Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kujitegemea Kiuchumi na Kukabiliana na Vikwazo vya Kiuchumi Chapa
07/11/2009

Faslu ya Kwanza: Kujitegemea Kiuchumi

Maana ya Kujitegemea Kiuchumi
Umuhimu wa Kujitegemea Kiiktisadi
Utangulizi wa Kujitegemea Kiuchumi
Faida za Uwekezaji wa Kiutamaduni katika Suala la Kujitegemea Kiuchumi
Masharti ya Kujitegemea Kuichumi
Ubeberu wa Kiuchumi
Nafasi ya Uchumi Imara katika Uhuru wa Kisiasa na Kiutamaduni

Faslu ya Pili: Vikwazo na Kususiwa Kiuchumi

Maendeleo Ndani ya Kususiwa Kiiktisadi
Athari za Vikwazo vya Kiuchumi katika Maendeleo ya Kiiktisadi
Upinzani dhidi ya Maendeleo na Ustawi wa Iran

Kujitegemea Kiuchumi na Kukabiliana na Vikwazo vya Kiuchumi


Faslu ya Kwanza: Kujitegemea Kiuchumi

Maana ya Kujitegemea Kiuchumi

Kujitegemea kiuchumi maana yake ni kwa taifa na nchi kujitegemea yenyewe kiuchumi kwa juhudi na bidii zake na kutomuhitajia mtu mwengine katika muktadha huo. Hilo halina maana kwamba madhali taifa linajitegemea kiuchumi, basi halipaswi kushirikiana na mtu yeyote yule kibiashara; hapana. Kushirikiana kiuchumi na watu wengine hakuna maana kuwa mtu ni dhaifu. Kununua kitu, kuuza kitu, kuamiliana kibiashara, kufanya mazungumzo ya kibiashara, yote hayo hayana maana kwamba anayeyafanya ni dhaifu. Lakini utendaji wa mambo hayo unapaswa kuwa kwa namna ambayo kwanza taifa litaweza kujidhaminia mahitaji yake muhimu, pili iweko mizani na mlingano sawa wa kiuchumi duniani na katika miamala ya kimataifa. Isiwe wepesi kwa wengine kumtelekeza kirahisi mtu huyo. Isiwe sahali kwao kumsusia, na wasiweze kumpigisha magoti ikawa tena kila wanachotaka wanamnywesha na yeye anapokea kirahisi na kidhalili. Inasikitisha kuona kwamba leo hii nchi zilizoendelea kiuchumi na zenye nguvu za kiuchumi ndizo hizo hizo zinazoendesha siasa za kikoloni na kibeberu ulimwenguni. Wakati wowote nchi hizo za kikoloni na kibeberu zinapoamua kubadilishana bidhaa na nchi nyingine na kufanya nayo muamala wa kibiashara, lazima zitaiburuza na kuilazimisha kufanya mambo isiyoyaridhia na yasiyo na manufaa kwa wananchi wake. Kujitegemea kiuchumi nchi fulani maana yake ni nchi hiyo kuweza kujidhaminia inachokitaka ndani ya nchi hiyo. Viwanda vyote vya nchi vifanye kazi ipasavyo, wafanyakazi wa nchi hiyo nao wahesabu kazi zao kuwa ni dhamana na jukumu la kibinaadamu, kidini na la dhati ya nafsi zao. Mfanyakazi si lazima awe ni mfanyakazi wa shirika na kiwanda fulani, bali mtu yeyote anayefanya kazi yenye kulinufaisha taifa huyo ni mfanyakazi. Mwandishi, msanii, mwalimu, mvumbuzi, muhakiki, wote hao ni wafanyakazi.

Juu ya ukurasa

Umuhimu wa Kujitegemea Kiiktisadi

Jambo lililo muhimu zaidi ya uhuru wa kisiasa ni kujitegemea kiuchumi. Viongozi nchini, Wabunge na wahusika wote wa masuala ya kiiktisadi inawabidi kutilia maanani kwamba wanapaswa kuacha kuwa tegemezi katika nyanja zote zinazohusiana na masuala ya uchumi, katika masuala ya miundombinu ya iktisadi na katika uga wa shughuli zote za kiuchumi.

Suala la kujitegemea kiiktisadi lina umuhimu wa hali ya juu sana kwa kila nchi. Wakati sekta ya kiuchumi ya nchi fulani inapokuwa mikononi mwa wageni na watu baki, maana yake ni kuwa mshipa wa uhai na lishe wa nchi hiyo uko mikononi mwa wengine na hakuna siku itaacha kuwa tegemezi.

Nchi nyingi za kimapinduzi katika karne ya hivi karibuni zilimili na kujiegemea kwenye kambi ya Mashariki. Nchi hizo zilijiegemeza kikamilifu kwa madola ya Mashariki. Kwa mfano wakati Uchina ilipofanya mapinduzi, katika kipindi cha miaka 10 na zaidi ya mapinduzi yake, Umoja wa Kisovieti ambao ulihesabiwa kama kaka wa nchi ya Uchina na ambao ulitoa mchango mkubwa wa kufanikiwa mapinduzi ya Wasoshalisti huko Uchina, uliisaidia sana kiuchumi na kiutaalamu nchi hiyo na daima ilikuwa inatuma wataalamu wa wasomi wake nchini Uchina. Nchi zilizosalia za kikomunisti nazo zilikuwa vivyo hivyo. Lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitegemea na inaendelea kutegemea tu nia na azma thabiti ya wananchi wake pamoja na vipawa vya aina yake vya wananchi wake katika jitihada zake za kujitoa kwenye utegemezi wa kiiktisadi.

Juu ya ukurasa

Utangulizi wa Kujitegemea Kiuchumi

Nchi zinazoamu kwamba inabidi zifikie kwenye daraja ya kujitegemea kiuchumi, hatua ya kwanza zinayochukua ni kuwa na mfumo wa utawala ulio huru kisiasa, yaani kuwa na utawala huru ambao hautoi mwanya wa kupenya ushawishi wa madola ya kibeberu ndani yake. Haitosheki na hapo bali huanza kupiga hatua pia kuelekea kwenye kujitegemea kiuchumi. Uhuru wa kiiktisadi ni mgumu zaidi ikilandanishwa na uhuru wa kisiasa na kwamba istikilali hiyo ya kiiktisadi inachelewa zaidi kupatikana ikilinganishwa na uhuria wa kisiasa. Wenyewe mnaona kwamba si jambo sahili kukata mizizi ya ushawishi na ubeberu wa kiuchumi wa madola makubwa na serikali zao za kiistakbari. Wakati nchi inapoamua kujitegemea kiuchumi, inahitajia kuwa na nguvukazi imara, vyanzo madhubuti vya kuzalisha mapato, suhula nyingi za aina kwa aina, elimu, utaalamu, ushirikiano wa kimataifa wa kisayansi na kiteknolojia na vitu vingine vingi vya anuwai kwa anuwai. Tumeshuhudia nchi za kimapinduzi na nchi ambazo ndio kwanza zimepata uhuru zikipata matatizo sana katika juhudi za kujiandalia utangulizi na zana zinazohitajika kwa ajili ya kuwa na uchumi huru na istikilali ya kiuchumi.

Nchi huru zinapaswa kuingia katika uga wa kujiimarisha kiviwanda na uzalishaji wa bidhaa. Ziweze kuingiza nchini mahitaji yake kwa kujua ni vitu gani vilivyo na maslahi kwake na izalishe vitu kulingana na vyanzo na suhula ilizo nazo. Inapaswa ipige hatua pia kuelekea kwenye uhuru na kujitegemea kikamilifu kiiktisadi kwa kutegemea juhudi zake na kwa nguvu za uongozi na uendeshaji wake wa mambo pamoja na mshikamano wa wananchi katika suala zima la kupigania uhuru na kujitegemea na kuzielewa vyema njama na mbinu za kipropaganda za maadui.

Juu ya ukurasa

Faida za Uwekezaji wa Kiutamaduni katika Suala la Kujitegemea Kiuchumi

Nguvukazi ni muhimu na ndiyo inayofanya kila kitu katika kila nchi. Kama nchi haina nguvukazi basi nchi hiyo haina kitu. Baadhi ya nchi ambazo zilifanya mapinduzi miaka mingi nyuma kabla ya Iran na kupata mafanikio mbalimbali katika masuala ya kiuchumi, kiviwanda, kiufundi na mithili ya hayo, awali ya mapinduzi yao, nchi hizo zilitegemea mno na kuwekeza sana kwenye suala la kulea nguvukazi kiasi kwamba baadhi ya nchi hizo leo hii zina uwezo wa kusafirisha nje nguvukazi zao mahiri. Hii haina maana kwamba nchi hizo hazina haja na nguvukazi hizo, hapana, bali nchi hizo zinatumia nguvukazi zao hizo kwa namna nyingine ya kujiletea maendeleo. Hali ya kiuchumi ya nchi hiyo iko kwa namna ambayo haiwezi kuwatumia inavyopasa wataalamu wake wote ilio nao, hivyo inastafidi na wataalamu wake hao kupitia kuwasafirisha nje ya nchi ili wakafanye kazi katika nchi nyingine. Licha ya kwamba nchi hizo hazina kipato kikubwa kama cha mafuta na kadhalika, lakini zinapata mafanikio mengi kutokana na kusafirisha nje nguvukazi yao.

Wakati leo hii tunapoona bajeti yetu ya fedha za kigeni au ya Riyali inaelekezwa upande wa kazi za kiutamaduni, inabidi tujuwe vyema kwamba, ijapokuwa katika kipindi kifupi bajeti hiyo haiwezi kuwa na faida kwa uchumi na mzunguko wa kiiktisadi nchini, lakini muda si mrefu utafika na matunda ya uwekezaji huo yatailetea manufaa nchi yetu. Kama kutakuwa na fikra sahihi na mipangilio mizuri, basi jambo hilo litakuwa ni kwa manufaa ya kiuchumi ya taifa. Yaani kama bajeti na suhula zaidi zitatumiwa katika kazi za kiutamaduni – hususan utamaduni wa elimu – basi nchi haitapata hasara kwani jambo hilo lenyewe ni aina fulani ya kulizalishia suhula taifa katika siku za usoni.

Juu ya ukurasa

Masharti ya Kujitegemea Kuichumi

Mosi ni kwamba kila mtu aliye na jukumu lolote nchini, inabidi afanye kazi zake vizuri sana. Imam Ali AS amesema:

 رحم الله امرء عمل عملا فاتقنه

Mwenyezi Mungu amrehemu mtu ambaye anafanya jambo kwa umakini wa hali ya juu. Yaani anaposhika kazi huifanya kwa bidii na umakini wa hali ya juu. Inabidi juhudi zifanyike kuhakikisha kwamba kazi inayotendeka inafanywa kwa usahihi na ukamilifu, kwa bidii na kutodharauliwa chochote. Hilo ni moja ya masharti ambayo kama litatimia, huweza kupatikana uhuru na istikilali ya kiuchumi.

Pili: (Kuwa wabunifu na wagunduzi) katika mazingira ya kazi na kufanya juhudi za kiuchumi kwa ajili ya nchi. Hivyo ni jambo la dharua kuwa wabunifu katika uchumi. Ni jambo zuri mno kwa viwanda vinavyomilikiwa na serikali na vile vinavyomilikiwa na watu binafsi kutenga sehemu japo ndogo ya mapato yao kwa ajili ya utafiti na kwa ajili ya kusukuma mbele uzalishaji ahasani na kuleta ubora wa bidhaa zinazozalishwa na viwanda hivyo. Kwa nini nchi zinazoendelea zikae zifunge mikono na kusubiri nchi za Ulaya au kutoka pembe nyingine ya dunia zifanye kitu halafu nchi zinazoendelea zifuate tu. Inabidi viwanda vya nchi hizo vifanye utafiti, inabidi viwe na ubunifu, visukume mbele gurudumu la uzalishaji aali, viwanda vipige hatua zaidi na ubora wa bidhaa na wingi wake nao uongezeke.

Tatu: Vituo vya kielimu vya nchi visaidie katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi. Wanafikra katika Vyuo Vikuu wajitokeze kuitumikia serikali. Serikali nayo iwatumie vyema wanafikra na wasomi wa Vyuo Vikuu. Wala wasiwe na mawazo kwamba madhali jambo fulani limefanyiwa utafiti na msomi fulani wa Ulaya au limesemwa na mwanafikra wa Ulaya basi daima ndilo hilo hilo tu. Tusisahau kwamba wasomi na wanafikra hao wa Ulaya wanaweza kusema kitu fulani hivi sasa lakini baada ya kupita miaka 20 au miaka 10 au miaka mitano mingine, akatokezea msomi mwingine na akabatilisha kikamilifu maneno ya wasomi hao. Kwa nini basi tuwe tunapokea chochote tu kinachosemwa na Wamagharibi bila ya masharti wala kutaamali wanayoyasema?! Mnapaswa kuchunguza maneno yao, yaliyo sawa myachukue na yaliyo batili muyaache. Wanauchumi wa nchi yoyote ile wanapaswa wafanye uchunguzi na kupata kile kinachokubaliana na hali ya nchi yao, itikadi zao, sifa maalumu za taifa lao na kile kinachooana na masuala ya kiuchumi ya nchi yao.

Juu ya ukurasa

Ubeberu wa Kiuchumi

Nchi zilizo chini ya uistikbari na ubeberu kamwe haziwezi kuwa na uchumi sahihi uliosimama kwenye misingi na mipangilio mizuri. Baadhi ya wakati zinaweza kuonekana kwamba zimenawiri kiuchumi kwa kiasi fulani kama tunavyoshuhudia katika baadhi ya nchi zilizo chini ya ubeberu, lakini ukweli wa mambo ni kuwa miundombinu yake ya kiuchumi ni mibovu kwa maana kwamba kama zitabanwa kidogo tu basi uchumi wote huporomoka na kuangamia kabisa. Mfano wa wazi ni kuwa bepari mmoja tu aliweza kuzifilisi nchi kadhaa za kusini mashariki mwa Asia kwa kipindi cha miezi miwili mitatu tu tena si nchi moja, bali nchi mbili au tatu hivi ambazo uchumi wake kwa kiasi fulani ulikuwa mzuri na umestawi. Rais wa moja ya nchi hizo alikuja Tehran kwa mnasaba fulani na alipokuja kuonana na mimi alisema inatosha kukwambia kwamba katika kipindi cha usiku mmoja tu nchi yetu yote imekuwa maskini! Akasema bepari mmoja wa Kimarekani – bepari wa Kiyahudi amefanya kama vile mtu aliyevuta kamba iliyofungwa kwenye kijumba cha mtoto wa sanamu alipoivuta tu kamba hiyo mambo yote yalivurugika. Hapo Wamarekani wakaamua kusaidia pale walipotaka kwa kupenyeza dola bilioni 50 au sitini hivi – wakapenyeza hapa bilioni 50, pale bilioni 30 na kule bilioni 20 - na pale ambapo hawakupataka na waliona hapana manufaa kwao hawakuingiza chochote na hivyo kuiweka kwenye mazingira magumu sana nchi hiyo. Tab'an tunaposema kwamba waliingiza pesa katika baadhi ya sekta za kiuchumi za nchi hiyo haina maana kwamba Wamarekani walikusudia kuufufua uchumi wa nchi hiyo, bali walipenyeza fedha hizo kwa kiasi ambacho watahakikisha kuwa uchumi wa nchi hiyo unaendelea kuwa kama kijumba cha mtoto wa sanamu, watakapoamua wakati wowote kuvuta tena kamba waweze kuvuruga kila kitu mara moja. Kwa ufupi ni kuwa madola ya kibeberu hayawezi kuruhusu uchumi wa nchi hiyo uwe makini na madhubuti!

Juu ya ukurasa

Nafasi ya Uchumi Imara katika Uhuru wa Kisiasa na Kiutamaduni

Mapinduzi ya Kiislamu yameliletea taifa la Iran uhuru wa kisiasa na kulipa nguvu na ari taifa hilo ya kusimama kidete kukabiliana na mfumo usio wa kiadilifu wa kibeberu duniani. Lakini kama taifa hili linataka kuulinda uhuru wake wa kisisa na kuupa kinga katika istikama na mapambano na mabeberu duniani, linapaswa kuimarisha misingi yake ya kiiktisadi. Misingi ya istikilali ya kiuchumi tayari tunayo humu nchini nayo inategemea uzalishaji, kufanyakazi bila kuchoka, ubunifu na ugunduzi katika sekta zote. Mambo hayo yanatakiwa yashuhudiwe kuanzia kwenye vituo vya utafiti na maabara hadi katika mazingira ya wafanyakazi viwandani, wakulima mashambani, wafanyakazi maofisini na katika sehemu zote. Ni baada ya kutendeka hilo ndipo maadui wenye chuki na uadui mkubwa na uhuru wa taifa la Iran watakaposhindwa kufanya lolote na kulazimika kufumba midomo yao na kubakia kuangalia kwa macho tu.

Juu ya ukurasa

Faslu ya Pili: Vikwazo na Kususiwa Kiuchumi

Maendeleo Ndani ya Kususiwa Kiiktisadi

Maendeleo yote ya Mapinduzi ya Kiislamu yamepatikana katika wakati ambapo maadui wa Iran – yaani Marekani na waitifaki wa Marekani – walipokuwa wanaitishia mtawalia Iran katika masuala ya kisiasa, ya kiuchumi na mengineyo. Daima wamekuwa wakiitishia Iran kwamba wataiwekea vikwazo vya kiuchumi. Maisha wamekuwa wakisema nyinyi mtakuwa kwa njaa. Azali wamekuwa wakitutisha kwamba njia ya maendeleo nchini mwetu itafungwa. Wamekuwa wakitoa makumi ya vitisho hivi na vile. Lakini Alhamdulillah maendeleo yote haya iliyo nayo Iran ya Kiislamu hivi sasa, yamepatikana licha ya kuweko vitisho vyote hivyo na juu ya kuweko uadui na mashinikizo yao ya kila namna.

Juu ya ukurasa

Athari za Vikwazo vya Kiuchumi katika Maendeleo ya Kiiktisadi

Tangu wakati vilipoanza vita (vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran wakati wa utawala wa Saddam Hussein) hadi hivi sasa, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umepiga hatua kubwa sana za kimaendeleo. Wanaitishia Iran kwamba wataiwekea vikwazo vya kiuchumi na kuisusia kiiktisadi! Lakini ni katika kipindi hicho cha kususiwa kiuchumi ndipo nchi hii ilipoweza kupiga hatua zote hizi za kimaendeleo. Vikwazo vya kiuchumi huitia ari nguvukazi ya waumini wenye ikhlasi na walio na vipaji mbalimbali ndani ya nchi na kuifanya nguvukazi hiyo iongeze juhudi za kulikwamua taifa lao. Ni katika kipindi kigumu zaidi cha kuwekewa vikwazo vya kiuchumi ndipo vijana wa Kiirani walipofanikiwa kutengeneza silaha ambazo hakuna nchi yoyote nyingine duniani iliyo nazo ukitoa Wamarekani na nchi mbili tatu nyingine duniani. Mfano mmoja ni haya makombora ya TOW ya kupigia vifaru ambayo vijana wa Kiirani wamefanikiwa kuyatengeneza katika mazingira magumu kabisa. Milango yote ilikuwa imefungwa lakini pamoja na hayo wameweza kutengeneza silaha kama hizo za kisasa. Tab'an maudhui ya nishati ya nyuklia imepata umaarufu zaidi kutokana na unyeti wa teknolojia hiyo duniani, lakini kuna kazi nyingine kubwa kama hizo zilizofanywa na vijana wa Kiirani ambazo umuhimu wake ni kama wa teknolojia ya nyuklia. Maendeleo na mafanikio yote hayo yamepatikana huku Iran ikiwa imesusiwa kiuchumi na ikiwa chini ya mashinikizo ya kisiasa na kiiktisadi. Pamoja na kwamba baadhi ya nchi zilikuwa na uhusiano wa kiuchumi na Iran lakini hazikuwa na nia njema na zilikuwa zinafanya kila njia kulikwamisha taifa hili. Pamoja na hayo vijana wa Kiirani wamefanikiwa kuliletea taifa lao maendeleo yote hayo. Baadhi ya wakati inabidi kushukuru kuona Iran imefungiwa milango katika baadhi ya sehemu kwani hilo huwatia ari vijana wake ya kufanya kazi kwa bidii zaidi. Kama milango yote itakuwa wazi basi ile sifa ya kupuuza mambo, usiri na uvivu aliyo nayo mwanaadamu hupata nguvu na kumzuia kufika popote. Shime na idili ya hali ya juu inahitajika kuweza kumuhamasisha mtu kufanya juhudi za kutenda kazi ipasavyo. Wale watu ambao daima wanakuja na vitu vipya wanafanikiwa kufanya hiyo kwa sababu mwenendo wao wa kielimu unawashajiisha kufanya hivyo na kiujumla unawawepeseshea na kuwasahilishia kazi. Fauka ya hayo watu hao ni wakoloni, wana pesa na wanaidhibiti dunia. Leo hii Wamagharibi wanaiburuza dunia kutokana na uwezo wao wa kielimu. Basi wana sababu yao ya kutilia mkazo elimu. Hivyo nchi zilizofanywa kubaki nyuma kielimu nazo zinapaswa ziwe na ari na zitie nia ya kweli ya kujikwamua na kujiletea maendeleo. Moja ya mambo yanayoweza kutia ari na ghera ni huko kufungwa milango katika baadhi ya mambo.

Juu ya ukurasa

Upinzani dhidi ya Maendeleo na Ustawi wa Iran

Kambi ya mabepari na wakoloni inatumia mabavu yake yote ya kisiasa na mbinde zake zote za kifedha na kiuchumi na mabanda yake yote ya kipropaganda ili kulishinikiza taifa la Iran kwa nia ya kulilazimisha lirudi nyuma na lisalimu amri. Mashinikizo hayo hayako dhidi ya haki ya Iran ya kustafidi na teknolojia ya nyuklia tu. Haki ya kuwa na teknolojia ya nyuklia ni moja kati ya haki nyingi za Iran. Bali wanachotaka wakoloni na mabepari hao ni kulilazimisha taifa la Iran lipuuze na liache kupigania haki ya heshima yake, haki ya uhuru wake, haki yake ya kujiamulia yenyewe mambo yake na haki yake ya kujiletea maendeleo ya kielimu. Hivi sasa taifa la Iran liko katika jia pana la maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia na linataka kufidia karne mbili ambazo ndani yake lilibakishwa nyuma kimaendeleo wakati wa tawala za mataghuti nchini Iran. Hivi sasa maadui hao wa Iran wamechanganyikiwa na wanaumia wanapoliona taifa la Iran - ambalo liko katika eneo nyeti kama hili duniani na linajulikana kwamba limebeba bendera ya Uislamu – linapiga hatua za kimaendeleo na ndio maana wanaliwekea mashikizo haya na yale. Lakini taifa la Iran limesimama kidete kukabiliana nao!

Juu ya ukurasa

 
< Nyuma   Mbele >

^