Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Mitazamo ya Kiongozi Muadhamu Kuhusu Demokrasia ya Kidini Chapa
16/08/2008

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Dondoo
Suala la msingi ni kwamba fikra ya Kiislamu katika mfumo wa Kiislamu haiwezi kutengana na mwelekeo wa wananchi. Mwelekeo wa wananchi katika utawala wa Kiislamu una msingi wa Kiislamu. Wakati tunaposema Mfumo wa Kiislamu tuna maana kwamba haiwezekani kutoorodheshwa wananchi ndani yake. Msingi na usuli wa haki za wananchi katika chaguo hili ni Uislamu wenyewe; hivyo demokrasia yetu - ambayo ni demokrasia ya kidini - ina falsafa na asasi yake.
Msingi wa demokrasia ya kidini unatofautiana na ule wa demokrasia ya Magharibi. Demokrasia ya kidini - ambayo ndio msingi wa chaguo letu na imetokana na haki na kutekeleza wajibu wa mwanaadamu kwa Mola wake - huwezi kusema ni mkataba tu. Watu wote wana haki ya kuchagua na haki ya kuainisha mustakbali wao. Demokrasia ya kweli ya wananchi ni demokrasia ya kidini ambayo inatokana na imani ya Mwenyezi Mungu na majukumu ya kidini.
Leo hii na katika mazingira kama haya yaliyopo tumeazimia kuionyesha na kuitangaza duniani nadharia ya kisiasa ya Uislamu na ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu - yaani demokrasia ya kidini. Neno Jamhuri lina maana ya demokrasia na Uislamu maana yake ni dini. Baadhi wanadhani kuwa wakati tulipokuja na fikra ya demokrasia ya kidini tulileta kitu kipya; hapana. Jamhuri ya Kiislamu maana yake ni demokrasia ya kidini. Uhakika wa demokrasia ya kidini ni kwamba, utawala unaongozwa kwa kuheshimu mafundisho ya Mwenyezi Mungu na kwa matakwa ya wananchi. Tatizo lililopo kwa tawala za kidunia ni kuwa ima ndani yake hamna miongozo ya Mwenyezi Mungu - mfano wake ni kile kinachoitwa demokrasia ya Magharibi ambayo inadai kuheshimu matakwa ya wananchi - au zina miongozo ya Mwenyezi Mungu ndani yake kama kweli imo ama ni madai yao tu - lakini haziheshimu maamuzi ya wananchi Tawala nyingine hazina lolote katika hayo mawili na hivyo ndivyo zilivyo tawala nyingi duniani. Yaani si wananchi wanapewa nafasi ya kuamua mambo ya nchi yao na si miongozo ya Mwenyezi Mungu inapewa umuhimu ndani yake.
Katika utamaduni wa Kiislamu watu bora ni wale wanaowanufaisha zaidi wenzao. Demokrasia ya kidini ni tofauti na demokrasia za udanganyifu na za kupumbaza watu, ila huwa ni tawala za kuhudumia watu kwa ikhlasi, pasina masimbulizi bali kwa kutarajia radhi za Mwenyezi Mungu na kutekeleza wajibu wa kidini. Demokrasia katika utawala wa Kiislamu ni demokrasia ya kidini yaani husimama juu ya misingi ya Uislamu na si mkataba tu. Ndani yake inabidi kujua mitazamo watu na kuheshimu maamuzi ya wananchi kila inapolazimu na hapo ndipo miongozo ya Uislamu huheshimiwa. Si mithili ya nchi za kidemokrasia za Magharibi kwamba demokrasia iwe sawa na mkataba ili iwe rahisi kutouheshimu. Katika utawala wa Jamhuri ya Kiislamu, demokrasia ni jukumu la kidini. Viongozi wanakula kiapo cha kidini cha kuheshimu sifa hiyo, wana jukumu na watakwenda kuulizwa na Mwenyezi Mungu. Huo ni miongoni mwa usuli na misingi mikuu ya Imam wetu mtukufu.
Demokrasia za Magharibi zina maana ya kulinda manufaa na matakwa ya matajiri na mabepari wanaodhibiti mustakbali wa jamii. Ni katika kalibu hiyo tu ndipo rai na matakwa ya wananchi yanapoheshimiwa. Lakini kama wananchi watakata shauri linalokwenda kinyume na manufaa ya mabepari na wenye nguvu za kifedha na kiuchumi - na kutokana na nguvu hizo kuwa na nguvu pia za kisiasa - basi hukosekana dhamana kabisa ya kuheshimiwa na kutekelezwa shauri hilo na kwa kawaida tawala za demokrasia hiyo hazipigi magoti mbele ya matakwa kama hayo ya wananchi. Matakwa na demokrasia zote hizo ziko ndani ya fremu moja ngumu isiyovunjika. Katika nchi za zamani za kisoshalisti - ambazo nazo zilikuwa zikidai ni nchi za kidemokrasia - fremu hiyo tunayoizungumzia hapa ilikuwa ni chama tawala.
Leo hii demokrasia ya kidini ndicho kigezo na kifaa bora cha kuweza kutumiwa na maafisa wa serikali kila pale wanapopaswa kurekebisha mwenendo. Mosi serikali inabidi iundwe kwa misingi ya matakwa na kura za wananchi. Hilo lina maana kuwa wananchi ndio wanaochagua serikali na viongozi wa serikali kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Pili kuchaguliwa watu kama nyinyi na mimi kuwa viongozi, kuna maana kwamba tuna majukumu makubwa na mazito mbele ya waliotuchagua.
Demokrasia haipaswi kufungwa tu katika pingu za propaganda za kuwaburuza watu kwenye masanduku ya kupigia kura na halafu kuwasahau baada ya kuingia madarakani. Kupata kura za wananchi ni hatua moja ambayo inabidi ifuatiwe na hatua ya pili nayo ni aliyechaguliwa kutekeleza ipasavyo majukumu yake.
Sifa nyingine ya demokrasia ni kuepuka kuchupa mipaka na kufanya uadilifu uenee miongoni mwa wananchi. Yaani viongozi serikalini wapanue wigo wa mawasiliano yao na wananchi na wajaribu kuwafurahisha na kuvutia ridhaa ya watu.
Ukweli ni kwamba Mfumo wa Kiislamu - Mfumo ulio chini ya bendera ya tawhidi na dini - unaweza kuwafikishia watu demokrasia kwa njia ya wazi na bora kabisa, na ni tofauti kikamilifu na propaganda za mabeberu wa dunia ya demokrasia ya kiliberali. Wanachotaka kusema ni kuwa wao pekee yao ndio wenye demokrasia. Wanashindwa kuvumilia kuona umedhihiri Mfumo wa Kiislamu na kidini ukiwa na matukufu ya hali ya juu ya kiimani na kuweza kuweka misingi ya demokrasia. Kigezo cha demokrasia yetu hakitokani na tawala za Mashariki wala za Magharibi, bali kigezo chetu ni Uislamu na wananchi wetu wameuchagua Uislamu kwa kujua thamani yake.

 
< Nyuma   Mbele >

^