Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu Nishati ya Nyuklia Chapa
13/06/2010

 

 

 

 

 

 

Matumizi ya Kheri na Shari ya Elimu
Elimu Isiyo na Maadili
Maana Halisi ya Maendeleo
Nafasi ya Teknolojia ya Nyuklia
Teknolojia ya Kienyeji
Ushindani Usio Salama wa Nyuklia
Uhakika wa Makelele ya Nyuklia
Upigaji Makelele
Nguvu za Kimaada na Kimaanawi
Wajibu wa Kutokomezwa Silaha za Mauaji ya Umati
Vitisho vya Usalama wa Dunia
Mantiki ya Iran katika Kukabiliana na Mashinikizo ya Mabeberu
Matakwa ya Mataifa
Kupotezwa Haki ya Kisheria
Kutohitajia Iran Silaha za Nyuklia

Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu Nishati ya Nyuklia

Matumizi ya Kheri na Shari ya Elimu

Kama ustawi na maendeleo yatakuwa mikononi mwa taifa salama na kamili, bila ya shaka maendeleo na ustawi huo utakuwa ni chimbuko la kheri na baraka. Kama silaha za kisasa zitakuwa mikononi mwa mataifa yaliyokamilika na yanayotumia busara, bila ya shaka yoyote silaha hizo hazitakuwa na hatari yoyote. Amma swali linalojitokeza hapa ni kwamba ni akina nani wanaoyahatarisha mataifa ya dunia kutokana na nguvu hizo zenye madhara? Bila ya shaka na hali nayo itaendelea kuwa hivyo hivyo kila siku. Ima watatengeneza bomu la atomiki, na matokeo yake yatakuwa kama walivyofanya Wamarekani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na kuwaletea maafa makubwa kiasi chote kile Wajapani, au itakuwa kama vile ilivyotokea katika Umoja wa Kisovieti, kuvuja kiwanda cha atomiki na kupelekea idadi kubwa ya watu kuuawa na kupata madhara makubwa. Kama kunatokezea madhara yoyote ya atomiki, basi wanaoleta madhara hayo ni madola makubwa yenye nguvu zisizodhibitika. Kama nguvu za kibeberu za Marekani zitadhibitiwa duniani, bila ya shaka hatari ya atomiki nayo itapungua yenyewe kwa yenyewe.

Jina la atomiki, kama ambavyo linaashiria maendeleo na elimu ya mwanaadamu, inasikitisha kusema pia kuwa, jina hilo linakumbushia tukio la aibu kabisa katika historia, mauaji makubwa zaidi ya kizazi kuwahi kushuhudiwa katika historia kutokana na mwanaadamu kutumia vibaya teknolojia hiyo. Ijapokuwa nchi nyingi duniani zinazalisha na kujilimbikizia silaha za mauaji ya umati za nyuklia jambo ambalo lenyewe linaweza kuwa ni utangulizi wa kutenda uhalifu; na licha ya kuwa jambo hilo linahatarisha vibaya sana amani na usalama duniani, lakini ni dola moja tu hadi sasa ambalo limetenda uhalifu na jinai ya atomiki. Ni dola la Marekani pekee ndilo lililofanya uhalifu huo dhidi ya wananchi madhlumu wa Hiroshima na Nagasaki huko Japan katika vita visivyo na mlingano sawa; na ni Wamarekani pekee ndio waliowahi kufanya shambulizi la bomu la atomiki lisilo na chembe ya utu na ubinaadamu.

Juu ya ukurasa

Elimu Isiyo na Maadili

Jambo ambalo leo hii linayafanya maendeleo makubwa ya kielimu katika ulimwengu wa Magharibi yashindwe kumwokoa mwanaadamu ni kwamba maendeleo hayo hayaendi sambamba na utu na ubinaadamu. Kuweko mfungamano wa karibu baina ya elimu na hisia za kibinaadamu ni jambo muhimu sana na ni jambo la lazima katika sehemu zote. Bila ya shaka yoyote mwanaadamu hataweza kustafidi inavyotakiwa na elimu yake popote pale alipo kama atashindwa kuwa na umaanawi, maadili, ubinaadamu na hisia za utu. Elimu isiyo na umaanawi na maadili, huwa bomu la atomiki. Huwaletea balaa wanaadamu wasio na hatia. Hugeuka kuwa silaha za maangamizi na hutumika dhidi ya raia na watu wa kawaida kama ilivyoshuhudiwa huko Lebanon, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na katika maendeo mengine duniani. Elimu ya aina hiyo hugeuka kuwa mada angamizi za kemikali kama zile zilizotumika huko Halabcha Iraq na katika mendeeo mengine duniani na kupelekea kuuawa wanawake, watoto wadogo na vijana wadogo. Mada ambazo hazichagui mwanaadamu wala mnyama wala kitu chochote chenye uhai, bali zinaangamiza kila kitu! Yote hayo yametokea wapi? Hizi mada angamizi, zote zimetokea kwenye vituo vya kielimu na ni kutoka katika nchi hizo hizo za Ulaya! Ni nchi hizo ndizo zilizotengeneza mada hizo na kuupatia utawala ambao ulikuwa haujali chochote.

Leo hii silaha na anuwai kwa anuwai ya maendeleo ya elimu, yameshindwa bali hayawezi kumnufaisha na kumletea kheri mwanaadamu. Hayana uwezo wa kuziletea furaha familia. Hayawezi kuwafanya wana, watoto, wanawake na wanaume wafurahie maisha. Yote hayo ni kwamba maendeleo hayo hayana maadili wala umaanawi ndani yake.

Juu ya ukurasa

Maana Halisi ya Maendeleo

Kuashiki umaanawi na kuwa na mfungamano na Mwenyezi Mungu ni sababu muhimu na kubwa zaidi ya kuyafanya maendeleo ya taifa fulani yapate maana halisi ya maendeleo. Kama hilo litakosekana, basi maendeleo yote yanayojulikana kwa lugha iliyoenea leo duniani yataingia katika mkondo ghalati na yatatumika vibaya. Yaani inawezekana nchi fulani ikawa na maadili mazuri ya kijamii, ikawa na desturi nzuri na heshima katika jamii yake, lakini wakati inapopata utajiri na elimu, ikawa utajiri na elimu yake hiyo inatumika dhidi ya taifa jengine na kwa ajili ya kuangamiza watu wengine. Kufanya hivyo ni makosa na hilo si sahihi katika mantiki yetu. Sisi hatukubaliani na suala la kutumia elimu kwa ajili ya kutengeneza silaha kama bomu la atomiki ambalo wakati linapotua sehemu fulani, halichagui mkosa wala asiye mkosa, mtu mwenye silaha, wala mtoto mdogo, mtoto mchanga, watu madhlumu wasio na hatia au vitu kama hivi, bali kazi yake ni kuangamiza kila kitu tu. Elimu inayotumika katika njia hiyo, na suala la nchi kupigania kuwa na elimu ya aina hiyo, na kutaka kuleta mabadiliko kwa kutumia elimu hiyo, yote hayo sisi hatukubaliani nayo na sisi hatupendi mabadiliko ya aina hiyo. Kumuabudu Mwenyezi Mungu, kuashiki umaanawi na hisia za kibinaadamu ni kitu muhimu sana katika kila mabadiliko. Inabidi hisia za utu na mapenzi yapewe nguvu ndani ya wanaadamu na inabidi sote tupige hatua kwa ajili ya kulifanikisha suala hilo.

Juu ya ukurasa

Nafasi ya Teknolojia ya Nyuklia

Elimu ya atomiki na teknolojia ya nyuklia ni miongoni mwa maendeleo makubwa aliyopata mwanaadamu ambapo inabidi, bali ni lazima maendeleo hayo yatumikie ustawi wa mataifa ya dunia na yaziletee maendeleo na uneemevu wa kweli, jamii zote za mwanaadamu. Upana wa matumizi ya elimu na teknolojia ya nyuklia unaweza kukidhi mahitaji makubwa sana ya tiba, nishati na viwanda ambapo kila moja ya mambo hayo lina umuhimu mkubwa kwa mwanaadamu. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, teknolojia ya nyuklia ina nafasi muhimu na kubwa katika maisha ya kiuchumi. Umuhimu wa teknolojia hiyo huongezeka katika siku zinavyosonga mbele na kadiri mahitaji ya kiviwanda, tiba na nishati yanavyoongezeka. Ni kwa kiwango hicho hicho ndivyo unavyoongezeka umuhimu wa kufanya juhudi kubwa zaidi za kumiliki teknolojia ya nyuklia na kuitumia kwa njia sahihi na nzuri. Mataifa ya Mashariki ya Kati kama yalivyo mataifa mengineyo duniani, yana kiu ya kuwa na amani, usalama na maendeleo. Mataifa hayo nayo yana haki ya kujidhaminia nafasi nzuri katika uchumi na maendeleo ya vizazi vijavyo kupitia teknolojia ya nyuklia. Yamkini moja ya malengo ya kupotoshwa suala la miradi ya nyuklia ya Iran yenye mnalengo ya amani kunakofanywa na madola ya kibeberu ni kujaribu kuyazuia mataifa mengine ya eneo hili yasitilie maanani wala kuipa uzito mkubwa haki yao ya kweli ya kustafidi kwa njia za amani na teknolojia ya nyuklia.

Juu ya ukurasa

Teknolojia ya Kienyeji

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejipatia yenyewe teknolojia ya nyuklia licha ya kuweko upinzani mkubwa sana wa maadui. Iran tangu zamani ni mwanachama wa wakala wa atomiki na imetia saini makubaliano ya kimataifa kuhusu atomiki, na ilitarajiwa kuwa kwa kufanya hivyo, na kwa mujibu wa sheria, Iran ina kila haki ya kusaidiwa katika upande wa teknolojia hiyo muhimu. Lakini Wazayuni wachochezi pamoja na Marekani na madola mengine duniani yalisimama wima yakitaka Iran isisaidiwe kabisa. Iran ikajifunga kibwebwe, ikatumia vijana wake, wasomi na wanafikra wake, vipaji vinavyochemka vya watu wake, vipawa vinavyong’ara vya Wairani na baada ya kupitia miaka kadhaa imefanikiwa kupata teknolojia hiyo bila msaada wa yeyote, naam teknolojia ya nyuklia salama na isiyo ya kutengeneza bomu la atomiki. Teknolojia ya nyuklia ya ustawi wa elimu imo katika matawi mengi yenye sifa maalumu nyingi za kipekee. Watu wanaotaka kutengeneza bomu la atomiki, wanaweza kufuata tawi moja kati ya matawi mengi ya teknolojia hiyo na kuendelea na tawi hilo hadi kufikia kwenye utaalamu wanaoutaka. Lakini nchi ya Iran haitaki bomu la atomiki bali inapinga pia silaha za kemikali. Hata wakati Iraq ilipoivamia na kuishambulia Iran kwa silaha za kemikali, jambo hilo halikuifanya Iran itengeneze silaha za kemikali. Hii ni kwa sababu mambo hayo yanakinzana kikamilifu na misingi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Juu ya ukurasa

Ushindani Usio Salama wa Nyuklia

Wachina hivi sasa wamepiga hatua nzuri za kisayansi na wamepata maendeleo mazuri katika uwanja huo. Hata hivyo tukumbuke kuwa mwaka 1948 – mwaka ambao iliundwa Uchina mpya na Uchina ya Kikomunisti – Wachina hawakuwa na chochote kile! Lakini Umoja wa Kisovieti – nchi ambayo wakati huo ilishakuwa mbele katika upande wa aidiolojia na ambayo ilishapata maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia – iliwapatia Wachina kila ilichokuwa nacho na wakati huo ulikuwa ni wakati wa Stalin. Kuweko nchi kubwa kama Uchina – tab’an wakati huo haikuwa na idadi kubwa ya watu kama walioko leo hii lakini kivyovyote vile ilikuwa ni nchi kubwa, pana na yenye watu wengi – pembeni mwa nchi kubwa kama Umoja wa Kisovieti katika kitovu cha bara la Asia, lilikuwa ni jambo muhimu mno kwa Urusi ya Kikomunisti. Hivyo kila ambacho Warusi walikuwa nacho, waliwapatia pia Wachina, hata teknolojia ya nyuklia. Lakini kwa upande wa Iran, teknolojia hiyo imepata taifa hilo kwa kutegemea vijana wake lenyewe. Wachina wamepata nishatia ya nyuklia kama zawadi kutoka kwa Warusi kama ambavyo Wachina na Warusi wameipatia pia Korea Kaskazini. Naam, hivyo ndivyo ilivyokuwa, maendeleo ya nchi kama Uchina yamepatikana kwa uuangaji mkono mkubwa sana na wa kipekee wa nchi nyingine. India nayo ni vivyo hivyo tab’an imepata teknolojia hiyo kutoka upande mwingine. Wakati zilipozuka hitilafu baina ya Urusi na Uchina – hitilafu kubwa sana zilizodumu kwa makumi ya miaka baina ya madola hayo mawili makubwa ya kikomunisti tangu baada ya ya kumalizika kipindi cha utawala wa Stalin huko Urusi kama vile hitilafu za kambi za Mashariki na Magharibi na hata pengine hitilafu za Urusi na Uchina zilikuwa mbaya zaidi – hitilafu hizo ziliwafanya Warusi waamue kuisaidia India ambayo ni jirani na Uchina, jambo ambalo liliwafanya Wachina nao waamue kuisaidia Pakistan ambayo nayo ni jirani na India na ni mpinzani wake mkubwa! Yaani kilichochochea yote hayo na kupelekea India na Pakistan zipate teknolojia ya nyuklia ni hitilafu kubwa zilizojitokeza baina ya madola mawili makubwa ya kikomunisti ya Uchina na Umoja wa Kosovieti. Naam Wachina waliwapatia Wapakistan nishati ya nyuklia na Warusi nao wakaipatia India teknolojia hiyo na maendeleo mengine mengi. Yaani, India na pia Pakistan, zote mbili zimepata teknolojia hiyo kutoka kwa wengine.

Juu ya ukurasa

Uhakika wa Makelele ya Nyuklia

Leo hii mtu anaweza kujiuliza, katika kadhia ya nishati ya nyuklia – ambapo maadui wanajaribu sana kuzusha makelele mengi duniani kuhusu nishati hiyo – msimamo wa nchi nyingine duniani kuhusiana na Iran ni upi hususan nchi za Asia, Mashariki ya Kati na nchi za Kiislamu? Hivi sasa na kama ilivyo kawaida yao, Wamarekani wanadai kuwa dunia inapinga suala la Iran kurutubisha urani! Lakini hapana! Inaonekana Wamarekani dunia hawaijui. Walimwengu na hata tawala za mataifa ya dunia ambopo mfano wake mdogo tu ni zaidi ya nchi 100 zisizofungamana na upande wowote na karibu nchi 50 za Kiislamu wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC na nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Upande wowote pamoja na kundi jingine kubwa lenye wingi mutlaki katika nchi za dunia zinaunga mkono suala la kutolewa nishati ya nyuklia katika udhibiti wa madola machache yenye majigambo na yanayodai kuwa na haki ya kumiliki kila kitu duniani. Kundi hilo kubwa sana la nchi za dunia, linaishajiisha na kuipongeza kwa udhati wa moyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa msimamo wake wa kishujaa na kusimama kwake kidete katika suala hilo. Taifa la Iran likiwa katika njia yake ya kujiletea fakhari, na kwa nguvu hamasa, juhudi na fikra zake, limeyaweka katika wakati mgumu madola ya Magharibi yaliyojifumia mambo ya kutaka kudhibiti kila kitu. Hivi sasa taifa la Iran limeziweka chini ya alama ya kuuliza fikra za Wamagharibi kuhusu jambo hilo na kila leo inaendelea kupiga hatua na inazidi kupiga mbizi katika kufanikisha malengo yake matukufu. Ikisha taifa la Iran itaupa ulimwengu wa Kiislamu na mataifa ya Kiislamu zawadi yenye thamani kubwa ya kimaanawi na kuilazimisha kambi ya kiistikbari na kibeberu ilegeze kamba na kurudi nyuma.

Juu ya ukurasa

Upigaji Makelele

Wazayuni maghasibu ambao wanaikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina pamoja na jopo linalotawala huko Marekani ambalo chuki na uadui wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hauna kiasi, mabeberu ambao wako tayari kutumia njia yoyote chafu na mbaya kwa ajili ya kufikia malengo yao, wameanzisha nara na kaulimbiu duniani wakidai kuwa “Iran inataka kumiliki silaha za atomiki!” Propaganda zao hizo zimewafanya walimwengu na tawala nyingi kuwa na wasiwasi na hisia kali. Baada ya mekelele yao hayo, Wazayuni na watawala wa Marekani walitaka waone dunia imeungana na ionekane kuwa walimwengu na watu wote duniani wana woga na juhudi za Iran za kujipatia teknolojia ya nyuklia.

Kitu ambacho hadi sasa Jamhuri ya Kiislamu imekubaliana nacho ni kuwa waje na kuona kwa karibu kazi ya urutubishaji urani ambayo inafanyika katika sehemu maalumu nchini. Wataalamu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki nao wamekuja na wameona na wamefanya ukaguzi wao. Iran nayo imewaruhusu kutembelea sehemu zote wanazowaza kuwa kunafanyika kazi ya urutubishaji wa urani, yote hayo yamefanyika ili kuwathibitishia kuwa propaganda za Wazayuni ni uongo mtupu. Hiyo kwa kweli ni moja ya njia za amani za kuilinda teknolojia ya nyuklia.

Juu ya ukurasa

Nguvu za Kimaada na Kimaanawi

Kila taifa duniani linapaswa kujizatiti na kujiimarisha ili liweze kulinda malengo yake matakatifu. Tab’an maana ya nguvu katika mantiki ya dini na umaanawi inatofautiana sana kabisa na maana nguvu inayotolewa na mantiki ya kimaada. Umaada unaziona nguvu kuwa zimo katika zana na vifaa vinavyogusika. Wanaona nguvu zinapatikana katika atomiki, katika silaha za kemikali, katika silaha za vijidudu na katika zana nyingine mbali mbali za kisasa za kimaada. Lakini nguvu haziishii kwenye mambo hayo. Bali sehemu kubwa ya nguvu inapatikana ndani ya wanaadamu wenyewe ambao wanataka kustafidi na kutumia nguvu hizo. Kwa vile mwanaadamu ana majimui ya haki na anafanya juhudi kubwa za kupata haki na kufanikisha malengo na matukufu aali na kwa vile yuko tayari kutumia uwezo wake wote kufanikisha jambo hilo, bila ya shaka yoyote yeye mwanaadamu ndiye kitovu cha nguvu ya kweli na ya asili. Majiumi ambayo inafanya juhudi kubwa za kupata haki na matukufu yanayotakiwa, haiwezi kutumia nguvu kwa njia za kihayawani, wala kudhulumu, wala kufanya ubeberu, wala haiwezi kutumia nguvu zake kuwadhalilisha wanaadamu wengine. Aidha watu wenye sifa hizo hawawezi kutumia nguvu zao kuvamia na kukalia kwa mabavu ardhi za watu wengine wala kuwapora utajiri wao na kuiba maliasili zao na wala hawajipi haki ya kumiliki vitu vya watu wengine. Hayo ndiyo maadili ya nguvu za kimaanawi. Lakini nguvu za kimaada hazina hata harufu ya umaadili na hazijali kabisa umaanawi na akhlaki. Nguvu za kimaada hazitumiki kwa ajili ya kulinda haki na matukufu ya kweli. Mantiki ya watu wenye nguvu za kimaada, ni mantiki ya msituni. Kwa vile wana nguvu za kimaada, watu hao wanahisi kuwa haki ni yao wao tu wakati fikra hiyo ni ghalati. Mlingano huo kwa kweli ni batili.

Juu ya ukurasa

Wajibu wa Kutokomezwa Silaha za Mauaji ya Umati

Wakati kwa mara ya kwanza katika historia, Marekani iliporipua bomu la kwanza la nyuklia huko Hiroshima na Nagasaki nchini Japan, shambulizi hilo lilileta maafa makubwa mno ya kibinaadamu na ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika historia. Shambulio hilo lilihatarisha vibaya mno amani ya mwanaadamu na ndio maana walimwengu wote walikubaliana kwa kauli moja kwamba inabidi silaha hizo hatari na angamizi zitokomezwe kabisa. Kutumiwa na Marekani bomu la nyuklia si tu kulipelekea kuuawa kwa umati kundi kubwa la watu na kupatikana uharibifu mkubwa, lakini pia bomu hilo halikuchagua mwanajeshi wala asiye mwanajeshi, halikuchagua mkubwa wala mdogo, halikuangalia mwanamke wala mwanamme na halikubagua ajuza wala kitoto kichanga. Athari mbaya zilizo dhidi ya ubinaadamu za shambulizi hilo zilivuuka mipaka ya kisiasa na kijiografia na kuvitia hasara isiyofidika hata viumbe vilivyokuja baadaye. Ndio maana ikaamuliwa kuwa matumizi ya aina yoyote ile ya silaha za atomiki, bali hata kutoa vitisho tu vya kutumia silaha hizo, ni uvunjaji mkubwa wa misingi ya wazi kabisa ya kibinaadamu. Jambo hilo ni uvunjaji usio na kificho wa misingi ya urafiki na ni dhihirisho la wazi la jinai za kivita.

Juu ya ukurasa

Vitisho vya Usalama wa Dunia

Kutokana na kuwa madola machache makubwa duniani yanaendelea na juhudi zao za kumiliki silaha za nyuklia zilizo dhidi ya binaadamu kwa madai ya kujizatiti kijeshi na kiusalama, sasa tena hapana shaka hata chembe kwamba ni muhali kupatikana ushindi katika vita vya nyuklia na kwamba mapigano katika vita kama hivyo si jambo linalokubalika kiakili bali ni kitendo kilicho dhidi ya ubinaadamu. Lakini licha ya mambo kuwa wazi kiasi chote hicho katika upande wa kimaadili, kiakili, kibinaadamu na hata kijeshi, na licha ya walimwengu kutaka kwa kusisitiza kwamba silaha za nyuklia zitokomezwe duniani, lakini kuna madola machache duniani ambayo mawazo yao na ndoto zao zinawaambia kwamba hayawezi kupata usalama bila ya kuwa na silaha za nyuklia. Madola hayo yainapuuza mambo yote hayo na kufikiria tu kujilimbikizia silaha hizo za mauaji ya umati.

Kung’ang’ania madola hayo suala la kumiliki, kuongeza na kupanua zaidi nguvu zao za silaha angamizi za nyuklia, nguvu ambazo hazina faida yoyote isipokuwa kutia hofu na kufanya ugaidi dhidi ya halaiki ya watu sambamba na kuleta usalama bandia, wa uwongo na wa kibazazi, uliosimama juu ya msingi wa kujilinda na kujidhaminia usalama kupitia uangamizaji usioepukika wa wote, kwa kweli kunazidi tu kuutia ulimwengu katika jinamizi la nyuklia. Vyanzo vya nje kama vile vya kiuchumi na kibinaadamu, vinatumika katika mashindano yasiyo ya kimantiki ili kila dola kubwa liweze kupata nguvu za kimagube za kuweza kuwaangamiza wapinzani wao kwa zaidi ya mara elfu kumi, na kuwaangamiza wakazi wengine wa sayari za dunia wakiwemo wao wenyewe. Si bure kuona kwamba stratijia hiyo imepewa jina la “kujilinda juu ya msingi wa maangamizi yasiyoepukika ya upande wa pili” au mkakati wa kiwendawazimu.

Katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya madola yanayomiliki silaha za nyuklia yamekwenda mbali zaidi na kupindukia nadharia ya kujihami mbele ya madola mengine yenye silaha za nyuklia chini ya msingi wa “maangamizi yasiyoepukika ya upande wa pili” na kufikia hadi kuwa mikakati na stratijia za nyuklia za madola hayo sasa zinatishia hata kutumia silaha za nyuklia dhidi ya vitisho vinavyodaiwa kutolewa na wasioheshimu makubaliano ya Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Atomiki NPT. Wakati ambapo wavunjaji wakuu wa mkataba huo ni madola makubwa ambayo mbali na kukanyaga ahadi zao katika kipengee cha 6 cha mkataba huo kinachoyataka madola hayo kutokomeza silaha zao za nyuklia, hata yanashindana katika kueneza kwa urefu na upana silaha angamizi za nyuklia huku kila dola moja likitaka kumpiku mwenzake katika suala hilo. Miongoni mwa uvunjaji mkubwa na wa wazi wa vipengee vya mkataba wa NPT unaofanywa na madola hayo ni kuusaidia na kuupa silaha za nyuklia utawala wa Kizayuni wa Israel na kuunga mkono siasa za utawala huo ghasibu. Kwa kitendo chao hicho, madola hayo yanahusika moja kwa moja na uenezaji wa kweli wa silaha hizo na yanakanyaga moja kwa moja ahadi zao yalizozitoa kulingana na kipengee cha kwanza cha mktaba huyo. Vile vile kwa uvunjaji wao huo wa mkataba wa NPT, madola hayo yameliingiza eneo la Mashariki ya Kati na dunia nzima kiujumla katika hatari kubwa ambapo dola linaloongoza katika uvunjaji huo wa makubaliano ya NPT ni dola la kibeberu na vamizi la Marekani.

Juu ya ukurasa

Mantiki ya Iran katika Kukabiliana na Mashinikizo ya Mabeberu

Wamarekani inabidi hili walielewe vyema kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaki vita. Misingi ya mfumo wa Kiislamu inapinga masuala ya vita. Iran haipendi na haitaki vita vya aina yoyote ile. Hilo inabidi kila mtu alijue. Msimamo huo unakubaliwa kwa kauli moja na viongozi wote wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wote wanaamini kwamba ni jukumu lao kujiweka mbali na vita. Misingi ya Uislamu inaifanya Iran itoe ujumbe wa urafiki, amani, mapenzi, usalama na utulivu kwa walimwengu, kwani taifa la Iran lina mambo mengi ya mazuri ya kuwafaidisha wengine katika masuala hayo. Mtu asiye na kitu cha kusema katika mambo kama hayo ndiye anayetaka kuvuruga hali ya mambo ili sauti ya haki isimfikie mtu yeyote. Ili asiweko mtu yeyote atakayepata habari kuwa kuna watu duniani wanasema maneno ya haki. Mtu wa kutumia mabavu siku zote moyo wake hupenda kuona hakuna utulivu na kuna mazingira ya fujo, lakini mtu anayetumia mantiki na aliye na mengi mazuri ya kusema, siku zote hupenda uweko utulivu, kusiwe na fujo, bali uweko unyamavu na ubaridi ili maneno yake yaweze kusikika na kuzingatiwa.

Kambi ya mabepari na wakoloni inatumia uwezo wake wote wa kisiasa, unatumia nguvu zake zote za kifedha na kiuchumi na unatumia mabanda yake yote ya kipropaganda kushinikiza na kutoa mibinyo kwa ndoto kuwa labda kuna siku itaweza kulifanya taifa la Iran lirudi nyuma na kusalimu amri si tu katika haki yake ya nyuklia – haki ya nyuklia ni moja ya haki za taifa la Iran – bali kambi hiyo inataka Iran iache kupigania haki ya utukufu wake, haki ya uhuru wake, haki ya uwezo wake wa kujiamulia inachopenda, haki yake ya kujiletea maendeleo ya kielimu, katika mambo yote hayo, kambi ya kikoloni na kibepari inataka ilione taifa la Iran limesalimu amri ya kurudi nyuma. Taifa la Iran hivi sasa limo katika barabara kubwa ya kujiletea maendeleo ya kisayansi na maendeleo ya kiteknolojia na linataka kuona kuwa linafidia karne mbili lilizobakishwa nyuma na tawala za kitaghuti nchini Iran. Sasa mabeberu wamechanganyikiwa na hawataki kuliona taifa hili la Iran – ambalo liko katika eneo hili nyeti duniani likiwa limepandisha juu bendera ya Uislamu – linapata maendeleo hayo na ndio maana hawasiti hata kidogo kulisakama na kulishinikiza. Lakini taifa la Iran liko imara na halitetereki. Wamarekani wamejaribu na imewabainikia kuwa zana za kijeshi, bomu la atomiki na vitu vingine kama hivyo ni kitu kidogo sana, bali si lolote si chochote mbele ya azma na irada ya mataifa huru. Tawala zinaweza kuogopa, majeshi yanaweza kutishika, lakini watu na mataifa; aslan waabadan! (Kamwe hayawezi kushtushwa)!

Juu ya ukurasa

Matakwa ya Mataifa

Moyo wa taifa la Iran nao ni moyo wenye matumaini makubwa. Hii hii shaari, hii kaulimbiu na nara iliyoenea katika pembe zote za Iran kuhusiana na nishati ya nyuklia ambayo inasema “nishati ya nyuklia ni haki yetu isiyopingika” si kitu chepesi na cha kawaida. Mataifa mengi sana duniani aslan hata hayajui teknolojia ya nyuklia ni nini, na hata hayajui maana ya haki yao isiyopingika ni kitu gani na hata wakijua hawawezi kuchukua hatua zozote katika uwanja huo. Lakini taifa la Iran linajua nishati ya nyuklia kwamba ni kitu chenye thamani kubwa sana na ni nembo ya maendeleo kulingana na maendeleo ya leo ya kisayansi duniani na kama mtu atashindwa kuwa nayo basi amezubaa. Wananchi wa Iran wanajua pia kuwa hiyo ni haki yao isiyoporeka wala kupingika na ndio maana wanapiga nara na shaari hiyo. Kwa udhati wa nyoyo zao, wananchi wa Iran wanawataka viongozi wao kulinda haki yao hiyo na wanajua pia kuwa nchi yao inao uwezo wa kufuatilia na kupata haki yao hiyo isiyopingika bila ya kuwategemea wengine na bila ya kuwanyooshea wengine mkono wa kuomba. Hili kwa hakika ni jambo muhimu mno. Huo ndio moyo na hayo ndiyo matumaini ya taifa la Iran.

Hivi sasa mataifa mengine duniani yanaliangalia taifa la Iran kwa jicho la matumaini, yanapata nguvu kutoka kwa taifa la Iran, yanapata msukumo kutoka kwa taifa hilo na yanapata mbinde kutokana na misimamo thabiti ya taifa la Iran. Leo hii nara na kaulimbiu zilizo dhidi ya mabeberu zinazotolewa na taifa la Iran zimeenea kote ulimwenguni. Leo hii katika kila nchi kati ya nchi za Kiislamu bila ya kujali ni utawala gani unaotawala katika kila nchi, wananchi wa nchi hizo wanaziangalia kwa jicho la heshima na kujivunia, shabaha, malengo matukufu, shaari na kaulimbiu, zilizobuniwa na taifa la Iran, naam kaulimbiu za kupinga dhulma, za kupinga ubeberu, za kuwatetea wanaodhulumiwa, za kulitetea taifa la Palestina sambamba na kupapambana na saratani iliyoenea kila mahala ya Uzayuni. Huo ndio moyo wa mataifa ya Waislamu na huko ndiko kuzidi kupanuka Mapinduzi ya Kiislamu. Hata hii kaulimbui na shaari ya nishati ya nyuklia iliyobuniwa na taifa la Iran – ya kwamba taifa la Iran limesimama imara mbele ya mashinikizo ya maadui na linatetea vilivyo haki zake – nayo pia, leo hii imeenea katika ulimwengu wa Kiislamu. Kwa mujibu wa kile kinachoakisiwa kutoka kwa wasemaji wa nchi za Kiislamu na Kiarabu ni kwamba nishati ya nyuklia ni kitu kinachotakiwa na mataifa yote ya Kiarabu hivi sasa.

Juu ya ukurasa

Kupotezwa Haki ya Kisheria

Kupoteza na uporaji wa haki za wengine unaofanywa na Marekani katika eneo si wa aina moja wala mbili. Kuhusu nchi ya Iran na kuhusiana na hili suala la nyuklia – hili suala ambalo kwa miaka mingi sasa limeenea na kusikika sana duniani - Wamarekani wanafanya njama kubwa sana ya kuficha na kupotosha ukweli juu yake, wanafanya hila kubwa kutosema ukweli, wanafanya kila wawezalo kueneza uongo, wanakabiliana kwa njia na haki ya taifa jingine wakati hiyo kwa Iran ni haki yake ya kimaumbile na kisheria tena basi taifa hilo halikwenda kumpora yeyote haki yake hiyo, bali limeipata kwa nguvu na juhudi zake lenyewe! Taifa la Iran linasema, linachotaka ni teknolojia ya nyuklia. Sisi (taifa la Iran) tunataka kuwa na teknolojia ya nyuklia ili tuweza kuitumia katika masuala mbali mbali ya maisha yetu kwa njia za amani, lakini mabeberu ndio kwanza wanang’ang’ania kuwa taifa la Iran linataka bomu la nyuklia! Kitu gani kinawafanya mabeberu hawa waseme uongo?! Kwa nini wanafanya mambo ambayo yatazidi kulifanya taifa la Iran lizidi kuwachukia? Mara chungu nzima taifa la Iran na viongozi nchini wamekuwa wakitangaza kwamba, sisi hatuna haja na silaha za nyuklia na aslan jambo hilo halimo kabisa katika ajenda zetu za kiulinzi wala katika silisila ya mahitajio yetu ya silaha. Bali sisi tunaamini kuwa ni haramu kutumia silaha hizo. Sisi tunaamini kuwa kuwalinda na kuwaokoa wanaadamu kutokana na balaa hilo kubwa ni jukumu la kila mtu. Sisi tunaamini kuwa mbali na silaha za atomiki, silaha nyingine za mauaji ya umati kama vile silaha za kemikali na vijidudu nazo ni tishio kubwa kwa mwanaadamu. Taifa la Iran ambalo lenyewe ni muhanga wa kutumiwa silaha za kemikali dhidi yake, inahisi zaidi ubaya na hatari ya kujilimbikizia silaha hizo hata kuliko mataifa mengine yote na ndio maana taifa la Iran linatumia uwezo wake wote kukabiliana na silaha za aina hiyo.

Amma kichekesho kikubwa hapa ni kuona kuwa, muhalifu pekee duniani wa kutumia silaha angamizi za nyuklia anaeneza uongo duniani na anapita huku na kule akidai kuwa anapambana na suala la kuenea silaha za atomiki wakati ambapo kwa yakini, hachukui hatua yoyote ya maana katika uwanja huo na kamwe hatafanya hivyo. Kama madai ya Marekani ya kupambana na suala la kuenea silaha za nyuklia si uongo, mbona basi utawala wa Kizayuni unaendelea kukaidi sheria za kimataifa katika uwanja huo na hususan katika suala la mkataba wa NPT na umeigeuza ardhi unayoikalia kwa mabavu ya Palestina kuwa ghala la korija kwa korija za silaha za nyuklia?

Juu ya ukurasa

Kutohitajia Iran Silaha za Nyuklia

Kuna kuchanganya mambo katika mijadala inayohusiana na nyuklia na hakutenganishwi baina ya teknolojia ya nyuklia na silaha za nyuklia wakati ambapo hakuna uhusiano wowote kati ya mambo hayo mawili. Silaha za nyuklia zinahitajia urutubishaji wa zaidi ya asilimia 90 ya urani na unategemea teknolojia tata sana ambapo mtu hawezi kuingia tu katika mkondo huo ila baada ya kuazimia kikweli kweli kufanya hivyo. Lakini Jamhuri ya Kiislamu haina msukumo wowote na jambo hilo, hadi sasa haijafuatilia jambo hilo na haitalifuatilia. Iran haina haja kabisa na bomu la nyuuklia. Kwa miaka mingi Iran imekuwa ikiishinda na kuifelisha Marekani na je kuna mtu asiyeliona hilo? Je taifa la Iran limeishinda Marekani kwa kutumia silaha za nyuklia au limeishinda kwa kutumia imani thabiti, nia isiyotetereka, azma ya kweli, mwamko na mshikamano? Iran inajua inachotaka na inajua inachofanya na njia ya kufanyia inalotaka inaijua na imefanya hivyo bila ya kuogopeshwa na chochote. Hivi ndivyo Iran ilivyoweza kuishinda Marekani bila ya kuhitajika kuwa na bomu la nyuklia. Kuna uwezekano mabomu ya nyuklia yaliyokuwa yanamilikiwa na Umoja wa Kisovieti yalikuwa mengi zaidi ikilinganishwa na Marekani. Lakini je, haikushindwa?! Kushinda na kushindwa katika nyuga kuu duniani hakutegemei (silaha hizo wala) vitu kama hivyo.

Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu leo hii umetoa kigezo kwa ajili ya ulimwengu wa Kiislamu nacho ni kigezo cha demokrasia ya kidini, kigezo cha uhuru na heshima ya taifa. Leo hii ulimwengu wa Kiislamu umesimama dhidi ya Marekani kwa miaka kadhaa na leo huu mataifa mbali mbali yanatoa nara ya “Mauti kwa Marekani.” Hivi huko nyuma ni nani aliyekuwa akitoa shaari ya “Mauti kwa Marekani?” Ni nani aliyekuwa akifanya hivyo huko nyuma zaidi ya Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran? Lakini leo hii wote wanapiga nara hiyo. Nchi za Kiislamu ya Iran haikupata maendeleo yake kwa bomu la atomiki. Ushindi katika nyuga kubwa kubwa na za kihistoria ambao kumbukumbu yake itabakia milele, haupatikani kwa silaha hizo. Kwani hivi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel haumiliki silaha za nyuklia? Kwa mujibu wa taarifa zinazotolewa, utawala huo wa Kizayuni umejilimbikizia vichwa 200 au pengine 300 vya silaha za nyuklia. Lakini kwa miaka kadhaa sasa utawala wa Kizayuni umeshindwa kukabiliana na upande ambao hata kifaru hauna zaidi ya mawe, tab’an mawe yaliyoambatana na imani thabiti isiyotetereka. Kwa kweli Iran haitaki bomu la nyukli na kamwe haina haja nalo. Itake bomu la nyuklia kwa kazi gani? Ilifanyie nini bomu hilo? Wakati bomu la nyuklia linapotumika haliui adui tu, bali linaua hata wasio maadui na jambo hilo ni kinyume na mafundisho ya Uislamu, linakinzana na mwenendo na maadili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran? Bomu la nyuklia ambalo kazi yake ni kuangamiza kizuri na kibaya, ni bomu ambalo linateketeza kilicho kibichi na kikavu, bomu kama hilo kwa kweli si kitu ambacho kinahitajiwa na Jamhuri ya Kiislamu. Mfumo wa Kiislamu una kitu ambacho, bomu na shambulizi lolote la nje haliwezi kukifanya chochote bali litazidi kukiimarisha na kukitia nguvu tu kitu hicho nacho si kingine ghairi ya “wananchi.”

Juu ya ukurasa

 
< Nyuma   Mbele >

^