Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hijabu kwa Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu Chapa
16/02/2010

 Faslu Ya Kwanza: Hijabu Katika Utamaduni Wa Kiislamu

Mfumo wa Kimaumbile wa Mwanaadamu
Umuhimu wa Urembo katika Uislamu
Hijabu Kadhia yenye Thamani
Uhusiano baina ya Mwanamke na Mwanamme
Hairuhusiwi Kujishauwa
Hijabu na Maendeleo ya Kisiasa na Kijamii ya Mwanamke

Faslu Ya Pili: Hijabu Katika Utamaduni Wa Magharibi

Changamoto ya Hijabu katika Utamaduni wa Kiislamu na wa Magharibi
Kutothaminiwa Hijabu Barani Ulaya
Kutembea Uchi na Ulevi, Desturi ya Ulaya
Ukinzani katika Mambo Yanayoheshimiwa kwenye nchi za Magharibi
Kudhalilishwa Mwanamke katika Utamaduni wa Magharibi
Hijabu, Ufunguo wa Utamaduni wa Kiislamu
Kupigwa Marufuku Hijabu Barani Ulaya

Faslu Ya Tatu: Hijabu Katika Mfumo Wa Jamhuri Ya Kiislamu Ya Iran

Kupenya Utamaduni wa Hijabu
Kupandikizwa Utamaduni wa Magharibi
Kudhulumiwa Mwanamke wa Kiislamu
Hijabu na Maendeleo ya Kijamii ya Wanawake wa Kiirani
Ujumbe wa Wanawake Waislamu wa Iran

Hijabu kwa Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu

Faslu Ya Kwanza: Hijabu Katika Utamaduni Wa Kiislamu

Mfumo wa Kimaumbile wa Mwanaadamu

Hijabu ni kitu chenye thamani kinachokubaliana kikamilifu na maumbile ya mwanaadamu. Kutembea uchi na kujitumbukiza kwenye maingiliano yasiyo na mipaka kati ya jinsia mbili za mwanamme na mwanamke, na kuonyeshwa wazi wazi vitendo hivyo viovu mbele ya watu wengine, ni jambo lililo kinyume cha maumbile na si katika mambo ambayo dhati ya mwanaadamu inayataka.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaumba kwa maumbile maalumu mwanamme na mwanamke kwa kuzingatia maslahi na kuyafanya maisha ya mwanaadamu yawe mepesi na wote wawili waweze kuendesha maisha yao ulimwenguni kwa urahisi. Mwenyezi Mungu ameweka kazi maalumu kwa ajili ya wanaume na kazi maalumu kwa ajili ya wanawake (na baadhi ya kazi viumbe hao wawili wanashirikiana). Vile vile amemwekea mwanamme haki zake kama alivyomuwekea mwanamke. Kwa mfano vazi la Hijabu linaelekea zaidi kwa mwanamke kuliko mwanamme. Tab’an katika baadhi ya mambo mwanamme naye anatakiwa kuchunga Hijabu na afunike sehemu ya mwili wake, lakini suala la Hijabu linamhusu zaidi mwanamke. Kwa nini? Kwa sababu ya maumbile yake, sifa na hali maalumu ya mwanamke, uzuri na mvuto wake wa kimaumbile, na kama tunataka jamii isikumbwe na vurugu, isiharibike na kuchafuka, na iwapo tunataka tuwe na jamii ambayo haina ufuska na ufisadi, basi ni lazima tuhakikishe kwamba mwanamke anajisitiri vizuri. Kwa upande wa vazi hilo, mwanamme kiujumla hawi sawa na mwanamke, na hakuna masharti mengi katika mavazi yake. Hayo yote yanatokana na nafasi ya kimaumbile ya wawili hao na yanatokana na ile suna ya Mwenyezi Mungu aliyoiweka kwa ajili ya kuendesha vizuri maisha duniani.

Juu ya ukurasa

Umuhimu wa Urembo katika Uislamu

Uislamu umelipa umuhimu suala la urembo na mapambo. Kimsingi suala la kupenda vitu vizuri, vinavyovutia na vinavyopendeza ni suala la kimaumbile. Tab’an yumkini kukawa kuna tofauti kidogo kati ya maumbile hayo na vile suala la kupenda urembo na mapambo linavyoangaliwa leo hii. Leo suala hilo linaangaliwa kwa maana pana zaidi. Suala la kujipamba na kuvaa nguo za kupendeza ni jambo maalumu ambalo lina mvuto mahsusi kwa mwanaadamu na hasa vijana. Siku zote mwanaadamu anapenda vitu vizuri na mwenyewe siku zote anataka awe mzuri. Mara nyingi tumesikia maneno yasemayo:

«انّ اللَّه جميل و يحبّ الجمال»

“Mwenyezi Mungu ni jamali na anapenda ujamali.”

Zaidi hayo kuna riwaya nyingi tu katika vitabu vyetu vya hadithi zinazotilia mkazo suala la mapambo na watu kujiweka maridadi na watanashati. Katika mlango wa ndoa wa vitabu vya fikihi pia kunajadiliwa suala la mume na mke kujiweka wasafi na maridadi. Kuna baadhi ya watu wanadhani kuwa wanaume inabidi wakate nywele zao na wahakikishe kuwa siku zote lazima nywele zao ziwe fupi wakati si hivyo kwani kumepokewa hadithi inayosema kwamba:

«الشَعر الحسن من كرامة اللَّه فأكرموه»

“Nywele nzuri ni katika baraka za Mwenyezi Mungu basi zibarikini.”

Au kwa mfano imepokewa kwamba, wakati Bwana Mtume Muhammad SAW alipokuwa akitaka kwenda kuonana na marafiki zake, alikuwa kwanza akijiangalia kwenye chombo chenye maji na kuhakikisha amekaa vizuri ndipo halafu alikuwa akienda kuonana na marafiki zake. Wakati huo hakukuwa na vioo vingi kama ambavyo vipo kila mahala leo hii lakini pamoja na hayo alikuwa na njia ya kuhakikisha hatoki shaghalabaghala mbele ya marafiki zake. Jambo hilo linathibitisha kwamba umaridadi na utanashati, mavazi mazuri na mtu kupenda vitu vya kupendeza ni jambo linalohimizwa katika sheria ya dini tukufu ya Kiislamu. Lakini lililo baya na jambo lenye madhara katika suala hilo zima ni kwamba kujipamba huko na kujiweka wasafi kusiwe sababu ya kuzuka fitna, kuchupa mipaka, ufisadi na mambo ya kishetani.

Juu ya ukurasa

Hijabu Kadhia yenye Thamani

Suala la kulindwa mipaka ya kijinsia ni jambo lenye umuhimu mkubwa sana kwa Waislamu. Kwa hakika jambo hilo ni la kimsingi na muhimu sana. Hiyo ndiyo itikadi ya Waislamu kuhusu umuhimu wa kuweko mipaka kati ya mwanamme na mwanamke. Maingiliano yaliyo kinyume cha sheria ni haramu. Suala la kuweko mipaka ya kijinsia yaani baina ya mwanamme na mwanamke ni miongoni mwa mambo ya kimsingi ya dini. Tunachozungumzia sisi hapa hakiishii kwenye baibui na abaa tu, yaani tunachojadili hapa si kwamba mipaka hiyo iwe ya namna gani, (bali lililo muhimu ni kuchungwa mipaka, njia za kuchunga zinaweza kutofautiana). Kuna uwezekano jambo hilo likatofautiana kulingana na wakati na minasaba tofauti na kwenye maeneo mbalimbali kwa mujibu wa mila na desturi na miundo mbali mbali ya maisha. Nafasi ya mipaka hiyo ni miongoni mwa mambo ya kimsingi ya dini ya Kiislamu. Kadhia ya Hijabu nayo ni moja ya masuala yenye thamani kubwa. Suala la Hijabu ijapokuwa ni suala la utangulizi wa vitu vingine muhimu zaidi, lakini Hijabu yenyewe ni kitu chenye thamani kubwa. Sisi tunashikamana kiasi chote hiki na Hijabu kwa sababu wakati mwanamke anapochunga Hijabu, vazi hilo tukufu humsaidia kufikia kwenye daraja yake ya juu ya kimaanawi na humpa nguvu za kupambana na vishawishi na humsaidia asitumbukie katika mitego inayomwandama mara kwa mara.

Juu ya ukurasa

Uhusiano baina ya Mwanamke na Mwanamme

Uislamu umeweka Hijabu baina ya mwanamke na mwanamme. Hata kama wawili hao wanazungumza pamoja, wanafanya miamala mbali mbali, wanagombana, wanapendana, lakini kati yao kuna Hijabu na hifadhi maalumu. Hayo ndiyo mafundisho ya Uislamu na ni lazima yasingatiwe na yatekelezwe kivitendo. Kuvunja mipaka katika uhusiano wa mwanamke na mwanamme na kuvunjwa fingo la heshima ya kibinaadamu ya mwanamke na badala yake kiumbe huyo kugeuzwa kuwa ala na chombo cha kustareheshea matamanio ya kishetani ya wanaume na vile vile kugeuzwa chombo cha kuvutia wanaume kwa ajili ya kuuza bidhaa za mashirika mbali mbali ya wanaume, ni jambo lisilokubalika kabisa na limepigwa marufuku na dini ya Kiislamu.

Kwa hakika Uislamu unamtaka mwanamke achunge heshima na utukufu wake kiasi kwamba asiwe na haja kamwe ya kufikiria je wanaume wanamwangalia au hawamwangalii. Yaani mwanamke apande daraja na alinde hadhi yake kiasi kwamba suala la kuangaliwa au kutoangaliwa na wanaume lisiwe na maana yoyote kwake. Hivyo ndivyo unavyotaka Uislamu. Ukiangalia hata kijuu juu tu utaona kuna tofauti kubwa kati ya fikra hiyo ya Uislamu na suala zima linaloshuhudiwa leo ulimwenguni ambapo kuna watu maalumu wanakaa na kufikiria jinsi ya kuhakikisha nguo za mwanamke, urembo wake, mapambo yake, namna yake ya kuzungumza na jinsi anavyotembea yatawavutia vipi wanaume na kuwafanya wawaangalie wanawake hao. Oneni wenyewe jinsi ilivyo tofauti kubwa kati ya mambo hayo na fikra nzima ya Kiislamu ya kumpa heshima na utukufu wake mwanamke.

Juu ya ukurasa

Hairuhusiwi Kujishauwa

Uislamu unapiga marufuku suala zima la kudesa na kujishaua. Maana ya kujishaua hapa ni huko kujibodoa wanawake na kutia mikogo mbele ya wanaume kwa ajili ya kuwavutia, kuwashawishi kijinsia na kueneza fitna na ufuska. Kufanya hivyo ni miongoni mwa fitna yenye madhara makubwa. Madhara yake hayaishii kwa mtoto wa kike au mtoto wa kiume kutumbukia kwenye madhambi pekee, bali huo huwa mwanzo tu na hata tunaweza kusema hiyo ni hatua ya chini kabisa. Baada ya hapo madhara yake makubwa huzikumbwa aila na familia na kuzivuruga. Kimsinghi ni kuwa, mahusiano hayo yasiyo na mipaka wala yasiyo ya kisheria ni sumu angamizi kwa familia kwani aila inabakia kuwa hai pale tu yanapofunika mapenzi ndani ya familia hiyo. Aslan, familia hujengwa kwa mapenzi na mahaba. Kama mahaba hayo hayapo na iwapo yatatoka kwenye familia na kwenda kwa watu wengine, familia hupoteza nguzo yake kuu na kuifanya ikumbwe na zilzala kama zinavyoshuhudiwa familia za nchi ambazo haziweki hijabu na kizuizi kati ya wanawake na wanaume kama nchi za Magharibi hasa za nchi za Ulaya Kaskazini na Mrekani. Familia zinasambaratika na leo hii hilo limekuwa ni jakamoyo kubwa kwa nchi hizo. Jakamoyo hilo kwanza kabisa huwaathiri wanawake wenyewe. Tab’an wanaume nao hawasalimiki na wanakumbwa na matatizo mengi yatokana na jakamoyo hilo, lakini wanaodhurika zaidi na wanawake na baadaye hukikumba kizazi cha watoto wanaozaliwa. Wenyewe mnashuhudia jinsi kizazi cha vijana kilivyopotoka katika maeneo mbalimbali hususan nchini Marekani na Ulaya. Chanzo cha yote hayo ni suala hilo la kujishaua, kuzinza kichwa na kuweko mahusiano holela baina ya wanawake na wanaume.

Juu ya ukurasa

Hijabu na Maendeleo ya Kisiasa na Kijamii ya Mwanamke

Uislamu unamtaka mwanamke afikie daraja ya juu kabisa ya kifikra, kielimu, kijamii, kisiasa, na zaidi kuliko yote daraja ya juu ya heshima na umaanawi. Uislamu unataka uwepo wa mwanamke katika jamii na kwenye familia ya mwanaadamu uwe na faida ya juu na matunda ya maana kabisa. Mafundisho yote ya dini tukufu ya Kiislamu likiwemo suala la Hijabu yamesimama juu ya msingi huo. Vazi la staha la Hijabu halina maana ya kumtenga mwanamke. Kama kuna mtu ana mtazamo huo kuhusu Hijabu ajue kuwa mtazamo wake ni ghalati na ni kinyume kabisa na ukweli. Vazi la stara la Hijabu limeamrishwa na Uislamu ili kuepusha maingiliano na michanganyiko holela na isiyo sahihi kati ya mwanamke na mwanamme. Michanganyiko ya aina hiyo ina madhara kwa jamii, ina madhara kwa mwanamke na mwanamme, na madhara yake makubwa yanamwelekea mwanamke mwenyewe.

Juu ya ukurasa

Faslu Ya Pili: Hijabu Katika Utamaduni Wa Magharibi

Changamoto ya Hijabu katika Utamaduni wa Kiislamu na wa Magharibi

Nimekuwa nikisema mara kwa mara kwamba si sisi (Waislamu) ambao tunatakiwa kujitokeza na kutetea itikadi yetu bali ni utamaduni mbovu wa Magharibi ndio ulio na wajibu wa kujitokeza mbele na kutoa ushahidi wa madai yake. Kitu ambacho dini tukufu ya Kiislamu inampatia mwanamke ni kitu cha thamani ambacho mtu yeyote mwenye akili na msomi, mwenye insafu na uadilifu katika maamuzi yake, hawezi kukikana, bali lazima atakuwa anakiri kwamba ni kitu kizuri. Sisi Waislamu tunamtaka mwanamke awe na staha, awe na stara, ajifunike vizuri, asichanganyike ovyo na wanaume, wote wawili, mwanamme na mwanamke wachunge mipaka baina yao, walinde heshima ya mwanaadamu, mwanamke asijifanye bidhaa na kujiremba kwa ajili ya mwanamme baki, achunge hadhi na heshima yake na asiwe sababu ya kujiuza na kujitamanisha kwa wanaume kama bidhaa, hilo si kufu ya mwanaadamu aliyepewa heshima na Mwenyezi Mungu. Hivyo ndivyo sisi Waislamu tunavyotaka mwanamke awe. Lakini wao Wamagharibi wanamshawishi mwanamke ajishaue na ajikwatue na kujiremba kwa namna ambayo kila mwanamme akimuona avutiwe naye hasa wahuni wa mitaani. Jambo hilo kwa kweli ni baya sana. Linamvunjia heshima mwanamke. Hiyo si hadhi ya mwanamke wa Kiislamu, bali si hadhi ya mwanamke yeyote yule. Sasa wale watu ambao wanamshawishi mwanamke ajigeuze bidhaa ya kuvutia wanaume, wao ndio wanaopaswa kutoa dalili na ushahidi wa vitendo vyao hivyo vya kushajiisha zinaa na uasherati. Wamagharibi ndio wanaopaswa kuulizwa kwa nini mnamdhalilisha kiasi chote hiki mwanamke kiasi cha kumfanya awe chombo tu cha kuridhisha matamanio ya kijinsi ya wanaume! Wamagharibi na watu mfano wao wanapaswa kutoa hoja na ushahidi wa kuthibitisha vitendo vyao hivyo. Utamaduni wetu sisi Waislamu ni utamaduni ambao wanaadamu wenye heshima zao na hata wasomi wa Magaharibi wanakubaliana nao na vitendo vyao vinathibitisha hivyo. Katika nchi za Magharibi wako baadhi ya wanawake wanaojistahi na kuchunga heshima zao. Hawako tayari kujiuza na kuwa bidhaa ya kuridhisha matamanio ya kijinsia na ugube-gube wa wanaume wasiojiheshimu. (Lakini kinachoshuhudiwa zaidi katika nchi za Magharibi ni hayo maingiliano holela na michanganyiko ovyo ya wanaume na wanawake). Utamaduni mbovu wa Magharibi umejaa mambo kama hayo.

Juu ya ukurasa

Kutothaminiwa Hijabu Barani Ulaya

Kwa kweli inabidi ulimwengu wa Magharibi utujibu kwa nini katika kipindi chote cha historia tokea huko nyuma hadi hivi sasa wamekuwa wakimdhalilisha mwanamke. Huko Ulaya na katika nchi za Magahribi hadi hivi karibuni kabisa, wanawake walikuwa hawana haki ya kumiliki mali. Mwanamke wa Magharibi alikuwa hana haki ya kutumia kwa uhuru mali yake mwenyewe! Katika upande mwingine, mwanamme alikuwa ni mmiliki wa mali ya mwanamke na yeye mwenyewe mwanamke (alimilikiwa na mumewe). Yaani wakati mwanamke alipokuwa anaolewa, mali yake yote ilikuwa ikienda kwa mume na yeye hakuwa na haki ya kutumia mali yake hiyo. Hayo yaliendelea hadi pole pole mwanamke alipoanza kupewa haki ya kumiliki na kutumia mali yake anavyopenda na haki tena ameanza kupewa hivi karibuni tu mwanzoni mwa karne ya 20. Yaani licha ya kuwa suala hilo ni miongoni mwa haki za kimsingi kabisa za mwanaadamu, lakini mwanamke wa Magharibi alikuwa ananyimwa hadi karibuni kabisa, licha ya kuweko madai makubwa ya Wamagharibi kwamba wana ustaarabu mkongwe. Jengine ni hili suala la kuvuliwa nguo mwanamke wa Magharibi kwa sura ya ajabu kabisa vitendo ambavyo vinazidi kushtadi kadiri siku zinavyosonga mbele. Ni hayo maingiliano ovyo baina ya wanawake na wanaume kiasi kwamba madhara yake yamekuwa makubwa na hayadhibitiki tena. Yanafanywa hayo kwa madai ya kumpa uhuru mwanamke na kumpa heshima yake. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa kutoheshimiwa wala kuthaminiwa vazi la Hijabu katika nchi za Magharibi kunakwenda kinyume kabisa na heshima na hadhi ya mwanamke. Hilo ndilo linalotufanya sisi Waislamu kutilia mkazo sana suala la Hijabu. Lengo letu ni kumpa heshima mwanamke na kumpa hadhi yake ya kibinaadamu na sio kumdhalilisha.

Juu ya ukurasa

Kutembea Uchi na Ulevi, Desturi ya Ulaya

Leo hii duniani kuna hisia kali kuhusiana na vazi la mwanamke. Kama atatokezea mtu, shakhsia, mwanafalsafa, mwanajeshi, mwanasiasa akapinga suala la wanawake kutembea uchi, utaona kunazuka makelele mengi sana duniani! Hisia hizo kali hazionekani sana katika ada, desturi na masuala mengine mengi ya ufisadi. Kama kuna nchi itasema kwamba kwa mujibu wa siasa zake inapiga marufuku unywaji pombe na ulevi, utaona kunazuka makelele mengi duniani, au utaona watu wanaicheka nchi hiyo wakidai iko nyuma kimaendeleo! Utamaduni huu ni wa wapi? Hivi kufanywa kuwa ndiyo desturi mwanamke kutembea uchi, huku kuenea unywaji wa pombe kila mahala na kuonekana ndiyo desturi na jambo la kawaida ni utamaduni unaotokea wapi? Hiyo ni ada ya nchi za Ulaya na inatokana na utamaduni wa muda mrefu wa nchi hizo. Sasa hivi utamaduni na ada hiyo imeenea katika nchi nyingine mbali mbali ulimwenguni. Hivyo anapotokezea mtu akapinga tabia hiyo anaonekana kana kwamba amefanya makosa na madhambi makubwa sana!

Juu ya ukurasa

Ukinzani katika Mambo Yanayoheshimiwa kwenye nchi za Magharibi

Nchi za Magharibi ambazo zinadai zimeendelea na zinajigamba na kupiga propaganda kubwa kwamba zinayapa umuhimu mkubwa na kuyaheshimu masuala ya haki za binaadamu, leo hii haziwaruhusu hata wanawake wachache tu wa Kiislamu kuvaa vazi la staha la Hijabu na kutembea kwa uhuru katika shule zao! Linapofika suala la Hijabu na kujisitiri vyema wanawake wa Kiislamu, nchi hizo zinasahau kila kitu na zinajuzisha utumiaji nguvu na duru za nchi hizo hazioni tatizo lolote katika jambo hilo. Lakini wakati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaposema ni jambo la lazima kuvaa vazi la staha la Hijabu katika jamii yake, duru zote za Magharibi zinakuja juu na kupinga vikali jambo hilo! Kama inabidi mwanamke achunge vazi maalumu, basi mwanamke inabidi achunge vazi la Hijabu ambalo linampa stara na heshima na linamweka karibu zaidi na amani na usalama ikilinganishwa na kuvua Hijabu na kutembea uchi. Sasa angalau kwa uchache mambo hayo mawili yaangaliwe kwa namna moja, mwanamke awe huru kuvaa vazi lolote analopenda, lakini nchi za Magharibi hazifanyi hivyo, na hazina moyo wa kuvumilia kuona wanawake wakivaa vazi la Hijabu katika nchi hizo.

Juu ya ukurasa

Kudhalilishwa Mwanamke katika Utamaduni wa Magharibi

Msimamo wetu kuhusiana na mwanamke si wa kujihami, bali na wa kuingia kwenye medani na kutoa hoja kali. Wanachotulalamikia Wamagharibi ni kuwa kwa nini tunawavisha Hijabu wanawake? Kwa nini tunalifanya suala la Hijabu kuwa la lazima? Lakini wakati huo huo, hao hao wa Magharibi wanalifanya ni suala la lazima kutovaa Hijabu. Bali mambo huwa makubwa zaidi ya hayo kwao wao linapofika suala zima la mwanamke. Mwanamke katika utamaduni na ulimwengu wa Magharibi ametumbukizwa kwenye uduni, anadhalilishwa na kufanywa kiumbe hafifu. Kumfanya mwanamke kuwa bega kwa bega na mwanamme katika masuala ya kidiplomasia hakuwezi kufidia pigo kubwa aliloingizwa mwanamke wa Magharibi. Kumtumia mwanamke kama chombo na bidhaa ya kuenezea zinaa na kuwaridhisha kimatamanio ya kijinsia wanaume, ni kumdhalilisha vibaya sana mwanamke.

Juu ya ukurasa

Hijabu, Ufunguo wa Utamaduni wa Kiislamu

Ili kuzidi kuidhibiti kikamilifu nchi fulani na kuufanya udhibiti huo udumu ni lazima utamaduni wa nchi hiyo ubadilishwe. Inabidi utamaduni wa nchi hiyo uendane na utamaduni wa mabeberu na usalimu amri kikamilifu mbele ya utamaduni huo. Nchi za Magharibi zimejaribu sana kufanya jambo hilo dhidi ya mataifa ya Mashariki, tab’an hazikufanikiwa sana katika jambo hilo. Hivi sasa wanataka kufanya hivyo hivyo huko Afghanistan na bila ya shaka yoyote moja ya malengo yao makuu ni kuvuruga kabisa misingi mikuu inayojenga watu wa maana na kuwapa utambulisho watu wa nchi hiyo. Kabla ya jambo lolote wameanza na Uislamu. Wanapinga vazi la staha la Hijabu na suala zima la wananchi wa nchi hiyo la kushikamana na dini yao na kujifakharisha kwa mafundisho hayo. Ndiyo maana tunasema matukufu hayo ya Kiislamu inabidi yalindwe kwa nguvu zote.

Leo hii Wamagharibi wanailalamikia vikali Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa sababu imeifanya Hijabu kuwa ni jambo la lazima, lakini wakati huo huo hawazilalamikii nchi ambazo zinapinga vazi hilo tukufu na ambazo zinamlazimisha mwanamke atembee uchi! Wamagharibi wanafanya hayo kwa nini? Kwa sababu Hijabu inakwenda kinyume na utamaduni uliokubaliwa na Magharibi. Wamagharibi wana hisia kali sana kuhusu suala hilo.

Juu ya ukurasa

Kupigwa Marufuku Hijabu Barani Ulaya

Katika miaka ya hivi karibuni barani Ulaya – nchini Ufaransa na katika maeneo mengine kadhaa ikiwemo Ujerumani – kumekuwa kukishuhudiwa vita vikubwa dhidi ya vazi la staha la Hijabu. Katika upande mwingine, unaona wanapiga makelele makubwa kuhusu viwango vya kimataifa. Kwa mfano wanapotaka kusema jambo kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wanapotaka kusema kwamba Iran inabidi ifanye kitu fulani, utaona wanashikilia sana kusema “Lazima Iran ijiweke kwenye viwango vya kimataifa.” Lakini kumbe wanaposema viwango vya kimataifa, wanakusudia mambo yao hayo! Yaani mambo yanayokubaliana na utamaduni wao wa Magharibi. Hivyo mashinikizo na chagizo zote hizi za Magharibi zimekuwepo na zitaendelea kuwepo. Wamasharibi wanashambulia utamadui wowote usiokuwa wao na hususan utamaduni kama wa Kiislamu ambao ni madhubuti mno na unatoa changamoto kali popote unapoingia. Ni utamaduni usiotoa mwanya wa kushindwa hivyo Wamagharibi wanauwekea mashinikizo makubwa na kujaribu kuudunisha ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku uvaaji wa Hijabu.

Juu ya ukurasa

Faslu Ya Tatu: Hijabu Katika Mfumo Wa Jamhuri Ya Kiislamu Ya Iran

Kupenya Utamaduni wa Hijabu

Wanawake Waislamu katika nchi mbali mbali – ziwe za Kiislamu au zisizo za Kiislamu ambazo kuna wakati vazi tukufu la Hijabu halikuwa na nafasi yoyote kwao kutokana na kuzama sana katika propaganda za Magharibi na hata katika nchi za Ulaya kwenyewe – hivi sasa wanaelekea kwenye upande wa kuheshimu na kutunza vazi tukufu la Hijabu. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran tumekuwa tukishuhudia nchi nyingi hata za mbali ambazo zilikuwa zimeathiriwa na utamaduni wa Magharibi na wa nchi za Ulaya, zikielekea upande wa vazi la Hijabu na wanawake wa huko wanajaribu kuvaa Hijabu kama ya wanawake wa Iran. Nilipokuwa safarini katika eneo la Waislamu la kaskazini mwa Afrika niliona katika nchi moja watoto wa kike na akina mama wa nchi hiyo wakiigiza vazi la Hijabu kama ya Kiirani. Leo hii pia ulimwengu wa Magharibi nao, pole pole unaelekea upande wa kuheshimu vazi la staha la Hijabu ya Kiislamu.

Hivi tunavyoona kwamba katika baadhi ya nchi za Magharibi, bali hata katika baadhi ya nchi za Kiislamu na katika tawala zisizo za Kiislamu, vazi la Hijabu ya Kiislamu linapigwa vita kiasi chote hiki, lenyewe jambo hilo ni ushahidi kuwa vazi hilo tukufu linazidi kupata nguvu, na wanawake wanazidi kuingia hamu ya kujisitiri vizuri na kuvaa vazi la staha la Hijabu. Katika nchi jirani na nchi yetu pia, katika sehemu ambazo vazi la Hijabu lilikuwa halipewi umuhimu wowote, katika nchi za Kiislamu ambazo zilikuwa zimeghariki kwenye Umagharibi kiasi kwamba hata jina la Hijabu lilikuwa halisikiki ndani yake, baada ya kupita miaka 20 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu wanawake wa huko hasa wanawake wasomi na hususan wasichana wa Vyuo Vikuu, wameanza kupenda sana vazi la staha la Hijabu na unawaona wanachunga vazi hilo na kuliheshimu sana.

Juu ya ukurasa

Kupandikizwa Utamaduni wa Magharibi

Mtu ambaye aliuhudumia sana utamaduni wa Magharibi – yaani kwa hakika aliyeusaidia sana utamaduni wa Magharibi nchini Iran – na ambaye alipiga hatua kubwa ya kuusaidia ukoloni wa Uingereza zama hizo alikuwa ni mfalme Reza Khan. Laiti vitendo hivyo vinegelifanyika leo hii nchini Iran ingelikuwa ni kashfa kubwa mno. Lakini wakati huo mfalme mzima ghafla moja alizuka na kuamua kuondoa vazi la kitaifa la nchi yake! Nchi ya India na nchi nyingine mbali mbali duniani hadi leo zinachunga mavazi yao, zinajivunia na kuona fakhari kwa mavazi yao hayo, huzioni aibu kwa kuwa na mavazi yao. Lakini kwa upande wa Iran walikuja na mara moja wakatangaza tu kuanzia sasa mavazi fulani ni marufuku! Kwa nini? Kwa sababu eti kuvaa mavazi hayo kunamkwamisha mtu kielimu! Ajabu! Wasomi na wataalamu wakubwa wa Kiirani ambao hadi leo athari za kazi zao zinafundishwa na kusomeshwa barani Ulaya wamekulia katika utamaduni huu huu na kusomea kwenye mazingira haya haya. Kwani mavazi yana athari gani? Maneno gani haya wanatwambia hawa?! Wamekuja na mambo ya kichekesho kiasi chote hiki! Walikuja na kubadilisha kikamilifu vazi la taifa zima, wakatangaza kuanzia sasa wanawake hawana haki ya kuvaa Hijabu. Walifuta buibui la mwanamke! Walisema, mtu anayevaa buibui hawezi kuwa msomi, hawezi kuwa mtu aliyeelimika na wala hawezi kujihusisha na kazi za kijamii. Mimi ninawauliza, baada ya vazi la buibui kuondolewa nchini Iran, wanawake wa Kiirani walishirikishwa kiasi gani katika masuala la kijamii? Hivi kwani wanawake wa Kiirani waliruhusiwa kujihusisha na kazi za kijamii katika vipindi vya utawala wa Reza Khan na wanawawe? Si wanaume walishirikishwa na si wanawake. Wanawake wa Kiirani walianza kujihusisha na masuala ya kijamii na kulinyanyua taifa kwa mikono yao miwili na kuwaingiza wanaume kwenye medani ya mapambano, wakati wanawake hao walipoamua kuvaa mabuibui yao na kuingia uwanjani. Sasa vazi la buibui lina matatizo gani?! Vazi lina matatizo gani hata limzuie mwanamke asifanye kazi zake anavyopenda?! Ulikuwa ni ukosefu wa elimu na udikteta wa mfalme Reza Khan tu ndio uliomfanya aamue mara moja kubadilisha mavazi ya Wairani. Alifanya hivyo kwa sababu tu katika nchi za Magharibi pia wanawake hawajisitiri vizuri! Walileta utamaduni huo kutoka nchi za Magharibi. Hawakuliletea taifa hili kitu lilichokihitajia. Hawakuliletea taifa elimu, wala maendeleo, wala mwamko wa kufanya kazi, wala nguvu za kujilinda na hatari. Kiujumla ni kuwa kila nchi ina sifa zake maalumu, lakini hawakulizingatia hilo. Hata hicho kilichokuja kutoka Magharibi nacho walikikubali kibubusa bila ya hata kukichunguza na kukiangalia kwanza. Walisema tu kuwa madhali kimekuja kutoka kwa nchi za Magharibi, basi tukikubali tu. Aina ya mavazi, chakula, namna ya kuzungumza, namna ya kwenda yote hayo waliyabadilisha (nchini Iran na kuleta mambo mapya) kwa kuwa tu yametoka Magharibi. Jambo hilo ni sumu hatari sana na ni suala ambalo halikubaliki kabisa.

Juu ya ukurasa

Kudhulumiwa Mwanamke wa Kiislamu

Mwanamke katika jamii alikuwa akikandamizwa kikamilifu chini ya utawala dhalimu wa kifalme nchini Iran na kwa kweli alikuwa akidhulumiwa katika kila upande. Wakati mwanamke alipokuwa akitaka kuingia kwenye masuala ya kielimu alikuwa analazimika kwanza kuachana na masuala ya dini, taqwa na staha aliyokuwa nayo. Mwanamke alikuwa haruhusiwi kirahisi kuchunga vazi lake la Hijabu, kujistahi na wala kutekeleza mafundisho ya dini yake katika maeneo ya Vyuo Vikuu na kwenye vituo vya kielimu na kiutamaduni. Aslan mwanamke Muislamu aliyekuwa anachunga heshima ya Kiislamu na mavazi ya staha alikuwa haruhusiwi kutembea kwa amani na utulivu katika barabaraza za Tehran na kwenye miji mingi mikubwa ya Iran. Daima alikuwa akiandamwa kwa maneno ya kejeli na vitendo vya kuudhi kutoka kwa watu waliokuwa wameghariki kwenye ufisadi na uovu wa nchi za Magharibi. Walitenda mambo ambayo yalilifanya suala zima la kutafuta elimu humu nchini Iran kuwa haliwezekani kwa akina mama. Tab’an zilikuweko baadhi ya kesi ambazo hazikuwa na sura hiyo, lakini kiujumla ilikuwa ni vigumu mno kwa wanawake wa Kiislamu kuingia katika masuala ya kutafuta elimu ila pale walipoamua kuachana na vazi la Hijabu na wakati walipokubali kuachana na staha na mafundisho ya dini yao.

Juu ya ukurasa

Hijabu na Maendeleo ya Kijamii ya Wanawake wa Kiirani

Uislamu, Mapinduzi na Imam Khomeini (MA) alipokuja na harakati yake humu nchini, alimweka mwanamke katika vituo vikuu vya kazi za kisiasa na akawapa wanawake bendera ya Mapinduzi katika hali ambayo mwanamke aliweza kuchunga vizi lake la Hijabu, hadhi na staha yake ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na taqwa na kujiheshimu kikamilifu.

Mnashuhudia wenyewe jinsi mwanamke wa Kiislamu anavyoweza kufanya miujiza mikubwa wakati anaporejea katika maumbile na asili yake! Alhamdulillah ushahidi wa hayo unaonekana katika Mapinduzi yetu na katika Mfumo wetu wa Kiislamu leo hii. Alhamdulillah sasa hivi tunashuhudia idadi kubwa sana ya wasomi wa kike wakishiriki katika fani mbalimbali kwenye Vyuo Vikuu vyetu. Kuna idadi kubwa sana ya wanafunzi wa kike wa Vyuo Vikuu nchini ambao wako mstari wa mbele kielimu na wana vipaji vya hali ya juu. Wengine wamemaliza Vyuo Vikuu wakiwa na alama za daraja za juu, hivi sasa ni madaktari bingwa! Leo hii katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuna fani na kozi mbalimbali za kielimu zinazosomeshwa kwenye Vyuo Vikuu na wanawake wako huru kuchagua fani wanazopenda. Wanawake hao wanapata fursa hiyo huku wakiwa wanachunga staha na heshima zao, usafi na Hijabu zao tena kikamilifu. Vile vile wanajishughulisha na malezi ya watoto wao kwa njia za Kiislamu. Wanaendesha familia zao na kutunza waume zao kwa njia za Kiislamu na huku wakiendelea na kazi zao za kielimu na kisiasa. Kwa kweli mwanamke anaweza kufikia ukamilifu na utukukufu wake wa kweli kwenye mazingira ya Kiislamu na kwa moyo wa Kiislamu bila ya kujiingiza katika masuala ya anasa na kujidhalilisha kwa vitu vya kupumbaza vya kidunia.

Juu ya ukurasa

Ujumbe wa Wanawake Waislamu wa Iran

Wanawake wa Kiirani hususan wale ambao wamesoma na kufanya harakati mbali mbali katika fani tofauti wamefanya hayo ndani ya misingi ya Uislamu na sheria za Kiislamu, na muhimu kuliko yote waliofanya hayo ni wale wanawake ambao wanachunga vizuri vazi la staha la Hijabu. Ujumbe unaotolewa na wanawake hao kwa ajili ya akina mama na watoto wa kike wanaosoma kwenye Vyuo Vikuu ulimwenguni ni kwamba wanapaswa kufahamu kuwa elimu haina maana ya kutochunga mafundisho ya dini. Wala suala la kutafuta elimu halimlazimishi mtu kujiweka mbali na misingi ya kimaadili na wala hakuna maana ya kuruhusiwa maingiliano yasiyo ya kisheria kati ya wanawake na wanaume. Bali inawezekana kutafuta elimu kwa kuchunga kikamilifu sheria na maadili mazuri na kuweza kufikia daraja za juu kabisa za kielimu na kumfanya mwanamke wa Kiislamu kuwa mfano na kigezo cha ujumbe wa kimataifa wa Uislamu.

Juu ya ukurasa

 
Mbele >

^