Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Ujenzi wa Nchi na Ustawi wa Kiuchumi Chapa
01/11/2009

Sura ya kwanza: Ujenzi wa nchi na Ustawi wa Kiuchumi

Sharti la mafanikio katika maendeleo ya kiuchumi
Uislamu na Ustawi wa Kiuchumi
Kigezo cha ndani cha Ustawi
Maandalizi ya kiutamaduni kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi
Propaganda dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu
Hamu ya ustawi, hofu ya ustawi
Wajibu wa matabaka yote
Umuhimu wa kuwa na moyo wa kujiamini katika ujenzi wa nchi
Kasoro za kiuchumi za kipindi cha ujenzi wa nchi
Mabalaa ya kipindi cha ujenzi mpya wa nchi

Sura ya Pili: Mambo yenye taathira katika ustawi wa kiuchumi

Kazi

Ubora wa kazi
Thamani ya kazi katika utamaduni wa Kiislamu
Nafasi ya kazi katika ustawi wa kiuchumi

Mfanyakazi ya kibarua

Utukufu wa mfanyakazi ya kibarua
Wajibu wa utawala kwa wafanyakazi za kibarua
Thamani ya mfanyakazi ya kibarua katika jamii
Mfanyakazi ya kibarua katika mantiki ya mfumo wa Kibepari, Kisoshalisti na Kiislamu

Wanawake

Nafasi ya wanawake katika kipindi cha ujenzi mpya wa nchi
Shughuli za kiuchumi za wanawake
Harakati za kiuchumi za wanawake kwa mtazamo wa sheria za Uislamu

Iktisadi

Nafasi ya Iktisadi katika ustawi wa kiuchumi

Umaanawi

Ulazima wa kuwepo umaanawi pamoja na ustawi wa kiuchumi

Udhibiti

Udhibiti wa kiuchumi na kifedha

Mafuta

Ufungaji wa visima vya mafuta
Ulazima wa kutenganisha uchumi wa taifa na pato la mafuta

Uandaaji mipango

Ulazima wa kutenganisha uchumi wa taifa na pato la mafuta

Uongozi wa uendeshaji

Nafasi ya uongozi wa uwajibikaji katika ustawi wa kiuchumi

Moyo wa kujiamini

Umuhimu wa kuwa na moyo wa kujiamini katika ujenzi wa nchi

Mageuzi

Umuhimu wa mageuzi katika ustawi wa kiuchumi

Sekta ya Viwanda

Nafasi ya viwanda na ufundi katika ustawi wa kiuchumi

Umoja wa kitaifa

Umoja wa kitaifa, sharti la ustawi wa kiuchumi

Ujenzi wa Nchi na Ustawi wa Kiuchumi


Sura ya kwanza: Ujenzi wa nchi na Ustawi wa Kiuchumi

Sharti la mafanikio katika maendeleo ya kiuchumi

Jamhuri ya Kiislamu inatoa changamoto kuwa inao uwezo wa kuijenga nchi na kuitoa Iran kwenye hali ya kubaki nyuma kimaendeleo ya enzi za utawala dhalimu wa kifalme; na leo hii kila hatua inayopigwa katika njia ya maendeleo ya kielimu, kiviwanda na kiuchumi, na kila hatua inayopigwa katika uwanja wa kuijenga upya nchi, ni ithbati ya kuonyesha kuwa mfumo mtukufu wa Jamhuri ya Kiislamu uko katika haki, na pia ni ushahidi kuwa dai na changamoto iliyotoa ni ya kweli. Hata hivyo hatua yoyote itakayopigwa katika njia ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa nchi itaweza kupata mafanikio pale tu itakapopata ilhamu ya fikra na misingi ya Kiislamu, na kama itakuwa na muelekeo wa kudumisha na kuimarisha malengo matukufu, thamani na nara za Mapinduzi ya Kiislamu. Ni katika hali hiyo ndipo harakati ya ujenzi wa nchi itakuwa ni harakati ya kweli na ya uhakika ambayo itaweza kuifanya nchi isitumbukie kwenye lindi la njozi tupu za ustawi na kunasa kwenye kinamasi cha utegemezi na ufisadi wa kifedha, kisiasa na kiakhlaqi.

Juu ya ukurasa

Uislamu na Ustawi wa Kiuchumi

Uislamu unayapa mataifa uhuru na uwezo wa kujitawala, uhuru katika mazingira ya maisha yao- kuwa huru na kujikomboa na madola ya kidikteta na ya kiimla, kujikomboa na ujahili na imani potofu, kujikomboa na taasubi za kijahili na ufinyu wa kifikra- na vile vile kuwa huru na kujinasua na mitego ya kiuchumi na mashinikizo ya kisiasa ya Uistikbari. Uislamu unayapa mataifa ufanisi wa huduma za kijamii na maendeleo ya kiuchumi yanayoambatana na uadilifu wa kijamii.

Maendeleo ya kiuchumi yanayopanua ufa kati ya matabaka ya watu, sio maendeleo yanayokusudiwa na Uislamu. Ule mwongozo wa kiuchumi unaotayarishwa leo hii na nchi za Magharibi na kuwapatia watu duniani, ambao unayafanya baadhi ya matabaka yawe na hali bora ya maisha na ustawi wa kiuchumi, huku ukiyabinya matabaka mengine katika jamii na kuyafanya dhaifu na fakiri, si mwongozo unaokubaliwa na Uislamu. Hali bora ya maisha inayoambatana na uadilifu, inayofungamana na hisia za kuwa na usawa na udugu, hayo pia yanapatikana chini ya kivuli cha Uislamu.

Juu ya ukurasa

Kigezo cha ndani cha Ustawi

Kwa kuzingatia mazingira ya kiutamaduni, kihistoria, kiitikadi, turathi na imani za watu hawa, kigezo cha ustawi wa kiuchumi katika Jamhuri ya Kiislamu, ni kigezo kilichotoka ndani na maalumu kwa taifa la Iran; haifai kuiga popote pale; si kwa Benki ya Dunia wala Mfuko wa Fedha wa Kimataifa, si kwa nchi fulani ya mrengo wa kushoto wala nchi fulani ya mrengo wa kulia; kila mahali pana hali yake maalumu. Kuna tofauti kati ya kutumia tajiriba na uzoefu wa watu wengine, na kufuata vigezo vya kutwishwa na vya kuchochewa, na ambavyo vingi vyao vimeshapitwa na wakati.

Juu ya ukurasa

Maandalizi ya kiutamaduni kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi

Ustawi wa kiuchumi kwa maana yake sahihi katika jamii yetu unahitajia juhudi za kiutamduni. Kama mchunguzi na mtafiti wa kielimu hatokuwa na utamaduni wa kupenda kazi, moyo wa uchapaji kazi na mapenzi ya kazi kwa ile namna inayozungumziwa katika mazingira ya utamaduni safi, kuwepo kwa mtafiti huyo hakutokuwa na faida yoyote.

Ufumbuzi wa matatizo unapatikana kwa kutumia vipimo viwili vya "moyo wa kuthamini kazi" na "nidhamu ya kijamii". "Nidhamu ya kijamii" maana yake ni kuwepo nidhamu maalumu katika mambo yote yanayofanywa na watu wanaoendewa na wananchi. Yaani mlahaka wao na wananchi wanaowaendea uwe ni wa kufuata nidhamu maalumu, na wale watu waliobeba jukumu la kutekeleza kazi fulani wahakikishe nidhamu inatawala katika ufanyaji wa kazi hiyo. Yote hayo ndiyo yatakayoiletea furaha nchi na wananchi na ufanisi wa kazi zao.

Juu ya ukurasa

Propaganda dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu

Uistikbari unafanya propaganda dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Huenda hata isitimie hata wiki bila ya dazeni ya redio na televisheni hizo zilizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kusema kuwa uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu uko katika hali mbaya, unaporomoka na kusambaratika kabisa. Bila shaka ni kweli hayo kwamba una hali mbaya kwao wao. Ama kwa wananchi wa Iran, uchumi wa Iran uko katika hali ya kuchanua kiustawi; lakini kwa wachokozi na watu wanaotaka kufaidika na suhula za Iran kwa faida yao, bila shaka uko katika hali mbaya. Kuna mgogoro na hali mbaya gani kwa wananchi wa Iran? Wao wanashughulika kuijenga nchi yao, nchi ambayo katika zama za utawala wa kifalme- uwe ni ufalme wa Kipahlavi au wa Kiqajar- haikuthubutu kusimama mbele ya nchi nyingine duniani na kusema "mimi pia nipo, mimi pia nina uwezo wa kutengeneza, na nina uwezo wa kuchukua hatua". Ilikuwa ni nchi ya daraja la tatu na la nne inayosalimu amri kikamilifu, kiasi kwamba wakubwa wa nchi hii walikuwa wakiona fakhari kuyanyenyekea madola makubwa, ambapo wakati fulani ilikuwa ni Uingereza, wakati mwingine ikawa ni Marekani, na kuna wakati ilikuwa ni Russia!

Juu ya ukurasa

Hamu ya ustawi, hofu ya ustawi

Kwa kiwango kile kile cha hamu waliyonayo wananchi wa Iran katika kuijenga na kuishughulikia jamii yao na nchi yao, ndivyo maadui walivyo na khofu na ndivyo wanavyochukizwa na jambo hilo. Wao wanaelewa kuwa mafanikio ya taifa la Iran katika kujenga jamii yenye ustawi na iliyojaa neema za kimaada na kimaanwi, yatayashajiisha mataifa mengine kufuata njia ya taifa hilo adhimu, na hii maana yake ni kuvuruga na kufelisha tamaa za kikoloni na kiistikbari za madola makubwa duniani. Na hapo ndipo kinapoanzia kisa kirefu cha Uistikbari, chenye mikasa mingi ya njama, cha kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu. Vita vya kulazimishwa, mzingiro wa kiuchumi, uenezaji uwongo wa mtawalia katika vyombo vya habari duniani vyenye mfungamano na Uistikbari na Uzayuni, kuwaunga mkono wapinzani wa Mapinduzi -kuanzia wale wa mrengo wa kushoto wenye kufurutu mpaka hadi wale wenye kufurutu mpaka wa mrengo wa kulia, wanafiki waliohasirika na mfano wa hao- yote hayo yamefanywa ili kulizuia taifa la Kimapinduzi la Iran lisiweze kufikia kwenye ule mustakbali wenye kung'ara.

Juu ya ukurasa

Wajibu wa matabaka yote

Ikiwa mnataka nchi ya Iran ifikie kwenye ustawi kwa kuwepo hali bora ya huduma za jamii, hali nzuri ya kiuchumi, maendeleo ya pande zote, izza ya kisiasa, usalama wa kijamii, uhakika wa ajira, elimu na maendeleo ya kiutafiti kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine kuwepo umaanawi utakaoing'arisha na kuitia nuru nchi hii, kuna mambo mawili yanayopasa kuzingatiwa. Kuyafanyia kazi mambo mawili haya ni wajibu wa matabaka yote, hasa yale matabaka yenye uelewa. Wafanyabiashara, wakulima, wafanya kazi za ufundi, wafanyakazi za vibarua, wasomi, wahadhiri, watu wa masuala ya kiutamaduni pamoja mashekhe, wote kwa pamoja wanapaswa kuyazingatia mambo mawili haya:

Moja ni kwamba washiriki wote bega kwa bega katika ujenzi wa nchi. Na la pili ni kwamba wafanye jitihada katika kuzijenga nafsi zao.

 و توبوا الى‌اللَّه جميعاً ايّها المؤمنون لعلّكم تفلحون

“Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.”

Kufuzu na kufaulu kunapatikana kwa watu wote kulichukulia suala la kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, kunyenyekea na kutawasali kwa Mwenyezi Mungu kuwa ni njia safi ya kufuata. Hakuna hata moja kati ya mawili hayo linalojitosheleza peke yake.

Juu ya ukurasaa

Umuhimu wa kuwa na moyo wa kujiamini katika ujenzi wa nchi

Suala la mamudiri na viongozi wa nchi kuwa na moyo wa kujiamini ni suala la msingi katika Mapinduzi ya Iran, ambalo kama halitokuwepo misingi ya ujenzi wa nchi itatetereka. Viongozi wote wanaohudumu katika sekta na idara mbalimbali nchini wanapaswa kuzijenga nafsi zao ziwe na moyo wa kujiamini na wawe na imani kwamba Jamhuri ya Kiislamu, taifa la Iran na wale wote wenye mfungamano na nchi hii, wanao uwezo wa kuifikisha nchi kwenye kilele cha ustawi inaoutaka na kuuhitajia. Baadhi ya wakati yamkini baadhi ya viongozi na baadhi ya watu wanaohudumu katika sekta mbalimbali- iwe ni katika nyanja za kiuchumi au nyanja za kiutamaduni na nyinginezo- wakatekwa na baadhi ya upembuzi uliofanywa na watu wengine- hata kama mathalan ni msomi mmoja tu au mwandishi fulani- uliochapishwa kwenye jarida moja la kielimu. Upembuzi huo unaweza kuziteka fikra za watu, kiasi cha kuwafanya wapoteze hali ya kujiamini, na hivyo kughafilika na kuachana na ile mipango inayotokana na uzingatiaji wa hali halisi inayotawala nchini; kwa sababu kila nchi ina hali zinazowiyana na nchi hiyo.

Inapasa zifanyike jitihada ili kuwafanya wanafunzi wa tokea katika ngazi ya skuli hadi hadi Chuo Kikuu pamoja na wale watu ambao ndio kwanza wameanza shughuli za kazi wawe na moyo wa kujiamini na kuimarisha hali hiyo ndani ya nafsi zao, na kuonyesha kwamba inawezekana kutatua masuala ya nchi kwa kutumia uchanganuzi, upembuzi na ufahamu tulionao sisi wenyewe kuhusiana na masuala hayo. Haifai kushughulishwa na yale yaliyoandikwa na mwandishi fulani wa gazeti au yale yanayosemwa na mchambuzi fulani wa nje ya nchi kwamba lazima Iran ifuate njia hii ili iweze kujijenga na kutatua matatizo yake ya kiuchumi. Bila shaka fikra na mitazamo ya kielimu inayobainishwa mahali popote pale duniani na kwa lugha yoyote ile inapasa kuzingatiwa; lakini si kwa sura ya kuikubali kibubusa na bila ya kudadisi, bali ni kuikubali kwa msingi wa mtu kuifanyia upembuzi na uchanganuzi mitazamo hiyo, akailinganisha na kuitabikisha na mazingira tofauti ya nchi yetu, kisha ndipo akaitekeleza.

Juu ya ukurasa

Kasoro za kiuchumi za kipindi cha ujenzi wa nchi

Katika kipindi cha ujenzi wa nchi, kujitokeza baadhi ya kasoro za kiuchumi huwa ni jambo la kawaida. Hivyo ndivyo inavyokuwa kila mahali. Mfumuko wa bei na ughali wa maisha huongezeka, na uwezo wa kununua wa watu wengi hupungua. Kwa hivyo inapasa serikali ifanye juhudi maradufu za kutatua matatizo haya ya kiuchumi kwa maana maalumu ya utatuzi. Suala la mfumuko wa bei linapasa litatuliwe kwa kutumia njia maalumu. Nguvu ya sarafu ya taifa inapasa ihakikishwe inabaki juu kadiri inavyowezekana, kwa kufanya juhudi zaidi, ufatiliaji na kwa kutumia tadbiri zaidi. Bila shaka kazi hizi za msingi hutoa tija na kuonyesha matunda yake baada ya muda kupita; hata hivyo haiwezekani kukaa na kusubiri hadi wakati huo, na kughafilika na utumiaji wa njia za kutibu matatizo yaliyopo, zinazoweza kutoa jibu baada ya kipindi kifupi au cha kati na kati. Hii thamani ya sarafu ya taifa, yenyewe ni ufunguo wa kutatulia matatizo mengi ya nchi, na huu uwezo dhaifu wa kununua walionao wananchi wa matabaka ya chini na kushindwa kudhamini mahitaji yao ya maisha, unatokana na suala hilo.

Juu ya ukurasa

Mabalaa ya kipindi cha ujenzi mpya wa nchi

Katika kipindi cha ujenzi mpya wa nchi, hatari ya kupenda dunia huwa kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Katika kipindi cha ujenzi mpya wa nchi, huwepo mrundiko wa mali; kwa sababu kipindi cha ujenzi mpya ni kipindi cha kurundikana kazi, kipindi cha kurundikana utajiri, kipindi cha kuongezeka shughuli za kiuchumi, na kipindi ambacho kama mtu ataweza kufanya bidii na kujitumbukiza kwenye harakati za kiuchumi, njia huwa iko wazi kwa ajili yake. Katika kipindi kama hiki, wale watu ambao ni wapenda dunia, watu ambao nyoyo zao zimetekwa na mali na mapambo ya dunia, watu ambao huweka mbele manufaa na maslahi yao ya binafsi kuliko manufaa na maslahi ya nchi, taifa na maslahi ya Mapinduzi, huwa na fursa ya kutosha kuweza –Mungu aepushie mbali – kuelekea kwenye maisha ya fakhari, ukusanyaji na urundikaji mali na utajiri na kuzitumia vibaya fursa hizo. Kipindi cha ujenzi mpya wa nchi ni kipindi cha ustawi na maendeleo ya taifa, na ni kipindi cha kuijenga nchi. Lakini wakati huo huo kipindi hicho ni kipindi hatari kwa kuwaelekeza watu dhaifu kwenye maisha ya kifakhari, ukusanyaji na urundikaji mali na utajiri na kuzitumia vibaya fursa za kiuchumi. Kwa hivyo watu wote wajichunge na kujihadhari sana; kuanzia viongozi na wananchi wote kwa jumla.

Juu ya ukurasa

Sura ya Pili: Mambo yenye taathira katika ustawi wa kiuchumi

Kazi

Ubora wa kazi

Inabidi wafanyakazi za vibarua wapewe fursa ya kuweza kutoa mchango wao wa kazi kwa ajili ya kuutumikia mfumo wa utawala na kwa ajili ya harakati na ustawi wa kiuchumi wa wananchi, na kuweza kwa namnna iliyo bora kabisa kufanya kazi ya kuzalisha bidhaa zenye ubora. Imepokelewa kutoka kwa Mtume mtukufu (saw) kwamba amesema

 رحم‌الله امرء عمل عملا فأتقنه

Yaani rehma za Mwenyezi Mungu zinamshukia mtu ambaye huifanya kazi yake kwa namna iliyo bora kabisa. Wafanyakazi za vibarua wanapaswa kufanya kazi zao kwa namna iliyo bora kabisa. Waelewe kwamba malipo ya juhudi wanazofanya, yako kwa Mwenyezi Mungu; bila kujali kama mwajiri huyo wa serikali au asiye wa serikali atajali juhudi zinazofanywa na kibarua au la, na kama atampa malipo yanayolingana na juhudi alizofanya au hatofanya hivyo. Bila shaka anapaswa kujali na kuthamini juhudi zinazofanywa na wafanyakazi za vibarua na kuwapa malipo yao yanayolingan na juhudi wanazofanya. Pamoja na hayo huko kuifanya kazi kwa ufanisi kabisa ndilo jambo linalotakiwa na Mwenyezi Mungu.

Juu ya ukurasaa

Thamani ya kazi katika utamaduni wa Kiislamu

Kazi ni kitu chenye hadhi na daraja ya juu katika mafundisho ya Qur'an na Uislamu. Tab'an kazi si ile tu inayofanywa kiwandani au shambani au katika sekta nyinginezo; lakini kimsingi amali njema iliyotiliwa mkazo ndani ya Qur'an kwa kiwango chote hicho inajumuisha kazi hizo pia. Yaani wakati kibarua anapofanya kazi, kama ataifanya kazi hiyo kwa udhati wa moyo, kwa kujihisi kuwa hilo ni jukumu lake, kwa uzito unaostahiki, kwa juhudi na bidii, kwa nia ya kufanya ubunifu ndani yake na kwa lengo la kupata riziki ya kuendeshea maisha ya aila yake, hiyo yenyewe ni amali njema-

 «الّا الّذين امنوا و عملوا الصّالحات

Ila wale walioamini na kufanya amali njema- amali njema inajumuisha mambo hayo pia; je kuna jambo bora zaidi ya hilo? Kuna jambo bora zaidi kuliko mtu kufanya kazi ambayo pato lake la kuendeshea maisha yake linategemea kazi hiyo; wakati huo huo kazi hiyo hiyo ni amali njema ambayo ndani ya Qur'an imefungamanishwa na kuwekwa kwenye mlingano sawa na imani; yaani

 امنوا و عملوا الصّالحات

yaani walioamini na kufanya amali njema.

Juu ya ukurasaa

Nafasi ya kazi katika ustawi wa kiuchumi

Kazi inapasa kupewa uzito katika suala la ustawi wa kiuchumi; bila kupewa uzito kazi suala hilo halitowezekana. Bila kuwepo uwekezaji kazi hazitopatikana; lakini uwezekezaji wenyewe ni nguzo mojawapo ya kazi; nguzo kuu ni kazi inayofanywa na kibarua. Kazi ambayo haifanywi kwa moyo, kwa ustadi, kwa ufatiliaji na kukubali mazingira yake magumu, haiwezi kuiokoa nchi. Na bila ya kuwa na utendaji kazi wa aina hiyo nchi haiwezi kufika kule inakopaswa kufikia.

Leo taifa la Iran linataka liwe linajitawala na kujitegemea kiuchumi; linataka kuivua nchi na hali ya utegemezi wa mafuta. Leo taifa la Iran linataka hali ya uchumi wa nchi iratibiwe kwa namna ambayo kushuka kwa bei ya mafuta kusiweze kuwa na taathira ndani ya nchi ya Iran. Vipi utekelezaji wa mambo hayo utawezekana? Ikiwa taifa la Iran linataka lijivue na uhitaji na utegemezi wa pato la mafuta, jambo hilo halitowezekana pasina kuimarisha masuala ya kazi na mtazamo juu ya kazi.

Juu ya ukurasa

Mfanyakazi ya kibarua

Utukufu wa mfanyakazi ya kibarua

Inabidi katika utumiaji wetu wa istilahi zilizozoeleka za kidini na kijamii, tuwe tunalipa heshima maalumu neno "kibarua". Mfanyakazi wa kibarua ni mtu mwenye heshima na utukufu. Kibarua ni yule mtu anayefanya kazi ili taifa lake na nchi yake iweze kuwa na izza ya kujitawala. Hili ni suala ambalo watu wote wanapaswa kuliamini kwa dhati. Watu wote waelewe kuwa mfanyakazi ya kibarua ana umuhimu wa kiasi gani. Wafanyakazi za vibarua wanatoa mchango muhimu nchini. Sehemu kubwa ya mzigo wa uzalishaji uko mabegani mwa wafanyakazi za vibarua. Hili jina la "kibarua" linajumuisha watu wote wanaofanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya nchi, kwa ajili ya ustawi wa uzalishaji nchini, na kwa ajili ya kuboresha hali ya kazi nchini.

Hii kwamba katika jamii ya Kiislamu, viongozi wa Kiislamu wanaienzi kazi na kumuenzi na kumheshimu mfanyakazi ya kibarua, hili si suala la maneno matupu; si suala la kusifu tu. Ni kweli kwamba kuna watu duniani ambao yamkini kwa maneno matupu tu wanawapigia kifua wafanyakazi za vibarua; lakini kuna tofauti kati ya mtu anayetaka kutoa nara tupu kwa lengo la kuziteka nyoyo za umati fulani wa watu na yule mtu ambaye anaitakidi kwa dhati kuwa kazi ni amali njema na ni thamani ya kimaanawi na ya kidini. Mantiki ya Uislamu ni hii ya pili; yaani mfanyakazi ya kibarua ni mtu aliyemo kwenye ibada; na kazi yake anayofanya ni ibada.

Juu ya ukurasa

Wajibu wa utawala kwa wafanyakazi za kibarua

Ni hakika kwamba mojawapo ya wajibu ulionao mfumo wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuhakikisha kwamba tabaka hili la watu wanaojituma na kutaabika- ambalo linatoa mchango mkubwa zaidi katika uzalishaji na uendeshaji uchumi wa nchi- wanapata haki zao halali za kiutu na Kiislamu. Lazima hali ya kimaisha ya wafanyakazi za vibarua kwa upande wa kimaada na kimaanawi iboreshwe. Kwa kutekeleza sheria zilizo mujarab na kuongeza kiwango cha ajira inabidi ihakikishwe kuwa hakuna mtu mhitaji na mwenye dhiki katika jamii ya Iran. Wafanyakazi za vibarua ambao ni mojawapo ya matabaka ya wanyonge katika jamii inapasa wapewe kipaumbele katika uandaaji wa mipango ya ustawi wa kiuchumi. Ikiwa mfanyakazi ya kibarua atakidhiwa mahitaji yake kazi itafanyika kwa ubora na ufanisi zaidi.

Juu ya ukurasa

Thamani ya mfanyakazi ya kibarua katika jamii

Uhuru wa kujitawala na kujitegemea wa nchi unafungamana na kazi. Hakuna nchi yoyote na taifa lolote linaloweza kufika popote pale kwa kujipweteka, kwa kutofanya kazi na kutoijali kazi. Inawezekana watu wa taifa hilo wakaweza kujipatia pato lao kupitia njia fulani, na kidhahiri wakaweza kuendesha maisha yao kwa kuingiza bidhaa za kigeni katika nchi yao; lakini taifa hilo halitokuwa na uhuru wa kujitegemea. Izza ya taifa lolote lenye uhuru wa kujitegemea haiwezi kupatikana kwa njia yoyote ile ghairi ya ufanyaji kazi. Hii ndiyo thamani ya kazi. Mfumo wa utawala wa Kiislamu unamwangalia mfanyakazi ya kibarua kwa jicho hilo, na kwa jicho hilo unakuchukulia kuubusu mkono wa mfanyakazi ya kibarua kuwa ni tendo la thawabu. Mtu yeyote anayeubusu mkono wa kibarua amesibu na amefanya tendo sahihi; kwa sababu ameienzi mojawapo ya nyenzo za kulifanya taifa lake na nchi yake iwe na uhuru wa kujitegemea. Kazi ni kitu chenye thamani kiasi hicho.

Juu ya ukurasa

Mfanyakazi ya kibarua katika mantiki ya mfumo wa Kibepari, Kisoshalisti na Kiislamu

Katika mantiki ya nchi za Kibepari, kibarua ni wenzo na chombo cha kumtumikia mwajiri. Mantiki ya zile nadharia zilizosambaratika na kutoweka, zilizokuwa zikidai kuwa mtetezi wa wafanyakazi za vibarua, ni kuwepo vita kati ya mwajiri na kibarua. Ilikuwa ni kutokana na vita hivyo ndiyo tawala hizo zilikuwa zikitaka zijipatie mkate wao kisha wakilipa jina la uteteaji wa vibarua. Wakati ule katika mfumo eti wa Kisoshalisti wa Urusi ya zamani, masuala yale yale ya Kibepari, israfu zile zile, ubadhirifu ule ule wa fedha wa aina mbali mbali ulifanyika kwa kutumia jina la kibarua na kwa jina la kutetea tabaka la vibarua. Mantiki yao ilikuwa mantiki ya mkinzano na mgongano. Uislamu, mfumo wa Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu haikubaliani na yotote ile kati ya njia mbili hizo; inavyoitakidi ni kuwepo mihimili hiyo yote miwili yaani wa uandaaji kazi na kuanzisha soko la ajira na kazi, na vile vile wa kuwepo kwa nguvukazi. Yote miwili hiyo inapasa iwepo na kuwepo ushirikiano baina yao. Nafasi ya serikali ni kuweka mstari wa kati na kati wa kiadilifu kwa ajili ya ushirikiano huo; usitokee upande wowote utakaokiuka haki za upande wa pili. Hali itakapokuwa hivyo jamii itapiga hatua mbele kwa amani na upendo; havitaenea vile vitendo vya israfu na ufujaji, wala haitozoeleka na kuwa utamaduni wa kudumu hali ya tabaka moja kunyongeka kwa ajili ya tabaka jingine. Hii ndiyo mantiki ya mfumo wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Wanawake

Nafasi ya wanawake katika kipindi cha ujenzi mpya wa nchi

Katika kipindi cha kuijenga upya nchi ya Kiislamu- ambapo katika kipindi hiki wananchi na viongozi pia wanajaribu kuijenga upya Iran adhimu kwa namna inayostahiki kimaada, kwa upande wa nidhamu ya kijamii na pia kwa upande wa kimaanawi- rasilimaliwatu ndio mhimili wa kuutegemea zaidi. Yaani ikiwa nchi inataka kujijenga upya kwa maana halisi ya ujenzi mpya inapaswa ihakikishe inazingatia zaidi na inawapa umuhimu zaidi watu na rasilimaliwatu. Tunapozungumzia rasilimaliwatu inatupasa tuelewe kuwa nusu ya idadi ya watu wetu walioko nchini na nusu ya rasilimaliwatu ni wanawake. Ikiwa kutakuwepo mtazamo potofu juu ya mwanamke haitowezekana kutekeleza ujenzi mpya kwa maana yake halisi na kwa upeo wake mpana. Kwa upande mmoja, wanawake wenyewe nchini wanapaswa wawe na uelewa wa kutosha na unaohitajika kuhusiana na suala la mwanamke katika mtazamo wa Uislamu ili kwa kutegemea mtazamo aali wa dini tukufu ya Uislamu waweze kutetea haki zao kikamilifu; na kwa upande mwingine watu wote katika jamii wakiwemo wanaume katika nchi hii ya Kiislamu wanapaswa waelewe Uislamu una mtazamo gani kuhusiana na mwanamke, ushiriki wa mwanamke katika nyanja za maisha, harakati za wanawake, suala la elimu kwa wanawake, ufanyaji kazi na shughuli za kijamii, kiuchumi, kisasa na kielimu wa wanawake, nafasi ya mwanamke katika familia na nafasi ya mwanamke nje ya nyumba na familia.

Kulingana na ulazima unaojitokeza, mwanamke wa Kiislamu, kama alivyo mwanamme wa Kiislamu ana haki ya kutekeleza majukumu pale atakapohisi kuwa kuna uwazi na ikahitajika yeye kutimiza wajibu ulioko mabegani mwake. Kiasi kwamba ikiwa mathalan msichama anapenda awe tabibu, au ajishughulishe na shughuli za kiuchumi, au afanye kazi katika taaluma za kielimu, au afundishe katika Chuo Kikuu au ajitose kwenye shughuli za kisiasa, au awe mwandishi wa habari, mlango uko wazi kwa ajili ya kujishughulisha na kazi hizo. Yaani pale sharti la kuchunga murua, heshima, na kuepusha michanganyiko isiyo na kizuizi baina ya wanaume na wanawake linapozingatiwa, jamii ya Kiislamu imeweka mlango wazi kwa wote wawili mwanamke na mwanamme. Ushahidi wa jambo hilo ni athari zote za Kiislamu zilizopo zinazozungumzia suala hilo, pamoja na faradhi zote za Kiislamu ambazo zinawaweka mwanamke na mwanamme katika hali sawa ya kutekeleza majukumu ya kijamii. Wanawake nao wanapaswa wajihisi kuwa wana jukumu, na wayape umuhimu masuala ya Waislamu, jamii ya Kiislamu, masuala ya ulimwengu wa Kiislamu na masuala yanayojiri ulimwenguni; kwa sababu huo ni wajibu wa Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Shughuli za kiuchumi za wanawake

Kwa mtazamo wa Uislamu, mlango uko wazi kabisa kwa wanawake kujishughulisha na harakati za kielimu, kiuchumi na kisiasa. Ikiwa mtu atataka kutumia mtazamo wa Kiislamu kujengea hoja ili kumnyima mwanamke fursa ya kujishughulisha na masuala ya kielimu, kumbana asijishughulishe na harakati za kiuchumi, au kumzuia asishughulike na harakati za kisiasa na kijamii, atakuwa amekwenda kinyume na hukumu ya Mwenyezi Mungu. Kadiri mahitaji yao na uwezo wao wa kimwili unavyoruhusu, wanawake wanaweza kushiriki katika shughuli na harakati mbali mbali. Wanaweza kujishughulisha na harakati za kiuchumi, kisiasa na kijamii kadiri ya uwezo wao. Sheria tukufu za dini haziwakatazi kufanya hivyo. Tab'an kwa kuwa kimwili mwanamke yuko laini kulinganisha na mwanamme, hivyo kuna mambo kadhaa ya kumzingatia. Kumtwisha kazi nzito mwanamke ni kumfanyia dhulma. Uislamu hailuisii jambo hilo; kama ambavyo haujalikataza pia. Tab'an imenukuliwa kutoka kwa Imam Ali bin Abi Talib (alayhi ssalatu wassalam) kwamba amesema kuwa

 «المرأة ريحانة و ليست بقهرمانة.»

yaani mwanamke ni ua si mtumishi. Qahraman ni mtumishi mwenye kuheshimika. Hivyo anawahutubu wanaume kwamba wanawake ndani ya majumba yenu ni mithili ya ua nyororo ambalo inapasa liengwe engwe kwa hadhari na umakini mkubwa. Mwanamke si mtumishi wako hata uhisi kwamba inapasa umwache afanye kazi nzito. Hili ni suala muhimu.

Juu ya ukurasa

Harakati za kiuchumi za wanawake kwa mtazamo wa sheria za Uislamu

Katika uga wa shughuli za kijamii, unaojumuisha shughuli za kiuchumi, shughuli za kisiasa, shughuli za kijamii kwa maana yake maalumu, shughuli za kielimu, usomaji, usomeshaji, kufanya juhudi katika njia ya Mwenyezi Mungu, na kujishughulisha na harakati katika medani na nyanja zote za maisha, hakuna tofauti yoyote kwa mtazamo wa Uislamu kati ya mwanamke na mwanamme. Kwa mtazamo wa Uislamu, katika harakati zote zinazohusiana na jamii ya mwanadamu na harakati za kimaisha, mwanamke na mwanamme wamepewa ruhusa kwa kiwango sawa ya kujishughulisha na harakati hizo. Bila shaka kuna baadhi ya kazi haziwiyani na hali ya wanawake; kwa sababu maumbile yao ya kimwili hayawiyani na kazi hizo. Kama ambavyo kuna baadhi ya kazi haziwiyani na hali ya wanaume; kwa sababu hazikubaliani na hali zao za kimwili na kiakhlaqi. Nukta hii haina uhusiano wowote na suala kwamba mwanamke anaweza kujishughulisha na harakati za kijamii au la. Mgawanyo wa kazi unafanyika kulingana na suhula, hamu na mazingira yanayolingana na kazi hiyo. Ikiwa mwanamke atakuwa na hamu na shauku ya kufanya kazi anaweza kujishughulisha na harakati mbalimbali za kijamii na masuala yanayohusiana na jamii.

Hii kwamba tusema kuwa, kwa kutumia mtazamo wa Uislamu "tumpige marufuku mwanamke kujishughulisha na harakati za kiuchumi na kijamii," kufanya hivyo ni makosa. Uislamu haujasema kitu kama hicho. Lakini kwa upande mwingine Uislamu haujausia pia kwamba tumlazimishe mwanamke afanye kazi nzito na shughuli ngumu za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kama baadhi ya wanaume wanasema kuwa lazima mwanamke afanye kazi na awe na shughuli ya kumpatia pato lake, hayo ni makosa. Japokuwa hayakinzani na sheria ya dini. Lakini Uislamu hauusii jambo kama hilo.

Mtazamo wa Uislamu ni mtazamo wa kati na kati. Yaani kama mwanamke atakuwa na fursa na wasaa, bila kubanwa na suala la ulezi wa watoto, akawa pia na hamu, shauku na uwezo wa kimwili, na akataka kujishughulisha na harakati za kijamii, kisiasa au kiuchumi hakuna pingamizi yoyote. Ama kumlazimisha na kumwambia kwamba lazima ukubali kufanya kazi, na kila siku ufanye kazi kiwango fulani ili uweze kuwa na mchango wa kutoa katika kukidhi mahitaji ya familia, hilo si sawa. Uislamu haukumtaka mwanamke afanye jambo hilo pia. Hiyo pia ni aina fulani ya kumtwisha na kumlazimisha mwanamke. Mtazamo wa Uislamu ni kwamba haikubaliki kumlazimisha mwanamke ajishughulishe na harakati za kielimu, kiuchumi, kijamii na kisiasa; kama ambavyo haikubaliki pia kumwekea kizuizi katika jambo hilo. Kama wanawake wanataka kujishughulisha na harakati za kijamii na kisiasa, hakuna pingamizi. Tab'an kujishughulisha na harakati za kielimu ni jambo zuri zaidi na linafadhilishwa kulinganisha na harakati nyinginezo.

Juu ya ukurasa

Iktisadi

Nafasi ya Iktisadi katika ustawi wa kiuchumi

Iktisadi maana yake si kutotumia; maana ya Iktisadi ni kutumia kwa usahihi, kutumia katika mahali na wakati unaostahiki, kutoharibu mali, kutumia kwa ufanisi na kwenye kuwa na tija. Israfu katika mali na katika uchumi, ni mtu kutumia mali pasina utumiaji huo kuwa athari na ufanisi. Ni utumiaji usio na maana, ni matumizi ya ovyo, na kwa hakika ni ufujaji wa mali.

Inapasa kuwepo uhusiano katika jamii kati ya uzalishaji na utumiaji; uwepo uhusiano sahihi ambao utakuwa na faida kwa uzalishaji; yaani uzalishaji wa jamii daima uwe na ziada katika kile ulichozalisha kwa ajili matumizi ya jamii. Matumizi ya jamii yatokane na uzalishaji unaofanyika nchini; na ile ziada itumike kwa ajili ya ujenzi na ustawi wa nchi. Katika aya tukufu za Qur'an, imesisitizwa mara kadhaa juu ya kujiepusha na israfu katika masuala ya kiuchumi; na hii ni kutokana na suala hilo. Israfu ina madhara kwa uchumi, na vile vile ina madhara kwa utamaduni. Wakati jamii inaposibiwa na maradhi ya israfu, hali hiyo huwa na taathira hasi pia kwa upande wa kiutamaduni. Kwa hivyo suala la Iktisadi na kujiepusha na israfu si suala la kiuchumi tu; ni suala la kiuchumi na pia ni suala la kijamii, na vile vile ni suala la kiutamaduni; ni suala linalotishia mustakbali wa nchi.

Juu ya ukurasa

Umaanawi

Ulazima wa kuwepo umaanawi pamoja na ustawi wa kiuchumi

Mapinduzi ya Kiislamu yalikuja ili kuliletea taifa la Iran maisha mema. Maisha mema maana yake ni kile kitu ambacho Qur'an inakieleza kwamba: «فلنحيينه حياة" طيبه». Yaani “tutamhuisha maisha mema”. Haya ndiyo matunda na lengo kuu la Mapinduzi haya. Maisha mema maana yake ni taifa kuwa katika hali nzuri kwa upande wa kimaada na maisha ya kila siku, huduma za jamii, usalama, elimu, maarifa, izza ya kisiasa, kujitegemea kiuchumi, na maendeleo ya rasilimali na ya kiuchumi; na vile vile kwa upande wa kimaanawi, watu wanaoishi ndani ya taifa hilo wawe ni watu waumini, wamtambuao Mwenyezi Mungu, wachamungu na waliopambika kwa akhlaqi tukufu za kidini. Hayo ndiyo maisha mema.

Baadhi ya sehemu duniani wana maendeleo ya kiwango fulani ya kiuchumi na huduma bora za kimaada; lakini hawana umaanawi. Wakati umaanawi unapokosekana katika jamii, ustawi wa kiuchumi pia huwa hauna manufaa; hauwezi kuondoa ubaguzi wala kuleta uadilifu wa kijamii; hauwezi kutokomeza njaa wala kuondoa ufisadi. Maendeleo ya kiuchumi hayakamilishi kila kitu katika nchi.

Chukulieni mfano wa taifa la Marekani! Kwa upande wa shughuli za kiuchumi, uzalishaji wao ni wa kiwango cha juu. Wana maendeleo mazuri ya kielimu. Viwanda vyao vinafanya kazi vizuri. Wanasafirisha bidhaa ulimwengu mzima na pato lao la nchi ni zuri; lakini taifa hilo haliwezi kupata manufaa halisi yatokanayo na maendeleo hayo ya kiuchumi; kwa nini? Kwa sababu katika nchi hiyo hakuna usalama na umaanawi. Na ndiyo maana kuna kesi nyingi za kujiua na za uhalifu unaofanywa na vijana; watoto wa kuanzia umri wa miaka kumi na mbili na kumi na tatu wanaanza kujifunza kuua mtu; familia zinasambaratika; mke au mume hajihesabu kuwa ana mwenza. Mke hawezi kujihisi kuwa ana mume, wala mume hawezi kujihisi kuwa ana mke! Huko hakuna familia.

Leo Wamarekani wenyewe wanayasema hayo; majarida yao yanaandika, wanafikra na wanasiasa wao wanaeleza kuwa umaanawi umetoweka katika jamii ya Marekani. Kwa nini? Kwa sababu dini na imani havipo katika jamii hiyo. Ni sawa kwamba kuna neema za kiuchumi kwa kiwango fulani; hata hivyo hizo neema za kiuchumi pia si kwa watu wote. Sehemu kubwa ya pato la nchi hiyo ni maalumu kwa watu fulani, na waliosalia hawanufaiki na pato hilo.

Hii ndiyo ile jamii iliyo na neema za kimaada lakini haina umaanawi. Uislamu hautaki kujenga jamii ya aina hiyo. Uislamu unataka katika jamii uwepo umaada na uwepo umaanawi pia, kuwepo na pesa na ustawi wa jamii na iwepo imani na umaanawi pia, yawepo maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa kiakhlaqi na kimaanawi pia. Haya ndiyo maisha bora ya Uislamu.

Juu ya ukurasa

Udhibiti

Udhibiti wa kiuchumi na kifedha

Maana ya kudhibiti uchumi na rasilimali ni kukabiliana na ufujaji, ubadhirifu na israfu. Ufujaji wa rasilimali, ubadhirifu katika utumiaji na kufurutu mpaka katika matumizi si sifa nzuri asilani. Huo hauitwi ukarimu wala uungwana. Si kitu kingine ila ni "utovu wa udhibiti wa uchumi na rasilimali". Wale watu ambao wanaotumia fedha bila sababu; wanaotumia fedha kupindukia na ambao matumizi yao ni ya kupindukia na yasiyojali rasilimali ya taifa kwa upande wa suhula za kiuchumi, hao ni watu wasio na nidhamu na udhibiti katika utumiaji wa suhula za rasilimali na suhula za kiuchumi. Kwa hivyo hata katika mali za binafsi na mali iliyopatikana kwa njia ya halali, ufujaji na matumizi yasiyo na udhibiti hayafai. Ama wale watu wanaotumia mali za serikali, kwao wao ndiyo haifai zaidi. Wakuu wanaohusika wajihadhari sana na masuala ya utumiaji wa mali za umma; katika masuala yasiyohitaji kupewa kipaumbele- hata kama yanahitajika, lakini yakiwa si mahitaji ya dharura, basi wasitumie mali hizo. Katika hali ambayo kuna mahitaji ya kupewa kipaumbele na mahitaji yasiyohitaji kupewa kipaumbele, wasitumie rasilimali kwa mambo yasiyohitaji kupewa kipaumbele. Katika hali isiyo na haja wala mahitaji ya matumizi, basi kisitumike kitu. Katika hali ambayo kuna mahitaji, lakini mbali ya mahitaji yao yakawepo mahitaji muhimu zaidi, hapo pia rasilimali za fedha zisitumike kwa shida hiyo bali zitumike kwa shida na mahitaji yenye umuhimu zaidi.

Juu ya ukurasa

Mafuta

Ufungaji wa visima vya mafuta

Hamu na matamanio yangu hasa- ambayo bila shaka yamkini yasiweze kuthibiti kwa haraka- ni kuona Iran inafunga mlango wa visima vyake vya mafuta na kujenga uchumi wake kwa kutegemea mazao na bidhaa zisizotokana na mafuta. Yaani tujaalie kwamba nchi ya Iran haina bidhaa iitwayo mafuta. Bila shaka kazi hii yamkini isiweze kutekelezeka hivi karibuni na katika kipindi cha miaka hii. Kwa sababu katika enzi za utawala mbovu na tegemezi wa Kipahlavi maadui wa Iran walifanya uharibifu usiotasawarika, na wakaifanya nchi na taifa la Iran liwe tegemezi kwa mafuta kiasi kwamba isiwe rahisi kujivua na hali hiyo. Hata hivyo lazima ifike siku iwezekane kufanya hivyo, na siku hiyo ni pale taifa la Iran litakapoweza kujitegemea lenyewe kwa kutumia suhula lilizonazo na kutougawa utajiri na rasilimali zake bure bilashi kwa watu wanaotumia kihabithi utajiri wa taifa wa nchi nyingine.

Bahati mbaya jambo hilo haliwezekani kwa sasa. Kutokana na usaliti unaofanywa na baadhi ya nchi zinazozalisha mafuta, wale wanaoshirikiana nao, pamoja na wezi waporaji wa kimataifa, badala ya mafuta kuwa wenzo ulioko mikononi mwa nchi zinazoyazalisha, wa kutumiwa kwa ajili ya kupatia faida au kupatia manufaa ya kisiasa na kiuchumi, leo imekuwa ni kinyume chake, kwani mafuta yamekuwa wenzo ulioko mikononi mwa nchi wanunuzi! Yamekuwa ni sawa na bidhaa iliyododa, hali ya kuwa mafuta ni bidhaa ambayo kama haitopatikana duniani leo hii sehemu zote zitakosa joto na mwangaza, na shughuli za harakati na za kiviwanda zitasimama. Ustaarabu wa sasa wa kiviwanda umesimama juu ya msingi wa mashine. Kama mafuta hayatokuwepo, mashine hizo zitasita kufanya kazi. Mafuta ni yenye umuhimu kiasi hicho.

Juu ya ukurasa

Ulazima wa kutenganisha uchumi wa taifa na pato la mafuta

Ni lazima uchumi wa taifa la Iran utenganishwe na mafuta. Kwa sababu bahati mbaya, leo hii mafuta yamekuwa na mfungamano na siasa za kimataifa, makampuni, waporaji wakubwa, wanyonyaji na Waistikbari. Ukweli ni kwamba mafuta yako kwenye udhibiti wa watu hao. Kila pale wanapotaka hushusha bei yake na kuzidisha au kupunguza uzalishaji wake. Mafuta ni mali ya nchi wazalishaji lakini siasa zake zinapangwa na watu wengine!

Kuwa na uchumi usiotegemea mafuta si jambo linaloweza kufanyika kwa kipindi cha mwaka mmoja, miaka miwili au miaka mitano; ni jambo linalopasa kufanywa taratibu na hatua kwa hatua hadi kuhakikisha kuwa viongozi wa nchi hawalazimiki kuuza mafuta, ambayo ni hazina ya taifa la Iran, kwa ajili ya kufidia gharama za uendeshaji wa masuala ya nchi, utekelezaji wa kazi mbalimbali nchini, uingizaji bidhaa na utoaji huduma nchini, kugharamia elimu na bajeti ya serikali na kwa ajili ya kuagiza ngano na maziwa ya unga! Kufanya hivyo ni makosa; huu ni msingi uliokwenda upogo ulioanzishwa katika zama za utawala wa Kipahlavi. Huu ni mojawapo ya makumi ya usaliti uliofanywa na ufalme wa Kipahlavi! Waliufanya uchumi wa nchi hii tegemezi kwa mafuta kiasi kwamba si rahisi sasa kuirekebisha na kuibadilisha hali hiyo.

Juu ya ukurasa

Uandaaji mipango

Ulazima wa kutenganisha uchumi wa taifa na pato la mafuta

Katika mipango ya kiuchumi ya serikali nukta dhaifu inayoonekana zaidi mbele ya macho ya mtu ni kwamba kuanzia ile lahadha ya hatua ya utangulizi hadi wakati serikali inapotaka iwe imefikia kwenye malengo iliyokusudia, hapa katikati wale wanyonge katika jamii huwa wanakabiliwa na hali ngumu mno; hili ni jambo linalohisika kwa uwazi kabisa. Hadi wakati sera za kiuchumi za serikali zinapozaa matunda na kukaribia kwenye urari wa ugavi na mahitaji, na watu wote kuweza kunufaika na uzalishaji kwa namna sahihi, huenda ukawa umeshajitokeza ufa mkubwa. Katika kipindi chote hicho ni yale matabaka ya wanyonge wenye kipato cha chini ndiyo ya kwanza kuathirika.

Juu ya ukurasa

Uongozi wa uendeshaji

Nafasi ya uongozi wa uwajibikaji katika ustawi wa kiuchumi

Iran ya Kiislamu inao uwezo wa kuleta ustawi wa kiuchumi wenye uwiyano. Hii hali ya baadhi ya watu kudhani kwamba hakuna kinachoweza kufanyika, haiwezekani kupata maendeleo na haiwezekani kutatua matatizo yaliyopo, inatokana na makosa ya uoni na udhaifu wa nafsi. Ikiwa kutakuwa na uongozi wenye uchungu wa nchi na ufanisi wa utendaji, wenye hisia za uwajibikaji na unaotumia vipawa na ubunifu wa watu, tutamudu kuondoa vikwazo vyote vilivyopo. Kila mahali ambapo pamekuwa na uongozi wenye kuwajibika, wa watu waumini na wenye uchungu na nchi na ambao ulifanya kazi kwa hekima, busara, imani na uwajibikaji kwa wananchi na mfumo wa Kiislamu, basi Jamhuri ya Kiislamu ilipata mafanikio. Kutokana na uongozi wenye ufanisi wa kiutendaji, Iran iliweza kupiga hatua kwa kiwango cha kuridhisha katika uga wa mojawapo ya fani ngumu kabisa za kiufundi ambayo kuna wakati wataalamu wa ufundi wa nchi hii hawakuwa hata wakiiwaza akilini mwao. Watu wengi wa nje wakiwemo maadui na washindani wetu, hawako tayari hata kuukubali ukweli huo; lakini hatimaye watalazimika kuukubali kwa sababu athari zake zinashuhudiwa kila upande. Iran ilikuwa wapi na iko wapi hivi sasa katika sekta ya utaalamu wa kiulinzi? Katika kipindi cha vita Iran ilikuwa na matatizo ya uundaji hata zana za kawaida kabisa za kijeshi kwa ajili ya nchi hii; lakini leo hii baadhi ya zana ngumu kabisa kiuundaji -ambazo hazipatikani katika nchi nyingi ambazo zilikuwa zimeitangulia sana nchi hii katika utaalamu wa ufundi- zinaundwa na vijana hawa hawa wawajibikaji, na mamudiri wenye uchungu na nchi walioko katika sekta za ulinzi nchini. Uwezo wa kiufundi hauhodhiwi na sekta fulani tu. Ikiwa kutakuwepo vipawa na uwezo sehemu fulani suala hilo linaweza kujumuisha sekta nzima ya ufundi. Inaweza kufanyika hivyo pia katika sekta nyingine za uzalishaji. Makumi ya mabwawa yamejengwa katika nchi hii. Mwanzoni mwa Mapinduzi, moja kati ya mabwawa lilikuwa likivuja. Wakati ule baadhi ya watu walikutana na kutangaza kuwa: itabidi tuwaite wahandisi wale wale waliolijenga bwawa hilo kutoka nchi fulani ya Ulaya ili waje kuziba na kuzuia uvujaji wa maji uliopo katika bwawa hili. Lakini tunaona katika kipindi cha miaka hii kadhaa, rasilimaliwatu ya vijana waumini na wawajibikaji, na mamudiri hawa hawa wa Iran wenye uchungu na nchi wameweza kujenga mabwawa kadhaa. Katika sekta ya biashara na sekta nyinginezo za utoaji huduma, na vile vile katika sekta ya viwanda, madini na kilimo, inapasa hatamu za uongozi wa masuala ziwe mikononi mwa uongozi wenye kuwajibika na wenye uchungu na nchi. Hima, uwajibikaji, kuwa na imani kwa mfumo wa Kiislamu na kuwa na khofu ya kuulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu ni mambo ya lazima kuwa nayo mudiri na kiongozi ili mafanikio hayo yaweze kupatikana.

Juu ya ukurasa

Moyo wa kujiamini

Umuhimu wa kuwa na moyo wa kujiamini katika ujenzi wa nchi

Suala la mamudiri na viongozi wa nchi kuwa na moyo wa kujiamini ni suala la msingi katika Mapinduzi ya Iran, ambalo kama halitokuwepo misingi ya ujenzi wa nchi itatetereka. Viongozi wote wanaohudumu katika sekta na idara mbalimbali nchini wanapaswa kuzijenga nafsi zao ziwe na moyo wa kujiamini na wawe na imani kwamba Jamhuri ya Kiislamu, taifa la Iran na wale wote wenye mfungamano na nchi hii wanao uwezo wa kuifikisha nchi kwenye kilele cha ustawi inaoutaka na inaouhitajia. Leo hii bwawa kubwa kabisa katika eneo, ambalo ni bwawa la Kyarkhe limejengwa na vijana wa jeshi la walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Miaka kadhaa iliyopita wakati walipokuwa wakijenga bwawa la Kyarkhe, nilikwenda kulikagua, nikakuta juu ya mlima mkabala na bwawa wameandika kwa maandishi makubwa yaliyoweza kusomeka kutoka umbali wa kilomita kadhaa, maneno ya mwongozo wa Imam Khomeini (m.a) aliposema "tunaweza". Ni kweli kabisa, tunaweza!

Juu ya ukurasa

Mageuzi

Umuhimu wa mageuzi katika ustawi wa kiuchumi

Mageuzi ni suala muhimu na la lazima na ambalo inapasa lifanyike katika nchi ya Iran. Mageuzi ni sehemu ya dhati ya utambulisho wa Kimapinduzi na wa Kidini wa mfumo wa utawala wa Iran. Ikiwa hayatofanyika maguezi ya kina na ya mara kwa mara, mfumo utaharibika na kukengeuka mkondo sahihi. Mageuzi ni jambo la wajibu. Asili ya mageuzi ni kitu cha lazima na inapasa yafanyike. Yasipofanyika mageuzi ugawanyaji wa utajiri unakuwa si wa kiadilifu; huzuka watafutaji utajiri wa haraka haraka na wasio na huruma ambao hudhibiti sekta hii na ile ya mfumo wa kiuchumi wa jamii; ufakiri huenea; maisha huwa ya tabu na shida; maliasili za nchi huwa hazitumiki vizuri; wasomi na wenye vipawa hutoroka, na wale wanaobaki huwa hawatumiki ipasavyo. Lakini wakati yanapofanyika mageuzi madhara haya na athari hizi mbaya na nyinginezo mfano wa hizi huwa hazitokei.

Juu ya ukurasa

Sekta ya Viwanda

Nafasi ya viwanda na ufundi katika ustawi wa kiuchumi

Sekta ya viwanda ndicho kikosi cha mstari wa mbele katika harakati ya ustawi wa kiuchumi nchini. Sekta ya viwanda inapasa iendelezwe kwa kutumia tadbiri, uongozi na kwa kutoa suhula na fursa kwa mitaji ya wananchi ili waweze kuwekeza katika sekta ya uwekezaji vitega uchumi. Ufisadi wa rasilimali na wa kiuchumi ndani ya taasisi za viongozi wenye majukumu na baina yao wenyewe, husambaa hadi ndani ya mfumo wa uchumi wa nchi; kwa hivyo inapasa zichukuliwe hatua za kukabiliana nao. Vita hivi inapasa vipewe uzito unaostahiki. Hii ndiyo njia ya kujenga hisia za kuwepo dhamana na usalama kwa uwekezeaji salama wa vitega uchumi. Yeye mwekezaji hana nia ya kulitumia vibaya suala la uwekezaji, ana nia ya kulitumia kwa nia njema. Bila shaka kila mtu anayewekeza, anafanya hivyo ili kupata faida kupitia uwekezaji wake huo; na hilo halina ubaya; faida ni kitu cha halali. Inabidi itafautishwe kati ya faida halali na isiyo halali. Inapasa zichukuliwe hatua za kuzuia upataji wa faida haramu ambayo kwa sehemu kubwa hutokana na kutokuwepo uwajibikaji na kutokuwa na uchungu na nchi, na vile vile uyumbaji wa aina mbali mbali wa baadhi ya viongozi na mamudiri. Aidha tatizo la magendo inapasa lipigwe vita kwa maana ya halisi ya vita dhidi ya tatizo hilo.

Juu ya ukurasa

Umoja wa kitaifa

Umoja wa kitaifa, sharti la ustawi wa kiuchumi

Kama taifa litajitosa kwenye uwanja wa uchumi likiwa na umoja na mshikamano, hupata maendeleo. Hata kama litakabiliwa na vita na likalazimika kuingia vitani litaweza kupata maendeleo pia. Kwa kuwepo umoja wa kitaifa, heshima ya taifa huweza kulindwa kwa namna bora zaidi. Taifa huweza kufikia malengo yake yote matukufu chini ya kivuli cha umoja wa kitaifa. Hitilafu, mifarakano, utengano wa nyoyo, kukabiliana mrengo huu na ule, makundi haya na yale, na shakhsiya hawa na wale hakuwezi kujenga wala kusaidia chochote.

Juu ya ukurasa

 
< Nyuma   Mbele >

^