Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Maana ya Usimamizi Chapa
05/10/2009

Maana ya Usimamizi:

Umuhimu wa Usimamizi
Vipimo vya Usimamizi

Usimamizi na Mihimili Mitatu ya Dola

Usimamizi na Serikali
Usimamizi na Bunge
Usimamizi na Mahakama

Usimamizi juu ya Kiongozi Mkuu

Usimamizi juu ya Kiongozi Mkuu
Utaratibu wa Usimamizi wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu

Majukumu ya Usimamizi ya Baraza la Walinzi wa Katiba

Usimamizi wa Upitishaji wagombea
Usimamizi wa uchaguzi

Usimamizi wa Umma

Kuamrisha mema na kukataza maovu, moja ya madhihirisho ya usimamizi wa umma
Kuamrisha mema na kukataza maovu katika ngazi ya viongozi
Matunda ya usimamizi wa magazeti
Usimamizi juu ya magazeti

Usimamizi wa Mwenyezi Mungu

Maana ya Usimamizi


Maana ya Usimamizi:

Umuhimu wa Usimamizi

Usimamizi juu ya walio chini yake mtu ni jambo muhimu sana. Ninasisitiza na kutilia mkazo kwamba nyinyi ndugu wapenzi- ambao ni viongozi wa juu na wakurugenzi waandamizi- mulipe umuhimu mkubwa suala la usimamizi kwa walio chini yenu. Ni kuwa kwenu macho na makini na pale macho yenu yanapoangazia kikamilifu eneo la majukumu yenu ndipo mnapoweza kuwa na hakika wa usahihi wa kazi na maendeleo ya kazi hiyo. Ikiwa mtaghafilika kuna uwezekano wa kutokea kasoro katika sehemu ile ile mliyoghafilika nayo. Majimua za watu si kama mashine, kwamba mtu anapobonyeza kitufe tu mashine hiyo inaanza kufanya kazi yenyewe. Majimua za watu ni mjumuiko wa irada, fikra, mitazamo, dhuku, matashi na matamanio sahihi na ghalati. Kwa hivyo inawezekana kile mlichoamua na kupanga kifanyike katika majimua yenu kikakwama kutokana na kukabiliwa na kizuizi kinachotokana na matashi, fikra, vionjo, mitazamo na irada hizo mbali mbali. Ni mithili ya mkondo wa maji unaokumbana na jiwe; mchirizi mwembamba wa maji hurudi unakotoka unapokabiliana hata na changarawe. Kwa hivyo kizuizi hicho kinapasa kiondolewe. Na hilo haliyumkiniki ila kwa usimamizi. Usimamizi una umuhimu sana.

Juu ya ukurasa

Vipimo vya Usimamizi

Sheria na kanuni vinapasa viwe ndio vipimo katika suala la usimamizi na si dhuku na utashi wa binafsi. Msitumie kabisa utashi wa binafsi. Inapasa mfanye kazi kwa namna ambayo mtaweza kuwa na jibu mbele ya Mwenyezi Mungu mtukufu na waja wake. Uzingatiaji wa aina yoyote ile usije ukawa kikwazo cha utekelezaji wa sheria. Masuala ya kiakhlaqi yanapasa yachungwe pia; miongoni mwa hayo ni kwamba masuala ya binafsi ya watu yasichanganywe na yale masuala makuu; kwa mfano masuala ya kimrengo na kisiasa yasichanganywe na misimamo halisi ya Mapinduzi na iliyo dhidi ya Mapinduzi. Mapenzi na chuki pia ni hivyo hivyo; baadhi ya wakati mtu huwa anapendezwa na mtu fulani na anachukizwa na mtu mwingine; kwa kweli inapasa tutahadhari suala hili lisiingizwe katika kadhia za ngazi yoyote ile. Haifai kuwatuhumu watu pasina kufanya uchunguzi. Haifai kutoa hukumu ya kumhusisha mtu na kosa fulani kwa sababu tu ya mambo ya kidhahiri ya kawaida kabisa.

Juu ya ukurasa

Usimamizi na Mihimili Mitatu ya Dola

Usimamizi na Serikali

Huu ni usimamizi wa hii majimui ambayo iko chini ya udhibiti wenu nyinyi viongozi. Injini hii ya mfumo wa kiidara na injini hii ya mfumo wa utekelezaji, mbali na kwamba hiki ni chombo kisichoepukika, lakini kama hamtokichunga kitakuwa ni kitu hatari. Uchungaji huo ndicho kitu kitakachokuwezesheni nyinyi kuyafikia malengo kwa haraka na kwa urahisi. Kama hakutakuwepo chombo cha utekelezaji na usimamizi wenu, hamtoweza kulifikia lengo lolote; na wakati huo huo pale injini hii hii itakapoamua, inaweza kukukwamisheni msiweze kulifikia lile lengo mnalolifatilia; kutokana tu na jinsi muundo, na muhimu zaidi ya hilo, vile utakavyokuwa usimamizi wenu juu ya majimui hii. Kama mtaifanyia usimamizi, itakuwa chini ya mamlaka yenu; la kama mtaghafilika nayo, nyinyi mtakuwa chini ya mamlaka yake; na hata kama mtakuwa watu wazuri kiasi gani, hamtoweza kuidhibiti. Hatuwezi kusema kuwa watu wote unaowachagua uhakikishe kuwa ni watu wazuri; kwani itawezekana kweli, kwamba uweke kipimo cha aina moja kisha uwachukue wafanyakazi wenu elfu moja, elfu mbili au hata elfu kumi na kuwapima kuanzia mtu wa kwanza hadi wa mwisho kwa kutumia kipimo hicho hicho? Kitu kama hicho kinawezekana kweli? Na tujaalie umewachagua kwa kutumia kipimo hicho, kwani watu wazuri wanaendelea daima kubaki kuwa watu wazuri? Kwani wasiwasi wa shetani hauwezi kuwaathiri watu wazuri? Kwa hivyo kitu kinachotoa hakikisho, ni nyinyi kutumia wakati wenu kwa ajili ya usimamizi.

Ikiwa mudiri fulani wa juu ataugawa wakati wake, pengine itapasa kusema kuwa nusu ya wakati wake huo autumie kwa ajili ya kusimamia idara yake tu na nusu iliyobaki aitumie kwa kazi nyingine za kukaa na kufikiria mambo, kupanga sera, kutoa maagizo, kufanya vikao na mfano wa hayo. Usimamizi juu ya chombo hiki, maana yake ni kuwa karibu nacho muda wote; suala la ufatiliaji pia ni sehemu mojawapo ya usimamizi huo. Bila shaka usimamizi wa Rais kwa mawaziri usije ukagongana na uhuru wa utendaji wa mawaziri katika kazi zao. Kwa sababu majukumu ya mawaziri ni majukumu ya kisheria kwa sababu wamepigiwa na Bunge kura ya kuwa na imani nao na hivyo inapasa wawe na uhuru wa utendaji. Hata hivyo usimamizi huu unakuwepo hata kwa mawaziri pia. Uhuru wao wa utendaji uko pale pale, lakini usimamizi wa Rais pia unapasa uwepo kwa uzito wake kamili unaostahiki.

Juu ya ukurasa

Usimamizi na Bunge

Kupasisha sheria ambazo zinaipa jukumu na uwezo serikali wa kuendesha mambo kwa njia sahihi na kisha kusimamia utekelezaji wake kupitia njia za kisheria, ndilo jukumu la kwanza la Bunge; na utekelezaji wa jukumu hili unahitajia kuwepo ushirikiano na kuwa kitu kimoja kati ya Bunge na Serikali, na uungaji mkono wa Bunge kwa Serikali. (Kwa kweli) jukumu la Bunge ni kutunga sheria na kusimamia utendaji wa wakuu wa serikali; na kwa mujibu wa Katiba (ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran), Bunge ndilo msimamizi wa serikali. Ikiwa katika suala fulani, serikali itapiga hatua vibaya au ikafuata njia pogo; ikafuata njia isiyo sahihi, au Mungu aepushie mbali ikaitumia vibaya nafasi yake ukatokea ufisadi, Bunge ndicho chombo kinachoweza kuzuia kutokea ufisadi na ukengeukaji huo.

Mbali na kushirikiana na serikali tumishi na hasa Rais wa serikali hiyo, Bunge linatekeleza pia nafasi yake ya usimamizi, ambayo mfano wake hai ni hili suala la Ofisi Mkaguzi Mkuu. Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ni chombo muhimu sana. Bajeti kubwa mno ya taifa hili, ndilo pato pekee kubwa la umma linalokuwa chini ya mamlaka ya vyombo mbali mbali; inabidi ieleweke bajeti hii imetumikaje. Suala la uwekaji sawa hesabu ya bajeti na kuelewa ukweli na uwongo juu ya kazi iliyofanyika ni mojawapo ya nyenzo muhimu za usimamizi za Bunge; haifai kughafilika na jambo hili. Katika kutumia nyenzo za usimamizi, mawasiliano yanayofanywa na vyombo vya utekelezaji na vinavyofanyiwa usimamizi, yanapasa yafanyike kulingana na sheria. Baadhi ya mawasiliano yenye kukengeuka mkondo sahihi yana madhara kikamilifu kwenu nyinyi. Na hili linajenga dhana ndani ya fikra kwamba kuna mawasiliano yenye walakini na yasiyo sahihi kati ya baadhi ya vyombo vilivyoko chini ya usimamizi. Bila shaka yoyote hali hii itavuruga usimamizi, itavunja nguvu zake na kuondoa uwezo mkubwa wa Bunge ambao sheria umelipatia, na matokeo yake ni kwamba Bunge halitokuwa na athari tena.

Usimamizi wa Bunge ni kitu chenye ulazima sana; ama ufanyike kwa kutumia nyenzo hizi hizi za usimamizi kama vile Ofisi ya Mkaguzi Mkuu na vyombo kama hivyo, au wabunge wenyewe waifanye kazi hiyo moja kwa moja; kwa njia kama vile kuuliza masuali, kukumbusha na vitu vingine kama hivyo ambavyo ni nyenzo za usimamizi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge); nyenzo hizo zinahitajika sana na zina umuhimu sana. Hata hivyo nyenzo hizo zisije zikawa sababu ya kuleta mgongano kati ya vyombo hivyo viwili. Ushirikiano kutoka pande mbili kati ya vyombo vya utungaji sheria na utekelezaji unaweza kufungua njia ya maendeleo kwa nchi na kurahisisha na kuharakisha harakati zenye manufaa. Ni wazi kuwa kufanya hivyo hakuna maana ya kuzembea katika utekelezaji wa jukumu la usimamizi la Bunge. Bunge linapaswa kuhakikisha dhana njema linayojenga ya kuwa na imani na watendaji wakuu wa serikali iwe ni ya kutumia vipimo vya ushikaji dini na uswalihina wa mtu, utaalamu wake na ufanisi wake wa kazi, na uaminifu wake kwa mfumo na wananchi; na wala lisiwe na mzaha katika usimamizi wa kisheria juu ya utendaji wa viongozi hao. Uhusiano huo uwe ni uhusiano safi kiasi cha kuifanya serikali iwe inaliangalia Bunge kama mtatuzi wa masuala makubwa makubwa na kufaidika na hekima na uwezo wake wa kuzingatia maslahi katika utekelezaji wa majukumu yake magumu.

Juu ya ukurasa

Usimamizi na Mahakama

Mhimili wa Mahakama unapaswa kulikaribisha suala la usimamizi wa sheria. Sheria ni mojawapo ya nyenzo za usimamizi. Sheria, yenyewe ni kitu kilichorasimishwa ndani ya Mhimili wa Mahakama, na ni wenzo wenye taathira na umuhimu mkubwa mno kwa ajili ya usimamizi juu ya mhimili wa Mahakama. Sheria iwe ndiyo kipimo, na wala sheria zisikiukwe; zisitumike kwa watu maalumu tu; zisiwekewe mipaka maalumu; katika kueneza sheria, kisifutwe kitu chochote kile kwa sababu hii na ile. Alaa kulli hal mhimili wa Mahakama unapaswa kukaribisha aina yoyote ile ya usimamizi. Chochote kile kinachofanyiwa usimamizi, chochote kile kinachotolewa maoni, hata ukosoaji wa kiinsafu, vinapaswa kukaribishwa kwa mikono miwili. Hili ni jambo zuri sana. Yule ambaye faili lake ni safi- iwe ni katika masuala ya kifedha au masuala yasiyokuwa ya kifedha- haogopi kufanyiwa uchunguzi. Viruhusuni vyombo vinavyohusika na kazi hii, kama vile Idara ya ukaguzi na taasisi nyingine mbali mbali za usimamizi, na vile vile taasisi zilizoko nje ya vyombo vya Mahakama, kama vile wanafikra wa Hawza na Vyuo Vikuu na wataalamu wa sheria nchini watoe maoni yao, watoe mapendekezo na ukosoaji; hayo ndiyo yanayoimarisha mhimili wa Mahakama na kuupa ukakamavu. Alhamdulillah nguzo za mhimili wa Mahakama ni nguzo nzuri; misingi yake ni misingi mizuri sana na imetokana na mizizi mitukufu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kutegemea hukumu za Kiislamu; hauna woga wa kitu chochote na ni mhimili imara kabisa; kadiri unavyokabiliwa na changamoto zaidi za kisheria na changamoto za usimamizi ni bora kwake na zinazidi kuufanya uwe mkakamavu zaidi.

Juu ya ukurasa

Usimamizi juu ya Kiongozi Mkuu

Usimamizi juu ya Kiongozi Mkuu

Hakuna mtu yeyote aliye juu zaidi ya usimamizi. Kiongozi Mkuu mwenyewe, naye pia hayuko juu ya usimamizi; seuze vyombo vinavyohusiana na Kiongozi Mkuu. Kwa hivyo usimamizi unapasa kufanywa kwa wote. Usimamizi juu ya watu wanaotawala- kwa vile kwa kawaida utawala maana yake ni kukusanyika mali na madaraka; yaani mali za Baitul mal na nguvu za kijamii na nguvu za kisiasa huwa mikononi mwa sehemu fulani ya watawala- kuna kazi moja ya lazima na ya wajibu na ambayo inapasa kufanywa ili kuhakikisha watawala wanachunga amana, hawatumii vibaya madaraka yao na wala nafsi zao hazichupi mpaka. Tab'an ugawaji huu- wa taasisi zilizoko chini ya Kiongozi Mkuu na taasisi zisizo chini ya Kiongozi Mkuu- ni ugawaji usio sahihi; sisi hatuna kitu kama hicho. Kwa mujibu wa Katiba mihimili mitatu ya dola, ya Serikali, Mahakama na Bunge iko chini ya Kiongozi Mkuu. Vyombo vingine pia ni hivyo hivyo. Kuwa chini ya Kiongozi Mkuu maana yake si kwamba Kiongozi Mkuu ndiye anayeendesha taasisi fulani; lakini alaa kulli hakuna tofauti; lazima vyote hivyo viwe chini ya usimamizi. Bila shaka taasisi zote za serikali na za umma inapasa zisiwe na khofu yoyote ya kufanyiwa uchunguzi. Wahenga wamesema: "yule ambaye hisabu yake ni safi, ana sababu gani ya kuwa na khofu". Wahakikishe hisabu zao zinakuwa safi ili wasiwe na khofu ya kufanyiwa ukaguzi. Kwa hivyo sio hivyo kwamba taasisi zinazohusiana na Kiongozi Mkuu zinasameheka kuwa chini ya usimamizi.

Na huo usimamizi ufanyike kwa uzito unaostahiki. Huo ndio mtazamo wangu mimi, na mara kadhaa nimelieleza hilo pia kwa wajumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu, wajumbe wasiokuwa wa baraza hilo na watu wengine pia. Mimi ninapenda kuwepo usimamizi, na huwa ninalaumu sana pale watu wanapokwepa kufanya usimamizi kuhusiana na mtu au sehemu fulani. Kuhusiana na mimi mwenyewe pia, hufurahi zaidi kila unapofanyika usimamizi zaidi; yaani huwa sihisi hata chembe kwamba usimamizi unaniletea uzito fulani. Kwa hivyo hufurahi unapofanyika usimamizi huu. Na bila shaka kama mtu amefanya usimamizi na kutambua kitu fulani, njia ya kufanya ni kulipa taarifa Baraza la Wanazuoni Wataalamu; na bila shaka wao wataitumia taarifa hiyo.

Juu ya ukurasa

Utaratibu wa Usimamizi wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu

Kazi ya kwanza kiumuhimu kwa Wanazuoni Wataalamu ni kuchagua(Kiongozi Mkuu), na katika hatua ya pili ni kusimamia na kuchunguza hali ya hivi sasa ya Kiongozi Mkuu aliyepo ili waweze kuelewa na kuona kama je bado ana sifa zinazostahiki? Je elimu yake, uchamungu wake, uongozi wake, ikhlasi yake na ukweli na uaminifu wake, bado vingalipo au vimeshuka chini ya kiwango kinachotakiwa? Inapasa wayasimamie na kuyachunguza masuala hayo. Hii ndiyo kazi muhimu ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu. Hakuna chombo kingine chochote nchini kinachoweza kuifanya kazi hii muhimu na ambacho sheria imekipa idhini na jukumu la kuifanya kazi hiyo. Baraza la Wanazuoni Wataalamu lina tume ya uchunguzi; tume hiyo ya uchunguzi ndiyo yenye jukumu la kuchunguza kazi za Kiongozi Mkuu. Kazi ya tume hiyo si ya mwaka mara moja; wao wanafanya kazi yao wakati wote, nazo kazi anazofanya Kiongozi Mkuu zinaonekana mbele ya macho ya watu wote. Bahati nzuri taasisi ya Kiongozi Mkuu na kazi za Kiongozi Mkuu si mambo yaliyojificha; kwa sababu majukumu ya Kiongozi Mkuu na utaratibu wake wa utendaji unajulikana wazi. Nayo tume hiyo inakuja, inafanya utafiti, inachunguza na kuuliza masuali. Nyuma ya tume hiyo kuna Baraza la Wanazuoni Wataalamu ambalo tume hii inakwenda mbele yake na kuwasilisha ripoti yake. Katika siku moja hadi mbili ambapo wanakuwa na kikao, wajumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu huwa wanajadili mambo mengi. Si kwamba wanaishia kutoa taarifa moja tu. Ndani ya vikao hivyo hufanyika mijadala mingi na kutolewa mawazo na maoni mbali mbali. Kwa hivyo wao wanaifanya kazi yao. Na si jambo dogo kwa taasisi hiyo yenye uzito mkubwa kuwa na kikao mara mbili kwa mwaka. Hapo kabla vikao vya Baraza la Wanazuoni Wataalamu vilikuwa vikifanyika mara moja kwa mwaka, lakini tokea miaka kadhaa ya hivi karibuni, baraza hilo linafanya vikao mara mbili. Na nyuma ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu kuna wananchi pia.

Juu ya ukurasa

Majukumu ya Usimamizi ya Baraza la Walinzi wa Katiba

Usimamizi wa Upitishaji wagombea

Usimamizi wa upitishaji wagombea ni moja kati ya sheria. Usimamizi huu wa Baraza la Walinzi wa Katiba unafanyika kulingana na sheria na kwa kutegemea katiba. Misingi yake na chimbuko lake iko kwenye katiba, na ipo na imepitishwa pia katika sheria za kawaida. Usimamizi huu haufanyiki kwa raia na wananchi wa kawaida; sheria hii ipo ili kuhakikisha mtu asiyefaa, mtu mwenye madhara na mtu mbaya haingii kwenye chombo hiki nyeti. Usimamizi huu wa upitishaji wagombea hauhusiani na Bunge tu; unafanyika kwa ajili ya Urais pia. Usimamizi wa upitishaji wagombea uko kwa ajili ya kuhakikisha watu ambao kwa mujibu wa sheria za nchi, hawana sifa zinazostahiki za kuingia kwenye chombo hicho nyeti- iwe ni Bunge, Rais au sehemu nyinginezo ambapo huwa unafanyika usimamizi huu, kama vile Baraza la Wanazuoni Wataalamu na sehemu nyinginezo, wanazuiwa na kutoweza kuingia kwenye vyombo hivyo nyeti. Usimamizi wa uidhinishaji ni kitu kizuri; si kitu kibaya; wale wanaolaumu na kukosoa, madai yao ni kwamba Baraza la Walinzi wa Katiba linawakubali na kuwakataa watu kulingana na mielekeo ya kisiasa. Bila shaka jambo hili halina ukweli. Wao wahusika wa Baraza la Walinzi wa Katiba wamekuwa kila mara wakilikanusha dai hilo; mimi pia kwa kadiri ambavyo nimeshuhudia kazi zao kwa karibu, sijahisi kama kuna kitu kama hicho. Inawezekana mtu wakati fulani au mahali fulani akawa hakufahamu jambo sawa sawa au akafahamu kimakosa, ambapo hilo ni suala jengine; lakini msingi unaotumika ni msingi wa kisheria.

Juu ya ukurasa

Usimamizi wa uchaguzi

Kusimamia uchaguzi ni kazi yenye umuhimu mkubwa mno; kwa sababu uchaguzi safi unapelekea kupatikana Bunge safi; na Bunge safi linapelekea kutungwa sheria safi na kufanyika kazi safi nchini. Hata kama chombo fulani cha utendaji kitakuwa na ufanisi kiasi gani, lakini kama sheria inayokabidhiwa chombo hicho kwa ajili ya utekelezaji haitokuwa sheria safi, sahihi na murua hatimaye hali ya upogo itashuhudiwa ndani ya chombo hicho. Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu utabaki kuwa safi na salama kutokana na kulinda muelekeo wake wa Kiislamu na kuheshimu katiba yake; na hili linathibiti kwa utendaji wa Baraza la Walinzi wa Katiba. Ikiwa kuwa safi kwa mfumo wa utawala kunapatikana kwa kuwepo sheria sahihi na kuzingatiwa Uislamu ndani yake; endapo –na Mungu aepushie mbali- itatokezea Bunge likashindwa kutunga sheria zitakazoafikiana na Uislamu, na uendeshaji wa Bunge ukawa si uendeshaji mzuri na sahihi, bila shaka hilo litaathiri hali ya serikali na uendeshaji wa kiutendaji wa nchi. Kwa hivyo usafi wa mfumo wa utawala una mfungamano na usafi wa bunge. Bunge safi, lenye nguvu, lenye ufanisi wa utendaji, lenye wabunge waumini na linalofanya kazi kulingana na sheria litaweza kutoa msukumo wa kisheria kwa utawala kwa njia sahihi. Baraza la Walinzi wa Katiba, ni chombo na taasisi ya uhakika zaidi na ya kuaminika zaidi ambayo Mapinduzi yameupatia mfumo wa utawala nchini. Ili sisi tuweze kiujumla kuwa na uhakika juu ya usafi wa mfumo wa utawala, Baraza hili la Walinzi wa Katiba, ndicho chombo cha mfumo wa utawala ambacho ni muhimu zaidi, amilifu zaidi, murua zaidi na chenye taathira zaidi. Baraza la Walinzi wa Katiba ni msimamizi mwaminifu wa uchaguzi.

Juu ya ukurasa

Usimamizi wa Umma

Kuamrisha mema na kukataza maovu, moja ya madhihirisho ya usimamizi wa umma

Sehemu ambayo inawahusu wananchi wote, kwanza kabisa ni kuamrisha mema na kukataza maovu katika masuala ya kijamii. Tab'an katika masuala ya mtu binafsi, taqwa na uchamungu ni jambo lililousiwa mno na Amirul Muuminin; lakini katika uwanja wa masuala ya kijamii, huenda kukawa hakuna jambo walilosemezwa watu kwa uzito zaidi, kwa mkazo zaidi na kwa msisimko mkubwa zaidi kama suala la kuamrisha mema na kukataza maovu. Kuamrisha mema na kukataza maovu ni jukumu la watu wote. Kuamrisha mema na kukataza maovu, maana yake ni kuwaamrisha watu wengine kufanya mambo mema. Kukataza maovu, maana yake ni kuwakataza watu wengine kufanya mambo mabaya. Kuamrisha na kukataza kunafanyika kwa maneno na ulimi tu. Bila shaka kuna awamu nyingine ya kabla ya kutumia ulimi, ambayo ni awamu ya moyo, ambapo kama itakuwepo awamu hiyo kuamrisha mema kwa ulimi kutakuwa kumekamilika. Wakati wewe unapousaidia mfumo wa utawala wa Kiislamu kwa kuwaamrisha watu kufanya mema- mathalan kuwakirimu masikini, kutoa sadaka, kusitiri aibu za watu, kuwa na upendo, kuwa na mashirikiano na watu, kufanya mema, kuwa na huruma, upole na subira- na ukawa unawaambia watu fanyeni mambo haya; wakati moyo wako pia unapokuwa na mfungamano na shauku ya kufanya mambo hayo, uamrishaji wako huo unakuwa ni uamrishaji wa dhati na wa kweli. Wakati unapomkataza mtu maovu - kwa mfano kudhulumu, kukanyaga na kupora haki za wengine, kuponda mali ya umma, kutaka kuvunjia heshima maharimu wa watu, kusengenya, kusema uwongo, kufitinisha, kuwafanyia njama watu, kuchukua hatua dhidi ya mfumo wa Kiislamu, kushirikiana na adui wa Uislamu - na ukawa unamwambia usifanye mambo haya; wakati ndani ya moyo wako kunapokuwa na chuki juu ya mambo haya, ukatazaji huo unakuwa ukatazaji wa dhati na wa kweli, na wewe mwenyewe pia utendaji wako unakuwa kulingana na uamrishaji huo na ukatazaji huo. Ikiwa – na Mungu aepushie mbali- moyo hautokuwa pamoja na ulimi, hapo mtu huingia katika wale walioambiwa "Mwenyezi Mungu amewalaani waamrishaji mema wanaoacha (wao wenyewe) kufanya mema hayo." Mtu ambaye huwaamrisha watu kufanya mema lakini yeye mwenyewe akawa hatekelezi mema hayo; akawa anawakataza watu maovu lakini yeye mwenyewe akawa anayafanya mabaya hayo; mtu kama huyo analaaniwa na Mwenyezi Mungu na atakuwa na mwisho mbaya sana.

Ikiwa maana ya kuamrisha mema na kukataza maovu pamoja na mipaka yake itafahamika wazi kwa watu, itabainika kuwa kuamrisha mema na kukataza maovu ni mojawapo ya njia mpya zaidi, nzuri zaidi, yenye ufanisi zaidi na yenye kufaa zaidi kwa ajili ya maelewano ya kijamii; hii ni hali ya mashirikiano, huu ni usimamizi wa wananchi; huku ni kusaidia katika uenezaji wa kheri; huku ni kusaidia katika kupunguza shari na mabaya; ni kusaidia katika kuhakikisha kwamba katika jamii ya Kiislamu, dhambi na maovu yanabaki siku zote kuonekana kuwa ni maovu katika jamii. Hatari mbaya zaidi ni kutokea siku, ikafikia hadi katika jamii, tendo la madhambi likatambulishwa kuwa ni la thawabu; jambo jema likatambulishwa kuwa kitu kibaya, na utamaduni wa mambo ukabadilishwa. Wakati kuamrisha mema na kukataza maovu kunapoenea katika jamii hupelekea ovu libaki siku zote kuonekana katika mtazamo wa watu kuwa ni ovu na wala lisibadilike kuwa jambo jema na la thawabu. Njama iliyo mbaya zaidi dhidi ya wananchi ni watu kufanya mambo na kusema maneno mpaka ikafika hadi mambo ya kheri- mambo ambayo dini imewaamrisha watu na ambayo ndiyo yenye kuiletea nchi kheri na saada- yakabadilika na kuonekana katika fikra za watu kuwa ni mambo mabaya; na mambo mabaya yakaonekana kuwa ni mambo mema. Hii ni hatari kubwa mno.

Kwa hivyo faida ya kwanza kabisa ya kuamrisha mema na kukataza maovu ndiyo hii ya kuyafanya mambo mema yakabaki kuwa mema, na mabaya yakabaki kuwa mabaya. Kwa upande mwingine wakati maovu yanapoenea katika jamii na watu wakayazoea maovu hayo, mtu aliyeshika hatamu za uongozi wa jamii hukabiliwa na kazi ngumu pale anapotaka kuwaelekeza watu kwenye mambo mema ya kheri na saada; yaani hatoweza kufanya hivyo kabisa au hatoweza kwa urahisi na atalazimika kutumia gharama kubwa kwa ajili kuifanya kazi hiyo. Tumeambiwa kuwa: "Mutaamrisha mema na kukataza maovu au Mwenyezi Mungu atakusalitishieni juu yenu walio waovu miongoni mwenu, kisha wataomba walio wema kati yenu na wala wasiitikiwe dua yao." Lazima muamrishane mema na kukatazana maovu baina yenu, mulifanye jambo hilo lienee na kuzoeleka na mshikamane nalo. Kama hamtofanya hivyo Mwenyezi Mungu atakusalitisheni juu yenu watu waovu, mafasiki na walio vibaraka; wakati usipofanyika uamrishaji mema na ukatazaji mabaya, na uhalifu, wizi, uhaini, usaliti na udanganyifu vikaenea katika jamii na kuanza taratibu kuwa sehemu ya utamaduni wa jamii, hapo ndipo yanapopatikana mazingira ya watu wasiofaa kushika hatamu za uongozi.

Juu ya ukurasa

Kuamrisha mema na kukataza maovu katika ngazi ya viongozi

Bila shaka kuamrisha mema na kukataza maovu kuko katika ngazi mbali mbali, muhimu zaidi kati ya hizo ni ngazi ya viongozi; yaani lazima wananchi wawaamrishe viongozi mema na kuwakataza mabaya. Inatakiwa wananchi wawatake viongozi wafanye kazi nzuri; tena basi si kwa njia ya ombi na kusihi; bali wawatake hasa wafanye hivyo. Hii ndiyo ngazi muhimu zaidi. Bila shaka si ngazi hiyo pekee; bali pia kuna ngazi nyingine mbali mbali.

Ukatazaji maovu uko katika nyanja zote muhimu; kwa mfano kuna mambo ambayo watu wenye madaraka huyafanya kutokana na mamlaka waliyonayo; kama huu utumiaji mbaya wa rasilimali za umma; kutumia urafiki na kujuana katika masuala ya nchi, katika masuala ya uingizaji bidhaa nchini, katika masuala ya mashirika na katika utumiaji wa rasilimali za uzalishaji n.k; ni hili suala la viongozi kutumia usuhuba na urafiki. Kuna wakati linakuwa ni suala la watu wawili wafanya biashara wanaoshirikiana na wenye urafiki; hilo lina hukumu yake; na kuna wakati mtu ambaye ni kiongozi wa serikali mwenye madaraka ya kutoa idhini na kusaini jambo, ambaye anaanzisha uhusiano maalumu na mtu fulani; kufanya hivyo ni marufuku, ni dhambi na ni haramu; na kulikataza ni wajibu kwa watu wote watakaoyafahamu mambo hayo- katika hiyo idara yenyewe, katika kitengo hicho, iwe ni kwa aliye juu yake au aliye chini yake mtu; ili usiwepo mwanya kwa mtu mwenye kutumia vibaya mamlaka yake.

Juu ya ukurasa

Matunda ya usimamizi wa magazeti

Mfumo wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ni mfumo unaotokana na wananchi. Mfumo unaotokana na wananchi- ambao wanahusika moja kwa moja katika muundo wake wa asili- hauwezi kujitosheleza bila wananchi wake kuwa na uelewa. Unapaswa kuwaelewesha wananchi wake; unapaswa kuwafanya wawe na uwezo wa kuchanganua mambo na kuwashibisha kwa taarifa na utambuzi wa mambo ya lazima na yenye faida. Uelewa kwa mfumo kama huu ni kitu cha lazima na cha wajibu kama ilivyo hewa. Mfumo wetu uko namna hiyo. Kadiri wananchi watakavyokuwa na uelewa zaidi ndivyo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unavyofaidika zaidi. Kwa hivyo mfumo huu unahitajia utaratibu wa ueleweshaji watu.

Kwa kushiriki katika nyanja mbali mbali za kisiasa na kijamii, kwa kutumia utaratibu makini wa usimamizi, na kwa kujihusisha na kuonyesha muongozo kwa wakati unaofaa, watu wa jamii yetu wanapaswa kumfanya kila mtu aelewe majukumu aliyonayo. Hakuna shaka yoyote kuwa baina ya viongozi na wananchi kuna daraja kubwa la kuwaunganisha liitwalo kiujumla kama vyombo vya habari na hasa magazeti na machapisho. Bila shaka magazeti yetu ya ndani yanapaswa kufanya jitihada katika kuhakikisha yanawapatia wananchi taarifa sahihi na kwa wakati. Magazeti yetu yanapaswa kufanya juhudi kuhakikisha yanawapatia wananchi mambo yanayodhamini thamani zao, misingi yao ya asili na malengo yao matukufu. Kwa kuchukua hatua za uelimishaji ulio sahihi, magazeti yanaweza kuwafanya wananchi waelewe majukumu yao, na vile vile kuwafanya viongozi watambue majukumu mazito waliyonayo; kama ambavyo endapo itatokea kinyume chake, kwa magazeti kuchukua hatua za kichochezi, kwa kuzusha hali ya utatanishi na dhoruba ya kuchonganisha na kuleta mifarakano, yatayapotosha makundi yote mawili- yaani wananchi na viongozi pia- katika kuelewa majukumu yao makuu.

Mimi ninaitakidi kuwa magazeti ni kitu muhimu, cha lazima na kisichoweza kuepukika kwa jamii ya Iran na jamii yoyote ile inayotaka kuishi vizuri. Na kwa mtazamo wangu magazeti yana majukumu matatu makuu: jukumu la kukosoa na kusimamia, jukumu la kupasha habari za kweli na kwa uwazi kabisa, na jukumu la kuratibu ubadilishanaji wa fikra na mawazo katika jamii. Ninaamini kuwa uhuru wa uandishi na utoaji maoni ni haki ya wazi kabisa ya wananchi na magazeti. Sina shaka yoyote ile juu ya hili, na hii ni mojawapo ya misingi ya katiba iliyobainishwa wazi. Ninaamini kuwa ikiwa jamii itapoteza magazeti huru na yenye ustawi pamoja na uandishi huru na wenye ufahamu, itapoteza pia vitu vingine vingi. Kuwepo magazeti huru ni mojawapo ya alama za kupevuka kwa taifa, na kwa hakika magazeti yenyewe ni chachu ya ukuaji na upevukaji wa taifa; yaani kwa upande mmoja upevukaji na hali huru liliyonayo taifa hupelekea kupatikana magazeti huru; na kwa upande mwingine, yenyewe nayo, magazeti hayo huweza kuinua kiwango cha ukuaji na upevukaji wa taifa. Tab'an ninaitakidi pia kwamba sambamba na kuwepo thamani hii, kuna thamani nyinginezo pia ambazo hazipasi kupuuzwa na kukanyagwa kwa kuwepo uhuru wa magazeti na uhuru wa uandishi. Uhodari mkubwa ni mtu kuweza kudumisha kuwepo kwa uhuru, akaweza kuelewa ukweli halisi, akaweza pia kuwa na magazeti huru, na vile vile asitingwe na taathira zake mbaya. Inapasa tufuate mwendo wa aina hii.

Juu ya ukurasa

Usimamizi juu ya magazeti

Usimamizi wa magazeti ni jukumu na jambo la lazima. Huu ni msingi wa sheria mama ya katiba, sheria ya magazeti na sheria za kawaida pia. Bila usimamizi, bila shaka yoyote magazeti hayatoweza kukidhi matakwa na kuzingatia maslahi ya taifa. Baadhi ya watu wanadhani kwamba fikra za watu katika jamii ni eneo huru lisilo na mipaka wala kizuizi chochote na hivyo wanaweza kufanya humo chochote wanachotaka! Fikra za watu si panya wa maabara, wa kwamba kila mtu anaweza kumfanyia lolote analotaka. Kwa kutumia uchanganuzi usio sahihi, kueneza uvumi, tuhuma na uwongo, wanaziharibu imani, hisia, itikadi na matukufu ya watu. Hiyo si sawa. Kwa hivyo kuna ulazima wa kuwepo usimamizi huu ili yasije yakatokea mambo hayo. Hili ni jambo la wajibu.

Juu ya ukurasa

Usimamizi wa Mwenyezi Mungu

Akhera lazima iwe na taathira na nafasi maalumu kwetu katika uchukuaji hatua na upitishaji maamuzi yetu yote. Baadhi ya watu wanayapa uzito yale yanayosemwa na wananchi na usimamizi unaofanywa na wananchi; lakini hawaupi uzito usimamizi wa Mwenyezi Mungu na mambo yanayofungamana na hatima yetu ya hapo kesho. Katika umri wowote ule tulioko, sisi tuko kwenye ukingo wa mpaka wa uhai na mauti. Upande ule wa mpaka wa mauti kuna hesabu ya Mwenyezi Mungu na kusailiwa na kuhesabiwa katika mizani ya amali yenye umakini mutlaki. Inatupasa kuyafikiria hayo; uhai, maisha ya milele na hatima ya kweli iko huko; lazma tulipe uzito jambo hilo. Tumekuja hapa kwa siku chache kwa ajili ya kukustawisha huko twendako. Katika maneno tunayotamka, katika saini tunayotia, katika ushauri tunaotoa, katika maamuzi tunayopitisha na katika kuuzulu na kuteua tunakofanya, tuzingatie na kuipa uzito akhera, radhi za Mwenyezi Mungu na hesabu ya huko.

Baadhi ya watu wanadhani kuwa kwa dhati yake, madaraka au mali ni kitu kibaya; hali ya kuwa sio hivyo; madaraka na mali ni kama zilivyo hiba nyinginezo za Mwenyezi Mungu, ni mapambo ya maisha. Ni vipi tunayatumia madaraka haya? Kama tutayatumia vizuri, itakuwa ni kheri; kama tutayatumia kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, ni kheri; kama tutayatumia kwa ajili ya kueneza maadili mema, umaanawi, na yale yenye maslahi kwa ajili ya uokovu wa wanadamu, ni kheri; lakini kama tutayatumia kwa ajili ya kukidhi tamaa za binafsi na matamanio ya nafsi, na tukawa mithili ya wanyama wakali kwa kuyatumia dhidi ya huyu na yule, hapo yatakuwa ni shari; na kila madaraka yanapokuwa mengi zaidi, shari yake inakuwa nyingi zaidi; na kila yanapokuwa makubwa na ya juu zaidi, shari yake pia inakuwa kubwa zaidi.

Viongozi wa utawala wajue kwamba Mwenyezi Mungu yuko mbele ya macho yao anawaangalia katika kila hali. Waichukulie hesabu ya Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama kwa uzito mkubwa. Hesabu ya Mwenyezi Mungu ni hesabu ya haki. Mungu aepushie mbali, jambo dogo kabisa, kughafilika kidogo tu na uzembeaji mdogo tu, yote hayo yananakiliwa, yanahifadhiwa na kubakia kwenye faili na daftari la amali. Tendo moja moja kati ya hayo litapimwa na kuhesabiwa; kama ambavyo kila lahadha ya kipindi kigumu mnachopitisha katika utekelezaji wa majukumu yenu, kinanakiliwa na kuhifadhiwa kwenye daftari la amali zenu. Ule wasiwasi mnaokuwa nao kwa ajili ya kazi, zile juhudi na jitihada mnazofanya, yale mashinikizo mnayozibebesha fikra zenu, viwiliwili vyenu na familia zenu kwa sababu ya kuhakikisha mnafanya kazi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na katika njia yake yeye, hayo pia yamehifadhiwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu aepushie mbali, ikiwa mtapatwa na mghafala mdogo, uzembeaji au upuuzaji katika kazi yoyote ile miongoni mwa kazi zenu, au mkaacha kuzingatia maslahi ya juu ya wananchi na mfumo kwa sababu ya baadhi ya maslahi ya binafsi na ya kimakundi, yote hayo yanahifadhiwa mbele ya Mwenyezi Mungu mtukufu, na Mwenyezi Mungu mtukufu atakuja kutuuliza kuhusiana na mambo hayo.

Juu ya ukurasa

 
Mbele >

^