Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Mitazamo ya Kiongozi Mudhamu Kuhusiana na Mageuzi Chapa
27/07/2008

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu


Tunachosema sisi kuhusiana na Palestina ni kitu cha kimantiki na kinachokubalika kabisa. Miongo kadhaa iliyopita, Jamal Abdul Nasser - ambaye alikuwa shakhsia anayependwa sana katika ulimwengu wa Kiarabu - alikuwa akisema katika nara na kaulimbiu zake kwamba, sisi tutawatumbukiza baharini Mayahudi walioghusubu Palestina. Miaka kadhaa baadaye, Saddam Hussein - shakhsia ambaye alikuwa akichukiwa na bado anachukiwa mno katika ulimwengu wa Kiarabu - alikuwa akisema, tutaiteketeza kwa moto nusu ya ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Sisi hatukubaliani na maelezo yote hayo mawili. Kwa mujibu wa misingi yetu ya Kiislamu si mantiki na wala haingii akilini kuwatumbukiza Mayahudi baharini wala kuteketeza ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Tunachosema sisi ni kwamba lazima wananchi wa Palestina wapewe haki zao. Nchi hiyo ni ya wananchi wa Palestina; Palestina ni ya Wapalestina na mustakbali wa Palestina unapaswa kuainishwa na Wapalestina wenyewe. Hiyo ni medani ya kutahiniwa wanaojigamba kutetea demokrasia na haki za binadamu. Taifa la Palestina yaani watu ambao Palestina ni yao yaani Waislamu, Wakristo na Mayahudi na ardhi yao ya kihistoria, tarihi na jiografia yote hayo yanatilia mkazo kwamba watu hao wana haki ya kutoa mitazamo na fikra zao kuitishwe kura ya maoni mbele ya walimwengu na wajichagulie muundo wa utawala wanaotaka huko Palestina hapo ndipo tutaweza kusema serikali hiyo ni halali. Wale wote waliotenda jinai huko Palestina watafuatiliwa kisheria ndani ya serikali hiyo ambayo itapaswa kuchukua uamuzi nini inapaswa kufanya juu ya wale watu ambao wamehamia katika ardhi hizo za Palestina kutoka maeneo mbalimbali ulimwenguni. Hayo ndiyo maneno ya kimantiki. Leo hii mamilioni ya Wapalestina wamekuwa wakimbizi katika nchi nyingine na mamilioni ya wengine wanaishi maisha magumu sana kwenye kambi za wakimbizi; huku ardhi zao zikikaliwa kwa mabavu na watu wengine. Suala hili haliingii akilini; na wala si la kimantiki. Kupitia miaka khamsini au khamsini na tano tangu kuanza kufanyika hayo hakuhalalishi jinai hizo wala kupunguza makali ya uhalifu huo. Kupita wakati hakuweza kufuta haki kama ya Palestina katika uso wa dunia. Palestina na wananchi wa Palestina wako hai, na mustakabali wa Palestina uko wazi.
Wananchi wa Palestina wanapoaswa kutegemea nguvu zao za asili na wasichoke. Wananchi wa Palestina wasipokonywe imani, irada, mori na matumaini. Kama ambavyo kusini mwa Lebanon imerejea kwa Walebanon wenyewe baada ya kupita miaka ishirini na mbili, ni vivyo hivyo kuna uwezekano baada ya kupita miaka kadhaa baadhi ya sehemu ya ardhi ya Palestina itakombolewa na mwishoni ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zitarejea mikononi mwa wananchi wa Palestina. Leo hii baadhi ya watu wanaona jambo hilo liko mbali sana; jana pia baadhi ya watu walisema ni jambo lililoko mbali na haiwezekani kukombolewa kusini mwa Lebanon, amma eneo hilo limekombolewa!
Kuondoka Wazayuni katika eneo la Ukanda wa Gaza baada ya kulikalia kwa muda wa miaka 37 ni tukio muhimu sana. Ni vizuri mkijua kwamba hawakuondoa huko kwa hiari yao; bali ilikuwa ni kushindwa na kutokuwa na la kufanya. Hawakuwa na njia nyingine. Hivi sasa mashinikizo ya kisaikolojia ya kushindwa huko yameziathiri na kuzitingisha nguzo zote za wananchi na utawala wa Kizayuni. Wengine wanajaribu kuonyesha kuwa kuondoka utawala huo kwenye eneo la Gaza kumetokana na mazungumzo; madai hayo ni ya kitoto sana. Katika kipindi chote cha miaka sabini ya kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina, Wazayuni hawajawahi kurejesha hata mita moja kwa njia ya mazungumzo. Semeni mazungumzo gani yamepelekea kurejeshwa ardhi za Palestina?! Kuondoka huko kwa hakika kumetokana na mapambano ya Wapalestina. Tukio la kwanza lilikuwa la kuondoka na kukimbia kwa madhila Wazayuni kusini mwa Lebanon; hili pia ni tukio la pili ambalo limepatikana kutokana na mapambano.
Kadhia ya Palestina haiwezi kutatuliwa kwa njia hiyo, kwamba waondoke katika sehemu moja baadaye mambo yaishe, hilo haliwezekani. Mfano mtu amekuja na kukufukuza nyumbani kwako na kuikalia kwa mabavu nyumba yako, halafu baada ya muda akupatie chumba kimoja kidogo upenuni mwa nyumba yako, na sehemu iliyobakia ya nyumba yake aseme ni mali yake; hilo linawezekana kweli? Wameichukua Palestina na hivi sasa wamelazimika kuondoka katika sehemu fulani ya ardhi hiyo; hapo wengine wanaweza kusema si neno, madhali sasa mumetoa sehemu hiyo basi sehemu zilizobakia za Paelstina ni mali yenu! Kweli inawezekana jambo hilo? Kadhia ya Palestina haiwezi kutatuliwa kwa njia hiyo.
Kuhusiana na kadhia ya Palestina kuna nukta tatu muhimu na nimeziashiria nukta hizo. Nukta hizo tatu zitabakia kuwa ukumbusho wa kihistoria. Kwa ufafanuzi zaidi tu hapa nasema:
Nukta ya kwanza ni dhulma na jinai zisizo na mfano ambazo leo hii zinafanywa na Wazayuni dhidi ya wananchi wa Palestina. Bila ya shaka jambo hilo litabaki milele katika historia. Kijana mmoja ambaye baada ya kupata mateso na misiba mingi kutoka kwa Wazayuni anaamua kutoa muhanga maisha yake na hatimaye kuuawa shahidi ili kumpa pigo aliyeghusubu nyumba yao. Wazayuni wanakuja na kuharibu nyumba ya kijana huyo, pamoja na nyumba ya baba na mama yake na familia yake huitesa na kuisumbua; wanaingia kwenye kambi za wakimbizi na mijini wakitumia vifaru na kuharibu nyumba na mashamba na hatimaye kuwauwa watu. Leo hii kuwauwa vijana, watoto, vikongwe na vibikizee vya Kipalestina na raia wasio na hatia ni jambo la kawaida na la kila siku; na wala si jambo la ajabu. Kwa hakika hili ni tukio la kihistoria; na litabaki milele katika historia.
Nukta ya pili ambayo itaendelea kubaki katika historia ni subira na istikama ya wananchi wa Palestina. Wananchi wamezingirwa, na katika pembe zote wamejaa maadui; lakini bado wanaendelea kusimama kidete bila ya kutetereka. Wanastahamili njaa, wanavumilia machungu ya watoto na vijana wao, wanahimili kuharibiwa nyumba na mashamba yao na wanastahamili kubaki bila ya kazi. Hivi sasa mamilioni ya Wapalestina - si kwamba wote ni wanachama wa vyama na makundi ya kisiasa - bali ni taifa lenye mjumuiko wa wanawake, wanaume wakubwa kwa wadogo na wazee, wamesimama imara kabisa. Suala hilo pia litabaki katika historia. Nukta hiyo inang'ara katika kadhia hiyo na itavutia macho ya watu katika historia.
Nukta ya tatu ni kimya kinachonyeshwa na jamii ya kimataifa na madola mbalimbali! Hawa mabwana wa Ulaya ambao wanadai kuashiki haki za binaadamu kwa kiasi chote hiki; wanaodai nyoyo zao huumia sana wakati haki za binaadamu zinazpovunjwa, leo hii wanashuhudia kwa macho yao jinai hizo na wamefumba midomo yao, bali katika masuala mengi pia wamekuwa hata wakimsaidia dhalimu! Kwa hakika inashtusha na kushangaza! Kuhusu Marekani ndio hatusemi, kwani yenyewe ni mshirika wa jinai. Mikono ya serikali za Marekani imejaa damu za Wapalestina. Iwapo kutaundwa mahakama ya kutoa hukumu za jinai za Palestina, watuhumiwa katika mahakama hiyo hawatakuwa Wazayuni pekee, bali Marekani nayo itashitakiwa. Bush na wasaidizi wake na serikali nyingine za Marekani nazo zimo tena ni katika washtakiwa wakuu. Lakini hao ndio hatusemi. Suala hapa ni suala la jamii ya kimataifa, yaani Umoja wa Mataifa na mataifa ya Ulaya ambayo yamekuwa mstari wa mbele kupigia kelele haki za binadamu. Mataifa hayo yanapiga domo tu la haki za binaadamu lakini hayajui haki za binadamu ni nini na kimsingi hayaziheshimu. Tab-an suala hilo linayahusu pia mataifa mengine. Kwa hakika kimya cha mataifa ya Kiislamu nacho kinashangaza mno.
Leo hii Palestina inapambana kwa jina la Mwenyezi Mungu na inaendeleza mapambano hayo kwa baraka Zake. Kwa mara nyingine utadhihiri ushindi wa irada na azma ya watu ambao nyoyo zao zimejaa imani ya Mwenyezi Mungu dhidi ya madola yote ya kimaada na kupenda dunia. Ulimwengu utashuhudia jinsi wananchi wa Palestina wanavyosonga mbele hatua kwa hatua kuelekea kwenye malengo yao. Palestina ni ya taifa la Palestina. Leo hii taifa hilo liko katika uwanja wa mapambano. Katika ulimwengu wa Kiislamu pia kumehanikiza na kuchachawaa kelele za furaha kutokana na mafanikio wanayopata wananchi wa Palestina kimataifa kutokana na istikama na ushujaa wanaouonyesha.

 
< Nyuma   Mbele >

^