Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Dondoo za Miongozo ya Walii Amr wa Waislamu Kuhusu mwamko wa Kiislamu Chapa
01/02/2011

 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, mwaka jana alionana na makundi ya wanamapambano wa Kipalestina na kuzungumza nao kuhusu masuala mbali mbali ya kieneo na kimataifa. Miongoni mwa miongozo aliyoitoa katika mazungumzo hayo ni kwamba, ni jambo lisilo na shaka kuwa kwa mujibu wa matukio ya uhakika yaliyokadiriwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mashariki ya Kati mpya itaundika katika eneo na kwamba Mashariki ya Kati hiyo itakuwa ni Mashariki ya Kati ya Kiislamu.
Kutokana na matukio yanayoendelea hivi sasa nchini Misri, tumeona ni vyema tukuandalieni makala maalumu wasomaji wa mtandao huu wa Ayatullah Udhma Sayydi Ali Khamenei ikiwa ni katika kutupia jicho matukio yanayotokea hivi sasa katika nchi za Kiislamu za Mashariki ya Kati na kuyapima na miongozo ya Walii Amr wa Waislamu.
Katika sehemu hii nyingine ya makala hii tutatoa dondoo za hotuba za Ayatullah Udhma Khamenei kuhusiana na mwamko wa Kiislamu.

***

Hasira na Chuki za Wananchi wa Mashariki ya Kati dhidi ya Marekani
Hivi sasa tuko kwenye kipindi nyeti sana. Kama nitataka nikuelekezeni japo kidogo kuhusu mtazamo wangu juu ya hali hiyo - ambapo tab'an pengine itashindikana kutolea ushahidi mtazamo huo kwani muda wa kutoa maelezo hayo ni mchache - ninaweza kusema tu kuwa, hivi sasa vituo vya kibeberu duniani viko katika hatua za kukata roho na vinafanya juhudi zao za mwisho katika kukabiliana na harakati ya Kiislamu ambayo mfano wake wa wazi kabisa ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Juhudi na mipango yao imeshindwa katika mwahala mwingi na hivi sasa mabeberu wameemewa hawajui cha kufanya. Huu mkanda ambao mabeberu wameuzungusha kwenye masuala ya kimataifa umekatikia pabaya, umekatika katika sehemu nyeti zaidi dunianini nayo ni Mashariki ya Kati au pengine umelegea katika eneo hili. Kwa uchache mtu hawezi kukanusha kuwa umelegea, lakini kwa mtazamo wangu ni kuwa mkanda huo umekatika kabisa na wameemewa hawajui cha kufanya.
Kwa mtazamo wangu, leo hii mfumo wa kibeberu umekumbwa na hali hiyo katika kukabiliana na harakati ya Kiislamu. Mfumo huo umepoteza haiba yake kwani walimwengu leo hii tena wameshazijua hila na ujanja wao uliopitwa na wakati wanaotumia kuwapumbaza walimwengu. Leo hii hasira za wananchi katika jamii ya Marekani zinazidi kuongezeka dhidi ya ushawishi wa lobi zenye nguvu za Kizayuni nchini mwao. Tab'an viongozi na watawala nchini Marekani wanawashinikiza sana watu - naam, wanatumia namna maalumu ya kuwashinikiza wananchi - na wanawashughulisha wananchi na matatizo ya maisha kiasi kwamba wanashindwa hata kufurukuta lakini pamoja na hayo chuki na hasira za wananchi dhidi ya lobi za Kizayuni zinazidi kuongezeka. Habari hizi ninazozitoa ni za ukweli kabisa. Katika nchi za Ulaya pia, hasira za wananchi dhidi ya Wazayuni zinajitokeza kwa sura nyingine. Kwa upande wa nchi za Kiislamu usiseme, mambo yako wazi kabisa. Kwa upande wa nchi za Mashariki ya Kati ndio kabisa, hasira za wananchi dhidi ya Wazayuni ni kubwa zaidi. Watu wananchi chuki, wana hasira dhidi ya utawala wa Marekani na majimui ya tawala za kibeberu duniani. Hali hii nayo hawawezi kukabiliana nayo. Wanajaribu kuondoa hali hiyo, lakini wameshindwa.
(Sehemu ya hotuba aliyoitoa Ayatullah Udhma Khamenei mbele ya wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Iran tarehe 23/6/2010).
Soma hotuba kamili

Hawawezi Kuidhibiti Hali ya Mambo
Upande huu (wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) hivi sasa umeimarika zaidi ikilinganishwa na miongo mitatu iliyopita, umepata uzoefu mkubwa zaidi, umekuwa makini zaidi, mbinde zeke zimeongezeka sana na katika upande wa pili, adui amezidi kuwa dhaifu...
Leo hii hawawezi kufanya chochote tena, hawana hila za kufanya chochote, yaani hawawezi, hakuna uwanja wa kuwawezesha kufanya kitu na wala si kwa kuwa hivi sasa wamekuwa wema au wamekuwa na tabia njema, hapana, bali ni kwa sababu wanaona hakuna wanaloweza kufanya, wanaona kwamba mrengo huu adhimu unazidi kuimarika na kupata nguvu siku baada ya siku. Magharibi leo hii - nukta hii ni muhimu hapa - inaona kwamba ubeberu na mabavu yake iliyokuwa nayo huko nyuma yanalegalega yaani haya mataifa ya Magharibi na ya kibeberu ambayo katika siku za huko nyuma yalikuwa yanafanya yanavyotaka katika nchi za Kiislamu na za Kiarabu bila ya kizuizi chochote, leo hii yanahisi kwamba hayawezi kufanya tena chochote.
Wimbi hili la Kiislamu limeyafanya madola hayo yalazimike kuangalia upya vitendo vyao; hali imekuwa ngumu sana kwao. Katika baadhi ya nchi ambazo utegemezi wao kwa Magharibi unaonekana wazi zaidi - wananchi wa nchi hizo hilo wanalijua na hawaridhiki nalo - katika nchi hizo pia mabeberu wanataka warekebishe mambo lakini hawawezi, njia imefungwa mbele yao. Hiyo ndiyo hali inayoyakabili madola ya Magharibi hivi sasa.
(Sehemu ya miongozo ya Ayatullah Udhma Khamenei aliyoitoa tarehe 16 Septemba 2010 wakati alipoonana na wajumbe wa Baraza la Wanazuoni wanaomchagua Kiongozi Muadhamu).

Hii ni Tofauti na Kuingilia Masuala ya Ndani ya nchi Nyingine
Imam Khomeini alikuwa anaihesabu harakati na mwamko huu kuwa ni wa kimataifa. Alikuwa anasema kuwa Mapinduzi haya ni mali ya mataifa yote ya Kiislamu, bali pia na mataifa yasiyo ya Kiislamu. Imam hakuwa na wasiwasi hata kidogo na jambo hilo. Dhana hiyo inatofautiana kikamilifu na kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, kitu ambacho sisi hatufanyi. Fikra hiyo inatofautiana kabisa na suala la kupeleka nje Mapinduzi haya kwa njia za kikoloni, kitu ambacho sisi kamwe hatukifanyi, sisi si watu wa mambo kama hayo, bali maana ya fikra hiyo ni kuwa, harufu nzuri ya harakati hii ambayo ni rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu ifanywe ienee kote ulimwenguni. Mataifa ya dunia yajue jukumu lao ni nini. Mataifa ya Kiislamu nayo yajue heshima na utambulisho wao ni upi na uko wapi.
(Sehemu ya Miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa tarehe 4 Juni, 2010, katika maadhimisho ya siku ya kukumbuka alipofariki dunia Imam Khomeini (quddisa sirruh).
Soma hotuba kamili

Hatua Madhubuti za Umma wa Kiislamu
Kupanuka wimbi la mwamko wa Kiislamu duniani ni jambo la uhakika ambalo linatoa bishara ya mustakbali mwema kwa ajili ya umma wa Kiislamu. Tangu miongo mitatu iliyopita wakati wimbi hili lilipoanza kwa nguvu kubwa baada ya kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu (nchini Iran) taifa letu limekuwa likipiga hatua mbele kila kukicha na limeweza kuondoa vizuizi mbele yake na kufanikiwa kupata ushindi mkubwa katika medani mbali mbali.
Mbinu za maadui mabeberu zimezidi kuwa tata hivi sasa na wametenga fedha nyingi sana kwa ajili ya kukabiliana na Uislamu. Yote hayo yanatokana na kuwa, maaadui hawapendi kuona umma wa Kiislamu ukipata maendeleo. Adui anafanya propaganda kubwa za kueneza chuki dhidi ya Uislamu, anafanya hila mbali mbali za kuzusha hitilafu na mizozo kati ya makundi ya Kiislamu sambamba na kupalilia taasubu na utesi wa kimadhehebu, kuzusha uadui bandia kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni, kuchochea kitali na ugomvi kati ya tawala za nchi za Waislamu, kujaribu kushadidisha hitilafu na kuzigeuza hitilafu hizo kuwa uadui usioweza kutatuka, kutumia mashirika ya kijasusi kwa ajili ya kueneza vitendo vya ufisadi na uasherati yote hayo zikiwa ni radiamali za pupa zinazoonesha kuchanganyikiwa maadui mbele ya harakati makini na hatua madhubuti za umma wa Kiislamu za kuelekea kwenye mwamko, heshima na ukombozi.
(Sehemu ya ujumbe wa Walii Amr wa Waislamu kwa Mahujaji wa Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu mwaka 1431 Hijria).
Soma ujumbe kamili

Mapinduzi Yamejitanga Nje...
Sisi leo hii hatuna haja ya kuyatangaza nje Mapinduzi haya. Mapinduzi yetu yalitangazwa mara moja na inatosha! Hivi mnavyoona kwamba leo hii katika kila kona ya dunia, imani na mapenzi ya Kiislamu yanazidi kupata nguvu ni kwa sababu nchi za Kiislamu zimeamka. Hivi mnavyoona vijana wa Kiislamu katika nchi mbali mbali wamekuwa na mapenzi makubwa na masuala mazuri ya dini yao na Qur'ani Tukufu, yote hayo ni ushahidi kwamba Mapinduzi ya Kiislamu yalijitangaza nje tangu siku ya awali kabisa ya kutokea kwake.
Sisi hatutaki baada ya kupita miaka 14 tuwe ndio kwanza tunafikiria kuyatangaza nje Mapinduzi ya Kiislamu! Mapinduzi hutangazwa mara moja na jambo hilo limeshafanyika. Wakati ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulipopatikana na habari zake pamoja na mvuto wake kuenea kote ulimwenguni, hapo Mapinduzi haya yalijitangaza yenyewe nje. Ile kazi ambayo inakukasirisheni, jambo hili ambalo linazitesa nyoyo zenu, suala hili (la kutoka nje ya Iran Mapinduzi ya Kiislamu) ambalo linakuhamakisheni, tayari limeshafanyika tangu zamani! Nyinyi pia hamuwezi kufanya chochote, na hakuna mtu mwengine anayeweza kufanya kitu. Tayari kazi imeshatendeka!
(Sehemu ya khutba za Idi ‘l-Fitr alizotoa Ayatullah Khamenei tarehe 24 Machi, 1993).

Mustakbali Mwema ni wa Umma wa Kiislamu
Siku ambayo ulipatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, tawala za mataifa ya Kiislamu na wananchi wa mataifa ya Kiislamu hususan katika nchi za Kiarabu walikuwa wanauhesabu utawala wa Kizayuni (wa Israel) kuwa ni utawala usioshindika. Lakini wakati Mapinduzi ya Kiislamu yalipopata ushindi, utawala wa Kizayuni ulilazimika kusahau na kuweka pembeni haraka ile nara na kaulimbiu yake ya Nile hadi Furati.
Mataifa ya Kiislamu - kutoka Afrika hadi mashariki mwa Asia - yamepata fikra ya kuanzisha mfumo wa Kiislamu na utawala wa Kiislamu kwa miundo mbali mbali; hakuna ulazima kwa mifumo hiyo kuwa sawa sawa kabisa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu lakini wamepata fikra ya kuwa na utawala wa Kiislamu kwenye nchi zao. Katika baadhi ya nchi wamefaulu, baadhi yao wamepata bishara njema ya kufanikiwa harakati harakati zao za Kiislamu.
(Sehemu ya miongozo ya Ayatullah Udhma Khamenei katika maadhimisho wa siku ya kufariki dunia Imam Khomeini (quddisa sirruh) 25/5/2003).

Marekani na Nguvu za Kambi ya Uislamu
Wamarekani wanajua kuwa hawana mustakbali wowote katika ulimwengu wa Kiislamu. Wanafanya kila wanaloweza kuhakikisha mwamko wa Kiislamu haupelekei kutokea harakati za kimapinduzi, wanataka kuwapangia watu wa mataifa mengine mambo wanayotaka wao Wamarekani ili kuwabakisha nyuma watu hao.
Hivi karibuni Wamarekani wamekiri kwamba laiti kama wasingeliivamia Iraq, basi utawala wa Saddam ungelipinduliwa haraka na wanaharakati wa Kiislamu nchini humo na wakati huo Wamarekani wasingeliweza kufanya chochote. Jambo hilo linawatia kiwewe na kuwaogopesha sana Wamarekani. Wanachukua hatua za pupa kutokana na woga walio nao kuhusu matokeo ya mwamko wa Kiislamu katika ulimwengu wa Kiislamu. Harakati wanazofanya Wamarekani leo hii katika eneo, hazitokani na kuwa wana nguvu sana, bali zinatokana na na kuona kuwa nguvu za kambi ya Kiislamu ni kubwa. Wamarekani wanaogopa wanapoona mwamko wa Kiislamu na harakati za Kiislamu zinazidi kupata nguvu.
(Sehemu ya Miongozo aliyotoa Ayatullah Udhma Khamenei katika Haram ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) tarehe 4 Juni, 2005).

 
< Nyuma   Mbele >

^