Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hija: Faradhi Isiyo na Mfano Chapa
03/05/2009
Ifuatayo ni sehemu ya ujumbe wa Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alioutoa tarehe 20/4/1994 kwa ajili ya Mahujaji. 

Faradhi ya Hija, hakika ni faradhi isiyo na mfano. Kiasi kwamba endapo tutayatalii kwa kina mafundisho yote ya Kiislamu hatutoweza kupata yaliyo mfano wake. Hija ina hali maalumu ambapo upande wa kimaanawi una hali ya kipekee. Chukulia mfano wa sala moja unayosali huwa unamdhukuru Mwenyezi Mungu kwa dakika chache. Lakini katika Hija, tokea pale unapoanza kutekeleza amali za faradhi hiyo zinazochukua muda wa siku kadhaa, iwe unapokuwa ndani ya eneo la Kaaba au mwendo baina ya Safa na Marwa, au Arafa, au Mash'ar, au Mina au katika amali nyingine mbalimbali, au katika kutufu, au katika kitako na visimamo mbalimbali, au katika harakati za kutabaruku kutoka sehemu moja hadi nyingine - mambo yote hayo yanahesabiwa kuwa ni kumdhikiri Mwenyezi Mungu. Hiyo ni katika upande wa kimaanawi ambao unaonyesha kuwa dhikri ya Mwenyezi Mungu katika Hija ni kitu chenye uwanja mpana.

Kwa upande mwingine, upande wa kidunia na unaohusiana na maisha wa Hija nao pia hauna mfano wake. Yaani (Hija) si faradhi inayomhusu mtu binafsi au taifa moja tu, bali inauhusu ulimwengu mzima wa Kiislamu. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameainisha mahala maalumu, na katika wakati maalumu- yaani siku maalumu - na kuwaita Waislamu wote mahala hapo. Je, ingewezekana Waislamu wote kujumuika mahala hapo lakini si kwa pamoja, bali makundimakundi, na katika kipindi chochote cha mwaka na si siku maalumu? Kuna haja ya kuzingatiwa zaidi nukta hii ya Hija, kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu hakusema tu Waislamu wote wakutanike (wakati wowote) huko Makka, Mina, Mash'ar na Arafa. Kwa sababu kama msingi wa amri hiyo ungekuwa ni watu tu kuelekea na kukusanyika kwenye maeneo hayo, ingewezekana katika wakati wowote wa kipindi cha mwaka watu kuenda na kukusanyika huko. Kama ni hivyo, kwa nini basi Mwenyezi Mungu Mtukufu ameamuru Waislamu wote kwa pamoja wajumuike mahala hapo, tena basi katika siku maalumu? Hii ndiyo nukta muhimu na ya msingi.

Ni wazi kwamba lengo la kutakiwa uwepo mkusanyiko wa aina hiyo ni kwa ajili ya kutaka Waislamu wote wakutane na kuwa pamoja. Yaani wajihisi kuwa ni wamoja na umma mmoja na katika mtazamo mpana zaidi waweze kuhisi adhama inayotokana na kujumuika pamoja watu wa rangi na mataifa mbalimbali. Kama si kuzingatiwa suala hilo kusingekuwa na ulazima wa kutakiwa Hija itekelezwe katika siku maalumu na ya idadi maalumu. Na huko Umma wa Kiislamu - yaani kila taifa katika mataifa ya Umma wa Kiislamu - unatuma watu miongoni mwao katika siku moja waelekee mahala pamoja kwa lengo la kujumuika pamoja, (ni mahala pa kujiuliza) mjumuiko huo wa pamoja ni wa lengo gani? Hizo ni nukta za kutaamali ambazo kama alivyoeleza Imam Jaafar Sadiq (alayhi ssalatu wassalam): "Hufahamika hii (hija) na mfano wake katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu," - yaani kila Mwislamu anapaswa aelewe mafundisho ya Qur'ani na Uislamu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameliita kundi moja kutoka mataifa yote ya Kiislamu na kuwaambia: "Njooni katika siku hizi maalumu ili mjumuike na kukutanika pamoja." - "Kisha miminikeni kutoka mahali wamiminikapo watu wote" (2:199) yaani nyote muwe katika harakati ya pamoja. Miminikeni nyote kwa pamoja na mtufu pia nyote kwa pamoja. Mjumuiko huo wa pamoja una maana gani? Ni kwa ajili ya kufanya nini Waislamu kutoka pembe mbalimbali za dunia wakutanike mahala pamoja? Je, wakusanyike pamoja, na katika hali ya ukimya wawe wanatizamana wenyewe kwa wenyewe, na baada ya siku kadhaa warejee mijini kwao?! Kwa nini wakusanyike pamoja? Wakusanyike pamoja ili kuzungumzia hitilafu zao? Kujumuika huko ni kwa maana gani? Jibu ni kuwa kujumuika pamoja na mahala pamoja watu kutoka mataifa yote, mahala penyewe basi ni mahala patakatifu, kunaweza kuwa na maana na faida moja tu. Faida na maana hiyo ni kuwa wakusanyike pamoja ili kuweza kuchukua maamuzi juu ya mustakabali wa Umma wa Kiislamu, ambapo katika mjumuiko huo na wakiwa kama umma wachukue hatua za maana na za kivitendo. Hatua hizo za maana na za kivitendo zinaweza kuwa katika ubora gani? Katika ubora ambao endapo itafika siku - ambayo tuna matumaini kuwa itafika - mataifa ya Kiislamu yawe yamepiga hatua kubwa kimaendeleo kiasi kwamba wakati Waislamu wanapojumuika pamoja katika Hija, wakati wa kongamano hilo kubwa kabisa la watu, wawakilishi wa mataifa waweze kuunda majlisi kubwa ya maelfu ya watu, majlisi ambayo itaweza kupanga na kuwasilisha miswaada, miswaada ambayo itapasishwa na mahujaji wote kutoka nchi mbalimbali katika kongamano hilohilo la Hija na kisha kufikishwa kwa serikali na mataifa ya Kiislamu kwa ajili ya utekelezwaji.

Hii ndiyo hatua bora na ya maana zaidi ambayo kwa bahati mbaya leo hii haiwezi kutekelezeka. Sababu ni kuwa mataifa ya Kiislamu hayajaweza kupiga hatua kiasi hicho katika uwanja huo; na hasa kwa vile serikali zenyewe pia haziyasaidii mataifa yao. Sasa kama haiwezekani kuchukua maamuzi hayo ya kivitendo katika msimu wa Hija kwa sasa, basi ni wajibu gani unaopaswa kutekelezwa huko kwa sasa? (Wajibu uliopo) ni kuwa kadiri wanavyoweza wawakilishi wa mataifa ya Kiislamu waonyeshe mshikamano kuhusiana na masuala ya ulimwengu wa Kiislamu, ambapo mbali na kusisitiza juu ya suala la umoja baina yao, waonyeshe kujibari na kujiweka mbali kwao na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu. Hii ndiyo hatua ndogo kabisa iliyobainishwa na Uislamu ambayo inatarajiwa na inawezekana kutekelezwa katika Hija.

(Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu kwa maafisa waandalizi wa Hija. 20/4/1994)
 
< Nyuma   Mbele >

^