambao ni huu uhusiano usio sawa na usio wa haki baina ya matabaka mawili haya. Tukitaka kuwajua waabudiwa na waungu wa jamii mbalimbali katika historia, tusihangaike kuwatafuta miungu wa aina ya mtu, mnyama au kitu katika jamii hizo, bali inatosha kuona mfano mzuri sana wa waungu na waabudiwa wao ambao ni haohao wastakabari waliowakandamiza wastadhaafu (wanyonge), wakawatia utumwani, wakawatawala na wakawafanya wawaabudu (wawatumikie) ili washibishe unyonyaji wao na tamaa zao za kumiliki.

Katika jamii kama hizo, dini hasa ya watu ni shirki (ushirikina), kwa sababu kuna idadi kubwa ya miungu au waungu wenye kuwa na uwezo na amri juu ya watu, ambao hufumba macho yao na kuziba masikio yao na kuwaelekeza kwenye njia ya matakwa yao kwa utiifu kamili.

Shirki maana yake ni kumtii na kumwabudu mwingine badala au pamoja na Mwenyezi Mungu. Shirki maana yake ni kuweka mambo yote ya maisha katika udhibiti wa mwingine ghairi ya Mwenyezi Mungu. Shirki maana yake ni kusalimu amri mbele ya kudura na nguvu zisizokuwa za Mwenyezi Mungu, na kuzitegemea katika kutimiziwa mahitaji na kupata mwongozo.

Tawhidi inapingana kabisakabisa na shirki, kwa kuwa inakana na inakataa miungu na waungu hao, inapinga kuwatii, inapinga utawala na mamlaka yao, inakataza kutaka msaada kutoka kwao, na mwishowe, inataka uwakatae kabisa na badala yake ujitolee kwa moyo wote mbele ya Mwenyezi Mungu.

Nara ya kwanza iliyopigwa na Mitume wote wa Mwenyezi Mungu ilikuwa ni kukana shirki na kukiri Tawhidi:

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولاً أَنِ اعْبُدُواْ اللّهَ وَاجْتَنِبُواْ الطَّاغُوتَ... (النحل 36

"Na kwa hakika tulimtuma Mtume katika kila umma, ya kwamba: 'Mwabuduni Allah na waepukeni mataghuti  [watawala  wenye kumwasi Mungu].'"  (an-Nahl, 16:36)

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ. (الأنبياء 25

"Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimpa wahyi ya kwamba: 'Hakuna mungu (aabudiwaye) ila Mimi, basi niabuduni.' " (al-Ambiyaa, 21:25)

Kwa hivyo, kwa kutangaza shaari hiyo, Mitume waliishutumu mifumo ya kifasidi na ya kishirikina, na wakawahimiza watu wapambane dhidi ya mataghuti ambao ni watetezi wa mifumo hiyo, waasi wa thamani halisi za kibinadamu, na ambao huwalazimisha watu wafuate mfumo wao usio na thamani ili waweze kuhifadhi maslahi yao ya kidhalimu.

Kwa hakika, kukataa shirki ni kukataa mifumo yote ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ambayo ni misingi ya asili ya jamii ya kishirikina. Itikadi ya kishirikina ni kifuniko au kisingizio cha kuhifadhi na kuendeleza hali isiyofaa katika jamii.

Kuwapinga waungu na masanamu maana yake ni kuwapinga watu wote ambao wanawakandamiza na kuwastadhaafisha watu, kwa kutumia mabavu au ujanja, ili wapate kuyatosheleza matamanio yao.

Musa alipotangaza shaari hiyo na aliposema kuhusu utawala mkuu na wa pekee wa Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu, alitangaza vita dhidi ya Firauni na akamkataa. Hapana shaka kwamba wanabaraza wa Firauni walimshutumu Musa kwa kuwapinga waungu wao, na wakamtuhumu kwa kosa la kuwapinga masanamu na waungu wao wa kimila.

وَقَالَ الْمَلأُ مِن قَوْمِ فِرْعَونَ أَتَذَرُ مُوسَى وَقَوْمَهُ لِيُفْسِدُواْ فِي الأَرْضِ وَيَذَرَكَ وَآلِهَتَكَ... (الأعراف 127)

"Na wakasema wakuu wa utawala wa Firauni: 'Je, utamwacha Musa na watu wake walete ufisadi katika ardhi na kukuacha wewe na waungu wako?' " (al-A'raaf, 7:127)

Lakini Firauni mwenyewe pamoja na kikundi chake cha wafisadi, walijua vizuri sana kwamba hao 'waungu' — yaani masanamu yasiyokuwa na roho — hawakuwa kitu isipokuwa ni kisingizio tu kwa ajili ya kudai uungu wao, na njia muhimu ya kudumisha uungu wao. Kwa hivyo, ilikuwa ni mantiki kabisa kwa Firauni kujibu mwito wa Musa wa kujitolea kwa Mwenyezi Mungu Mmoja, Muumba wa mbingu na ardhi na Mola wa mashariki na magharibi, kwa kumtisha kumfunga na kumwua, na kuwatishia wafuasi wake kuwaadhibu kwa mateso makali. 

 قَالَ لَئِنِ اتَّخَذْتَ إِلَهًا غَيْرِي لَأَجْعَلَنَّكَ مِنَ الْمَسْجُونِينَ. (الشعراء 29 

"[Firauni]   akasema:   'Kama   ukijichagulia mungu mwingine   ghairi  yangu,   kwa  hakika   nitakuweka miongoni mwa wafungwa.' " (ash-Shu'araa, 26:29)

Firauni akamjibu haya mshauri wake ambaye alimshawishi achukue hatua kali ya kumtia adabu Musa na Wana wa Israili:

...قَالَ سَنُقَتِّلُ أَبْنَاءهُمْ وَنَسْتَحْيِي نِسَاءهُمْ وَإِنَّا فَوْقَهُمْ قَاهِرُونَ (الأعراف 127

"[Firauni] akasema: 'Hivi karibuni tutawaua wavulana wao na tutawaacha hai wanawake wao, na bila shaka sisi ni wenye nguvu juu yao.' "(al-A 'raaf, 7:127) Firauni  akawaambia  haya  wachawi wake ambao walimwamini Musa bila yeye kutegemea:

لأُقَطِّعَنَّ أَيْدِيَكُمْ وَأَرْجُلَكُم مِّنْ خِلاَفٍ ثُمَّ لأُصَلِّبَنَّكُمْ أَجْمَعِينَ. (الأعراف 124

"Kwa hakika nitaikata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha,  kisha nitawasulubini nyote." (al-A'raaf, 7:124)

Unyama huo unaofanywa dhidi ya jina la Allah na mwito wa Tawhidi, unamaanisha kwamba ujumbe huu wa uhuru na ukombozi hauna maana nyingine isipokuwa:

Kuamini kwamba Allah tu Ndiye Mwenye utawala na mamlaka ya pekee juu ya maisha.

Kuwakataa wengine wote wanaodai uungu, na kukubali kuwa mja wa Allah tu.

Kukata minyororo yote ya utumwa wa wengine ghairi ya Allah.

Hii ndiyo roho, asili, kiini, na maana halisi ya itikadi ya Tawhidi ambayo ni kipengee kinachong'ara kabisa cha Umoja wa Mwenyezi Mungu.

TAMATI

 
< Nyuma

^