Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Umoja wa Kiislamu na Madhara ya Utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu Chapa
08/03/2010

 “Hamu yangu kubwa ni kuyaona maisha yangu yamo katika njia ya umoja wa Waislamu na kufa kwangu kumo katika njia ya Umoja wa Waislamu” (Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei).

 

 

 

Nafasi na Uwezo wa Umma wa Kiislamu
Maana ya Umoja na Mshikamano wa Kiislamu

Mihimili ya Umoja na Mshikamano wa Kiislamu

Tawhidi
Utambulisho wa Kiislamu
Dini ya Kiislamu
Qur’ani
Mtume Mtukufu (Rehema na amani za Allah ziwe juu yake na Aali zake)
Ahlul Bayt (Amani iwe juu yao)

    Mtu Mkubwa katika Historia ya Mwanaadamu

Sunna na Sira ya Maasumu (Amani iwe juu yao) 

    Kauli Moja na Usafi wa Nyoyo
    Ndugu katika Dini na Mwenza katika Uanaadamu

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Faida za Umoja na Mshikamano wa Kiislamu

Ushindi na Heshima ya Waislamu
Kuyashinda Matatizo
Kujistawisha Kiuchumi na Kuwa na Nguvu za Kisiasa
Kujitawala na Kupata Ufanisi

Mambo Yanayozusha Mifarakano

Shirki
Shetani
Ujinga na Kuelewa Vibaya
Taasubu za Kikabila
Watu Wenye Madaraka
Makundi Yanayoeneza Mifarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu
Baadhi ya Tawala za Nchi za Kiislamu
Wanachuoni na Maulamaa wa Kiislamu Kutojali Maslahi ya Waislamu
Watu Vibaraka na Wenye Ushawishi katika Umma wa Kiislamu
Madhehebu Bandia na ya Kupandikiza
Kuvunjiwa Heshima Matukufu ya Kiislamu
Kupaliliwa Hitilafu za Kikabila

Hatari za Utengano Katika Umma wa Kiislamu

Tamaa ya Maadui wa Uislamu
Kukandamizwa Umma wa Kiislamu
Kutetereshwa na Kusalitiwa Uislamu na Waislamu
Kutomjua na Kumdharau Adui wa Kweli

Njia za Kuleta na Kukuza Umoja

Njia za Kuleta na Kukuza Umoja

Njia za Utatuzi wa Kiutamaduni

    Kuchora Vipengee vya Shakshia ya Mtume Mtukufu (SAW)
    Kuwa Makini Mbele ya Adui
    Umuhimu wa Maulamaa Kuwa na Kauli Moja
    Umuhimu wa Maulamaa Kuwa na Muono Mpana
    Kutoyapa Nguvu Masuala ya Hitilafu

Njia za Utatuzi wa Kisiasa

    Umoja na Mshikamano Mbele ya Adui wa Pamoja

Njia za Utatuzi wa Kiuchumi

Watu wa Mstari Waliotoa Mchango Mkubwa Katika Suala Zima la Kuleta Umoja

Ayatullah Udhma Burujerdi na Sheikh Mahmoud Shaltut
Sayyid Jamaluddin Asad Abadi
Imam Khomeini (MA)

Madhihirisho ya Umoja na Mshikamano wa Kiislamu

Kustawi Umma wa Kiislamu
Wiki ya Umoja
Siku ya Kimataifa ya Quds
Sikukuu za Kiislamu
Darut Taqrib

Umoja wa Kiislamu na Madhara ya Utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu

“Hamu yangu kubwa ni kuyaona maisha yangu yamo katika njia ya umoja wa Waislamu na kufa kwangu kumo katika njia ya Umoja wa Waislamu” (Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei).

 

 Nafasi na Uwezo wa Umma wa Kiislamu

Mataifa haya ndugu na yanayopendana yanayotokana na vizazi tofauti vya watu weusi, weupe na njano, mataifa ambayo yanazungumza makumi ya lugha tofauti yote kwa pamoja yanajiona kuwa ni sehemu sawa katika umma mmoja mkubwa wa Kiislamu na yanajifakharisha kwa jambo hilo. Siku zote watu wa mataifa hayo yanaelekea kwenye upande mmoja wakiswali na kunong’ona na Mola wao kwa lugha moja wakiwa wameungana katika Kitabu kimoja wakipata somo na ilhamu kutoka katika Kitabu hicho kitakatifu.

Majimui hiyo ambayo jina lake ni umma wa Kiislamu ina utamaduni tajiri wenye urithi adhimu na mkubwa sana. Una njia bora kabisa za ufanisi na mafanikio ya kipekee na licha ya kuwa na sura za watu na mataifa mengi tofauti, umma huo una njia bora kabisa za mshikamano wa kiajabu ambazo zinashuhudiwa katika nguzo na pembe zake zote yakiwa ni matunda ya mafundisho na ushawishi wa Uislamu na tawhidi maalumu na safi katika sehemu zake zote.

Umma wa Kiislamu una zana na njia nyingi za kuweza kulinda haki na uwepo wake. Waislamu wanaunda idadi kubwa ya watu duniani, wana utajiri mkubwa, wana watu wakubwa wakubwa na muhimu sana na wana rasilimali ya kimaanawi ambayo inawapa nguvu ya kuweza kusimama kidete mbele ya mabeberu. Waislamu wana utamaduni na ustaarabu wenye historia kongwe ambao hauna mfano wake duniani. Waislamu wana suhula nyingi sana ambazo zinawapa uwezo wa kimaumbile na kiasili Waislamu hao, wa kuweza kujihami na kujilinda. Leo hii ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kufanya juhudi zake zote kwa ajili ya kujiletea heshima, uhuru wake, maendeleo yake ya kielimu, nguvu zake za kimaanawi yaani kushikamana vilivyo na dini na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kuwa na yakini kwamba Mwenyezi Mungu Yuko pamoja nao na atawanusuru tu. Waislamu wanapaswa kuingia kwenye medani mbali mbali wakijua kwamba Mwenyezi Mungu amewaahidi ushindi na nusura kutoka Kwake. Mwenyezi Mungu anasema:

 وَلَيَنصُرَنَّ اللَّهُ مَن يَنصُرُهُ إِنَّ اللَّهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ

Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayemsaidia Yeye (anayeilinda dini Yake). Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu. (al Hajj; 22:40).

Waislamu wanapaswa kuingia kwenye medani hizo kwa kutegemea ahadi hiyo ya Mwenyezi Mungu. Jambo hilo halina maana ya kuchukua silaha tu, bali kazi hiyo ni kazi ya kifikra, ni kazi inayotaka kutumia akili na busara, ni kazi ya kielimu, ni kazi ya kijamii, na ni kazi ya kufanya kazi za kisiasa na kuhakikisha yote hayo yanafanyika kwa jina la Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano katika umma wa Kiislamu. Kama mambo yatatendeka hivyo basi mataifa yote yatanufaika na tawala zote za Kiislamu zitafaidika.

Juu ya ukurasa

Maana ya Umoja na Mshikamano wa Kiislamu

Neno umoja ni kitu rahisi na kilicho wazi nalo ni neno lenye maana ya kushirikiana makundi mbali mbali ya Kiislamu na kujiepusha na mizozo na migongano. Maana ya umoja baina ya Waislamu ni kutokataana na kutotoa mwanya wa kudhibiatiw Waislamu. Maana ya umoja kati ya Waislamu ni kutofarikiana na kuanza kufanyiana uadui wao kwa wao.

Maana ya umoja kati ya mataifa ya Kiislamu ni kuwa na msimamo mmoja katika masuala yanayohusiana na ulimwengu wa Kiislamu, kuwa na harakati za pamoja, kusaidiana mataifa hayo na kutotumia rasilimali na utajiri wao dhidi ya mataifa mengine ya Kiislamu.

Umoja wa Waislamu hauna maana ya kwamba Waislamu na madhehebu tofauti za Kiislamu waachane na mitazamo yao maalumu ya kiitikadi na kifikihi bali umoja wa Waislamu una maana nyingine mbili tofauti na lazima maana hizo mbili zipatikane kwa wakati mmoja. Mosi ni kuwa, makundi mbali mbali ya Kiislamu ambapo kila kundi lina mtazamo wake tofauti wa kiitikadi na kifikihi yote yashikamane barabara mbele ya maadui wa Uislamu. Yasaidiane na yawe na fikra moja mbele ya maadui hao. Pili ni kwamba kila kundi la Kiislamu lihakikishe kuwa linakurubiana na makundi mengine ya Kiislamu ili kuleta maelewano na kulinganisha mitazamo yao ya kifikihi na halafu kuitabikisha pamoja. Kuna fatwa nyingi za kifikihi za maulamaa wa Kiislamu ambazo kama zitaangaliwa kiutaalamu na kielimu, zinaweza kufanyiwa mabadiliko kidogo na kuzifanya zikurubiane sana na fatwa za madhehebu mengine ya Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Mihimili ya Umoja na Mshikamano wa Kiislamu

Tawhidi

Katika jamii ya kitawhid, Mwanzo wa kila kitu, Mmiliki wa uwepo, Mfalme wa ulimwengu, Msimamizi wa mambo yote, Mwenye nguvu juu ya kila kitu ni Mwenyezi Mungu Mmoja Ambaye harakati zote na matukio yote ulimwenguni yanategemea matakwa na nguvu Zake Yeye Mmoja tu. Wanaadamu wote - wawe weusi, wawe weupe, wawe ni wenye damu tofauti na vizazi mbali mbali na hali zisizofanana za kijamii – wote wana uhusiano wa karibu baina yao kwani wote wana mfungamano na Mwenyezi Mungu Mwenye sifa tulizotangulia kuzitaja. Wote wana mfungamano na mahala pamoja na wote wanapata msaada kutoka katika sehemu moja. Hayo ni matunda ya kimaumbile ya imani ya tawhidi. Katika mtazamo huo, si kwamba ni wanaadamu pekee wenye mfungamano wa karibu, bali kwa mtazamo wa kitawhidi, vitu vingine vyote ulimwenguni, wanyama na vitu visivyo na uhai na ardhi na mbingu, vyote vina mfumangamano wa pamoja na wa karibu. Hivyo kile ambacho mwanaadamu anakiona, anakihisi na anakikamata na kukidiriki, kinatoka katika upeo mmoja, katika ulimwengu mmoja, katika majimui moja na yako katika dunia moja salama na mazingira ya amani.

Juu ya ukurasa

Utambulisho wa Kiislamu

Leo hii Waislamu wote katika kila kona ya dunia – iwe ni katika nchi za Kiislamu au katika maeneo ambayo idadi yao ni chache – wanahisi kuwa na hamu kubwa sana ya kurejea kwenye Uislamu wao na wanajihisi kuwa wamepata upya utambulizo wao wa Kiislamu. Leo hii wasomi katika ulimwengu wa Kiislamu ambao wamekatishwa tamaa na fikra za kisoshalisti na za Kimagharibi hivi sasa wanaelekea zaidi katika upande wa Uislamu na wanaona ni Uislamu ndio unaoweza kutatua matatizo ya wanaadamu. Hivi sasa nyoyo za umma wa Kiislamu zinaelekea zaidi upande wa Uislamu jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa mfano wake kwa karne nyingi. Baada ya nchi za Kiislamu kudhibitiwa kisiasa na kwa utamaduni ghalati wa Magharibi na Mashariki katika kipindi kirefu cha makumi ya miaka, hivi sasa nyoyo za Waislamu zinaona Uislamu umepata uhai mpya na mtazamo wa vijana katika ulimwengu wa Kiislamu unaelekea zaidi upande wa kuheshimu na kutekeleza mafundisho ya Uislamu. Hili ni jambo la hakika ambalo hata Wamagharibi na mabeberu wa dunia wanakiri kwamba lipo na ndivyo hali ilivyo hivi sasa. Kitu ambacho kinawaogopesha wakuu wa kibeberu duniani ni utambulisho wa Kiislamu na ni kule kuona Waislamu wanajitambua na wanashikamana na mafundisho ya dini yao. Lakini jambo hilo ndilo linalowapa Waislamu umoja na mshikamano.

Juu ya ukurasa

Dini ya Kiislamu

Uislamu unaufanya umma wa Kiislamu uhisi kuwa na mfungamano na umoja na kulifanya wimbi hili kubwa la watu bilioni moja na mamia ya mamilioni ya Waislamu liwepo na lishiriki katika masuala mbali mbali ya ulimwengu wa Kiislamu.

Katika dini tukufu ya Kiislamu, umoja ni kitu cha msingi kabisa. Umoja unashuhudiwa kuanzia katika dhati ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Ambaye Ndiye asili na Dhihirisho la umoja na upweke, hadi katika athari za upweke huo ambapo ulimwengu mzima wa uwepo na ujudi wake unaelekea na kurejea kwa kituo hicho adhimu na kitukufu. Mwenyezi Mungu anasema:

کلٌّ إِلَينا راجِعُونَ

– wote wanarejea na wanaelekea kwenye Dhati Tukufu ya Mwenyezi Mungu

(Sehemu ya aya ya 93 ya sura ya 21 ya al Anbiyaa inayosema kundi la wafuasi wao walijitumbukiza katika mifarakano na wakalikata jambo lao mapande mapande baina yao lakini mwisho wa yote wote watarudi kwa Mwenyezi Mungu).

Vile vile Mwenyezi Mungu anasema:

 وَإِلَي اللَّهِ الْمَصيرُ

Na kwa Mwenyezi Mungu ndiyo marejeo ya viumbe wote (an Nur; 24:42).

Hivyo umoja inabidi uwepo kwa misingi ya Uislamu na kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu na si kwa misingi ya ndoto na kuzingatia masuala yasiyo na maana ya kikabila ambayo kwa hakika hayana faida yoyote. Nguvu na umadhubuti wa umma wa Kiislamu unaweza kupatikana kwa njia hiyo. Umoja inabidi ujengwe juu ya misingi ya kuutumikia na kuutia nguvu Uislamu vinginevyo umoja huo utakuwa pumba usio na maana yoyote.

Juu ya ukurasa

Qur’ani

Qur’ani inawausia Waislamu kuwa na umoja. Qur’ani imewaonya Waislamu kwamba kama watapoteza umoja na mshikamano wao basi watapoteza heshima, utambulisho na nguvu zao. Inasikitisha kuona kuwa leo hii katika ulimwengu wa Kiislamu kuna matatizo mengi mno yanayoukabili ulimwengu huo. Njama zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu leo hii ni kubwa sana. Kama leo tunaona wanafanya njama kubwa kiasi chote hiki na kwa mpangilio maalumu dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu tujue kuwa jambo hilo linatokana na kuamka umma wa Kiislamu. Kwa hakika mwamko wa Waislamu unawatia woga na wasiwasi mkubwa maadui wa Uislamu. Mabeberu wa kimataifa, watu wenye tamaa katika nchi za Kiislamu, uingiliaji wa kigeni katika masuala yanayohusu tawala za nchi za Kiislamu, yote hayo yanatokana na kwamba wanauogopa sana umoja wa umma wa Kiislamu.

Qur’ani tukufu inakariri sana maneno yanayosema:

«يا ايُّها الّذينَ آمَنوا»

 “Enyi ambao mumeamini” hakuna maneno yanayosema:

«يا أيُّها الَّذينَ تَشَيَّعوا»

 “Enyi ambao ni Mashia”

au

 «يا أيُّها الّذينَ تَسَنَّّنوا»!

“Enyi ambao ni Masuni!”

Bali ugha ya Qur’ani ni “Enyi waumini.” Waumini wa kitu gani? Waumini wa Qur’ani, waumini wa Kiislamu, waumini wa Mtume Muhammad SAW. Kila mmoja ana itikadi na mitazamo yake tofauti na wenzake lakini Waislamu wote wanakusanyika pamoja kwenye mihimili hiyo. Wakati Qur’ani Tukufu inaposema:

«وَاعْتَصِمُوا بِحبل‌الله جَميعاً وَ لا تَفَرَّقُوا»

Shikamaneni nyote na kamba ya Mwenyezi Mungu (Qur’ani, Uislamu, Mtume na kila kitu kinacholeta umoja) wala msifarikiane (Aal Imran; 3:103), inawakusudia waumini na Waislamu wote, haikikusudii kikundi kimoja tu cha Waislamu.

Wakati Qur’ani Tukufu inaposema:

«وَ إِنْ طائِفَتانِ مِنَ الْمُؤْمِنينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَينَهُما»

Wakati makundi mawili ya waumini yanapogombana suluhisheni baina yao (al Hujurat, 49:9), huwa inawakusudia Waislamu na waumini wote, haikusudii kikundi fulani tu. Ni kwa kutumia misingi hiyo ndio maana Uislamu una uwezo mkubwa wa kuondoa mazingira na misingi ya ugomvi na mizozano ya taasubu za kimadhehebu na kidini, mizozo ambayo inawatesa wanaadamu wote hivi sasa.

Qur’ani Tukufu inasema:

«&«وَاعْتَصِمُوا بِحبل‌الله جَميعاً وَ لا تَفَرَّقُوا»

Shikamaneni nyote na kamba ya Mwenyezi Mungu wala msifarikiane (Aal Imran; 3:103).

Kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu ni amri inayowahusu Waislamu wote lakini Qur’ani haukutosheka na kusema shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu tu bali inasisitiza zaidi ikisema katika kushikamana huko na kamba ya Mwenyezi Mungu Waislamu wanapaswa kufanya hivyo kwa umoja wao «جميعاً» wote kwa pamoja washikamane katika kamba hiyo. Kujumuika huko pamoja ni wajibu kwa Waislamu wote.

Hivyo sambamba na kwamba ni wajibu kwa Waislamu kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu, ni wajibu pia kwao kushikamana na kamba hiyo kwa pamoja na kwa wote «جميعاً» sio kila Muislamu peke yake peke yake, bali washirikiane pamoja katika kushikamana na kamba hiyo. Umoja na Mshikamano wa aina hii inabidi ujulikane vyema na utekelezwe kwa umakini na usahihi kabisa. Maana halisi ya kushikamana kunakotakiwa na Uislamu inaonekana katika aya inayosema:

«فَمَنْ يکفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَ يؤْمِنْ بِاللَّهِ فقد استَمْسَک بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقي»

Anayemkufuru taghuti (shetani na kiumbe chochote kiovu) na akamwamini Mwenyezi Mungu, kwa hakika huwa ameshikamana na kishiko chenye nguvu. (al Baqarah; 2:256).

Hiyo ndiyo maana ya kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu. Kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu maana yake ni kumwamini Mwenyezi Mungu na kumkufuru taghuti.

Juu ya ukurasa

Mtume Mtukufu (Rehema na amani za Allah ziwe juu yake na Aali zake)

Uwepo mtakatifu wa Bwana Mtume Muhammad (rehema na amani za Allah ziwe juu yake na Ahul Bayt wake) ni nukta bora kabisa ya kupatikana umoja na mshikamano kati ya Waislamu. Huko nyuma nimewahi kuzungumzia pia suala hili kwamba ulimwengu wa Kiislamu unaweza kuungana na kuwa kitu kimoja kwa kutumia uwepo mtakatifu wa Mtume Muhammad SAW. Nukta hii inakusanya mapenzi yote ya Waislamu. Bwana Mtume ndiye nembo ya mahaba na mapenzi katika ulimwengu wa Kiislamu. Ndio maana tunaona kalamu za watu wanaopewa pesa na Wazayuni zilivyojikita sana kwenye suala la kumvunjia heshima mtukufu huyo wa daraja ili kuwafanya Waislamu wasimpende Bwana Mtume na waone ni jambo la kawaida kuvunjiwa heshima mbora huyo wa viumbe. Bwana Mtume ni nukta ya asili. Wanasiasa, watu wenye vipaji vya kielimu, kiutamaduni, waandishi, watungaji wa tungo za kishairi na wasanii wetu wanapaswa kuitilia mkazo sana nukta hiyo na kuwafanya Waislamu wote waungane na wakurubiane kupitia mtukufu huyo. Masuala ambayo yana tofauti yasipewe umuhimu, na Waislamu wasikufurishane wala wasiseme wenzao si Waislamu. Nyoyo za umma mzima wa Kiislamu unapata uchangamfu na uhai mpya kwa mapenzi ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Nyoyo zetu sote zina mapenzi makubwa sana kwa Mtume wetu mtukufu.

Juu ya ukurasa

Ahlul Bayt (Amani iwe juu yao)

Miongoni mwa sababu ambazo zinaweza kuwa mhimili wa umoja na mshikamano wa Waislamu ni kauli yao moja kuhusu suala la kuwafuata Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Waislamu wote wanawapenda na wanawakubali watu wa nyumba ya Bwana Mtume.

Ulimwengu wa Kiislamu unaweza kutumia mhimili wa nukta mbili zinazohusiana na Ahlul Bayt kuweza kuleta umoja na maridhiano. Nukta ya kwanza ni mapenzi ambalo ni jambo la hisia za ndani ya moyo na kiitikadi na Waislamu wameamrishwa kuwapenda Ahlul Bayt AS. Waislamu wote wanaitii amri hiyo. Hivyo nukta hiyo inaweza kuwa ni nukta moja kuu ya kukusanya hisia za Waislamu wote pamoja. Nukta ya pili ni mafunzo ya dini na ilmu ya maarifa na hukmu za Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa Qur’ani na Hadithi ya ath Thaqalayn ambapo Waislamu wote wa Kishia na Kisuni na makundi mbali mbali ya Kiislamu yameinukuu na kuihadithia hadithi hiyo.

Juu ya ukurasa

Mtu Mkubwa katika Historia ya Mwanaadamu

Kumpenda Amirul Muminin Ali bin Abi Talib (Alayhiswalatu Wassalaam) na kuwa na hisia nzuri kuhusiana na mtu huyo mkubwa katika historia ya mwanaadamu na historia ya Uislamu si jambo linalowahusu Waislamu wa Kishia peke yao, wala si suala linalowahusu Waislamu wa Kisuni peke yao, bali ni jambo ambalo linawahusu wapenda uhuru wote ulimwenguni hata wasio Waislamu. Kuna watu muhimu ambao hata si Waislamu wameonyesha mapenzi yao kwa mtukufu huyo, wameandika vitabu kuhusu Imam huyo wa Mashariki na Magharibi wamemtungia mashairi n.k. Hivyo ni kosa kubwa sana kama mtu kama Imam Ali AS atageuzwa kuwa nukta ya hitilafu baina ya Waislamu. Mtukufu huyo ni shakhsia kubwa ambaye Waislamu wote, makundi yote ya Kiislamu yanampenda kwa moyo wao wote. Mapenzi hayo yanatokana na kuwa mtukufu huyo ana sifa kubwa sana ambazo mtu yeyote mwenye insafu analazimikia kunyenyekea anapofika mbele ya sifa hizo. Hivyo ndivyo alivyo Imam Ali AS na hayo ndiyo yanayopaswa kuwaunganisha Waislamu.

Juu ya ukurasa

Sunna na Sira ya Maasumu (Amani iwe juu yao)

Kauli Moja na Usafi wa Nyoyo

Asili ya tatu (yaani Amirul Muminin Ali AS) amenukuliwa akisema katika sehemu ya pili ya wasia wake kwa wanawe wawili Hasan na Husain AS kwamba “wasuluhishe mambo baina yao” yaani watendeane mema na wasizozane. Wakinaishiane nyoyo, wawe na kauli moja na usiweko utengano na mfarakano baina yao. Aliwapa wanawe wasia huo ambao una ushahidi pia katika matamshi na miongozo ya Mtume Muhammad SAW. Ni jambo lililo wazi kwamba alisisitiza sana juu ya jambo hilo na alikuwa na woga nalo. Hii si kwa sababu kusuluhisha baina ya watu kuna umuhimu mkubwa zaidi kuliko kuwa na mipangilio mizuri, hapana, bali sababu yake ni kuwa suala la suluhu baina ya watu ni kitu kinachoweza kuathirika haraka zaidi ndio maana katika usia wake huo kwa wanawe Hasan na Husain AS, Amirulmuminin Ali AS akanukuu maneno ya Bwana Mtume SAW akiwaambia: Nimemsikia babu yenu akisema, kusuluhisha na kuleta amani baina ya watu ni bora kuliko sala zote na kuliko saumu zote. Hapo Bwana Mtume anasisitiza kwamba kama mnazipa umuhimu sana sala na funga, basi jueni sambamba na ibada hizo muhimu kuna na jambo jengine muhimu zaidi na lenye thawabu kubwa zaidi. Jambo hilo ni nini? Ni kusuluhisha na kuleta amani baina ya watu. Kama mtaona sehemu fulani katika umma wa Kiislamu kuna hitilafu na mfarakano, fanyeni haraka kuondoa mfarakano huo. Kufanya hivyo ni bora zaidi kuliko funga na sala na thawabu zake ni kubwa zaidi.

Juu ya ukurasa

Ndugu katika Dini na Mwenza katika Uanaadamu

Ujumbe wa dini tukufu ya Kiislamu ni ujumbe wa umoja, amani na udugu. Amirul Muminin Ali AS amenukuliwa akisema maneno ambayo ubora wake utabakia milele kwa ajili ya wanaadamu wote. Amenukuliwa akisema: Mtu ambaye unamuona mbele yako ima ni ndugu yako katika dini au ni mwenzako katika uanaadamu na kwa ufupi ni mwanaadamui mwenzako. Wanaadamu wote wanapaswa kuwa wamoja waoneane huruma hususan wakati watu hao wanapokuwa ni wa kundi moja. Ndio maana Uislamu unawaamrisha Waislamu wawafanyie wema hata watu ambao si Waislamu na hata kama hawakubaliani na itikadi za dini yao. Mwenyezi Mungu anasema:

لا يَنْهَاكُمُ اللَّهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ

Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu. (al Mumtahina, 60:8).

Hiyo ndiyo mantiki ya Uislamu. Yaana hata kama mtu hauamini Uislamu na ana itikadi nyingine zisizokubaliwa na Uislamu, inabidi Waislamu wamtendee wema. Mwanaadamu siye aliye na haki ya kumhukumu mtu kwa itikadi yake na hapa si mahala pake. Imepokewa hadithi katika Biharul Anwar inayosema:

 «وَالْحَکمُ اللَّهُ، وَ الْمَعْوَدُ إِلَيهِ الْقِيامَة»

Na hukumu ni ya Mwenyezi Mungu na ahadi ya mtu huyo asiyeamini Uislamu ni siku ya kiyama.

Kwa upande wake, Imam Ali AS anasema mtu unayemuona mbele yako ima ni mwenzako na ni ndugu yako katika itikadi na dini yako au ni mwanaadamu mwenzako hata kama hakubaliani na itikadi yako. Huo ndio Uislamu.

Juu ya ukurasa

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Adui ametumia njia zote kutaka kuzusha hitilafu katika jamii ya Kiislamu, lakini leo anashuhudia kutukia tukio ambalo hajawahi kulishuhudia mfano wake nacho ni kituo cha umoja na mshikamano kwa ajili ya Waislamu wote nayo ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Bendera hii inayopepea juu na sauti hii inayotoka kwa uwazi kabisa na kitu hiki kilichojitokeza kikiwa na Katiba na kaulimbiu na vitendo vinavyotabikiana na Uislamu, kama ilivyotarajiwa kimeweza kuzivutia nyoyo za Waislamu katika kila kona ya dunia. Leo hii ukitoa katika Iran ya Kiislamu, hakuna sehemu nyingine duniani ambako sheria za Kiislamu zinafuatiliwa kwa nguvu kiashi chote hiki. Lengo la maneno hayo hapa si wananchi wa nchi nyinginezo kwani Waislamu popote walipo wanaipenda dini yao na wako tayari kutekeleza vilivyo mafundisho ya dini yao. Lengo hapa ni siasa na tawala ambazo hata kama zimeanza kwa jina la Uislamu, lakini wakati zilipokabiliwa na mawimbi makali ya mashambulizi ya kimataifa, zimelegeza kamba na kurudi nyuma.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kuanza kuenea fikra za mapinduzi hayo katika kila kona ya ulimwengu wa Kiislamu, moja ya njama kubwa zilizofanywa na mabeberu katika kukabiliana na wimbi hilo kubwa la Kiislamu lililotokana na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ni kuanza kujaribu kuwaweka mbali Waislamu wengine na Waislamu wenzao wa Kishia. Ilikuwa ni kujaribu kueneza propaganda kuhusu Ushia na kutaka kuonyesha kuwa ni kikundi tu na kuyato madhehebu hayo katika maana yake ya Uislamu na wakati huo huo kuanzisha unafiki na chuki baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni. Lakini sisi tangu awali tulizijua hila na kedi hizo za kishetani na tangu wakati huo tumekuwa tukisisitiza sana juu ya umuhimu wa kuweko umoja na mshikamano kati ya makundi mbali mbali ya Waislamu ili kuzivunja nguvu fitna hizo na Alhamdulillah tumepata mafanikio makubwa katika juhudi zetu hizo ambapo moja ya mafanikio hayo ni kuundwa kwa Baraza la Kimataifa la Kuyakurubisha pamoja Madhehebu ya Kiislamu. Tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu hadi leo hii, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa daima ikizitaka nchi za Kiislamu kuungana na kuwa kitu kimoja. Kama tunaiona Iran daima inafanya juhudi za kuhakikisha kuwa inalinda na kuhifadhi udugu na urafiki wake na tawala nyingine za nchi za Kiislamu si kwa sababu serikali na wananchi wa Iran wana haja kubwa sana na kuwepo udugu na urafiki huo, au haiwezi kuishi bila ya umoja huo, hapana bali ni kwa sababu Iran inaona kuwepo kwa udugu na urafiki huo kuna faida kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Faida za Umoja na Mshikamano wa Kiislamu

Ushindi na Heshima ya Waislamu

Mataifa ya Kiislamu nayapaswa kujua nguvu zao ambazo ni hizo nguvu za imani na mshikamano kati ya nchi za Kiislamu. Waislamu inabidi watumie vizuri nguvu zao hizo. Nchi za Kiislamu kama zitakuwa kitu kimoja zitaweza kuwa na nguvu kubwa na wakati huo tena adui hatathubutu kusimama mbele ya nchi hizo wala kuzifanyia ubeberu. Kama Waislamu watashikamana na kuishi kiudugu na kupendana hata kama wana mitazamo tofauti kuhusu baadhi ya mambo, lakini kama hawataruhusu tofauti zao hizo kutumiwa vibaya na maadui, basi ulimwengu wa Kiislamu utaishi kwa fakhari na kwa heshima kubwa.

Mataifa yoyote yale ambayo yatajipamba kwa sifa hiyo na kukabiliana vilivyo na matatizo yanayojitokeza, basi madola ya kimataifa – Marekani na mfano wa Marekani hayataweza kamwe kufanya chochote dhidi ya mataifa hayo. Wananchi wanapoamua hupata ushindi siku zote. Huo ndio ukweli wa mambo. Kama ulimwengu wa Kiislamu utataka kuifanya harakati makini ya umma wa Kiislamu ipate ushindi na kusonga mbele vile inavyotakiwa, basi unapaswa kutilia maanani njia za kufanikisha jambo hilo na moja ya njia hizo ni umoja na mshikamano.

Juu ya ukurasa

Kuyashinda Matatizo

Kama Waislamu watashikamana, kama wataamka, kama watatilia maanani nguvu zao kama wataamini kwamba wanao uwezo wa kubadilisha hali waliyo nayo hivi sasa, kama watajiamulia wenyewe mustakbali wao na kama wataangalia kwa kina jinsi baadhi ya mataifa kama taifa kubwa la Iran lilivyoweza kujiamulia lenyewe mustakbali wake na kama Waislamu hawatakubali kudhibitiwa na madola makubwa ya kibeberu, basi bila ya shaka yoyote masaibu na matatizo yote yanayoukabili ulimwengu wa Kiislamu nayo yatamalizika. Hilo ndilo jambo la kimsingi na muhimu zaidi hivi sasa.

Isiwe ni suala la kujidhalilisha, wala la kusalimu amri, wala la mazungumzo ya kujidunisha na wala njia yoyote nyingine ambayo watu wasioona mbali wanajaribu kuwapendekezea Waislamu. Hayo hayawezi kuwafikisha popote Waislamu. Utatuzi pekee wa matatizo ya Waislamu si mambo hayo bali njia pekee ya kutatua matatizo ya Waislamu ni umoja na mshikamano wa kweli, ni kusimama kidete na kuutii inavyopasa Uislamu na matukufu na misingi ya dini hiyo tukufu. Ni mapambano na istikama mbele ya mashinikizo na vikwazo vikubwa vya maadui ndiyo mambo yanayoweza kumshinda adui tab’an hilo linataka uvumilivu na kupita muda.

Leo hii utatuzi wa matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu ni kurejea kwenye Uislamu na umaanawi na kwenye sheria na mafundisho ya Kiislamu. Hilo ni moja na pili ni kushikamana Waislamu na kuwa kitu kimoja ambapo mshikamano nao ni amri na ni miongoni mwa mafundisho muhimu ya Uislamu. Dini tukufu ya Kiislamu imesisitiza sana juu ya haja ya kuweko umoja kati ya Waislamu basi lengo lake ni kutaka kuondoa bugudha, chuki na uhasama katika safu za waumini wa dini hiyo ya Mwenyezi Mungu.

Juu ya ukurasa

Kujistawisha Kiuchumi na Kuwa na Nguvu za Kisiasa

Nchi za Kiislamu hazina mgogoro wa maslahi baina yao. Nchi hizo zinapounda majimui moja ya Kiislamu, zinapokuwa ni kambi moja ya Kiislamu na zote zinapokuwa na uhusiano mzuri, suala hilo huwa zuri kwa wote na si kwa jamii fulani tu. Nchi kubwa za Kiislamu nazo zitaweza kufaidika zaidi zinapokuwa ndani ya majimiu moja ya Kiislamu, nchi dhaifu, ndogo na maskini nazo zitaweza kufaidishwa na jambo hilo. Bila ya shaka kama ulimwengu wa Kiislamu usingeliwasaidia Waislamu wenzao wa Bosnia leo hii tusingelisikia habari zozote kuhusu Waislamu wa Bosni barani Ulaya kwani wangeliangamizwa kikamilifu na kufutwa kabisa katika uso wa dunia.

Ulimwengu wa Kiislamu ni mkubwa na mpana unaanzia magharibi kabisa yaani magharibi mwa Afrika hadi mashariki kabisa yaani mashariki mwa bara la Asia. Eneo lote hilo ni la ulimwengu wa Kiislamu. Maeneo na nukta nyeti kabisa duniani zimo mikononi mwa Waislamu. Moja ya sehemu hizo ni hili eneo la Ghuba ya Uajemi ambapo dunia nzima imepanga safu kwa ajili ya kujaza shehena zao kutokana na utajiri wa eneo hili na kurejea makwao. Dunia nzima inategemea mafuta ya eneo hili. Kama Waislamu wataungana na kuwa kitu kimoja, bila ya shaka yoyote ulimwengu wa Kiislamu utanufaika sana.

Juu ya ukurasa

Kujitawala na Kupata Ufanisi

Hivi sasa, kuna njama nyingi sana za maadui wanaotaka kuhakikisha kuwa Waislamu hawaungani na hawaafikiani bali wanataka kuwaona Waislamu siku zote wanafanyiana uadui. Njama hizo zimeongezeka sana wakati huu ambapo Waislamu wana haja kubwa ya kuwa na umoja na mshikamano kuliko wakati mwingine wowote. Ni jambo lililo wazi kwamba lengo la njama hizo za maadui ni kukwamisha juhudi za Waislamu za kurejesha heshima yao na kujiletea ufanisi hususan kwa kuzingatia kuwa leo hii Waislamu wanaonekana wanafanya juhudi za kulifanikisha kivitendo jambo hilo. Ni jambo lililo wazi kwamba kama Waislamu wataamua kushikamana vilivyo na Uislamu, hawezi hata siku moja kufanya hivyo kama hitilafu hizi zilizopo baina yao zitaendelea kuwepo. Kizuizi kibaya na cha hatari zaidi katika njia ya heshima, ufanisi na kutawala dini tukufu ya Kiislamu ni mtengano baina ya Waislamu ima wa jamii moja au wa nchi na nchi. Ndio maana maadui wanafanya kila njia kuwagombanisha Waislamu na kuwafanya kila mmoja wao amuone mwenzake ni adui yake.

Juu ya ukurasa

Mambo Yanayozusha Mifarakano

Shirki

Fikra zenye uchafu wa shirki zilikuwa pia zikiwagawanya watu. Watu katika jamii ambayo imejengeka juu ya misingi ya shirki hukumbwa na ubaguzi na kila mmoja huwa ni mgeni kwa mwenzake. Wakati katika jamii iliyochafuliwa kwa fikra za shirki inapotokezea fikra ya uhusiano wa wanaadamu na chanzo cha ulimwengu na nguvu isiyoshindika na inayodhibiti kila kitu ulimwenguni (yaani Mwenyezi Mungu), huwa pia ni jambo la kawaida kushuhudiwa watu wakitengana katika jamii hiyo, huyu akiwa anamwamini Mwenyezi Mungu Mmoja, mwengine akiwa na imani ya mungu mwingine na mwengine vivyo hivyo. Katika jamii iliyojengeka juu ya misingi ya shirki, watu wa matabaka na makabila mbali mbali ndani ya jamii hiyo hutenganishwa kwa ukuta usioweza kuvunjika na kwa shimo ambalo huwa linazuia kikamilifu kupatikana mfungamano na umoja baina ya watu wa jamii hiyo.

Juu ya ukurasa

Shetani

Kila mahala ambapo pana hitilafu baina ya waumini na baina ya waja wema wa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka yoyote mahala hapo huwa pana shetani na adui wa Mwenyezi Mungu. Popote mtakapoona pana hitilafu, basi jaribuni kuchunguza na hamtasumbuka hata kidogo kumuona shetani katika sehemu hiyo. Ima shetani atakuwa ameingia ndani ya nafsi zetu wenyewe ambazo zinajulikana kwa jina la nafsi zinazoamrisha maovu na ambazo kwa kweli ni mashetani wabaya na hatari kabisa dhidi yetu. Hivyo nyuma ya pazia la hitilafu zote, kuna watu kujiona au kupenda jaha na cheo au kedi na ukaidi wa watu au mashetani wa nchi yaani mikono ya adui na ubeberu na madola dhalimu ya ukandamizaji.

Juu ya ukurasa

Ujinga na Kuelewa Vibaya

Kama mnauona umma wa Kiislamu umekumbwa na mifarakano basi jueni kuwa Waislamu hawajui vizuri maana ya umoja na mshikamano uliomo katika dini yao. Leo hii ni zama ambazo umma wa Kiislamu iwe ni watu muhimu kisiasa au kiutamaduni au kidini au iwe ni matabaka mbali mbali ya wananchi wa kawaida wa umma wa Kiislamu, kila mmoja anapaswa kuwa macho sana kuliko wakati mwingi wowote. Kila mmoja wetu anapaswa kuzijua vizuri hila za adui na anapaswa kupambana nazo vilivyo. Moja ya hila zinazotumiwa sana na adui ni kupalilia moto wa hitilafu. Maadui wanafanya kila njia; wanatumia pesa nyingi, wanafanya juhudi zao zote bila kufumbia macho fursa yoyote wanayoipata yote hayo ikiwa ni kutaka kuhakikisha kuwa Waislamu wanashughulishwa tu na hitilafu zisizoisha baina yao ili kwa mara nyingine maadui hao waweze kutumia mghafala, ufahamu mbaya na potofu na taasubu ili kutugombanisha.

Katika baadhi ya madhehebu ya Kiislamu leo hii kunashuhudiwa baadhi ya watu wenye mitazamo finyu. Watu hao wanajiona wao tu ndio wenye haki na waliobakia wote katika ulimwengu wa Kiislamu wanawaona ni makafiri. Sasa kitu cha kuuliza hapa ni kwamba hivi kila mtu anayetangaza hadharani mapenzi yake makubwa kwa Bwana Mtume huyo ni kafiri?! Je, kila mtu anayesoma Maulidi na kusherehekea siku aliyozaliwa Mtume Muhammad SWA huyo ni kafiri kwa watu hao wenye mitazamo finyu?! Sisi tunafurahi sana kuona Alhamdulillah, baada ya kuepuka hitilafu hizo tunaweza sasa kuwanyooshea mikono ya udugu na urafiki Waislamu wenzetu wote.

Juu ya ukurasa

Taasubu za Kikabila

Baadhi ya wakati unaona katika mataifa ya Waislamu watu wanayapa umuhimu zaidi masuala ya ukabila, utaifa, lugha, damu na vitu kama hivyo kuliko masuala ya kimsingi ya Uislamu. Bila ya shaka yoyote mambo hayo hayaashirii kitu kingine ghairi ya kutengana baadhi ya watu wa umma wa Kiislamu na Waislamu wengine. Wenyewe tumeshuhudia jinsi suala la taasubu za kuchupa mipaka za Ufarsi, Uirani na kurejea kwenye fikra na ngano ghalati zinazohusiana na kizazi, nasaba na damu lilivyoleta madhara makubwa katika kipindi cha tawala za huko nyuma nchini Iran. Mtu unajiuliza fikra hizo zilikuwa na maana gani? Fikra hizo ziliiletea faida gani Iran? Kwa kweli hazikuleta faida yoyote isipokuwa madhara tu. Madhara makubwa zaidi yalikuwa ni kutengana taifa la Iran na mataifa mengine ya Kiislamu na hali ikawa mbaya kiasi kwamba zilizuka chuki na mizozo baina ya taifa la Iran na mataifa mengine ya Kiislamu. Maadui walihakikisha hali hiyo inayakumba pia mataifa ya Kiarabu. Maadui hao hawakuishia hapo bali walihakikisha pia hali kama hiyo inashuhudiwa baina ya kabila na kabila na hadi leo wanaendelea na njama zao hizo.

Juu ya ukurasa

Watu Wenye Madaraka

Hitilafu, mivutano, mizozo, ugomvi na kukwamishana kumekuwepo tangu karne nyuma hadi hivi sasa kati ya mataifa na makundi mbali mbali ya Waislamu na siku zote mambo hayo yamekuwa na madhara makubwa kwa Waislamu. Historia ya ulimwengu wa Kiislamu inaonyesha kuwa, chanzo na asili au tuseme sehemu kubwa ya ugomvi na mivutano hiyo inatokana na tawala za wapenda mambo ya kimaada na ya dunia. Hitilafu hizo zinazoanzia kwenye mambo ya awali yaani suala la Qur’ani na mfano wake hadi kwenye hitilafu nyinginezo ambazo zimekuwa zikishuhudiwa wakati wote kati ya makundi ya Kiislamu na hususan baina ya Waislamu wa Kisuni na Kishia takriban chanzo chake hitilafu hizo zilizozikumba nchi zote za Kiislamu ni tawala za nchi hizo. Tab’an kuna na vitu vingine vinachangia katika hitilafu hizo kama vile ujinga na kutojua, taasubu zisizo na mashiko ya mantiki, uchochezi n.k, lakini yote hayo ni mambo madogo madogo tu na hakuna lolote lililoleta maafa makubwa ya umwagaji wa damu katika historia. Maafa makubwa ya umwagaji wa damu yaliyoshuhudiwa katika historia chanzo chake ni mabwana wakubwa ambao ni manufaa yao kuweko hitilafu na ugomvi kama huo unaopelekea hata umwagaji mkubwa wa damu. Wakati madola ya kikoloni yalipozivamia nchi za Kiislamu – baadhi yao moja kwa moja na baadhi yao kwa njia isiyo ya moja kwa moja – ilidhihirika wazi kwamba madola hayo nayo yalikuwa yanatafuta suala hilo hilo la kushadidisha ugomvi usioisha baina ya Waislamu ili yaweze kuzidhibiti nchi za Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Makundi Yanayoeneza Mifarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu

Duniani leo pesa zinatumika kwa ajili ya kujenga msikiti wa madhara (Masjidudh Dharara ambao ulijengwa na maadui kwa ajili ya kuzusha fitna na mifarakano kati ya Waislamu. Mwenyezi Mungu akamtumia wahyi Mtume Wake kumjulisha njama hizo na kumuamrisha asiingie wala asisali katika msikiti huo bali uvunjwe kabisa na hivyo ndivyo ilivyojiri). Sasa hivi pesa nyingi zinatumika kwa ajili ya kuandaa makundi, kuanzisha vituo mbali mbali hata vya kijeshi kwa lengo la kuutia pigo umoja na mshikamano wa Kiislamu na kuzusha ugomvi na mapigano kati ya makundi ya Kiislamu. Vitendo vya watu hao ni mithili ya vitendo vya ibilisi na shetani ambaye kwa kiburi kikubwa alimwambia Mwenyezi Mungu Muumba wa ulimwengu akisema:

…وَلَاُغْوِينَّهُمْ أَجْمَعينَ…

…Na nitawapoteza (wanaadamu) wote… (al Hijr; 15:39).

Na hivyo ndivyo anavyofanya shetani, kuwazaini, kuwaghilibu na kuwapoteza waja wa Mwenyezi Mungu. Hawa nao wamejipanga na kujizatiti vilivyo kwa ajili ya kuzusha hitilafu.

Kwa kweli dhihirisho la mwamko wa Kiislamu si wale watu ambao leo hii wanaonyesha sura ya ugaidi katika ulimwengu wa Kiislamu. Watu ambao wanafanya jinai zote hizi huko Iraq, watu ambao katika ulimwengu wa Kiislamu wanafanya maovu mbali mbali kwa jina la Uislamu dhidi ya Waislamu, watu ambao kazi yao kuu ni kuzusha hitilafu baina ya Waislamu kwa madai ya Usuni na Ushia, kwa madai ya ukabila; kwa vyovyote vile haiwezekani kuwaita watu hao kuwa ni dhihirisho la mwamko na nembo ya Uislamu, na hilo hata mabeberu wenyewe wanalijua vyema. Hao hao watu ambao wanaionesha sura ya Uislamu kuwa ni dini isiyo na uvumilivu wala isiyopenda maendeleo huko Magharibi, wenyewe wanajua vyema kwamba uhakika wa Uislamu ni tofauti na hivyo wanavyoupigia propaganda wao.

Leo hii mikono ya kueneza fitna katika ulimwengu wa Kiislamu inafanya njama za kuchafua sura ya madhehebu ya Ahlul Bayt tena kwa namna ambayo ni tofauti kabisa na uhakika wa madhehebu hayo. Leo hii kuna maulamaa wengi wa Kifalme na vibaraka wa madola makubwa katika nchi mbali mbali ambao wanafikia hadi ya kuwaita Waislamu wa Kishia kuwa ni makafiri. Leo hitilafu baina ya Waislamu wa Kisuni na Kishia ndiyo shabaha ya Marekani, ndiyo shabaha ya mabeberu wa dunia na ndilo lengo la tawala vibaraka wa madola makubwa.

Juu ya ukurasa

Baadhi ya Tawala za Nchi za Kiislamu

Mtu unajiuliza vyanzo vyote hivi vya maliasili, utajiri wote huu, silaha zote hizi zinazomilikiwa na nchi za Kiislamu na mataifa ya Kiislamu kwa nini hazitufanyi kuwa na nguvu na kutufanya tuweze kujilinda? Sababu yake ni kuwa hakuna umoja baina yetu. Sasa kwa nini hatuna umoja? Kwa sababu tawala za nchi za Kiislamu ambazo inabidi zidhamini umoja huo, kila moja ina malengo yake tofauti. Baadhi ya tawala hizo zina malengo ya utaifa, baadhi yao zimeathiriwa na fikra za kukufurisha wenzao na baadhi yao hazina malengo kabisa ya Kiislamu. Hata hivyo wananchi wenyewe wa mataifa ya Kiislamu nyoyo zao ni moja. Huwezi kushuhudia wananchi wa mataifa mawili ya Kiislamu wakiwa na ugomvi baina yao. Baada ya mataifa mawili ya Iran na Iraq kushuhudia vita vya miaka minane, sasa hivi mataifa hayo mawili yanaishi salama kwa pamoja na yanapendana. Vita huwa havitokani na wananchi, hitilafu haziwahusu wananchi, bali zinatokana na tawala ambazo zina malengo yasiyo ya Kiislamu. Hapa ndipo panapopasa kutibiwa.

Juu ya ukurasa

Wanachuoni na Maulamaa wa Kiislamu Kutojali Maslahi ya Waislamu

Uhakika wa mambo ni kuwa, wamewaweka Waislamu wa Kisuni na Kishia katika hali ya kuzozana kwa muda wa miaka elfu sasa, kiasi kwamba kila upande uko dhidi ya upande wa pili, wanayavunjia heshima matukufu ya upande wa pili na kwa vile tayari kuna mazingira ya kuweza kushadidi hitilafu baina ya matabaka mbali mbali ya Waislamu wawe wa Kisuni au wa Kishia, adui anatumia fursa hiyo kwa ajili ya kushadidisha hitilafu na kuzifanya kubwa kati ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe kama ambavyo tunawaona katika baadhi ya nchi za Kiislamu wanavyomshawishi mtu fulani wa Kishia aseme maneno yatakayochochea hisia za Waislamu wa Kisuni na hapo hapo atokezee msomi mmoja wa Kisuni naye ashawishiwe kusema maneno mabaya dhidi ya Waislamu wa Kishia, alimradi inasikitisha sana kuona hali hiyo inaendelea kuwepo katika nchi za Kiislamu. Sasa laiti kama maulamaa wa Kiislamu wangelitekeleza vizuri majukumu yao katika uwanja huo na wasitosheke na kusema tu umeshawabainikia uhakika wa itakadi yao fulani, hivyo hawawajibiki kufanya kitu kingine. Pia wasitosheke na kusema kwamba tayari tuna uhusiano mzuri na maulamaa wenzetu wa Kishia au Kisuni hivyo hilo linatosha. Hapana inabidi udugu huo wa Kiislamu upaliliwe na ustawishwe katika pembe zote ili ifike wakati wawaambie maadui kwamba hata mkifanya njama za kuzusha ugomvi kati ya Waislamu basi njama zao hizo hazitaathiri chochote na hazitakuwa na athari yoyote mbaya kwa Waislamu kwani matabaka mbali mbali ya wananchi watazibatilisha tu.

Juu ya ukurasa

Watu Vibaraka na Wenye Ushawishi katika Umma wa Kiislamu

Inasikitisha kuona kuwa katika ulimwengu wa Kiislamu kuna watu wako tayari kufanya uovu wowote ule ili tu wajikurubishe na wajipendekeze kwa Marekani na vituo vya madola ya kibeberu. Wako tayari kuzusha ugomvi na hitilafu kati ya Waislamu kama wa Kishia na Kisuni ili wawafurahishe mabeberu. Leo hii mimi ninaona mikono katika baadhi ya nchi jirani na Iran ambayo yanafanya kwa makusudi hila zilizopangiliwa vizuri ili kuzusha hitilafu baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni na wanachochea hisia za ukabila na umadhehebu ili kuwagombanisha watu na kuzusha kitali baina ya mirengo mbali mbali ya kisiasa, yote hayo kwa ajili ya kuwaridhisha mabeberu. Inabidi tuwe macho. Watu wa matabaka mbali mbali, tawala, Waislamu wote, mirengo mbali mbali ya kisiasa, wasomi na watu muhimu katika jamii, wote wanapaswa kuwa macho mbele ya njama na hila za adui na wasiruhusu adui kuzusha hitilafu na ugomvi baina yao kwa visingizio vyake tofauti.

Juu ya ukurasa

Madhehebu Bandia na ya Kupandikiza

Maulamaa wa Kiislamu wanapaswa wajihadhari sana. Wachukue tahadhari mbele ya madhehebu haya bandia na ya kupandikiza ambayo lengo lake ni kuvuruga umoja kati ya Waislamu. Wawe makini sana mbele ya dola hizi za mafuta zinazotumika kwa ajili ya kuzusha mizozo na mifarakano. Wajihadhari na mikono hii michafu ya vibaraka wanaolenga kuvuruga umoja wa Kislamu na kuivunja «عُرْوَة الْوُثْقي» (kishiko madhubuti ambapo Mwenyezi Mungu anasema katika sehemu moja ya aya ya 256 ya Sura ya Pili al Baqarah kwamba: “Basi anayemkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisichovunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua). Pambaneni na watu wa aina hiyo wasiopenda umoja na mshikamano kati ya Waislamu. Kupambana na mikono hiyo kutawezekana tu kama Waislamu tutashikamana na umoja na kufuata njia ya kutuunganisha. Bila ya kufanya hivyo hakuna mafanikio yoyote tutakayopata.

Bila ya shaka njia za muda mrefu za hitilafu na mivutano ambazo zimekuwepo kwa miaka mia moja, au mia mbili au mia tano huweza kuleta dini ya kikoloni ili kuutia jeraha kubwa mwili wa ulimwengu wa Kiislamu jeraha ambalo kutibiwa kwake huwa si jambo rahisi. Mfano wake ni kama makundi ya Kiwahabi na madhehebu na dini nyinginezo za kupandikiza ambazo ndizo zinazoleta na kushadidisha mifarakano katika ulimwengu wa Kiislamu.

Tangu mwanzo Uwahabi ulizuka kwa lengo la kuutia pigo umoja wa Kiislamu na kuzusha kambi mithili ya Israel katika jamii ya Waislamu. Kama ambavyo wameipandikiza Israel ili kupambana na Uislamu, wameleta pia serikali ya Kiwahabi na watawala hawa wa Najd ili waweze kupata kituo cha usalama ndani ya jamii ya Kiislamu ambacho kitakuwa ni tegemezi kwao na hivyo ndivyo tunavyoshuhudia.

Juu ya ukurasa

Kuvunjiwa Heshima Matukufu ya Kiislamu

Kwa mtazamo wa Uislamu, kuyavunjia heshima matukufu ya upande huu na ule ni mstari mwekundu. Watu ambao kwa kutojua kwao au kutokana na kukumbwa na mghafala, wanashuhudiwa baadhi ya wakati wakitumia taasubu pofu na zisizo na maana kuvunjia heshima matukufu ya wenzao iwe ni Masuni au Mashia, hawajui wanachokifanya. Watu wa aina hiyo ni silaha nzuri mno anayoweza kuwa nayo adui.

Masuni na Mashia kila mmoja ana maadhimisho yake ya kimadhehebu wana mila zao maalumu, wana desturi zao mahsusi. Wanatekeleza majukumu yao ya kidini na lazima watekeleze lakini wajue kuwa kuna mstari mwekundu. Mstari huo mwekundu ni kuwa hawapaswi hata kidogo kuruhusu kuvunjiana heshima matukufu yao. Haijalishi ni nani anayefanya hivyo, iwe ni baadhi ya watu waliokumbwa na mghafala kati ya Waislamu wa Kishia, au watu waliokumbwa na ugonjwa huo kati na Waislamu wa Kisuni ambao kila mmoja anamkanusha mwenzake, hili halipaswi kuruhusiwa kuendelea. Kwani hilo ndicho kitu ambacho adui anataka kukiona kinadumu na kinaendelea. Watu hao nao wanapaswa kuwa macho na wajihadhari na vitendo vyao.

Juu ya ukurasa

Kupaliliwa Hitilafu za Kikabila

Hitilafu za kikabila na utaifa zinazotokana na hisia za kuchupa mipaka za utaifa, mara nyingi hupaliliwa na wasomi vibaraka.

Kikawaida kuna baadhi ya mambo yako dhidi ya umoja – tofauti wa kikabila, tofauti za kimadhehebu na koo, tofauti za kisiasa – mambo ambayo inabidi Waislamu wakabiliane nayo vilivyo. Maadui wanatumia mambo hayo kwa ajili ya kushadidisha hitilafu baina ya Uislamu na hizo ndizo siasa za kila siku za maadui. Mkono wa adui, njama za adui, mipango ya adui inaweza kutekelezeka tu kwenye mgongo wa tofauti kama hizo. Ugonjwa huu lazima utibiwe. Watu wenye busara katika umma wa Kiislamu kutoka makundi yote hawapaswi kuruhusu kuenea mawimbi ya fitna kati ya Waislamu mawimbi ambayo yanachochewa kila leo na maadui wa Uislamu. Watu wenye hekima katika umma wa Kiislamu inabidi wafanye juhudi zao zote kuhakikisha kuwa mapenzi, udugu na mshikamano baina ya Waislamu hauhatarishwi na maadui wa dini hiyo ya Mwenyezi Mungu.

Juu ya ukurasa

Hatari za Utengano Katika Umma wa Kiislamu

Tamaa ya Maadui wa Uislamu

Leo hii hatari kubwa zaidi inayoukabili ulimwengu wa Kiislamu ni mifarakano. Wakati tutakapokuwa tumetengana na kufarikiana, ndipo adui anapoingia tamaa ya kutuvamia. Pendekezo letu sisi kwa tawala na serikali zote katika ulimwengu wa Kiislamu, kwa matabaka yote ya wananchi katika mataifa ya Kiislamu, ni umoja, mshikamano na kukurubiana kiudugu na kimapenzi. Inabidi kufumbia macho tofauti zilizopo na kutozipa umuhimu. Kuna baadhi ya hitilafu zinaweza kutatuliwa, hivyo tukae pamoja na kuzitatua. Kuna baadhi ya hitilafu haziwezi kutatuliwa katika kipindi cha muda mfupi, hizo inabidi tuzifumbie macho na kutozipa uzito. Kitu hicho ndicho hasa kinachoweza kuwatia hasara Wazayuni na Wamarekani na ndio maana wanafanya njama zao zote kupambana na fikra hiyo.

Juu ya ukurasa

Kukandamizwa Umma wa Kiislamu

Kama leo tunashuhudia taifa la Palestina limekumbwa na masaibu yote haya, kama tunaona leo hii mwili wa taifa la Palestina unachururika damu na tabu na mashaka yanayolikabili taifa hilo yanazichoma nyoyo za watu wenye ubinaadamu duniani, tujue kuwa hayo yote yanatokana na kutokuweko kauli moja kati ya Waislamu. Laiti kama kungelikuwa na msimamo mmoja kati ya Waislamu, basi hali hiyo isingelitokea. Kama leo nchi za Kiislamu ya Iraq imeingia kwenye makucha ya mataifa ya kibeberu ni kutokana na kuwa hakuna umoja kati ya Waislamu. Kama leo hii tunaziona nchi za Mashariki ya Kati zinatishiwa kijeuri na kujiba na Marekani, tujue kuwa ni kutokana na hitilafu zilizopo baina ya Waislamu.

Juu ya ukurasa

Kutetereshwa na Kusalitiwa Uislamu na Waislamu

Kama kuna mtu anatetereshwa na kuogopeshwa na madola yenye nguvu duniani, basi ajue kuwa mtu huo anahisi yuko peke yake na hakuna mtu wa kumsaidia. Kama tunaona kuna tawala na mataifa yana woga, tujue kuwa hiyo ndiyo sababu yake na kama watu nao wanaonekana kuogopa kusema chochote mbele ya maadui chanzo cha kuogopa kwao huko ni hayo tuliyotangulia kusema. Lakini kama mataifa na tawala za nchi za Kiislamu zitapendana na kuishi kwa kusaidiana, na kama tawala hizo zitaona kwamba wananchi wao wako pamoja nao wamesimama kidete kuzitetea na kama wananchi nao wataona serikali zao zimeazimika kweli kweli kulinda na kutetea haki zao, na kama mataifa hayo yataona kweli kwamba kuna mataifa mengine yako pamoja nao, yana misimamo na kauli moja nao, wakati huo hakuna atakayekuwa na woga juu ya mabeberu na mabeberu hao hawataweza tena kuwateteresha na kuingiza hofu katika nyoyo za viongozi wa nchi za Kiislamu. Madhara makubwa kabisa ya mifarakano ni kwamba humvunja nguvu mwanaadamu. Mwenyezi Mungu anasema: Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri. (al Anfal; 8:46). Naam, mizozo huwapokonya watu na taifa; hamasa na uchangamfu wake na hulipotozea nguvu zake.

Juu ya ukurasa

Kutomjua na Kumdharau Adui wa Kweli

Leo hii ni siku ya kuungana na kushikamana ulimwengu wa Kiislamu. Adui amewekeza kiasi kikubwa mno cha fedha kwa ajili ya kuuvunja hata huu umoja dhaifu uliopo leo baina ya Waislamu. Nchi ya Iraq na maeneo mengine ya Kiislamu nayo kwa namna fulani zimekumbwa na njama hizo. Maadui wanafanya hayo ili wazushe ugomvi kati ya makabila mbali mbali ya Waislamu, kati ya makundi ya Kiislamu, kati ya koo za Waislamu, kati ya mataifa ya Kiislamu kwa kutumia visingizo mbali mbali na kupelekea hawa wawaue wale na wale wawauwe hawa, hawa wawachukie wale na wale wawe na chuki na hawa, Waislamu wachukiane wao kwa wao. Yote hayo wanayafanya ili kuwafanya Waislamu washughulishwe na mambo mengine na wamsahau adui mkuu wa ulimwengu wa Kiislamu ambao ni wale watu na madola ambayo yanataka kulidhibiti kikamilifu eneo hili nyeti la Mashariki ya Kati.

Kama wapenzi wa Qur’ani na Uislamu – kutoka madhehebu na kundi lolote lile – watakuwa wanasema kweli, na kama kweli wana uchungu na wanataka kuona Qur’ani na mafundisho yake yanatekelezwa inavyotakiwa, basi wanapaswa kujua kwamba makelele yote haya na kalamu zote hizi za vitimbakwiri na fedha zote hizi chafu na khabithi ambazo zinatumika katika baadhi ya nchi kwa ajili ya kuzusha hitilafu, ndizo zinazokwamisha kupata hadhi yake Uislamu na hiyo ni kazi inayofanywa na adui.

Juu ya ukurasa

Njia za Kuleta na Kukuza Umoja

Njia za Kuleta na Kukuza Umoja

Umoja una hatua mbili; na hatua yake ya kwanza ni hatua ya maneno na matamshi. Hatua hii ya kusema na kutamka kwa maneno ni rahisi na haina tatizo lolote. Ijapokuwa kuna baadhi ya watu hawako tayari hata kufanya jambo hilo jepesi, na ijapokuwa kuna watu wanawakufurisha wazi wazi Waislamu wenzao, na hata kama kuna watu hawako tayari hata kutamka kwa maneno tu masuala yanayohusiana na umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu, lakini pamoja na yote hayo, bado ukweli utabakia vile vile kwamba hatua hiyo ni rahisi na haina matatizo yoyote. Hatua ya pili ni kufanyia kazi mambo ya kuleta umoja na kwa hakika jambo hilo linataka juhudi kubwa sana. Ni kazi nzito lakini ni kazi ya wajibu. Kuna mambo mengi ambayo kimsingi yanataka kuharibu na kuvuruga umoja baina ya Waislamu na inabidi tuseme kwa masikitiko makubwa kwamba, kunatumika fedha nyingi sana za kuyatia nguvu mambo hayo, na zinatumika dola nyingi za mafuta ili kueneza mambo hayo ya kuwafarakanisha Waislamu. Alaakullihaal, kwa vile jambo hilo la kuleta umoja na mshikamano kivitendo ni la wajibu na lina udharura mkubwa hususan katika kipindi na zama tulizo nazo hivi sasa, inabidi kuvumilia mashaka yote katika njia ya kuufanikisha wajibu huo.

Juu ya ukurasa

Njia za Utatuzi wa Kiutamaduni

Kuchora Vipengee vya Shakshia ya Mtume Mtukufu (SAW)

Waislamu duniani wanaweza kuungana kirahisi na kiwepesi zaidi kuliko kitu kingine chochote chini ya jina la Mtuma Muhammad (Rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake). Hiyo ni miongoni mwa sifa maalumu za mtukufu huyo. Mimi nimesema mara nyingi kwamba Bwana Mtume ni makutano ya mapenzi na hisia za Waislamu wote. Waislamu wote wanampenda sana Bwana Mtume. Ewe Mola wetu! Wewe ni Shahidi kwamba nyoyo zetu zimejaa kiwango kisicho na mfano cha mapenzi kwa Bwana Mtume. Inabidi mapenzi hayo yatumike vizuri. Inabidi mapenzi hayo yawe ni njia ya utatuzi.

Maulamaa wa Kiislamu, wasomi wa Kiislamu, waandishi, malenga na watungaji wa tungo, wasanii katika ulimwengu wa Kiislamu, leo hii wana jukumu la kuhakikisha kuwa, wanamtangaza vizuri Bwana Mtume Muhammad SAW kwa kadiri ya uwezo wao na kuwabainishia Waislamu na wasio Waislamu uadhama wa sifa tukufu za mbora huyo wa viumbe. Jambo hilo bila ya shaka yoyote litasaidia katika juhudi za kuleta umoja katika umma wa Kiislamu na kuongeza kasi ya kuvutika zaidi kizazi cha vijana wa umma wa Kiislamu katika upande wa kutekeleza na kuheshimu vilivyo mafundisho ya dini yao.

Kama maulamaa wa Kiislamu wanaamini kwamba Qur’ani imesema: Na hatukumtuma Mtume yeyote yule ila atiiwe kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (an Nisaa; 4:64), kama wanakubali kuwa Bwana Mtume Muhammad SAW hakuja kutoa nasaha tu na kuamrisha mambo halafu watu wasimtii na wala wasimuheshimu basi wajue kuwa Mtume amekuja ili atiiwe na aongoze jamii na maisha ya mwanaadamu, aunde serikali na mfumo wa utawala na kuwaongoza watu katika malengo matukufu ya kuumbwa kwao. Hivyo maulamaa wana jukumu kubwa la kumtangaza inavyopasa mbora wa shani na mtukufu huyo wa daraja.

Juu ya ukurasa

Kuwa Makini Mbele ya Adui

Qur’ani tukufu inatufundisha ikisema: “Enyi Waislamu mlio na nyoyo zilizoamka, kamwe msimsahau adui yenu. Msisahau kuwa mna adui. Msisahau kwamba adui anakuvizieni. Msisahau kuwa kama mtatetereka na kama mtaonyesha udhaifu, basi adui atakushambulieni.” Adui ameamua kutumia njia zote katika mashambulizi yake: njia za kiuchumi, njia za kiutamaduni, njia za kisiasa na njia za kiusalama. Mataifa ya Kiislamu inabidi yaamke. Mwenyezi Mungu anasema:

 «ألَمْ أَعْهَدْ إِلَيکمْ يا بَني‏ آدَمَ أَنْ لا تَعْبُدُوا الشَّيطانَ إِنَّهُ لَکمْ عَدُوٌّ مُبينٌ»

Je! Sikuagana nanyi, enyi wana wa Adamu, kuwa msimwabudu shetani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu. (Yaasin; 36:60).

Msisalimu amri mbele ya adui, msighafilike na adui na daima kaeni mkijua kuwa mna adui. Pamoja na sisitizo lote hilo, lakini Mwenyezi Mungu anasema kuhusiana na shetani huyo kwamba:

 «إِنَّ کيدَ الشَّيطانِ کانَ ضَعيفاً»

Hakika hila za shetani ni dhaifu (an Nisaa; 4:76).

Mwenyezi Mungu anatufundisha kuwa, shetani huyu huyu ambaye inabidi kuwa macho naye na kama hamtakuwa macho naye basi mtashitukia ametuvamieni na kukushambulieni, na licha ya kuwa Mwenyezi Mungu anasisitiza kwamba mtekeleze wajibu wenu, lakini vitimbi na hila za shetani huyo ni dhaifu sana na haviwezi kufanya lolote. Mwenyezi Mungu anasema:

 «إِنَّما سُلْطانُهُ عَلَي الَّذينَ يتَوَلّوْنَهُ»

Hakika madaraka yake (shetani) ni juu ya wanaomfanya rafiki yao, na wale wanaofanya ushirika naye. (an Nahl; 16:100).

Nguvu za shetani zinakuwa juu ya wale watu tu wanaomuogopa, juu ya wale watu ambao tu wanamtegemea na wale wenye urafiki naye. Lakini mtu ambaye anamtegemea Mwenyezi Mungu na kutawakali kwake, basi inabidi shetani amuogope yeye na sio yeye amuogope shetani.

Juu ya ukurasa

Umuhimu wa Maulamaa Kuwa na Kauli Moja

Katika upande wa kifikihi pia inabidi kuwe na mabadilishano ya mawazo baina ya madhehebu tofauti kwani kufanya hivyo kunaweza kuyaunganisha madhehebu hayo katika milango mengi sana ya kifikihi, kutazikurubisha fatwa za wanavyuoni bali hata kuzifanya kuwa za namna moja. Baadhi ya makundi ya Kiislamu yamefanyia utafiti mkubwa sana baadhi ya milango ya kifikihi na kuzama sana katika milango hiyo, Waislamu wengine wanaweza kupata faida kubwa sana kutokana na utafiti wa Waislamu wenzao hao. Baadhi ya wakati kuna uwezekano kukawa kuna nukta mpya zimevumbuliwa na baadhi ya makundi ya Kiislamu katika baadhi ya hukumu na fatwa za Kiislamu kutoka katika Kitabu na Sunna, kama utakuweko ubadilishanaji mawazo baina ya makundi ya Kiislamu, uvumbuzi wa Waislamu hao unaweza kuwafaidisha sana Waislamu wengine na kuzifanya fatwa za Waislamu zikurubiane na ziwe moja. Huwa tunashuhudia baadhi ya wakati kunaripotiwa habari kuhusu fatwa za madhehebu fulani, fatwa za ajabu ambazo ni ngeni kwa madhehebu hayo. Kuna uwezekano wafuasi wa madhehebu hayo wasiwe na haja ya kuwa na fatwa kama hizo au ikawa hawazipi umuhimu. Sasa kwa nini basi sisi Waislamu – wanavyuoni wa Kiislamu – hawakai pamoja na kuibuka na fatwa zinazofanana?

Juu ya ukurasa

Umuhimu wa Maulamaa Kuwa na Muono Mpana

Maulamaa wa Kiislamu wanapaswa kuonyesha kivitendo mfano wa umoja wa Kiislamu na wakae pamoja na kuandaa hati ambayo itaungwa mkono na kuthibitishwa na maulamaa wote na wasomi wote katika ulimwengu wa Kiislamu na watu muhimu kisiasa wenye ikhlasi na sauti katika ulimwengu wa Kiislamu na baadaye wahakikishe kwamba vipengee vya hati hiyo vinatekelezwa kivitendo ili asije akatokezea Muislamu yeyote atakayethubutu kumkufurisha Muislamu mwenzake na mtu anayetamka neno la tawhidi hata kama madhehebu yao yanatofautiana.

Ndugu wa Kiislamu iwe ni nchini Iran, au nchini Iraq, au nchini Pakistan, au nchini Lebanon, au huko Palestina, au katika maeneo yoyote mengine duniani, pamoja na kutofautiana madhehebu yao lakini wote wanajua kwamba mtazamo wa maulamaa wa kweli wa Kiislamu ni kwamba, “Kuchafua mikono kwa damu ya Mwislamu mwenzako, ni miongoni mwa madhambi makubwa yasiyoweza kusamehewa.” Watu ambao wanachafua mikono yao kwa damu za ndugu zao Waislamu kwa jina la kufuata Uislamu! Kwa jina la kushikamana na Uislamu! Kwa kweli vitendo vya watu hao ni kutoka katika Uislamu. Inabidi watu wote wajue kwamba udugu uliopo baina ya taifa la Iran na mataifa mengine ya Kiislamu ni udugu wa kweli kabisa. Tofauti za kimadhehebu zitaendelea kuwepo, Mshia ataendelea kuwa Mshia na Msuni ataendelea kuwa Msuni, hata kati ya Waislamu wenyewe wa Kisuni na Waislamu wenyewe wa Kishia kuna tofauti za mitazamo baina ya wao kwa wao kabla ya kuweko tofauti za mitazamo baina ya madhehebu yao, lakini wote hao wanapaswa kdumisha udugu baina yao chini ya bendera ya «لا‌اله‌الاّاللَّه‌و‌محمّد‌رسول‌اللَّه» (Hakuna Mwenyezi Mungu wa kweli ila Allah na Muhammad ni Mtume wa Allah). Waislamu wanapaswa kudumisha umoja baina yao na kukabiliana kwa pamoja na maadui wa Uislamu na ili waweze kusimama kidete mbele ya maadui wa umma wa Kiislamu.

Juu ya ukurasa

Kutoyapa Nguvu Masuala ya Hitilafu

Kaulimbiu na shaari ya Uislamu wa asili ambao ndio uliojenga msingi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran maana yake ni kuwa, licha ya kuweko tofauti za kiakida na misingi ya kimadhehebu baina ya Waislamu, lakini Waislamu hao wanapaswa kuwa na kauli moja na washikamane katika masuala yanayowaunganisha na wajiepushe kutonesha hisia za Waislamu wenzao. Utamaduni huu wa kidini wenye maana hii, wenye mtazamo huu, yaani uhuru, uadilifu, demokrasia na kuleta umoja katika ulimwengu wa Kiislamu na katika umma wa Kiislamu ni miongoni mwa medani zetu za jihadi na inabidi tufanye jitihada kubwa kuhakikisha kuwa kaulimbiu na shaari hizo zinafanikiwa.

Waislamu Kishia na Kisuni ambao kimsingi ni ndugu wanapaswa kuweka pembeni tofauti zao. Wasioneshe hitilafu zao katika jamii ya kimataifa na mbele ya walimwengu. Wadhihirishe umoja baina yao na waonyeshe mshikamano katika umma wa Kiislamu. Watu ambao wanafanya kazi ya tablighi wanapaswa kuhakikisha kuwa kazi yao hiyo wanaifanya kwa ufanisi wa hali ya juu, watumie lugha madhubuti ya kimantiki ili kwa njia hiyo waweze kuzivutia nyoyo za watu katika haki na uhakika.

Popote mtakapokuwa na mkamwona mzungumzaji, mtoa hotuba, gazeti na mwandishi wa makala anatumia maneno yake na anatumia ufasaha wake wa maneno kwa ajili ya kuwatia woga na wasiwasi watu ili avuruge umoja kati yao basi jueni kuwa mtu huyo anafanya makosa. Hata mkijua hivyo tu inatosha, hata si lazima mchukue hatua. Jueni kwamba watu wanaofanya mambo hayo, wanafanya makosa na wamo katika njia isiyo sawa.

Juu ya ukurasa

Njia za Utatuzi wa Kisiasa

Umoja na Mshikamano Mbele ya Adui wa Pamoja

Umoja katika umma wa Kiislamu ni miongoni mwa matumaini makubwa matukufu na kwa yakini nyoyo zote katika maeneo yote ya ulimwengu wa Kiislamu zinatweta kwa hamu ya kuona lengo hilo linafanikishwa. Hata hivyo kuna vitu vya lazima inabidi vitekelezwe kwanza kwa ajili ya kulifikia lengo hilo. Hii ni kusema kuwa kazi ya kulifikia lengo hilo ni nzito na ni kilele kilicho juu sana, na fauka ya hayo, kuna vizuizi vingi katika njia hiyo. Hata hivi leo na katika zama na siku hizi tunazoishi hivi sasa kuna mirengo mbali mbali tofauti duniani ambayo yanafanya njama za kuwagombanisha na kuwafarakanisha Waislamu. Mirengo hiyo inafanya kila njia kuhakikisha kuwa inazusha ugomvi kati ya nchi mbili za Kiislamu na kupelekea kuzuka vita kati ya nchi hizo za Kiislamu. Wakati zinaposhindwa kuzusha vita hivyo basi inazusha vita vya kisiasa au vita vya kiitikadi na kimadhehebu au chuki na uhasama wa kikabila. Tab’an kazi hiyo haifanywi na watu wa mitaani wasio na uzito wowote, bali inafanywa na vituo vyenye nguvu ambavyo ndivyo vinavyodhibiti fedha, siasa na usalama wa kimataifa. Hivyo kwa hakika juhudi za kuleta umoja baina ya Waislamu haziwezi kamwe kutenganishwa na udharura wa kufanya jitihada kubwa za kukabiliana na mawimbi hayo mazito ya mirengo isiyopenda kuona Waislamu wanashikamana.

Kufanyika kikao cha viongozi wa nchi za Kiislamu mjini Tehran ni uthibitisho wa kuweko umoja, mshikamano uongozi makini na ushirikiano wa kidugu kati ya viongozi nchini baina ya wao kwa wao na baina ya viongozi hao na wananchi. (Viongozi wa Marekani) nao wameona nguvu na uwezo wetu wa kufanya kazi kubwa, nzito na tata. Kwa kweli mabeberu wanaiona dini tukufu ya Kiislamu na mwamko wa Waislamu ni hatari kwao. Ndio maana popote wanapoona pana umoja, basi wanafanya haraka kuushambulia kwa mawimbi makubwa ya mashambulio na haijalishi Waislamu hao ni Masuni au Mashia. Mabeberu wanaiangalia Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kwa jicho lile lile wanaloiangalia harakati ya Hizbullah ya Lebanon. Mabeberu wanawaangalia kwa jicho moja Waislamu walioshikamana na mafundisho ya dini yao popote wanapokuwa ni sawa tu wawe Mashia au Masuni, hakuna tofauti kwa mabeberu hao.

Juu ya ukurasa

Njia za Utatuzi wa Kiuchumi

Kazi yoyote itakayofanyika leo kwa ajili kuzikusanya pamoja nguvu za Kiislamu kwa nia ya kuuweka umma mkubwa wa Kiislamu katika mazingira tofauti, kazi hiyo huwa ni khidma kwa Uislamu na huwa ni kuzitumikia nchi za Kiislamu na ubinaadamu kiujumla. Hali ni hiyo hiyo kwa kazi za mabenki na za wakuu wa benki kuu za nchi za Kiislamu na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu na Jopo la Huduma za Fedha.

Kama nchi za Kiislamu zitashikiana kikweli kweli, basi kushikamana kwao huo kutakuwa na faida kubwa sana. Wala sisi hatusemi kwamba lazima nchi hizo ziwe na umoja kwa maana ya siasa zinazotawala nchi zao, la, bali tunachosema sisi ni kwa nchi za Kiislamu kuwa na uhusiano wa kirafiki baina yao. Kwa mfano nchi hizo zilichukulie kwa uzito mkubwa suala la soko la pamoja na wachukue maamuzi ya kweli ya kutatua matatizo yao katika suala hilo. Wafanye juhudi za pamoja za kuondoa matatizo yaliyopo na iwapo watafanya hivyo basi watakuwa wametatua sehemu kubwa ya matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu. Kwa maneno mengine tunaweza kuwa, kama nchi za Kiislamu zitafanya hivyo, basi matatizo mengi yanayoukabili ulimwengu wa Kiislamu yatapungua ugumu, ukali na mkwamo wake.

Juu ya ukurasa

Watu wa Mstari Waliotoa Mchango Mkubwa Katika Suala Zima la Kuleta Umoja

Ayatullah Udhma Burujerdi na Sheikh Mahmoud Shaltut

 Kati ya watu muhimu na waliokuwa mstari wa mbele katika suala zima la kuleta umoja na mshikamano kati ya Waislamu walikuwa ni shakhsia wawili wakubwa ambapo mmoja ni mwanachuo mkubwa wa zama zake na marjaa wa Waislamu wote wa Kishia wakati huo naye ni Ayatullah Udhma Burujerdi. Mwingine ni mwanachuoni na mufti mkubwa wa Waislamu wa Kisuni ambaye alikuwa ni kiongozi shujaa na mwenye fikra pana katika Chuo Kikuu cha al Azhar nchini Misri Allama Sheikh Mahmoud Shaltut. Marhum Ayatullah Burujerdi ni mmoja wa waasisi na waanzilishi wa Taasisi ya Darut Taqrib ya Misri. Marhum Shaltut naye alikuwa hivyo hivyo. Alikuwa ni miongoni mwa waasisi wa taasisi hiyo ya kuyakurubisha pamoja madhehebu mbali mbali ya Kiislamu. Kazi ya kuyakurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu ni wajibu na jukumu la maulamaa wote wa Kishia na Kisuni.

 

 

 

 Miaka mingi imepita tangu wakati wa zama za Ayatullah Burujerdi (Mwenyezi Mungu awe radhi naye) na baadhi ya wanavyuoni na maulamaa wakubwa wa Kisuni wa nchini Misri. Maulamaa hao waliona kuna haja ya kuweka pembeni tofauti za kimadhehebu wakasisitiza kwamba mwache Mshia aendelee kuwa Mshia na mwache Msuni aendelee kuwa Msuni, lakini Waislamu washirikiane na wafanye kazi zao bega kwa bega. Wakati huo nia thabiti ya marjaa mkubwa wa Kishia na ushujaa na muono wa mbali wa Mufti mkubwa wa Misri ni vitu ambavyo vilitoa mchamgo mkubwa katika suala hilo na kwa hakika hatua waliyochukua ilikuwa ya mahala pake kabisa. Leo hii pia, watu wakubwa na wanafikra, maulamaa wakubwa wa Kiislamu, wasomi, mamufti na wanasiasa, wote kila mmoja wao ana jukumu kubwa katika suala hilo.

Watu wawili hao wakubwa waliubainisha uhakika huo karibu miaka khamsini iliyopita na walifanya juhudi za kuutekeleza kivitendo. Lau kama wanasiasa wangelizipa umuhimu juhudi hizo, basi pengine leo hii ulimwengu wa Kiislamu ungeliweza kushuhudia matokeo mabaya ya mizozo na mifarakano kati ya Waislamu. Na labda msiba wa Palestina usingelishuhudiwa na pengine matukio ya kusikitisha yanayoshuhudiwa leo katika ulimwengu wa Kiislamu yasingelitokea.

Juu ya ukurasa

Sayyid Jamaluddin Asad Abadi

Sayyid Jamaluddin Asad Abadi alikuwa ni shakhsia mkubwa sana ambaye historia yetu ya huko nyuma inaonyesha kuwa aliwalingania Waislamu kushikamana na kuwa kitu kimoja. Sayyid Jamaluddin alikuwa anaamini kwamba kama ulimwengu wa Kiislamu unataka kuhuisha maisha yake ya kimaanawi na kisiasa basi hauna njia nyingine isipokuwa kuungana na kushikamana. Safari za shakhsia huyo mkubwa, maneno yake, mazungumzo na hotuba zake zilikuwa zinalenga kwenye jambo hilo. Masuni wanasema Sayyid Jamaluddin Asad Abadi alikuwa ni Msuni na Mashia wanasema kwamba alikuwa ni Mshia. Hivyo madhehebu yote mawili yanamkubali na yanajivunia naye. Sayyid Jamaluddin Asad Abadi alikuwa ni Sayyid na Sharifu wa Kishia Muirani ambaye alikuwa na kauli moja na mwanachuoni, mufti na aalim mmoja wa Kishafi na sauti yao ya umoja na mshikamano ilienea ulimwengu mzima. Sayyid Jamaluddin alinyanyua juu bendera ya kuuhuisha Uislamu. Hivyo linalobainika wazi hapa ni kuwa suala la kunyanyua bendera ya kuhuisha Uislamu haina Usuni na Ushia.

Juu ya ukurasa

Imam Khomeini (MA)

 Malengo makubwa na matukufu ambayo yalikuwa yakibainishwa na Imam Khomeini (MA) yalikuwa ni kupambana na ubeberu wa kimataifa, kulindwa mlingano madhubuti katika njia ya “Si Mashariki si Magharibi” kutilia mkazo sana suala la uhuru wa kweli na wa pande zote wa taifa yaani kujitosheleza kwa maana halisi ya neno, kusisitiza sana juu ya umuhimu wa kulindwa misingi ya dini na sheria na fikihi ya Kiislamu, kuleta umoja na mshikamano, kuyapa umuhimu mataifa ya Kiislamu na yanayodhulumiwa duniani, kuupa heshima Uislamu na mataifa ya Kiislamu, kutoingiwa na hofu na kutoogopeshwa na madola makubwa duniani, kuleta uadilifu na usawa katika jamii ya Kiislamu, kuwaunga mkono bila kuchoka watu wanaonyongeshwa pamoja na matabaka dhaifu katika jamii na wajibu wa kuwashughulikia ipasavyo watu wa matabaka hayo. Sote tumeshuhudia kwamba, Imam Khomeini alishikamana na aliendelea na misingi hiyo kwa uzito wa hali ya juu pasina kuzembea hata kidogo. Ni wajibu wetu kuendeleza njia na kazi sahihi na za kudumu za Imam.

 

 

 

Juu ya ukurasa

Madhihirisho ya Umoja na Mshikamano wa Kiislamu

Kustawi Umma wa Kiislamu

Hija ni dhihirisho na nembo ya umoja na mshikamano kati ya Waislamu. Hatua ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ya kuwamrisha Waislamu wote kwa kila mwenye uwezo baina yao aende akakusanyike na Waislamu wenzake katika eneo maalumu na ashirikiane na Waislamu wenzake katika amali na harakati mbali mbali ambazo zote ni nembo ya kuishi kwa pamoja, kuwa na mpangilio mzuri na kuwa mshikamano, na kuwafanya waweze kupitisha nyakati zao za usiku na mchana wakiwa wamekusanyika pamoja; bila ya shaka yoyote lengo la jambo hilo na athari zake kuu ni kupenyeza na kutia nguvu hisia za umoja na ujamaa katika moyo wa kila Muislamu. Jambo hilo kwa kweli ni kuonyesha kustawi na kupata nguvu maisha ya kijamii ya Waislamu, ni kuonyesha udharura na haja ya Waislamu kuwa na umoja na umuhimu wa umma wa Kiislamu kuingiza hisia za utukufu wa mshikamano na umoja katika akili ya kila Muislamu.

Hija ni nembo ya umoja na mshikamano wa umma wa Kiislamu. Hija ni ibada muhimu ya kuondoa ukuta na pazia la hitilafu na kuyajaza mapengo ambayo ima yamewekwa na maadui, au yametokana na taasubu na fikra zisizoona mbali za Waislamu wenyewe. Hija inauweka umma wa Kiislamu katika njia ya umoja wa Kiislamu kupitia amali zake mbali mbali hususan ya kujibari na kujiweka mbali na maadui wa Mwenyezi Mungu, sambamba na kujibari na washirikina na mikono yote ya shirki na kufru.

Juu ya ukurasa

Wiki ya Umoja

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewaambia Waislamu duniani njooni tuujaribishe kwa pamoja umoja na mshikamano katika kipindi cha tarehe 12 hadi 17 Mfunguo Sita. Kuna hadithi moja ambayo inakubaliwa na Waislamu wengi wa Kisuni na baadhi ya Waislamu wa Kiishia inayosema Bwana Mtume Muhammad SAW alizaliwa mwezi 12 Mfunguo Sita. Kuna na riwaya nyingine inayosema kuwa mtukufu huyo wa daraja alizaliwa mwezi 17 Mfunguo Sita ambayo inakubaliwa na Waislamu wengi wa Kishia na baadhi ya Waislamu wa Kisuni. Alaakullihaal, siku hizo mbili yaani tarehe 12 na 17 Mfunguo Sita zinahesabiwa kuwa ni siku aliyozaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW. Sasa badala ya sisi Waislamu kukaa na kuzozana kuhusu siku aliyozaliwa mtukufu huyo, tunapaswa kukifanya kipindi cha baina ya siku hizo mbili kuwa kipindi cha Umoja wa Kimataifa wa Kiislamu. Kama ngome hiyo madhubuti itajengwa, hakuna dola lolote litakalothubutu kuingia kiuadui katika mipaka ya nchi na mataifa ya Kiislamu.

Sisi hatusemi kwamba Waislamu wa Kisuni duniani waache madhehebu yao na wawe Mashia, wala Waislamu wa Kishia duniani waache madhehebu yao na kuwa Masuni. Tab’an ni jambo lililo wazi kwamba kama kuna mtu amefanya utafiti na kupata yakini juu ya akida na itikadi fulani huwa ni wajibu wake kufuata uhakika na yakini aliyo nayo. Hayo yanahusiana na mtu na Muumba wake. Lakini tunachosema sisi katika Wiki ya Umoja na ambacho ni ujumbe wa umoja ni kwamba Waislamu waungane na wasifanyiane uadui. Msingi na mhimili mkuu ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Bwana Mtume Muhammad SAW na sheria za Kiislamu. Maneno haya hayana lolote baya ndani yake. Hayo ni maneno ambayo kila mtu mwenye akili timamu, mwenye insafu na asiye na malengo yake binafsi, lazima atakubaliana nayo.

Juu ya ukurasa

Siku ya Kimataifa ya Quds

Siku ya Kimataifa ya Quds ni dhihirisho jengine la kweli la umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu. Hiyo ni siku ya kuungana umma wa Kiislamu chini ya bendera ya kuikomboa Quds Tukufu. Yaani ulimwengu wa Kiislamu unaoanzia magharibi mwa dunia huko yaani Indonesia hadi magharibi mwa ulimwengu wa Kiislamu yaani katika nchi kama ya Nigeria barani Afrika, popote ambapo Waislamu watapata nafasi, basi utawana wanaitumia siku hiyo kutangaza misimamo yao thabiti kuhusiana na Quds Tukufu. Leo hii Waislamu wanaguswa sana na kadhia ya Palestina na wanaifuatilia kwa msukumo mkubwa sana. Sababu ya kushuhudiwa hali hiyo ni kwamba ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa umeamka. Ndio maana unatuona tunaipa umuhimu mkubwa siku hiyo na tunaitumia siku hiyo kufikisha sauti zetu kwa walimwengu kuhusiana na ukandamizaji unaofanywa dhidi ya taifa madhlumu la Palestina. Inabidi tuzitie nguvu nyoyo na roho zetu kwa ilhamu na baraka za mwezi Mtukufu wa Ramadhani na tujiimarishe kiimani na kuzidi kupata nguvu kutokana na ahadi za kweli za Mwenyezi Mungu.

Juu ya ukurasa

Sikukuu za Kiislamu

Idi na sikukuu za Kiislamu ni kwa ajili ya kuhuisha hisia za umoja na mshikamano baina ya Waislamu. Sikuu za Kiislamu ni siku ambazo Waislamu kote ulimwenguni wanazisherehekea.

Sikukuu za Kiislamu zina pande mbili ambapo upande mmoja ni kumzingatia na kuelekea kwa Mwenyezi Mungu katika upande wa kimaanawi na upande mwingine ni ule wa kuwakusanya pamoja Waislamu wote kwenye mhimili mmoja. Inabidi sikukuu na idi zote za Kiislamu pamoja na minasaba yetu yote mengine iwe na sifa hiyo maalumu kwa ajili yetu, yaani ziziunganishe nyoyo zetu Waislamu sote na kuzikurubisha pamoja. Leo hii Waislamu wanahitajia zaidi kuziunganisha nyoyo zao na safu zao kuliko wakati mwingine wowote.

Juu ya ukurasa

Darut Taqrib

Mimi ninaamini kuwa, kuyakurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu ni jambo la lazima, la wajibu na la dharura kabisa katika malengo ya dola ya Kiislamu na ninaamini kuwa, kitendo chochote cha kuharibu umoja na mshikamano ni pigo kubwa kwa umma mzima wa Kiislamu. Taasisi ya Darut Taqrib nayo tumeipendekeza kwa lengo hilo hilo. Darut Taqrib ambayo ilikuweko nchini Misri, kwa mtazamo wetu ilikuwa azizi na yenye heshima kubwa sana. Hivi sasa pia ina heshima. Hata hivyo inasikitisha kuona kuwa tangu huko nyuma hadi hivi sasa hawairuhusu taasisi hiyo ifanye kazi zake vizuri. Taasisi hiyo ilikuwa hai wakati fulani tu yaani ule wakati ambao ilikuwa ikitoa jarida lililojulikana kwa jina la Risalatul Islam na wakati ilipokuwa inaongozwa na Marhoum Shaltut na Sheikh Saliim na viongozi wengine wazuri wa al Azhar. Wakati huo taasisi hiyo ilifanya harakati nzuri. Marhoum Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa ni Marjaa Taklidi, alikuwa ni nguzo madhubuti ya Darut Taqrib. Rais wa al Azhar kwanza alikuwa ni Sheikh Saliim ambaye ndiye aliyeasisi na kwa hakika ndiye aliyeandaa mazingira ya kuundwa Darut Taqrib na baada yake akafuatiwa na Sheikh Mahmoud Shaltut aliyekuwa Rais wa al Azhar na pia Mufti wa Misri. Sheikh Shaltut mwenyewe ndiye aliyeongoza Darut Taqrib katika zama zake. Hizo ndizo zilizokuwa nguzo za Darut Taqrib. Leo hii ulimwengu wa Kiislamu unahitajia mno taasisi hai kama hiyo. Lengo la taasisi hiyo liwe ni kwa makundi mbali mbali ya Kiislamu kukurubiana katika upande wa kifikra na kiitikadi. Kuna mitazamo mengi ya makundi ya Kiislamu kama itajadiliwa na kufanyiwa mazungumzo baina ya makundi hayo inaweza kuleta matunda mazuri sana ya kuyafanya makundi yote hayo yakubaliane nayo. Pengine baadhi ya suutafahumu zikaondoka na baadhi ya itikadi zikafanyiwa marekebisho na baadhi ya fikra zikakurubishwa zaidi kwa kuzingatia ukweli wa mambo. Tab’an kama mazungumzo na mijadala baina ya makundi hayo ya Kiislamu yataishia kwa kupatakikana matunda kama hayo itakuwa ni bora zaidi kuliko kufanyika kwa sura nyingine lakini kama hayo hayatawezekana, basi angalau Waislamu wataweza kushirikiana katika mambo mengi mengine yanayowaunganisha. Kwa uchache hizo ndizo zitakazokuwa faida za mazungumzo baina ya makundi hayo. Hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kujiepusha na masuala ya kuleta mifarakano kati ya Waislamu.

Juu ya ukurasa

 
< Nyuma   Mbele >

^