Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hija kwa Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Chapa
23/11/2009

Sifa Maalumu ya Hija

Maarifa, Hidaya ya Kwanza ya Hija
Hija Nembo ya Umma wa Kiislamu
Sifa Maalumu ya Kipekee
Kushikamana Kitaifa na Kimataifa
Kutatua Matatizo ya Jamii za Kiislamu
Mahudhurio Yenye Maana Maalumu

Upeo wa Kimaanawi wa Hija 

Adabu za Hija
Uzoefu wa Kimaanawi
Kukomboka na kuwa Huru kutoka katika Madhihirisho ya Majivuno
Fursa ya Kujijenga Kinafsi
Ibada ya Kupambana na Mghafala
Hija ya Nabii Ibrahim
Safari ya Kimwili na Kiroho

Malengo Jumla ya Hija

Kuchunguza Masuala Muhimu ya Ulimwengu wa Kiislamu
Mshikamano wa Waislamu na Woga wa Mabeberu
Ujumbe wa Tawhidi na Umoja
Malengo ya Pande Zote ya Hija
Kuwa Mbali na Malengo

Hija Sababu ya Kupatikana Umoja

Uadhama wa Hisia za Umoja
Maana ya Mkusanyiko huo Adhimu
Kutumiwa Vibaya Wenzo wa Umoja
Vizuizi katika Njia ya Umoja
Njama za Wakoloni za Kuzusha Mifarakano

Kujibari na Kujiweka mbali na Washirikina

Nguzo Kuu ya Hija
Fursa ya kuwa na Muono wa Mbali
Moyo Unaotawala Amali ya Hija
Kupinga Kujibari

Hija kwa Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu


Sifa Maalumu ya Hija

Maarifa, Hidaya ya Kwanza ya Hija

Ijapokuwa baraka za Hija zinavienea vipengee vyote vya maisha ya mwanadamu, na ijapokuwa mvua hiyo ya rehema isiyo na kikomo inaeneza baraka zake zisizo na mwisho kwenye maisha binafsi ya mwanaadamu ya kiroho na kwenye fikra za kiumbe huyo hadi kwenye upeo wa kisisa na kijamii na katika upande wa nguvu za kitaifa za Waislamu na ushirikiano baina ya mataifa yote ya Kiislamu, lakini pengine tunaweza kusema kuwa ufunguo wa yote hayo na uhakika wake, ni maarifa. Hidaya ya kwanza kabisa ya Hija kwa mtu anayetaka kujua uhakika wa mambo na kufaidika ipasavyo na nguvu kubwa aliyozawadiwa na Mwenyezi Mungu ya kumuwezesha kuelewa uhakika wa matukio na mambo mbalimbali, ni maarifa na utambuzi wake wa kipekee ambao kwa kawaida hauwezi kupatikana sehemu nyingine yoyote isipokuwa katika Hija. Ni hija ndiyo inayoipa uwezo huo idadi kubwa ya Waislamu na hakuna tukio lolote la kidini duniani linaloweza kumzawadia kwa wakati mmoja mwanaadamu, kiwango kikubwa cha maarifa kama inavyofanya Hija.

Juu ya ukurasa

Hija Nembo ya Umma wa Kiislamu

Msimu wa Hija unapowadia kila mwaka huja na shauku na hali maalumu ya kipekee na huzipa nyoyo zenye mapenzi na matumaini za Waislamu wote ulimwenguni hisia za aina yake za kuona kwamba wakati wa kwenda katika Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu umewadia. Waislamu hupata shauku kubwa ya kuona umefika wakati wa kwenda kufanya ibada katika maeneo matakatifu na kwenda kuweka mapaji yao ya uso juu ya ardhi takatifu kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mola wao. Ni siku maalumu ambazo watapata fursa ndani yake ya kuwa chini ya kivuli cha dhikri na kunong’ona na Muumba wao na kujibidiisha kiibada mbele ya kimbilio la rehema na maghufira. Wanahisi zimefika siku za kwenda kuonana na ndugu zao kutoka pande zote nne za dunia na kutoka katika maeneo ya mbali; na kwa njia hiyo kuuona utukufu wa uma wa Kiislamu kwa macho yao, na kuishi ndani ya uadhama huo kimwili na kihisia.

Hija ni nembo ya umma wa Kiislamu. Ni chuo cha kufundisha watu namna ya kuishi na kuamiliana na wengine. Inatoa funzo la namna umma mkubwa unavyopaswa kuendeana na wengine kwa ajili ya kujidhaminia ufanisi wake. Inawezekana kuiongoza Hija kwenye lengo moja kuu kwa kutumia harakati yenye shabaha maalumu na kwa muono mpana na wa namna kwa namna wa Waislamu wote. Lengo la muundo wa harakati hiyo ni kuwafanya Waislamu wamkumbuke Mwenyezi Mungu wakati wote na washikamane vilivyo. Makusudio ya harakati hiyo ni kuunda kambi madhubuti ya kimaanawi kwa ajili ya maisha ya furaha na ufanisi kwa wanaadamu wote. Mwenyezi Mungu anasema:

 جَعَلَ اللَّهُ الْكَعْبَةَ الْبَيْتَ الْحَرَامَ قِيَامًا لِّلنَّاسِ وَالشَّهْرَ الْحَرَامَ وَالْهَدْيَ وَالْقَلائِدَ ذَلِكَ لِتَعْلَمُواْ أَنَّ اللَّهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ وَأَنَّ اللَّهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

Mwenyezi Mungu ameifanya al Kaaba, hii Nyumba Tukufu, ni simamio la watu, na kadhaalika Miezi Mitukufu, na wanyama wa dhabihu, na vigwe. Hayo ili mjue ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo katika ardhi, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. al Maida (5:97).

Juu ya ukurasaaa

Sifa Maalumu ya Kipekee

Ijapokuwa siri iliyojificha ndani ya Hija na manufaa ya amali hiyo ni makubwa mno na si rahisi kwa mtu kuweza kuyataja yote lakini kati ya manufaa hayo mengi kuna sifa maalumu ya kipekee ambayo kila jicho linaloona mbali linaweza kuiona kwa kuangalia mara moja tu. Sifa ya kwanza ni kwamba Hija ndiyo ibada pekee ambayo ndani yake Mwenyezi Mungu anawataka Waislamu wote, kwa kila mwenye uwezo kati yao kutoka katika kila kona ya dunia kwenda kukusanyika mahala pamoja na huku wakiwa katika siku maalumu waweze kufanya juhudi na harakati aina kwa aina kwa umoja wao. Naam, waweze kuungana na kufanya ibada kwa pamoja katika sehemu za ibada zinazohitajia utulivu, katika visimamo na katika vikao vyao ndani ya ibada. Mwenyezi Mungu anasema:

 ثُمَّ أَفِيضُواْ مِنْ حَيْثُ أَفَاضَ النَّاسُ وَاسْتَغْفِرُواْ اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

Kisha miminikeni kutoka pale wanapomiminika watu, na muombeni Mwenyezi Mungu msamaha; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. al Baqarah (2:199).

Juu ya ukurasaa

Kushikamana Kitaifa na Kimataifa

Wakati sehemu fulani ya watu wa taifa moja wanapofunga safari kwa pamoja kuelekea kwenye sehemu maalumu kwa lengo moja na kisha kurejea makwao bila ya shaka yoyote mshikamano baina yao kutaka na kukataa unakuwa mkubwa na kiwango cha umaanawi, akhlaki na maadili mema ya kitaifa kinaongezeka kati yao. Hilo halishuhudiwi katika upeo wa kitaifa tu, bali linajitokeza pia katika upeo wa kimataifa na sababu ni kuwa mataifa yote duniani yana mambo yanayofanana kama ambavyo yana pia mambo yanayotofautiana. Mambo hayo yanayowatofautisha, baadhi ya wakati huwapelekea kutengana na kuzuka hisia za chuki baina yao. Sasa katika mazingira kama hayo Hija hupelekea hitilafu hizo kufifia sana na badala yake hupata nguvu yale mambo ya pamoja yanayoyashirika mataifa mbalimbali. Ndio maana tukasema hatuna sisi wanaadamu ibada yoyote ile yenye upeo mpana na uadhama mkubwa kama Hija.

Juu ya ukurasa

Kutatua Matatizo ya Jamii za Kiislamu

Sifa zote njema na hamdu zote zinamstahikia Mwenyezi Mungu Mtukufu Ambaye amewaneemesha waja Wake na kuwataka wawe wanakusanyika kwa pamoja kila mwaka katika Nyumba Yake Takatifu kwa ajili ya ibada maalumu. Ambaye amemwamrisha Mtume Wake kutoa mlingano wa adhana ya Hija na kuwaita watu kutoka kila kona ya dunia; Ambaye ameifanya Nyumba ya Mwenyezi Mungu kuwa salama na eneo la amani kwa waishio ndani yake na watu wa mbali, akaitakasa na masanamu yote ya kipindi cha ujahilia na kuifanya ni eneo la kutufu waumini na sehemu inayokusudiwa na watu wa mbali na wa karibu. Akaifanya Nyumba hiyo kuwa dhihirisho la udugu na ujamaa, bainisho la mapenzi na eneo la kujumuika kwa wingi umma wa Kiislamu. Baytullah ambayo ni kibla cha Waislamu, na eneo la kufanya amali za kutufu na Saai, wakati wa ujahilia wa kwanza ilifanywa kuwa soko la biashara, na marikiti ya kuonyesha umwinyi na uluwa wa watu wa eneo hilo na licha ya kuweko watu waliotaka kudhibiti kila jambo, lakini watu waliofika katika eneo hilo tukufu walikuwa na haki sawa na wenyeji wao kila walipoingia ndani ya eneo hilo. Hija ni nembo ya umoja na utukufu wa Waislamu. Ni ibada inayowashikamanisha na kuwafanya kuwa kitu kimoja Waislamu. Hija ina uwezo wa kuondoa masaibu na matatizo mengi yanayowakabili watu na jamii za Waislamu masaibu ambayo yanatokana na Waislamu wenyewe kujiweka mbali na misingi na matukufu yao. Matatizo yanayowakabili Waislamu hivi sasa ni kama vile kupenda mambo ya wageni, kudharau na kusahau yaliyo yao, kila mmoja wao kumwangalia mwenzake kwa jicho baya pamoja na kusikiliza kila wanacholishwa na kuamrishwa na maadui wao wa pamoja. Msiba mwengine unaowakabili Waislamu ni kutoguswa na kutokuwa na hisia zinazotakiwa kuhusiana na mustakbali wa umma wa Kiislamu bali hawajui mambo jumla yanayounda umma wa Kiislamu na hawana habari na matukio na hali ilivyo katika nchi zao za Kiislamu. Waislamu leo hii hawako macho na hawaonyeshi uelekevu unaofunzwa na dini yao katika kukabliana na njama za maadui wa Uislamu na Waislamu. Bali kuna na masaibu mengine mengi hatari ambayo yameshuhudiwa yakiwakabili Waislamu katika kipindi kizima cha historia kutokana na nchi zao kudhibitiwa na watu baki na kutokana na Waislamu kujiweka mbali na mafundisho ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao ya kisiasa na katika kuainisha mustakbali wao. Misiba hiyo imekuwa ikiutishia umma wa Kiislamu na imeongezeka na kuchukua mkondo wa sura mbaya zaidi katika karne za hivi karibuni tangu madola makubwa ya kikoloni yalipovamia maeneo ya Waislamu, na tokea eneo hili nyeti lilipoingiliwa na maadui walioweka vibaraka wao waabudu dunia na wasioheshimu dini katika kila sehemu ya eneo hili.

Juu ya ukurasa

Mahudhurio Yenye Maana Maalumu

Mahudhurio ya Waislamu katika amali ya Hija inabidi yawe na maana yake inayotakiwa kwani kama lengo la Hija lingelikuwa ni Waislamu kushiriki kwenye amali hiyo tukufu kwa ajili tu ya kufanya mambo ya kiroho, kimaanawi na kumtaja Mwenyezi Mungu kwa dhikri na ibada nyinginezo, Waislamu wangeliweza kufanya ibada hizo hata ndani ya nyumba zao. Hivyo kuna hekima na maana maalumu ya Mwenyezi Mungu kuwaamrisha Waislamu wakusanyike mahala pamoja kwa ajili ya ibada. Hekima yake hasa ni yale manufaa ambayo Waislamu wanatakiwa kuyashuhudia katika kipindi kizima cha amali ya Hija. Kwa hakika Hija inaweza kuleta mabadiliko ya ndani ya moyo wa kila Muislamu na kumtunuku nguvu na moyo wa tawhidi, kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuwa na mfungamano wa karibu na Allah kama ambavyo inaweza pia kuviunganisha pamoja viungo vililivyotenganishwa vya umma wa Kiislamu na kuvifanya kuwa mwili mmoja madhubuti na wenye nguvu kubwa. Hija inawapa fursa Waislamu kutambuana na kuelezana masaibu yao na pia kujadiliana njia za kujiletea maendeleo na kusaidiana katika kutatua matatizo yanayowakabili Waislamu wa maeneo tofauti. Tunaweza kusema kwa uwazi kabisa kwamba amali hii tukufu ya Kiislamu kama itatumiwa vizuri, pekee inaweza kumudu baada ya muda si mrefu kuufanya umma wa Kiislamu uweze kupata heshima yake, uwe na nguvu na uweze kutatua matatizo yake mengi.

Hija katika asili na dhati yake ina sifa mbili kuu, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kifikra na kiamali na kujiweka mbali na taghuti na shetani kwa mwili na kwa roho. Amali na vitendo vyote vinavyotendeka katika ibada ya Hija vinafanyika katika kalibu ya sifa hizo mbili maalumu na kwa kweli huo ndio muhtasari wa mafundisho ya Kiislamu na miongozo ya Mitume na Manabii wote.

Juu ya ukurasa

Upeo wa Kimaanawi wa Hija

Adabu za Hija

Wameghafilika kukubwa kulioje wale watu ambao wanaitumia ibada ya Hija na siku za kuhiji na kipindi cha kutekeleza amali tukufu ya Hija kama wenzo wa kujinufaisha kwa masuala ya kidunia na hivyo kufifiliza ile sifa maalumu ya Hija. Inabidi amali ya Hija itekelezwe kwa umakini, kwa kuuhudhurisha moyo na kwa adabu na desturi yake maalumu. Mbali na ibada ya Hija na amali zinazotekelezwa na Waislamu ndani yake, kuna adabu na nidhamu maalumu ndani ya ibada hiyo tukufu na ndiyo roho na moyo wa Hija. Kuna baadhi ya Waislamu wanatekeleza amali hizo za ibada ya Hija, lakini wanaisahau ile roho na ule uhakika wa ibada hiyo. Adabu ya Hija ni unyenyekevu, dhikri na mazingatio. Adabu ya Hija ni hujaji kuhisi kuwa yuko mbele ya Mwenyezi Mungu katika lahadha na sekunde zote. Adabu ya Hija ni kuomba hifadhi katika mamlaka iliyojaa amani ya Mwenyezi Miungu mamlaka ambayo Allah amewaandalia waumini wanaoshikamana na kujikabidhi kwa Dhati Takatifu ya Mwenyezi Mungu. Inabidi kuitambua na kuidiriki vilivyo bustani hiyo na anapaswa muumini aingie ndani yake kikamilifu. Inabidi Hija ieleweke hivyo. Adabu ya Hija ni kuishi kwa salama na amani. Ni jambo lililopigwa marufuku kukandamiza waumini na kugombana na ndugu zake mtu. Ni marufuku pia kufanya uasi na ugomvi katika Hija. Adabu ya Hija ni kuzama katika maana ya kweli ya Hija na kuitumia vilivyo ibada hiyo katika kipindi chote cha maisha ya Waislamu. Adabu ya Hija ni kudumisha udugu na kupendana, kushikamana na kuwa kitu kimoja. Hija ni fursa ya kuleta umoja kati ya mataifa ya Kiislamu. Mshikamano kati ya matabaka na mataifa mbalimbali ya Waislamu unaweza kupatikana tu kupitia amali ya Hija. Kundi kubwa mno la watu kutoka kila pembe ya dunia wanamiminika katika maeneo matakatifu huko Makka na Madina kutokana na mapenzi yao makubwa kwa al Qaaba, mapenzi yao makubwa kwa eneo aliloishi na kuzikwa Bwana Mtume, na kutokana na hamu yao kubwa ya kumtaja Mwenyezi Mungu na kwa mapenzi yao makubwa ya kutufu na kwenda Safa na Marwa. Kwa kweli inabidi itumiwe kikamilifu fursa hiyo muhimu mno ya kujenga udugu na mapenzi kati ya Waislamu.

Juu ya ukurasa

Uzoefu wa Kimaanawi

Hija kwa kila hujaji ni fursa ya kuingia katika anga isiyo na kikomo ya kimaanawi. Hija humtoa Muislamu kutoka katika vipengee vyote vya maisha yake ya kawaida yaliyochafuliwa na mambo mbalimbali na kutoka katika maisha yake yaliyojaa matatizo na mashaka na kumuingiza katika anga safi iliyojaa unyofu ya kimaanawi na kujikurubisha kwa Mola Muumba. Hija humpa fursa hujaji ya kufanya riadha na mazoezi hayo kimaanawi. Tangu Muislamu anapoingia katika amali ya Hija, vitu vyote ambavyo katika maisha yake ya kila siku huwa ni mubaha na yanaruhusiwa, hujitenga nayo ndani ya kipindi cha kuhiji. Mengi ya mambo hayo ingawa yanaruhusiwa, lakini baadhi ya wakati huwa chanzo cha mghafala na mengine hata huwa kiini cha kuporomoka pale mtu asipokuwa macho.

Kukomboka kutokana na uchafu wa mambo ya kimada na kumuona Mwenyezi Mungu katika kila kitu ijapokuwa kwa siku chache, ni akiba kubwa kwa mwanaadamu. Adabu na matendo yote yaliyomo katika amali ya Hija yamewekwa kwa ajili ya kuwa hujaji apate uzoefu huo wa kimaanawi na apate utamu na ladha ya kuvutia ya utukufu huo, mdomoni na moyoni mwake.

Umaanawi unaopatikana katika Hija ni hii dhikri na kumtaja Allah jambo ambalo mithili ya roho, limejikita katika kila hatua na kitendo cha amali ya Hija. Chemchem hiyo iliyojaa baraka inabidi iendelee kuchemka hata baada ya kumalizika amali ya Hija. Inabidi matunda yanayopatikana katika Hija yapewe nafasi ya kuendelea hata nje ya ibada hiyo.

Juu ya ukurasa

Kukomboka na kuwa Huru kutoka katika Madhihirisho ya Majivuno

Mambo yote yanayosababisha majinato, majivuno na usodawi humwondokea Muislamu katika Hija na mosi ni libasi na nguo zake. Cheo, uliwa, ukuu, mavazi na nguo za fakhari na vitu vyote kama hivyo huwekwa pembeni na kila mmoja unamuona katika vazi moja. Usijiangalie katika kioo wakati wa kuhiji kwani kufanya hivyo kunaweza kukufanya uingie ndweo, kiburi na majinato. Usitumie uturi na manukato kwani hivyo ni vitu vinavyoweza kukuletea majivuno. Usikimbilie kivulini kukwepa jua na wala usikimbie mvua wakati unapotembea kwani huko ni kuonyesha kupenda raha na starehe na mambo mengine kama hayo. Yote hayo ni mambo ambayo yanakuwa haramu kwa hujaji baada ya Ihram na ni mambo ambayo ni chanzo cha matamanio ya nafsi na kijinsia. Mahujaji wanajinyima yote hayo kwani ni nembo za majivuno na usodawi, bali ni chemchemu ya ubaguzi. Mambo yote hayo anakatazwa kuyatenda hujaji baada ya Ihram.

Juu ya ukurasa

Fursa ya Kujijenga Kinafsi

Hatua ya kwanza kabisa wanayoipiga mahujaji katika Hija ni kujijenga kinafsi. Ihram, kutufu, sala, Mash’arul Haram, Arafa na Mina, kuchinja, kumpiga mawe shetani na kunyoa yote hayo yamewekwa kwa ajili ya kumfanya hujaji awe mnyenyekevu na ajue udhaifu wake mkubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na pia ajue umuhimu wa dhikri, unyenyekevu na kujikurubisha kwa Allah. Si sahihi hata kidogo kughafilika na amali hizo zilizojaa maana na zenye umuhimu mkubwa. Anayesafiri kuelekea kwenye maeneo matakatifu ya ibada ya Hija anapaswa kujihisi na kujiona yuko mbele ya Mwenyezi Mungu katika amali zote za ibada ya Hija. Licha ya kwamba huwa yuko katikati ya mamilioni ya mahujaji wenzake, lakini hujaji anatakiwa ajihisi kwamba yuko peke yake na Muumba wake tu, ampige teke kikamilifu shetani na hawaa za nafasi na kusafisha takataka zote za husda, tamaa, woga, muhu na hanjamu za nafsi. Anatakiwa amshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na uongofu Wake, auimarishe moyo wake kwa ajili ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, atie nia ya kuwa mpole kwa waumini wenzake na ajitenge na maadui wao. Aazimie kikweli kweli kukabiliana na maadui wa haki na atie nia ya kujijenga kinafsi na kusimama kidete katika jitihada za kutengeneza yaliyomzunguka. Afunge mkataba na Mwenyezi Mungu wa kujenga dunia na Akhera yake.

Hija ni fursa kubwa ambayo tunaweza kuitumia kubainisha uhakika huo na uhakika mwingine mwingi mfano wake ambapo kwa baraka za maarifa ya Kiislamu na uongofu wa dini hii takatifu tuliotunukiwa sisi taifa la Kiislamu la Iran tunaweza kuyafikisha hayo kwa walimwengu na kutumia jambo hilo kuwaamsha. Kuna watu wengi wameamka katika ulimwengu wa Kiislamu na inabidi tuhakikishe kwamba Waislamu walioamka wanapata hisia kwamba wana wafuasi katika kila kona ya ulimwengu wa Kiislamu ili kwa njia hiyo waweze kupata nguvu, ujasiri na ushujaa unaotakiwa. Yote hayo yanawezekana chini ya kivuli cha kimaanawi cha Hija. Hivyo msighafilike wala msisahau kutumia vyema umaanawi wa Hija, na maarifa aali yaliyomo katika dua, ziara na aya tukufu za Qur’ani.

Juu ya ukurasa

Ibada ya Kupambana na Mghafala

Hija ni fursa ya kipekee. Ibada zote ni fursa kwa mwanaadamu ya kujijua dhati yake na kuondoa usahaulifu ndani ya nafsi yake. Kutokana na kumsahau Mwenyezi Mungu Mtukufu Ambaye Ndiye Haki ya kweli na Muumba na Msimamizi wa kila kitu, wanaadamu hukumbwa na ugonjwa wa mghafala na kusahau uhakika na dhati yao. Mwenyezi Mungu anasema:

 ولا تكونوا كالذين نسوا الله فانساهم انفسهم اولئك هم الفاسقون

Wala msiwe kama wale waliomsahau Mwenyezi Mungu, na Yeye akawasahaulisha nafsi zao. Hao ndio wapotovu. (al Hashr 59:19)

Hili ndilo tatizo kubwa linalowakabili wanaadamu hivi sasa. Wanaadamu leo hii wamejisahau kutokana na kumtaghafali na kumsahau Mwenyezi Mungu. Mahitaji ya mwanaadamu, uhakika wa mwanadamu na malengo ya kuumbwa mwanaadamu yamefunikwa kabisa na mambo ya kidunia na kupelekea kusahauliwa kikamilifu. Vitu ambavyo vinaweza kumfanya mwanaadamu asighafilike na amkumbuke Mwenyezi Mungu wakati wote kwa kujua uhakika wake, malengo ya kuumbwa kwake na dhati ya moyo wake, ni dua, ibada na unyenyekevu wake mbele ya Mwenyezi Mungu. Hija ni ibada bora kabisa ya kuweza kumfikisha huko mwanaadamu kwani muda aliowekea hujaji, eneo analofanyia ibada hiyo, harakati na amali zenyewe za Hija; kila kimoja kinaifanya ibada hiyo kuwa ya kipekee. Mwanaadamu huhisi kuwa na amani na usalama moyoni mwake kutokana na unyenyekevu, mazingatio, uchaji na kuzama kwake katika kumdhukuru na kunong’ona na Mola wake katika ibada hiyo adhimu na ya aina ya kipekee. Hayo ndiyo mahitaji na ndilo jambo kubwa linalotakiwa na mwanaadamu; utulivu wa nafsi. Madola yaliyojiweka mbali na masuala ya kidini na kimaanawi yamemletea mwanadamu jahanamu isiyostahamilika. Mwanadamu anaweza kujikomboa kutoka katika jahanamu hiyo kwa kwenda katika amali ya Hija ambako ataweza kutabaradi na kupata tuo la nafsi ndani ya bustani hiyo ya amani na katika eneo hilo takatifu na kwenye wakati huo mahsusi aliotunukiwa na Mola Mlezi.

Naam, ni sawa kabisa kwamba Hija ni ibada na ni dhikri na ni dua na istighfari, lakini ibada, dhikri na istighfari hiyo inabidi izidi kuwatia nguvu Waislamu na kuwaletea maisha bora na kuwaokoa kutoka katika minyororo ya ukandamizaji na unyanyasaji ili siku baada ya siku Mwenyezi Mungu aweze kupuliza roho ya heshima na utukufu ndani ya umma wa Kiislamu. Ibada hiyo inapaswa kuwafanya Waislamu wawe imara na waondokewe na uvivu na kujipweteka. Hiyo ndiyo Hija iliyosimama kwenye misingi sahihi ya dini na ni Hija ya namna hiyo ndiyo inayotajwa na Amirul Muminin Imam Ali AS kwamba ni mbeba bendera ya Uislamu na jihadi ya kumtia nguvu kila asiye na uwezo na ndiyo ibada ya kuondoa umaskini na ufukara. Imam Ali AS anaitaja pia Hija kuwa ni ibada ya kuwakurubisha na kuwashikamanisha kikamilifu Waislamiu kutoka kila kona ya dunia.

Juu ya ukurasa

Hija ya Nabii Ibrahim

Hija ya Nabii Ibrahim AS ni ile Hija ambayo ndani yake Waislamu wanajiweka mbali na mifarakano na kupiga hatua kuelekea kwenye umoja na mshikamano. Wanakusanyika pamoja katika al Kaaba ambayo ni jengo la kuwakumbusha tawhidi na upweke wa Mwenyezi Mungu na ni nembo ya kujiweka mbali na washirikina na kuwachukia waabudu masanamu. Waislamu wanatakiwa kutekeleza ibada ya Hija kwa namna inayotakiwa, wanatakiwa watufu na kufanya amali za Hija kwa sura yake halisi ya batini na dhahiri na kuitumia ibada hiyo kwa ajili ya kuuletea uma wa Kiislamu manufaa yaliyokusudiwa.

Hija na Nabii Ibrahim AS ndiyo ile Hija ya Mtume Muhammad SAW ambayo ndani yake roho na dhati yake ni kuelekea kwenye tawhidi na umoja, mambo ambayo yanashuhudiwa katika amali na vitendo vyake vyote. Hija ni chemchemu ya baraka na uongofu na ni nguzo kuu katika maisha na uhai wa umma wa Kiislamu. Hija ni ibada iliyojaa manufaa na ni ibada iliyosheheni dhikri na kumtaja Mwenyezi Mungu. Hija ambayo ndani yake mataifa ya Kiislamu yataweza kuhisi uwepo wa umma mmoja wa Kiislamu unaotakiwa na Bwana Mtume Muhammad SAW na kuhisi udugu na kuwa kitu kimoja huyafanya mataifa hayo ya Kiislamu yasihisi kuwa dhaifu wala kushindwa na chochote katika juhudi za kujiletea ufanisi. Naam, Hija ya Nabii Ibrahim AS ni ile Hija ambayo ndani yake Waislamu wanajiweka mbali na mifarakano na kujikurubisha kwenye umoja na mshikamano.

Juu ya ukurasa

Safari ya Kimwili na Kiroho

Hija si safari ya starehe. Hija ni safari ya kimaanawi. Ni safari ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu kimwili na kiroho, naam kwa yote mawili, kimwili na kiroho. Kwa wacha Mungu safari ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu haiwi safari ya kimwili tu, bali huwa safari ya kiroho pia. Ndio maana tukasema safari ya Hija ya kwenda kwa Mwenyezi Mungu inabidi iwe safari ya kimwili na kiroho. Sasa kama tutakwenda kwa viwiliwili vyetu tu katika safari hiyo na tukaziacha roho zetu nyuma itakuwa hatukufanya lolote la maana. Mwenyezi Mungu hayuko pamoja na watu ambao kutokana na kushiriki sana katika amali hiyo tukufu na kutokana na kupata taufiki ya kwenda kuhiji na kuona kwa karibu Nyumba ya Mwenyezi Mungu, Hija kwao imekuwa jambo la kawaida tu lisilo athari na tofauti yoyote kwao na wala haiwaletei tena yale mapinduzi ya ndani ya nyoyo na ya kujenga nafsi. Hilo kwa kweli si jambo sahihi hata kidogo.

Hija ina sifa mbili kuu katika dhati na asili yake. Kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kifikra na kivitendo na kujiweka mbali na taghuti na shetani kimwili na kiroho. Amali zote zinazofanyika ndani ya Hija zinalenga katika mambo hayo mawili na hilo kwa hakika ndio muhtasari wa Uislamu na mafundisho ya Mitume wote wa Mwenyezi Mungu.

Juu ya ukurasa

Malengo Jumla ya Hija

Kuchunguza Masuala Muhimu ya Ulimwengu wa Kiislamu

Maudhui muhimu ambayo mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu wanapaswa kuihesabu kuwa ni moja ya malengo ya Hija ni masuala muhimu yanayoendelea katika ulimwengu wa Kiislamu. Kama Hija ni kongamano kubwa na adhimu la kila mwaka kwa Waislamu wote duniani, basi ni jambo lisilo na shaka kwamba suala muhimu na la kupewa kipaumbele cha kwanza katika kongamano hilo ni masuala ya Waislamu yaliyoko wakati huo katika kona yoyote ile duniani. Katika propaganda za mabeberu na wakoloni, suala hilo linazungumzwa kwa namna ambayo si tu haiyafanyi masuala hayo kuwa funzo la kuwaamsha Waislamu kote ulimwenguni lakini pia hata kama katika matukio hayo itakuweko nia mbaya na uadui wa mabeberu ndani yake, mambo hayo hayapelekei kufichuliwa wakosa wa kweli na baadhi ya wakati hata wakosa wenyewe hawajulikani kabisa. Hija inabidi iwe ni sehemu ya kufichuliwa usaliti wa kipropaganda, iwe ni sehemu ya kufichuliwa uhakika wa mambo na iwe ni uga wa kuwaamsha Waislamu na kuwafanya watetee vilivyo haki zao. Vipi moyo wenye kiu ya baraka za Kawthar ya Bwana Mtume Muhammad (SAW), wenye kiu na Zamzam ya Husain na ambao wana shauku ya kunywa katika chemchem hiyo iliyojaa baraka, wataendelea kuwa na ati ati na kutoamini malengo ya kisiasa ya Hija? Hija isiyo na kujibari na kujiweka mbali na washirikina, Hija isiyo na umoja na mshikamano, Hija isiyo na harakati wala istikamana, Hija ambayo haitakuwa tishio kwa ukafiri na shirki, hiyo si Hija kwa sababu itakuwa imekosa maana yake halisi ya Hija.

Juu ya ukurasa

Mshikamano wa Waislamu na Woga wa Mabeberu

Moja ya malengo makuu ya Hija katika Nyumba ya Mwenyezi Mungu ni kuwaunganisha Waislamu na kuwafanya kuwa kitu kimoja. Mwenyezi Mungu anasema: ***

 وَ أَذِّنْ فِي النَّاسِ بِالْحجّ يأْتُوک رِجالاً وَ عَلي‏ کلِّ ضامِرٍ يأْتينَ مِنْ کلِّ فَجٍّ عَميقٍ

Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali. (al Hajj – 22:27)

Waislamu kutoka kona zote za dunia hukusanyika pamoja katika siku maalumu na katika amali mahususi kama vile Arafa, Mash’ar, Mina na Masjidul Haram, sasa kwa nini mabeberu wanaogopa mno wanapowaona Waislamu hao wanafanya hayo kwa umoja wao, kwa nini wanaogopa wasije Waislamu wakaidiriki na kuitekeleza kivitendo falsafa ya amali hizo?! Suala ni kuwa mabeberu wanaogopa mshikamano wa Waislamu, wana hofu kuona Waislamu wanakuwa na fikra moja na misimamo mimoja. Mabeberu wakiongozwa na Marekani wanaona umoja wa Waislamu ni hatari kwa ukoloni na ubeberu wao ulimwenguni. Huo ndio uhakika ambao Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu awe radhi naye) alikuwa akiuzungumzia mara kwa mara na kwa msisitizo mkubwa.

Juu ya ukurasa

Ujumbe wa Tawhidi na Umoja

Hija ni ibada ya kuwakurubisha pamoja Waislamu na kuzifikisha sauti zao kote ulimwenguni. Jambo ambalo linaziunganisha nyoyo zote hizo ni ule ujumbe ambao ulitokeza kwa mara ya kwanza katika ardhi hiyo na kuenea katika sehemu zote za dunia na kujenga historia. Ujumbe huo ni ujumbe wa tawhidi na umoja. Naam tawhidi ya Mungu Mmoja na umoja wa Umma wa Kiislamu. Naam, tawhidi kwa maana ya kupinga miungu ya mataghuti na mabeberu na wakandamizaji na umoja kwa maana ya dhihirisho la heshima na nguvu za Waislamu. Hija kila mwaka inafunua pazia la ujumbe huo wa milele katika fremu na kalibu ya mkusanyiko mkubwa wa Waislamu na kuuweka wazi ujumbe huo adhimu kwa walimwengu wote kwa namna ambayo hakuna maandishi wala matamshi yoyote yanayoweza kufanya jambo kama hilo kwa kiwango hicho kinachofanywa na Hija. Msimu wa Hija unapowadia, Waislamu wote katika kila sehemu ya ulimwengu wa Kiislamu kwa mara nyingine wanapaswa kujikumbusha uhakika kwamba maendeleo, heshima na utukufu wa pande zote wa nchi za Kiislamu unaweza kupatikana tu kwa mambo hayo mawili, mosi, tawhidi katika upeo wake wote wa mtu binafsi, wa jamii na kisiasa, na pili, umoja kwa maana yake sahihi na inayoweza kutekelezeka kivitendo katika dunia ya leo.

Juu ya ukurasa

Malengo ya Pande Zote ya Hija

Hija ina malengo makubwa na ya aina yake. Malengo yake yanaanza kushuhudiwa tokea kwenye dhikri na uwepo wa kimaanawi na ucha Mungu kwa kila Muislamu wakati anapokuwa faragha, peke yake yeye na Mola wake hadi katika suala zima la hujaji kujihisi yuko pamoja na Waislamu wenzake na kuona kwa karibu nguvu za mshikamano wa umma wa Kiislamu na utukufu unaotokana na adhama ya makutano hayo makubwa ya Waislamu. Aidha malengo yake yanaonekana pale hujaji anaposhuhudia kwa karibu juhudi za kila Muislamu za kutafuta shifaa kutokana na majeraha na magonjwa ya kimaanawi yaani madhambi mbalimbali pamoja na kupata hamu ya kufanya juhudi za kugundua ponyo na tiba ya masaibu na madhara yaliyoujeruhi umma mzima wa Kiislamu. Malengo ya Hija aidha ni kumfanya kila Muislamu kuguswa na kuwa na uchungu na hali ya mataifa mengine ya Waislamu yaani viungo vyote vya mwili mmoja wa umma mkubwa wa Kiislamu, vyote kwa pamoja vinashuhudiwa ndani ya Hija na katika kalibu ya amali na matendo mbalimbali yanayotekelezwa ndani ya ibada hiyo tukufu.

Juu ya ukurasa

Kuwa Mbali na Malengo

Inabidi tuseme kwa masikitiko na kwa uchungu kwamba utekelezaji wa ibada hiyo ya Mwenye Mungu leo hii una tofauti kubwa na uko mbali sana na sura yake halisi inayotakiwa. Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu awe radhi naye) alifanya juhudi kubwa na za maana katika uwanja huo na alionyesha sura halisi na ya wazi ya Hija ya Nabii Ibrahim AS, Hija yenye kuleta utukufu na heshima na Hija inayojenga na kuleta mabadiliko ya wazi mbele ya macho ya uma wa Kiislamu. Fikra hiyo ya Imam Khomeini imeweza kuleta matunda mazuri katika ulimwengu wa Kiislamu. Hata hivyo na licha ya kuwa fikra hiyo imeenea sana lakini pamoja na hayo inabidi kufanyike juhudi kubwa zaidi za kuweza kuyafanya mataifa yote ya Waislamu yatekeleze ibada ya Hija katika muundo na sura yake halisi na inabidi jitihada hizo zifanywe na maulamaa wa kidini, wanafikra na kwa msaada wa viongozi wa nchi zote za Kiislamu. Kila mmoja anapaswa kutoa mchango wake katika jukumu hilo muhimu mno.

Juu ya ukurasa

Hija Sababu ya Kupatikana Umoja

Uadhama wa Hisia za Umoja

Hija ni nembo na ni dhihirisho la umoja na mshikamano kati ya Waislamu. Maana ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ya kuwataka Waislamu kwa kila mwenye uwezo waende wakakusanyike katika sehemu maalumu na katika muda na wakati mahsusi ili waweze kutekeleza kwa pamoja amali na harakati ambazo ni nembo ya kuishi salama kwa pamoja na ni utaratibu uliopangiliwa vyema na Mwenyezi Mungu na ili wote waweko pamoja usiku na mchana maana ya jambo hilo na athari yake ya kwanza ya wazi ni kudungwa na kuingizwa hisia za umoja na ujamaa katika nafsi ya kila Muislamu, pamoja na kuonyesha utukufu na nguvu za mshikamano wa Waislamu sambamba na kuinywesha akili ya kila mmoja wao hisia za taadhima na hadhi yao. Ni kwa kuwa na hisia hizo ndipo hata kama Muislamu atakuwa anaishi peke yake katika pango la jabali kamwe hatahisi kwamba yuko peke yake. Ni kwa kuwa na hisia kama hizo ndipo Waislamu katika kila nchi ya Kiislamu watakapoweza kupata ushujaa wa kupambana na maadui wote wa Uislamu yaani mifumo ya kibeberu ya kisiasa na kiuchumi katika ulimwengu wa kibepari na vibaraka na vitimbakwiri vyao. Ni wakati huo ndipo Waislamu wataweza kukabiliana vilivyo na hila za kishetani na fitna za mafatani zinazoongezeka kila siku na ambazo lengo lake hasa ni kuzusha mifarakano katika safu za Waislamu silaha; (ya tenganisha utawale) ambayo, ndiyo zana kuu inayotumiwa na wakoloni wa Magharibi dhidi ya mataifa mengine ulimwenguni. Ni kwa kuwa na hisia hizo za adhama na utukufu ndipo madola ya nchi za Waislamu kwa kutegemea wananchi wao yatakapohisi hayana haja tena ya kutegemea watu baki kutoka nje na kwa njia hiyo itawezekana kuondoa misiba mikubwa inayoyakumba mataifa ya Kiislamu kutokana na uchochezi wa mabeberu na wakoloni wanaoweka tawala wanazotaka katika mataifa ya Kiislamu. Ni kwa kuwa na hisia hizo za umoja, ujamaa na kufanya mambo kwa pamoja ndipo uafiriti na njama za wakoloni wa jana na leo yaani njama za kufufua na kueneza hisia kali za utaifa zitakapokomeshwa. (Ni kwa kuwa na hisia hizo za umoja na ujamaa) ndipo itakapowezekana kuondoa utengano mkubwa na mpana uliopandikizwa katika mataifa ya Waislamu. Ni kwa hisia hizo ndipo fikra za huyu ni Mwarabu, huyu ni Mwajemi, huyu ni Mturuki, huyu ni Mwafrika, huyu ni Muasia n.k, zitakapokosa maana na nafasi katika nyoyo za Waislamu. Kwa kweli ni fikra hizo za kibaguzi ndizo zinazozokwamisha kushuhudiwa sura halisi ya umoja wa Kiislamu. Kila mmoja anafadhilisha utaifa wake na visingizio vingine kama hivyo kuliko Uislamu wake mambo ambayo yanawapotezea Waislamu nguvu zao.

Juu ya ukurasa

Maana ya Mkusanyiko huo Adhimu

Ijapokuwa katika Uislamu kuna ibada za jamaa na za pamoja kama vile sala za jamaa, sala za Ijumaa na sala za Idi, lakini mkusanyiko mkubwa wa Hija na huku kupewa umuhimu mkubwa ndani yake mambo kama dhikri, tawhidi na kuwakusanya mahali pamoja Waislamu kutoka kila kona ya dunia kuna maana kubwa mno. Ni jambo lenye maana kubwa kuona kwamba mataifa yote ya Waislamu na umma mzima wa Kiislamu licha ya kuweko tofauti kubwa za lugha zao, mataifa yao, ada na desturi zao, hisia zao, madhehebu yao tofauti lakini wote kwa pamoja wanatakiwa kukusanyika katika eneo moja na kutekeleza kwa umoja wao amali maalumu ambazo hazina sura ya kimaanawi na kunyenyekea na dhikri na kumzingatia Mwenyezi Mungu tu, bali zina sura pia ya kimatendo, kimwamko na kiharakati. Ni jambo lililo bayana kwamba kwa mujibu wa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu, mshikamano wa nyoyo na roho haupatikani tu katika medani za siasa na jihadi bali mshikamano huo unaonenaka pia katika safari ya kwenda kwenye Nyumba ya Mwenyezi Mungu na kukusanyika pamoja nyoyo za Waislamu wa maeneo tofauti ya dunia na yote hayo yana umuhimu mkubwa. Ndio maana Qur’ani Tukufu ikasema: ***

 وَ اعْتَصِمُوا بِحبل‌الله جَميعاً

Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja (al Imran 3:103)

Kushikamana tu na kamba ya Mwenyezi Mungu hakutoshi, bali inatakiwa kushikamana huko kuambatane na kitu kinachoitwa Jamii’an yaani wote kwa pamoja. Shikamaneni kwa pamoja na kamba ya Mwenyezi Mungu; nyote jibidiisheni kwa pamoja kuelekea kwenye nukta salama ya mafunzo, malezi na miongozo ya Mwenyezi Mungu. Ni jambo muhimu sana watu kuwa pamoja; nyoyo kuwa na umoja, roho kuwa kitu kimoja, fikra kuwa za namna moja, miili nayo kushikamanishwa pamoja. Wakati mnapotufu yaani kuzunguka mara kadhaa katika eneo moja maalumu mujue kuwa hiyo ni ishara ya harakati ya Waislamu kukusanyika wote pamoja sehemu moja kuuzunguka mhimili wa tawhidi. Kazi zetu zote, hatua tunazochukua na hima yetu yote inabidi ilenge kwenye mhimili wa tawhidi wa Mwenyezi Mungu na kuizingatia Dhati Takatifu na Mola Mlezi. Darsa hiyo inahusu vipengee vyote vya maisha.

Juu ya ukurasa

Kutumiwa Vibaya Wenzo wa Umoja

Ni ubaya mkubwa ulioje kuona mtu anautumia vibaya wenzo wa umoja kwa ajili ya kuzusha mifarakano na utengano. Maneno haya yanawahusu watu wote. Haya hayahusiana tu na lile kundi la watu wanaokufurisha wenzao, wenye taasubu na misimamo mikali ambao hukaa huko Madina na kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu wa Kishia, bali maneno haya yanawahusu watu wote. Watu wanaoshughulikia masuala ya Hija yaani viongozi wa misafara ya Hija na masheikh wanaofuatana na mahujaji kila mmoja anapaswa kuchukua tahadhari wasije wakawa sababu za kuzifanya nyoyo za Waislamu zijae chuki na uhasama dhidi ya Waislamu wenzao. Ni kitu gani huweza kuujaza moyo wa Muislamu wa Kishia chuki dhidi ya ndugu yake asiye Mshia na kitu gani huweza kuujaza moyo wa Muislamu wa Kisuni uhasama dhidi ya ndugu yake asiye Msuni? Hayo ndiyo mambo ambayo wahusika wa Hija wanapaswa kuyazingatia na kujiepusha nayo ili kuifanya ibada ya Hija kuwa wenzo wa kuleta mshikamano, kuwa sababu ya kupatikana umoja, iwe ni wasila wa kuzishikamanisha nyoyo, nia na malengo katika ulimwengu wa Kiislamu. Si sahihi hata chembe kuifanya Hija kuwa sababu ya mifarakano, kuwa wasila wa kubughudhiana au kuwa wenzo wa kutengana. Inataka uelekevu na mwamko wa hali ya juu kuweza kulijua vyema suala hilo pamoja na madhihirisho na ushahidi wake wa nje.

Juu ya ukurasa

Vizuizi katika Njia ya Umoja

Watu ambao wanataka kueneza mifarakano, fitna na fikra potofu na taasubu na chuki dhidi ya wengine wajue kwamba wao ni vitimbakwiri na vibaraka wa mabeberu watake wasitake, wawe wanalijua au wawe hawalijui hilo. Watu hao ndio wanaohatarisha usalama wa Waislamu na kuangamiza hazina hii kubwa ya Hija. Watu ambao wanaweka vizuizi hivi na vile katika njia ya umoja na kuzuia uma wa Kiislamu kushuhudia kumea na kustawi heshima, utukufu na nguvu za umoja na mshikamano wa Kiislamu, ndio wao wanaohatarisha usalama wa hazina hii kubwa. Wale watu ambao hawaruhusu kupatikana umoja na neema ya utukufu wa umma wa Kiislamu tena basi utukufu ambao inapiganiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu na wala si utukufu unaopiganiwa katika njia ya majivuno wala kuwakoloni na kuwadhalilisha wengine na wala si utukufu wa kuzusha vita dhidi ya wanyonge duniani, bali ni utukufu katika njia ya matukufu ya Mwenyezi Mungu; watu wanaoweka vizuizi na mikwamo hiyo na kuzuia kushukudiwa utukufu unaotakiwa katika ulimwengu wa Kiislamu, si tu wanawadhulumu Waislamu bali wanaudhulumu utu na ubinaadamu. Leo hii ulimwengu wa Kiislamu umepata pigo kubwa kutokana na kudharauliwa hazina kubwa ya Hija.

Juu ya ukurasa

Njama za Wakoloni za Kuzusha Mifarakano

Leo hii moja ya malengo makuu ya mabeberu wakiongozwa na Marekani katika ulimwengu wa Kiislamu ni kuzusha hitilafu katika safu za Waislamu. Silaha kubwa inayotumiwa ni kuzusha mifarakano kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni. Mnashuhudia wenyewe jinsi vikaragosi na vibarakala wa wakoloni duniani wanavyovuruga mambo huko Iraq wakieneza sumu za chuki na uhasama kwa lengo la kuzusha mifarakano kati ya wananchi wa Iraq. Mnaona jinsi vibaraka hao wanavyojaribu kupanda mbegu ya unafiki kati ya Waislamu wa nchi hiyo. Ni kwa miaka mingi sasa mkono wa ukoloni, mkono wa kupenda makubwa wa madola ya kibeberu ya Magharibi unafanya njama hizo. Hija ni fursa nzuri ya kuweza wakoloni hao kueneza chuki kati ya Waislamu wa Kisuni na Kishia ili kumfanya Msuni awe na uhasama na Mshia na Mshia amchukie Msuni na iwe kila upande unavunjia heshima matukufu na vitu vinavyopendwa na mwenzake. Kwa kweli kuna haja ya kuwa macho kikamilifu. Mwamko huo hauhitajiki katika Hija tu, bali ni jambo la lazima pia katika kipindi kizima cha mwaka na katika medani na nyuga zote. Inabidi Waislamu sasa wakae pamoja baada ya kupita karne nyingi za mifarakano. Si sahihi kwa Waislamu kuwa mithili ya watu wanaopigana vitani walio na nyoyo zilizojaa chuki baina yao, huyu anamtukana yule na yule anamtukana huyu. Hakuna jambo lolote linaloweza kuhalalisha kitendo cha Muislamu kuajiri watu na kuwa lipa fedha ili wazushe mifarakano katika safu za Waislamu. Inabidi watu wawe macho, masheikh watukufu wanaoongoza misafara ya Hija wajue kuwa wana jukumu kubwa katika jambo hilo na inabidi waelewe njama zinazofanywa na maadui. Ni mghafala na kosa kubwa kama mtu atamtumikia adui na kumtekelezea malengo yake kwa madai ya kulinda na kutetea haki. Kuna baadhi ya watu wanapewa pesa na hivyo wanageuka kuwa vibarakala na mamluki wa kufanya kazi hiyo na kuna wengine kutokana na mitazamo yao finyu na elimu yao ndogo wanaathiriwa na taasubu na kuanza kushambulia itikadi na matukufu ya upande wa pili. Kama Waislamu watakuwa hivyo, basi mabeberu watakuwa wamefanikiwa kufikia malengo yao na hilo ndilo wanalolitaka. Maadui wanataka tupapurane sisi kwa sisi ili nyoyo zao zipate kutulia.

Juu ya ukurasa

Kujibari na Kujiweka mbali na Washirikina

Nguzo Kuu ya Hija

Katika amali tukufu ya Hija, kama ilivyo dhikri ya Mwenyezi Mungu kwa amri ya Allah aliposema:

 فَاذْکرُوا اللَّهَ کذِکرِکمْ آباءَکمْ أَوْ أَشَدَّ ذِکراً

…basi mtajeni Mwenyezi Mungu kama mlivyokuwa mkiwataja baba zenu au mtajeni zaidi.… (al Baqarah 2:200) - kujibari na kujiweka mbali na washirikina nako ni nguvu muhimu ya Hija - kama inavyosema Qur’ani Tukufu kwamba:***

 وَ أَذانٌ مِنَ اللَّهِ وَ رَسُولِهِ إِلَي النَّاسِ يوْمَ الْحَجِّ الْأَکبَرِ أَنَّ اللَّهَ بَري‏ءٌ مِنَ الْمُشْرِکينَ وَ رَسُولُه

Na ni tangazo kutokana na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kwa wote siku ya Hija Kubwa kwamba Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanajibari na hawana jukumu lolote kwa washirikina.(at Tawba 9:3)

Mwenyezi Mungu anakataza sana kufanyika harakati yoyote ile ambayo inaweza kuleta mtengano kati ya Waislamu ambao Uislamu unawahesabu kuwa wote ni ndugu. Harakati yoyote ile inayoweza kuzidisha uadui na mfarakano kati ya Waislamu haikubaliki hata chembe. Unyeti wa jambo hilo ni mkubwa kiasi kwamba hata masikhara na matani ya kawaida tu kati ya ndugu Waislamu yamepigwa marufuku na ni haramu katika Hija. Mwenyezi Mungu anasema:

 فَلا رَفَثَ وَ لا فُسُوقَ وَ لا جِدالَ فِي الْحجّ‏

…basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika Hija. (al Baqarah 2:197).

Naam, kama ambavyo inatakiwa katika suala la kujibari na kujiweka mbali na washirikina yaani maadui wa jengo la umma mmoja wa tawhidi, ni vivyo hivyo, misuguano na malumbano kati ya ndugu Waislamu yaani kati ya sehemu zinazounda jengo hilo moja la tawhidi, imepigwa marufuku katika Hija. Ni kwa namna hiyo ndivyo ujumbe wa umoja na mshikamano katika Hija ulivyozidi kupata maana na kuonekana kwa uwazi kabisa. Kwa kweli Hija ni moja ya taratibu bora kabisa za Uislamu za kupambana na mghafala. Sura ya kimataifa ya amali ya Hija inatoa ushahidi wa ujumbe ambao umma wa Kiislamu unapaswa kuupata katika Hija nao ni udharura wa kulinda utambulisho wa mshikamano wao na kujiweka mbali na mghafala.

Juu ya ukurasa

Fursa ya kuwa na Muono wa Mbali

Inabidi fursa ya Hija ya kuleta mwamko katika uwanja huo na kutangaza kujibari na kujiweka mbali na ubeberu wa Marekani isisahaulike kabisa. Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa ujue kuwa unakabiliwa na mambo gani. Inabidi mambo hayo yawe ni wasila na sababu ya kupatikana harakati yenye nguvu katika jamii za Kiislamu. Propaganda zenye mielekeo ya kikoloni zinajaribu kuonyesha kwamba watu wengine hawana faida yoyote na hawawezi kufanya chochote kwani mabeberu wamedhibiti kila kitu na hakuna njia ya kuwashinda. Lakini uhakika wa mambo hauko hivyo. Uhakika wa mambo ni kwamba umma wa Kiislamu uko hai, una nguvu kubwa kiasi kwamba si nguvu za Marekani wala mabavu yanayozishinda nguvu za Marekani; yanayoweza kuufanya chochote umma wa Kiislamu.

Mataifa yote yanapaswa kuonyesha kuwa pamoja kwao na kufungamana kwao na maslahi ya ulimwengu wa Kiislamu kwa namna yoyote yanayoweza na sambamba na kusisitiza juu ya umoja baina yao, mataifa hayo yatangaze wazi kujibari na kujiweka mbali na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu. Hilo ndilo jambo la daraja ya chini kabisa ambalo kwa uchache linaweza kufanywa katika amali ya Hija iliyoainishwa na Uislamu. (Basi inabidi Waislamu wafanye angalau jambo hilo).

Juu ya ukurasa

Moyo Unaotawala Amali ya Hija

Suala la kujibari si kitu ambacho tumekitoa nje na kukiingiza ndani ya Hija. Kujibari ni sehemu ya Hija, ni roho ya Hija na ndio maana kuu ya mkusanyiko huo mkubwa wa Waislamu. Kuna baadhi ya watu wanapenda sana kusema katika magazeti yao, katika matamshi yao na katika propaganda zao kwenye maeneo mbalimbali ya dunia kwamba: “Nyinyi mumeingiza masuala ya kisiasa katika Hija.” Watu hao wana maana gani kusema kwamba: ‘Nyinyi mumeingiza masuala ya kisiasa katika Hija?!’ Kama wanakusudia kusema kwamba sisi tumeingiza masuala ya kisiasa katika ibada ya Hija na ambayo hayakuwemo, basi inabidi wakubali kuwa amali hiyo tukufu tangu kale haikuwa kabisa na masuala ya kisiasa ndani yake (jambo ambalo historia ya amali hiyo inathibitisha kinyume chake).

Kujibari na kujiweka mbali na washirikina, kuyakataa masanamu na watu wanaoabudu mifinyango ndiyo roho inayotawala katika Hija ya waumini. Katika kila sehemu ya Hija kunaonekana wazi suala la hujaji kuukabidhi kikamilifu moyo wake kwa Mwenyezi Mungu na kujibidiisha kufanya jitihada kubwa katika njia ya Mwenyezi Mungu pamoja na kujibari na kujiweka mbali na shetani ikiwa ni pamoja na kumpiga mawe shetani na kujiweka mbali naye. Katika kila sehemu ya amali ya Hija kunashuhudiwa mambo yanayoonyesha umoja na mshikamano kati ya watu wa Kibla kimoja na namna ya kuweza kuondoa hitilafu mbaya zinazoweza kusababishwa na hitilafu zao za kimaumbile. Hija imejaa mambo ya kuleta mapenzi na kustawisha mshikamano na udugu wa kweli wa kiimani baina ya Waislamu. Hija hutoa fursa ya kujikumbusha na kuingia katika chuo cha mafunzo na maarifa hayo makubwa.

Juu ya ukurasa

Kupinga Kujibari

Kwa mtazamo wangu ni jambo lisilokubalika kabisa kwa serikali ambayo ina jukumu la kuwahudumia mahujaji wa Nyumba ya Allah kuzuia kutekelezwa amali ambazo ni chemchemu ya mshikamano wa Waislamu; amali ambayo itayaletea heshima mataifa yote ya Kiislamu. Amali ambayo ni ushahidi wa kuwachukia mabeberu na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu. Swali linalojitokeza hapa ni kwamba jambo hilo linawanufaisha watu na mrengo gani kati ya mirengo iliyoko duniani leo hii? Je kuyatetea na kuyaunga mkono mataifa yaliyodhulumiwa ni kosa? Je kufichua njama za Marekani na wastakbari wengine zilizo dhidi ya Uislamu na Waislamu ni dhambi? Je kuwaita na kuwalingania Waislamu umoja na mshikamano na kuwafanya Waislamu waonyeshe hasira zao dhidi ya watu wanaoeneza fitna na mifarakano katika safu za Waislamu si amri ya wazi ya Qur’ani tukufu? Wanaoweza kufaidika na hatua ya kuzuia kutekelezwa jukumu hilo muhimu ni Marekani na Uzayuni. Sauti ya juu ya kujibari inayotolewa leo na Waislamu katika amali ya Hija ni sauti ya kujiweka mbali na mabeberu na vibaraka wao ambao kwa bahati mbaya wana ushawishi mkubwa katika nchi za Kiislamu na wanayatwisha mataifa ya Kiislamu tamaduni, siasa na mifumo yao ya maisha iliyo na uchafu mwingi. Wamevunja misingi ya tawhidi ya kivitendo katika maisha ya Waislamu na kuwafanya wawaabudu wasio Mwenyezi Mungu. Wameifanya tawhidi ya Waislamu ibakie kuwa jina na maneno matupu yatokayo midomoni mwa Waislamu hao. Wamepelekea maana halisi ya tawhidi na athari zake zisionekane tena katika maisha ya kila siku ya Waislamu.

Juu ya ukurasa

 
< Nyuma   Mbele >

^