Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
PALESTINA Chapa
22/10/2009

Sura ya kwanza: Historia ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu Palestina

Jinsi Palestina ilivyoghusubiwa
Ukweli uliopinduliwa
Njia kuu zilizotumika kuivamia na kuikalia kwa mabavu Palestina

Sura ya Pili: Umuhimu wa Palestina

Umuhimu wa suala la Palestina
Umuhimu wa Baitul Muqaddas
Mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusu Palestina
Imam Khomeini na suala la Palestina

Sura ya Tatu: Kuiunga mkono Palestina

Matokeo ya mfarakano ndani ya umma wa Kiislamu
Jukumu la kuwatetea wananchi wa Palestina

Ulimwengu wa Kiislamu na suala la Palestina

   Uungaji mkono wa ulimwengu wa Kiislamu kwa Palestina
   Uungaji mkono wa serikali za nchi za Kiislamu kwa Palestina
   Uungaji mkono wa taifa la Iran kwa wananchi wa Palestina
   Utumiaji wa vyombo vya uenezi katika kuiunga mkono Palestina

Sura ya Nne: Utatuzi wa suala la Palestina

Utatuzi wa kidiplomasia wa suala la Palestina
Mashinikizo kwa utawala wa kizayuni
Utumiaji wa silaha ya mafuta
Misaada ya kifedha kwa wananchi wa Palestina

Njia ya kuiokoa Palestina

Njia ya kuiokoa Palestina
   Mapambano, njia ya kuliokoa taifa la Palestina
   Mwamko wa wananchi wa Palestina
Utaifa wa Kiarabu na suala la Palestina

Sura ya Tano: Amani na mapatano

Mbinu ya amani
Mpango wa mapatano baina ya Palestina na Israel
Mantiki ya mapatano baina ya Waarabu na Israel
Sababu ya kutofanikiwa Intifadha ya Kwanza
Matokeo ya mpango wa mapatano wa Oslo
Usaliti kwa malengo matukufu ya Palestina
Usaliti wa watawala wa Kiarabu kwa Palestina

Sura ya Sita: Mapambano na Istiqama

Nguvu ya wananchi wa mataifa
Mapambano ya wananchi mashujaa wa Palestina
Mhimili mkuu wa mapambano na utawala wa kizayuni
Kigezo cha wanamapambano wa Kipalestina
Jihadi, wajibu wa umma wa Kiislamu
Intifadha ya Msikiti wa al-Aqsa
Sababu ya mapambano ya Palestina (Intifadha ya Msikiti wa al-Aqsa)
Palestina, mhimili mkuu wa harakati ya mwamko wa Kiislamu
Mapambano, sharti la ukombozi

Sura ya Saba: Hatima ya Palestina

Kubakia Palestina na kutoweka Israil
Mustakbali wa yakini
Ushindi wa damu dhidi ya upanga

PALESTINA


Sura ya kwanza: Historia ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu Palestina

Jinsi Palestina ilivyoghusubiwa

Palestina iligeuzwa kuwa milki mutlaki ya Wazayuni kupitia mchakato wa kihistoria uliojumuisha makumi ya mikakati iliyobuniwa na maadui. Kikundi kimoja cha Mayahudi wenye satwa na ushawishi duniani kilijiwa na fikra ya kuasisi nchi huru kwa ajili ya Mayahudi. Tab'an kabla ya Palestina walifikiria kwenda Uganda na kuanzisha nchi yao huko. Baada ya muda wakajiwa na wazo la kuelekea Tripoli mji mkuu wa Libya; kwa hivyo wakaenda kuzungumza na Wataliano ambapo wakati huo Tripoli ilikuwa mikononi mwao; lakini Wataliano waliwakatalia; hivyo hatimaye wakakubaliana na Waingereza. Wakati ule Waingereza walikuwa na malengo muhimu ya kikoloni katika Mashariki ya Kati; hivyo wakahisi litakuwa jambo zuri kama watu hao watakuja katika eneo hili, huku nao wakitaka kutatua tatizo walilokuwa nalo. Kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi hii kumetokana na mpango mmoja kabmabe, wa pande kadhaa na wenye lengo la kuzuia usipatikane umoja na mshikamano kati ya Waislamu, na kuepusha zisije zikaundwa tena nchi za Kiislamu zenye nguvu. Kuna ushahidi pia unaoonyesha kuwa Wazayuni walikuwa na uhusiano wa karibu na Manazi wa Ujerumani; na huu utoaji wa takwimu za utiaji chumvi kuhusu mauaji ya Mayahudi, yenyewe ilikuwa mbinu ya kutaka kupata huruma za fikra za walio wengi na kuandaa mazingira ya kuivamia Palestina na kuhalalisha jinai za Wazayuni. Hata kuna ushahidi unaoonyesha kuwa kundi la wahuni wasio Mayahudi kutoka Ulaya ya Mashariki, walitumia jina la Uyahudi na kuhamia Palestina, ili kwa kutumia kisingizio za kuwaunga mkono manusura wa waathirika wa ubaguzi wa rangi, kuanzisha utawala wenye uadui na Uislamu kwenye kitovu cha ulimwengu wa Kiislamu; na baada ya karne kumi na tatu kuweza kuanzisha ufa baina ya mashariki na magharibi ya ulimwengu wa Kiislamu. Hapo awali Waislamu walighafilika na jambo hilo; kwa sababu hawakuwa na habari juu ya kiini cha mpango wa Wazayuni na waungaji mkono wao wa Magharibi. Utawala wa Othmaniyya ulishindwa; mkataba wa "Sykes-Picot" ukasainiwa kwa siri ili kuzigawanya nchi za Kiislamu za Mashariki ya Kati kati ya washindi wa vita; Shirikisho la Mataifa (The League of Nations) likaiweka Palestina chini ya himaya ya Waingereza; na wao pia wakawapa Wazayuni ahadi ya kuwasaidia; na kwa kutekeleza mipango iliyokwisharatibiwa vyema wakawachukua Mayahudi na kuwapeleka Palestina kisha wakawahamisha Wapalestina kwenye nyumba na makaazi yao.

Ilivyokuwa imepangwa ni kwamba awali Mayahudi waingie Palestina na kuishi kama tabaka la wachache, kisha waanze kujipanua taratibu na hatimaye kutwaa sehemu moja ya ardhi hiyo, na ardhi yenyewe basi ni ile nyeti kabisa- kwa sababu nchi ya Palestina iko katika sehemu nyeti- na kuunda utawala, na kisha kuwa mmoja wa waitifaki wa Uingereza na kuzuia ulimwengu wa Kiislamu na hasa ulimwengu wa Waarabu usiweze kuungana na kuwa na umoja katika eneo hilo. Adui anayepata himaya na uungaji mkono wa aina hiyo kutoka nje, huweza kuzusha hitilafu kwa kutumia mbinu za kijasusi na njia mbali mbali, na kwa kweli aliweza kuifanya kazi hiyo kwa kukurubiana na huyu ili kumpiga yule, kumbana huyu na kumkandamiza mwingine. Kwa hivyo katika hatua ya kwanza hayo yalifanyika kwa msaada wa nchi ya Uingereza na baadhi ya nchi nyingine za Magharibi. Kisha baadaye walijtenga taratibu na Uingereza na kuungana na Marekani, na hadi leo hii Marekani imewachukua na kuwaweka Wazayuni chini ya ubawa wake. Hivyo ndivyo walivyoweza kuunda nchi na kuja kuivamia na kuifanya milki yao nchi ya Palestina. Utwaaji wao waliufanya kwa namna ifuatayo: kwanza hawakuja kwa kutumia vita; kwanza walikuja kwa kutumia hila; walikwenda kuzinunua ardhi kubwa za Palestina na ambazo zilikuwa ni ardhi zilizostawi na zenye rutuba ambapo wakulima wa Kiarabu ndio waliokuwa wakilima katika mashamba hayo. Wakazinunua ardhi hizo kwa bei kubwa zaidi kulinganisha na bei yake ya asili kutoka kwa wamiliki wenyewe wa maeneo hayo makubwa ya ardhi ambao walikuwa huko Ulaya na Marekani; wao pia walikuwa wakiisubiri kwa hamu kubwa fursa hiyo, hivyo wakaamua kuwauzia Mayahudi. Tab'an walikuwa na madalali pia ambao imeelezwa kuwa mmoja wa madalali hao ni huyu "Sayyid Dhiyaa" (Sayyid Dhiyaauddin Tabatabai) maarufu, aliyekuwa mshirika wa Reza Khan katika mapinduzi ya kijeshi ya 1921 ambapo baada ya kuondoka hapa alielekea Palestina akawa dalali wa kununua ardhi za Waislamu kwa ajili ya Mayahudi na Waisrael! Kwa hivyo walizinunua ardhi, na baada ya ardhi hizo kuwa milki zao, wakatumia njia ambazo kwa kweli ni za kinduli zilizotokana na nyoyo zao za kihabithi na kikatili, na taratibu wakaanza kuwafukuza wakulima katika mashamba hayo. Walikuwa wakienda maeneo mbali mbali ambako waliwapiga na kuwaua watu, na ni wakati huo ndipo walipoziteka kwa kutumia uwongo na udanganyifu na kuzivutia upande wao fikra za walio wengi duniani.

Juu ya ukurasa

Ukweli uliopinduliwa

Katika propaganda zinazofanywa duniani wamejaribu kuonyesha kuwa Mayahudi waliokwenda Palestina na kuitwaa ardhi ya nchi hiyo, ni watu waliodhulumiwa, wenye haki, walioonewa na kukabiliwa na mbinyo; lakini Waarabu wanaojaribu kuzitwaa tena nyumba zao, ni watu makatili na watumiaji mabavu ambao hawaheshimu sheria.

Wakati Wazayuni na Mayahudi wa Urusi walipokuwa wanataka kuhamia Palestina, hawakuwa wakisema kuwa watu hao ni magahasibu; hao wanaokwenda huko si wazaliwa wa Wapalestina, na kwamba hao ni raia wa Urusi, ni raia wa Ukraine, ni raia wa nchi za Ulaya na Marekani, ambao kila mmoja ana mahali pake, nyumba yake, mali zake, pesa zake na maisha yake katika nchi yake. Pamoja na hayo wanakwenda Palestina ili kunyakua haki ya Mpalestina fulani, wanaitwaa nyumba yake na kuifanya mali yao, wanapora na kughusubu mali zake na ardhi yake na kumkosesha fursa ya kuanzisha familia yake; hilo hawakuwa wakilisema! Zaidi ya hayo, katika vyombo vyao vya habari, vibaraka wa Wazayuni na Marekani wanaonyesha picha za baadhi ya wanawake na watoto wa Kiyahudi wakiwa katika hali ya uchovu ili walimwengu waseme: "Ajabu! Hawa Waarabu wanaamiliana namna hivi na watu hawa masikini waliodhulumiwa?!

Juu ya ukurasa

Njia kuu zilizotumika kuivamia na kuikalia kwa mabavu Palestina

Utwaaji wa kuighusubu Palestina uliofanywa na Wazayuni umefanyika kwa kutumia njia kuu tatu: moja kati ya njia hizo ilikuwa ni kuwafanyia ukatili Waarabu. Mlahaka wao na wamiliki halisi wa ardhi hiyo ulikuwa ni wa kikatili na utumiaji nguvu. Hawakuwa wakiamiliana nao kwa murua hata chembe.

Njia ya pili ilikuwa ni kusema uwongo kwa fikra za walio wengi duniani. Uwongo huu kwa fikra za waliowengi duniani ni mojawapo ya mambo ya kushangaza. Watu hao wamesema uwongo kupitia vyombo vya habari vya kizayuni vilivyokuwa mikononi mwa Mayahudi- ambapo uwongo huo waliousema kabla na baada ya ya kuivamia Palestina – kiasi kwamba ni kutokana na uwongo huo waliweza kuwateka baadhi ya mabepari wa Kiyahudi! Kuna watu wengi mno ambao waliuamini uwongo wao huo. Walimdanganya hata huyu mwandishi wa kijamii wa Kifaransa Jean-Paul Sartre. Huyu Jean-Paul Sartre aliandika kitabu ambacho niliwahi kukisoma miaka thelathini iliyopita. Aliandika kuwa: "Watu wasio na ardhi, ardhi isiyo na watu"! Yaani Mayahudi walikuwa watu wasio na ardhi; wakaenda Palestina ambayo ilikuwa ardhi isiyo na watu! Maana yake ni nini kwamba haikuwa na watu? Ardhi hiyo ilikuwa na watu na wakifanya kazi. Kuna ushahidi mwingi pia juu ya suala hilo. Mwandishi mmoja wa kigeni anaeleza kuwa katika ardhi yote ya Palestina kulikuwa na mashamba ya ngano ambayo yalikuwa mithili ya bahari ya kijani, na yalionekana kadiri ya upeo wa macho ulivyoweza kuona. Wametaka kuonyesha ulimwenguni kuwa Palestina ilikuwa ni mahali mithili ya kihame, gofu na sehemu yenye hali mbaya; na kwamba wao ndio waliokwenda kupastawisha! Ni uwongo waliuotoa kwa fikra za walio wengi! Kila mara walikuwa wakijaribu kujionyesha kuwa ni watu waliodhulumiwa; katika majarida ya Marekani kama vile 'Time' na 'Newsweek', kama litatokea tukio dogo kabisa kuhusiana na familia ya Kiyahudi; huchapishwa picha kubwa na maelezo marefu na kutolewa taarifa za kina mpaka za umri, kama ni wa mtu aliyekufa, pamoja na kukuza hali ya unyonge ya watoto wake; lakini huwa hawaashirii chochote kuhusiana na mamia na mamia ya kesi za ukatili wanaofanyiwa vijana wa Kipalestina, familia za Kipalestina, watoto wa Kipalestina na wanawake wa Kipalestina ndani ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na huko ndani ya Lebanon!

Njia ya tatu ni kutumia mbinu na hila ya mazungumzo, chambilecho wao wenyewe kutumia "lobi." Nayo ni kukaa na kuzungumza na serikali hii, shakhsiya yule, mwanasiasa huyu, mwanafikra yule, mwandishi huyu na mshairi yule! Kazi yao hadi sasa imekuwa ikifanyika kwa kutumia mihimili hiyo mitatu na kuweza kuinyakua nchi hii kwa kutumia hila na hadaa hizi na zile ambapo madola ya kigeni nayo, na kwa sehemu kubwa Uingereza, yamekuwa pamoja nao. Umoja wa Mataifa, na kabla yake Shirikisho la Mataifa- ambapo Umoja wa Mataifa uliundwa baada ya vita kwa ajili ya masuala eti ya amani- ukiachilia mbali kesi chache tu, umekuwa muda wote ukiwaunga mkono watu hao. Katika mwaka huo huo wa 1948, Shirikisho la Mataifa lilipasisha azimio la kuigawa Palestina bila ya sababu yoyote. Likaamua asilimia hamsini na saba ya ardhi ya Palestina iwe mali ya Mayahudi; hali ya kuwa kabla ya hapo walikuwa wakimiliki kama asilimia tano tu ya ardhi ya Palestina! Nao wakaunda dola, na baada ya hapo yakajiri matukio mbali mbali ya kushambulia vijiji, miji, nyumba pamoja na kuwashambulia watu wasio na kosa lolote. Tab'an serikali za Kiarabu zilikuwa na taksiri pia. Vilitokea vita kadhaa. Katika vita vya mwaka 1967, kwa msaada wa Marekani na madola mengine, Waisrael waliweza kutwaa sehemu kubwa ya ardhi za Misri, Syria na Jordan. Baadaye katika vita vya mwaka 1973 ambavyo walivianzisha wao, kwa msaada tena waliopata kutoka kwa madola hayo, wakashinda vita hivyo na kuzitwaa ardhi nyingine.

Juu ya ukurasa

Sura ya Pili: Umuhimu wa Palestina

Umuhimu wa suala la Palestina

Kusema kweli leo katika maisha ya Waislamu, na katika upeo wa Kiislamu, hakuna suala lolote lenye umuhimu na lenye kuishughulisha akili zaidi kama suala la Palestina. Kwa miaka kadhaa wameweza hatua kwa hatua kuwafanya Waislamu waizoee hali ya kuporwa na kughusubiwa sehemu ya nyumba yao. Na suala si kughusubiwa nyumba tu ya Waislamu; bali kadhia ni kubwa zaidi ya hivyo. Suala ni kwamba maadui wa ulimwengu wa Kiislamu wameifanya sehemu ya nyumba ya Waislamu kama ngome kwa ajili ya kushambulia safu za Waislamu, na kwa ajili ya kukabiliana na malengo yao na kupambana na harakati zao. Katika kadhia ya Palestina lengo hasa ni kuiokoa Palestina; yaani kuifuta serikali ya Israel. Hakuna tofauti yoyote kati ya ardhi za kabla ya mwaka 1967 na baada yake. Kila shubiri ya ardhi ya Palestina ni shubiri moja ya nyumba ya Waislamu. Utawala wowote usiokuwa utawala wa wananchi wa Palestina na utawala wa Waislamu katika ardhi ya Palestina, ni utawala ghasibu. Maneno ni yale yale aliyoyasema Imam Khomeini: "Israel inapasa ifutwe". Ikiwa Mayahudi wa Palestina wataukubali utawala wa Kiislamu, na waishi huko. Suala si chuki dhidi ya Mayahudi. Suala ni juu ya kughusubiwa nyumba ya Waislamu. Laiti marais na viongozi wa Waislamu wasingeathiriwa na madola ya ulimwengu, wangeliweza kulitekeleza suala hili muhimu; lakini bahati mbaya hawakufanya.

Juu ya ukurasa

Umuhimu wa Baitul Muqaddas

Mbali ya suala la Palestina, Baitul Muqaddas, nayo pia ina umuhimu mkubwa. Leo hii zinatekelezwa njama za kila aina na Wazayuni kwa lengo la kuughusubu na kuumeza mji huu mtakatifu na kufuta athari zake za Kiislamu, lakini mji huu ni miliki ya Waislamu wote, na Quds yote ni mji mkuu wa Palestina nzima; na Waislamu hawatoruhusu njama chafu za maadui zifanikiwe, bali watakabiliana nazo.

Juu ya ukurasa

Mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusu Palestina

Kwa mtazamo wa Kiislamu: Kwa mtazamo wa Kiislamu, suala la Palestina ni suala la msingi na ni faradhi ya kidini kwa Waislamu wote. Maulamaa wote wa Kishia na Kisuni, waliotangulia na wa sasa wanaeleza bayana kuwa ikiwa sehemu fulani ya ardhi ya Waislamu itachukuliwa na maadui wa Uislamu, hapo huwa ni wajibu kwa Waislamu wote kuipigania mpaka wahakikishe wanairejesha ardhi hiyo iliyoghusubiwa. Kila mtu, vyovyote anavyoweza, na kwa kadiri ya uwezo wake, ana wajibu kuhusiana na suala la Palestina. Kwanza kabisa ana wajibu kwa mtazamo wa Kiislamu. Ardhi, ni ardhi ya Kiislamu; imeporwa na maadui wa Uislamu na ni lazima irejeshwe. Pili kuna Waislamu milioni nane, baadhi yao ni wakimbizi na baadhi yao wako ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, na hali yao ni mbaya zaidi kuliko ya wale walio wakimbizi. Hawathubutu kutembea kikawaida huku na huko; hawana ruhusa ya kutoa maoni yao; wala hawaruhusiwi kuwa na mwakilishi na kiongozi wa kuendesha masuala yao ya nchi; mara nyingi wanazuiliwa hata kutekeleza Sala zao. Msikiti wa al-Aqswa ambao ni kibla cha Waislamu unakabiliwa na hatari; kuna wakati miaka kadhaa nyuma waliuchoma moto; baadaye wameanza kutekeleza kile walichokiita mashimo ya njia za chini kwa chini na kufanya mambo mbali mbali yaliyo kinyume cha sheria; na kimsingi hasa wanataka kuibadilisha kabisa sura ya Kiislamu ya msikiti wa al-Aqswa ambao ni kibla cha Waislamu.

Kwa mtazamo wa kiutu: Hali ya dhulma inayozikabili familia za Wapalestina zinamfanya kila mtu awe na jukumu juu ya suala hilo; ni hali ya dhulma waliyonayo watu walioko ndani ya Palestina; kwa sababu dhulma ambazo Wazayuni wanawafanyia wananchi wa Palestina hazina kiasi, na ajabu ni kwamba haya mashirika ya kutetea haki za binaadamu, nayo yamekufa! Hawa Wamarekani, baadhi ya hawa Wamagharibi na wale wengine wanaodai kuwa wana kazi ya kueneza ujumbe wa demokrasia duniani, wamepoteza heshima zao katika kadhia hii; kwa sababu hivi sasa kuna taifa la watu ambao hawana uwezo wa kuchangia chochote katika masuala yanayohusu nchi yao na ardhi yao, na matakwa yao hayasikiki popote; taifa hilo ni taifa la Palestina. Kwa mtazamo wa kiutu, ni watu wanaodhulumiwa; upande mmoja wanakabiliwa na utawala wa kibaguzi unaowafanyia kila aina ya dhulma; na upande wa pili kuna huu uzushi na uwongo mkubwa wa Marekani, mashirika ya ulimwengu na wale wanaoitwa eti wanafikra wa Kimagharibi wanaotoa madai ya kuzungumzia demokrasia!

Kwa mtazamo wa kiusalama: Suala la Israel ni la hatari ya kiusalama, na si hatari kwa watu wake yenyewe tu bali kwa eneo zima; kwa sababu wazayuni wana maghala ya silaha za atomiki na wangali wanaendelea kuunda silaha hizo! Umoja wa Mataifa nao umetahadharisha mara kadhaa lakini hawajajali; tab'an kwa sehemu kubwa, hiyo imetokana na msukumo na uungaji mkono wa Marekani; yaani sehemu kubwa ya dhima ya madhambi yanayofanywa na Wazayuni na serikali yao ghasibu inabebwa na utawala wa Marekani. Katika kipindi chote hiki cha miongo kadhaa ya kuweko Wazayuni madarakani, katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yamepasishwa maazimio zaidi ya thelathini dhidi ya Israel, ambayo yote Marekani imeyapigia kura ya "veto".

Kwa mtazamo wa kiuchumi: Israel ni hatari kwa eneo. Wazayuni wanaoitawala Palestina wana nadharia waliyoipa jina la "Nadharia ya Mashariki ya Kati Mpya". Nini maana ya Mashariki ya Kati mpya? Maana yake ni Mashariki ya Kati itakayojengwa huku mhimili wake mkuu ukiwa nchi ya Israel, ambapo Israel itaweza hatua kwa hatua kuziweka chini ya udhibiti wake wa kiuchumi nchi za Kiarabu, nchi za eneo na maeneo ya mafuta ya Ghuba ya Uajemi! Hilo ndilo lengo la Waisrael. Baadhi ya nchi zimeghafilika. Wakati yanapotolewa malalamiko dhidi yao husema, kwani sisi tumeanzisha uhusiano na wao! Sisi tumetoa ruhusa ya kuja wafanyabiashara wao tu! Kimsingi hilo hasa ndilo wanalotaka. Wao wanataka Israel, kwa uungaji mkono wa Marekani na kwa msukumo wa maghala yake hatari, iutumie mghafala na udhaifu wa baadhi ya nchi ili iweze kuingia katika nchi hizo na kuvitia mkononi vituo vya kiuchumi na rasilimali zao za fedha. Hii ni hatari kubwa kwa eneo. Ni hatari kubwa zaidi kuliko hatari nyingine zote. Mwenyezi Mungu asijaalie kufika siku hiyo na inshallah hatojaalia ifike, na mataifa ya Kiislamu pia hayatoruhusu kitu kama hicho kitokee; lakini mpango wao ni kutumia uchumi ili waweze kuzitia mkononi taasisi zote za utawala katika nchi hizo.

Kwa hivyo kwa mtazamo wa Kiislamu, kwa mtazamo wa kiutu, kwa mtazamo wa kiuchumi, kwa mtazamo wa kiusalama na kwa mtazamo wa kisiasa, leo hii kuwepo kwa Israel ni hatari kubwa kwa mataifa na nchi za eneo.

Juu ya ukurasa

Imam Khomeini na suala la Palestina

Tokea wakati ilipoanza harakati ya Kiislamu katika mwaka 1962 wakati ule ambapo suala la Palestina lilikuwa halijaanza kuzungumziwa hata na tabaka la weledi na wasomi, Imam Khomeini alikuwa akisema kuwa lazima watu wote wahisi kuwa kuna ulazima wa kukabiliana na hatari ya ubeberu wa Israel; lazima watu wote wasimame kidete na kukabiliana nao. Baada ya hapo pia aliendeleza njia hiyo hiyo, na hii ilikuwa mojawapo ya nara na kauli mbiu ya shakhsiya yule mkubwa wa Kiislamu. Harakati ya Imam Khomeini (Quddisa sirruh) iliupa uhai mpya kadhia ya Palestina, na kwa mara nyingine msukumo wa imani ya Kiislamu ambayo daima huambatana na Jihadi ya kujitolea muhanga ukadhihiri katika kadhia hiyo. Imam Khomeini hakuwahi hata mara moja kuyachelea madola ya watumiaji mabavu duniani katika suala la kuwatetea wanyonge wa dunia. Katika kipindi chote alikuwa akilitaja suala la Palestina kuwa ni suala kuu. Katika wasia wake na hotuba yake, Imam (Khomeini) ameonyesha waziwazi jinsi anavyokipa umuhimu kilio cha kuomba msaada kwa Waislamu cha mataifa yanayodhulumiwa; akitetea waziwazi haki za wanaodhulumiwa, haki za wananchi wa Palestina na kila taifa jengine linalodhulumiwa. Hii ndio njia na mwenendo wa Imam; huu ndio mwenendo wa Imam, na hizi ndizo nasaha na wasia wa Imam. Kijana mmoja wa Kipalestina alikuwa anaeleza kuwa: leo ndani ya jela za ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, wafungwa wanasoma mashairi ya kuonyesha mapenzi kwa Imam na ya kumkumbuka kiongozi mwenye heshima kubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kumbukumbu ya Mapinduzi na Imam, na kumbukumbu ya mapambano ya Jihadi ya taifa la Iran ziko pia ndani kabisa ya seli hizo.

Juu ya ukurasa

Sura ya Tatu: Kuiunga mkono Palestina

Matokeo ya mfarakano ndani ya umma wa Kiislamu

Laiti leo Waislamu wangekuwa na umoja, na lau kama wangeshikamana na umaanawi wa Uislamu, adui asingeweza kuwatesa wananchi wa Palestina ndani ya ardhi yao, na kuwanyanyasa, kuwaudhi na kuwakandamiza waziwazi kama hivi. Masuala ya Palestina yanaungulisha moyo wa kila mtu mwenye ghera na kumkosesha raha na utulivu, hata kama hatokuwa mtu wa kushikamana sana na dini.

Juu ya ukurasa

Jukumu la kuwatetea wananchi wa Palestina

Kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina na mapambano yao ya kishujaa katika hali ya kudhulumiwa, ni wajibu wa Kiislamu kwetu sote. Leo wananchi wa taifa moja la Kiislamu, wanaomba msaada kwa umma wa Kiislamu huku wakiwa katikati ya uwanja wa mapambano na nyuso zao zikiwa zimeroa damu. Sitokisahau kilio cha yule mama wa Kipalestina aliyekuwa mbele ya kamera ya mwandishi wa habari akipiga mayowe kwa sauti iliyomkauka na kusema: «يا للمسلمين ...»yaani "Enyi Waislamu nipateni!"

Waislamu wote na Waarabu wanapaswa kuunga mkono haki ya kisheria ya mapambano ya wananchi wa Palestina. Hii ni nukta inayopasa kutiliwa mkazo katika jumuiya za kimataifa ya kwamba watu wasio na ulinzi ambao wamevamiwa na kuporwa haki zao wana haki ya kupambana ili kurejesha haki zao. Kwa hivyo kuendeleza wananchi wa Palestina Intifadha na mapambano ni haki yao ya kisheria ambayo inaheshimiwa na kukubaliwa na sheria za kimataifa pia, pamoja na kwamba bahati mbaya, kwa kawaida sheria hizo hutafsiriwa kwa muelekeo wa kukidhi matakwa ya Uistikbari na madola yenye nguvu duniani.

Waislamu hawawezi tena kuendelea kukaa kimya na kuangalia tu ukandamizwaji wa kila siku wa wananchi wa Palestina. Lazima Israel ieleweshwe kwamba kuendeleza ukandamizaji dhidi ya wananchi wa Palestina na katika maeneo wanayoishi Wapalestina, kutakabiliwa na radiamali kali, nzito na ya kivitendo ya Waarabu na Waislamu wote.

Juu ya ukurasa

Ulimwengu wa Kiislamu na suala la Palestina

Uungaji mkono wa ulimwengu wa Kiislamu kwa Palestina

Suala la Palestina ndilo suala kuu kwa Waislamu kimataifa. Kwa miaka kadhaa, maadui wameweza hatua kwa hatua kuwafanya Waislamu waizoee hali ya kuporwa na kughusubiwa sehemu ya nyumba yao. Na suala si kughusubiwa nyumba tu ya Waislamu; bali kadhia ni kubwa zaidi ya hivyo. Suala ni kwamba maadui wa ulimwengu wa Kiislamu wameifanya sehemu ya nyumba ya Waislamu kama ngome kwa ajili ya kushambulia safu za Waislamu, na kwa ajili ya kukabiliana na malengo yao na kupambana na harakati zao. Suala lililopo hapa si huzuni na majonzi tu ya taifa fulani, kutokana na kudhulumiwa na kuachwa bila makaazi; kinachozungumziwa ni kughusubiwa kwa nchi; kinachozungumziwa ni kuwekwa dondandugu la kansa kwenye kitovu cha nchi za Kiislamu na katika nukta ya makutano kati ya Mashariki na Magharibi ya ulimwengu wa Kiislamu; kinachozungumziwa hapa ni dhulma ya kuendelea, ambayo imevigubika vizazi vya wananchi Waislamu wa Palestina kimoja baada ya kingine. Leo hii ambapo mapambano ya kumwaga damu yanayotokana na umma wa wananchi katika ardhi ya Palestina yameonyesha ishara ya kuwa hatari na tishio kubwa kwa wavamizi wasio na hisia, wasio na khofu ya kutenda jinai na wasiojua utu, yamewafanya maadui watumie mbinu kali zaidi na tata zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma; na hivyo Waislamu ulimwenguni kote wanapaswa kulipa uzito zaidi suala hili na kufikiria hatua ya kufanya.

Kimsingi uundaji wa dola la Kiyahudi- au kwa usahihi hasa dola la Kizayuni- katika nukta hii ya ulimwengu wa Kiislamu, umefanyika kwa kuzingatia malengo ya muda mrefu ya Uistikbari. Sababu hasa ya kuasisiwa utawala huu katika sehemu hii nyeti ambayo takriban ndiyo kitovu cha ulimwengu wa Kiislamu- yaani upande wa magharibi ya Uislamu ambao ni Afrika unaunganishwa na upande wa Mashariki ya Uislamu ambayo ni hii Mashariki ya Kati, Asia na Mashariki na ambayo ni nukta ya njia tatu kati ya Asia, Afrika na Ulaya- kulifanyika ili kuhakikisha kuwa kwa muda mrefu ujao udhibiti wa wakoloni wa wakati ule- ambao kiranja wao ilikuwa ni serikali ya Uingereza- kwa ulimwengu wa Kiislamu unaendelea kuwepo.

Njia sahihi ya kupambana na utawala ghasibu ni hii ambayo leo hii Wapalestina wenyewe wameitambua, na ndiyo waliyoshikamana nayo barabara, na ni jukumu la Waislamu wote kuwasaidia katika mapambano haya matakatifu. Leo hii hakuna udhuru wowote utakaokubalika, utakaotolewa na serikali za nchi za Kiislamu wa kuzifanya zisilijali suala la Palestina. Utawala ghasibu, umefikia kiwango cha juu kabisa cha ushenzi na ukatili, na umethibitisha kuwa ili kuweza kufikia malengo yake hatari ya kujipanua, uko tayari kufanya jinai yoyote ile. Mapambano ya Kiislamu ya wananchi wa Palestina, nayo pia yameshaondoa udhuru kwa kila mtu na kuonyesha kuwa licha ya mbinyo na mashinikizo ya kila upande ya adui, uhaini na usaliti wa wanaojidai kuwa ni marafiki, mmea wa istiqama na mapambano haujakauka, bali umekita mizizi na kustawi pia. Kwa hivyo ni wajibu wa nchi zote na mataifa kulichukulia kwa udhati wa moyo suala la Kiislamu la Palestina kuwa ni mojawapo ya masuala yenye kipaumbele cha kwanza kwao na kulipatia msaada kwa kadiri ya uwezo wao.

Kati ya madhehebu zote za Kiislamu, hakuna hitilafu yoyote juu ya suala hili; na mafakihi wote wamekubaliana kuwa ikiwa kipande kimoja cha ardhi ya Kiislamu kitatenganishwa na maadui wa Uislamu na ardhi nyingine ya Kiislamu, na kipande hicho kuwa chini ya utawala wa maadui wa Uislamu, Waislamu wote waelewe kwamba mi wajibu wao kufanya jitihada na kupigana Jihadi ili kukirejesha kipande hicho cha ardhi kwenye ardhi za Kiislamu. Taifa la Palestina- ambapo macho yote ya ulimwengu wa Kiislamu leo hii yameelekezwa kwake- lielewe kwamba nyoyo za umma wa Kiislamu zinalipongeza na kuliombea dua; na lau kama njia ingekuwa wazi kwa ajili ya kulisaidia, leo umma wa Kiislamu ungeelekeza misaada yake huko; bila kujali kama serikali nyingine zingeliafiki hilo au la. Umma wa Kiislamu hautoiacha Palestina, hautowaacha mkono wananchi wa Palestina na wala hautowapa kisogo vijana wa Palestina.

Juu ya ukurasa

Uungaji mkono wa serikali za nchi za Kiislamu kwa Palestina

Matarajio yaliyopo kwa serikali za nchi za Kiislamu ni kulipatia taifa hilo suhula zinazohitajika kwa ajili ya kujihami, na inatarajiwa kuziona serikali hizo zinatoa mashinikizo ya kisiasa kwa watu ambao wanatetea maslahi ya Wazayuni duniani. Wanaweza kuifanya kazi hii katika uhusiano baina ya pande mbili, katika jumuiya za kimataifa, katika hotuba zao rasmi na katika mazungumzo yao ya faragha. Kwa vile mvamizi na mchokozi hayuko tayari kuacha jinai zake, taifa la Palestina –ambalo ndilo lenye haki na linatetea haki yake- lazima liwe na uwezo wa kujitetea.

Juu ya ukurasa

Uungaji mkono wa taifa la Iran kwa wananchi wa Palestina

Daima taifa la Iran limekuwa, na litaendelea kuwa mtetezi wa mataifa yanayodhulumiwa na yaliyoko kwenye minyororo ya Uistikbari. Taifa la Iran daima limekuwa, na litaendelea kuwa bega kwa bega na wananchi Waislamu, wanamapambano na shujaa wa Palestina dhidi ya Wazayuni wafanya jinai, na linawausia ndugu zao wa Palestina kuwa kwa kutawakal na kumtegemea Mwenyezi Mungu, waendeleze njia ya Mwenyezi Mungu ambayo ni mapambano na adui ghasibu na waungaji mkono wake, hadi kuliangamaiza dola ghasibu la kizayuni. Taifa adhimu na askari waumini na wa kujitolea wa Iran wanalichukulia suala la kulihami taifa la Palestina kuwa ni wajibu wa kidini, na wanaamini kuwa hakuna lengo lolote katika njia ya Mwenyezi Mungu lisiloweza kufikiwa.

Juu ya ukurasa

Utumiaji wa vyombo vya uenezi katika kuiunga mkono Palestina

Baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, katika kila pembe ya dunia, Mayahudi walitengeneza mamia, bali maelfu ya filamu ili kujionyesha wao wenyewe kuwa ni watu waliodhulumiwa, na kuwaonyesha wale waliokuwa dhidi yao- kama ni kweli au si kweli- kuwa ni watu madhalimu. Dhulma wanayofanyiwa wananchi wa Palestina leo hii halijawahi kufanyiwa taifa lolote lile; na hii ni katika hali ambayo kwa bahati mbaya fikra za walio wengi duniani hazina habari kuhusiana na dhulma hii. Dhulma hii inapasa ibainishwe. Lazima zitengenezwe filamu na kufanyika kazi za sanaa ili walimwengu wote wajue ni nini kinachoendelea.

Juu ya ukurasa

Sura ya Nne: Utatuzi wa suala la Palestina

Utatuzi wa kidiplomasia wa suala la Palestina

Ili kulipatia utatuzi tatizo hili sugu/bughranj la Palestina, kuna njia mbili ambazo zimekuwa zikipendekezwa kila mara: moja ni njia potovu ya ufumbuzi, na nyingine njia sahihi ya ufumbuzi. Njia potovu ya ufumbuzi ni hii ya kufanya mazungumzo na kufikia mwafaka na ghasibu huyu ambaye si mwenye kuheshimu thamani za kiutu wala si mtekelzaji wa sheria za kimataifa na maazimio ya jumuiya za kimataifa. Njia hii ya ufumbuzi ni potovu kwa sura yoyote ile ya kidhahiri itakayokuwa nayo. Israel imeonyesha kuwa haiheshimu chochote kile inachokisaini; hata kama watafikia mwafaka na kusaini pia, hawadumu katika kuheshimu makubaliano hayo. Njia hii ya ufumbuzi ambayo ni ya kutia mawindo kinywani mwa mvamizi na mchokozi huyu na kumvimbisha zaidi ili apate uwezo wa kupiga hatua ya pili, si njia ya ufumbuzi; hii ndiyo tajiriba ya miaka sitini ya kadhia ya Palestina. Maazimio yamepasishwa katika Umoja wa Mataifa; na pamoja na kwamba Marekani ambayo ni mtetezi wa Wazayuni imeyasaini kidhahiri maazimio hayo, lakini ghasibu huyu hakuyatekeleza.

Ama njia ya ufumbuzi ya kimantiki ni njia ambayo dhamiri zote zenye mwamko duniani, na watu wote wanaoelewa masuala yanayojiri leo hii ulimwenguni hawana budi kukubaliana nayo ni ile ya kuitisha kura ya maoni kwa ajili ya wananchi wenyewe wa Palestina; watu wote walioondolewa katika ardhi yao ya Palestina; tab'an ni wale ambao wao wenyewe wanataka kurejea katika ardhi ya Palestina na kurejea majumbani kwao. Hili ni suala la kimantiki. Hawa watu wanaotangatanga huko Lebanon, Jordan, Kuwait, Misri na katika nchi nyingine za Kiarabu, warejee kwenye nchi yao na nyumbani kwao huko Palestina, na pia wale watu ambao kabla ya mwaka 1948 ambao ni mwaka ulipoundwa utawala bandia wa Israel walikuwa Palestina- wawe ni Waislamu, Wakristo au Mayahudi- watakiwe maoni yao. Iitishwe kura ya maoni ya kuwataka watu hao waamue aina ya serikali wanayotaka itawale katika ardhi ya Palestina. Hii ni demokrasia. Vipi demokrasia inakuwa nzuri kwa ulimwengu mzima lakini isiwe ni kitu kizuri kwa watu wa Palestina?! Vipi watu wote duniani wana haki ya kuamua juu ya mustakbali wao lakini wananchi wa Palestina hawana haki hiyo?! Hakuna mtu mwenye shaka kuwa utawala ulioko leo hii katika ardhi ya Palestina ni utawala uliokuja madarakani kwa mabavu, hila, hadaa na mashinikizo; hakuna mtu yeyote mwenye shaka juu ya hilo. Wazayuni hawakuja kwa kutumia njia za amani; kwa kiwango fulani walitumia mbinu na hila, na kwa kiwango fulani walitumia mashinikizo, mabavu na silaha ili kutwaa madaraka; kwa hivyo ni utawala wa mabavu na wa kulazimisha. Kwa hivyo wananchi wa Palestina wakusanywe na kupiga kura ili kuchagua aina ya serikali inayopasa kutawala katika nchi hiyo. Serikali hiyo na utawala huo uundwe, kisha uamue kuhusu watu waliohamia kwenye ardhi ya Palestina baada ya mwaka 1948; uamuzi wowote itakaochukua utekelezwe. Ikiamua wabaki basi watabaki, kama itaamua waondoke basi waondoke. Huu pia ni uamuzi wa wananchi, na pia ni demokrasia na haki za binaadamu, na pia ni hali inayoafikiana na mantiki inayotawala hivi sasa duniani.

Juu ya ukurasa

Mashinikizo kwa utawala wa kizayuni

Ghasibu huyu hakubali kutumiliwa lugha nzuri ya njia ya ufumbuzi wa kimantiki! Na hapa ndipo inapobidi wale wote wanaohusika na kadhia hii wajihisi kuwa wana jukumu; kuanzia nchi za Kiarabu, nchi za Kiislamu, wananchi wa mataifa yote ya Kiislamu ulimwenguni na hasa hasa wananchi wenyewe wa Palestina pamoja na jumuiya za kimataifa, kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha kuwa njia hii ya ufumbuzi wa kimantiki inatekelezwa; na inawezekana kutekelezwa. Baadhi ya watu wanaweza kusema kuwa kitu hiki ni ndoto na njozi tu na wala hakiwezekani; hapana! kinawezekana. Baada ya kupita miaka arubaini na ushee nchi za bahari ya Baltik ambazo zilikuwa sehemu ya Urusi ya zamani zilirejea katika hali yao ya asili na zikawa huru. Nchi za eneo la Qafqazi, kwa kipindi cha karibu miaka mia moja kabla ya kuundwa Shirikisho la Kisovieti zilikuwa chini ya utawala wa Urusi ya Tsar lakini baadaye zikarejea katika hali ya asili na kujipatia uhuru wao. Hivi sasa Qazaqistan, Azarbaijan, Georgia na nchi nyinginezo zimekuwa huru; zinajiendeshea mambo yao zenyewe. Kwa hivyo hili ni jambo linalowezekana. Isipokuwa kuna ulazima wa kuwepo irada, azma, uthubutu na ushujaa. Wananchi wa mataifa ni mashujaa, hawana khofu na wako tayari. Kwa hivyo hapa sasa ni jukumu la serikali; wa kwanza na wa mbele kabisa kuliko wote ni serikali za nchi za Kiarabu. Leo hii serikali za nchi za Kiarabu zinao uwezo wa kujitokeza mbele, zikapata uungaji mkono na mapenzi ya wananchi wao katika kadhia ya Palestina. Ikiwa utawala na serikali inaungwa mkono na watu wake, Marekani haiwezi kuwa na uwezo tena wa kuifanya chochote. Serikali hiyo itakuwa haiiogopi tena Marekani, na wala haitohisi kuwa inalazimika kufanya au kutofanya kitu kwa kuichelea Marekani.

Juu ya ukurasa

Utumiaji wa silaha ya mafuta

Miongoni mwa hatua muhimu zinazoweza kuchukuliwa na serikali za nchi za Kiarabu ni kuyatumia mafuta kwa zile nchi zinazouza mafuta nje. Haya maneno waliyoyaeneza Wamagharibi ulimwenguni kwamba msitumie silaha ya mafuta si maneno sahihi. Mafuta ni mali ya mataifa na yanapaswa kuyatumia kwa faida yao wenyewe. Wamarekani wameitumia kama silaha ngano na bidhaa zao nyingine za chakula; ikiwa sehemu nyingi duniani pia wanafanya hivyo, kwa nini nchi za Kiislamu na Kiarabu zisiwe na haki hiyo? Na wafanye hivyo kwa sura ya kuonyesha mfano tu kwa muda wa mwezi mmoja; kwa kuonyesha uungaji mkono kwa wananchi wa Palestina kwa kukatisha usafirishaji wa mafuta kwa nchi zote zenye uhusiano mzuri na Israel. Leo hii dunia inatumia mafuta ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya nishati ya uendeshaji vitu kama viwanda, nishati ya utoaji mwanga kama umeme na nishati ya utoaji joto ambavyo ni vitu vitatu vikuu kwa ajili ya maisha. Ikiwa nchi za ulimwengu hazitokuwa na mafuta, harakati za uendeshaji viwanda, utoaji mwanga na utoaji joto zitasimama.

Juu ya ukurasa

Misaada ya kifedha kwa wananchi wa Palestina

Misaada ya kifedha kwa Wapalestina haizihusu serikali tu, kwamba serikali fulani isema "e bwana! Mimi nimetoa dola milioni kumi, dola milioni ishirini au dola milioni hamsini", hali ya kuwa wala haijulikani imetoa pesa hizo kupeleka wapi, imezitoa vipi na imempa nani. Leo wananchi wa Palestina wanahitajia chakula na wanahitajia dawa. Wananchi wa Palestina si ombaomba. Ni wananchi wa taifa lenye heshima yake, lakini wako chini ya ukandamizaji wa adui. Watu wote wana wajibu wa kuwasaidia. Chukulia mfano katika nchi zote za Kiislamu- katika nchi ya Iran na nyinginezo- kama kila mtu miongoni mwa wananchi atatoa tuman elfu moja tu kuwasaidia wananchi wa Palestina uone nini kitatokea! Toman bilioni elfu moja zitakuwa na taathira kiasi gani kwa wananchi wa Palestina na maisha ya wananchi wa Palestina! Wawatayarishie pia na kuwapelekea vyakula, madawa, suhula na kila wanachohitajia kwa ajii ya mapambano na istiqama.

Juu ya ukurasa

Njia ya kuiokoa Palestina

Njia ya kuiokoa Palestina

Mambo ambayo utawala ghasibu umeifanyia nchi na wananchi wa Palestina katika kipindi cha miaka kadhaa ya hivi karibuni yanatosha kuwa uzoefu wa kuthibitisha kuwa hakuna matumaini yoyote ya kuiokoa Palestina kwa kutumia njia ya kuyategemea madola yanayodhibiti ulimwengu na vibaraka wao katika eneo.

Mapinduzi adhimu ya Kiislamu ya Iran yameonyesha kuwa ufunguo wa kutatulia matatizo makubwa uko mikononi mwa wananchi wa mataifa yenyewe, na kwamba endapo irada ya watu itamtegemea Mwenyezi Mungu na kuwa na imani na ahadi ya Mola itaweza kuzishinda tadbiri na malengo ya madola ya kibeberu. Hivi sasa baada ya matukio kadhaa yaliyojiri katika maeneo kadhaa duniani, nafasi ya wananchi wa mataifa imezidi kuthibitika. Irada ya wananchi wenyewe tu wa Palestina ndiyo inayoweza kusimama kukabiliana na unduli wa utawala wa kizayuni ulioighusubu Palestina; na kwa kusimama kwao kiume kumfanya adui arudi nyuma na kukubali kushindwa. Wananchi wa Palestina hawawezi na wala wasitarajie kupata uhuru wao na haki zao kupitia mikutano na makongamano ya viongozi wa nchi za Kiarabu. Kama vikao na mikutano hiyo haitokuwa na madhara na mwisho mbaya kwa wananchi madhulumu wa Palestina, basi kwa uchache haina maana wala haitokuwa na faida yoyote kwao wao.

Juu ya ukurasa

Mapambano, njia ya kuliokoa taifa la Palestina

Uokozi wa Palestina hautopatikana kwa kuupigia magoti kuuomba Umoja wa Mataifa au madola yenye nguvu, au kwa usahihi zaidi, kuupigia magoti na kuuomba utawala ghasibu wa kizayuni; njia pekee ya kuiokoa Palestina ni mapambano na kusimama kidete; ni kwa kuwepo umoja wa kalima wa Wapalestina na kalima ya umoja ambayo ni hazina na akiba isiyomalizika ya harakati ya Jihadi.

Nguzo kuu za mapambano haya, kwa upande mmoja ni makundi ya Jihadi ya Palestina na wananchi wote waumini na wanamapambano wa Palestina walioko ndani na nje ya nchi hiyo; na kwa upande mwingine ni serikali na wananchi wa mataifa ya Kiislamu ulimwenguni kote hususan maulamaa wa kidini, wanafikra, wenye vipawa wa kisiasa na wasomi wa Vyuo Vikuu. Endapo nguzo mbili hizi imara zitasimama mahali pake sawa sawa, hakuna shaka yoyote kuwa dhamira zilizoamka katika kila pembe ya dunia na nyoyo na fikra ambazo hazijatekwa na kasumba za propaganda za ukiritimba wa habari wa Uistikbari na Uzayuni, zitasimama kuusaidia upande wa haki na uliodhulumiwa, na kuvifanya vyombo vya Uistikbari vikabiliwe na dhoruba kali ya hisia, fikra na harakati. Mapambano na subra za mujahidina na wananchi wa Palestina, na uungaji mkono na misaada ya kila hali watakayopata kutoka nchi zote za Kiislamu vitaweza kuliondoa jinamizi la kishetani la kughusubiwa Palestina. Nguvu kubwa ya umma wa Kiislamu inaweza kutatua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu likiwemo tatizo sugu na lenye kuhitaji utatuzi wa haraka la Palestina.

Juu ya ukurasa

Mwamko wa wananchi wa Palestina

Bahati nzuri kwa kiwango kikubwa, mwamko wa Kiislamu wa wananchi wa Palestina umeweza kutoa mwanga mzuri kwa upeo wa mustakbali. Leo hii kizazi kipya cha taifa la Palestina kinapambana kwa jina la Mwenyezi Mungu na kwa kushikamana na imani ya Uislamu; na mapambano haya yanatoa matumaini makubwa mno kiasi kwamba kama inavyoshuhudiwa, maadui- wawe ni watawala wa kizayuni, Marekani, waungaji mkono wengine wa Israel au hata wasaliti wa eneo- wamechanganyikiwa na kushtushwa na harakati hii mpya, na hivyo wanatumia kila mbinu kwa lengo la kuharibu na kufifilisha muelekeo halisi wa mapambano. Pamoja na hayo, dini itaiokoa Palestina. Uislamu utairejesha tena Palestina kutoka mikononi mwa wavamizi.

Kizazi kipya cha Palestina kimeshauelewa ukweli huu, kwamba ikiwa kinataka kujivua na hali hii ya madhila, udunishwaji, udhalilishwaji na mashinikizo yanayoelekezwa dhidi yake, basi njia ya kufanya ni kupambana na kukabiliana na adui; njia ya kufanya si kukaa kwenye meza ya mazungumzo, kwani hao wanaofanya mazungumzo pia hawana walichokipata.

Juu ya ukurasa

Utaifa wa Kiarabu na suala la Palestina

Baadhi ya wakati husikika baadhi ya watu wakisema: suala la Palestina ni suala la Waarabu. Nini makusudio ya maneno haya? Kama makusudio ni kuonyesha kuwa Waarabu wanahisi wana uhusiano wa karibu zaidi wa kidugu, na wana hamu zaidi ya kutoa mchango, na wanafanya jitihada zaidi katika suala la Palestina, hilo ni jambo la kupendeza; lakini kama makusudio ya maneno hayo ni ile hatua ya viongozi wa baadhi ya nchi za Kiarabu ya kutokipa umuhimu hata chembe kilio cha "Enyi Waislamu nipateni" cha wananchi wa Palestina, na katika kadhia muhimu kama maafa ya Gaza kushirikiana na adui ghasibu na dhalimu na hata kuwapigia makelele watu wengine wanaotaka kutekeleza wajibu wao wa kuitikia kilio hicho kwa kuwaambia 'kwa nini nyinyi mnatoa msaada kwa Gaza,' katika hali kama hiyo hakuna Muislamu yoyote wala Mwarabu yoyote mwenye ghera na mwenye dhamira atakayekubali maneno hayo. Na si hayo tu, bali hatoacha kumlaumu na kumkemea pia msemaji wa maneno hayo.

Juu ya ukurasa

 Sura ya Tano: Amani na mapatano

Mbinu ya amani

Hii leo mbinu ya Wazayuni na waungaji mkono wao- serikali ya Marekani ikiwa ndiye muungaji mkono wao mkuu- ni kutumia neno zuri na la kupendeza la 'amani'. Bila shaka amani ni kitu kizuri sana; lakini amani hiyo ifanywe wapi, na itekelezwe na mtu gani?! Ikiwa mtu ameuvunja mlango na kuingia nyumbani kwako kwa nguvu, akakupiga wewe wenyewe, akamvunjia heshima ahli wako na watoto wako, kisha akavichukua vyumba viwili na nusu kati ya vyumba vyako vitatu, halafu akwambie, kwa nini wewe unakwenda kumshtakia huyu na yule bila sababu yoyote; kila mara unaanzisha mzozo na ugomvi; njoo tufanye suluhu; je kweli hiyo itakuwa suluhu na amani?! Dhati ya utawala huu ni uchokozi na uvamizi. Utawala wa kizayuni kimsingi umeundwa na unaendelea kuwepo kwa msingi wa utumiaji mabavu na ufanyaji ukatili, na bila ya hayo usingeweza kwenda mbele, na baada ya hapo pia hautoweza kwenda mbele. Wanasema watafute suluhu na amani na utawala huu! Lau kama wao wazayuni wangetosheka na haki yao- yaani nyumba hii yaani Palestina wangeikabidhi kwa mwenye nyumba mwenyewe na kwenda zao; au wakaiomba serikali ya Palestina na kusema kuwa turuhusuni baadhi yetu au sisi sote tubaki katika nchi hii- hakuna mtu atakayepigana vita na wao. Sababu ya kupigana vita na wao inatokana na kuingia kwenye nyumba ya watu wengine kwa mabavu na kuighusubu; kisha wakawatoa nje wenye nyumba na hivi sasa wanawafanyia dhulma. Hivi sasa wanazifanyia dhulma pia nchi zote za eneo na wamekuwa tishio kwa nchi zote. Kwa hivyo, hiyo suluhu na amani wanayoitaka, ni utangulizi kwa ajili ya uvamizi unaofuatia! Ikiwa itafikiwa suluhu na amani, itakuwa ni utangulizi wa kuhakikisha hapo baadaye wataweza kuanzisha tena uchokozi na uvamizi kwa namna nyingine.

Juu ya ukurasa

Mpango wa mapatano baina ya Palestina na Israel

Moja kati ya masuala yanayozungumziwa hii leo ili kadhia ya Palestina isahaulike na ili isizungumziwe katika fikra za waliowengi za umma wa Kiislamu ni haya mazungumzo eti ya amani yanayoendelea baina ya kundi moja la Wapalestina na Waisarel; yaani kadhia ya kufanya mapatano na serikali eti ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Hii pia ni mojawapo ya mbinu na hila chafu kabisa ya mtego wa Waisrael ambao bahati mbaya umewanasa baadhi ya Waislamu na baadhi ya Wapalestina wenyewe. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu kulingana na matumaini makubwa kabisa waliyopewa Wapalestina katika moja ya mazungumzo hayo, endapo Israel itatekeleza yale yote iliyoahidi, watakachopata Wapalestina ni asilimia nne tu na ushei ya ardhi ya Palestina! Yaani katika nchi hii ya Palestina ambayo ni mali ya Wapalestina na ambayo ardhi yake yote mmiliki wake ni wananchi wa Palestina na ni haki yao wao, ni asilimia yake nne tu ndiyo watakayopewa wao; na hiyo asilimia nne yenyewe basi ni ya aina gani?! Asilimia nne hiyo haiko mahali pamoja, bali imetawanyika! Kisha wale watu waliowaita na kuwaambia njooni muunde serikali hapa hawakuwapa ruhusa waendeshe mambo yao kama serikali inavyokuwa. Wamewataka watu hao waende huko ili kuwachunga Wapalestina wa eneo hilo wasije wakachukua hatua dhidi ya utawala wa Israel! Yaani eneo dogo kabisa na la sehemu tofauti, lililoekewa mipaka na vizuizi, na lisiloweza kundeshwa kama nchi, limetolewa na kupewa watu hao likiwa na kila kasoro na mapungufu! Kisha wao wametakiwa kuhakikisha kuwa mbali na hatua zinazochukuliwa na vyombo vya usalama vya Israel, na wao pia wachukue hatua dhidi ya wanamapambano wa Palestina walioko ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu! Usaliti wa watu hawa wanaofanya hivyo kwa jina la Wapalestina, ni mbaya zaidi, mkubwa zaidi na wa uovu zaidi kuliko usaliti wote iliofanyiwa Palestina hadi leo hii! Na wala hakuna kazi yoyote pia waliyowafanyia, wala wanayoweza kuwafanyia wananchi hao.

Juu ya ukurasa

Mantiki ya mapatano baina ya Waarabu na Israel

Serikali za nchi za Kiarabu zilikuwa zikisema kuwa sisi si Wapalestina zaidi kuliko Wapalestina wenyewe! Chochote kile wanachotaka wao wenyewe ndicho kinachopasa kufanywa. Kwanza kabisa tunawaambia kuwa suala la Palestina ni suala la ulimwengu wa Kiislamu. Mbali na upande wake wa kisiasa, kiusalama na kiuchumi, ni suala la utekelezaji wajibu wa kidini na Kiislamu. Kubwa zaidi ya yote hayo ni suala la Mwenyezi Mungu;lakini hata kama mtu atakuwa hamwamini Mungu na akawa anachotaka yeye ni kufanya kitu tu kwa ajili ya wananchi wa Palestina, na aje aone wananchi wenyewe wa Palestina wanasemaje. Leo taifa halisi la Palestina ni wale watu ambao wenzao waliotiwa nguvuni wako kwenye jela za utawala ghasibu, na wao wenyewe wako wanapiga nara na kutekeleza operesheni katika mabarabara, kwenye msikiti wa al-Aqsa, katika masoko na kwenye kila pembe ya ardhi inayokaliwa kwa mabavu. Ama wale watu wachache waliotekwa kwa tamaa, wakakubali kwenda kufanya mapatano si taifa la Wapalestina hata isemwe kuwa sisi si Wapalestina zaidi kuliko Wapalestina wenyewe.

Juu ya ukurasa

Sababu ya kutofanikiwa Intifadha ya Kwanza

Wakati ule –wa Intifadha ya kwanza- wingu la kufanya mapatano lilikuwa limeanza kutanda taratibu katika eneo; kundi moja la watu lilikuwa limejiegemeza kwa Marekani, na kundi jengine pia lilikuwa likiitakidi kuwa haiwezekani kusimama kidete na kukabiliana na mashinikizo ya kisiasa na propaganda za kimataifa, na kwamba hakuna njia nyingine yoyote ghairi ya mapatano; tena basi kwa kufuata masharti ya Marekani na Israel. Baada ya matukio kadhaa yaliyojiri wakati ule katika eneo; yakajitokeza mazingira ya kuutilia nguvu zaidi mtazamo huo. Wakati ule (wa Intifadha ya kwanza) kila mara zilikuwa zikizungumziwa njia za aina mbili kuhusiana na jinsi ya kukabiliana na Israel: kukabiliana kijeshi majeshi ya Waarabu na Israel- ambapo ilikuwa ikielezwa kuwa tajiriba zote kuhusiana na suala hilo zilikuwa zimegonga mwamba- na njia ya kufanya mapatano ambayo ingepelekea kuthibiti kwa matakwa ya Israel kwa njia za amani, ambapo pamoja na kukubali kuondoka katika sehemu fulani tu ya ardhi ilizozivamia na kuzikalia kwa mabavu, suala hilo lingehakikisha pia uwezo wa kijeshi wa nchi za Kiarabu hauongezeki; sawa na kile kilichotokea Camp David. Wakati ule utumiaji wa mbinu ya mapambano haukuwa ukizungumziwa, bali ilikuwa ikielezwa kwamba suala hilo halikuwa likikubaliwa na wananchi waliowengi.

Juu ya ukurasa

Matokeo ya mpango wa mapatano wa Oslo

Wananchi wa Palestina walipata hasara kubwa katika Intifadha yao ya kwanza na kutoa roho nyingi za mashahidi na majeruhi katika njia ya Uislamu na ya ukombozi wa ardhi za Kiislamu; lakini hatimaye mazungumzo ya Oslo yaliisimamisha Intifadha hiyo. Leo hii hata Wapalestina waliokuwa wapangaji na watetezi wa mpango wa Oslo hawautetei tena mpango huo; na sababu ni kuwa walifahamu vyema kwamba Israel ilikuwa ikitaka kutatua matatizo yake tu; yaani iweze kujivua na hali ya kukabiliana na wanamapambano wanaotumia mawe, na kupunguza kiwango cha mapigo inayopata. Na kama kuna kitu kidogo kabisa ambacho ilitoa kuupatia upande wa Palestina, basi ilifanya hivyo ili tu kuzima moto wa Intifadha na kupunguza kiwango cha udhaifu wake wa kuweza kupata kipigo kirahisi. Kwani mara baada ya kuhisi kuwa tatizo lake limetatuka, na kudhani kwamba wananchi wa Palestina hawana uwezo tena wa kuanzisha tena Intifadha na mapambano ya kukabiliana nayo, iliamua kusitisha hata hizo fursa chache ilizotoa kuupatia upande wa Palestina, na hivyo kudhihirisha waziwazi dhati yake halisi ya kutaka kujipanua. Mwenendo wa mapatano na mpango wa Oslo viliwaweka wananchi wa Palestina katika hali iliyowafanya waelewe kuwa hawana njia nyingine ya kufanya ghairi ya kuanzisha mapambano.

Juu ya ukurasa

Usaliti kwa malengo matukufu ya Palestina

Wanachojaribu kufanya ni kuhakikisha kitu kinachojulikana kama taifa la Palestina kinasahaulika moja kwa moja; kana kwamba haijawhi kuwepo ardhi yoyote ile iitwayo Palestina wala halijawahi kuwepo taifa lolote ambalo ni mmiliki wa ardhi hii! Hivyo ndivyo walivyotayarisha utangulizi wa kazi hiyo, na kwa kweli mtu anatazama kwa masikitiko, mastaajabu na mshangao mkubwa kuona kwamba kuna baadhi ya watu wanaosalimu amri juu ya suala hilo, na kwamba leo hii anatokea mtu duniani anayekubaliana pia na suala hili lisiloingia akilini, la kidhalimu na la kijinga lililokubaliwa na wale waliokubali kusalimu amri! Hii ni hali inayotokea hii leo, kwamba kuna kikundi cha watu wanaoitwa eti Wapalestina, ambao wameletwa kwenye kijisehemu cha ardhi kubwa ya Palestina ambacho ni asilimia nne ya ardhi ya nchi ya Palestina, kisha wakapewa mamlaka bandia, pungufu na ya kimaonyesho tu ya utawala; na kwa upande wao wakataka kadhia ya Palestina, suala la ardhi na suala la taifa la Palestina lisahauliwe na kuachwa kabisa, na kwamba mtu yeyote yule kati ya Wapalestina atakayetaja jina la taifa la Palestina, jina la nchi na historia ya Wapalestina, basi watu hao waliokubali kufanya mapatano hayo yenye madhara makubwa, wana jukumu la kumkandamiza na kumnyamazisha mtu huyo!

Juu ya ukurasa

Usaliti wa watawala wa Kiarabu kwa Palestina

Wazayuni na waungaji mkono wao, wa mbele kabisa akiwa ni Marekani wamebuni mpango wa kutoa nara za kuleta mapatano ambao kimsingi lengo lake ni kuimarisha ukaliwaji wa kimabavu na kighasibu wa Palestina na kuweza kuuburuza kadiri walivyoweza upande wa Wapalestina. Huko nyuma baadhi ya serikali za nchi za Kiislamu zilifika hadi hata kuuendea kinyume mrengo wa nchi zilizokuwa mstari wa mbele wa mapambano! Kimya cha kuridhia, kilichoonyeshwa na aghalabu ya viongozi wa nchi za Kiarabu, ambao katika baadhi ya wakati kiliambatana na usaliti wa waziwazi, pamoja na misimamo ya kidhalili na kisaliti ya wanaojidai kuwa viongozi wa taifa la Palestina, yote hayo ni vikufu vilivyoungana pamoja vya mnyororo wa dhulma, uhaini, uchupaji mipaka na usaliti unaotaka kuifanya ardhi ya Kiislamu ya Palestina iendelee kughusubiwa milele, na wananchi wake madhulumu na wanaoteseka waendelee kubaki milele katika hali ya ufungwa na ukimbizi. Kimya na mapatano yaliyochanganyika na usaliti yaliyofanywa na nchi nyingi za Kiarabu, na hata kujionyesha baadhi yao kuwa hawajali wala hawashughulishwi na hatima ya Palestina vimepelekea hali kufikia hadi ambayo, baada ya miaka kadhaa ya kuficha na kukana, utawala ghasibu wa kizayuni, hivi sasa unatamka tena hadharani dai lake la kuunda dola kubwa la Israel, na kukariri bila haya wala aibu nia yake chafu ya kutaka kuvamia na kughusubu ardhi nyingine mpya za nchi za Kiislamu.

Juu ya ukurasa

 Sura ya Sita: Mapambano na Istiqama

Nguvu ya wananchi wa mataifa

Uistikbari hautambui kwamba kuna nguvu ambayo ni kubwa zaidi kuliko nguvu za silaha zao. Na nguvu hiyo ni wananchi wa mataifa; ni nguvu ya umma. Taifa lolote lile lenye imani juu ya asili fulani, mantiki na msingi fulani wa kifikra, na likawa limeshikamana barabara na mantiki hiyo, hakuna nguvu yoyote- iwe nguvu ya atomiki, kubwa zaidi au ndogo zaidi ya atomiki- itakayoweza kulishinda taifa hilo. Watu hao wameipuuza nguvu ya wananchi wa mataifa, na nguvu ya Mwenyezi Mungu muweza aliyetukuka ambaye yuko pamoja na irada, azma na hatua zinazochukuliwa na wananchi wa mataifa:

«كلا نمد هؤلاء و هؤلاء»

Mwenyezi Mungu anasema: "Wote hao tunawakunjulia -hawa na hao", yaani kundi lolote lile litakalojituma kwa ajili ya kuyafikia malengo linayoyaitakidi, litapata msaada wa Mwenyezi Mungu mtukufu. Ikiwa kundi hilo ni la watu wanaomwamini Mwenyezi Mungu, hapo tena huwa ni vigumu zaidi mara kumi kukabiliana nalo na kulishinda.

Juu ya ukurasa

Mapambano ya wananchi mashujaa wa Palestina

Mapambano ambayo yameanzishwa leo hii na wananchi wa Palestina si mapambano kati ya jeshi moja na jeshi jengine, hata tuweze kusema kuwa jeshi hili lina idadi hii ya vifaru, na jeshi lile lina idadi ile; ni hili lenye vifaru vingi zaidi au lile. Bali ni mapambano ya viwiliwili na roho za watu wasioyakhofu mauti. Kila kijana aliyejitolea muhanga, anayesimama na kukabiliana na utawala vamizi wa kizayuni ni tishio kwa wazayuni mithili ya divisheni nzima ya jeshi. Mtu kama huyo huwezi kumshinda kwa kifaru, kombora, ndege ya kivita na helikopta ya Apache. Wakati mtu –hata akiwa mtu mmoja- anapokuwa hana khofu ya mauti na akawa amejiweka tayari kujitoa muhanga katika njia ya Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya kutekeleza wajibu wake, hugeuka kuwa hatari kubwa kabisa kwa wapenda dunia wasio na insafu.

Kujitolea huku kufa shahidi hakufanyiki kutokana na hisia za jazba; kunafanyika kutokana na imani ya Uislamu, imani ya Siku ya Kiyama na imani juu ya maisha baada ya kifo. Mahali popote ulipo Uislamu kwa maana yake halisi, huwepo hatari hiyo kwa Uistikbari. Ili kuidhibiti Palestina, Uistikbari unalazimika kupambana na Uislamu. Na kupambana na Uislamu, maana yake ni kupambana na ulimwengu wa Kiislamu, na mapambano ya aina hiyo hayawezi kuufikisha popote. Hakika ya kadhia hii ni kwamba kuna taifa la watu ambalo wamelitoa katika nyumba yake na kuliacha bila makaazi, na taifa hili lina haki ya kurudi ili kuichukua tena nyumba yake. Mapambano haya ni mapambano ya kupigania haki. Marekani inayaita mapambano haya kuwa ni "ugaidi"; lakini ule unyama wanaofanyiwa wanamapambano wa Kipalestina na Wazayuni, haiuiti kuwa ni ugaidi!

Leo hii taifa la Palestina ni taifa madhulumu, ambalo pamoja na kudhulumiwa ni shujaa mno; na ni haki kabisa kuliita: "taifa shujaa la Palestina". Taifa hili linapambana peke yake, katika hali ya upweke huku likiwa mikono mitupu, na kuweza kuyashinda madola yenye nguvu za kimaada duniani, yenye kila aina ya zana za mauaji na ukandamizaji.

Juu ya ukurasa

Mhimili mkuu wa mapambano na utawala wa kizayuni

Lengo kuu la mapambano na utawala ghasibu linapasa liwe ni hili:

- kuufungia utawala ghasibu ndani ya mipaka ya ardhi unazozikalia kwa mabavu, na

- kuendelezwa mapambano ya wananchi wa Palestina ndani ya nchi yao, na kuwafikishia kila aina ya msaada wanaouhitajia hadi kufikia ushindi kamili

Juu ya ukurasa

Kigezo cha wanamapambano wa Kipalestina

Ni zaidi ya miaka hamsini sasa tangu Palestina ivamiwe na kukaliwa kwa mabavu; miaka hamsini iliyopita, alikuwepo kijana wa Kipalestina pia. Huyu kijana wa Kipalestina aliyojitokeza namna hii hivi sasa katika medani ya mapambano, amejifunza hivi kutoka kwa nani na anafuata kigezo cha mtu gani? Kigezo chake ni kijana mwanamapambano, muumini na mwenye ikhlasi wa Lebanon. Katika maandamano wanayofanya katika Ukanda wa Gaza na katika Ufukwe wa Magharibi wa mto Jordan- ambalo ni moja ya maeneo wanayoishi Wapalestina- wanabeba na kuinua juu picha ya kiongozi wa Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah. Waliichukua bendera ya Hizbullah ya Lebanon na kuitundika juu ya kuba la Msikiti wa al-Aqsa. Japokuwa Wazayuni hawakuruhusu ibakie hapo lakini walikwenda kutundika. Kwa hivyo yeye amekuwa mfano wa kuigwa na kijana wa Kipalestina. Watazamaji wengi zaidi wa televisheni ya al-Manar ya Hizbullah ya Lebanon wako ndani ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu! Sio tu wanaangalia vipindi vyake bali pia vinawaburudisha kama anavyoburudika mtu mwenye kiu ya maji kwa funda la maji baridi.

Juu ya ukurasa

Jihadi, wajibu wa umma wa Kiislamu

Hakuna fakihi yoyote katika Uislamu aliye na shaka na mtazamo tofauti, kwamba wakati adui anapovamia na kushikilia ardhi ya Waislamu, akatishia usalama wa ardhi ya Kiislamu katika nchi mojawapo, ni wajibu wa Waislamu wote kupambana na adui huyo kwa kuanzisha Jihadi kubwa na ya pande zote, ili kumtoa katika ardhi hiyo ya Kiislamu na kumtia adabu. Endapo umma wa Kiislamu utazinduka utaelewa kuwa hili ndilo balaa kubwa zaidi lililowashukia Waislamu katika zama za hivi karibuni. Hukumu ya Uislamu juu ya kadhia hiyo iko wazi kabisa. Hakuna Muislamu yoyote mwenye shaka juu ya hukumu inayohusiana na kadhia ya Palestina. Hii ndiyo hukumu iliyotajwa katika vitabu vyote vya Fik-hi ambavyo vimezungumzia suala la Jihadi. Ikiwa makafiri watakuja, wakauteka au kuuzingira mji wa Waislamu, hakuna yeyote katika mafakihi wa Kiislamu, waliopita na wa sasa, aliye na shaka kama suala hili ni wajibu kwa Waislamu wote au la. Madhehebu zote za Kiislamu zina mtazamo mmoja juu ya suala hili. Jihadi ya kuanza ni wajibu wa kifayah (unaotosha kutekelezwa na baadhi tu ya Waislamu); lakini katika hali nyinginezo ghairi ya hiyo ambapo Jihadi ya kujihami ndiyo kielelezo cha wazi zaidi cha kujitetea, huwa ni wajibu wa Waislamu wote.

Juu ya ukurasa

Intifadha ya Msikiti wa al-Aqsa

Intifadha ya kwanza ilisimamishwa kutokana na taathira za ulaghai uliofanywa na Wazayuni na waungaji mkono wao, wa kutoa ahadi kwa Wapalestina kuwa watapata fursa fulani fulani kupitia njia za amani na vile vile kutokana na ushawishi wa wafanya mapatano pamoja na mashinikizo ya Marekani na Magharibi; lakini baada ya kupita miaka kumi tangu kipindi hicho imedhihirika kuwa juhudi zote zilizokuwa zikifanywa na waungaji mkono wa Uzayuni duniani zilikuwa ni kwa ajili ya kuunusuru utawala wa Israel na mashinikizo yaliyotokana na mashambulio ya Waislamu; na yale waliyowaahidi wafanya mazungumzo wa Kipalestina, hayakuwa chochote ghairi ya mazigazi tu.

Intifadha ya Msikiti wa al-Aqsa ilikuwa ni mwanzo wa mabadiliko makubwa katika mapambano ya wananchi wa Palestina. Mapambano ya Palestina yameshuhudia misukosuko mingi, yamevuka njama za aina mbali mbali, yameshinda changamoto kali na kukabiliana na anuai za milio ya silaha na ngurumo za mizinga na ndege za kivita za adui; na leo hii yamefika mahali yametambua vyema kuwa njia pekee ya kujikomboa na kujinasua kutoka kwenye makucha ya watenda jinai wa kizayuni na waungaji mkono wao ni Jihadi na mapambano ya kudumu; na huo ndio mkakati na stratijia inayoungwa mkono na fikra za waliowengi katika ulimwengu wa Kiislamu.

Wazayuni walikuwa wameratibu mlingano wa nguvu kwa msingi wa kuwadunisha na kuwadhalilisha wananchi wa Palestina, lakini Wapalestina wakaweza kusimama dhidi ya mlingano huo na dhidi ya mikataba ya udhalilishaji ya utawala wa kizayuni, mfumo wa kibeberu wa Marekani na wafanya mapatano waliofeli; na kwa kuchagua njia ya izza na heshima wakaweza kuufanya utawala wa watenda jinai wa Israel uandamwe na mgogoro kwa upande wa ndani, na kukabiliwa na Intifadha na mapambano kwa upande wa mipakani.

Mhimili mkuu wa Intifadha ya al-Aqsa ni Baitul Muqaddas; yaani cheche iliyoamsha ghadhabu za wananchi wa Palestina ilikuwa ni utovu wa adabu uliofanywa na Wazayuni wa kuuvunjia heshima msikiti wa al-Aqsa. Wananchi wa Palestina ambao walielewa jukumu nyeti walilonalo la kulinda moja ya maeneo matakatifu zaidi ya kidini ya Waislamu, walijitokeza uwanjani na kujitolea muhanga kwa kuuwasha mwenge wa mapambano na istiqama dhidi ya wavamizi wa kizayuni.

Mwenendo wa mapatano – na kwa usahihi zaidi mpango wa Oslo- ulisababisha kuzuka mfarakano baina ya Waislamu; lakini Intifadha hii yenye baraka imeweza kurejesha umoja wa kitaifa katika jamii ya Wapalestina. Matabaka yote ya wananchi yanashiriki katika mapambano hayo, na mirengo ya Kiislamu na kitaifa imeshikamana pamoja.

Juu ya ukurasa

Sababu ya mapambano ya Palestina (Intifadha ya Msikiti wa al-Aqsa)

Sababu ya mapambano ya Palestina si Jamhuri ya Kiislamu wala wananchi wa Lebanon; sababu ya mapambano ya Palestina ni Wapalestina wenyewe; sababu ya mapambano na Intifadha ya Palestina ni mrundiko wa majonzi na machungu yaliyokusanyika ndani ya nyoyo za kizazi cha vijana hawa ambao leo hii wamejitokeza uwanjani kwa ukakamavu na matumaini. Taifa la Iran linawapongeza vijana hawa na linawahisi kama watu wake; Palestina ni sehemu ya mwili wa Uislamu, na taifa la Iran linawahisi wananchi wa Palestina na vijana wa Palestina kama ndugu zake wa damu; lakini ni wao wenyewe ndio wanaoendesha na kuendeleza Intifadha.

Juu ya ukurasa

Palestina, mhimili mkuu wa harakati ya mwamko wa Kiislamu

Katika miongo miwili ya hivi karibuni, mwamko wa Kiislamu, au kwa maneno mengine, harakati ya mwamko wa Kiislamu, imedhihiri kwa nguvu na uwezo kamili katika uga wa eneo na katika ulimwengu wa Kiislamu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kwa kujitokeza harakati ya Imam Khomeini (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake). Leo hii mhimili mkuu wa harakati hii, ni suala la Palestina. Intifadha ya al-Aqsa imeweza kuwavuta na kuwaleta pamoja kwenye uwanja wa mapambano hata wale walioko nje ya mipaka ya kijografia ya Palestina na nje ya taifa la Palestina, pamoja na wananchi wa mataifa yote ya Waislamu na Waarabu. Maandamano ya mamilioni ya watu katika mataifa ya Kiislamu kutoka mashariki hadi magharibi ya ulimwengu wa Kiislamu (ya kuunga mkono Intifadha ya al-Aqsa) yameonyesha kuwa wananchi wa Palestina wanaweza kutegemea uungaji mkono wao, na wakati huo huo yameweza kutoa mchango mkubwa katika kuleta umoja baina ya Waislamu.

Siku ilipoanzishwa harakati ya mapambano ya Kiislamu nchini Lebanon kwa hima ya wananchi mashujaa wa Kilebanon na kwa muongozo na uungaji mkono wa Imam Khomeini, Israel ilikuwa imeuvamia na kuukalia kwa mabavu mji mkuu wa Lebanon Beirut, na kuanzisha satua yake katika masuala ya kisiasa ya nchi hiyo. Siku zile wakati wanamapambano wa Kiislamu walipokuwa wakipiga nara za «زحفاً زحفاً نحوالقدس» yaani "mbele kwa mbele kuelekea Quds", baadhi ya watu waliokuwa wamelala waliwaita wanamapambano hao kuwa ni watu wenye fikra finyu, na wakawa wanawauliza kwa kejeli kwamba: Hivi kweli inawezekana kuelekea Quds, wakati nyinyi Walebanon hamuwezi kuingia kwenye mji mkuu wa nchi yenu? Ilichukua kipindi cha miaka kumi na nane tu tokea siku ile hadi siku ya ushindi wa kihistoria wa wanamapambano wa Kiislamu dhidi ya Israel. Miaka kumi na nane si muda mrefu katika historia ya mapambano ya mataifa.

Juu ya ukurasa

Mapambano, sharti la ukombozi

Intifadha ya Msikiti wa al-Aqsa ni mapambano ya wananchi ambayo yalionyesha kuwa Wapalestina wamekatishwa tamaa na njia zote za kufanya mapatano, na wakaelewa kwamba mapambano, ndio njia pekee ya kufikia ushindi. Mapambano, yakiwa ni kigezo na njia ya mafanikio ya kufuata kwa umma wa Kiislamu, yaliweza kwa mara ya kwanza kabisa kuzikomboa ardhi zilizokuwa zikikaliwa kwa mabavu pasina kutoa chochote kwa Israel, na kuufanya utawala wa kizayuni usiweze kufikia lengo lake la kutundika bendera yake katika mji mkuu wa nchi ya Kiarabu, yaani Lebanon. Katika makubaliano ya Camp David, Israel iliondoka katika ardhi ya Misri kwa sharti kwamba Misri isipeleke jeshi lake huko kaskazini mwa Sinai; lakini huko kusini mwa Lebanon, ilikuwa ni Israel, ambayo kutokana na kukhofu nguvu za wanamapambano wa Kiislamu, ndiyo iliyoomba kwa kusihi jeshi la Lebanon lipelekwe kwenye mpaka wa Palestina na Lebanon; yaani harakati ya mapambano iliweza kurejesha kikamilifu mamlaka ya utawala wa kitaifa ya nchi hiyo huko kusini mwa Lebanon na katika maeneo mengine yaliyokuwa yakikaliwa kwa mabavu.

Juu ya ukurasa

Sura ya Saba: Hatima ya Palestina

Kubakia Palestina na kutoweka Israil

Leo viongozi wa utawala ghasibu unaoikalia kwa mabavu nchi ya Kiislamu ya Palestina na waungaji mkono yao yaani Marekani, ambayo inawaunga mkono wazayuni hao kijinga, kibubusa na bila mpaka wala masharti yoyote, wanajaribu kuhakikisha wanalifuta katika historia na kumbukumbu za watu jina la Palestina, ili kisibakie asilani ndani ya akili za watu kitu kinachoitwa Palestina. Tokea Palestina ilipovamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu katika mwaka 1947 na kudhibitiwa kikamilifu mwaka 1948 na serikali ya kizayuni kuingia madarakani hadi hii leo, wameshindwa kuifanya kazi hiyo na wala hawatoweza kuifanya kwa miongo kadhaa ijayo. Wao hawatoweza kulifuta jina la Palestina. Ni wao wenyewe ndio watakaofutwa katika kumbukumu za historia, lakini Palestina na taifa la Palestina halitofutika. Wao wanadhani kuwa Palestina na taifa la Palestina vitatoweka. Taifa la Palestina litabaki, Palestina pia itaendelea kuwepo, na kwa rehma za Mwenyezi Mungu bendera ya Palestina pia itapepea kwa hima ya vijana wa Kiislamu wa Palestina na Lebanon. Uzayuni na serikali ghasibu na bandia ya kizayuni iliyoko Palestina zitatoweka tu. Wananchi wa Palestina wanapaswa kuomba msaada kwa Mwenyezi Mungu mtukufu na kutawakal kwake yeye Mola. Vijana wa Kipalestina, vijana wa Lebanon, vijana wote wa ulimwengu wa Kiislamu na wanafikra wote, wanapaswa kuifuata njia hiyo.

Wazayuni maghasibu na madhalimu wanapaswa waelewe kuwa hawawezi kukishinda kizazi hiki cha vijana waumini wa Kiplaestina na wa Kilebanon. Mapambano ya wananchi wa Palestina yanayotokana na imani na kushikamana na subra, hayawezi kusimamishwa kwa mapatano ya kisiasa, mashinikizo ya kijeshi na kiusalama au makelele ya matarumbeta ya propaganda. Kama ambavyo nguvu ya istiqama na kusimama kidete ya taifa adhimu la Iran haiwezi kuvunjwa kwa kutumia mbinu zilizofeli, zilizochakaa na kupitwa na wakati ambazo zimekuwa zikikaririwa mara kadhaa na Wazayuni na waungaji mkono wao katika miongo miwili iliyopita.

Juu ya ukurasa

Mustakbali wa yakini

Hali ya leo ya Palestina inatoa bishara njema ya mustakbali wa yakini ambao Mwenyezi Mungu amewaahidi Mujahidina wa kweli na waliosimama imara; na hii ni ahadi isiyobadilika. Utawala dhalimu, na wenye uso wa kikatili, wa kizayuni, na nyuma yake sera za Marekani na Uzayuni wa kimataifa, wanadhani kwamba wataweza kulishinda taifa la Palestina kwa vitendo vyao vya jinai na maafa wanayoyasababisha, na kulilazimisha lisalimu amri. Hili ni kosa kubwa; na wale wanaolifanya watakuja kupata kipigo kikali katika siku za usoni.

Palestina ni mali ya wananchi wa Palestina, na leo au kesho utawala wa maghasibu utalazimika kusalimu amri mbele ya ukweli huo. Leo vijana Waislamu na wanamapambano wa Palestina wanabeba jukumu kubwa na la kihistoria, na wanatakiwa wawe na imani kamili ya kupata nusra ya Mwenyezi Mungu na kuthibiti ahadi yake ya uhakika; na walitunukie taifa na nchi yao mustakbali wa kweli kutokana na imani yao, matumaini waliyonayo na Jihadi wanayopigana hii leo. Kwa kuendelezwa mapambano ya wananchi Waislamu wa Palestina na uungaji mkono wa ulimwengu wa Kiislamu, kwa rehma za Mwenyezi Mungu Palestina itakombolewa, na Baitul Muqaddas, Msikiti wa al-Aqsa na maeneo mengine ya ardhi hiyo ya Kiislamu yatarejea mikononi mwa ulimwengu wa Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Ushindi wa damu dhidi ya upanga

Fikra za waliowengi katika ulimwengu wa Kiislamu nazo pia zielewe kuwa: Marekani na madola mengine ya Kiistikbari hayawezi kujiingiza kwenye kadhia ya nchi za Kiislamu kwa sababu za kuwa na uchungu na nchi hizo, kwa kuzitakia mema na kwa ajili ya usuluhishi. Msimamo wao ni msimamo wa kiadui na wa kumuunga mkono dhalimu na mchokozi. Jukumu la Waislamu halimaliziki. Jukumu hili ni jukumu la kudumu na la wote. Wanapaswa kuwapatia wananchi Waislamu wa Palestina nyenzo wanazohitajia, wawasaidie na kuwapa moyo ili waweze kuendeleza Jihadi yao ya kishujaa. Kwa kupambana, kwa kutoonyesha kuchoka, kwa kusimama kidete na kwa ushujaa wake linaoonyesha, leo taifa la Palestina limethibitisha kuwa damu inaweza kusimama kukabiliana na upanga, na inshaallah litathibitisha kuwa damu ni mshindi dhidi ya upanga.

Juu ya ukurasa

 
< Nyuma   Mbele >

^