Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Haki na Nafasi ya Mwanamke katika Jamii Chapa
13/02/2010

Faslu Ya Kwanza Nafasi Ya Mwanamke Katika Jamii

Nafasi ya Mwanamke katika Jamii ya Mwanaadamu
Mtazamo Sahihi Kuhusiana na Mwanamke
Kudhulumiwa Mwanamke katika Historia
Suala la Mwanamke Duniani
Nafasi ya Hijabu katika Ukamilifu wa Kijamii wa Mwanamke
Jukumu na Nafasi ya Mwanamke
Misingi ya Harakati za Kijamii za Wanawake
Nafasi ya Mwanamke katika Ustawi wa Taifa
Wajibu wa Kutafuta Elimu
Mwanamke Kazini

Faslu Ya Pili Nafasi Ya Mwanamke Katika Familia

Malezi ya Kiislamu ya Mwanamke
Haki ya Kujichagulia Mume
Mifano Miwili ya Ujahilia katika Ndoa
Nafasi ya Kupata Utulivu
Umuhimu wa Mwanamke katika Familia
Ushawishi wa Nguvu za Kimaumbile za Mwanamke
Kitovu cha Mapenzi
Kugawana Majukumu
Umuhimu wa Kwanza ni wa Kazi za Nyumbani
Jukumu la Kulea Watoto
Simulizi ya Ua na Bustani
Kudhulumiwa Mwanamke Ndani ya Familia

Haki na Nafasi ya Mwanamke katika Jamii

Faslu Ya Kwanza Nafasi Ya Mwanamke Katika Jamii

Nafasi ya Mwanamke katika Jamii ya Mwanaadamu

Kadhia ya mwanamke na muamala wa jamii mbali mbali duniani kuhusu mwanamke ni suala ambalo limekuwepo kwa karne nyingi katika jamii na tamaduni mbali mbali ulimwenguni. Daima wanawake wamekuwa wakiunda nusu ya watu duniani. Mwanamke amekuwa akikabiliana na mashaka ya maisha ya dunia kama anavyofanya mwanamme. Kikawaida mwanamke huwa anafanya kazi kubwa zaidi za kimaumbile ikilinganishwa na mwanamme. Kazi za kimsingi za kimaumbile kama vile kuendeleza kizazi cha mwanaadamu na kulea watoto inafanywa na mwanamke. Hivyo suala la mwanamke ni suala muhimu sana na limekuwepo kwa muda mrefu sana baina ya wanafikra na katika maadili na mila na desturi za mataifa yote duniani.

Juu ya ukurasa

Mtazamo Sahihi Kuhusiana na Mwanamke

Inabidi kumwangalia mwanamke kwa jicho la binaadamu mwenye heshima ili kwa njia hiyo iweze kujulikana ukamilifu na haki na uhuru wa mwanamke ni upi. Inabidi mwanamke aangaliwe kwa jicho la kiumbe mwenye uwezo wa kuwa chemchemu ya ustawi wa jamii kwa kulea watu muhimu wenye heshima ili kwa njia hiyo iweze kujulikana haki ya mwanamke ni nini na uhuru wake ni upi. Inabidi mwanamke aangaliwe kwa jicho la kiungo muhimu na kikuu katika ujenzi wa familia na kwamba ingawa mwanamke na mwanamme, wote wawili wana nafasi muhimu ya kujenga familia bora, lakini suala la utulivu katika familia, utengemano na ushuwari katika mazingira ya ayali na kutabaradi mlango wa familia yoyote ile ni mambo ambayo yanawezekana kwa kuwepo mwanamke na maumbile maalumu aliyojaaliwa kuwa nayo. Inabidi mwanamke aangaliwe kwa jicho hilo ili iweze kubainika vipi mwanamke anaweza kufikia ukamilifu wake, na ziweze kujulikana vizuri haki zake.

Juu ya ukurasa

Kudhulumiwa Mwanamke katika Historia

Mwanamke amekuwa akidhulumiwa katika kipindi chote cha historia na katika jamii mbalimbali za mwanaadamu. Hayo yote yanatokana na ujinga wa mwanaadamu mwenyewe. Tabia ya watu majahili na katika jamii ambayo hakuna sheria ya kuwadhibiti watu, siku zote sheria inayotawala huwa ya mwenye nguvu kumkandamiza dhaifu. Hali huwa hivyo ila inapotokezea kwa mtu mwenyewe – na hii ni mara chache sana hutokezea – anapokuwa na imani sana na anapokuwa na ubinaadamu, au zinapokuwepo sababu za nje kama vile sheria za kumdhibiti mwanaadamu kama tulivyotangulia kusema. Kwa kawaida hali inakuwa hivyo, kwa mwenye nguvu kumdhulumu mnyonge na dhaifu katika jamii za kijahilia.

Inasikitisha kuona kuwa katika kipindi chote cha historia, kumekuwa kukishuhudiwa dhulma dhidi ya mwanamke kwa njia mbali mbali na mara nyingi dhulma hiyo inafanyika kutokana na kuwa mwanaadamu hajajua heshima ya mwanamke wala umuhimu wake. Mwanamke mwenyewe anapaswa ajue dhati na nafasi yake, na si sahihi hata kidogo kuelemezewa dhulma zote kwa sababu tu yeye ni mwanamke. Kitendo hicho ni kibaya sana. Ni sawa tu vitendo hivyo dhidi ya mwanamke vitafanywa kwa sura ya ukandamizaji wa moja kwa moja au vitafanywa kwa ukandamizaji usio wa moja kwa moja kama vile kumsukuma mwanamke katika upande wa anasa na kupenda matumizi na mapambo yasiyo na maana jambo ambalo linambebesha mwanamke magharama mazito mazito na kumdhulumu kwa kumfanya kuwa kama bidhaa na chombo cha matumizi. Hiyo ni dhulma kubwa anayofanyiwa mwanamke. Pengine tunaweza kusema kuwa, hakuna dhulma kubwa anayofanyiwa mwanamke kama hiyo kwani jambo hilo linamfanya mwanamke asahau kikamilifu malengo na shabaha za ukamilifu wake na kujishughulisha tu na mambo madogo madogo na ya kipuuzi.

Juu ya ukurasa

Suala la Mwanamke Duniani

Mwanaadamu licha ya kutoa madai haya na yale na licha ya kufanyika juhudi mbalimbali kwa ikhlasi na nia njema; licha ya kuweko kazi mbali mbali kubwa na pana za kiutamaduni hususan kuhusu kadhia ya mwanamke, lakini bado mwanaadamu hadi hivi sasa ameshindwa kupata njia sahihi na ya moja kwa moja kuhusu suala la jinsi mbili za mwanamke na mwanamme na jinsi ya kuamiliana na jinsi hizo mbili za mwanaadamu kwa njia sahihi.

Kwa maneno mengine ni kwamba, kupenda makubwa, upotofu, suutafahumu mambo ambayo yanafuatiwa na dhulma, uonevu, ukatili, matatizo ya kiakili, shida zinazohusiana na familia na mashaka yanayotokana na kuchanganyika kiholela wanaume na wanawake hadi hivi sasa ni miongoni mwa mambo ambayo mwanaadamu ameshindwa kuyatatua. Yaani mwanadamu ambaye amepiga hatua kubwa katika elimu za nyota na kwenye vina virefu vya baharini na licha ya kwamba mwanaadamu huyo amekuwa akijigamba sana kwa kuwa na utaalamu wa ndani kabisa katika masuala la kisaikolojia na ya kiakili pamoja na masuala ya kijamii, ya kiuchumi na mengineyo - na kwa hakika amepiga hatua kubwa kweli katika elimu hizo - lakini pamoja na hayo ameshindwa kuamiliana vizuri na suala la mwanamme na mwanamke.

Juu ya ukurasa

Nafasi ya Hijabu katika Ukamilifu wa Kijamii wa Mwanamke

Katika dini tukufu ya Kiislamu kuna stara na hifadhi baina ya mwanamke na mwanamme. Hii haina maana kwamba mwanamke asijihusishe kabisa na masuala ya dunia au awaachie wanaume tu wafanye hivyo, hapana, Uislamu unaruhusu mwanamme na mwanamke kuishi kwa pamoja katika jamii na kufanya kazi pamoja na wanakutana katika sehemu zote na wanashirikiana katika kutatua matatizo ya kijamii, wanashirikiana hata katika masuala ya vita (na kulinda mataifa yao), wanafanya kazi bega kwa bega za kifamilia na kulea watoto wao, lakini pamoja na hayo Uislamu unawataka wachunge stara na hifadhi iliyowekwa na Mwenyezi Mungu nje ya mazingira ya familia bali hata ndani ya familia. Hii ni moja ya sifa maalumu za dini tukufu ya Uislamu ya kutoa vigezo vikuu vya kufuatwa.

Iwapo jambo hilo halitachungwa, matokeo yake yatakuwa ni uduni na ugoigoi kama ambao leo hii unazikabili jamii za Magharibi. Kama jambo hilo halitazingatiwa, basi mwanamke atazorota na kubakia nyuma katika harakati ya kuelekea kwenye matukufu ambayo leo hii wanawake wa Iran ya Kiislamu wanashuhudiwa kuwa nayo.

Suala la Hijabu halina maana ya kumdhalilisha na kumtenga mwanamke na masuala ya duniani. Mtu yeyote mwenye mawazo kama hayo ajue kwamba anakosea kikamilifu. Suala la Hijabu lina maana ya kuondoa maingiliano na mchanganyiko usiokubalika na wa kiholela kati ya wanaume na wanawake katika jamii. Michangayo kama hiyo isiyoheshimu sheria ina madhara kwa jamii na ina athari mbaya pia kwa mwanamke na mwanamme na hususan mwanamke mwenyewe. Kuchunga vazi la staha la Hijabu kunamsaidia mwanamke kupata hadhi na cheo chake cha kimaanawi na humuepusha mwanamke kutumbukia kwenye mitego, magube na ghururi za kidunia. Hivyo harakati yoyote inayofanyika kwa ajili ya kumlinda na kumtetea mwanamke, inabidi nguzo yake kuu iwe ni kulinda staha na heshima ya mwanamke. Staha ya mwanamke huwa sababu ya kupata utukufu na heshima mwanamke huyo mbele ya wengine na hata mbele ya wanaume waasherati na wahuni. Staha ya mwanamke humzawaida kiumbe huyo heshima na utu. Uislamu unalipa umuhimu mkubwa suala la stara ya mwanamke. Tab’an staha ya wanaume nayo ni kitu muhimu. Tukumbuke kwamba staha haihusiani tu na wanawake. Wanaume nao wanapaswa kuwa na staha.

Katika yale maeneo ambayo wanawake hawachungi vazi la staha la Hijabu, maeneo ambayo wanawake wanatembea uchi na kujiweka wenyewe kwenye mazingira ya kuvunjiwa heshima, jambo la kwanza linalowakumba wanawake hao linakuwa ni ukosefu wa usalama. Ukosefu huo wa usalama huwakumba kwanza wanawake kabla ya wanaume na vijana (wa kiume). Hivyo Uislamu unamwamrisha mwanamke achunge vazi la Hijabu ili mazingira anayoishi mwanaadamu yawe ya salama na amani, na ili mwanamke katika mazingira hayo aweze kufanya kazi zake kwa amani na utulivu katika jamii, na ili mwanamme naye aweze kutekeleza inavyopasa majukumu yake bila ya vishawishi wala matatizo yoyote.

Juu ya ukurasa

Jukumu na Nafasi ya Mwanamke

Katika jamii ya Kiislamu, uwanja uko wazi kwa mwanamme na mwanamke. Ushahidi wa jambo hilo ni athari nyingi za Kiislamu zilizopo kuhusu suala hilo na mambo yote ya wajibu ambayo Uislamu unawaamrisha mwanamme na mwanamke kutekeleza kwa pamoja bila ya ubaguzi. Wakati Bwana Mtume Muhammad SAW anaponukuliwa akisema: Mtu yeyote asiyeshughulishwa na masuala ya Waislamu basi si Muislamu, jambo hilo huwa haliwahusu wanaume tu, bali linawahusu pia wanawake. Wanawake nao wana wajibu wa kushughulikia masuala ya Waislamu katika jamii ya Kiislamu na masuala ya ulimwengu wa Kiislamu pamoja na kadhia nyinginezo kama ilivyo kwa wanaume. Wanawake kama wanaume wana wajibu wa kuhisi kuwa wana majukumu mbele ya masuala yanayouhusu Uislamu. Mfano wa wazi ulionyeshwa na Bibi Fatimatuz Zahra (Salamullahi Alayha), binti wa Bwana Mtume Muhammad SAW ambaye tangu katika kipindi cha utoto wake na hata baada ya Bwana Mtume kuhajiri Makkah na kuhamia Madina, ndani ya mji wa Madina na katika masuala yote ya wakati huo ya baba yake, ambaye alikuwa kituo kikuu cha matukio ya kisiasa na kijamii, bibi Fatimatuz Zahra SA alishiriki katika matukio yote hayo jambo ambalo linaonyesha jinsi mfumo wa Kiislamu unavyompa nafasi muhimu mwanamke.

Kwa mujibu wa aya tukufu ya Qu’ani Tukufu iliyomo kwenye Suratul Ahzab hakuna tofauti yoyote kati ya mwanamke na mwanamme si katika suala la Uislamu, wala imani, wala dua, wala unyenyekevu, wala kutoa sadaka, wala kufunga, wala subira, wala istikama, wala katika kuchunga heshima za wengine, wala katika dhikri na kumtaja Mwenyezi Mungu. Mwanamme na mwanamke wako sawa sawa katika mambo yote hayo. Kazi za wanawake katika jamii ni kazi zinazoruhusiwa kabisa bila ya matatizo yoyote bali ndivyo inavyotakiwa lakini inabidi sheria za Kiislamu na mipaka ya dini hiyo tukufu ya Mwenyezi Mungu ichungwe. Wakati katika jamii jinsia zote mbili yaani mwanamke na mwanamme wanapokuwa wameelimika kundi la watu walioelimikia katika jamii linakuwa kubwa mara mbili ikilinganishwa na jamii ambayo wanaume tu ndani yake ndio walioelimishwa. Wakati wanawake katika jamii wanapokuwa ni watu waliosoma na walioelimika, walimu katika jamii hiyo huwa mara mbili ya wale wanaokuwepo wakati wanawake wanaponyimwa elimu. Hali huwa hivyo hivyo Katika kazi za ujenzi wa taifa na za kiuchumi na katika mipango maalumu inayohitajia kufikiriwa kwa kina na michango ya watu mbalimbali kwenye jamii. Aidha huwa hakuna tofauti yoyote baina ya mwanamke na mwanamme katika masuala ya nchi na ya miji na ya vijiji na ya majimui ya watu na ya ndani ya familia na katika kupanga na kufikiria njia bora za kuyaendesha. Wote wana majukumu na kila mmoja anapaswa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Juu ya ukurasa

Misingi ya Harakati za Kijamii za Wanawake

Harakati yoyote ile ya kijamii, inaweza kuitwa ni harakati sahihi na inaweza kufikia kwenye malengo sahihi pale tu inapokuwa imefanywa kwa umakini mkubwa, mazingatio, kujua vyema maslahi na pale tu itakaposimama juu ya misingi sahihi na ya busara. Harakati yoyote yenye shabaha ya kufanikisha malengo ya kulinda haki za wanawake nayo, kama zinavyotakiwa kufanya harakati nyinginezo, inapaswa kuzingatia mambo hayo niliyotangulia kuyasema. Yaani inabidi isimame juu ya msingi wa busara na wa kuzingatia uhakika wa maumbile yaani kukitambua kitiba na hulka ya mwanamke, pamoja na dhati na silika ya mwanamme. Vile vile kutambua vyema majukumu na kazi zinazomuhusu mwanamke pamoja na majukumu na wajibu ambao ni maalumu kwa mwanamme. Vile vile kuelewa mambo ambayo jinsia hizo mbili yaani mwanamme na mwanamke wanaweza kuzifanya kwa pamoja. Hayo yote yanapaswa kufanywa kwa busara na kwa kutumia akili na sio kutumia hamasa tu. Kama harakati itafanywa kwa hamasa na kufuata mkumbo tu na kama harakati hiyo itachukuliwa maamuzi yasiyo ya busara, basi bila ya shaka yoyote itakuwa na madhara kwa wanaadamu wa jinsi zote mbili za mwanamme na mwanamke mwenyewe.

Juu ya ukurasa

Nafasi ya Mwanamke katika Ustawi wa Taifa

Kama nchi inataka kujijenga kwa maana halisi ya kujijenga, basi inapaswa macho yake yote yalenge kwenye wanaadamu na nguvukazi yake. Wakati tunapozungumzia nguvukazi, tunapaswa kuzingatia pia kwamba nusu ya nguvukazi ya nchi na ya taifa ni akina mama. Sasa kama kutakuwa na mtazamo ghalati kuhusiana na mwanamke, ni wazi kwamba haitayumkinika kuijenga inavyopaswa nchi. Wanawake wenyewe wanapaswa kujua vyema nafasi yao na jinsi dini tukufu ya Kiislamu inavyowaangalia kwa utukufu ili kwa njia hiyo waweze kutumia vizuri heshima wanayopatiwa na Uislamu kwa ajili ya kulinda kikamilifu haki zao. Vile vile watu wote katika jamii wake kwa waume lazima watambue mtazamo wa Uislamu kuhusu mwanamke, uwepo wa mwanamke katika medani za maisha, kazi za wanawake, kuelimishwa wanawake, kazi na shughuli za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kielimu za mwanamke pamoja na nafasi ya mwanamke katika familia na nafasi yao nje ya familia.

Juu ya ukurasa

Wajibu wa Kutafuta Elimu

Wanawake wanaweza kutafuta elimu kwa kiwango wanachotaka. Kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba watoto wa kike hawapaswi kuelimishwa wala kupewa nafasi ya kutafuta elimu. Ni walakini na ni makosa kufikiria hivyo. Watoto wa kike wanapaswa kutafuta elimu katika yale mambo yenye faida kwao na katika zile elimu wanazozipenda. Jamii nayo inahitajia kuwa na watoto wa kike walioelimika kama ambavyo inawahitajia watoto wa kiume walioelimika. Tab’an inabidi mazingira ya kutafuta elimu yawe salama. Ni jambo lililo wazi kwamba miongoni mwa mambo ya lazima ya kutafuta elimu ni kuchunga na kuheshimu misingi ya kimaadili katika suala zima la maingiliano baina ya wanaume na wanawake. Inawezekana kutafuta elimu na kufikia daraja za juu za kielimu kwa kuchunga kikamilifu misingi ya kimaadili. Miongoni mwa kazi muhimu na za kimsingi kabisa kwa akina mama ni usomaji wa vitabu. Inabidi ipatikane njia bora ya kuhakikisha kuwa akina mama wanajizoesha na kujibidiisha kusoma vitabu wanapokuwa majumbani. Ni vitabu vya maarifa ya kibinaadamu vinavyoweza kuwa rahisi kwa akili kuvisoma na kuvielewa na humjenga kimaarifa na kiakili anayevisoma na kumuweka kwenye mazingira mazuri na sahihi.

Elimu ni kitu azizi sana na mimi ninapenda sana kuona wanawake katika jamii ya Kiislamu wanaelimika na wanatafuta elimu katika masomo yote. Kuna baadhi ya akina mama walikuwa wanadhani kwamba kama mwanamke atatafuta elimu, basi anapaswa kutafuta elimu katika yale mambo pekee yanayohusiana na elimu za wanawake. Walikuwa wanadhani kuwa, inabidi wanawake wasomee tu mambo yanayohusiana na magonjwa maalumu ya wanawake na masuala kama ya ukunga wakati ambapo ukweli wa mambo hauko hivyo kwani wanawake wana jukumu la kutafuta elimu katika fani na masomo mengine mengi tu ya tiba kama vile utibabu wa moyo, mishipa na mengineyo mengi. Jambo hilo ni wajibu wa kisheria na kijamii kwa mwanamke.

Juu ya ukurasa

Mwanamke Kazini

Uislamu unakubaliana na suala zima la mwanamke kufanya kazi. Si tu unakubali, lakini pengine hata inaweza kuwa ni wajibu kwake kufanya kazi kila pale ambapo kazi itakuwa haivurugi shughuli za kimsingi na muhimu zaidi za mwanamke yaani kulea watoto na kuchunga familia. Kuna baadhi ya watu huchupa mipaka katika misimamo yao. Wako akina mama wanaosema kuwa, kwa vile kujishughulisha na kazi za kijamii kunatuzuia kushughulikia nyumba zetu, basi na sisi hatupaswi kufanyi kazi za kijamii. Baadhi ya wengine wanasema kinyume cha hayo, wanasema, madhali nyumba, mume na watoto hawawaruhusu kufanya shughuli za kijamii, basi inabidi waache kuwashughulikia waume na watoto wao na wajishughulishe tu na masuala ya kijamii. Kwa kweli mitazamo yote hiyo miwili ni ghalati. Si sahihi kupoteza hili kwa ajili ya lile wala kupoteza lile kwa ajili ya hili.

Tab’an suala la kufanya kazi kwa akina mama si suala la daraja la kwanza. Ijapokuwa Uislamu haumzuii mwanamke kufanya kazi na kubeba majukumu nje ya familia – isipokuwa katika masuala na kesi maalumu ambapo baadhi yake wanavyuoni wameafikiana juu yake na baadhi yake kuna tofauti kati ya wanachuoni – lakini lililo muhimu ni kujua tu kazi nje ya familia si kitu cha daraja la kwanza tab’an na suala muhimu hapa ni kwamba je, mwanamke ana kazi au hana. Naam, suala kuu ni lile suala la kimsingi ambalo leo hii inasikitisha kuona kuwa limetoweka kabisa katika nchi za Magharibi. Jambo hilo ni kwa mwanamke kupata utulivu anaotaka, kuhisi kuwa na usalama unaotakiwa na kuona anapata nafasi ya kuonyesha kipaji chake bila ya kukandamizwa katika jamii na katika familia ya nyumbani kwao na wakati anapoolewa na kwenda nyumbani kwa mumewe. Watu wanaofanya kazi katika uwanja wa masuala ya wanawake, wanapaswa kufanya shughuli zao katika misingi kama hiyo.

Juu ya ukurasa

Faslu Ya Pili Nafasi Ya Mwanamke Katika Familia

Malezi ya Kiislamu ya Mwanamke

Kama jamii ya Kiislamu itafanikiwa kumlea mwanamke kwa malezi ya Kiislamu, bila ya shaka yoyote mwanamke ataweza kupata hadhi na utukufu wake wa kweli. Kama mwanamke katika jamii ataweza kupata elimu na maarifa na ukamilifu wa kimaanawi na kimaadili ambao ameekewa na Mwenyezi Mungu na dini tukufu ya Kiislamu basi malezi ya watoto katika jamii yataweza kufanyika kwa njia iliyo bora na kwa unyoofu wa hali ya juu. Malezi hayo yataweza kuifanya jamii ipate maendeleo na kufanikiwa kukabiliana kirahisi na matatizo ya kimaisha kwa maana ya kwamba mwanamke na mwanamme wote watafanikiwa na kustarehe katika maisha yao kama hilo litatendeka. Suala hapa si kumuweka mwanamke katika vita dhidi ya mwanamme. Lengo ni kuwafanya wanawake na wasichana waingie katika mkondo na kwenye harakati ambayo wakati mwanamme naye anapoingia kwenye mkondo na harakati hiyo anatokezea kuwa mtu mkubwa na mwenye hadhi katika jamii. Hilo linawezekana pia kwa mwanamke, na dini tukufu ya Kiislamu imelithibitisha hilo kivitendo.

Miongozi mwa kazi muhimu zinazopasa kutendwa ni kuwafunza wanawake mambo mazuri ya kufanya wanapokuwa ndani ya nyumba zao, yaani jinsi ya kuamiliana na waume na watoto wao. Kuna wanawake ambao ni watu wazuri wapole, wenye subira, wastahamilivu na wenye tabia nzuri, lakini hawajafunzwa njia nzuri za kuamiliana na waume na watoto wao ndani ya nyumba zao. Mbinu hizo za kitaalamu ambazo inabidi wanawake wafunzwe ni mbinu ambazo zimepatikana kwa uzoefu wa muda mrefu wa binaadamu na hivi sasa zimefikia kwenye hatua nzuri. Kuna na baadhi ya watu wana uzoefu mzuri katika suala hilo. Watu hao wanapaswa kuchunguza na kutalii njia za kuweza watu wengine kuzitumia kuwaongoza wanawake katika kutekeleza inavyopasa majukumu yao ndani ya familia.

Juu ya ukurasa

Haki ya Kujichagulia Mume

Uislamu unamzingatia na kumwangalia kwa jicho maalumu mwanamke kama mwenza na sehemu muhimu katika familia. Kabla ya yote Uislamu unalizingatia suala la kuchagua mume. Kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya Kiislamu, mwanamke yuko huru kuchagua mume wa kumuoa na mtu yoyote hawezi kumtwisha mwanamke jambo lolote katika suala zima la kujichagulia mume wa kumuoa. Yaani hata makaka wa mwanamke na baba yake wanapotaka kumtwisha na kumlazimisha aolewe na mtu wanayempenda wao hawawezi kuanya hivyo, yaani hawana haki ya kufanya hivyo.

Tab’an katika jamii ya Kiislamu na katika kipindi chote cha historia kumekuwa kukishuhudiwa ada na desturi zisizo sahihi na kwamba kitu kinachofanywa na watu wasiojua kitu katika jamii za Waislamu, hakipaswi kuhesabiwa kuwa ni katika mafundisho ya Uislamu. Hizo ni ada na desturi za kijahilia. Waislamu wasiojua kitu hufuata mila na desturi za kijahilia na kufanya mambo ambayo hayana uhusiano wowote na Uislamu na mafundisho yaliyojaa nuru ya dini hiyo tukufu ya Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Mifano Miwili ya Ujahilia katika Ndoa

Ni makosa kwa mtu kumlazimisha mtoto wa kike aolewe na binamu yake kwa mfano bila ya ridhaa ya mtoto mwenyewe wa kike. Kama ambavyo ni makosa pia kwa mtu kumkatalia mtoto wa kike kuolewa na binamu yake kwa mfano kwa sababu tu huyo ni mtoto wa ami yake. Vile vile ni makosa kumzuia mtoto wa kike kuolewa na mtu mwingine kwa sababu tu amekataa kuolewa na binamu yake kwa mfano. Mtu yeyote anayefanya hivyo na anayesaidia katika jambo hilo huwa amefanya jambo la haramu lililo kinyume cha sheria. Kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na kwamba vitabu vya fiqhi katika Uislamu vina kauli moja katika suala hilo.

Kama mtu kutoka kabila moja akawa anataka kuondoa hitilafu zilizozuka katika kabila lake na kabila jengine – tujaalie kuwe kumezuka hitilafu, ugomvi na umwagaji wa damu kati ya makabila hayo mawili – na mtu akataka kuondoa hitilafu na chuki baina ya makabila hayo kwa kumlazimisha binti wa kabila hili aolewe na mvulana wa kabila la pili bila ya kuomba ruhusa kutoka kwa binti mwenyewe, kufanya hivyo ni kinyume cha sheria. Kama binti mwenyewe atakubali hapo hapana matatizo, (lakini kama itakuwa ni kulazimishwa, basi Uislamu hauruhusu jambo hilo). Kama binti mwenyewe atakubali kuolewa na mvulana wa kabila la pili ili kupitia ndoa hiyo, hitilavu na ugomvi uweze kuondoka katika makabila hayo mawili, hilo halina mushkeli wowote. Lakini kama watamlazimisha binti kufanya hivyo huku mwenyewe hataki na hajaridhia, kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Nafasi ya Kupata Utulivu

Kitu muhimu zaidi ambacho mwanaadamu anakihitajia ni utulivu. Saada na ufanisi wa mwanaadamu unapatikana pale mtu huyo anapokuwa mbali na mahangaiko na wasiwasi wa moyoni na wakati kiumbe huyo anapokuwa na tuo mtimani mwake. Hilo anaweza kulipata mwanamme na mwanamke kupitia familia.

Katika sura ya 30 ar Rum aya ya 21, Qur’ani tukufu inasema:

“Na katika ishara Zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanaofikiri.”

Yaani miongoni mwa ishara na dalili za kuwepo Mwenyezi Mungu na kuwepo uwezo Wake mkubwa ni kukuumbieni nyinyi wanaadamu wake na waume zenu <ازواجا> kutoka katika jinsi yenu wenyewe kwa ajili yenu wanaume na wanawake. Ni kutokana na nyinyi wenyewe «من انفسكم» si kutoka jinsi nyingine na viumbe wengine wowote bali ni kutoka katika uhakika mmoja, kutoka katika asili moja na kutoka katika dhati moja. Tab’an katika baadhi ya sifa kuna tofauti baina ya mwanamme na mwanamke. Baada ya hapo Mwenyezi Mungu anasema, «لتسكنوا اليها» ili mpate utulivu kwao. Yaani pea mbili na jinsi mbili za maumbile ya mwanaadamu zimeumbwa kwa lengo maalumu na kubwa. Lengo hilo ni kupatikana utulivu na utuvu ili mwanamke aweze kuishi pamoja na jinsi nyingine ya kiume ndani ya familia na mwanamme kadhalika; ili kwa kufanya hivyo waweze watu wa jinsi hizo mbili kupata utulivu unaotakiwa. Mwanamme naye wakati anaporejea nyumbani na kupata mazingira ya utulivu ndani ya familia, akaona hali ya amani imetawala katika familia yake, akiona mke mpole, mwenye huruma na mapenzi na mwaminifu yuko pembeni yake, mume huhisi kuwa na utulivu. Hali ni hiyo hiyo kwa upande wa mwanamke. Mwanamke naye anapopata mume anayependana, anayemwamini na kuhisi kuwa na utulivu na amani anapokuwa pamoja naye hujihisi kupata mafanikio makubwa na jambo hilo humletea ushuwari katika fuadi, na uhenezi moyoni mwake. Kuwa na aila na familia kunawadhaminia wote wawili mambo hayo. Mwanamme anamuhitajia mwanammke kuweza kupata utulivu na mwanamke naye anamuhitajia mwanamme katika kupata ushuwari kupitia kufunga ndoa na kujenga familia. «لتسكنوا اليها» Wote wawili wanahitajiana kwa ajili ya kupata utulivu na kutabaradi.

Juu ya ukurasa

Umuhimu wa Mwanamke katika Familia

Kwa hakika, mwanamke ndiye anayelea familia na kuiongoza. Msingi mkuu unaounda familia ni mwanamke na si mwanamme. Inawezekana kuweko familia bila ya mwanamme. Yaani wakati mwanamme anapokosekana katika familia au anapokuwa amefariki dunia, kama mwanamke atakuwa na akili na umakini, anaweza kuilinda na kuiendeleza vyema familia. Lakini wakati mwanamke anapokosekana katika familia, mwanamme hawezi kuilinda na kuiendesha familia hiyo. Hivyo mwanamke ndiye anayeilinda familia.

Sababu inayoifanya dini tukufu ya Kiislamu kulipa kipaumbele kikubwa suala la umuhimu wa mwanamke katika familia ni hiyo kwamba kama mwanamke atashikamana na familia yake, akawa anaipenda na kulipa umuhimu suala la malezi ya watoto, kushughulikia watoto wake, kuwanyonyesha, kuwalea mwenyewe kwa mapenzi ya mama hadi wanapokuwa wakubwa, kuwanywesha mambo ya kiutamaduni kama vile hadithi, simulizi, visa vya Qur’ani, hekaya zenye mafunzo ndani yake na ikawa ni kuwalisha mambo hayo watoto wake kila inapopatikana nafasi kama anavyotilia umuhimu wa kuwatayarishia chakula kizuri cha kujenga mwili, basi bila ya shaka yoyote ataweza kujenga familia na kulea kizazi bora na chenye watu madhubuti katika jamii. Hicho ndicho kipaji alichojaaliwa kuwa nacho mwanamke na suala hilo halikinzani hata kidogo na suala la kutafuta elimu na kufundisha pamoja na kufanya kazi na kuingia katika siasa na mambo kama hayo. Inabidi katika mipango na ratiba zote za kijamii, suala la familia liwe ndio msingi. Naam, suala la kuwa mama, suala la kuwa mke, suala la kuongoza na kusimamia familia ni mambo muhimu, ya kimsingi na ya kupewa kipaumbele cha kwanza kabisa. Yaani hata kama mwanamke atakuwa mtaalamu na daktari bora kabisa au akawa na umahiri na utaalamu wa hali ya juu kabisa katika elimu nyinginezo lakini akawa hajihusishi na masuala ya nyumbani, jambo hilo huwa ni nuksani kubwa kwake. Mhimili na asili ya mambo yote kwa mwanamke ni kuwa msimamizi wa nyumba na familia. Kama itabidi tutoe mfano japo usiofanana kikamilifu, tunaweza kusema kwamba mwanamke ni kama malkia katika sega na mzinga wa nyuki.

Juu ya ukurasa

Ushawishi wa Nguvu za Kimaumbile za Mwanamke

Wana wanawake ushawishi na mvuto maalumu na usioweza kuelezeka kwa waume wao, isipokuwa labda katika baadhi ya kesi tu zisizo za kawaida. Tab’an hii haina maana kwamba kama mwanamke anamdhibiti mumewe ndio isemwe mwanamke ana ushawishi na mvuto maalumu. Ushawishi na mvuto tunaouzungumzia hapa ni kile kipaji na sifa maalumu aliyoumbwa nayo mwanamke na Mola wake. Mimi baada ya kuchunguza sana nimeamini kuwa mwanamke ana nguvu zaidi kuliko mwanamme.

Hivyo ndivyo ninavyoamini mimi. Mtu ambaye mwishowe huwa mshindi wakati yanapotokezea makabiliano – na kama makabiliano hayo nayo yatachukua muda mrefu – basi ni mwanamke. Yaani hatima ya yote, mwanamke atatumia mbinu, hila na kile kipaji maalumu alichozawadiwa na Mwenyezi Mungu kumshinda mwanamme. Hilo ni moja ya mambo yanayoyafanya maumbile kuwa na mvuto wa kipekee na ni miongoni mwa siri za huluka na maumbile. Mbali na uwezo wao wa kuiingiza katika medani idadi yao, yaani ile asilimia yao 50, wanawake wana nguvu pia za kuingiza uwanjani asilimia nyingine 50 ya watu, nao ni wanaume.

Hii ni kusema kuwa mwanamme yuko tayari mkewe na mwanawe wabakie nyumbani lakini yenye aende katika medani. Kwa mfano wakati huo sisi tulipokuwa uwanjani tukiendesha mapambano, tulikuwa hatuko tayari kuwachukua wake zetu katika medani. Tulikuwa tukisema: “Nyinyi bakieni nyumbani, sisi wenyewe tutakwenda kufanya kazi hii.” Lakini wakati mwanamke anapokwenda katika medani, huenda huko yeye akiwa amemtanguliza mbele mumewe. Mwanamke ana kipaji hicho. Sifa na shakhsia hiyo maalumu, athari hizo za kimaumbile, kung’ara huko katika medani ya mapambano ni sifa maalumu ambazo inabidi zilindwe na kuhifadhiwa hasa kwa vile mapambano yalikuwepo na yataendelea kuwepo.

Juu ya ukurasa

Kitovu cha Mapenzi

Silika waliyoumbwa nao mwanamke na mwanamme katika mazingira ya familia, ni hulka ambayo huleta utengamano baina ya mwanamke na mwanamme na utengamano huo ni mfungamano wa kimapenzi na kuhurumiana kama inavyosema Qur’ani Tukufu: «مودّة و رحمة» mapenzi na kuhurumiana.

Mahusiano sahihi ya mwanamme na mwanamke ni hayo ya mapenzi na kuhurumiana, ni uhusiano wa kirafiki, ni uhusiano wa shufaka na huruma. Yaani waingize urafiki baina yao, wapendane na wahurumiane.

Familia ndiyo sehemu ambayo inabidi hisia za upole na shufaka zinapaswa kulelewa na kunawirishwa, watoto nao wapate mapenzi na mahaba ndani yake. Mume naye ni mwanamme, na tabia na maumbile ya mwanamme nayo ni ghafi zaidi ikilinganishwa na ya mwanamke na katika baadhi ya sehemu yanakuwa dhaifu zaidi ikilinganishwa na ya mwanamme (hususan linapofika suala la uvumilivu). Marhamu pekee yanayoweza kulainisha ughafi wa maumbile hayo ya mwanamme ni nyonda na mahaba ya mwanamke. Tena basi hata sio mapenzi ya mama, bali ni mapenzi ya mke ndiyo yanayoweza kumnyoosha mwanamme vile inavyotakiwa. Hii ni kwa sababu mke humfanyia mumewe yaani mwanamme mtu mzima, yale yanayofanywa na mama lakini wakati mtu mzima huyo anapokuwa mtoto mdogo - (Mama hawezi kumfanyia mwanawe wa kiume mambo ambayo alikuwa akimfanyia wakati alipokuwa mtoto mdogo, lakini mke anafanya) - na kwa kweli wanawake wanaujua vyema udhaifu wa wanaume. Sasa kama katika familia atakosekana mtu kama huyo yaani mama wa familia, mke wa familia, basi familia hiyo lazima itapoteza sifa za kuitwa familia.

Juu ya ukurasa

Kugawana Majukumu

Maumbile ya mwanamke na mwanamme, kila moja ya maumbile hayo lina sifa zake maalumu. Mtu asitegemee kumuona mwanamme anafanya kazi za mwanamke na anakuwa na moyo wa mwanamke katika familia na wala isitarajiwe kwa mwanamke kufanya kazi za mwanamme na kuwa na moyo wa mwanamme ndani ya familia. Kila mmoja kati ya wawili hao ana sifa zake maalumu za kimaumbile na kiroho, ambapo maslahi ya mwanadamu, maslahi ya jamii, maslahi ya mfumo wa kijamii wa mwanamke na mwanamme yanataka sifa maalumu za mwanamme na mwanamke zichungwe vizuri ndani ya familia na kama zitachunga, wote wawili watafanikiwa yaani mwanamme na mwanamke. Lakini mtu yeyote hana haki ya kumdhulumu mwenzake wala kumkandamiza na wala kumtwisha matakwa yake. Baadhi ya wanaume wanadhani kwamba, mwamke ana wajibu wa kufanya kazi zote zinazowahusu wanaume. Tab’an ndani ya familia, mwanamke na mwanamme wanaopendana, huwa wanafanyiana kazi zao kwa mapenzi na shauku kubwa lakini kufanya kazi kwa mapenzi ni tofauti na mtu kudhania kuwa kufanya hivyo ni katika wajibu wa mwanamke au mtu kufikiri kuwa mwanamke ni kama boi na mtumishi wa ndani ya nyumba wa kumuhudumia mwanamme. Hakuna kitu kama hicho katika dini tukufu ya Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Umuhimu wa Kwanza ni wa Kazi za Nyumbani

Baadhi ya wanawake ni wafanyakazi, wanafanya kazi nje ya nyumba zao, wanafanya operesheni hospitalini, wanawahudumia wagonjwa wao, mwengine anafanya kazi za kitaalamu na kielimu, wengine wanafanya kazi za kuchora ramani na kuandaa mpango na miradi maalumu ya maendeleo, wengine wanafundisha vyuoni na mashuleni – yote hayo yana mahala pake – lakini pamoja na kuweko kazi zote hizo, inabidi masuala ya nyumbani nayo yazingatiwe. Tab’an kama vilivyo vitu vingine vyote, kazi za nyumbani nazo zinaweza kupunguzwa. Uwepo wa mwanamke nyumbani kwa masaa 24 una maana yake, lakini kama masaa hayo yatapunguzwa na kazi ya mwanamke ndani ya nyumba ikafanywa kwa ubora zaidi, hapo maana ya masaa hayo huwa nyingine. Kama mtaona kazi yenu fulani inaharibu kazi yenu nyingine, inabidi mkae na kufikiria njia ya kufanya. Hili nalo ni jambo la msingi isipokuwa katika baadhi ya kesi maalumu za dharura. Dharura zinapatikana katika mambo yote na masuala hayo huyatoa mambo katika mkondo wake wa kawaida. Lakini kati ya kazi zote zinazomuhusu mwanamke, suala la malezi ya watoto na kukuza moyo wa waume zao na kuwafanya waingie kwenye medani kubwa kubwa, ni muhimu zaidi kuliko kitu kingine chochote.

Juu ya ukurasa

Jukumu la Kulea Watoto

Miongoni mwa majukumu aliyo nayo mwanamke ndani ya familia na ndani ya nyumba yake ni suala la malezi ya watoto. Wanawake ambao hawataki kuzaa wala kulea watoto wao kutokana na kazi zao za nje ya nyumba, wanakwenda kinyume na maumbile ya mwanaadamu na kuwa kwao wanawake. Jambo hilo halimridhishi hata kidogo Mwenyezi Mungu. Wanafanya makosa makubwa wale watu ambao wanakwepa kuzaa na kulea na kunyonyesha na kuwapa mapenzi ya mama watoto wao kutokana tu na kujali zaidi kazi nyingine ambazo baadhi yake hata haziwakwamishi kufanya hivyo. Malezi ya huruma na mapenzi ya mama ndiyo njia bora kabisa ya kulea watoto. Wanawake ambao wanawanyima watoto wao neema hiyo ya Mwenyezi Mungu wajue wanafanya makosa kwani jambo hilo lina madhara kwa watoto wao, linawadhuru wanawake wenyewe na linailetea madhara pia jamii nzima. Ndio maana Uislamu haujuzishi jambo hilo. Moja ya majukumu makuu ya mwanamke ni kumpa mtoto malezi sahihi yaliyojaa mapenzi na huruma. Mwanamke anapaswa kubeba tumboni mwake kiumbe – kiwe cha kiume au cha kike – kwa namna ambayo baada ya kumzaa na kumlea hadi kuwa mkubwa, kiumbe huyo awe mwanaadamu bora kiroho, asiwe na matatizo yoyote na asihisi kuwa dhalili wala kukumbwa na mambo ya kumwangamiza kama tunavyoshuhudia leo hii kati ya vijana wa nchi za Magharibi za Ulaya na Marekani ambao wamekumbwa na mambo ya kuwaangamiza na wamezongwa na mabalaa ya kimaadili n.k, kiasi kwamba wanajikuta wametingwa vibaya na wanakosa njia za kujipapatua.

Wanawake wa nchi za Magharibi kutokana na kuwa hawalipi umuhimu suala la kujenga familia na kulea watoto, leo wamepelekea jamii za Magharibi kufika katika kiwango ambacho mamilioni ya vijana ni wahalifu, mafisadi na waovu kama inavyoshuhudiwa katika nchi za Ulaya na Marekani. Licha ya nchi hizo kuonekana kijuu juu kuwa zimestawi kimaendeleo na kuwa na majengo makubwa makubwa, viwanda vikubwa vikubwa vya atomiki, majumba marefu marefu ya mamia ya ghorofa, maendeleo makubwa ya kisayansi na kiteknolojia, lakini utawaona watoto wa nchi hizo wanatumbukia katika uhalifu, wizi, mauaji, magendo, kunajisi, na kuvuta sigara, bangi na mihadarati! Majakamoyo yote hayo ambayo yamezikumba nchi za Ulaya na Marekani yanatokana na nini? Yanatokana na kuwa mwanamke katika nchi za Magharibi, ameshindwa kujua thamani ya aila na familia.

Juu ya ukurasa

Simulizi ya Ua na Bustani

Kwa mujibu wa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu, (na kama ilivyonukuliwa kutoka kwa viongozi wa Kiislamu) mwanamme ana jukumu la kuamiliana na mwanamke kama ua. Uislamu unasema: «المرأة ريحانة» mwanamke ni ua. Suala hilo lakini halihusiani na medani za kisiasa, kijamii, kutafuta elimu na mashindano mengine mbalimbali ya kijamii na kisiasa, hapana, bali hilo linahusiana na maisha ya ndani ya familia na ndani ya ndoa. «المرأة ريحانة و ليست بقهرمانة» Maneno hayo yaliyopokewa na kuhadithiwa kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW yanavunja ule mtazamo wa makosa wa watu ambao walikuwa wanadhani kwamba ni wajibu na ni jukumu la mwanamke kufanya kazi zote za nyumba. Mwanamke ni mithili ya ua inabidi litunzwe vizuri. Iwapo mtu atataka kupigana vita na ua, ni wazi kuwa atalinyambua nyambua. Kama mtu atakuwa anajua maana ya ua ni nini na akalitunza na kuamiliana nalo vile inavyotakiwa, basi ua hilo huleta ulimbwende na umaridadi na hujipambanua kifakhari mbele ya vitu vingine. Hivyo inabidi kumwangalia mwanamke kwa jicho hilo katika ndoa na kwenye familia. Inabidi sifa maalumu za mwanamke na hisia zake na mahitaji yake yazingatiwe na asibebeshwe mambo ambayo hayaendani na maumbile yake. Mweanamke asilazimishwe kufikiri kama mwanamme, kufanya kazi kama mwanamme au kuwa na mahitaji kama ya mwanamme. Yaani Uislamu umezingatia sifa na hisia zote za wanawake kulingana na maumbile yao ya kike na wakati huo huo kumfungulia njia kiumbe huyo katika medani za elimu, medani za umaanawi, medani za taqwa, medani za kisiasa na nyinginezo. Vile vile Uislamu unamuhamasisha mwanamke kutafuta elimu, kama ambavyo unamshajiishi kuingia katika medani mbalimbali za kijamii na kisiasa. Vile vile Uislamu umemwambia mwanamme hana haki ya kumtwisha mwanamke kazi zisizo zake, kuchupa mipaka na wala kutumia mabavu ya kijahilia na yaliyo kinyume na sheria na vitu kama hivi. Huo ndio mtazamo wa Uislamu kuhusiana na mwanamke.

«المرأة ريحانة و ليست بقهرمانة» Mwanamke ni ua si “قهرمانة” na maana ya neno “قهرمانة “ hapa si ile maana tunayoijua sisi ya Kifarsi. Neno “قهرمانة“ hapa linatumika kwa maana ya Kiarabu ya mtendaji na mtekelezaji mkuu wa mambo. Yaani mwanamme katika familia asimuone mwanamke ndiye mwenye wajibu wa kutekeleza masuala yote ya ndani ya nyumba. Isidhaniwe kuwa mwanamme ni bosi ndani ya familia na hivyo kazi zote za ndani ya nyumba, kushughulikia watoto na mfano wa hayo ni wajibu wa mwanamke kuzifanya au kudhaniwa kuwa mwanamke ni kama kijakazi na boi ndani ya nyumba hivyo inabidi aamrishwe kama kijakazi. Mtazamo huo si sahihi hata kidogo.

Juu ya ukurasa

Kudhulumiwa Mwanamke Ndani ya Familia

Leo mwanamke duniani anakabiliwa na matatizo yasiyoisha na yasiyoweza kutatuka. Jamii ya mwanamke na hususan mwanamke wa leo duniani wanakabiliwa na mashaka na matatizo katika nyanja mbili. Uwanja wa kwanza ni uwanja wa familia na uwanja wa pili ni uwanja wa jamii. Hayo yanashuhudiwa katika nchi za Ulaya na Marekani na kwenye zile nchi ambazo zimefuata mkumbo na kuzifanya nchi hizo za Magharibi kuwa kigezo kwao. Katika baadhi ya maeneo hali hiyo inaonekana kwa uwazi sana na kuna sehemu nyingine hainaonekana kwa uwazi sana. Mwanamke anadhulumiwa ndani ya familia. Yaani wanaume kwa hakika wanawadhulumu wanawake katika familia. Dhulma kubwa wanayofanyiwa wanawake na waume zao katika familia ni kwamba mwanamme hamuhesabu mwanamke kuwa ni mwenza katika maisha yake. Hazifanyi hisia zake zimfikirie mkewe. Waume katika familia hizo wanajishughulisha tu na mambo yao yasiyo sahihi na hawaa na matamanio yao ya kinafsi na nguvu zao zote huzielekeza kwa wanawake wa nje ya ndoa zao. Wanapokuwepo nyumbani, maisha yanakuwa ya baridi yasiyo na mapenzi wala mvuto wowote na baadhi ya wakati huambatana na tabia mbaya na mashinikizo makubwa dhidi ya mwanamke. Wanajifanya kusahau kuwa nukta muhimu ni nukta ya muamala wa mke na mume. Utaona mtu anamlea mtoto wa kike kwa tabu na mapenzi makubwa ya baba na mama na wakati anapokuwa kijana, akiwa bado nyumbani kwa wazee wake, akiendelea kuhesabiwa kama mtoto katika familia mara anaolewa na kwenda kuishi kwa mumewe na kuanza maisha mapya kabisa. Wakati huo utaona baadhi ya wanaume wanatarajia wake zao wawe wanajua kila kitu, wanawabebesha mambo yote na wanawatarajia wajue kila kitu! Si sahihi hata kidogo kufanya kitu kama hicho.

Kama mwanamme katika familia atajiona mfalme na kama ataamua kumtumikisha mkewe kama boi, kijakazi na mtumishi wa ndani, ajue kuwa anafanya dhulma na inasikitisha kuona kuwa wanaume wengi wanafanya dhulma hiyo. Mwanamke anakabiliwa na dhulma kama hiyo pia anapokuwa nje ya familia. Kama mwanamke atakosa kuwa na mazingira mazuri ya amani na salama kwa ajili ya kutafuta elimu, kwa ajili ya kufanya kazi, baadhi ya wakati kwa ajili ya kutafuta riziki na kupumzika, kama atakoseshwa mazingira hayo, basi bila ya shaka yoyote atakuwa anadhulumiwa. Kama mwanamke hataandaliwa mazingira ya kutafuta elimu sahihi, kujielimisha na kupata maarifa, basi atakuwa anadhulumiwa. Kama hali itakuwa kwa namna ambayo mwanamke atashindwa kutekeleza mafundisho ya dini yake, kujielimisha, kuchunga maadili mema, kujistahi n.k, kutokana na mashikizo mbalimbali, huko nako kutakuwa ni kumdhulumu mwanamke. Kama mwanamke hatapewa uhuru na hataruhusiwa kutumia anavyopenda vitu anavyomiliki, hiyo nayo itakuwa ni dhulma dhidi yake. Kama mwanamke atalazimishwa kuolewa na mume asiyemtaka, yaani kama hataombwa idhini na hatashirikishwa katika kuchagua mtu wa kumuoa, huko nako kutakuwa ni kumdhulumu mwanamke. Kama mwanamke atanyimwa haki ya kuonyesha mapenzi yake kwa mwanawe na kupata mapenzi ya mwanawe itakuwa ni kumdhulumu ni sawa tu mwanamke huyo awe kwa mumewe au awe ameachika. Kama mwanamke atakuwa na kipawa na kipaji maalumu - kama vile cha kisayansi, kama cha uvumbuzi, kama cha ubunifu, kama cha kisiasa, kama cha kazi za kijamii – na akanyimwa fursa ya kutumia na kuonyesha kipaji chake hicho, huko nako ni kumdhulumu.

Juu ya ukurasa

 
< Nyuma   Mbele >

^