Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Nafasi Ya Mwanamke Katika Utamaduni Wa Kiislamu Na Utamaduni Wa Magharibi Chapa
08/02/2010

Faslu ya Kwanza – Mwanamke katika Utamaduni wa Kiislamu

Udharura wa Kuzingatiwa Mtazamo wa Kiislamu
Kuangalia Nafasi ya Mwanamke katika Mtazamo wa Kiislamu
Mwanamke katika Mazingira ya Kiislamu
Mipaka ya Uislamu
Ruwaza Kamili
Nafasi ya Kiroho ya Mwanamke
Sheria za Kiislamu Zinavyowalinda Wanawake
Kukinzana Tamaduni Mbili
Kubeba Jukumu Utamaduni wa Magharibi

Faslu Ya Pili: Mwanamke Katika Utamaduni Wa Magharibi

Mwanamke katika Sanaa na Fasihi ya Magharibi
Kinyume na Ustaarabu!
Jinsi Mwanamke Anavyodhulumiwa katika Jamii za Magharibi
Maisha ya Anasa Sababu ya Kupotoka
Maana ya Uhuru wa Mwanawake katika Utamaduni wa Magharibi
Harakati za Kutetea Haki za Wanawake katika Nchi za Magharibi
Mateso ya Wanawake katika Familia
Kuheshimiwa ndani ya Muundo wa Kudhalilishwa
Upinzani dhidi ya Utamaduni wa Wanawake wa Kiislamu
Umilikaji Mali Wanawake katika Utamaduni wa Ulaya na Utamaduni wa Kiislamu

Faslu Ya Tatu: Nafasi Ya Wanawake Katika Mfumo Wa Jamhuri Ya Kiislamu Ya Iran

Nafasi ya Wanawake katika Historia ya Zama Hizi ya Iran
Mwanamke katika Zama za Ufalme za Kipahlavi Nchini Iran
Nafasi ya Mwanamke katika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran
Mapinduzi ya Kiislamu na Nafasi ya Kijamii ya Wanawake
Nafasi ya Mwanamke katika Mtazamo wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu awe radhi naye)

Nafasi Ya Mwanamke Katika Utamaduni Wa Kiislamu Na Utamaduni Wa Magharibi

Faslu ya Kwanza – Mwanamke katika Utamaduni wa Kiislamu

Udharura wa Kuzingatiwa Mtazamo wa Kiislamu

Wakati zinapotupiwa jicho fikra mbali mbali duniani pamoja na mtazamo wa Kiislamu inadhihirika kwa uwazi kwamba jamii ya mwanaadamu itafanikiwa kufikia ukamilifu na daraja inayotakiwa katika suala la mwanamke na katika uhusiano wa mwanamke na mwanamme pale tu itakapotekeleza mitazamo ya Kiislamu kuhusu suala hilo pasina kuongeza wala kupunguza kitu na pasina kuchupa mipaka. Kitu ambacho ustaarabu wa kimaada leo hii unamfanyia mwanamke hakikubaliki kabisa, si kufu ya mwanamke na wala si kwa maslahi yake na pia si kitu kinachokubaliwa na jamii nzima.

Unachotaka Uislamu ni kuona ustawi wa kifikra, kielimu, kijamii, kisiasa na – muhimu kuliko yote – heshima na utukufu wa kimaanawi wa mwanamke unafikia kiwango cha juu kabisa na uwepo wake katika jamii na kwenye familia ya mwanaadamu – akiwa ni kiungo muhimu ndani yake – unakuwa wa kiwango cha juu kabisa na wenye matunda yanayotakiwa. Mafundisho yote ya Uislamu likiwemo suala la Hijabu yamesimama juu ya msingi huo. Wakati Mwenyezi Mungu Mtukufu anapotoa mifano ya watu wema na watu wabaya katika Qur’ani Tukufu anatumia wanawake katika kutoa mifano ya pande zote mbili. Mfano mmoja ni wa mke wa firauni na mfano mwingine na wa mke wa Nabii Nuh na Nabii Lut (Amani iwe juu ya Manabii hao wa Mwenyezi Mungu). Mwenyezi Mungu anasema:

وَضَرَبَ اللَّهُ مَثَلا لِّلَّذِينَ آمَنُوا امْرَأَةَ فِرْعَوْنَ

Na Mwenyezi Mungu amewapigia mfano walioamini - mkewe Firaun (Tahrim 66:11).

Na katika upande mwingine pia, kuhusiana na watu wabaya na waovu na ambao hawana maadili mazuri na wanaokengeuka maamrisho ya Mwenyezi Mungu, Qur’ani inatoa mfano wa wake za Nabii Nuh na Nabii Lut AS. Hapa panaweza kuzuka swali kwamba iko pia mifano ya wanaume, lakini Qur’ani imeamua kutoa mifano ya wanawake tu na mtu anaweza kujiuliza falsafa ya kutotolewa mfano mmoja kupitia mwanamke na mwingine kupitia mwanamme ni ipi. Lakini falsafa ya Qur’ani haiko hivyo hususan kwa kuzingatia umuhimu wa mwanamke katika jamii. Na ndio maana tunaiona Qur’ani katika mifano yote miwili - kwa ajili ya walioamini na kwa ajili ya waliokufuru – inatoa mifano ya wanawake.

Juu ya ukurasa

Kuangalia Nafasi ya Mwanamke katika Mtazamo wa Kiislamu

Mbinu na njia inayotumiwa na Uislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mwanamke ni mbinu ya kumpa heshima yake halisi mwanamke. Ni kumtukuza na kuzingatia maslahi yake kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu. Mbinu ya Jamhuri ya Kiislamu ni kuzingatia maslahi ya mwanamke na ya mwanamme pia. Uislamu unamwangalia mwanamke, mwanamme na viumbe wote kwa jicho moja la uhakika wa mambo na kwa kuzingatia maumbile ya kila mmoja ili yeyote asitegemee kupata kitu ambacho si chake.

Ili kuuweka wazi zaidi mtazamo wa Kiislamu kuhusu jambo hilo, tunaweza kumwangalia mwanamke kwa mitazamo mitatu. Mtazamo wa Kwanza ni nafasi ya mwanamke kama mwanadamu katika suala zima la ukamilifu wa kimaanawi na kinafsi ambapo katika mtazamo huo, mwanamke hana tofauti yoyote na mwanamme. Katika historia kuna wanawake wakubwa na watukufu kama ambavyo kuna wanaume pia wakubwa na watukufu. Mtazamo wa Pili ni katika upande wa shughuli na kazi za kijamii, kisiasa, kielimu na kiuchumi. Kwa mtazamo wa Kiislamu mlango wa kufanya kazi na juhudi za kielimu na kiuchumi na kisiasa uko wazi kikamilifu kwa ajili ya mwanamke. Kama atatokezea mtu na kutaka kuutumia Uislamu kumnyima mwanamke haki yake ya kujishughulisha kielimu na kufanya juhudi na kazi za kiuchumi, au kumkatalia mwanamke asijishughulishe na masuala ya kisiasa na kijamii, ajue kuwa Uislamu haukubaliani na jambo hilo na yeye atakuwa anakwenda kinyume na mafundisho ya Mwenyezi Mungu. Wanawake wana haki ya kujishughulisha na masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kadiri wanavyoweza. Sheria za dini tukufu ya Kiislamu hazimzuii mwanamke kufanya hivyo. Tab’an kutokana na mwanamke kuwa dhaifu kwa nguvu za mwili ikilinganishwa na mwanamme, ziko kazi za wawili hao ambazo baadhi ya wakati hutofautiana. Kumbebesha mwanamke kazi nzito ni kumdhulumu. Uislamu haunasihi wala kuhamasisha kufanya jambo kama hilo ijapokuwa pia hauharamishi suala hilo. Tab’an imenukuliwa kutoka kwa Imam Ali bin Abi Talib (Amani iwe juu yake) akisema kwamba:

اَلْمَرْأَةُ رَيْحانَةٌ وَ لَيْسَتْ بِقَهْرَمانَةٍ

Maana yake ni kuwa: Mwanamke ni ua na wala si mbabe. Neno (قَهْرَمانَة) hapa lina maana ya mtu mbabe kama yule anayejitokeza kifua mbele mbele ya watu akiwa tayari kutumia mabavu yake kubariziana na yeyote. Aidha lina na maana nyingine isiyokuwa hiyo. Maneno hayo ya Imam Ali AJS yanawalenga wanaume kwamba wanawake katika majumba yao ni mithili ya ua linalopaswa kutunzwa na kubembelezwa na kuchukuliwa kwa upole na tahadhari ya hali ya juu. Maneno hayo yanakusudia kumwambia wanaume kwamba mwanamke si mtumishi na kijakazi wa nyumba ambaye anapaswa kutumika kufanya kazi ngumu na kukabidhiwa yeye kazi nzito nzito. Nasaha hizo kwa kweli ni muhimu sana.

Ni makosa kwa mwanamme kuweka sharti wakati wa kuoa la kumlazimisha mwanamke afanye kazi na ajishughulishe na mambo ya kuiletea kipato familia. (Kwani jukumu la kulisha na kuendesha familia ni la mwanamme). Ijapokuwa suala hilo si haramu kisheria, lakini Uislamu hauusii wala kushajiisha jambo hilo. Ni makosa kutumia Uislamu kusema kwamba ni haramu kwa mwanamke kujishughulisha na kazi za kiuchumi na kijamii. Hakuna sehemu yoyote ile ambapo Uislamu umesema kitu kama hicho. Pamoja na kutomzuia mwanamke kufanya kazi na kujishughulisha na kazi za kiuchumi, kielimu na kadhalika, lakini wakati huo huo dini tukufu ya Kiislamu haimshajiishi mwanamke kufanya kazi ngumu na nzito za kiuchumi, kijamii au za kisiasa. Mtazamo wa Uislamu ni wa kati na kati. Uislamu haumkatazi mwanamke kufanya kazi za kijamii, kisiasa na kiuchumi iwapo suala la malezi ya watoto halitamzuia na iwapo atapenda na kuwa na hamu, nguvu na uwezo wa kimwili wa kufanya hivyo. Lakini kumlazimisha mwanamke afanye kazi ili awe na kipato, au kumlazimisha kwa siku afanye kazi masaa fulani ili achangie kipato cha familia, hata kama hataki, ni jambo ambalo halikubaliki kabisa. Kwa mujibu wa Uislamu, si jukumu la mwanamke kulisha familia au kuchangia kipato cha familia. Dini tukufu ya Kiislamu inaamini kwamba kufanya hivyo ni kumtweza na kumbebesha mzigo mwanamke.

Ninaziusia familia ziruhusu watoto wao wa kike watafute elimu. Mwenyezi Mungu apishie mbali, asije akatokezea baba na mama atakayemzuia mwanawe wa kike kutafuta elimu na kupata elimu ya juu kutokana na taasubu ya kidini! Hapana; dini ya Kiislamu haikufundisha kitu kama hicho. Kwa mujibu wa dini yetu tukufu ya Kiislamu, hakuna tofauti yoyote baina ya mwanamke na mwanamme katika upande wa kutafuta elimu. Iwapo mtoto wa kiume ana haki na kupata elimu ya juu, mtoto wa kike naye ana haki hiyo hivyo wote inabidi wapewe nafasi sawa. Watoto wa kike lazima wasome, lazima watafute elimu, wawe na mwamko, waweze kufikia daraja wanayostahiki na wajue dhati na heshima yao na hivyo waweze kufahamu kwamba propaganda za mabeberu wa dunia kuhusu mwanamke ni kiasi gani hazina mashiko, ni mapepe matupu yasiyo na chochote ndani yake. Hayo yatawezekana chini ya kivuli cha elimu na maarifa.

Mtazamo wa Tatu ni ule unaomwangalia mwanamke kwa jicho la kiungo katika familia. Mtazamo huu ndio muhimu zaidi. Uislamu haumruhusu mwanamme kumbana na kutumia mabavu dhidi ya mwanamke au kumtwisha kitu fulani. Mwanamme amewekewa haki zake maalumu katika familia jambo ambalo limefanyika kwa hekima ya hali ya juu kwa kuzingatia kikamilifu maslahi ya familia. Kama haki hizo zitafafanuliwa vizuri na kubainishwa kwa njia sahihi basi itakuwa ni rahisi sana kubaliwa na kila mtu. Mwanamke naye ameainishiwa haki zake mahsusi katika familia ambazo nazo zimezingatia kikamilifu maslahi ya familia. Mwanamme na mwanamke kila mmoja ana maumbile, tabia, roho na matamanio mahsusi kwa ajili yake. Iwapo kila mmoja kati yao atatumia vyema maumbile yake na kwa njia sahihi katika kuhudumia familia, basi ndoa yao itakuwa kamilifu, yenye uadilifu na bila ya mizozo wala migogoro yoyote. Iwapo mwanamme atachupa mipaka katika matendo na mambo yake, mambo yataharibika katika familia. Kama mwanamke naye atachupa mipaka katika masuala yake, mambo yatavurugika. Uislamu umewaweka mwanamme na mwanamke katika familia kama bawaba mbili za mlango, mithili ya macho mawili katika uso wa mwanaadamu na umewafanya kuwa mithili ya ngao mbili katika medani ya vita na mapambano ya maisha. Ni kama vile washirika wawili katika mlango wa duka. Kila mmoja kati ya wawili hao ana maumbile, sifa zake maalumu na tabia zinazotofautiana na mwenzake. Tofauti hiyo inashuhudiwa katika mwili, roho, fikra na hata katika masuala ya hisia na ghariza za kila mmoja kati yao. Iwapo jinsia hizi mbili (yaani mwanamme na mwanamke) zitachunga mipaka yao ziliyowekewa na Uislamu na kustahamiliana katika maisha yao ya pamoja, basi zitafanikiwa kuunda na kujenga familia madhubuti iliyojaa mapenzi, baraka na manufaa makubwa. Uislamu umekuja kumkomboa mwanaadamu na kila mmoja kumuweka kwenye nafasi yake anayostahiki.

Uislamu umekuja kuwazuia watu wasitumie vibaya nguvu zao za kimwili au uwezo wa kifedha kuwageuza wanaume na wanawake kuwa watumwa na vijakazi wao. Uislamu umekuja kumkomboa mwanamke na kumpa haki sawa na mwanamme kwa kuzingatia ustahiki wa kila mmoja wao. Qur’ani inatoa amri na kuwaweka kwenye fungu sawa wanaume na wanawake kama pale inaposema:

إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ وَالْخَاشِعِينَ وَالْخَاشِعَاتِ وَالْمُتَصَدِّقِينَ وَالْمُتَصَدِّقَاتِ وَالصَّائِمِينَ وَالصَّائِمَاتِ وَالْحَافِظِينَ فُرُوجَهُمْ وَالْحَافِظَاتِ وَالذَّاكِرِينَ اللَّهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا

Yaani: Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na wat'iifu wanaume na wat'iifu wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanao subiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na wanao funga wanaume na wanawake, na wanao jihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanao mdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa. al Ahzab (33:35).

Hivyo daraja zote hizo za kimaanawi katika Uislamu zinawahusu wote wawili, mwanamme na mwanamke kwa usawa kabisa. Hakuna tofauti yoyote kati ya mwanamke na mwanamme katika suala la ibada na kupanda daraja mbele ya Mwenyezi Mungu. Yeyote kati yao atakayejipinda katika ibada na uchaji Mungu, malipo yake na daraja yake mbele ya Mwenyezi Mungu itakuwa ni ya kiwango sawa na uchaji wake bila ya kubagua baina ya mwanamke na mwanamme. Qur’ani Tukufu inasema:

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَى وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُواْ يَعْمَلُونَ

Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda. (an Nahl - 16:97).

Katika baadhi ya sehemu, Uislamu hata umemtanguliza mwanamke mbele kuliko mwanamme. Kwa mfano wakati linapofika suala la baba na mama, mtoto ijapokuwa ni wajibu wake kuwatendea wema wazazi wake wote wawili, lakini wajibu wa kumtumikia na kumtendea mama ni mkubwa zaidi kwa mwana ikilinganishwa na wajibu wake kwa baba yake. Haki ya mama kwa mwanawe ni kubwa zaidi na wajibu wa mwana kwa mama yake ni mzito zaidi. Imepokewa kwamba wakati Bwana Mtume Muhammad SAW alipoulizwa swali kuhusu nani atendewe wema zaidi kati ya baba na mama, alimjibu muulizaji akisema mama yako, akauliza tena kisha nani, Mtume akamjibu mama yako; muulizaji akauliza tena halafu nani, Mtume akamjibu mama yako, akauliza tena kisha nani, Mtume akamjibu kisha baba yako. Hii yote ni kutaka kuonyesha kwamba haki ya mwanamke kama mama katika familia ni kubwa sana. Tab’an hilo halina maana kwamba kwa kufanya hivyo Mwenyezi Mungu anakusudia kufadhilisha jamii fulani kuliko nyingine, au kubagua kundi moja mbele ya jengine. Hilo limefanyika kutoka na tabu na mashaka mengi anayoyapata mwanamke. Bali huo ndio uadilifu wa Mwenyezi Mungu. Mwanamke anasumbuka zaidi, hivyo ni mahala pake kupewa haki zaidi. Mwanamke anataabika sana, hivyo na thamani yake inabidi iwe juu. Yote hayo yametendeka chini ya msingi wa uadilifu wa Mwenyezi Mungu. Aidha mtindo na mkakati wa Uislamu katika masuala ya fedha, kama vile haki ya familia na haki ya kusimamia ayali katika mkabala wa jukumu la kuongoza aila ni mpango wa kiadilifu kabisa. Sheria ya Uislamu katika masuala hayo haikutoa mwanya wa kudhulumiwa hata chembe mwanamke na mwanamme. Umemwekea mwanamke haki zake anazostahiki kama ulivyomwekea mwanamme haki hizo. Amemwekea mwanamme majukumu yake kama alivyomuwekea mwanamke. Watu wenye dhuku na hamu ya kuchunguza uhakika wa mambo hayo wanaweza kuuona kwa uwazi uhakika huo. Na hayo wameyaandika katika vitabu vyao mbalimbali.

Jinsia ya mtu yaani kuwa kwake mwanamme au kuwa kwake mwanamke si muhimu kwa Uislamu. Lililo muhimu mbele ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu ni utukufu wa kibinaadamu, maadili mema, kudhihiri vipaji, kutekeleza wajibu aliopewa kila mtu awe mwanamme au mwanamke na kwamba kuweza kulijua vyema hilo inabidi kuyajua vilivyo maumbile. Uislamu nao unayajua vilivyo maumbile ya mwanamke na mwanamme. Kilicho muhimu katika Uislamu ni uadilifu yaani kuchungwa kikamilifu haki sawa na uadilifu kati ya wanaadamu wa jinsia zote za kike na kiume. Lililo muhimu ni usawa katika haki lakini baadhi ya wakati sheria zinazohusiana na mwanamke zinatofautiana na zile za mwanamme kama ambavyo kimaumbile kuna tofauti baina ya mwanamme na mwanamke. Hivyo uhakika mwingi zaidi na ukweli mkubwa zaidi wa maumbile na silika za mwanaadamu zinapatikana katika mafundisho na maarifa ya dini tukufu ya Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Mwanamke katika Mazingira ya Kiislamu

Leo hii anachotakiwa kufanya mwanamke katika jamii ya Kiislamu ya Iran ni kujielimisha awe na utambuzi mzuri wa kisiasa, afahamu kazi za kijamii na ajitokeze vilivyo katika medani zote. Anapokuweko nyumbani awe ni mama wa familia mwenye kumshughulikia mumewe na wanawe na anapokuwa nje ya nyumba awe ni mfano na kigezo cha adhama, utoharifu na kujiepusha na yaliyokatazwa. Mwanamke wa aina hiyo ndiye ambaye Jamhuri ya Kiislamu na jamii ya Kiirani inataka iwe naye. Yaani mwanamke anapokuwa nyumbani awe ni mlezi wa watoto na mke wa kumletea utulivu mume wake na yeye apate utulivu kutoka kwa mumewe na wakati anapokuwa nje ya nyumba sambamba na kulinda kikamilifu utoharifu na heshima yake, ashiriki vilivyo katika medani zote za kijamii, kielimu, kisiasa na za utumishi. Sharti la kwanza la kuhakikisha hilo linafanikiwa ni kuchungwa na kulindwa hijabu. Bila ya hijabu hakuna chochote kinachoweza kutendeka. Bila ya hijabu mwanamke hawezi kupata faragha inayotakiwa ya kumuwezesha kutekeleza masuala hayo niliyotangulia kuyasema.

Mwanamke wa Kiislamu anapewa heshima kubwa katika mazingira ya jamii ya Kiislamu na katika mafundisho ya kijamii ya Waislamu ambapo dhihirisho wazi la heshima hiyo ni stara na hijabu. Siku zote wastara haumbuki. Daima mtu anayechunga hijabu husitirika na heshima yake hulindwa. Uislamu ndiyo dini inayowapa wanawake wote heshima, staha na stara hiyo.

Juu ya ukurasa

Mipaka ya Uislamu

Uislamu umeweka mipaka maalumu katika shughuli za kijamii, na mipaka hiyo inahusiana na mwanamke mwenyewe na wala haihusiani na suala la kuruhusiwa au kutoruhusiwa mwanamke kufanya shughuli zake hizo za kijamii. Mipaka hiyo inahusiana na michanganyiko ya wanawake na wanaume ambapo Uislamu una hisia kali na unaguswa mno na mambo hayo. Uislamu unaamini kwamba mwanamke na mwanamme inabidi wawekeane mipaka tena katika sehemu zote, barabarani, ofisini, katika maeneo ya biashara n.k. Maingiliano na kuchanganyika wanaume na wanawake hakuwezi kuwa sawa na kuchanganyika wanaume kwa wanaume au wanawake kwa wanawake. Basi jambo hilo inabidi lichungwe vyema. Wanaume wanapaswa kulichunga hilo na wanawake nao wana jukumu la kulichunga vilivyo suala hilo. Kama kuguswa huko unakoguswa Uislamu kuhusiana na suala zima la maingiliano na mchanganyiko wa wanaume na wanawake kutachungwa na kuzingatiwa vilivyo na kwa njia sahihi, basi kazi zote ambazo wanaume wanaweza kuzifanya katika masuala ya kijamii, mwanamke naye ataweza kuzifanya. Tab’an kama uwezo wa kimwili na hamu na fursa ya kufanya hivyo atakuwa nayo.

Juu ya ukurasa

Ruwaza Kamili

Tukio la bonde la Abu Talib yaani Shib Abu Talib lilitokea wakati Bibi Fatimatuz Zahra (Salamullahi Alayha) alipokuwa na umri wa miaka sita saba hivi. Tukio hilo lilitokea kwenye kipindi kigumu sana katika historia ya mwanzoni mwa Uislamu, yaani katika kile kipindi ambacho ndio kwanza Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa ameanza kuwalingania watu dini tukufu ya Kiislamu kwa uwazi bila ya kificho na katika wakati ambao pole pole watu wa Makkah, hususan vijana na hasa hasa watumwa na wajakazi, walikuwa wakimiminika kwa wingi upande wa Bwana Mtume. Kipindi hicho kilikuwa ndicho kile kipindi cha mateso dhidi ya Waislamu ambapo mabwana mataghuti wa Kikureish waliona mbinu zao zote za mateso zimeshindwa na hawana njia nyingine isipokuwa kumuwekea vikwazo vya kiuchumi Bwana Mtume na masahaba wake ikiwa ni pamoja na kuwafukuza katika mji wa Makkah, na hivyo ndivyo walivyofanya. Hivyo idadi kubwa ya Waislamu ambapo wakati huo idadi yao ilishafikia makumi ya familia, akiwemo Bwana Mtume mwenyewe na watu wa familia yake na hata Abu Talib – licha ya kwamba alikuwa miongoni mwa mabwana wa Kikureish – walifukuzwa mjini Makkah. Janab Abu Talib alikuwa na kijibonde kidogo na alimtaka Bwana Mtume na masahaba wengine waende kwenye kijishamba hicho. Hali ya hewa ya Makkah ni kwamba mchana kuna joto sana na usiku kunakuwa na baridi ya kupindukia isiyostahamilika. Waislamu walikaa miaka mitatu katika jangwa hilo na kuvumilia shida zake nyingi. Walivumilia njaa kali kupita kiasi! Miongoni mwa siku nzito alizokumbana nazo Bwana Mtume ni hizo alizozipitisha katika Bonde la Abu Talib. Katika kipindi hicho, kazi ya Bwana Mtume Muhammad SAW haikuishia tu kwenye kuongoza mjumuiko fulani tu wa watu, lakini alilazimika pia kulinda kazi yake mbele ya watu waliokumbwa na mtihani huo mzito.

Ilikuwa ni katika kipindi hicho kigumu mno ndipo Janab Abu Talib ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kumuunga mkono na kumlinda Bwana Mtume Muhammad SAW alipofariki dunia. Bibi Khadijatul Kubra naye ambaye alikuwa na msaada mkubwa wa kiroho na kifedha kwa Mtume alifariki dunia wiki moja tu baada baada ya kufariki dunia ami yake Bwana Mtume yaani Bwana Abu Talib! Yalikuwa ni matukio ya ajabu kwa maana ya kwamba Mtume Muhammad SAW alibakia peke yake, yeye kama yeye!

Bibi Fatimatuz Zahra (Salamullahi Alayha) akawa sasa ni kama mama, na kama mshauri wa baba yake; alikuwa ni mliwazaji mkuu wa mtukufu huyo. Ni wakati huo ndipo Bibi Fatimatuz Zahra alipopata lakabu ya “Ummi Abiha” kwa maana ya mama wa baba yake yaani wakati huo huo alikuwa mwana na wakati huo huo alikuwa kama mama kwa ajili ya Bwana Mtume. Hayo yanahusiana na kipindi hicho. Yaani mtoto wa miaka sita saba alipambika kwa sifa hizo kubwa. Tab’an ni jambo linalojulikana wazi kwamba katika mazingira ya Kiarabu na katika maeneo ya joto, wasichana huwa wakubwa mapema kimwili na kiroho, tunaweza kusema kwamba mtoto huyo wa miaka sita saba anaweza kufanana na mtoto wa miaka kumi au kumi na mbili wa zama zetu hizi. Huko ndiko kunakoitwa ni kuhisi majukumu. Je hilo haliwezi kuwa kigezo kwa kila kijana? Kwamba ahisi haraka wajibu wa kubeba jukumu la masuala yanayomzunguka na awe mkakamavu katika mambo yake. Atumie haraka rasilimali kubwa ya ukakamavu aliyo nayo. Hivyo ndivyo alivyofanya Bibi Fatimatuz Zahra SA alipotumia vyama hazina hiyo kubwa kufuta majonzi makubwa aliyokuwa nayo baba yake ambaye takriban alikuwa na karibu miaka 50 tena. Je, hilo haliwezi kuwa ni kigezo na ruwaza kwa kila kijana?

Bibi Fatimatuz Zahra (Salamullahi Alayha) na Amirul Muuminin Imam Ali (Alayhis Salaam) walioana na kuwa mke na mume. Katika kipindi cha miaka tisa ya ndoa yao, kulitokeza vita vingi vikubwa na vidogo. Imepokewa kwamba vita 60 vilitokea katika kipindi hicho ambapo Imam Ali AS alilishiriki katika aghlabu ya vita hivyo. Sasa fikirieni wenyewe hali aliyokuwa nayo Bibi huyo nyumbani kwake. Mume wakati wote yuko katika medani ya vita na siku ambayo hakuwa katika kitali, bado alikuwa ni kana kwamba yuko vitani kwa jinsi mapambano ya kuupigani Uislamu yalivyokuwa yamemjenga na kumwingia. Tena basi hali yao ya kimaisha haikuwa nzuri. Kwa hakika walikuwa wakiishi maisha ya kimaskini kabisa licha ya kwamba Bibi Fatima alikuwa ni binti wa Kiongozi, alikuwa ni binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Lakini pamoja na hayo alibeba jukumu kubwa.

Mtu anapaswa kuwa na moyo mkubwa kiasi gani hata aweze kumwandalia anachotaka mume kama huyo na kumfanya moyo wake usiwe na wasiwasi wala hofu na familia wala mashaka ya maisha? Aidha mtu anapaswa kuwa na moyo mkubwa kiasi gani hata aweze katika mazingira kama hayo, kumpa utulivu kamili mumewe, kumchangamsha na kulea watoto bora kabisa kama alivyofanya mtukufu huyo?! Mtu anaweza kusema kwamba; lakini Imam Hasan na Imam Husain AS walikuwa ni maimamu na dongo lao ni la uimamu. Mtu huyo anaweza kujibiwa kwamba Bibi Fatimatuz Zahra SA alimlea pia Bibi Zaynab AS na bibi huyo mtukufu hakuwa Imam, hapo atasemaje? Alimlea Bibi Zaynab kwa miaka tisa. Kama mnavyojua, baada ya kufariki dunia Bwana Mtume Muhammad SAW, Bibi Fatimatuz Zahra SA naye hakuishi muda mrefu tena.

Hayo ndiyo malezi, huko ndiko kumtunza mume na huko ndiko kulea na kujenga familia iliyo bora ambayo itabakia kuwa mfano katika kipindi chote cha historia. Je hayo hayawezi kuwa ruwaza njema kwa ajili ya binti wa kike na kwa ajili ya akinamama majumbani au mtu aliyepewa jukumu la kuendesha nyumba? Kwa hakika hayo ni mambo muhimu sana.

Juu ya ukurasa

Nafasi ya Kiroho ya Mwanamke

Miaka karibu 1400 nyuma bwana Mtume Muhammad SAW alilea binti na mtoto wa kike aliyejaa utukufu na ubora kiasi kwamba alipata hadhi na heshima ya kubusiwa mkono wake na Mtume wa Mwenyezi Mungu! Kitendo cha Bwana Mtume Muhammad SAW cha kuubusu mkono wa Bibi Fatimatuz Zahran SA kamwe hakipaswi kuhesabiwa kuwa kimetokana tu na mapenzi ya baba kwa mwanawe. Itakuwa ni kosa kubwa kama mtu atadhani kwamba Bwana Mtume aliubusu mkono wa Bibi Fatima kwa kuwa ni bintiye na kwa sababu alikuwa anampenda sana. Hivi kwani inawezekana kweli kwa mtu mtukufu kama Bwana Mtume tena mwenye uadilifu na hekima kubwa mno alizotunukiwa na Mola Muumba ainame tu na kuubusu mkono wa bintiye bila ya kutaka kutoa funzo lolote kuhusu kitendo chake hicho?! Hapana haiwezekani. Hapo pana kitu kingine na maana nyingine kabisa! Kitendo hicho kilibainisha kwamba binti huyo mdogo, mwanamke huyo ambaye wakati alipofariki dunia alikuwa na umri wa baina ya miaka 17 hadi 25, alikuwa katika kilele ya utukufu wa kimaanawi na hakuwa mwanamke wa kawaida. Namna hivi ndivyo Uislamu unavyomwangalia mwanamke.

Juu ya ukurasa

Sheria za Kiislamu Zinavyowalinda Wanawake

Sheria za Kiislamu ziko wazi kabisa katika suala la familia kiasi kwamba kuweko sheria hizo katika Uislamu inakuwa ni heshima kubwa kwa mwanaadamu sheria ambazo mtu anapoziangalia anahisi fakhari na utukufu mkubwa. Sheria za Kiislamu zinamlinda mwanamke tangu mwanzoni kabisa mwa masuala ya ndoa na tokea wakati wa kuchagua mtu wa kuoana naye. Kutokana na kuwa baadhi ya wanaume walikuwa wakitumia mabavu na kuwakandamiza wanawake, Uislamu ulipokuja, ulikuja na sheria za kupambana kabisa na tabia hiyo. Sheria hizo za Kiislamu zinaendelea kumlinda mwanamke hata baada ya kuoana na kujenga familia. Kwa mujibu wa Uislamu, mwanamme na mwanamke katika ndoa ni watu wawili wanaoshirikiana katika maisha, na wana wajibu wa kuamiliana kimapenzi baina yao. Mwanamme hana haki ya kumkandamiza mwanamke na mwanamke naye hana haki ya kumkandamiza mwanamme. Sheria za Kiislamu katika upande wa mahusiano ya mume na mke ndani ya familia ni za kina sana na zinaangalia mambo kwa undani na umakini wa hali ya juu. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameweka sheria hizo kwa kuzingatia maumbile ya mwanamke na mwanamme. Kuna baadhi ya mambo tu ndiyo yanayompa haki mwanamme ya kumwamrisha mwanamke. Mwanamme amepewa haki ya kumzuia mkewe asitoke nje ila kwa idhini yake tab’an kwa sharti kwamba wakati wa kufunga ndoa kusiwe kumewekwa sharti lolote kuhusiana na jambo hilo. Hiyo ni moja ya siri kuu na za kina za sheria za Mwenyezi Mungu. Haki hiyo ya kumzuia mwanamke asitoke ndani ila kwa idhini, amepewa mume tu hata baba hakupewa. Kwa mujibu wa sheria, baba hawezi kumlazimisha binti yake asitoke nje ila kwa idhini yake lakini jambo hilo linavyomwajibikia mwanamke kwa mumewe. Baba hana haki hiyo, kaka hana haki hiyo, dada hana haki hiyo, lakini mume anayo kwa mkewe. Tab’an wanawake wanaweza wakaweka masharti wakati wa kufunga ndoa na masharti hayo yakawa wajibu kutekelezwa ndani ya ndoa.

Juu ya ukurasa

Kukinzana Tamaduni Mbili

Kwa hakika si utamaduni wa Kiislamu ambao inabidi uthibitishwe usahihi wake bali ni utamaduni bandia wa Magharibi ndio ulio na jukumu la kujitetea na kuthibitisha usahihi wake. Haki ambazo Uislamu unampatia mwanamke ni kitu ambacho hakuna msomi wala mtu yeyote mwenye insafu na mwadilifu katika mambo yake anayeweza kukana kwamba kitu hicho ni kizuri na ni kwa maslahi ya mwanamke. Uislamu unampa heshima yake mwanamke kwa kumtaka achunge staha na hadhi yake, ajisitiri vyema, achunge heshima yake, asijipambe na kujipodoa kwa ajili ya wanaume bali afanye hivyo kwa mumewe ili mwanamke asije akawa chachu ya matamanio yasiyo sahihi ya wanaume. Jambo hilo halina ubaya wowote, bali linampa heshima na utukufu wake mwanamke wa Kiislamu. Uislamu unamkataza mwanamke kuwa na maingiliano ya kiholela na mwanamme ili kuepusha uasherati, ufuska na matendo maovu katika jamii. Hiyo ndiyo heshima ya mwanamke. Sasa wale watu ambao wanamshawishi mwanamke ajipodoe na kujiremba kiasi kwamba awapendezeshe wanaume wote wakiwemo wa vichochoroni na wa masokoni kwa lengo la kujiuza kwao ili washibishe matamanio yao ya kiasherati; watu hao ndio wanaopaswa wajitetee na wajibu kwa nini wanamkashifu na kumdhalilisha kiasi chote hicho mwanamke?! Wao ndio wanaopaswa kujibu na sio Uislamu ambao unamtunza na kumpa heshima na staha yake mwanamke. Utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu ni utamaduni ambao unakubaliwa na watu wakiwemo wasomi wa nchi za Magharibi na hata vitendo vyao pia vinaonyesha hivyo. Hata katika nchi za Magharibi kuna wanawake wenye heshima zao, wako makini, wanajistahi na hawako tayari kutumika kwa ajili ya kushibisha matamanio ya kiasherati ya wanaume. Kiujumla ni kwamba ni utamaduni wa Magharibi ndio unaopaswa kutoa ushahidi wa usahihi wake na si utamaduni wa Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Kubeba Jukumu Utamaduni wa Magharibi

Inabidi kukabiliana kwa nguvu zote na utamaduni wa Magharibi unaomdhalilisha mwanamke. Hiyo ni miongoni mwa kazi za wajibu. Magharibi inamdhalilisha na kumfanya duni mwanamke. Magharibi inampotezea hadhi yake mwanamke. Huwa wanasema uongo pale wanapodai kuwa, wao wanazipa haki sawa jinsi mbili za mwanaadamu yaani mwanamme na mwanamke. Hapana, bali madai hayo ni hila na udanganyifu tu wa kisiasa na kiutamaduni. Wanatumia mbinu hiyo kumfanyia khiana mwanamke. Ni Uislamu ndio unaompa hadhi na heshima yake mwanamke pale dini hiyo tukufu inapomvisha vazi la staha la Hijabu linalolinda heshima ya mwanamke. Aidha Uislamu unamtaka mwanamke asiwe dhalili na asijilegeze mbele ya mwanamme, bali awe mkakamavu. Qur’ani inasema:

 فلا تخضعن بالقول

…wala msiligeze sauti…

Suala hapa ni ulegevu. Mwanamke hapaswi kujilegeza anapokuwa mbele ya mwanamme, bali anapaswa kuwa imara na mkakamavu. Hii haina maana kwamba yanapofika masuala ya kimaumbile na masuala ya ghariza baina ya mume na mke, kusiwe na suala la kujilegeza. Hayo ni masuala ya kimaumbile na yana mahala pake na hakuna tatizo lolote katika hilo. Lakini tunachozungumza hapa ni suala la miamala ya kawaida baina ya mwanamke na mwanamme isiyo hiyo ya ghariza za kimaumbile. Lakini wanachotaka Wamagharibi ni kumfanya mwanamke kuwa duni mbele ya mwanamme na ndicho hicho kinachoshuhudiwa katika nchi za Magharibi leo hii. Hicho kwa kweli tayari wameshakifanya na si kwamba ndio kwanza wanataka kukifanya. Mbinu wanayotumia ni kumpiga mnada mwanamke mbele ya wanaume wakimhamasisha kwa kumwambia mwanamke ajipitishepitishe mbele ya wanaume kwa namna ambayo watavutiwa naye. Wanadai wanampa haki zake mwanamke, wanampa uhuru wa kufanya analotaka, lakini ukweli wa mambo ni kwamba wanamdhalilisha. Na hayo ni yale yanayoonekana nje, hatusemi tena hali ilivyo ndani ya familia katika uhusiano wa mke na mume. Mtu unaposoma habari zao unasisimkwa na mwili na kuhuzunishwa mno. Mwanamke hupigwa ovyo katika familia hizo, mwanamke anadhalilishwa, ni jambo jepesi sana kuuawa mwanamke kwa kijambo kidogo tu, hayo ni sehemu ya mambo ya kawaida katika historia ya nchi za Magharibi.

Juu ya ukurasa

Faslu Ya Pili: Mwanamke Katika Utamaduni Wa Magharibi

Mwanamke katika Sanaa na Fasihi ya Magharibi

Wamagharibi wamekumbwa na ugonjwa wa kuchupa mipaka katika suala zima la juhudi zao za kutaka kutambua na kudiriki maumbile halisi ya mwanamke na jinsi ya kuamiliana naye. Kimsingi mtazamo wa Magharibi kuhusu mwanamke ni mtazamo uliojengeka juu ya msingi ya utovu wa usawa na ukosefu wa uadilifu. Kaulimbiu na shaari zinazopigwa huko Magharibi ni nara tupu na hazina ukweli wowote ndani yake. Huko magharibi mwa dunia kuna fikra na mtazamo maalumu kuhusu mwanamke ambao asili na chanzo chake ni barani Ulaya. Kama fikra hiyo itashuhudiwa katika sehemu yoyote ile nyingine duniani basi ijulikane wazi kwamba chanzo chake ni Ulaya. Na utamaduni wa Magharibi nao huwezi mtu kuuelewe kwa kuangalia kaulimbiu na shaari tu zinazopigwa kudai ni za kumlinda mwanamke. Bali mtu inabidi apige mbizi ndani ya sanaa na fasihi ya Magharibi ndipo ataweza kuujua vyema utamaduni wa Magharibi. Mtu yeyote anayefuatilia na anayeijua fasihi ya Ulaya, mashairi ya nchi za Ulaya, riwaya zake, simulizi na tamthilia zake atakuwa anajua kwamba utamaduni wa Ulaya kuanzia kipindi cha karne za kati na baada ya hapo hadi kufikia katikati ya karne za hivi sasa, ulikuwa unamwangalia mwanamke kama kiumbe cha daraja la pili! Watakuwa wanasema uongo kama watadai kwamba hali haikuwa hivyo. Katika tamthilia maarufu za mwanafasihi mashauhuri wa Uingereza Shakespeare na fasihi nyinginezo za Magharibi utashangaa kuona jinsi lugha ya kumdunisha na kumdhalilisha mwanamke inavyotumika kwa wingi. Katika fasihi ya Magharibi mwanamme anatajwa kuwa bwana na lodi wa mwanamke anayemmiliki kiumbe huyo na kila alicho nacho. Baadhi ya mifano ya utamaduni huo inashuhudiwa hadi leo hii.

Wazungu si tu kwamba walikuwa wanamdhalilisha na kumbagua mwanamke katika upande wa kazi, shughuli za viwandani na mfano wa mambo hayo, bali walimdhulumu pia mwanamke katika upande wa sanaa na fasihi. Mtu anapoangalia simulizi za Magharibi, riwaya, picha za kuchora na kazi nyinginezo nyingi za sanaa, anashuhudia mwenyewe jinsi utamaduni wa Magharibi ulivyokuwa unamwangalia vibaya mwanamke. Mtu anaweza kujiuliza je hakukuwa na mambo mazuri na yenye thamani za juu yaliyowahusu wanawake hata wadhalilishwe kiasi hicho? Je zile huruma za wanawake, upole wao, uraufu, urahimu na uhenezi waliopambwa nao wanawake na Mola wao ulikuwa hauonekani? Je, sifa ya kuwa mama na kazi ya malezi iliyokuwa inafanywa na wanawake huko Ulaya ilikuwa haionekani? Je, sifa wanayoiona Wamagharibi kuhusiana na mwanamke ni hiyo ya kuhusiana na matamanio ya kinafsi tu na ambayo wanadai ni mapenzi?! (Ambapo ni ghalati na makosa kudai kuwa hayo ni mapenzi, bali kwa hakika huo ni uasherati!). Hivyo ndivyo walivyotaka wamlee na kumlazimisha mwanamke awe, yaani awe chombo tu kuwavutia na kuwastarehesha wanaume. Hata mwanamke alipotumiwa kama mfanyakazi wa chini, hakutarajiwa kufanya kitu kikubwa kwani waliamini hana uwezo huo na alitumika kama nguvu kazi rahisi na ya kiwango cha chini. Katika simulizi za Magharibi na katika tungo za kishairi za Ulaya mara nyingi sana inashuhudiwa mume anamuua mkewe kutokana na hitilafu ndogo tu za kitabia na hakuna mtu yeyote anayemlaumu mume kwa kufanya hivyo! Binti naye hakuwa na haki yoyote ya kujiamulia mambo yake mbele ya baba yake. Katika hizo hizo tamthilia za Magharibi kinachoonekana ndani yake ni kwamba binti fulani analazimishwa kuolewa, au mwanamke fulani anauliwa na mumewe, au utaona kunasimuliwa habari ya familia fulani ambayo ndani yake mwanamke yuko chini ya mashinikizo yasiyo na kifani na vitu kama hivi. Hayo ndiyo yanayoshuhudiwa katika tamthilia zao. Hiyo ndiyo fasihi ya Magharibi. Utamaduni huo uliendelea kutawala barani Ulaya hadi katikati ya karne hii. Tab’an mwishoni mwa karne ya 19 Milaadia, kulianza kushuhudiwa harakati mbalimbalia huko Ulaya zilizopewa jina la kumkomboa mwanamke.

Juu ya ukurasa

Kinyume na Ustaarabu!

Utamaduni wa Kirumi unaotawala hivi sasa huko Magharibi unakubaliana na mambo yote isipokuwa mawili matatu ambapo moja kati ya mambo hayo na labda linaweza kuwa ndilo kubwa na muhimu zaidi, ni kuhifadhiwa na kulindwa hali ya kuoanishwa jinsia mbili za mwanaadamu yaani mwanamke na mwanamme. Yaani utamaduni huo unajizuia kikamilifu kuingilia hicho kitu kinachoitwa ni harakati ya ukombozi. Wana hisia kali sana kuhusiana na jambo hilo na kazi zote si muhimu kwao isipokuwa suala hilo. Kwa mtazamo wao, mtu atakuwa amepitwa na wakati na atakuwa amebaki nyuma kiutamaduni na kiustaarabu kama hatakubaliana na fikra hiyo. Iwapo itatokezea nchi yoyote ambayo ndani yake wanawake watawekewa mipaka fulani ya kutenganishwa na wanaume, basi Wamagharibi watapiga kelele nyingi wakidai nchi hiyo haijastaarabika. Kwa hakika na kwa mujibu wa mtazamo wao, ni kweli kwani ustaarabu wao umejengeka juu ya magofu ya ustaarabu huo wa Kirumi, hawana kitu kingine. Lakini fikra hiyo ni kinyume kabisa na thamani za kibinaadamu na haitabikiani kivyovyoe vile na uhakika wa mambo.

Juu ya ukurasa

Jinsi Mwanamke Anavyodhulumiwa katika Jamii za Magharibi

Kama nilivyotangulia kusema, mwanamke katika jamii yenye utamaduni wa Magahribi anatumika kama chombo cha kustarehesha wanaume na sio kama mtu huru ambaye hashughulishwi na mambo ya watu wengine, bali anashughulishwa na mambo yake mwenywe. Anachukuliwa kama kiumbe ambaye inabidi arekebishe mienendo yake kwa namna ambayo atawapendezesha wanaume wapita njia wa mitaani na wa masokoni. Vile vile amefanywa kiumbe cha kubebeshwa mzigo wa maudhi na izara za harakati chafu za wanaume asiowajua na ambao hawajali maneno na matendo yao wanapoonana na mwanamke! Hiyo ndiyo hatima iliyomkumba mwanamke katika jamii kama hizo. Tab’an ziko baadhi ya kesi zisizokuwa hivyo, lakini lililozoeleka katika jamii hizo ni hilo. Mwanamke hana heshima yoyote mbele ya mwanamme. Inapofika suala la wajibu wa kufanya kazi, hakushuhudiwi tofauti yoyote baina ya mwanamke na mwanamme. Mwanamke atatumikishwa kwa kiwango kile kile anachotaka mwajiri bila kutofautisha baina yake na mwanamme. Yaani waajiri hawajali kwamba kutokana na hali yake ya kimaumbile, mwanamke anatofautiana na mwanamme hasa linapofika suala la kufanya kazi zinazohitajia kutumia nguvu. Lakini linapofika suala la mwanamme kutaka astareheshwe na mwanamke, utaona mwanamme amewekewa suhula nyingi na kurahisishiwa njia zote kiasi kwamba mwanamke hana jinsi yoyote ya kujitetea.

Juu ya ukurasa

Maisha ya Anasa Sababu ya Kupotoka

Ninavyoamini mimi ni kwamba, kumili upande wa kupenda mambo ya kidunia, ya anasa na ya kileo na kuchupa mipaka katika masuala ya kujiremba, kujikwatua na kujionyesha mbele ya wanaume ni miongoni mwa sababu kuu za kupotoka jamii na kuvunganyika wanawake. Ili Wamagharibi wamfanye mwanamke kuwa kiumbe mwenye sifa wanayoitaka wao, wanalazimika wakati wote walete mitindo mipya na kushughulisha mitazamo, macho, nyoyo na akili za wanawake katika masuala hayo yasiyo na maana. Sasa mtu atakapokuwa wakati wote ameshughulishwa na mambo hayo atapata muda gani wa kufikiria matukufu na mambo hasa ya thamani? Bila ya shaka hapati muda wowote wa kufanya hivyo. Mwanamke ambaye fikra zake zote ni kutafuta njia ya kuwavutia wanaume, atapata muda gani wa kufikiria mambo ya maana?! Wakoloni wa Ulaya hawapendi hata kidogo kuona wanawake wa jamii za ulimwengu wa tatu wanakuwa na fikra nzuri au wanakuwa na malengo mazuri katika maisha yao. Vijana wa kike katika jamii za Kiislamu wanapaswa kuwa macho kabisa ili wasije wakatumbukia katika mtego huu usioonekana lakini ulio hatari kabisa, naam mtego wa utamaduni na fikra za Kimagharibi. Jamii ya akina mama inapaswa kujihadhari sana na mtego huo.

Juu ya ukurasa

Maana ya Uhuru wa Mwanawake katika Utamaduni wa Magharibi

Kaulimbiu kuu inayoshuhudiwa katika nchi za Magharibi leo hii ni uhuru wa mwanamke. Neno uhuru lina maana pana na linajumuisha kuachiliwa huru baada ya kutekwa au kuwa kifungoni, uhuru katika maadili – kwani maadili nayo ni aina fulani ya kifungo na kubana vitu – na pia uhuru kutokana na ushawishi utokanao na kutumiwa vibaya na mwajiri kama vile mwanamke kulipwa mshahara mdogo n.k. Uhuru pia unajumuisha kuwa huru kutokana na sheria ambazo zinamfanya mwanamke alazimike nazo mbele ya mumewe. Neno uhuru linaweza kutumika katika mambo yote hayo. Sasa swali linalojitokeza hapa ni kwamba ni aina gani ya uhuru inayojaribu kuonyeshwa na shaari zote hizi zinazotolewa kuhusiana na mwanamke; ambazo zinajumuisha sehemu kubwa ya matakwa na mahitaji maalumu ambayo baadhi yake yanakinzana kikamilifu?

Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa, katika ulimwengu wa Magharibi mambo mengi yanayotumika kwa jina la uhuru ni mabaya, yana madhara na hayatumiki kwa njia sahihi. Kwani hudaiwa ni uhuru kutoheshimu misingi na mipaka ya familia, hudaiwa ni uhuru kujiweka mbali kikamilifu na ushawishi wa mwanamme, aidha inadaiwa ni uhuru kutoheshimu misingi na mipaka ya ndoa, ya familia na kulea watoto wakati linapofika suala la kufanikisha malengo ya matamanio na hawaa za muda mfupi za kinafsi, lakini hiyo si maana sahihi hata kidogo ya uhuru. Hivyo ukitoa maneno matupu yanayosemwa katika ulimwengu wa Magharibi, uhuru unaotambuliwa na nchi hizo ni kama vile wanawake kutoa mimba ambapo nukta hiyo ni muhimu mno kwani licha ya kwamba kidhahiri inaonekana ni nyepesi na ndogo, lakini batini yake ni hatari mno. Hiyo ndiyo nara na matakwa ambayo hivi sasa ni maarufu na yanatolewa kwa wingi katika nchi za Magharibi, na ndio maana wameipachika jina la harakati ya uhuru na ukombozi wa mwanamke.

Ulimwengu wa kibeberu uliotitia ujahili unafanya kosa kubwa unapodhani kwamba heshima na thamani ya mwanamke inapatikana kwa kiumbe huyo kujipodoa na kujipiga mnada kwa wanaume ili macho yaliyojaa hawaa za nafsi yamwangalie, yaburudike na yamfurahikie. Upogo na upofu wa kile ambacho leo kinadaiwa ni “uhuru wa mwanamke” duniani na ambacho kimeuteka utamaduni wa Magharibi leo hii kimesimama juu ya msingi kwamba mwanamke aweke wazi maugo yake ya mwili mbele ya wanaume ili wanaume waweze kujistarehesha kijinsia. Huo ndio unaodaiwa ni ukombozi wa mwanamke. Watu ambao wameghiriki katika utamaduni wa kijahilia, potofu na haribifu wa Magharibi wanadai kuwa wanalinda na kutetea haki za binaadamu lakini kumbe wanamkandamiza na kumdhulumu mwanamke.

Juu ya ukurasa

Harakati za Kutetea Haki za Wanawake katika Nchi za Magharibi

Wakati harakati za kuwatetea wanawake kwa sura kama hiyo ya kuwadhulumu na kuwakandamiza wanawake linapongia kasi na kuimarika, ni jambo lililo wazi kwamba hupelekea kujitokeza pia masuala ya kuchupa mipaka. Ndio maana katika kipindi cha makumi kadhaa ya miaka ya tangu zilipojitokeza harakati hizo kumekuwa kukishuhudiwa kushamiri ufuska, uzinzi na kutoheshimu sheria huko Magharibi kwa madai ya uhuru na ukombozi wa mwanamke kiasi kwamba leo hali imekuwa mbaya mno na inawatisha wanafikra wa Magharibi! Leo hii watu wanaoumizwa na hali hiyo, watu wanaozitakia kheri jamii za Magharibi, watu wenye hisia za kibinaadamu katika nchi hizo wanasikitishwa na kuumizwa mno na hali hiyo na tab’an hawawezi kuizuia. Sasa badala ya Wamagharibi kumkomboa na kumpa uhuru mwanamke, wamezidi kumtumbukiza katika matatizo makubwa zaidi. Kitendo cha Wamagharibi cha kutoa uhuru usio na mipaka, kueneza ufasiki na uasherati na kutoweka mipaka katika maingiliano ya wanaume na wanawake kimevuruga kabisa misingi ya familia katika nchi za Magharibi. Wakati mwanamme anapokuwa huru kushibisha kirahisi matamanio yake ya kijinsia katika jamii, na wakati mwanamke anaporuhusiwa kukutana kimwili na kujamiiana na wanaume hawa na wale bila ya tatizo lolote ni wazi kwamba watu wa aina hiyo hawawezi kuwa wenza wazuri katika ndoa. Hali ikiwa hivyo, misingi ya familia huangamia.

Kwa kweli harakati za kumlinda mwanamke huko Magharibi ni harakati zisizo na faida, ni harakati zisizo za kimantiki, ni harakati zilizosimama juu ya msingi wa upofu na kutojua kitu, ni harakati zisizo na misingi ya mafundisho ya kidini na ni harakati zisizojali maumbile na dhati ya mwanamme na mwanamke na ndio maana zimeleta madhara makubwa kwa wote, kwa wanawake na kwa wanaume na madhara makubwa zaidi wamepata wanawake wenyewe wanaodaiwa kukombolewa. Ni wazi kwamba mambo hayo hayastahiki kuigwa. Huo ni utamaduni ambao hauna wanunuzi katika nchi za Kiislamu, hakuna mtu mwenye welewa wa kweli atakayekubaliana na utamaduni kama huo katika ulimwengu wa Kiislamu. Utamaduni kama huo inabidi ufutwe.

Juu ya ukurasa

Mateso ya Wanawake katika Familia

Leo hii pia wakati mwanamke anapooana na mwanamme na kwenda nyumbani kwake huko Magharibi, hata jina la familia yake linabadilishwa na mwanamke analazimika kuchukua jina la familia ya mumewe. Mwanamke ataendelea kuwa na jina la familia yake hadi pale anapoolewa, akishaolewa tu, hupokonywa jina la familia yake na kupewa la familia ya mumewe. Hiyo ndiyo mila ya Wamagharibi. Lakini nchini Iran hali hiyo haikuweko huko nyuma na hivi sasa pia haipo. Katika utamadunia wa Ulaya, wakati mwanamke alipokuwa anaolewa na akatokezea kuwa na mali na vitu mbalimbali, si tu kwamba mwili wake ulikuwa mali ya mumewe, lakini mali na milki yake yote alipokonywa na kupewa mumewe! Huo ni ukweli na uhakika ambao Wamagharibi hawawezi kuukana hata kidogo. Hayo pia yalikuwemo kwenye utamaduni wa Magahribi. Katika utamaduni wa Magharibi wakati mwanamke alipokuwa ameolewa na kwenda nyumbani kwa mumewe, mume kwa hakika alikuwa anamiliki hata roho ya mwanamke huyo! Ndio maana katika simulizi za Magahribi na katika mashairi ya nchi za Ulaya mara nyingi mnashuhudiwa kesi zinazoonyesha kwamba mume amemuua kirahisi mkewe kutokana na kosa dogo tu na ilikuwa hatokezei mtu yeyote kumlaumu muuaji huyo! Binti naye alipokuwa katika nyumba ya baba yake hakuwa na maamuzi yoyote yale. Tab’an hata katika wakati huo pia, maingiliano ya wanaume na wanawake katika jamii za Magharibi yalikuwa huru kwa kiasi fulani, lakini baba ndiye pekee aliyekuwa na haki na uamuzi wa kumwozesha na kuchagua mume amtakaye kwa ajili ya binti yake hata kama ni kinyume cha matakwa ya binti huyo.

Ndani ya familia za Magharibi pia, hata yule mwanamke ambaye ni mfanyakazi kama mumewe na wote wakawa wanafanya kazi kwa masaa sawa, yeye naye anadhulumiwa! Vipi anadhulumuliwa? Ni kwa sababu watu hao wawili, mmoja ni mwanamme na mwingine ni mwanamke. Ni watu wawili, wote wanafanya kazi na ikifika usiku wanarejea nyumbani na kulala na asubuhi ya siku ya pili yake wanakwenda kazini kama kawaida. Lakini kinachosahaulika hapo ni kwamba watu hao wawili si kwamba ni wanaume tu, bali ni mwanamme na mwanamke. Mwanamke na mwanamme, kila mmoja wao kuna kitu kingine anahitajia. Ni sawa, mwanamme naye anadhulumika, lakini anayedhulumika zaidi ni mwanamke. Kwani mwanamme huyu ambaye ni mume wa mwanamke anayejitegemea kiuchumi, utampata ana uhusiano wa kijinsia na wanawake kadhaa nje ya ndoa. Pengine uhusiano na maingiliano yake na wanawake wengine ni mkubwa na bora zaidi kuliko baina yake na mkewe! Hilo bila ya shaka yoyote ni pigo kubwa sana kwa mwanamke! Anachotaka mwanamke ni kuwa na uhusiano na maingiliano ya kimapenzi, kushibana na ya karibu sana na mwenzake katika ndoa. Anataka kusiwe na mtu yeyote kati yao na uhusiano wake na mumewe uwe wa karibu zaidi kuliko na mtu mwingine yeyote. Hicho ni moja ya vitu vikubwa sana anavyoporwa mwanamke katika familia kama hiyo.

Juu ya ukurasa

Kuheshimiwa ndani ya Muundo wa Kudhalilishwa

Hutokezea baadhi ya wakati ikaonekana kana kwamba mwanamke katika jamii ya Magharibi anapewa heshima anayostahiki mfano wake ni ile inayoitwa heshima kwa wanawake kama wacheza filamu au wakati wanawake wanaposhirikishwa katika mashindano ya warembo n.k. Utaona kama vile wanaheshimiwa, lakini heshima hiyo ndiyo hiyo tunayoisema ni heshima ndani ya muundo wa kudhalilishwa. Au udhalilishaji ndani ya muundo wa heshima na mfano wa mambo hayo unaonekana wazi katika maisha binafsi ya watu na kwamba watu wanaweza kuona kwa macho yao na kujua maana hasa ya “Udhalilishaji katika muundo wa heshima” na “Heshima katika muundo wa kudhalilisha.” Heshima katika muundo wa kudhalilisha ni moja ya matatizo makubwa yaliyopo. Wakati mwanamke anapotumbukia katika mtego wa mahusiano yasiyo na mipaka kati ya mwanamme na mwanamke, matokeo yake huwa kama yale yaliyokuwa yakishuhudiwa nchini Iran wakati wa utawala wa Kipahlavi na tawala za kifalme nchini Iran wakati wanawake waliposukumwa upande wa kutembea uchi katika jamii, kubwikia mitindo hii na ile, kuhibu anasa kupindukia na kupenda kujiremba kwa sura tofauti. Kujiweka msafi na kujipamba kwa kiwango kinachotakiwa ni jambo zuri na Uislamu hauzuii jambo hilo. Lakini inabidi kitu hicho kitendeke kwa kiwango kinachotakiwa isiwe tena kwa sura ya kushindana, kuoneana choyo, na isiwe kwa namna ya mikinzano na kumfanya mwanamke ajifunge tu na mambo hayo kwani kufanya hivyo huwa chanzo cha upotofu. Malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kinyume kabisa na kitu hicho.

Juu ya ukurasa

Upinzani dhidi ya Utamaduni wa Wanawake wa Kiislamu

Ni kitu gani kinawapelekea Wamagharibi wamfanyie uadui mkubwa mwanamke wa Kiislamu? Ni hijabu yake. Wamagharibi wana uadui mkubwa mno na Hijabu sahihi ya mwanamke wa Kiislamu kuliko kitu kingine chochote. Kwa nini? Kwa sababu utamaduni wao haukubaliani na vazi hilo. Hivi ndivyo walivyo Wazungu. Wanachoshikilia na kukiamini wao ni kwamba kila ambacho wao wanakikubali ni sahihi na dunia nzima inabidi iwafuate wao! Wanachotaka ni kuona ujahili na ujinga wao unafunika maarifa yote duniani. Wanataka kueneza utamaduni wa mwanamke wa Ulaya katika kila kona ya dunia nao ni utamaduni wa mitindo ya kisasa, ufujaji wa mali, kujipodoa na kujianika mbele ya kadamnasi ya wanaume, kufungua njia zote za kuchochea na kuhamasisha maingiliano haramu ya kijinsia baina ya mwanamke na mwanamme; vitu hivyo ndivyo wanavyotaka kuvieneza ulimwenguni kupitiwa mwanamke. Ndio maana unawaona wanalalamika sana kila panapotokezea mahala fulani duniani pakapinga malengo yao hayo. Wamagharibi hawana uvumilivu! Licha ya majigambo yao makubwa, lakini Wamagharibi hawawezi kuvumilia wala kusubiria upinzani wowote ule dhidi yao.

Wamagharibi wameweza kuathiri maeneo yote duniani isipokuwa katika maeneo yenye Uislamu wa kweli. Katika ulimwengu maskini wa Afrika na Amerika ya Latini na mashariki mwa Asia na kwenye sehemu zozote za watu, Wamagharibi wameweza kupandikiza utamaduni wao. Sehemu pekee waliyoshindwa kufanya hivyo ni katika maeneo yenye Uislamu wa kweli, na mfano wa wazi kabisa ni katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ndio maana wanapambana kwa nguvu zao zote na jambo hilo.

Juu ya ukurasa

Umilikaji Mali Wanawake katika Utamaduni wa Ulaya na Utamaduni wa Kiislamu

Hadi miaka sitini au sabiini iliyopita, katika maeneo yote ya Ulaya na katika nchi za Magharibi, mwanamke alikuwa akidhibitiwa kikamilifu na mwanamme – ima mumewe au mwanamme mwengine kama vile mmiliki wa kiwanda na shamba – na mwanamke hakupewa haki yoyote aliyopaswa kuwa nayo mtu anayeishi katika jamii iliyostaarabika. Wanawake walinyimwa haki ya kujiamulia mambo yao, haki ya kumiliki, haki ya kufanya miamala n.k. Baadaye tena ndipo walipokuja kumwingiza mwanamke katika medani ya kazi na maisha na shughuli za kijamii. Hatimae iliainishwa haki mwanamke kumiliki mali huko Ulaya, ambapo kwa mujibu wa ripoti za uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa elimu jamii wa huko huko Ulaya ni kwamba jambo hilo lilifanyika kutokana na kuwa viwanda ambavyo vilikuwa vimeanza kupanuka na kutumia teknolojia ya kisasa, vilihitajia kuwa na vibarua na wafanyakazi wengi wa daraja la chini. Wafanyakazi wa aina hiyo nao walikuwa wachache. Hivyo ili kuwavutia wanawake kufanya kazi viwandani, na ili viwanda hivyo viweze kupata nguvukazi viliyohitajia, walilazimika kutangaza kwamba mwanamke ana haki ya kumiliki mali! Tab’an pamoja na hayo, mwanamke alipewa mshahara wa chini kabisa licha ya kazi ngumu aliyofanya. Ilikuwa ni mwanzoni mwa karne ya 20 ndipo Wazungu walipompa mwanamke haki ya kumiliki kitu chake, lakini wakati huo huo wakafungua njia zote za kumpotosha mwanamke na matokeo yake ikawa ni kutelekezwa mwanamke katika jamii akakosa pa kushika. Huu ndio huo mtazamo ghalati wa kuchupa mipaka na hiyo ndiyo dhulma kubwa aliyofanyiwa mwanamke wa Magharibi na barani Ulaya.

Amma katika Uislamu hali haikuwa hivyo kabisa. Katika Uislamu mwanamke anamiliki mali yake mwenyewe. Ni sawa tu jambo hilo limridhishe mumewe au lisimridhishe, baba yake akubaliane nalo au asikubaliane nalo – yote ni sawa – hakuna kitu cha kumzuia asimiliki mali yake na kutumia mali yake hiyo vile anavyopenda. Hiyo ni mali yake na haina uhusiano wowote na mtu mwingine. Uislamu uko mbele kwa karne 13 katika suala zima la kulinda na kutetea uhuru na kujitegemea kiuchumi mwanamke, ikilinganishwa na aidiolojia nyinginezo. Uislamu ulimpa haki hiyo mwanamke karne 13 zilizopita, (tangu ilipodhihiri dini hiyo tukufu ya Mwenyezi Mungu, vipi leo wanatokea watu na kudai bila ushahidi kwamba Uislamu unamnyima haki yake mwanamke?).

Juu ya ukurasa

Faslu Ya Tatu: Nafasi Ya Wanawake Katika Mfumo Wa Jamhuri Ya Kiislamu Ya Iran

Nafasi ya Wanawake katika Historia ya Zama Hizi ya Iran

Nchini Iran, nafasi ya mwanamke ni kubwa sana kutokana na mazingira maalumu yaliyojitokeza hivi sasa na pengine katika matukio mengine mengi makubwa. Iwapo tutaiangalia historia ya miaka 150 iliyopita ya mwanamke wa Kiirani – historia ambayo ni muhimu sana na ni yenye mafunzo mengi – tutaona kuwa, harakati na ushiriki wa mwanamke katika baadhi ya medani muhimu sana, ni mkubwa mno na ulisaidia kwa kiwango kikubwa sana. Mfano mmoja ni kushiriki vilivyo wanawake katika mapambano dhidi ya ubeberu yaliyoongozwa na maarhum Mirzai Shirazi nchini Iran. Hata hapa mjini Tehran, maandamano ya wanawake hao yalikuwa makubwa sana. Hii inaonyesha kwamba wanawake nchini Iran walikuwa macho na walifanya harakati mbali mbali kwa jina la Uislamu, hata kabla ya matukio yanayohusiana na Mapinduzi ya Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Mwanamke katika Zama za Ufalme za Kipahlavi Nchini Iran

Mwanamke alidhulumiwa katika nyanja zote wakati wa utawala muovu wa Kipahlavi nchini Iran. Wakati mwanamke alipotaka kuingia katika uga wa kielimu, alilazimishwa aachane na itikadi zake za kidini, ucha Mungu na staha yake aliyotunukiwa na Uislamu. Mwanamke wa Kiislamu alikuwa hawezi kuvaa kirahisi vazi lake la hijabu na kujisitiri vyema katika maeneo ya Vyuo Vikuu na vituo vingine vya elimu. Katika barabara za Tehran na baadhi ya miji mikubwa ya Iran ilikuwa haiyumkini kwa mwanamke wa Kiislamu kujisitiri vyema na kutekeleza mafundisho ya dini yake. Hilo halikuwa rahisi pia hata kwa wale ambao hijabu zao hazikuwa kamili. Wanawake hao walikuwa hawasalimiki na kejeli, maneno machafu na masimbulizi ya watu waliokuwa wamezama katika ufuska na ufasiki wa Kimagharibi. Hali waliifanya kuwa nguvu kwa wanawake wa Kiislamu kiasi kwamba ilikuwa haiwezekani kwa wanawake wengi wa Kiislamu kutafuta elimu nchini. Ilikuwa si rahisi kwa mwanamke wa Kiirani kuingia katika uga na uwanja wa kutafuta elimu ila kwa kuvua hijabu yake na kuachana na taqwa na staha ya Kiislamu.

Katika uwanja wa kisiasa na kwenye uga wa kazi za kijamii pia, hali ilikuwa ni hiyo hiyo. Wakati mwanamke alipotaka kuwa na cheo katika masuala ya kijamii na kisiasa nchini Iran wakati wa utawala wa kifalme wa Kipahlavi, alilazimika aachane kabisa na suala la kuvaa hijabu na kutekeleza mafundisho ya Kiislamu ambayo dini hiyo tukufu inamtaka ayatekeleze. Tab‘an ilitegemea kipaji cha mwanamke mwenyewe ni cha kiasi gani. Kama alikuwa mlegevu sana, alikuwa analazimishwa kuporomoka kiasi chote hicho. Kama alikuwa ni mtu wa msimamo na mwenye kulinda itikadi yake, aliweza kukwepa baadhi ya mambo, lakini daima aliwekwa chini ya mashinikizo ya kila namna ya mazingira ya kijamii yaliyokuwa yamepandikizwa wakati huo.

Wakati wa utawala wa kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran sambamba na kuwa idadi kubwa ya wanawake hawakuwa na elimu, na walishindwa kujua chochote katika masuala ya kijamii kutokana na kuwa hawakuelimishwa wala walikuwa hawapewi mwanya wa kufuatilia masuala ya kijamii na wala hawakuwa na mapenzi na mustakbali wa nchi yao na walikuwa hawajui kamwe kwamba mwanamke anaweza kuwa na nafasi katika kuainisha mustakbali wa nchi yake, pamoja na yote hayo, lakini kidhahiri ulikuwa unawaona wanawake hao kama vile ni wanawake wa Ulaya na katika baadhi ya mambo walikuwa hata wanawashinda wanawake wa Ulaya. Akikutokezea mbele yako ungelidhani labda ni mtu fulani kutoka Ulaya ndio kwanza amewasili nchini Iran, lakini ukikaa naye na kumuuliza maswali mawili matatu ulikuwa unamuona mwanamke huyo ima hakusoma kabisa, au elimu yake ni ndogo sana! Walimlazimisha mwanamke ajikweze na kujionyesha mbele ya watu kana kwamba ni mtu muhimu sana, lakini uhakika wake ni kwamba hakuwa na chochote cha maana zaidi ya heshima bandia. Huko ilikuwa ni kuporomoka mwanamke na kamwe hayo hayakuwa maendeleo ya mwanamke. Je, kuna dhulma kubwa kushinda hii ya kumchukua mwanamke na kuanza kumremba kichwa chake kwa mitindo hii na ile ya nywele na kumvisha nguo na dhahabu na mapambo mengine halafu kumfanya kama bidhaa na ala ya kufanikishia malengo mbalimbali ya wanaume na wakati huo huo kumkataza asiingie katika medani za siasa, maadili bora na malezi sahihi? Hilo ndilo lililokuwa likitendeka katika utawala wa kifalme wa Kipahlavi nchini Iran kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Nafasi ya Mwanamke katika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamekuja kuondoa mitazamo yote batili kuhusiana na mwanamke na kwamba wanawake wamekuwa ni askari wa mstari wa mbele wa Mapinduzi ya Kiislamu. Laiti kama wanawake hawangelikuwa mstari wa mbele katika Mapinduzi ya Kiislamu na lau kama wasingelikuwa na ule mwamko waliokuwa nao, bila ya shaka Mapinduzi haya yasingeliweza kufikia ushindi. Kama wanawake wasingelikuwepo, basi nusu ya nguvu ya wanamapinduzi – yaani wanawake - isingelijikeza katika medani. Si hayo tu, lakini pia wanawake walikuwa na nafasi muhimu ya kuwahimiza watoto wao, waume zao, makaka zao na mazingira ya ndani ya familia kujiunga na wanamapinduzi. Ni jambo lililo wazi kwamba mwanamke ana nafasi muhimu sana katika upande wa utamaduni wa ndani ya familia. Ulikuwa ni uwepo huo wa wanawake ndio ulioweza kuvunja misingi ya adui na mapambano yakapata sura yake halisi. Wanaume iwe waume au watoto wa kiume nyumbani waliathiriwa na wanawake ima wake zao au mama zao na hivyo kupata nguvu ya kujiunga na wanamapinduzi. Hayo ndiyo maumbile ya mwanamke. Kiujumla ni kuwa hata mwanamke asiyejua kusoma na kuandika ana ushawishi maalumu katika familia. Ushawishi wake huo si kama ule wa mwalimu kwa mwanafunzi wake wala kwa mkuu na watu walioko chini yake. Ushawishi wa mama kwa wanawe ni maalumu na ni wa aina nyingine kabisa na ambao unaendelea kuwepo hata baada ya mama kuwa bikizee na mkongwe sana. Yaani kama mwanamke atataka kutumia roho yake ya umama na ushawishi wake aliojaaliwa kuwa nao na Mwenyezi Mungu kwa mwanawe, anaweza kufanya hivyo na athari zake zikawa za ajabu, labda tu dhati ya mwanamke mwenyewe iwe ni dhaifu au asitake kutumia ushawishi wake huo. Kiujumla ni kwamba mama ana athari kubwa kwa mwanawe. Maneno yake, mapenzi yake, mazungumzo yake yanayotokana na mapenzi yake kwa mwanawe hupenya, na kujikita vilivyo katika akili ya mwanawe.

Wakati harakati na mwamko wa Kiislamu ulipofika kwenye hatua ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na wakati wanawake kama unavyofundisha Uislamu walipojitokeza mstari wa mbele kuunga mkono harakati hiyo, Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) alisema: Laiti kama wanawake hawangelishiriki kwenye mwamko na harakati hiyo, basi Mapinduzi ya Kiislamu yasingelifikia ushindi. Katika suala zima la kuasisiwa na kuimarika Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran pia, wanawake katika baadhi ya matukio makubwa hata waliwashinda wanaume, badhi ya wakati walikuwa bega kwa bega na wanaume na baadhi ya wakati wanaume waliwashinda wanawake. Mfano wake ni katika vita (vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Iran), katika matukio mbali mbali ya kisiasa na kwenye masuala ya kijamii katika sehemu zote hizo, nafasi na ushiriki wa mwanamke umekuwa ni jambo la kawaida kabisa.

Shakhsia ya kijamii ya mwanamke ambaye ni kiungo muhimu katika majimui hiyo adhimu, ina umuhimu mkubwa. Huko nyuma walikuwa hawalizingatii kabisa suala hilo na wala walikuwa hawalitilii maanani jambo hilo muhimu. Ilikuwa hata hakufikiriwi nafasi ya mwanamke katika majukumu makuu ya jamii, na wao wenyewe nao walikuwa hawajitokezi na kutaka kuwa na nafasi katika masuala hayo. Lakini leo hali imebadilika. Wanawake wote wa vijijini na mijini na hata wa maeneo yaliyoko mbali, wanajiona wana nafasi muhimu katika suala zima la kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu na wafuasi wake. Hakuna tofauti yoyote katika jambo hilo kati ya mwanamke na mwanamme, bali baadhi ya wakati unaweza ukaona wanawake wana imani zaidi, wana hamasa zaidi na wana mwamko mkubwa zaidi katika masuala ya jamii, ya nchi yao na yale mambo yanayowahusu wao.

Juu ya ukurasa

Mapinduzi ya Kiislamu na Nafasi ya Kijamii ya Wanawake

Ulipokuja Uislamu, yalipotokezea Mapinduzi, ilipojitokeza harakati ya Imam (Khomeini – Mwenyezi Mungu amrehemu) nchini Iran, mwanamke wakawa katikati ya shughuli za kisiasa na Imam akawapa akinamama bendera ya Mapinduzi ya Kiislamu na wakati huo huo mwanamke wa Kiislamu nchini Iran amekuwa akijishughulisha na kazi zote hizo huku akiwa anachunga kikamilifu vazi lake la Hijabu pamoja na takwa, kuheshimu mafundisho ya dini na staha na heshima yake ya Kiislamu.

Kwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu mwanamke leo hii yumo kwenye mkondo mzuri sana. Leo mwanamke wa Kiirani anaweza kuingia katika medani ya kutafuta elimu na kupanda daraja mbali mbali za kielimu na wakati huo huo akiwa anaweza kuchunga kikamilifu mafundisho ya dini yake tukufu ya Kiislamu kama vile Hijabu, taqwa, heshima, staha na utukufu wa mwanamke wa Kiislamu. Leo mwanamke nchini Iran anashiriki vilivyo katika masuala ya kisiasa, kijamii, kijihadi na anasaidiana na wanaume katika kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu na kama mwanamme, anajitokeza vilivyo kwenye medani mbalimbali na wakati huo huo akiwa na utulivu kamili huku akilinda thakafa, Hijabu, hadhi, murua na ustahifu aliotunukiwa na dini yake ya Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Nafasi ya Mwanamke katika Mtazamo wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu awe radhi naye)

Mwalimu mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu yaani Imam Khomeini (Quddisa Sirruh) alikuwa anaipa umuhimu mkubwa sana nafasi ya mwanamke katika Mapinduzi ya Kiislamu – iwe ni wakati wa kudhihiri kwake Mapinduzi hayo au baada ya kutokea mapinduzi hayo – na alikuwa anaamini kwamba nafasi ya mwanamke katika suala zima la kuifikisha jamii katika ukamilifu wake wa Kiislamu na kimapinduzi ni kubwa sana na huo kwa kweli ndio ukweli wenyewe wa mambo. Sasa ili kuweza kutekeleza vilivyo jukumu lake hilo, mwanamke wa Kiirani na mwanamke wa Kiislamu anapaswa kuendelea na jitihada zake kubwa za kupambana na mitego ya misingi ya utamaduni wa Magharibi. Mwanamke wa Kiislamu anapaswa kuwa imara na madhubuti na asikubali kutekwa na fikra potofu za Magharibi fikra mbaya ambazo lengo lake hasa ni kufanikisha siasa angamizi na za kikoloni za Magharibi. Usanifu makini na wa busara unahitajika ili kuweza kutofautisha baina ya nafasi na heshima ya kielimu, kiutamaduni, kijamii, kisanaa na kisiasa ya mwanamke na kuporomoka kwake kimaadili hadi kufanywa kuwa chombo na ala ya kufanikishia malengo ya kisiasa na shabaha binafsi za wanaume.

Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu siku zote alikuwa akijaribu kumpa mwanamke katika jamii ya Kiirani - ambapo wanawake ni nusu ya jamii ya nchi hii na katika nyakati nyeti hata huzidi nusu ya jamii yote nchini – heshima yake ya kweli ambayo ilikuwa imepuuzwa na ilikuwa imefunikwa na kufichwa katika sura mbali mbali. Imam Khomeini alikuwa akisisitiza sana juu ya kupatiwa mwanamke heshima na nafasi yake hiyo. Alikuwa akiwahimiza sana watu hususan wanawake wenyewe, wafanye juhudi kubwa za kuhakikisha kuwa jambo hilo muhimu linafanikishwa.

Juu ya ukurasa

 
< Nyuma   Mbele >

^