Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Ukristo Katika Miongozo ya Ayatullah Udhma Khamenei Chapa
16/11/2009

Mlango wa Kwanza:  Nabii Isa Masihi (AS)

Mtume Mkubwa wa Mwenyezi Mungu
Nabii Isa (Amani Iwe Juu Yake) Mtume Mkubwa wa Mwenyezi Mungu
Maryam Ruwaza Njema kwa Wanadamu
Bibi Maryam Dhihirisho la Usafi
Sifa Maalumu ya Kisa cha Isa bin Maryam (AS)
Mshika Bendera ya Hidaya
Mkombozi wa Watu kutoka katika Dhulma
Mlinganiaji wa Bahati Njema
Kuzaliwa Mtukufu Isa Masiya (AS)

Mlango wa Pili: Uislamu na Uksristo

Kutambuliwa Haki ya Mtume wa Uislamu na Mtawala wa Kikristo
Ibada Zinazofanana kati ya Uislamu na Ukristo
Matamshi ya Busara na Hekima ya Nabii Isa (AS)
Kufanyia Utafiti Mambo Yanayofanana kati ya Uislamu na Ukristo
Mitazamo ya Pamoja ya Uislamu na Ukristo Kuhusiana na Uhuru
Washika Bendera ya Kutetea Uadilifu na Watu Madhlumu
Kuwa na Mawasiliano na Allah, Dharura ya Maisha ya Mwanaadamu
Umaanawi, Nukta ya Pamoja ya Dini za Mwenyezi Mungu
Kukabiliana Ukristo na Uislamu
Dini ya Rehma, Huruma na Upole

Mlango wa Tatu: Ukristo Katika Zama Mpya

Masihi Baina Yetu
Njia ya Kuweza Kupenya Ukoloni
Mwisho wa Maarifa ya Kidini, Mwanzo wa Maarifa ya Kielimu
Wasioamini Ukristo
Asili ya Kupinga Umaanawi
Hatua ya Kanisa ya Kupuuza Ukosefu wa Uadilifu Duniani
Natija ya Kujiweka Mbali na Mafundisho ya Masihii Isa
Madai ya Uongo

Mlango wa Nne: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wafuasi wa Ukristo Walio Wachache

Taathira ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa Ulimwengu wa Kikristo
Kuishi Kwa Amani Wafuasi wa Dini Tofauti Nchini Iran
Kuwa Pamoja na Wananchi Wenzetu wa Kikristo
Hisia za Kupendana na Kuwa Karibu

Ukristo Katika Miongozo ya Ayatullah Udhma Khamenei


Mlango wa Kwanza:  Nabii Isa Masihi (AS)

Mtume Mkubwa wa Mwenyezi Mungu

Thamani ya Nabii Isa (AS) kwa mtazamo wa Waislamu, bila ya shaka si ndogo na haishindwi na ile waliyo nayo Wakristo ambao ni wafuasi wa kweli wa mtukufu huyo.

Mtume huyu mkubwa wa Mwenyezi Mungu alikipitisha kipindi chake chote wakati alipokuwepo hapa duniani baina ya watu kwa hima kubwa ili aweze kupambana na dhulma, uchupaji mipaka, ufisadi na watu wanaotumia mabavu. alisimama kidete kukabiliana na dhulma na maovu yaliyokuwa yakifanyiwa mataifa mbalimbali. Tabu alizokumbana nazo Mtume huyu Mkubwa wa Mwenyezi Mungu kuanzia katika kipindi chake cha utotoni hadi kuondoka kwake duniani zote zilikuwa katika njia hiyo hiyo. Itakumbukuwa kuwa Mwenyezi Mungu alimpa Utume Nabii Isa AS tangu akiwa mtoto.

Juu ya ukurasa

Nabii Isa (Amani Iwe Juu Yake) Mtume Mkubwa wa Mwenyezi Mungu

Waislamu wanamkubali na kumtambua Nabii Isa kuwa ni Mtume Mkubwa wa Mwenyezi Mungu (kama wanavyomkubali Wakristo). Mayahudi hawawezi kusema kwamba, Nabii Mussa (AS) ni mali yetu na hawahusu watu wengine; hapana. Wakristo wote ulimwenguni wanamkubali Nabii Mussa (AS); kama ambavyo Waislamu kote duniani wanamheshimu na kumkubali Nabii huyo wa Mwenyezi Mungu.

Kuhusiana na Nabii Isa pia ni hivyo hivyo; kwa maana kwamba, Nabii Isa Masiya (AS) si wa Wakristo tu, bali Mtume huyo ni wa Waislamu pia. Wananchi Waislamu wa Iran wanampenda na kumtukuza Nabii Isa (AS) na wanamheshimu sana Mtukufu huyo. Wakristo wa Iran - iwe ni Maashuri, iwe ni Wakristo wa maeneo ya kaskazini na Orumieh – wote wanaamini kwamba, asili ya Ukristo inaanzia hapo. Wanasema kuwa, kituo cha Mtukufu Nabii Isa kilikuwa hapa na kwa hakika Ukristo ulienea kuanzia hapa. Pengine kuamini kwao huko ni sawa kwa upande wa historia.

Juu ya ukurasa

Maryam Ruwaza Njema kwa Wanadamu

Wakati Qur'ani Tukufu inapozungumzia kiigizo kwa ajili ya wanadamu kwa upande wa imani, haidhukuru kiigizo hicho kutoka baina ya wanaume; bali inakitolea mfano kutoka miongoni mwa wanawake; Mwenyezi Mungu Mtukufu anawataja wanawake wawili kama mfano na ruwaza njema kwa wanadamu kwa upande wa imani, lakini hakufanya hivyo miongoni mwa wanawake mahiri. Hii ina maana maana kwamba, katika medani ya ubinadamu na ukamilifu wa kimaanawi, wakati Mwenyezi Mungu anapotaka kubainisha mfano bora, hazungumzii Mitume, shakhsia wakubwa, na shakhsia wa kielimu na wa kidini; bali anatolea mfano wanawake wawili ambapo mmoja kati ya wanawake hao ni mke wa Firauni. Mwanamke mwingine wa pili ni Maryam mama wa Nabii Isa (AS) na binti ya Imran. Maryam ni mwanamke ambaye katika rika lake la ujana alikabiliwa na tuhuma na dhana mbaya ya kutenda dhambi kutoka kwa wakazi wote wa mji na kitongoji chake. Lakini mwanamke huyo mtukufu hakutetereka bali alisimama imara na madhubuti kama mlima na akalishika vilivyo Neno la Allah na Roho (Nabii Isa AS) ambavyo Mwenyezi Mungu alimpulizia mtukufu huyo kwa uwezo na nguvu Zake Allah zisizo na mpaka, na akamlea barabara mwanawe aliyekuwa kama tochi ya kuumulika ulimwengu uliokuwa na giza totoro.

Juu ya ukurasa

Bibi Maryam Dhihirisho la Usafi

Kuna nukta moja katika kisa cha Bibi Maryam (Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake) kwenye Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani ambayo imenivutia mno. Waislamu wanamtaja Bibi Maryam katika ibara zao wakisema kuwa Bibi mwema huyo ni dhihirisho la usafi, utakasifu na utoharifu – yaani mwanamke msafi kabisa - katika Qur'ani kuna sehemu kadhaa amezungumziwa Bibi Maryam (SA). Mwenyezi Mungu anasema: ''Na Mariamu binti wa Imrani, aliyelinda ubikira wake, na tukampulizia humo kutoka roho yetu, na akayasadiki maneno ya Mola wake Mlezi na Vitabu vyake, na alikuwa miongoni mwa wat'iifu''. At-Tahriim 66:12

Suala la Maryam kulinda ubikira wake, staha, heshima, usafi na utakasifu wake wa mwili, limesisitizwa mno katika Qur'ani. Sasa swali la kujiuliza hapa ni kwamba kwani mazingira yalikuwa vipi wakati huo? Kwa mtazamo wangu hiki ni kitu muhimu sana. Naam; Binti mdogo alikuja ndani ya maabadi na kuishi hapo hadi ujanani mwake wake. Kulikuwa na sababu na msukumo gani kwamba, Maryam kwa ujudi wake wote asimame kwa nguvu zake zote kukabiliana na nguvu ya hali ya juu kabisa ya Mwanaadamu? Ni wazi kwamba kama haikuwa ya hali ya juu kabisa ya Mwanaadamu, Qur'ani isingelitilia mkazo kiasi chote hiki nguvu hiyo. Sasa jambo kubwa la kujifunza hapa ni huku kujitokeza Bibi Maryam na kusimama kidete kukabiliana na ushawishi wote mbaya uliokuwepo wakati huo kiasi kwamba Qur'ani inamsifu ikisema: "alilinda ubikira wake''. Hili ni jambo lenye umuhimu mkubwa; ni darsa, ibra na funzo kubwa kwa watu wote.

Bibi Maryam (SA) aliweza katika wakati nyeti kupambana na mtihani ule na kuhifadhi usafi wake na utakasifu wake, kiasi kwamba, aliacha taathira kubwa kiasi chote hiki katika historia, kama ambavyo mfano mwingine ni ule wa kijana wa kiume - Nabii Yusuf (AS) - ambapo hilo nalo limeelezwa katika Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani.

Juu ya ukurasaa

Sifa Maalumu ya Kisa cha Isa bin Maryam (AS)

Mimi binafsi kila ninaposoma au kusikia Sura Tukufu ya Maryam kuanzia katika kipindi cha ujana mpaka sasa hali yangu huwa hivi hivi yaani huathirika mno; kwani tukio hili ni tukio lisilo la kawaida. Kisa cha kuzaliwa Nabii Isa (AS) katika mazingira kama yale na eneo lile na ile hali na nafasi iliyokuwa ikitawala katika historia na jamii ya wakati ule; wakati yote hayo yanapokusanyika pamoja na mtu anapotilia maanani adhama na utukufu waliokuwa nao watukufu hao, kwa hakika humuwia vigumu kupata maneno sahihi ya kuelezea kisa hicho na hakuna bayani ambayo inaweza kutoa wasifu wa tukio hilo kama inavyostahiki, isipokuwa bayani ya sanaa!

Tukio hili ni miongoni mwa yale matukio ambayo ni ya ajabu mno na machache kuwahi kutokea; nafasi ya Bibi Maryam, nafasi ya Janabi Zakaria, hali ya kijamii ya wakati huo, kuchomoza jua lile lililokuwa liking'ara katika mbingu ya ujudi wa Mwanaadamu, akili ya Mwanaadamu na uhai wake - ambayo ni mafundisho ya Nabii Isa (AS) - na hasa kwa kuzingatia kwamba, mafundisho ya Nabii Isa (AS) hayana tofauti yoyote na mafundisho ya Nabii Mussa (AS); kwa maana kwamba, mafundisho yake yalikuja kukamilisha mafunndisho yaliyotangulia. Mengi ya mafundisho hayo yalikuwa ni ya kukariri yaani ni yale yale ya huko nyuma. Wakati mafundisho hayo yalipokuwa yakitolewa na Nabii Isa AS, wafuasi wa Nabii Mussa (AS), walipinga sana mafundisho hayo na walikuwa wakiyaona kama ni bidaa kutokana na upotofu mkubwa waliokuwa nao; wakati ambapo, mafundisho hayo yalitoka katika chimbuko na chanzo kile kile yaani Wahyi na Ufunuo. Kisa cha Nabii Isa AS kinabainisha kwa uwazi kabisa athari mbaya za upotofu, athari za kutumia vibaya nguvu, ufahamu mbaya na kujiona.

Juu ya ukurasa

Mshika Bendera ya Hidaya

Ile Kalima ya Mwenyezi Mungu (yaani Nabi Isa Masihi AS) alikuwa mshika bendera ya hidaya ya uongofu katika kipindi cha upotofu, ujahili, dhulma na upuuzaji wa thamani za kibinaadamu na alichukua jukumu la kuwa mwokozi wa wanadamu. Katika kipindi hicho, Nabii Isa alisimama kidete kupambana na udikteta, dhulma na uonevu na alikuwa akifanya hima na jitihada kwa ajili ya kuhakikisha kuwa uadilifu, usawa, rehma na tawhidi vinakuweko katika jamii. Leo hii wanaomwamini Mtume huyo mkubwa wa Mwenyezi Mungu - yaani Wakristo na Waislamu - ili kusimamisha mfumo unaostahiki kuwepo ulimwenguni, ni lazima washikamane na mafundisho ya Mitume sambamba na kueneza mafundisho ya watukufu hao na fadhila na thamani za kibinadamu kwa mujibu wa mafundisho ya walimu hao wa wanadamu.

Juu ya ukurasa

Mkombozi wa Watu kutoka katika Dhulma

Nabii Isa Masihii (AS) alikuwa na muujiza na alibaathiwa na kupewa Utume kwa ajili ya kumkomboa Mwanaadamu na kumuokoa kutoka katika giza la shirki, kufru, ujahili na dhulma na kumuongoza katika nuru, maarifa, uadilifu na kumwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja pasina kumshirikisha na kitu kingine. Katika muda wake wote alioishi na watu, Isa Masiya (AS) alifanya hima ya kupambana na mabaya na kuwaita watu katika mambo mema na hakusita hata kidogo kufanya hima katika uwanja huo. Hili ni somo na darsa ambayo Wakristo na Waislamu ambao waanaamini Utume wa Nabii Isa (AS) wanapaswa kujifunza.

Leo hii Mwanaadamu anahitajia zaidi mafundisho hayo kuliko wakati mwengine wowote ule. Uislamu ambao ni kamilisho la mafundisho ya Isa Masihi AS, umeweka mbele katika daawa yake masuala ya kheri, marekebisho na ukamilifu pamoja na ifanisi wa Mwanaadamu humu duniani na kesho Akhera. Mwanaadamu aliyepotea kwa kuwa na nguvu zisizo na mpaka za maumbile na ambaye amepata nguvu hizo kwa baraka za elimu aliyopewa na Mwenyezi Mungu, anafanya kinyume kabisa na malengo aliyoumbiwa na kupewa nguvu hizo. Leo hii majukumu ya wafuasi wa dini za Mwenyezi Mungu ni mazito zaidi. Madola ya kibeberu na yenye satua ulimwenguni kimsingi yamekuwa yakibana anga ya mataifa na watu madhulumu na hayaachi kufanya dhulma yoyote dhidi ya mataifa hayo kwa madai ya kulinda dini ya Kikristo.

Juu ya ukurasa

Mlinganiaji wa Bahati Njema

Nabii huyo mukhtari wa Mwenyezi Mungu, alikuwa akiwaita na kuwalingania watu kwenye mema na kheri zao na alikuwa akiwatahadharisha watu juu ya matamanio ya nafsi na kujitumbukiza katika mambo machafu na sifa mbaya za kiroho, dhulma na mambo mabaya na machafu. Madola ya kifisadi ya kibeberu na watumiaji mabavu walikuwa wakimuudhi, kumtuhumu na kumvunjia heshima Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu na hata kufikia hatua ya kutaka kumuua na baada ya Mwenyezi Mungu kumpa hifadhi, Hawariyyun (wanafunzi) na wafuasi wake kwa miaka kadhaa waliteseka na kutaabishwa na watu waliokuwa wakipinga mafundisho ya Nabii Isa (AS) ambayo yalikuwa dhidi ya ufisadi, dhulma, shirki, kufuata hawaa na matamanio ya nafsi, kupenda vita na kuwahadaa watu maadui ambao walitaka kuyafutilia mbali mafundisho ya mtukufu huyo.

Wale ambao walikuwa ni mafasidi, madhalimu, washirikina, wafuasi wa matamanio ya nafsi, wapenda vita na wahadaaji wa watu walikuwa hawako tayari kuivumilia dini ya Mwenyezi Mungu wala Mtume wa Allah (Masihi Isa AS) na mafundisho yake.

Juu ya ukurasa

Kuzaliwa Mtukufu Isa Masiya (AS)

Mamia ya miaka ya kukifanyika sherehe za kukumbuka kuzaliwa Isa Masihi (AS) imepita. Kwa nini kuzaliwa kwake kuna umuhimu na thamani kubwa?

Ni kutokana na kuwa, hicho kilikuwa ni kipindi muhimu, nyeti na chenye kuainisha, nukta ya kurejea na nukta ya kona na kupinda katika historia. Yaani historia ilikuwa ikienda katika mstari wake; lakini katika lahadha hii ikapinda na kuelekea upande mwingine. Hii ni nukta ya kukata kona na nukta ya kuelekea upande mwingine. Sisi kila mwaka huwatumia salamu za mkono wa baraka na kheri ndugu zetu Wakristo hapa nchini na Wakristo wengine ulimwenguni kwa mnasaba wa kukumbuka kuzaliwa Nabii Isa (AS); hata hivyo kutokana na kuwa kwa mujibu wa nadharia ya Wakristo wengi wanaoishi hapa nchini tarehe ya kuzaliwa Nabii Isa AS si tarehe 25 Desemba kama wanavyoamini Wakristo wengine ulimwenguni, bali ni katika kumi la kwanza la mwezi Januari - ambapo Waarmenia ni miongoni mwa waliomo katika kundi hili - sisi huwa hatufuati tarehe hiyo ya 25 Desemba na ndio maana hatutumi salamu za pongezi siku hiyo, bali husubiri mpaka ufike mwezi Januari hapo ndipo tunapotuma salamu zetu za pongezi, kheri na baraka ili tuendane na nadharia ya ndugu zetu wa hapa nchini.

Inshallah, kumbukumbu ya kuzaliwa Nabii Isa (AS) inabidi iwe ni siku ya baraka kwa Wakristo na Waislamu wote ulimwenguni. Ala Kulli Haal, katika siku kumi hizi ni siku za kukumbuka ya kuzaliwa Nabii Isa Masiya Inshallah Waislamu na Wakristo wote watajifunza muamala na mwenendo wa Mtukufu huyo na kumfahamu vyema Isa Masiya (AS) na hivyo kumfuata Nabii huyo mteule wa Allah.

Juu ya ukurasa

Mlango wa Pili: Uislamu na Uksristo

Kutambuliwa Haki ya Mtume wa Uislamu na Mtawala wa Kikristo

Imehadithiwa kuwa, siku moja wajumbe wa Najashi - Mfalme wa Uhabeshi ambaye alikuwa ni Mkristo - walikuja kwa Bwana Mtume Muhammad SAW mjini Madina ukiwa na ujumbe kutoka kwa mtawala huyo. Najashi alikuwa Mfalme wa Uhabeshi (Ethiopia ya sasa) na alikuwa kama walivyokuwa watawala wengine wengi katika zama hizo ambao aghlabu yao walikuwa ni Wakristo na hakukuwa na mtawala wa Kiislamu; lakini wakati wajumbe wa Najashi walipowasili, Mtume SAW alisimama kutoka mahala alipokuwa amekaa na kuanza kuwahudumia yeye mwenyewe wageni hao. Masahabna walipoona hivyo wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Sisi tupo, tupe idhini sisi tuwahudumie wageni hawa. Mtume SAW akawajibu kwa kusema: Hapana, Wakati ule ambapo Waislamu walihajiri na kuelekea Uhabeshi (Ethiopia ya sasa), mfalme wao aliwapokea kwa heshima na taadhima Waislamu hao na akawatendea wema na kuwakirimu mno; hivyo ninataka kufidia wema na ukarimu wa mfalme wao kwa Waislamu wale. Huku ndiko kutambua haki na kuthamini wema tunaofanyiwa.

Juu ya ukurasa

Ibada Zinazofanana kati ya Uislamu na Ukristo

Mwenyezi Mungu anasema katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani kwamba: ''Enyi mlioamini! Mmeandikiwa (mmefaradhishiwa) Saumu, kama walivyoandikiwa (walivyofaradhishiwa) waliokuwa kabla yenu ili mpate kumchamngu'' al-Baqarah 2:183.

Tunafahamu kwamba, Sala na Zaka si mambo ambayo yalikuwa makhsusi kwa Uislamu; bali Mitume waliokuweko kabla ya Bwana Mtume SAW, katika sheria na hukumu zao walikuwa na Sala na Zaka. Mwenyezi Mungu anasema katika kitabu kitakatifu cha Qurani kwamba:

''Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia Sala na Zaka maadamu ni hai'' Maryam 19:31

Hiyo ni kauli nya Nabii Isa AS kama ilivyokuja katika Qur'ani akionyesha kwamba, aliusiwa na Mwenyezi Mungu kusimamisha Sala na kutoa Zaka. Kuna aya nyingine pia katika Qur'ani ambazo zinaonyesha maana hii. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya Qur'ani ambayo madhumuni yake ni kwamba:

Saum ni kama ilivyo Sala na Zaka, ni katika orodha ya ibada na hukumu ambazo si makhsusi kwa umma wa Kiislamu; bali umma zilizotangulia na Mitume wa huko nyuma nao waliamrishwa kutekeleza ibada ya Saum.

Juu ya ukurasaaa

Matamshi ya Busara na Hekima ya Nabii Isa (AS)

Miongoni mwa riwaya zilizopokewa kutoka kwa Ahlul Bayt (AS) kuna baadhi ya kauli ambazo zimenukuliwa kutoka kwa Nabii Isa (AS). Sehemu fulani ya kauli hizo, zinapatikana katika vitabu vyote vya hadithi vya Kiislamu na ni miongoni mwa sehemu zenye maana kubwa za riwaya na hadithi za Waislamu.

Kauli hizi zimejaa maana, ni johari, zina nguvu na zenye hekima na busara tele. Wakristo hawadai kwamba, maneno ya Nabii Isa (AS) ni yale tu yaliyoko ndani ya vitabu vya Injili. Mbali na vitabu vya Injili vilivyopo, kulikuwa na injili zaidi na kauli ambazo zipo katika riwaya za Kiislamu na katika vitabu vya Kiislamu zinazonasibishwa na Nabii Isa (AS) ni sehemu ndogo tu ya maneno yaliyopotea ya Injili.

Ala Kulli Haal, kauli zilizonukuliwa kutoka kwa Ahlul Bayt (AS) zinazohusiana na Nabii Isa AS, Wakristo wanapaswa kuzitazama kwa jicho la itibari; wazichukue na wawe nazo na kisha wazitumie na kuzifanyia kazi. Yamkini hatua hii ikawa wenzo wa wafuasi wa dini mbili hizi kukurubiana zaidi. Waislamu wanaweza kuwapatia zawadi walimwengu wote ya sehemu ya risala ya Mtukufu Nabii Isa Masiya (AS). Kauli ambazo ni za Nabii Isa AS ambazo zimekuja na kunukuliwa katika riwaya za Kiislamu zimejaa hekima, maana na madhumuni aali. Mimi huko nyuma nilikuwa nikiitupia jicho mno Injili; Injili hizi hizi zilizopo - Injili nne za Wakristo - kuna ibara zilizojaa hekima. Ni kweli kwamba, Waislamu wanaamini na kuitakidi kwamba, kuna baadhi ya mambo si sahihi katika Injili; lakini mtu hakatai maneno yenye hekima na busara ndani yake.

Juu ya ukurasa

Kufanyia Utafiti Mambo Yanayofanana kati ya Uislamu na Ukristo

Kuyafanya mafundisho ya kidini yapenye na kujikita katika nyoyo za vijana na yaingie vyema katika jamiii, kwa hakika ni fikra sahihi kabisa. Dini ni hadia na atia kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kila ambavyo jamii itaweza kuwafanya watu wake wastafidi na wafaidike na zawadi hiyo ya Mwenyezi Mungu kwao, ndivyo jamii hiyo itakavyofanikiwa kupata mambo mengi mema na mazuri. Kuamiliana na vijana ni kazi nyeti, tab'an hatima yake nayo ni njema. Kuna mambo mengi yanayfanana baina ya Uislamu na Ukristo na baina ya dini zote za Mwenyezi Mungu.

Mazungumzo baina ya Waislamu na Wakristo katika mikutano ya pande mbili au pande kadhaa ambayo inafanyika, inaweza kutafuta nukta zinazofanana kati ya dini mbili hizi.

Pengine litakuwa ni jambo zito kwa mitazamo ya dini mbili kukurubishwa pamoja, lakini inawezekana kuzitambua nukta ambazo zinakaribiana au ambazo zinashabihiana kikamilifu. Gharadhi katika mazungumzo haya isiwe ni kuthibitisha kwamba, dini fulani iko katika haki au kuonyesha kwamba, dini fulani iko katika batili; bali lengo liwe ni kuzifikia nukta za pamoja ambazo zinajumuisha sehemu muhimu ya masuala ya maisha.

Juu ya ukurasa

Mitazamo ya Pamoja ya Uislamu na Ukristo Kuhusiana na Uhuru

Suala la uhuru wa Mwanaadamu daima ni moja ya mambo yanayohangaikiwa sana na Mwanaadamu. Uhuru huu ni nini na mpaka wake umeenea hadi wapi? Dini zina mambo mengi ya kusema kuhusiana na kadhia hii na leo hii moja ya mambo ambayo yanaweza kuwa ni shabaha ya dini za Uislamu na Ukristo ni suala hili la uhuru wa Mwanaadamu. Leo hii tunashuhudia kuvuka mipaka (ifrat) na kuzembea kupita kiasi (tafrit) katika uwanja huu.

Madikteta na vibaraka wao wanaoonekana na wasionekana wamekuwa wakichukua na kudhibiti uhuru wa watu. Katika sehemu nyingine utaona watu wanapatiwa uhuru mwingi kupita kiasi katika maisha yao - ambapo jina lake sio uhuru; bali ni ufisadi. Kwa mtazamo wa dini, pande zote mbili zinahesabiwa kuwa ni kwenda kinyume. Uislamu na Ukristo pia, katika kukataa pande mbili hizo za uhuru, zina mitazamo inayokaribiakia. Leo hii moja ya majukumu muhimu na ya kimsingi ya watu wote ambao wana mapenzi na mustakabali mwema wa wanadamu na kizazi cha vijana, ni wao kukabiliana na ufisadi ambao unaongezeka siku baada ya siku; hususan vyombo vya Kikristo ambavyo viko barani Ulaya - vina jukumu zito katika uwanja huu. Kuna makundi ambayo yanaeneza ufisadi na ni mahala pake kabisa kwa vyombo vya kanisa - hususan kanisa Katoliki - kutokana na ukubwa lilio nao na nguvu lilizo nazo lipambane vikali na kwa njia za kimantiki na wimbi hili la kuenea ufisadi, wimbi ambalo kimsingi halijazuka leo. Kama vyombo vya kanisa barani Ulaya vitasimama kupambana na ufisadi, kuna nchi nyingi zisizo za Ulaya ambazo zitavishukuru mno vyombo hivyo; kwani baadhi ya ufisadi na mambo machafu huingia mahala fulani vikitokea mahala kwingine.

Juu ya ukurasa

Washika Bendera ya Kutetea Uadilifu na Watu Madhlumu

Endapo dini itaingia katika uwanja wa kutetea uadilifu na watu madhlumu sehemu muhimu ya mvuto wa dini itadhaminiwa kikamilifu. Kila mahala duniani vijana huvutiwa na kuraghibika kutokana na kushuhudia harakati ya kiadilifu. Uadilifu ni mali ya dini. Mashujaa wakubwa wa ulimwengu katika njia ya uadilifu ni watu wa dini. Nabii Isa (AS) alitumia umri wake wote kwa ajili ya kuhakikisha uadilifu unatawala katika jamii. Mtume wa Uislamu alitumia umri wake wote katika njia ya kuleta uadilifu. Shakhsia wakubwa wa Ukristo mwanzoni mwa Ukristo, walijitolea mno katika njia ya uadilifu. Vitabu vya dini - iwe ni Taurati, Injili au Qur'ani - zimekokoteza mno juu ya uadilifu, kuupigania na kuutafuta kwa kila hali.

Bila ya litakuwa ni jambo lenye mvuto sana kama leo hii mambo hayo yatakuwa nara na shaari za kidini ya viongozi wa kidini wawe wa Kikristo au wa Kiislamu au wa Kiyahudi ambao wanaheshimu mafundisho ya Taurati – tab'an hapa hatuwakusudii Wazayuni; kwani Wazayuni hawaheshimu na wala hawana mfungamano na kitu chochote kinachohusiana na uadilifu.

Juu ya ukurasa

Kuwa na Mawasiliano na Allah, Dharura ya Maisha ya Mwanaadamu

Mwanaadamu hawezi kuishi bila ya kufungamana au bila ya kuwa na mawasiliano na Mwenyezi Mungu. Mfano wake ni ulimwengu wa Kikomonisti. Siku ambayo mfumo wa Kimaksi uliokufuru, ulipopoteza nguvu zake katika Umoja wa Kisovieti, makanisa yalijaa watu. Walikuwa wakidhani kwamba, kama wangeondoa mashinikizo kutoka kwa wananchi, kwa kuzingatia propaganda zao za miaka 70, wananchi wenyewe wasingekuja makanisani. Hilo ndilo lililokuwa kosa lao. Baada ya kupita miaka 70 kwa mara nyingine tena wananchi wamemiminika makanisani. Endapo leo mutakwenda nchini Russia au katika nchi za Ulaya Mashariki, mutaona kuwa, makanisa yamejaa idadi kubwa ya watu. Kimsingi harakati ya wananchi wa Poland dhidi ya Wamaksi ilikuwa ni harakati ya mapambano ya Kidini.

Juu ya ukurasa

Umaanawi, Nukta ya Pamoja ya Dini za Mwenyezi Mungu

Dini za Mwenyezi Mungu licha ya kuwa zina tofauti baina yao, lakini zina nukta za pamoja ambazo zinafanana. Miongoni mwa nukta muhimu mno baina ya dini, ni kuzingatia umaanawi; kitu ambacho ndiyo iliyokuwa risala ya kwanza ya dini kwa ajili ya wanadamu. Dini zimewafanya wanadamu wazingatie mambo ambayo yako katika mbele ya macho yao, masikio yao yanasikia, mwili wao unahisi, lakini vina mpaka. Zikawafanya wazingatie kwamba, kuna uhakika mkubwa zaidi, ambao ni zaidi ya vitu ambavyo wao wanaweza kuviona na kuvihisi. Leo uwepo wa kimaanawi ulimwenguni unahisika; lakini aghalabu ya harakati ulimwenguni, ziko kinyume na hilo.

Kama watu ambao ni wafuasi wa dini, wataweza kuuondoa mghafala huo hata kwa kiwango Fulani tu, watakuwa wametoa huduma kubwa; hapa ndipo ambapo panapopatikana nukta ya pamoja ya Uislamu na Ukristo. Mazungumzo ya viongozi wa dini mbalimbali yanapaswa kutilia mkazo nukta hii. Dini za kweli, hazikufanya juhudi za kuwaweka mbali wananchi na masuala ya kidunia; lakini ziliwafahamisha kwamba, juhudi zote hizi za dunia zinaweza kuwa katika kalibu ya kuelekea na kufikia daraja ya kimaanawi; hivyo dini zikang'arisha nyoyo zao kwa uhakika. Mghafala wa Mwanaadamu kwa uhakika huu, ni kwa madhara yake na madhara haya hayawezi kulinganishwa na madhara yoyote yale. Leo hii Mwanaadamu amekumbwa mno na mghafala huu; yaani harakati adhimu na pana ya ulimwengu wa kimaada, ni mambo ambayo yamemfanya mwanaadamu akabiliwe na mghafala huu mkubwa.

Juu ya ukurasa

Kukabiliana Ukristo na Uislamu

Hakuna hali ya kukabiliana baina ya Uislamu na Ukristo na wala hali hiyo haitofikia. Kama kusudio la kukabiliana Uislamu na Ukristo ni kukabiliana baina ya madola ambayo ni ya Kiislamu na ya Kikristo tunapaswa kusema hapa kwamba, hali hii ya kukabiliana si zaidi ya kukabiliana baina ya madola mawili ya Kikristo. Hata hivyo inasikitisha kuona kuwa, kuna hamu na shauku ya kupenda vita duniani. Ingawa hata hivyo katika kipindi hiki cha miaka 70 ya hivi karibuni, katika ulimwengu wa Kikristo wenyewe kumetokea vita tena na vimewakumba pia Waislamu. Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran unawaita na kuwalingania Waislamu kwenye umoja, na huu umoja sio dhidi ya Wakristo au dini na mataifa mengine, la hasha, bali ni kwa ajili kukabiliana na wavamizi na wapenda vita, kwa ajili ya kutekeleza maadili, umaanawi na kuhuishwa utumiaji akili, uadilifu wa Kiislamu na maendeleo ya kielimu, kiuchumi na kurejesha heshima na izza ya Kiislamu.

Mfumo wa Kiislamu wa Iran unawakumbusha walimwengu kwamba, Quds ilikuwa katika mikono ya Waislamu katika kipindi cha Khulfa-i-Rashideen na kwamba, Wakristo na Mayahudi walikuwa wakiishi kwa utulivu na usalama kamili. Lakini hivi sasa, Quds na vituo vingine vinakaliwa kwa mabavu Wazayuni na viko chini ya misalaba ya Wazayuni. Inajaribu kuwafumbua macho watu kuona ni kwa namna gani damu ya Waislamu isivyothaminiwa na Wazayuni?!

Juu ya ukurasa

Dini ya Rehma, Huruma na Upole

Uislamu si dini ambayo iko dhidi ya dini nyingine. Uislamu ndiyo dini ambayo wakati ilipodhibiti maeneo yasiyo ya Waislamu, watu wa dini nyingine walishukuru kutokana na rehma za Uislamu na kusema, nyinyi muna huruma kwetu sisi kuliko sheria zetu wenyewe za hapo kabla. Katika eneo la Shamat, wakati wakombozi wa Kiislamu walipowasili na kuingia katika maeneo hayo, Mayahudi na Wakristo ambao walikuwa wakiishi katika eneo hilo, waliwaambia nyinyi Waislamu mna huruma kwetu kuliko wenzetu waliokuwa wakitutawala. Waislamu waliwafanyia wema na walikuwa na huruma kwa wananchi. Uislamu ni dini ya huruma na mapenzi, dini ya rehma; ni rehma kwa walimwengu wote. Uislamu unauambia Ukristo kwamba:

‘’Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimwabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu.’’ Al-Imran 3:64

Uislamu unawabainisha watu wa dini nyingine (watu wa Kitabu) juu ya mambo yanayofanana baina yao. Uislamu hauko dhidi ya mataifa mengine, hauko dhidi ya dini nyingine; bali uko dhidi ya utumiaji mabavu, utendaji dhulma, dhidi ya uistkbari na dhidi ya udhibiti na satua za kimabavu. Lakini mabeberu, waistikbari na madhalimu wamekuwa wakijaribu kufanya njama za kuthibitishia ulimwengu kinyume chake. Watu hao wamekuwa wakitumia suhula zote; kuanzia Hollywood (Kitengo cha Uzalishaji Filamu nchini Marekani) hadi katika nyenzo za propaganda na utangazaji, na mpaka katika wenzo na suhula kama silaha na vikosi vya kijeshi kwa ajili ya kutangaza kinyume cha hivi na kuionyesha dunia kwamba, ukweli wa mambo ni huo wanaousema wao.

Juu ya ukurasa

Mlango wa Tatu: Ukristo Katika Zama Mpya

Masihi Baina Yetu

Laiti Nabii Isa Masihi (AS) angekuwa baina yetu leo hii, asingelichelewa hata lahadha moja kupambana na viongozi wa dhulma na wastakbari ulimwenguni, na katu asingevumilia hali hii ya baa la njaa na kuwa wakimbizi watu huku mabilioni ya watu wakiteseka na kutaabika kutokana na siasa na sera za madola makubwa yanayoendesha vita, ufisadi na kueneza chuki baina ya watu.

Juu ya ukurasa

Njia ya Kuweza Kupenya Ukoloni

Moja kati ya njia za kimsingi za ukoloni, uistikbari na wanaounga mkono ni kuondoa katika nyoyo za watu imani ya matumaini na mapambano. Mara kadhaa wametaka kuzima taa hii; lakini hawakuweza. Ukoloni na Uistikbari umefanya njama na hujuma kubwa mno katika uwanja huu - sio nchini Iran tu bali katika maeneo yote ya ulimwengu wa Kiislamu - ili uzime taa hii. Ripoti moja muhimu ya miaka ya nyuma na sio mpya, inaonyesha kuweko juhudi za makundi ya wahubiri wa Kikristo ambayo yalikuwa yakitokea Ulaya na kutumwa katika maeneo ya kaskazini mwa Afrika, ili yakasafishe njia ya ukoloni katika maeneo hayo. Makasisi walikuwa wakienda katika maeneo ya mbali na katika vijiji vya ndani katika baadhi ya maeneo barani Afrika na kubakia huko kwa miaka kadhaa.

Walibakia huko kwa ajili ya nini? Hivi lengo lao la kuyatanasarisha makabila ya Kiafrika lilikuwa ni lipi? Nani asiyefahamu kwamba makasisi hao walikuwa wakiandaa mazingira ya kupenya mkoloni. Walikwenda ili kuwatanasarisha wenyeji na wakazi wa asili wa maeneo hayo, ili makundi ya kikoloni yaweze kwenda katika maeneo hayo na kufanya kazi zao kwa urahisi na wepesi. Makasisi walikuwa wakifahamu vyema kwamba, wanafanya kazi gani - si kwamba, walikuwa hawafahamu malengo ya kazi yao hiyo - lakini tazameni walistahamili na kuvumilia masaibu mengi mno kwa ajili ya kazi hii; masaibu ambayo katu yasingeweza kufidiwa kwa fedha; kwa mfano mtu aende na kukaa mahala miaka saba, katika eneo ambalo ni jirani na jamii ya wala watu na kuishi huko! Mtu unaweza kuyavisoma vitu hivi katika vitabu, na kuviona katika baadhi ya ripoti, na katika baadhi ya filamu na kuvisoma katika baadhi ya hadithi na visa.

Moja kati ya masikitiko ya wanaoshikamana na dini ulimwenguni ni kwamba, madola yenye satua na nguvu ya nchi za Kikristo, kidhahiri yalikuwa yakihubiri na kutangaza dini ya Kikristo lakini kibatini yalikuwa yakitumia mahubiri ya dini hiyo kama wenzo wa kupeleka mbele malengo ya kikoloni na kulisafishia njia gari la ukoloni. Makundi ya wahubiri wa Ukristo - ambayo kijuu juu yalikuwa yakihubiri Ukristo; lakini ukweli ni kuwa yalikuwa yakiandaa uwanja na mazingira yanayotakiwa na walilenga kuwafungulia njia wakoloni wa Ulaya waliotoka katika nchi mbalimbali barani Ulaya wakati huo, waingie katika nchi za Kiislamu na kudhibiti nguvu za kisiasa - walitumwa katika pembe mbalimbali duniani na jambo la kusikitisha ni kwamba, wahubiri hao walifanikiwa mno katika maeneo mengi waliyotumwa.

Juu ya ukurasa

Mwisho wa Maarifa ya Kidini, Mwanzo wa Maarifa ya Kielimu

Katika Ulaya ya Kikristo, kuanza harakati ya maarifa ya kielimu, kulikwenda sambamba na kufikia tamati na kuporomoka maarifa ya kidini; yaani kuanza kwa marhala hii kulikuwa na maana ya kufikia tamati marhala ile. Yamkini hilo ndilo lililopaswa kutokea; kwani maarifa ya kidini katika mazingira ya Kikristo yalikuwa yametawaliwa na upotofu, taasubi na yalipinga kikamilifu maendeleo ya kielimu. Katika zama hizo barani Ulaya, msomi alikuwa akitiwa mbaroni, kufungwa jela, kutandikwa viboko na kuchomwa moto kwa kosa la kufanya uvumbuzi fulani wa kielimu, zama hizo zilikuwa mbali mno na zama zetu hizi. Kwa karne kadhaa mtawalia msomi barani Ulaya alikuwa akionekana kuwa ni mchawi na alipokuwa akipatikana alikuwa huchomwa moto. Athari ya jambo hilo inaonekana sana katika upande wa fasihi na katika historia ya elimu ya Magharibi.

Wakati anga ya kidini ya jamii, viongozi na wenye majukumu ya kidini walikuwa wakiamiliana hivi na elimu, basi ni jambo la kawaida maarifa ya dini hukabiliwa na hatima mbaya pale elimu ilipopata nguvu na duru hiyo ya utawala wa kidini kumalizika kabisa.

Hata hivyo dini ambayo wanafikra wa Ulaya wanaipinga, haikuwa ikioana na maisha ya mwanaadamu; kwani dini hiyo ilikuwa imejaa upotofu; ndiyo ile dini ambayo ilimhukumu adhabu ya kunyongwa Galileo Galilei na ikachukua uamuzi wa kumtesa mwingine; kutokana na kuwa amefanya uvumbuzi wa kielimu! Hivyo huo hayakuwa mafundisho sahihi ya Masihi Isa, bali ilikuwa ni dini iliyopotoshwa na kuchanganywa na mambo mengine. Tatizo halikuwa ni kujiweka mbali na dini hiyo, bali tatizo lilikuwa ni kutenganishwa dini hiyo na masuala ya kimaanawi, akhlaqi, elimu, sera, mfumo wa maisha na mahusiano ya mtu na jamii kwa ujumla.

Juu ya ukurasa

Wasioamini Ukristo

Hivi sasa mtu hapaswi kuwa na shaka kwamba, shauku na malengo ya msalaba yako chini ya hila, ghilba na hadaa za demokrasia na haki za binaadamu na madola yote ya Magharibi au aghalabu ya madola hayo, yanatumia wenzo huo kwa ajili ya kufikia malengo yao ya kisiasa. Tutakuwa ni wafinyu wa fikra kama tutadhani kwamba, shauku na msukumo wa vitendo vya utumiaji mabavu huko Bosnia (ishara ya jinai dhidi ya Waislamu nchini Bosnia zilizofanywa na wanamgambo wa Kikristo wa Serbia) na mahala kwingine kokote duniani kwamba, chimbuko lake ni imani na mafundisho ya Nabii Isa Masihi (AS)

Watu ambao leo wana uadui na kila alama na kila nembo ya Uislamu au wanawafanyia uadui Waislamu, hawamwamini Isa Masihi (AS) pamoja na mafundisho yake ya kweli. Wao wanachokifikiria na kukiamini ni nguvu zisizo na kikomo, maslahi na manufaa yao na uadui wao usio na mwisho na wako dhidi ya nguvu yoyote ambayo ni tishio kwao! Lakini mikono yao iliyotapakaa damu, leo imepamba safu za Ukristo kukabiliana na na Uislamu na inatumia jina la dini kukabiliana kiimani na kiitikadi na Waislamu. Leo dini hiyo imenyanyua juu bendera ya uadui kwa nguvu zake zote dhidi ya Uislamu.

Juu ya ukurasa

Asili ya Kupinga Umaanawi

Katika dunia kama hii na yenye sifa kama hizi (za kuzingatia mambo ya kidunia na kuyaweka mambo ya kimaanawi), Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imedhihiri ikiwa na misingi imara na madhubuti ya kimaanawi. Hili ndilo jambo muhimu. Sasa mfumo huu uwe ni wa Kiislamu au Kikristo hilo linakuja katika daraja ya pili. La muhimu ni kwamba, asili ya kupambana na umaanawi ing'olewe kikamilifu na juhudi zote zielekezwe upande huo. Hilo ndilo muhimu. Inasikitisha kuona hata viongozi wa kidini ulimwenguni, wanafanya harakati zisizokubaliana na umaanawi. Fikirieni wenyewe hali inayojitokeza wakati kanifa linapofikia hatua ya kuremba vitu na kuwavutia vijana katika upande huo usio wa kimaanawi! Kufikia hadi ya kuanzisha disko pembeni mwa kanisa! Hakuna Mkristo yeyote ambaye aliwahi kufikiria kwamba viongozi wa kanisa wangeliweza kufikia hadi hiyo! Lakini hivyo ndivyo hali ilivyo hivi sasa!

Mmoja wa waandishi mashuhuri katika ulimwengu wa Kiarabu ameandika kuwa:

"Nimeshuhudia kwa macho yangu kwamba, usiku mmoja katika disco linalofungamana na kanisa, kasisi alijitokea katika disco hilo. Wanandoa vijana walikuwa wameshughulishwa na kucheza muziki. Alikuja na kutazama kama kila kitu kinakwenda vizuri au la? Inaonekana kuwa, mwanga wa taa za ndani ya disco ulikuwa mkali. Alikuja na kupunguza kwa mikono yake mwanga wa taa hizo ili mwanga mdogo uwe ukimulika sehemu ya kuchezea disco. Kisha akawageukia wahudumu wa kanisa na kuwapa maagizo kwamba, watu wote wakienda basi wafunge milango. Baada ya hapo alielekea katika bweni lake la kulala kwenda kupumzika."

Mwandishi huyu wa Kiarabu anaendelea kusimulia akiandika:

''Kesho au keshokutwa yake, nilikwenda kwa kasisi yule usiku na kusema, baba! Inaonekana hali ya mambo imekuwa vingine? Akasema hapana. Kimsingi kazi yetu ni ya kisiasa ili vijana wavutiwe na kanisa! Bila ya shaka umeona ni kwa kiwango gani vijana wengine wengi walivyokuja kanisani?"

Naam, hii ina maana kuwa huko ni kuelekea upande wa kujiweka mbali na mambo ya kimaanawi hata ndani ya ulimwengu wa viongozi wa kidini. Mfano wa kiongozi kama huyo wa Kikristo, yumkini ukatokea pia kati ya viongozi wa Kiislamu. Upo uwezekano wa kupatikana kwa watu kama hao - iwe ni kwa upande wa Kisuni au Kishia.

Sasa katika mazingira na anga kama hii na kipindi fulani katika historia, ghafla limetokea tukio na kuja mfumo ambao umesimama juu ya misingi ya kimaaanawi. Mfumo huu, umeingiza kwenye medani ya maisha ya watu, masuala ya kimaanawi, na wakati huo huo, serikali, bajeti na sera zake pia zimejengeka na kuandaliwa kwa msingi wa umaanawi. Huenda ikawezekana kusema kuwa: hakuja wahi kuja mfumo kama huu duniani, ukiacha zama fulani fupi tu. Tab'an, utawala wa kidini kama utawala wa kidini tu, daima umekuweko katika sehemu fulani Fulani duniani ya dunia (na zaidi katika ulimwengu wa Kikristo). Lakini mfumo na serikali ya Kiislamu ya Iran ni tofauti kabisa na tawala hhizo. Utawala ule kwa hakika ulikuwa utawala wa kidini na wa viongozi wa kidini, na sio utawala wa kuheshimu thamani za kidini na za kimaanawi.

Juu ya ukurasaaa

Hatua ya Kanisa ya Kupuuza Ukosefu wa Uadilifu Duniani

Leo hii vyombo vya Ukristo vimenyamaza kimya na kupuuza masuala muhimu kabisa yanayowakabili wanadamu. Leo hii katika uga wa dunia, kuna dhulma na ukosefu wa uadilifu mwingi tu lakini cha kujiuliza ni je Ukristo unafanya nini kukabiliana na hilo? Kanisa limekuwa likizungumzia amani, limekuwa likipiga nara za amani. Nara hizo ni nzuri sana; lakini hilo halitoshi. Kando ya nara na kaulimbiu za amani kunapaswa kuweko pia shaari za uadilifu. Leo hii Mwanaadamu amekuwa mateka wa dhulma na ukosefu wa uadilifu. Kuna madola makubwa ambayo yamekuwa yakidhulumu mataifa na watu wengi ulimwenguni. Watu wa Ulaya wao wenyewe ndio walioanzisha vita vikubwa, kisha wanatoa na kupiga nara za amani! Hivi sasa makumi ya miaka imepita tangu vita hivyo vimalizike, lakini bado wanatumia kisingizio cha nara za amani. Katika hali ambayo, nara ambazo zinahitajiwa na wanadamu hivi sasa ni nara ya uadilifu; lakini katu hawatamki wala shaari hizo. Vyombo vya Kikristo na Papa vile vile wamekuwa wakilitazama kwa macho tu jambo hili, na kwao hakuna tofauti uadilifu umetendeka duniani au la! Mfumo wa Kiislamu nchini Iran, haukubaliani kabisa msimamo wa viongozi wa makanisa katika wanaonyamazia kimya vitendo vya Magharibi na Uistikbari wa Kimagharibi. Viongozi hao wana jukumu kubwa katika hilo. Mimi nilimtumia ujumbe Papa (Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani) na kumwambia atilie mkazo na kusisitiza juu ya suala la uadilifu. Leo hii ujumbe wa dini zote ni kutaka kuweko uadilifu; na hiyo ndiyo risala na ujumbe wa asili wa Nabii Mussa, Isa na Mtume wa Uislamu (Amani iwe juu yao wote).

Juu ya ukurasa

Natija ya Kujiweka Mbali na Mafundisho ya Masihii Isa

Kwa watu wa Ulaya ni kidogo, lakini Wamarekani wana na mielekeo ya kidhahiri tu juu ya dini, majina ya kidini na kanisa; na wamekuwa na ufahamu wa kijuu juu tu kuhusiana na dini. Hawa hawaoni tofauti yoyote kuchanganya mambo mazuri na mabaya katika dini. Kwa mfano wako tayari kuomba msaada wa Nabii Isa au Bibi Maryam (AS) ili wakubaliwe haja zao; lakini wakati huo huo kando yake utawaona wanafanya makumi ya madhambi na mambo yasiyokubalika kidini! Fauka ya hayo hakuna hoja yoyote ya kimantiki katika uombezi na uokozi wao. Msingi wa Ukristo - kwa mujibu wa kile ambacho ni mashuhuri - umejengeka juu ya amani na upendo; lakini nyinyi tazameni katika ulimwengu wa Magharibi ndiko ambako kunatokea chanzo cha vita vingi, ndiko kunakoshuhudiwa chuki na ukosefu wa mapenzi, kuongezeka khiyana na usaliti, mauaji na jinai; katika hali ambayo inadaiwa huko ndiko kuliko na imani ya Kikristo! Kwa msingi huo ni wazi kwamba, msingi wa kazi zao umewekwa ili kuitenganisha jamii na kuiweka mbali na mafundisho ya dini yao.

Katika ulimwengu wa Magharibi - kwa mujibu wa takwimu zao wenyewe, - umri wa waraibu na watumiaji wa madawa ya kulevya unazidi kushuka kuna wakati ulikuwa miaka 18 na kisha ukawa miaka 16 na sasa umekuwa miaka 13! Kiwango hicho hicho kimekuwa kikishuhudiwa katika jinai, upuuzaji na kutojali mambo, kupuuzwa maadili ya kijamii na kifamilia kama baba na mama… Yote hayo ni matunda ya wa kuwatenganisha na kuwaweka mbali wanajamii na mafundisho ya Nabii Isa Masiya (AS).

Tunaweza kusema kwamba mwanaadamu amefanikiwa kupata nguvu za atomiki na asizitumie silaha za atomiki kwa ajili ya uharibifu, vifo na mauaji ya umati lakini kwa sharti kwamba teknolojia hiyo iwe katika mamlaka na milki ya watu ambao wanaheshimu na kufuata misingi ya akhlaqi, maadili na dini na wawe ni watu wenye imani. Laiti hayo yangelikuwa mikononi mwa watu wa aina hiyo, hali isingekuwa hivi ilivyo hivi sasa; lakini watu hao hawakuwa hivyo, na kwa utaratibu huo hili halijawa na hapo ndipo tunapoona ni kwa kiasi gani mataifa yametaabika na kukumbukwa na masaibu!

Inapita takriban miaka 50 sasa tangu kugunduliwa kwa bomu la atomiki duniani; lakini hadi sasa woga wa uwepo wa bomu la nyuklia ulimwenguni ungali hai katika nyoyo za watu ambao wanalifahamu hilo na inavyoonekana hali hiyo itaongezeka na hakuna uwezekano wa hali hiyo kupungua. Hivi karibuni vyombo vya Kikristo duniani vilitoa takwimu zinazobainisha kwamba, katika karne za hivi karibuni, Wakristo wameuawa kuliko kipindi chochote kile cha Ukristo; mimi nilikuwa na hamu kubwa ya kumuuliza aliyetoa takwimu hizi kwamba, Wakristo hao waliuawa na akina nani? Je ni Waislamu ndio waliowauwa Wakristo hao? Je ni Mabudha ndio waliowauwa Wakristo hao? Au ni Wakristo wenyewe ndio waliowauwa wenzi wao? Katika vita vya kwanza na vya pili dunia wananchi wa Ulaya waliuawa na akina nani? Ni Wakristo ndio waliouwana wao kwa wao. Ni watu wa Ulaya wenyewe, walikuwa ni Wamagharibi wenyewe ndio waliowaangamiza Wakristo hao na ni wao ndio ambao mbali na kuangamiza Wakristo wengi, wameangamiza pia wasiokuwa Wakristo na wasiokuwa watu wa Ulaya! Haya ndiyo matunda ya kuweko pengo la umaanawi na ni hivi ndivyo hivi pengo hilo linavyokuwa na maafa makubwa na matokeo mabaya kama haya. Mfumo wa Kiislamu wa Iran unataka kuionyesha dunia kizazi chenye mfano na uthibitishe kivitendo kwamba, inawezekana kulifuatilia hili na kupata elimu na kisha kuitumia elimu hiyo kwa ajili ya manufaa ya mwanaadamu kadiri inavyowezekana na wakati huo huo, kufungamana na dini na thamani za kiakhlaqi na kimaanawi.

Juu ya ukurasa

Madai ya Uongo

Leo hii watu wengi ambao wanapiga makele kuwa ni wafuasi wa Nabii Isa (AS) wamekwenda njia isiyokuwa ya Nabii Isa (AS). Gharadhi ya mafundisho ya Nabii Isa bin Maryam (AS) ni kuongoza kuelekea kwenye kumuabudu Mwenyezi Mungu na kukabiliana na mafirauni pamoja na mataghuti. Hii leo kuna watu ambao wanatoa madai ya kumfuata Mtume huyo mkubwa wa Mwenyezi Mungu katika hali ambayo wanaongoza ufirauni na utaghuti uliokuwa ukipigwa vita na Nabii Isa (AS). Watu wenye satua wamekuwa wakitumia jina la Masihi Isa na kidhahiri wamekuwa wakionyesha kuwa wanaamini mafundisho ya Nabii Isa AS; lakini katika muamala wao hawatekelezi hata kidogo mafundisho hayo. Dini ya Mwenyezi Mungu na akhlaqi za zilizoamrishwa na Mwenyezi Mungu katu hazionekani katika vyombo vyao vya utawala wa kisiasa vinavyotawala ulimwengu wa Kiistikbari - ulimwengu wa dhulma, ulimwengu wa Kibeberu kwa maana halisi ya neno, dunia ya uvamizi na kukiuka haki za wengine na ulimwengu ambao umekuwa ukitumia elimu kadiri uwezavyo kwa ajili ya kufanya jinai zote hizi.

Hii leo elimu iko mikononi mwa watu ambao hawajui chochote kuhusiana na ubinaadamu. Elimu na teknolojia iko kwa ajili ya kuhudumia malengo ambayo mia kwa mia ni kwa madhara ya jamii ya mwanaadamu na kwa maslahi ya matajiri, wenye fedha na wenye nguvu na satua.

Juu ya ukurasa

Mlango wa Nne: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wafuasi wa Ukristo Walio Wachache

Taathira ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa Ulimwengu wa Kikristo

Mapinduzi yetu si tu kwamba yaliwafanya Waislamu wazidi kuithamini dini yao ya Kiislamu, bali yalikuwa mazuri pia kwa Ukristo. Mapinduzi yetu yamezifanya nchi ambazo kwa miaka mingi zilikuwa mbali na dini yao ambayo ni Ukristo, zirejee upande wa umaanawi na kuheshimu dini. Kiwango hiki hiki kikapelekea kusambaratika Kambi ya Mashariki na jengo la utawala wa Kimaksi ulimwenguni. Ni kwa kiwango gani tukio hili lilikuwa la kustaajabisha na ni kwa namna gani lilikuwa na engo kubwa na pana? Nafasi isiyo ya kawaida ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo ni kutokana na kwamba, imesimama kidete mbele ya ulimwengu ambao nguvu na uwezo wa kimaada uko mikononi mwa mielekeo ya kupinga mafundisho ya Mitume na ambao hauna imani yoyote na aklaqi, umaanawi na dini - na huu ndio uhakika wenyewe.

Juu ya ukurasa

Kuishi Kwa Amani Wafuasi wa Dini Tofauti Nchini Iran

Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umepelekea kuweko maelewano na kuishi pamoja kwa salama na amani wafuasi wa dini mbalimbali; wakiwemo Mayahudi, Wakristo na Wazartoshti hawa wote wanaishi kando ya Waislamu na katika kivuli cha mfumo wa Kiislamu na wanashirikiana na mfumo unaotawala bila ya matatizo yoyote.

Hata hivyo wana majukumu pia; serikali ya Kiislamu nayo ina jukumu mbele ya watu hao wakiwa kama raia wa Kiirani, majukumu ambayo inapaswa kuyatekeleza na imekuwa ikiyatekeleza. Mfumo wa Kiislamu hauna malalamiko yoyote kwa raia wake hao wafuasi wa dini za wachache nchini.

Wairani hao hutoa tamko mara moja kila zinapozuka propaganda za uongo dhidi ya uhakika huo. Tumeshuhudia Waarmenia wa Iran au baadhi ya makundi mengine ya Kikristo yakitoa matamko mbalimbali kuitetea na kuihami Jamhuri ya Kiislamu na kwa hakika hizi ni miongoni mwa fakhari za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Juu ya ukurasa

Kuwa Pamoja na Wananchi Wenzetu wa Kikristo

Nina furaha kubwa kutokana na kuwa ndugu zetu na wananchi wenzetu Wakristo wanahisi kwamba, wana amani, utulivu, furaha na kuishi katika hali ya kuridhika, na wakiwa pamoja na wananchi wenzao wanajishughulisha na kazi zao, kwa hakika tuna furaha mno na kimsingi hili ndilo ambalo tunalitaka sisi. Sisi tunataka kuona kwamba, wafuasi wa dini za walio wachache katika nchi yetu, iwe ni Wakristo, Mayahudi na Wazartoshti wajihisi kwamba, wana amani na utulivu na wanapata haki zao zote kama raia, na hili Alhamdulilah limetendeka na bila ya shaka nyinyi munalishuhudia hili. Aidha tunashukuru mno na tuna furaha kutokana na hatua yenu ya kuonyesha huzuni, ghamu na masikitiko yenu kufuatia mtetemeko wa ardhi wa Bam. Kimsingi hivi ndivyo inavyopaswa kuwa.

Katika kipindi cha miaka minane ya kujihami kutakatifu, Waarmenia wa Iran walikuwa na nafasi muhimu katika uwanja wa mapendekezo ya kiufundi; kwani Waarmenia wanaoishi mjini Tehran na katika maeneo mengine hapa nchini wamebobea katika masuala ya kiufundi. Mimi hata kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu nilikuwa na taarifa na ufahamu wa karibu kuhusiana na kazi za Waarmenia na nilikuwa nikifahamu kwamba, wamebobea katika masuala ya motokari, ufundi na spea za magari. Katika kipindi cha vita pia walikuja na kutwambia kwamba, tumekuja kufanya kazi. Mwaka 59 au 60 (kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani) walikwenda katika mji wa Ahwaz na kuweka kambi huko; mimi nilikwenda na kutembelea kambi yao. Kuna siku pia tulikuwa tukitoka Tehran kuelekea Ahwaz, nikaona takriban watu mia moja wa jamii ya Waarmenia na walitwambia kuwa, sisi tunaelekea vitani; tuchukueni na sisi vitani. Mimi nikatoa agizo wapandishwe kwenye ndege na kupelekwa vitani. Hivyo basi, hakuna la kustaajabisha kwetu kwamba, nyinyi katika msiba wa Bam mulitoa matamshi kama haya. Hata hivyo mimi nina mawasiliano na maingiliano binafsi na baadhi ya familia za Kiarmenia na Kiashuri mjini Tehran na kwa kuwa watoto wao waliuawa shahidi vitani basi tuna uhusiano wa karibu na nilikuwa nikienda majumbani mwao na ninafahamiana nao; na ninafahamu kwamba, wana hisia nzuri kuhusiana na nchi yao na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Inshallah Mwenyezi Mungu akupeni nyinyi tawfiki na sisi pia, ili tuweze kwenda katika njia sahihi. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujumuishe sote katika rehma, hidaya na mapenzi Yake. Tufikishieni pia salamu zetu za pongezi na baraka kwa ndugu na marafiki wa Kiarmeni kwa mnasaba wa kukumbuka kuzaliwa Nabii Isa Mashi (AS). Inshallah, nakutakieni mafanikio mema.

Juu ya ukurasa

Hisia za Kupendana na Kuwa Karibu

Mimi binafsi ninawapenda na niko karibu na Waarmenia wa Iran. Sisi tunawapenda Wafuasi wa Nabii Isa AS. Katika kipindi chote cha Mapinduzi na vita vya kulazimishwa, Waarmenia walitusaidia sana. Bila ya shaka nyinyi mumesikia hili, lakini mimi nimelishuhudia kwa macho yangu tena kwa karibu. Mimi katika medani ya vita niliwaona Waarmenia wengi ambao wakiwa na mapenzi maalumu na kwa hima walikuwa wakisaidiana na sisi tena chini ya mvua na katika pirika pirika za kurushwa makombora na mizinga.

Tena hili linahusiana na watu ambao hata hawakuwa askari; bali walikuwa ni watu wa kawaida tu ambao walijitolea kwa moyo wao na kwenda vitani. Sisi kwa upande wetu tunaamiliana na wafuasi wa dini za walio wachache nchini kama tunavyoamiliana na ndugu zetu, tunaamiliana nao kirafiki na kwa muamala mzuri kabisa na wa kibinadamu. Tunakwenda hata katika nyumba zao. Binafsi kwa miaka kadhaa kikawaida mimi huenda katika nyumba za familia mashahidi wa Kikristo kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka mpya wa Kikristo. Kwetu sisi ni sawa tu mtu huyo awe ni Muashuri au Muarmenia, tunakwenda katika nyumba yake; tunakaa pamoja nao na kuzungumza nao huku tukila nao pamoja.

Juu ya ukurasa

 
< Nyuma   Mbele >

^