Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu Kuhusu Utamaduni Chapa
13/08/2008

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Utangulizi

Utamaduni maana yake ni mila na desturi ambazo zinatawala maisha yangu na yako. Utamaduni maana yake ni imani na itikadi za kienyeji za watu na jamii fulani. Fikra zao, imani zao na matukufu yao ndiyo mambo ambayo yanaweka misingi ya utamaduni wa nchi na ni mambo hayo ndiyo yanayolifanya taifa ima kuwa shujaa, huru na linalojivunia matukufu yake au kuwa hawafu, mwoga na dhaifu.
Utamaduni ndilo chimbuko kuu la utambulisho wa mataifa. Ni utamaduni ndio unaoweza kuliletea maendeleo taifa, kulikuza, kulipa nguvu, elimu, na teknolojia na kulifanya litembee kifua mbele na kujivunia fakhari zake. Kama utamaduni wa nchi utaporomoka na nchi hiyo kupoteza utambulisho wake, basi hata kama itatokezea wengine kupeleka maendeleo katika nchi hiyo hawataweza kuifanya nchi hiyo kuwa na nafasi bora mbele ya walimwengu na wala hawataweza kuifanya ilinde manufaa yake.
Utamaduni wa uma una sehemu mbili. Sehemu moja inahusiana na masuala yaliyo bayana na wazi ambayo kila mtu anayaona ambayo kwa hakika yana mfungamano na hatima ya taifa na yanaathiri lakini baada ya kupita muda mrefu. Yaani yanaleta athari katika mwenendo wa maisha na harakati za baadaye za taifa. Mfano wa mambo hayo ni mavazi, jinsi ya kuvaa na kigezo cha mavazi cha jamii fulani na hayo ni sehemu ya misdaki na mifano ya wazi ya utamaduni wa watu wote kiujumla. Aidha ujenzi wa nyuma katika jamii au maisha ya nyumbani ya watu nayo ni sehemu ya utamaduni wa jamii.
Sehemu ya pili ya utamaduni wa uma ni mithili ya hiyo ya kwanza kwamba inagusa na kuathiri mustakbali wa taifa, lakini athari zake zinaonekana haraka, huwa wazi kabisa na pengine papo hapo. Ijapokuwa mambo yenyewe yanayohusiana na sehemu hiyo ya utamaduni wa uma hayaonekani kwa uwazi sana, lakini athari zake kwa jamii na mustakbali wake, zinaoekana jahara kabisa. Miongoni mwa mambo hayo na kwa hakika yaliyo muhimu zaidi miongoni mwake ni maadili yaani hulka na tabia za mtu binafsi na silika na ruwaza za watu wote katika jamii.
Mfano mwingine wa utamaduni wa uma ni kwamba insani katika jamii fulani wawe ni watu ambao ni wasamehevu na wasijali zaidi manufaa yao binafsi bali waweko tayari hata kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya wananchi wenzano na nchi yao. Yaani hisia za manufaa ya wote ndani ya taifa hilo ziwe mbele zaidi ya hisia za kujinufaisha binafsi.
Hivyo nafasi ya utamaduni ni mithili ya nafasi ya roho katika mwili wa jamii - mwili mkubwa wa mwanaadamu. Kuyadhibiti mataifa mengine kupitia kutwisha tamaduni baki si jambo lililoanza juzi, bali limekuwepo kwa muda mrefu lakini katika karne moja mbili zilizopita, Wamagharibi wamekuwa wakitumia maendeleo yao ya kielimu kupanga na kuratibu kazi zao kwa muundo maalumu likiwemo suala hilo la kuyadhibiti mataifa mengine kupitia kueneza utamaduni wao. Wanajua wanachofanya katika jambo hilo na wanaelewa ni wapi pa kulenga zaidi.
Mataifa yote hai duniani yanaafikiana kwamba kama taifa litaacha utamaduni wake wa kitaifa ukanyagwe na kushambuliwa na watu baki, bila ya shaka yoyote taifa hilo litaangamia. Taifa linaloweza kushinda ni lile ambalo utamaduni wake nao hushinda. Ni ushindi wa kiutamaduni ndio unaoleta ushindi wa kiuchumi, kisiasa, kiusalama, kijeshi na kila kitu.
Udhibiti wa kiutamaduni ni mbaya zaidi kuliko udhibiti wa kiuchumi na kisiasa. Kwa nini? Kwa sababu wakati taifa moja linapolidhibiti taifa jingine kiutamaduni, utambulisho wa taifa lililodhibitiwa hutoweka. Kama taifa litatengwa na kupokonywa historia yake, mapisi yake, utamadunia wake, heshima yake, fakhari zake za kielimu, kidini, kisiasa na kiutamaduni, na kama litaporwa lugha yake, abjadi zake, uandishi wake na historia yake ya kiutamaduni, taifa hilo huwa tayari kwa ajili ya kupokea chochote inacholishwa. Taifa hilo halifufuki tena ila watakapotokezea watu muhimu wa kuweza kufufua utambulisho wake.
Maana ya mashambulizi ya kiutamaduni ni kwamba kundi moja - la kisiasa na kiuchumi - linashambulia misingi ya kiutamaduni ya taifa fulani kwa malengo yake ya kisiasa na kwa ajili ya kulidhibiti taifa hilo. Kundi hilo huingiza vitu vipya katika nchi na taifa hilo lakini kwa kutumia nguvu na mabavu na kwa nia ya kuvifanya vitu hivyo vichukue nafasi ya utamaduni na itikadi za taifa jingine. Hayo ndiyo mashambulizi ya kiutamaduni. Lengo la mabadilishano ya kiutamaduni ni kushibisha utamaduni wa taifa jingine na kuukamilisha. Lakini lengo la mashambulizi ya kiutamaduni ni kufuta kabisa utamaduni wa mataifa mengine. Katika mabadilishano ya kiutamaduni, taifa linaloigiza kitu kutoka kwa mataifa mengine hutafuta vitu linavyopenda na vyenye faida kwake, kwa mfano kitu kama elimu n.k, na kuviigiza.
Mabadilishano ya kiutamaduni yanatupa fursa ya kuchagua, lakini katika mashambulizi ya kiutamaduni adui ndiye anayeamua nini cha kuchukua. Tunatumia mabadilishano ya kiutamaduni kujikamilisha, yaani kukamilisha utamaduni wetu, lakini mashambulizi ya kiutamaduni yanafanyika ili kuangamiza utamaduni wa watu. Mabadilishano ya kiutamaduni ni kitu kizuri, lakini mashambulizi ya kiutamaduni hayana jema ndani yake. Mabadilishano ya kiutamaduni hushuhudiwa wakati taifa linapokuwa na nguvu na uwezo, lakini mashambulizi ya kiutamaduni huja wakati taifa linapokuwa dhaifu.
Utamaduni wa Magharibi ni mjumuiko wa mambo mazuri na mabaya. Yeyote yule hawezi kudai kuwa utamaduni wa Magharibi wote ni mbaya; hapana; utamaduni wa Magharibi ni mithili ya utamaduni wa Mashariki, una mazuri na mabaya. Taifa elekevu na lenye akili huchukua yaliyo mazuri na kuyaingiza katika utamaduni wake na kuyaacha yaliyo shakii na mapotevu.
Utamaduni wa Kiislamu ni utamaduni mtukufu na wenye thamani kubwa ambao unaweza kuifikisha jamii ya mwanaadamu katika fakhari za hali ya juu na kuifanya kuwa azizi, bora, nyerezi na aali. Umma wa Kiislamu nao unaundwa na mataifa, vizazi na madhehebu tofauti. Ustaarabu mkongwe kabisa na utamaduni wa zamani zaidi ulikuwepo katika eneo hili ambalo wanaishi Waislamu. Anuwai na namna nyingi hizi za watu waliotawanyika katika maeneo mbalimbali ya kijiografia wako katika eneo nyeti na muhimu la sayari ya dunia na hilo pekee linaweza kuwa nukta ya kujivunia umma huu mkubwa wa Waislamu na wanaweza kutumia urithi, utamaduni na historia yao ya pamoja katika kujistawisha kwa upana zaidi.

 
< Nyuma   Mbele >

^