Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Nafasi ya Sanaa na Msanii Chapa
31/07/2010

Uhakika wa Sanaa
Thamani za Sanaa
Sanaa Kama Wenzo
Wenzo wa Kustawisha Fikra
Sifa Maalumu Kuu ya Sanaa
Vipawa vya Sanaa
Jukumu la Msanii
Kwenda Sambamba na Wakati

Sanaa ya Uwajibikaji

Uwajibikaji Mbele ya Watu
Uwajibikaji Mbele ya Sanaa
Uwajibikaji Mbele ya Madhumuni
Uwajibikaji Mbele ya Tafakuri
Uwajibikaji Mbele ya Malengo

Sanaa na Dini

Maana ya Sanaa ya Kidini
Mwelekeo wa Sanaa ya Kidini
Qur’an katika Upeo wa Sanaa

Sanaa na Siasa

Kutumiwa Vibaya Sanaa Kisiasa
Sanaa Inayotumikia Ubeberu

Uchumi na Sanaa

Uchumi na Sanaa
Mtazamo wa Kimaada juu ya Sanaa

Nafasi ya Sanaa na Msanii

Uhakika wa Sanaa

Uhakika wa sanaa – iwe sanaa yoyote ile – ni atia na ni kipaji kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ijapokuwa kudhihiri kwa sanaa kunatokana na jinsi sanaa yenyewe itakavyobainishwa, lakini huo si uhakika wote wa sanaa. Kabla ya kubainishwa, kuna hisia na utambuzi na udiriki wa sanaa yenyewe na kwamba mambo yote yanachimbukia hapo. Baada ya kuonekana, kutambuliwa na kubainishwa uzuri, unyofu na uhakika wa sanaa, hapo ndipo zinapoweza kuzuka maelfu na nukta ndondogo na nyembamba sana ambazo baadhi ya wakati hawawezi kuziona nukta hizo isipokuwa wasanii wenyewe. Mtu asiye msanii anaweza kushindwa kuona hata nukta moja kati ya hizo na sababu yake ni kuwa msanii ana kurunzi na kipaji cha kipekee cha kuweza kupenya ndani kabisa na kuona nukta hizo nyembamba, ndogondogo na uhakika halisi. Hiyo ndiyo huitwa sanaa ya kweli na ya uhakika kutokana na kuwa imechimbuka kutoka katika udiriki, ubainifu na utambuzi wa kweli.

Juu ya ukurasa

Thamani za Sanaa

Kabla ya mtu yeyote mwingine, thamani za sanaa na nafasi yake ya kweli inabidi wasanii wenyewe waitambue na kuipa heshima yake. Wasanii wanapaswa kujua thamani ya tweka, furumu na shehena yenye thamani kubwa iliyomo ndani ya dhati zao. Namna ya kuheshimu na kujua thamani ya kipaji hicho nayo ni kule kuupa usanii hadhi yake na kuuweka katika nafasi unayostahiki. Katika hadithi tukufu iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Sajjad AS, mtukufu huyo amesema: Roho na kuchunga kwako thamani za utu ndivyo vitu vyenye adhama na utukufu wa hali ya juu sana na hakuna kitu chochote kinachoweza kuwa kufu ya roho hiyo isipokuwa pepo iliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu, hivyo usiruhusu kitu chenye thamani kubwa kama hiyo kwenda kuwa chakula cha moto. Sanaa ni miongoni mwa nukta za fakhari na zenye thamani kubwa katika moyo wa mwanaadamu. Inabidi kujua thamani ya kitu hicho na kukitumia tu kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Tab’an wakati inaposemwa kitumike kwa ajili ya Mwenyezi Mungu inabidi mtu achunge zisije ghafla kazi zake zikamshukuma upande wa riyaa na kujionesha.

Juu ya ukurasa

Sanaa Kama Wenzo

Leo hii wale watu ambao wana ujumbe maalumu kwa ajili ya watu – ni sawa tu uwe ni ujumbe wenye rehema au ujumbe wa kishetani – wenzo mkubwa wanaotumia huwa ni sanaa. Kilicho muhimu sana hapa ni kuwa, kama zilivyo nyenzo nyingine, sanaa nayo inabidi mwelekeo wake uwe wa kina sana, wa wazi na sahihi na isije sanaa ikaenda kombo na kukosea njia. Hivyo kwa msaada wa sanaa, leo hii tunaona ulimwengu unaeneza mambo ya batili kabisa katika fikra za majimui kubwa ya watu na kuyafanya mambo hayo yaonekane ni haki. Ni wazi kwamba hilo halingewezekana kama kusingelitumika sanaa. Hii sinema nayo ni sanaa, hii televisheni nayo ni sanaa, ndani ya vitu hivyo kunatumika anuwai kwa anuwai za mbinu za kisanii ili kuhakikisha ujumbe wa batili unazifikia fikra za walimwengu kwa sura ya kitu cha haki.

Hivyo sanaa ni wenzo na ni zana yenye thamani kubwa sana. Ni mpiko na ala, lakini uzito wa mzega huo huwa mkubwa kiasi kwamba baadhi ya wakati, wenyewe unakuwa na thamani ya aina yake kwani kama wenyewe hautakuwa na thamani kubwa, hauwezi kuwa wenzo laiki wa kufikishia kiwango kinachotakiwa cha mambo yaliyokusudiwa kuzifikia nyoyo za watu.

Juu ya ukurasa

Wenzo wa Kustawisha Fikra

Sanaa ina lugha pana ambayo hakuna lugha yoyote nyingine yenye upana kama huo. Si lugha ya sayansi, wala lugha ya kawaida, wala lugha ya mawaidha yenye upana kama wa lugha ya sanaa. Inabidi sanaa ipewe umuhimu na kila leo inabidi ipanuliwe na inabidi pafanyike juhudi za kuhakikisha muundo wa kujivunia wa sanaa ndio unaotumiwa. Bila ya kuwepo sanaa, matamshi ya kawaida hayawezi kupata nafasi yake katika akili ya mtu yeyote yule sisemi tena wakati sanaa inapokuwa na mvuto na athari za kudumu. Sanaa ni ala na wenzo mzuri sana wa kufikisha na kupanua fikra sahihi. Sanaa ni ala, ni zana ni chombo; naam chombo muhimu mno. Si sahihi kuipuuza sanaa na kudharau wajibu wa kuiendeleza na kuipanua sanaa, na si sahihi kudhani kwamba sanaa ni dhambi au kufikiri ni makosa kuwa msanii na vitu kama hivyo. Sanaa ni miongoni mwa viumbe bora kabisa vya Mwenyezi Mungu na ni miongoni mwa usanii wenye thamani kubwa wa Mwenyezi Mungu ambapo inabidi thamani ya jambo hilo ijulikane na inabidi pia tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa neema hiyo. Sanaa ni wenzo ambao hauna budi kutumiwa katika mambo yote, hata katika tablighi ya kawaida.

Juu ya ukurasa

Sifa Maalumu Kuu ya Sanaa

Sifa maalumu kuu ya sanaa ni kwamba inatoa athari zake kwa msemaji na msikilizaji hata kama katika mambo mengi msemaji hatalizingatia hilo, na ijapokuwa katika aghlabu ya wakati, msikilizaji hatalihisi hilo. Athari za tungo za kishairi, michoro na aina nyingine za sanaa, sauti ya kuvutia na muziki mzuri – ambapo yote hayo ni katika sanaa – huziathiri nyoyo za wanaosikiliza bila wenyewe kujua na kwa hakika athari ya namna hiyo ndiyo bora kabisa. Mwenyezi Mungu amechagua bayana fasaha kabisa yaani Qur’ani kwa ajili ya kubainisha mafundisho bora kabisa. Mwenyezi Mungu angeliweza kutumia maneno ya kawaida tu kubainisha Qur’ani na mafundisho ya Kiislamu lakini hakufanya hivyo, bali amevibainisha vitu hivyo kwa kutumia lugha ya fasaha kabisa na bayana bora kabisa ya kisanii. Qur’ani yenyewe inasema kwamba, humwezi kuleta mithili ya maneno na muundo wa kisanaa kama wa Qur’ani. Maana ya maneno hayo iko wazi kabisa.

Juu ya ukurasa

Vipawa vya Sanaa

Tab’an sanaa si katika utajiri ambao unapatikana mara moja kwa kijasho cha uso na girisi mikononi. Madhali mtu hana ile atia na kipaji cha sanaa, hata akijitahidi vipi bado ataendelea kubakia katika asili yake ile ile ya kimaumbile. Kipawa na kipaji cha kisanii si kitu ambacho mtu anaweza kukichuma bali huwa ni atia maalumu anayotunukiwa msanii na Mwenyezi Mungu Mbora wa kuumba. Mwenyezi Mungu Ndiye Ambaye humpa mwanaadamu neema zote hata kama njia ya kumfikia neema hizo huwa ni jamii, baba, mama, mazingira anayoishi na vitu vingine kama hivyo. Msanii hufanya juhudi zake, lakini hiyo fursa na hima ya kufanya juhudi nayo hupewa na Mwenyezi Mungu. Msanii anapaswa kufanya juhudi za kukuza kipaji chake cha usanii ndani ya nafsi yake.

Kila msanii peke yake ni kama dunia nzima na sifa hiyo maalumu ya msanii imo ndani ya nafsi yake. Kama mtu angelipata fursa ya kudiriki dhati ya wasanii angeliweza kuona shani za dunia na maajabu yake. Dunia iliyojaa furaha na majonzi, mtumaini na wasiwasi ndani yake na si kwa sababu tu vitu hivyo vina mvuto wa kipekee katika nyoyo na macho, hapana kwani vitu vingi vingine vya kawaida visivyo vya kisanaa vinaweza kuvutia nyoyo na macho, bali ni kwa sababu sanaa ni atia na gawio kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Juu ya ukurasa

Jukumu la Msanii

Sanaa ni uhakika wenye fakhari kubwa na kwa kawaida mtu anayepewa kipaji hicho na Mwenyezi Mungu huwa ni kama ambavyo watu wengine walivyopewa utajiri mwingineo hivyo; anapaswa kujua uzito wa jukumu alilopewa yaani ajue thamani ya neema alizopewa na Mwenyezi Mungu na atekeleze jukumu lake kwa mujibu wa neema hizo. Majukumu hayo si lazima yote yawe ni ya wajibu wa kidini na kisheria, hapana, kwani kuna majukumu mengi ambayo mtu anatekeleza kwa kusukumwa tu na nafsi yake. Wakati mwanaadamu ana macho, hiyo ni neema ambayo baadhi ya watu hawanayo. Lakini pamoja na kwamba macho hayo yanampa mambo mazuri na yana ladha hizi na zile kwa mwanaadamu, lakini pia mwanaadamu ana majukumu ambayo anapaswa kuyatekeleza kutokana na kuwa na neema hiyo ya macho. Si lazima dini imwambie mwanaadamu majukumu yake, wala si lazima kuwe na aya ya Qur’ani iliyoshuka kwa ajili ya jukumu hilo, hayo ni mambo ambayo nafsi ya mwanaadamu mwenyewe inayajua. Aidha hakuna mtu duniani ambaye hatamlaumu tajiri wakati atakapomuona anawakandamiza maskini au hawajali wala kuwapa umuhimu wowote. Wakati ambapo tajiri huyo anaweza akasema kwamba utajiri huo ameupata kwa jasho lake na ni mali yake, lakini pamoja na hayo udhuru wake huo haukubaliki. Hii ni kwa sababu madhali amepewa utajiri, basi lazima ajue kuwa utajiri huo una majukumu yake ambayo anapaswa kuyatekeleza.

Juu ya ukurasa

Kwenda Sambamba na Wakati

Mimi katika masuala ya sinema na sanaa za kuigiza na za picha huenda nisiwe na welewa wa kutosha juu yake, lakini si maamuma katika masuala ya tungo za kishairi na riwaya na visa. Kama hata hivi sasa mtaaiangalia fasihi za Sovieti basi haraka na bila ya kuchelewa mtaona kwamba kuna pazia katikati yake, yaani kuna ukingo na kigingi katikati yake. Katika pande zote mbili zinazotenganishwa na ukingo huo katika fasihi hiyo, kuna kazi kubwa kubwa zimefanyika. Lakini wakati unapoangalia kazi za mwandishi Sholokhov au Alexei Tolstoy utaona kuwa zina ladha nyingine. Huyu Alexei Tolstoy ni mwandishi bingwa kabisa na ameandika riwaya nzuri sana. Ni miongoni mwa waandishi wa Mapinduzi ya Sovieti na ndani ya maandishi yake kuna ladha ya zama mpya. Kwani ni kweli katika kitabu cha “Vita na Amani” cha Leo Tolstoy unaziona athari za taifa la Urusi, lakini huwezi kuziona athari za miaka 60 ya hivi karibuni ndani yake. Uandishi wake unahusiana na kipindi maalumu bali hiyo ni athari nyingine kabisa na kamwe haihusiani na sehemu nyingine. Sasa ni kitu gani kinachoonesha shakhsia ya leo ya Urusi? Ni hizi athari za Sholokhov na ni hizi athari za Alexei Tolstoy. Hivyo msanii wa kila zama kazi zake huhusiana na zama zake kwani msanii ambaye ameishi katika zama tofauti na asijue atumie vipi kalamu yake kulingana na zama anazoishi, huyo si msanii, kwani kazi zake haziwezi kuhusishwa na zama alizomo ndani yake.

Nahisi ni vyema nitumie mfano hai ili niweze kukufafanulieni kwa vizuri zaidi na kwa ukamilifu jambo hilo. Mimi kuna wakati nilisoma kitabu cha riwaya kinachoitwa “Moyo wa Mbwa” kilichotungwa na mwandishi wa Kirusi. Riwaya hiyo ni ya kubuni ya kielimu lakini kamwe haikuwa ni sanaa ya zama hizi, bali ni kama vile ilikuwa imenukuliwa kama ilivyo kutoka sanaa za huko nyuma. Siwezi kusema kuwa imenukuliwa kutoka katika athari za Marekani, Uingereza au Ufaransa, lakini ni wazi kuwa sanaa hiyo inahusiana na kipindi cha kabla ya Mapinduzi (ya Urusi) ya mwezi Oktoba na wala si athari za zama hizi. Riwaya hiyo ni fupi, lakini usanii uliotumika ndani yake ni wa hali ya juu. Riwaya hiyo pia imetarjumiwa nchini Iran na imechapishwa lakini riwaya hiyo ya “Moyo wa Mbwa” ni ya kupinga fikra za mapinduzi na iliandikwa imam mwaka 1925 au 1926 yaani mwanzoni kabisa mwa mapinduzi ya Urusi. Mwandishi katika riwaya hiyo anapinga na kulalamikia mapinduzi hayo na baadhi ya mambo yake kiasi kwamba hata anayakejeli na kuyafanyia tashtiti istihzai mapinduzi hayo. Huo ni mfano wa baadhi ya athari kama hizo tulizozishuhudia humu nchini. Kamwe athari hiyo haikuwa sehemu ya fasihi na sanaa ya Kirusi. Riwaya hiyo ingeliweza kuenea kote ulimwenguni. Mtu hawezi kusema kuwa kulikuwa na nguvu za chuma nyuma ya pazia au ukandamizaji wa kuzuia kuenea riwaya hiyo, au haikuenea kwa sababu kilikuwa ni kipindi cha Stalin, hapana, lakini pamoja na hayo riwaya hiyo haiukuenea. Kwa nini haikutokezea kuwa moja ya athari kubwa duniani wakati ambapo “Dan Aaram” imeenea sana duniani ikiwa ni athari kubwa na imetarjumiwa katika lugha zote duniani kutokana na kuwa kwake athari ya kimapinduzi?

Juu ya ukurasa

Sanaa ya Uwajibikaji

Uwajibikaji Mbele ya Watu

Kuna baadhi ya watu wanasema kwamba kuna ukinzani na mgongano katika maneno yanayounda istilahi ya Sanaa ya Uwajibikaji. Neno sanaa lina maana ya kile kitu ambacho kinatokana na mawazo huru ya mwanaadamu, na neno uwajibikaji lina maana ya mtu kujifunga na kile ambacho anapaswa kukitenda. Sasa maneno hayo mawili yanaweza kuwa na uhusiano gani baina yake?! Wako watu wenye mawazo hayo na wanaoona haiwezekani maneno hayo mawili kukutana. Lakini ni wazi kwamba mawazo hayo si sahihi na ni makosa kufikiria hivyo. Jukumu la kuwajibika msanii liko juu ya mabega yake kwa kuwa kwake tu mwanaadamu hata kabla ya kufikiria kipaji chake cha kisanii. Ni wazi kuwa kabla ya msanii kuwa msanii, yeye kabla ya yote ni mwanaadamu. Mwanaadamu naye hawezi kusema kuwa hana majukumu wala ulazima wa kuwajibika. Jukumu la kwanza kabisa alilo nalo mwanaadamu linahusiana na wanaadamu wenzake. Ijapokuwa kuna majukumu yanayomuhusu mwanaadamu kuhusiana na maumbile, ardhi na mbingu, lakini jukumu lake kubwa ni kuhusiana na wanaadamu wenzake.

Juu ya ukurasa

Uwajibikaji Mbele ya Sanaa

Msanii ana majukumu katika pande zote, katika upande wa muundo na kalibu ya usanii wake na katika matilaba na shabaha. Mtu mwenye gawio na kipaji cha sanaa, hapaswi kutosheka na daraja ya chini. Hilo ni jukumu na ni jambo la wajibu. Msanii mvivu na asiyewajibika na ambaye hafanyi idili ya kukuza kipaji na kazi zake za kisanii, bila ya shaka yoyote atakuwa hakutekeleza wajibu wake wa kisanii katika upande wa muundo na kalibu yake. Ni jukumu la msanii kuwajibika na kufanya juhudi bila kuchoka katika kazi zake. Tab’an inawezekana baadhi ya wakati mtu akafanikiwa kufikia katika hatua ambayo hawezi kwenda mbele zaidi ya hapo wala kufanya juhudi zaidi ya hizo zilizo nje ya uwezo wake – hilo si neno – lakini mtu anapaswa kuwajibika na kutimiza wajibu wake wa kunyanyua na kustawisha masuala yake ya kisanii kadiri inavyomyumkinikia. Uwajibikaji huo hauwezi kupatikana bila ya kuweko shauku na mapenzi na hisia za kuwajibikiwa na kitu ambapo hiyo shauku, mapenzi na hisia za wajibu wa kutekeleza majukumu nazo ni nguvu ambazo humwezesha mwanaadamu kutenda kazi na hazimruhusu kufanya uvivu na wala utepetevu na ugoigoi.

Juu ya ukurasa

Uwajibikaji Mbele ya Madhumuni

Kama mwanaadamu ni mwenye heshima na ni azizi, basi moyo, akili na fikra yake nayo ni azizi na ni yenye kuheshimika. Haiwi sawa kumpa mlengwa kila kitu kwa sababu tu ana kiu na yuko tayari kusikiliza maneno ya msanii. Inabidi izingatiwe vizuri ni kitu gani msanii anataka kumpatia mlengwa. Ninachopenda kukisisitizia hapa ni maadili na fadhila. Kama sijasahau, nilisoma maneno ya (Romain Rolland 26 Januari 1866 – 30 Disemba 1944 ambaye jina lake la kweli ni L Sen Zhost mwandishi wa Ufaransa) ambapo alisema kwamba kazi ya kisanii, asilimia yake moja ni ya sanaa na asilimia yake 99 iliyosalia ni maadili au kama tahadhari niseme kwamba, asilimia yake 10 ndiyo sanaa na asilimia 90 iliyosalia ni akhlaki na maadili. Lakini kama mtaniuliza mimi nitasema kwamba, kazi ya sanaa asilimia yake mia moja ni akhlaki na maadili. Wala maneno haya hayakinzani. Inabidi kazi ya sanaa ifanywe kwa kuzingatia maadili ya kisanii mia kwa mia na asilimia yake yote mia ijazwe kwa madhumuni matukufu, yenye kuleta mafunzo mazuri, yenye gharadhi na yenye kujenga. Kitu ambacho kinawagusa na kuwaumiza watu wenye uchungu katika masuala ya sanaa ni suala hilo kwamba, msanii anatumia kisingizio cha kile kinachodaiwa ni uhuru katika sanaa na kuvunja misingi ya kimaadili na kiakhlaki. Kisingizio hicho hakikubaliki kabisa na hili ni jambo muhimu sana kuzingatiwa. Hivyo uwajibikaji katika sanaa ni kitu muhimu sana.

Juu ya ukurasa

Uwajibikaji Mbele ya Tafakuri

Msanii anapaswa kujua kuwa ana jukumu mbele ya uhakika maalumu. Uhakika huo ni upi? Suala la msanii kujua yuko katika daraja gani katika upande wa tafakuri ili kwa njia hiyo aweze kuuona na kuutambua ima uhakika wote au sehemu ya uhakika huo, huo ni mjadala mwingine. Tab’an kadiri tafakuri, fikra na utambuzi wa kiakili unapokuwa mkubwa ndivyo utakavyomwezesha kutumia vizuri zaidi ule utambuzi wa ndani kabisa wa sanaa. Hafez Shirazi (mshairi maarufu wa Kiirani wa karne ya saba Hijiria) hakuwa msanii tu, bali katika tungo zake kunashuhudiwa pia mafunzo na maarifa mengi. Maarifa hayo nayo hayawezi kupatikana kwa kuwa msanii tu, bali misingi inayotakiwa ya kifalsafa na kifikra nayo inahitajika. Inabidi kuwe na kigezo, kuwe na nukta ya kukimbilia, kuwe na sehemu ya kushikilia yenye fikra kuu na aali ya kuweza kuutia nguvu utambuzi huo wa kisanii ndipo baadaye ubainishaji wa sanaa uweze kupata msukumo na nguvu. Jambo hilo inabidi lishuhudiwe katika sekta zote za sanaa. Kuanzia sanaa ya usanifu majengo hadi uchoraji na ubunifu na hadi kwenye kazi za sinema, tamthilia, ushairi, muziki na sekta nyingine za sanaa, kote huko kunashuhudiwa maana hiyo. Baadhi ya wakati mnaweza kuona jengo limejengwa kwa usanii wa hali ya juu, lakini baadhi ya wakati pia mnaweza kuona jengo lisilo na usanii wa aina yoyote ile mkahisi hakuna fikra wala tafakuri yoyote iliyotumika ndani yake. Wajenzi wa majengo hayo mawili kama watatakiwa kujenga jengo moja, bila ya shaka kila mmoja atakuja na fikra yake. Hivyo kama ujenzi wa mji fulani watapewa watu wawili wenye fikra hizo tofauti, matokeo yake yatakuwa nusu ya mji huo inatofautiana kikamilifu na nusu yake ya pili.

Juu ya ukurasa

Uwajibikaji Mbele ya Malengo

Uwajibikaji katika sanaa ni uhakika ambao inabidi kuuheshimu na kuukubali. Si sawa kufuatilia vivi hivi tu masuala ya sanaa bila ya kuwa na msukumo wala malengo maalumu au kufuatilia sanaa kwa shabaha za kutaka kufanya kitu kipya kila leo na baadhi ya wakati hata kama kitu hicho ni kibaya au kinatokana na fikra zisizo sahihi hata kidogo. Wekevu uliomo kwenye sanaa - yaani msanii kwa kawaida ana wekevu na umahiri maalumu ambao unatofautina na furaha za kawaida na hali hiyo haiwezi kushuhudiwa ila kwa msanii tu – wekevu huo utaweza kuonekana kwa sura yake halisi pale tu msanii atakapojua anafuatilia kitu gani na anataka kufanya nini kiasi kwamba msanii mwenyewe aweze kuridhishwa na kuuhisi umahiri wake katika kazi yake ya kisanii. Ili kulifanikisha hilo, inabidi kuzingatiwe maadili ya kibinaadamu na fadhila na maarifa aali ya kidini.

Juu ya ukurasa

Sanaa na Dini

Maana ya Sanaa ya Kidini

Sanaa ya kidini ni ile sanaa ambayo ina uwezo wa kuchora na kuonyesha kwa uwazi malengo matukufu ya dini na tab’an Uislamu una uadhama bora na matukufu zaidi ya kidini. Hayo ndiyo yale matukufu ambayo yanamdhaminia mwanaadamu saada, ufanisi, haki zake za kimaanawi, utukufu wake wa kibinaadamu, taqwa na ucha Mungu sambamba na uadilifu wa kijamii. Lakini hapa inabidi tuwe macho ili tusije tukachanganya baina ya sanaa ya kidini na ile sanaa kujuburisha, kukalifisha na kutoona mbali.

Sanaa ya kidini haina maana kabisa ya sanaa ya kurembesha mambo na kujidhihirisha kidini na bila ya shaka yoyote sanaa ya aina hiyo haioani na mafundisho na matakwa ya kidini. Hakuna faida yoyote ya kuweko sanaa zinazodaiwa ni za kidini mia fil mia, lakini ikawa ndani yake kumetumika maneno ya kujamilisha tu yasiyo ya kidini hata chembe. Si sahihi kufikiria kuwa sanaa ya kidini ni ile tu inayochora na kuakisi kisa cha kidini au ambayo itazungumzia suala la kidini kwa mfano kama vile kuwazungumzia watu wa dini na kadhalika. Sanaa ya kidini kwa kweli ni ile sanaa ambayo itaweza kusambaza mafundisho matukufu ya dini kwa binaadamu na kutia hima ya kuheshimiwa mafundisho ya dini hizo hususan ya Kiislamu. Sanaa ya kidini ni ile inayozifanya nyoyo safi zinazoeneza uhakika huo wa kidini ziongezeke, na fikra za kuheshimu dini ziimarike na zidumu katika nyoyo za watu. Maarifa hayo ni maarifa matukufu na makuu ya kidini. Hayo ndiyo matukufu ambayo Mitume na Manabii wote wa Mwenyezi Mungu walibeba jukumu kubwa na zito kwa ajili ya kuyaeneza katika maisha ya watu. Si sahihi hata kidogo kwetu kukaa tu na kutojali wala kushughulikia suala la kuendelea na njia hiyo tukufu ya binaadamu wasafi kabisa kati ya binaadamu wote duniani yaani Mitume na Manabii wa Mwenyezi Mungu na watu wenye ikhlasi na wapigania jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Sanaa ya kidini ni ile ambayo inaeneza maarifa hayo. Sanaa ya kidini ni ile ambayo inalitangaza suala la uadilifu kuwa ni jambo la thamani mno na hata kama mtu hatataja neno lolote la dini wala kunukuu aya ya Qur’ani na wala Hadithi yoyote ile kuhusiana na uadilifu lakini sanaa yake ikawa ni ya kushajiisha uadilifu basi hiyo itakuwa ni sanaa ya kidini. Kwa mfano hakuna ulazima wowote wa kutumika majina na vitu vya kidini katika mazungumzo na uigizaji ndani ya filamu au tamthilia ndipo filamu au mchezo huo wa kuigiza uitwe wa kidini. Hapa hakuna ulazima huo. Bali mtu anaweza kutumia njia bora kabisa za kisanii kwa ajili ya kuhamasisha na kushajiisha uadilifu katika jamii na hiyo bila ya shaka itakuwa ni sanaa ya kidini na itaweza kusemwa kuwa msanii huyo amefanya usanii wake kwa kuzingatia sanaa ya kidini.

Juu ya ukurasa

Mwelekeo wa Sanaa ya Kidini

Kuna baadhi ya watu wana fikra potofu na wana dhana kwamba mtu kuwa msanii maana yake ni kutojali maadili yoyote bora na kutozingatia kabisa masuala ya kidini. Fikra hiyo ni ghalati. Kitu ambacho kinazingatiwa mno katika sanaa ya kidini ni kuhakikisha kuwa sanaa hiyo haihudumii hata kidogo matamanio ovyo ya nafsi, machafuko, ukatili, uasherati, kubadilishwa maumbile ya mwanaadamu na kueneza mafundisho mabaya katika jamii. Uhakika wa mambo ni kuwa sanaa ni katika madhihirisho bora kabisa ya kazi ya uumbaji ya Mwenyezi Mungu. Kitu ambacho kinaonekana kina walakini katika sanaa na ambacho watu wenye busuri, hekima na muono wa mbali wamekuwa wakikikemea mara kwa mara ni kutoka sanaa katika mkondo sahihi na kuingia katika mkondo ghalati. Ni jambo baya kuipeleka sanaa upande wa hawaa za nafsi, matendo maovu na maadili duni. Lakini kama sanaa itakwenda sambamba na roho ya kidini na iwapo misingi ya dini ndiyo itakayoiongoza sanaa, basi bila ya shaka yoyote sanaa itakuwa ni maumbile bora kabisa yanayotokana na kazi ya uumbaji ya Mwenyezi Mungu.

Juu ya ukurasa

Qur’an katika Upeo wa Sanaa

Bwana Mtume Muhammad SAW alitumia njia zote hata za usanii kwa ajili ya kufikisha fikra bora ya Uislamu tena basi akiwa amejizatiti kwa chombo bora kabisa na cha fakhari kabiri na adhimu sana yaani Qur’ani Tukufu. Moja ya siri za mafanikio makubwa ya Qur’ani Tukufu, ni sanaa kubwa iliyomo ndani ya Kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Qur’ani Tukufu ina sanaa ya upeo wa juu kabisa. Kwa hakika Qur’ani ni chimbuko na chemchemu ya sanaa bora na ya kuvutia kabisa ambapo mwanaadamu si rahisi kuweza kuidiriki kikamilifu. Kama mwanaadamu ataiangalia na kuizingatia Qur’ani Tukufu tangu awali hadi akheri na kama atafanya hivyo pia katika upande wa miongozo ya Bwana Mtume Muhammad SAW, bila ya shaka yoyote ataona kwa uwazi kabisa mawimbi ya fikra za tawhidi, uadui dhidi ya shirki na dhidi ya kuabudu masanamu na mashetani - vitu ambavyo ndiyo madhihirisho ya uovu na uwi.

Tab’an kama Mtume Muhammad SAW angelikaa na watu na kuzungumza nao lugha isiyo na sanaa, bila ya shaka asingelikosa watu wa kumsikiliza, lakini athari ya maneno na miongozo yake zisingelikuwa na ukubwa ule wa radi, mimweso, ngurumo na tufani kubwa kama ilivyoshuhudiwa. Kazi hiyo si ya maneno ya kawaida, bali hiyo ni kazi ya sanaa. Hiyo kwa hakika ndiyo faida ya kazi za usanii.

Juu ya ukurasa

Sanaa na Siasa

Kutumiwa Vibaya Sanaa Kisiasa

Siasa katika dunia ya leo inafanya ushakii wa kutumia vibaya sanaa. Kama tutasema wanasiasa hawafanyi hivyo tutaonekana hatujui yanayoendelea. Si kuwa wanasiasa wa leo tu ndio wanaotumia vibaya sanaa, bali wanasiasa wa huko nyuma pia walikuwa wakifanya vivyo hivyo. Huko nyuma kulitolewa sanadi kati ya sanadi nyingi za Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani na baadaye kutarjumiwa kwa Kifarsi. Ni sanadi na nyaraka zilizohusiana na mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 28 Mordad (Mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia) na tarjama ya sanadi hizo nikaletewa. Tab’an wakati mapinduzi hayo yalipotokea mimi sikuwa na umri mkubwa, nilikuwa na kama miaka kumi na nne au kumi na tano hivi na sikumbuki mambo mengi kuhusu mapinduzi hayo. Hata hivyo lakini nimesikia habari za mapinduzi hayo kutoka kwa watu wengi, vile vile nimesoma sehemu nyingi kuhusu mapinduzi hayo lakini sehemu zote hizo sikupata habari za tukio hilo kwa ufasaha na ufafanuzi kama ule uliomo kwenye sanadi na nyaraka hizo. Na sababu yake ni kuwa, walioandika nyaraka hizo ndio hao hao waliopanga, wakasimamia na kuendesha mapinduzi hayo na kuzituma kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani na Shirika la Kijasusi la Marekani CIA. Sanadi hizo ni za Wamarekani. Tab’an operesheni ya mapinduzi hayo ilifanywa kwa kushirikiana pamoja maafisa wa Marekani na Uingereza, na hilo limeakisiwa kikamilifu katika sanadi hizo. Amma nukta ninayokusudia kuizungumzia mimi hapa kutoka katika yale yaliyomo kwenye sanadi hizo ni kwamba, Kim Rosvelt anasema: “Wakati tulipofika Tehran tulikuwa na sanduku moja kubwa lililojaa makala mbali mbali ambazo ilibidi zitarjumiwe kwa Kifarsi kwa ajili ya kuchapishwa katika magazeti tofauti ya Iran. Tulikuja pia na michoro mbali mbali ya vikatuni!” Sasa hebu nyinyi wenyewe kaeni mufikiri ni kiasi gani CIA ilivyotumia vibaya sanaa kwa ajili ya kuangusha serikali ya kisheria ya wananchi nchini Iran. Serikali hiyo ndiyo iliyokuwa pekee ya kisheria katika kipindi cha utawala wa wafalme wa Kipahlavi na ambayo iliingia madarakani kwa kura za wananchi. Lakini serikali hiyo haikupendwa na Wamarekani kwani ilijali na kupigania maslahi ya wananchi. Wamarekani walidai kuwa serikali hiyo inaweza kuwa kama pazia la chuma la Umoja wa Kisovieti hivyo waliamua kuipindua kwa kutumia kila silaha waliyoiona ingeliwasaidia. Inaonekana Wamarekani waliona wangelikosa wachoraji wazuri wa vikatuni wa kuweza kuwatekelezea kazi yao na wa kuweza kuwaamini ndio maana waliamua kuja na vikatuni vilivyokuwa tayari vimeshachorwa tangu huko walikotoka ili kuvitumia katika mapinduzi yao hayo! Sanadi na nyaraka hizo zinaongeza kusema: “Sisi tulikitaka kitengo cha usanii cha CIA kitutayarishie vitu hivyo!” Tab’an miaka kama miwili au mitatu hivi iliyopita pia, Waitaliano waliandika kitabu ambacho kimetarjumiwa pia kwa lugha ya Kifarsi. Kitabu hicho aidha kimezungumzia kuweko kitengo maalumu cha sanaa katika Shirika la Kijasusi la Marekani CIA na ndani ya kitabu hicho mna maelezo kuhusu kazi mbali mbali zinazofanywa na kitengo hicho. Hivi ndivyo siasa inavyotumia vibaya sanaa.

Juu ya ukurasa

Sanaa Inayotumikia Ubeberu

Kwa masikitiko makubwa inabidi niseme kuwa, maadui wa Uislamu na maadui wa Iran na heshima na staha yetu huko nyuma walitumia vibaya sanaa dhidi yetu na hivi sasa pia wanaendelea kutumia vibaya kazi za kisanii. Wanatumia vibaya tungo za kishairi, michoro, visa, filamu, tamthilia na aina nyingine mbali mbali za kazi za sanaa kama silaha ya kukanyagia utukufu, kujaribu kuangamiza haki na uadhama wa kimaanawi na Kiislamu na kuwasukuma watu katika upande wa kupenda mambo ya kimaada na kidunia na kutojali kabisa masuala ya kiroho na kidini bali kuzingatia tu mahusiano ya kimaada na starehe za kidunia.

Sinema ambayo ni moja ya sanaa za kisasa zilizopiga hatua kubwa kabisa, hivi sasa inadhibitiwa na mabeberu. Taasisi kubwa kabisa na yenye uwezo mkubwa zaidi wa kutengeneza sinema duniani leo hii ni ile ya Kimarekani ya Hollywood. Mtu anapojiuliza, Hollywood inawatumikia akina nani, majibu yake huwa rahisi kuyapata. Ni rahisi kujua Hollywood inatumikia fikra gani na iko mrengo gani. Kazi ya taasisi hiyo ni kutumikia waenezaji wa ufuska na ufisadi, waenezaji wa mambo yasiyo na maana, kueneza fikra za watu wanaotaka kumvua utambulisho wake mwanaadamu, inatumikia machafuko, kuyagombanisha mataifa mbali mbali na kuwashuhgulisha watu wa matabaka ya chini katika masuala ya kipuuzi na kupoteza wakati ili matabaka ya juu ya watu yaweze kuishi kwa raha bila kusumbuliwa na matabaka ya chini. Taasisi hiyo kubwa ya sinema na utengenezaji filamu ambayo ina makumi ya mashirika na makampuni makubwa makubwa ya kutengeneza filamu, imeajiri wacheza filamu, wasanii, wasimamiaji wa sinema, waandishi na watungaji mbalimbali na kuwekeza fedha nyingi sana katika upande huo kwa shabaha ya kutumikia lengo lao maalumu. Lengo hilo ni la kufanikisha gharadhi za kisiasa za kiistikbari na kibeberu za Marekani. Suala hilo kwa hakika si asighari hata kidogo.

Hata kama wanasema kuwa sanaa inabidi isihusishwe kivyovyote vile na masuala ya kisiasa wala kuegemea upande fulani wa kisiasa, lakini matendo yao yanakwenda kinyume kabisa na maneno yao. Ukweli wa mambo ni kuwa, mabeberu duniani siku zote hizi wanatumia vibaya na kwa manufaa yao masuala ya sanaa, sinema, michezo ya kugiza, mashairi, uandishi, nathari, falsafa n.k. Naam yote hayo wanayatumia katika njia ya kufanikisha malengo yao ya kiistikbari na kupora utajiri na mali za mataifa mengine. Kama ambavyo Marekani inatumia nguvu zake za kijeshi kama nembo ya uwekezaji duniani, nguvu za kiuchumi za dola hilo la kibeberu nazo ni hayo mashirika yanayozisaidia serikali mbali mbali zinazoingia madarakani nchini Marekani. Mashirika hayo yanatumia kila njia yanayoweza kuyaonyesha mataifa mengine duniani kuwa Marekani ni kigezo cha kuigwa. Yanajaribu kuwaonesha walimwengu kuwa hawana kitu na inabidi wapate kigezo cha kufanikishia mambo yao na kigezo hicho ni Marekani.

Juu ya ukurasa

Uchumi na Sanaa

Uchumi na Sanaa

Hali ya wasanii wenyewe katika upande wa maisha yao nayo si nzuri sana hivyo, na mara nyingi hata huwa si nzuri kabisa. Hata watu ambao wanawekeza katika masuala ya sanaa huwa mara nyingi wanapokuwa wameshikamana na vitu maalumu wanashindwa hata kurudisha fedha walizowekeza. Kwa kweli inabidi kuwasaidia watu hao na kama hawakusaidiwa huamua kufanya jambo lolote lile litakaloweza kuwadhaminia fedha za kuweza kuendelezea kazi zao. Lililo muhimu kwao wakati huo ni kupata watazamaji wengi zaidi na tab’an jambo hilo si kwamba ni zuri wakati wote. Kukimbilia kwenye mambo ya kifuska, kueneza fikra za maingiliano haramu ya kijinsia na mambo kama hayo katika utengenezaji filamu ni jambo ambalo kwa kiasi fulani linafanyika kwa lengo la kufanikisha fikra hiyo ya kuvutia watazamaji wengi zaidi. Lakini msanii hapaswi kumpa kijana kitu ambacho kitamsukuma kwenye ufuska na ufisadi. Kufanya hivyo kunakwenda kinyume kabisa na fikra ya kumfanya mtu awe huru kuamua na kuchagua anachotaka. Masuala ya kuchochea fikra za watu hayampi mtu uhuru wala fursa ya kufikiri na kuchukua maamuzi anayopenda. Bali humsukuma mtu moja kwa moja upande maalumu bila ya kuwa na nguvu zozote za kuamua. Inabidi kazi za kisanii zifanyike kwa sura ambayo msanii ataweza kuwaonyesha watu kazi zake za kisanii bila ya kuchochea hisia wala kufanya jambo ambalo mtazamaji atalazimika kuvutika upande wake bila ya kuwa na uhuru wa kuamua. Kama kazi ya kisanii itamvutia mtu bila ya kutumia vitu kama hivyo, hapo ndipo mtu atakapoweza kujua kuwa kazi hiyo ya kisanii imefikia kwenye kiwango bora.

Juu ya ukurasa

Mtazamo wa Kimaada juu ya Sanaa

Katika ulimwengu wa kimaada unaodhibitiwa na fikra za kupenda dunia, thamani za kimaanawi huwa hazipewi nafasi na siku zote utajiri wote wa kimaanawi unapimwa kwa fedha. Suala muhimu katika ulimwengu huo ni fedha, kwa hivyo kila kitu kinapimwa thamani yake kwa kuangalia kitaingiza kiasi gani cha fedha. Utaona inatazamwa elimu fulani itaingiza fedha kiasi gani, inaangaliwa kazi fulani ya kisanii ina uwezo wa kuingiza kiasi gani cha fedha na vitu kama hivi. Lakini hali haiko hivyo katika upande wa Uislamu. Dini ya Kiislamu haitumii vigezo kama hivyo. Hapa sitaki kusema kuwa kuna matatizo katika suala la kuweko muamala wa kubadilisha elimu, sanaa na maliasili nyingine za kimaanawi kwa fedha. Hapana, kwani elimu ni njia ya kuwa na maisha bora, sanaa ni chombo cha kuwa na ustawi katika maisha. Kuweko miamala kama hiyo hakuna tatizo lakini pamoja na kuwepo miamala hiyo, maliasili zenyewe hizo za kimaanawi zina hadhi na heshima kubwa katika Uislamu. Yaani msanii hata kama watu hawatakuwa wanajua kazi zake za kisanii na hata kama hakutakuwa na mtu yeyote atakayekuwa anatumia usanii wake, lakini bado Uislamu utakuwa unamuheshimu na kumuhesabu kuwa kiumbe cha thamani katika upande wa kimaanawi. Inawezekana kwamba katika jamii fulani kutokana na umaskini au ukosefu wa uzoefu watu wasiweze kuonesha uwezo na vipaji vyao vya kisanii au kuwekeza inavyotakiwa katika suala hilo, lakini kuweko wasanii tu katika jamii hiyo ni jambo linalothaminiwa sana na Uislamu. Hali hiyo inashuhudiwa katika jamii nyingi duniani. Lakini suala hilo la kukosekana uwekezaji na vitu kama hivyo, halipaswi kufanywa kuwa sababu ya kuzuia kuchemka vipaji vya kielimu na kisanii katika jamii.

Juu ya ukurasa

 
< Nyuma   Mbele >

^