Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hija na Kukabiliana na Matishio Mawili Chapa
03/05/2009
Ifuatayo ni sehemu ya Ujumbe wa Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alioutoa tarehe 23/4/1996 kwa ajili ya Mahujaji wa Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu.

Hija, ambayo ni chemchemu isiyokauka ya takwa na umaanawi, kheri na baraka hutoa rehma na baraka zake kila mwaka kwa ulimwengu wa Kiislamu na pia kwa kila Mwislamu aliyefanikiwa kuitekeleza, ili kila mtu na kila mjumuiko wa watu uweze kufaidika na chemchemu hiyo kwa kadiri ya ustahiki wao na uwezo walionao.

Mahujaji wa nyumba ya Mwenyezi Mungu sio wao peke yao wanaofaidika na chemchemu hiyo ya rehma isiyokauka. Endapo faradhi hii tukufu itafahamika na kutekelezwa sawasawa, mataifa na umma mzima wa Kiislamu katika kila pembe ya dunia watafaidika na baraka zake.

Wanadamu siku zote hupata madhara kutokana na njia mbili: ya kwanza, kutoka ndani ya nafsi zao ambayo hutokana na udhaifu wa kibinaadamu, matamanio yaliyoshindwa kudhibitiwa, hali ya shaka na kutokuwa na imani kabisa pamoja na silka na hulka zinazomharibu mtu. Na njia ya pili, inatokana na maadui wa nje ambao kutokana na mwenendo wao wa ubabe, utumiaji mabavu na udhalimu huyavuruga na kuyachafua mazingira ya maisha ya watu na mataifa mbalimbali, na kutokana na vita, dhulma na uburuzaji husababisha mabalaa na majanga kwa watu na mataifa hayo. Mazingira ya jamii za Kiislamu - iwe ni watu au mataifa - daima yamekuwa yakiandamwa na matishio mawili hayo ambayo leo hii yanakabiliwa zaidi na matishio hayo kuliko wakati mwingine wowote.
Kwa upande mmoja, kuenezwa kwa makusudi ufuska na uchafu katika nchi za Kiislamu na kuzitwisha utamaduni wa kimagharibi kunakopata msukumo pia wa baadhi ya tawala tegemezi, kuanzia kwenye tabia za mtu binafsi, ujenzi wa miji, mazingira ya kijamii, magazeti na kadhalika; na kwa upande mwengine, kutoa mashinikizo ya kijeshi, kisiasa na kiuchumi kwa mataifa ya Kiislamu na kufanya mauaji huko Lebanon, Palestina, Bosnia Herzegovina, Kashmir, Chechneya, Afghanistan na kwengineko, ni ushahidi wa wazi wa kuwepo kwa matishio mawili haya katika mazingira ya ulimwengu wa Kiislamu. Hija ni mto unaotiririka maji muda wote na ishara ya milele ya Mwenyezi Mungu ambao Waislamu wanaweza kuutumia hadi mwisho wa maisha yao kujisafisha na vumbi na uchafu walionao na kujiponya na machungu, mateso, na maradhi yaliyowasibu; na kwa msaada wa hazina hiyo ya milele kuweza kujilinda na kujikinga katika kila zama na matishio yote mawili hayo.

Katika Hija, takwa, dhikri, unyenyekevu na mazingatio kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndio wenzo wa kukabiliana na tishio la kwanza; na kujumuika pamoja, umoja na kuhisi adhama na nguvu za umma mkubwa wa Kiislamu ambayo Hija ndiyo dhihirisho lake ndio wenzo wa kukabiliana na tishio la pili.

Kila pale hali mbili hizo zinapoimarishwa na kupata nguvu katika Hija, kinga na uwezo wa watu na jamii za Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na matishio mawili hayo unakuwa imara zaidi. Na kila pale hali mojawapo au hali zote hizo mbili zinapodhoofika au kukosekana kabisa, ndivyo vivyo hivyo Umma wa Kiislamu nao - iwe ni kwa watu mmojammoja au mataifa na nchi kwa juml a- unavyoweza kudhurika kwa urahisi zaidi.

Katika maandiko ya sheria tukufu za Kiislamu na ndani ya Qur'ani Tukufu, hali zote mbili hizo za Hija zimefafanuliwa bila kubakisha shaka yoyote kwa wale wanaofunua macho yao (kuona) na walio na nyoyo zenye insafu. Baada ya kutolewa amri ya: "Basi mtajeni Mwenyezi Mungu kama mlivyokuwa mkiwataja wazee wenu; bali mtajeni zaidi (Mwenyezi Mungu", (2:200) imekuja amri ya: "Na ni tangazo litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, kujuvywa watu siku ya Hija kubwa ya kwamba Mwenyezi Mungu yu mbali na washirikina (makafiri); na pia Mtume Wake (yu mbali nao)", (9:3) sambamba na aya ya: "Nyama zao (wanyama hao wanaochinjwa) hazimfikii Mwenyezi Mungu wala damu zao, lakini inamfikia (Kwake Mwenyezi Mungu) taa, (utawa) yenu. Namna hivi tumewatiisha kwenu, ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa sababu ya huku kukuongozeni. Na wape habari njem wafanyao mema", (22:37) na kisha imeteresmhwa aya ya kutia matumaini isemayo: "Ili washuhudie manufaa yao." (22:28).

Kila hatua, agizo au kampeni yoyote ya kujaribu kufifilisha au hata kufuta kabisa moja kati ya hali mbili hizo ni sawa na kukabiliana na aya na maamrisho ya Qur'ani Tukufu.

(Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu kwa mnasaba wa kutekelezwa ibada adhimu ya kimaanawi na kisiasa ya Hija. 23/4/1996).
 
< Nyuma   Mbele >

^