Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Kuhusu Ulimwengu wa Kiislamu Chapa
06/07/2008

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Matunda ya kwanza ya kisiasa-kiuchumi ya Uislamu ni umma wa Kiislamu ambao ulianzia katika mji mtakatifu wa Madina na kisha kutia mguu na kuchepuka kwa kasi ya ajabu ukaenea na kustawi kote ulimwenguni. Ilikuwa hata nusu karne haijapita tangu alipozaliwa mwana huyu mbarikiwa lakini karibu nusu ya eneo zima la staarabu tatu kubwa za kale alizopakana nazo yaani Iran, Urumi na Misri zilipata nuru ya mwana huyo, na karne moja baadaye, ukajiunda ustaarabu unaong'ara na utawala mtukufu wenye nguvu katikati ya dunia ambao kwa upande wa mashariki ulipakana na ukuta wa Uchina na upande mwingine ukafika kwenye fukwe za Bahari ya Atlasi. Kaskazini ukasonga hadi kwenye kingo za Siberia na kwa upande wa kusini ukaenda hadi kusini mwa Bahari ya Hindi. Katika karne za tatu na nne Hijria na baada ya hapo ustaarabu huo ulizidi kung'ara kiasi kwamba licha ya kupita miaka elfu, bado baraka zake za kielimu na kiutamaduni zinaonekana kwa uwazi katika ulimwengu huu ulioendelea.

Mjumuiko huu una utamaduni tajiri na urithi wenye thamani kubwa unaokwenda sambamba na kuchanua na kustawi kwa namna ya kipekee ndani ya mabadiliko na aina kwa anuwai za ustawi, umejipamba kwa mshikamano na umoja wa kustaajabisha uliotokana na kupenya Uislamu na tauhidi mahsusi na khalisi katika kila nukta na pembe zake. Mataifa haya ndugu yanayopendana yanayoundwa na vizazi vyeusi, vyeupe na njano na vinavyozungumza makumi ya lugha, yote ni sehemu za umma mkubwa wa Kiislamu zilizo na haki sawa na yanajifakharisha kwa hilo. Kila siku mataifa hayo yanaelekea upande mmoja na kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa lugha moja. Mafunzo yao yanatoka katika kitabu kimoja cha Mwenyezi Mungu na wanapata ilhamu kutoka katika kitabu hicho kinachobainisha uhakika wote na kukidhi haja na takilifu zote:
ونزلنا عليك الكتاب تبيانا لكل شيء وهدى ورحمة وبشرى للمسلمين
Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinachobainisha kila kitu, na ni uwongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu. (an Nahl: 89).

Eneo la kijiografia la mjumuiko huo wa binaadamu, ni moja ya maeneo tajiri zaidi - kama si tajiri lao - katika maliasili na vyanzo vya kimaumbile. Faharasa ya (kitabu cha) suhula za umma wa Kiislamu, inakusanya mamia ya anwani na milango mikubwa ya kibinaadamu, kiutamaduni, kimaada, kiuchumi, kisiasa na kijamii na kila anayezama na kuangalia kwa kina anaweza kuuona wazi ukweli huo.

Hivi sasa wenye vipawa vya kisiasa na kifikra katika dunia ya Kiislamu, wana jukumu zito. Wasomi wa Kiislamu wana wajibu wa kufikisha kwa watu ujumbe wa ukombozi wa Kiislamu kwa njia rahisi, yenye mvuto na bora zaidi. Waibainishie kwa namna bora dhati ya Uislamu na mataifa ya Kiislamu. Wawafikishie vijana mitazamo ya Kiislamu kuhusu mambo kama haki za binaadamu, uhuru na demokrasia, haki za mwanamke, kupambana na ufisadi, kuondoa ubaguzi, kukabiliana na kubaki nyuma kielimu na umaskini. Wafichue kwa wote hila za vyombo vya Magharibi kuhusu kupambana na ugaidi na kukabiliana na silaha za mauaji ya umati. Leo hii kielimu na kinadharia, ni ulimwengu wa Magharibi ndio unaopaswa kuwekwa ‘kiti moto' na kusailiwa na walimwengu kuhusu mambo hayo.

Maadui majabari wa umma wa Kiislamu, ni waongozaji wa taasisi za kibeberu na madola vamizi yanayopenda makubwa ambao wanauhesabu mwamko wa Kiislamu kuwa tishio kubwa kwa maslahi yao yasiyo halali, ya kibeberu na kidhulma katika ulimwengu wa Kiislamu. Mataifa yote ya Kiislamu na juu yao wanasiasa na maulamaa wa kidini, wanafikra na viongozi wa kitaifa wa nchi za Kiislamu, wanapaswa kupanga safu madhubuti iliyoshikamana vilivyo kukabiliana na adui huyo mshari. Wanapaswa kutumia vingee vyote vya nguvu zao na kuufanya umma wa Kiislamu kuwa na mbinde zake halisi. Utambuzi na maarifa, umakini na kuwa macho, kuhisi na kuheshimu majukumu, kutawakali na kuwa na matumaini na ahadi za Mwenyezi Mungu, kudharau matamanio ya kughururisha yasiyo na thamani, kutafuta radhi za Allah, kutekeleza wajibu na... vyote hivyo ni vipengee vikuu vya kuweza kupata nguvu uma wa Kiislamu ambavyo vinaweza kuufikisha uma huo kwenye heshima, izza, uhuru, kujitegemea na maendeleo ya kimaada na kimaanawi na kumfanya adui ashindwe katika siasa zake za kupenda makubwa na za kutaka kuzidhalilisha nchi za Kiislamu.

Hali hii mpya ina sehemu na vipengee viwili. Mosi ni fikra na utambulisho wa Kiislamu kimataifa ambao hivi sasa umekuwa na nguvu, heshima na harakati zaidi na sasa Uislamu umejitokeza duniani kuwa moja ya uhakika mkubwa zaidi kote ulimwenguni. Pili ni kwamba madola ya kibeberu yanaonyesha hadharani chuki na uhasama wao dhidi ya Uislamu na malengo yake na kiutafiti ni kwamba moja ya awamu kuu katika mfumo mpya wa dunia uliopendekezwa na Marekani baada ya kusambaratika ukomunisti, ni awamu ya kupambana na Uislamu na kukabiliana na kustawi kila uchao harakati za Kiislamu.

Ukweli wa mambo ni kuwa, katika kipindi cha muongo mmoja miwili iliyopita, Waislamu wa mashariki na magharibi mwa ulimwengu wa Kiislamu bali hata katika nchi zisizo za Kiislamu, wameanzisha harakati mbalimbali za kiuhakika na za kweli kabisa ambazo kiujumla wake inabidi ziitwe harakati ya "Kuhuisha Uislamu." Ukweli ni kuwa, kizazi hiki kipya kilichosoma na chenye utambuzi wa zama ambacho kinyume na matarajio wa wakoloni wa jana na mabeberu wa leo, si tu hakijaachana na Uislamu, bali kimezidi kushikamana na dini hiyo tukufu. Kizazi hicho kinatumia maendeleo ya elimu ya mwanaadamu na mara nyingi kwa mtazamo mpana na wa kina zaidi kinatafuta heshima na fakhari zake zilizopotea. Harakati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuzidi kupata nguvu na kuwa kwake imara ni kilele cha harakati hiyo jadidi na thabiti yenye misingi madhubuti, ambayo ina mchango mkubwa sana katika kutanuka na kuenea mwako wa Waislamu. Hilo ndilo linaloifanya kambi ya kibeberu ambayo siku zote ilikuwa ikijionyesha inakwepa kukabiliana na itikadi na matukufu ya mataifa mengine, kuuchegama waziwazi Uislamu leo hii kwa kutumia mbinu zote ulizo nazo na baadhi ya wakati hata kwa ukandamizaji na ukatili.

Adui mstakbari ambaye anaona mwamko wa Kiislamu ni tishio kwa tamaa na manufaa yake yasiyo halali, ana silaha kali ya kukabiliana na wimbi hilo nayo ni silaha ya kisaikolojia yaani kujaribu kukatisha tamaa, kudharaulisha utambulisho na kuzikuza kupindukia nguvu na uwezo wake wa kimaada. Leo hii na katika siku za usoni, kunatumika na kutatumika maelfu ya njia za propaganda ili kujaribu kuwakatisha tamaa Waislamu kuhusu mustakbali wao na kuwaburuza kwenye mustakbali unakubaliana na nia chafu za maadui wa Uislamu. Vita hivi vya kisaikolojia na kiutamaduni ndiyo silaha kubwa ambayo imetumiwa na wakoloni wa Magharibi katika kuzidhibiti nchi za Kiislamu hadi leo hii. Bila ya shaka propaganda mpya zenye uungaji mkono kimataifa ndiyo silaha bora kabisa wanayoitumia mabeberu. Leo hii kuna idadi kubwa sana ya vyombo vya sauti, picha na magazeti ambavyo vimejikita zaidi katika kuufanyika uadui Uislamu, na kila leo vyombo hivyo vinaongezeka. Kazi kubwa wanayofanya wataalamu mamluki ni kuandaa na kueneza mambo ya kupotosha watu, kutoa maelezo ya uongo kuhusu masuala mbalimbali na kuipaka matope harakati ya Kiislamu na watu watukufu ndani ya Uislamu. Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikikabiliwa mfululizo na propaganda hizo chafu za kiadui kwa miaka mingi sasa tangu yalipopata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Tab-an watu na makundi mbalimbali ya binaadamu yanaathirika katika pande mbili. Mosi kwa ndani yao wenyewe jambo ambalo ndilo chimbuko la udhaifu wa kibinaadamu, wasiwasi, kukosa imani, kutegemea wageni, kujisahau, kuhadaika kirahisi, kumsahau Mwenyezi Mungu, kuwa mateka mikononi mwa wapenda dunia, kuwa na mtazamo kuhusu ndugu, kusadiki maneno ya adui dhidi yao na kutoguswa na kuumwa na mustakbali wa umma wa Kiislamu. Bali katika karne za hivi karibuni, daima Waislamu wamekuwa wakikabiliwa na vitisho vinavyotokana na kutokuwa na welewa wa kutosha kuhusu umma wa Kiislamu, kutofuatilia habari za matukio ya nchi nyingine za Kiislamu, kutokuwa macho mbele ya njama za maadui dhidi ya Uislamu na Waislamu, hitilafu za kikabila na hisia za kuchupa mipaka za utaifa ambazo sana zinaenezwa na kutiwa nguvu na wasomi waovu na waandishi vibaraka, bali hatari zaidi ni yale maradhi angamizi mengine ambayo yamekuwa tatizo sugu katika kipindi chote cha Uislamu na ambayo yanatokana na kudhibitiwa nchi za Kiislamu, maisha ya kisiasa na mustakbali wa Waislamu na watu wasio wastahiki ambao hawajali mafundisho ya Mwenyezi Mungu. Vitisho hivyo vimeongezeka kwa ujio wa madola ya kikoloni ya wageni katika eneo yakisaidiwa na vibaraka mafasidi na waabudu dunia.

Upande wa pili ni athari zitokazo kwa adui wa nje ambaye anayafinya na kuyabana maisha ya mataifa mengine tunia kutokana na kuchupa kwake mipaka, kupenda makubwa, uchokozi na uadui wake. Mazingira ya Kiislamu - Iwe watu au mataifa - daima yamekuwa yakikabiliwa na vitisho hivyo viwili na hivi sasa yanakabiliwa zaidi na vitisho hivyo kuliko huko nyuma. Kueneza kwa makusudi ufisadi katika nchi za Kiislamu na kuyatwisha mataifa ya Kiislamu utamaduni wa Magharibi kunakofanywa na baadhi ya tawala vibaraka kunasaidia katika hilo na kwa upande mmoja kunaathiri mwenendo wa mtu hadi mji na mazingira yote ya maisha ya watu, vyombo vya habari n.k, na kwa upande wa pili kunayawekea mashinikizo ya kijeshi, kisiasa na kiuchumi baadhi ya mataifa ya Waislamu na kufanya mauaji katika nchi za Lebanon, Palestina, Iraq, Afghanistan na kwengineko, yote hayo ni ushahidi wa wazi wa kuweko vitisho hivyo viwili vinavyoyakabili mazingira ya Kiislamu.

Hata hivyo kadhia muhimu zaidi hivi sasa ni ya Palestina ambayo ni muhimu katika kipindi chote cha nusu karne iliyopita katika ulimwengu wa Kiislamu na pengine ndilo suala lililo muhimu zaidi kwa binaadamu. Makusudio hapa ni mtihani na dhulma linayofanyiwa taifa hilo, makusudio ni hasira za nchi, makusudio ni kulaani kuwekwa donda ndugu la kansa katika kitovu cha nchi za Kiislamu na katika makutano ya mashariki na magharibi mwa ulimwengu wa Kiislamu. Makusudio hapa ni dhulma isiyokoma ambayo hivi sasa imevikumba vizazi viwili mfululizo vya taifa hilo la Kiislamu.

Kwa maneno mengine ni kuwa utawala ghasibu wa Kizayuni, ni hatari kubwa zaidi ya hivi sasa na ya siku za usoni kwa ulimwengu wa Kiislamu na ni wajibu kwa Waislamu kufikiria njia za kuweza kupambana na kuondoa dhulma kubwa kiasi chote hiki. Tab-an ingawa sisi hatuna shaka kwamba katika siku za usoni na wala si usoni sana, taifa la Palestina litaweza kupata haki yake iliyoghusubiwa na kuporwa, chini ya kivuli cha kujitolea kwake na mwamko katika ulimwengu wa Kiislamu, lakini azma na irada ya tawala na mataifa ya Kiislamu ndiyo itakayoweza kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu kuharakisha kushuhudiwa mustakbali huo mwema na kulipunguzia masaibu taifa la Palestina.

 
< Nyuma   Mbele >

^