Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika Mkutano wa Maulamaa na Mwamko wa Kiislamu
29/04/2013

Ifuatayo ni hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Mkutano wa Kimataifa wa 'Maulamaa na Mwamko wa Kiislamu.

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Na hamdu na sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu. Na rehma na amani zimshukie Bwana wetu Muhammad al Mustafa, na Aali zake wema, na masahaba zake wateule na wenye kuwafuata wao kwa wema mpaka Siku ya Malipo.
Ninakukaribisheni wageni wapenzi na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mrehemevu azitie baraka juhudi hizi za pamoja na kuzijaalia kuwa hatua athirifu kwa ajili ya uneemevu wa Waislamu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuitikia wanaomwomba.
Maudhui ya "Mwamko wa Kiislamu" ambayo mtaizungumzia katika mkutano huu leo hii, iko kwenye nafasi ya kwanza ya faharasa ya masuala ya Ulimwengu wa Kiislamu na Umma wa Kiislamu; ni kadhia kubwa na aali mno ambayo kama kwa idhini ya Mwenyezi Mungu itabaki salama na itaendelea, itaweza baada ya muda si mrefu kuuchomozea umma wa Kiislamu na hatimaye ulimwengu wote wa wanadamu Ustaarabu wa Kiislamu.
Kile kilichoko mbele ya macho yetu leo hii na ambacho hakiwezi kukanushwa na mtu yeyote yule mjuzi na mwelewa ni kwamba hivi sasa Uislamu hauko tena pembeni ya mlingano wa kijamii na kisiasa wa ulimwengu, bali uko kwenye kitovu hasa, una nafasi ya juu na muhimu katika matukio ya dunia na unatoa mtazamo mpya katika uga wa maisha, siasa, utawala na mabadiliko ya kijamii; na katika dunia ya sasa ambayo imeacha uwanja mtupu katika uga wa kifikra na kinadharia baada ya kufeli kwa Ukomunisti na Uhuria (Uliberali), (Uislamu) unatazamwa kuwa ni kitu muhimu na chenye maana kubwa. Hii ni taathira ya kwanza kabisa iliyotokana na matukio ya kisiasa na ya kimapinduzi ya Kaskazini mwa Afrika na eneo la Kiarabu (Mashariki ya Kati) katika mlingano wa dunia, na yenyewe inatoa bishara njema ya hakika kubwa zaidi zitakazojiri katika mustakabali.
Mwamko wa Kiislamu ambao wasemaji wa kambi ya Uistikbari na ya wenye fikra mgando wanajiepusha na wanaogopa hata kuutaja kwa ndimi zao, ni hakika ambayo ishara zake hivi sasa zinaweza kuonekana takribani ulimwengu mzima. Ishara zake za wazi zaidi ni hamu kubwa ya fikra za waliowengi na hasa katika matakaba ya vijana ya kuhuisha heshima na adhama ya Uislamu na kupata uelewa wa kuitambua sura halisi ya Mfumo wa Ubeberu wa Kimataifa na kudhihirika sura isiyo na haya, ya kidhalimu na ya kiistikbari ya madola na taasisi ambazo kwa muda wa zaidi ya miaka mia mbili zillikuwa zimeushikilia na kuushindilia makucha yake yaliyotapakaa damu Ulimwengu wa Mashariki, wa Kiislamu na usio wa Kiislamu. Na kwa kujificha nyuma ya kizoro cha ustaarabu na utamaduni wakaufanya utambulisho wa mataifa kuwa mhanga wa uchu wao wa kikatili na wa kichokozi wa kupenda madaraka.
Matawi ya mwamko huu wenye baraka ni mengi mno na yenye mtawanyiko wenye siri; lakini kilichoonekana katika matunda yake ya papo kwa papo katika nchi kadhaa za Kaskazini mwa Afrika kinaweza kuzipa nyoyo hakikisho la kupatikana matunda makubwa na tija ya kina katika mustakabali. Kila mara kuthibiti kimiuijiza kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu huwa ni ishara ya matumaini inayotoa bishara ya kuthibiti ahadi kubwa zaidi. Simulizi za Qur'ani kuhusu ahadi mbili ambazo Mwenyezi Mungu alimpa mama yake Musa (AS) ni mfano wa mbinu hii ya Mola Mlezi.
Katika wakati ule mgumu ilipotolewa amri ya kulitia majini sanduku lililobeba mtoto mchanga, kauli iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu ilitoa ahadi kwamba: انّا رادّوه اليك و جاعلوه من المرسلين Hakika Sisi tutamrudisha kwako na tutamfanya miongoni mwa Mitume. (Al - Qasas, 28:7). Kuthibiti kwa ahadi ya kwanza ambayo ni ahadi ndogo zaidi iliyoupa furaha moyo wa mama ilikuwa ishara ya kuthibiti ahadi ya Utume, ambayo ilikuwa ni kubwa zaidi na tab'an iliyohitaji juhudi kubwa na subira ya muda mrefu ya kuvumilia mateso. فرددناه الى امّه كى تقرّ عينها و لا تحزن و لتعلم انّ وعد اللَّه حقّ Basi tukamrudisha kwa mama yake ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike. Na ajue ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. (Al - Qasas, 28:13). Ahadi hii ya kweli ni ile risala kubwa (ya Utume) iliyothibiti baada ya miaka kadhaa na kubadilisha mkondo wa historia.
Mfano mwengine ni ule unaokumbusha nguvu yenye kushinda ya Mwenyezi Mungu katika kuwasagasaga walioishambulia Nyumba Tukufu (Al Kaaba) ambapo Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume wake mtukufu, na ili kuwashajiisha anaowahutubu watekeleze amri wanayopewa ya kwamba: فليعبدوا ربّ هذا البيت Basi nawamuabudu Mola Mlezi wa Nyumba hii (Al Quraish: 106:3) anasema: أ لم يجعل كيدهم فى تضليل Kwani hakujaalia vitimbi vyao kuharibika? (Al Fiil: 105:2). Au katika kumpa moyo Mtume wake mpenzi na ili awe na imani na ahadi yake anasema: ما ودّعك ربّك و ما قلى Mola wako Mlezi hakukuacha, wala hakukasirika nawe. (Wadhuha: 93:3) na kwa njia hiyo kumkumbusha neema zake za kimiujiza ya kwamba: أ لم يجدك يتيما فأوى. و وجدك ضالّا فهدى (Kwani hakukukuta yatima akakupa makaazi? Na akakukuta umepotea akakuongoa? Wadhuha: 93:6 - 7). Na mifano mingine kama hii iko mingi sana ndani ya Qur'ani.
Wakati ule Uislamu ulipopata ushindi nchini Iran na ukaweza kuiteka ngome ya Marekani na Uzayuni katika moja ya nchi nyeti zaidi za eneo hili lenye umuhimu mkubwa mno, watu wenye ibra na hekima walitambua kwamba kama itakuwepo subira na basirat (uono wa mbali) utafika wakati wa kupatikana ushindi mwengine mmoja baada ya mmoja; na wakati huo ukafika.
Ukweli halisi wa matukio yenye kung'ara yanayojiri katika Jamhuri ya Kiislamu ambayo maadui zetu wanayakiri, yote hayo yamepatikana chini ya kivuli cha kuwa na imani juu ya ahadi ya Mwenyezi Mungu, subira, muqawama na kutegemea msaada wa Mwenyezi Mungu. Kila mara wananchi wetu walipokabiliwa na wasiwasi wa wenye nyoyo dhaifu katika vipindi vya hofu na wahka, waliokuwa wakitoa wito wa انّا لمدركون Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana! (Ashuaraa: 26:61) wao walipaza sauti zao juu kwa kusema: كلاّ انّ معى ربّى سيهدين Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa! (Ashuaraa: 26:62).
Leo tajiriba hii yenye thamani kubwa inaweza kutumiwa na mataifa yaliyosimama kukabiliana na Uistikbari na Udikteta na yakaweza kuziangusha au kuziteteresha tawala mbovu, za uhewalla bwana na zenye utegemezi kwa Marekani. Kusimama imara, kuwa na subira, uono wa mbali na imani juu ya ahadi ya و لينصرنّ اللَّه من ينصره انّ اللَّه لقوىّ عزيز Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anaye msaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu. (Al Hajj: 22:40) kutauwezesha Umma wa Kiislamu kuyakata masafa ya njia hii ya kujivunia hadi kufikia kwenye kilele cha Ustaarabu wa Kiislamu.
Hivi sasa katika mkutano huu muhimu ambao umehudhuriwa na majimui ya maulamaa wa umma kutoka nchi na madhehebu mbalimbali za Kiislamu, ninahisi ni mahala pake kubainisha nukta kadhaa zenye ulazima katika masuala ya Mwamko wa Kiislamu:
Jambo la mwanzo ni kwamba wimbi la kwanza la Mwamko katika nchi za eneo hili lililoanza sambamba na kuanza kuingia viranja wa Ukoloni, kwa sehemu kubwa liliongozwa na maulamaa wa dini na warekebishaji wa kidini. Majina ya viongozi na shakhsia mashuhuri kama vile Sayyid Jamaluddin, Muhammad Abdou, Mirza Shirazi, Akhund Khorasani, Mahmoud al Hassan, Muhammad Ali, Sheikh Fadhlullah, Haj Agha Nurullah, Abul A'ala Maududi na makumi ya mashekhe wengine wakubwa na mashuhuri, mujahidina na wenye ushawishi kutoka nchi za Iran, Misri, India na Iraq, yameorodheshwa na kubakia milele katika kurasa za historia.
Katika zama hizi pia jina adhimu lenye kung'ara la Imam Khomeini linaangaza mithili ya nyota yenye mwanga mkubwa kwenye kilele cha Mapinduzi ya Kislamu. Wakati huohuo kuna mamia ya maulamaa maarufu na maelfu ya maulamaa wasio maarufu pia ambao leo na jana yake wametoa mchango katika matukio ya kuleta mageuzi makubwa na madogo katika nchi mbalimbali. Orodha ya waleta mageuzi (muslihina) ya kidini kutoka matabaka ya watu wasiokuwa mashekhe kama Hassan al Banna na Iqbal Lahore nayo pia ndefu na ya kuajabiwa. Mashekhe na shakhsia weledi wa dini katika kila mahali wamekuwa merejeo ya kifikra na ngome ya subira ya kiroho kwa watu, na kila pale yalipojiri matukio makubwa wameshika nafasi ya mbele ya uongozaji. Wamekuwa mstari wa mbele wa safu za wananchi katika kukabiliana na hatari, na kuzidisha mshikamano wa kifkra baina yao na watu, na muongozo wao umekuwa na taathira zaidi katika kuwaonyesha watu njia. Kama ambavyo hali hii ina faida na baraka kwa harakati ya Mwamko wa Kiislamu, kwa kiwango hichohicho haipendezi na inawakereketa maadui wa umma na wale wenye uadui na Uislamu na wapinzani wa kutawala thamani za Kiislamu, na kwa hivyo wanajaribu kuyaondoa marejeo haya ya kifikra nje ya ngome za kidini na badala yake kuanzisha mihimili mipya ya marejeo kwa ajili ya mwamko huo ambayo kutokana na tajiriba waliyopata wamebaini kuwa yanaweza kuamiliana nao kirahisi juu ya misingi na thamani za kitaifa! suala ambalo halitotokea katu kwa maulamaa wenye taqwa na shakhsia waaminifu wa kidini.
Hali hii inalifanya jukumu walilonalo maulamaa wa dini liwe zito zaidi. Wao wanapaswa kuwa macho na makini sana; na kwa kuzing'amua mbinu na hila za hadaa za adui, kuzifunga kikamilifu njia zao za ushawishi na kuzima hila za adui. Kukaa kwenye kitanga cha marembo ya kila aina cha mapambo ya dunia ni moja ya madhara makubwa kabisa. Kujichafua kwa kujikumbatisha na kukubali kufanyiwa ihsani na wenye mali na madaraka na kukubali fadhila za mataghuti wa matamanio ya nafsi na madaraka ndio hatari kubwa zaidi itakayoleta mtengano na wananchi na kupoteza imani na mapenzi yao. Umimi na uchu wa madaraka unaowavuta wenye nyoyo dhaifu na kuwaelekeza kwenye mihimili ya madaraka ndio chanzo cha kujichafua kwa ufisadi na upotofu. Inapasa kila mara waihisi masikioni mwao aya hii ya Qur'ani isemayo: تلك الدّار الأخرة نجعلها للّذين لايريدون علوّا فى الأرض و لا فسادا و العاقبة للمتّقين Hayo ndiyo makaazi ya Akhera, tumewafanyia wale wasio taka kujitukuza duniani wala ufisadi. Na mwisho mwema ni wa wachamngu. (Al Qasas: 28: 83).
Leo katika zama za harakati zenye kutia matumaini za Mwamko wa Kiislamu, baadhi ya wakati yanashuhudiwa matukio yanayoashiria hatua za kivitendo za Marekani na Uzayuni za kutaka kuanzisha marejeo yasiyo ya kuaminika ya kifikra kwa upande mmoja, na kwa upande mwengine zinashuhudiwa harakati za Maqaruni wenye matamanio ya nafsi wenye lengo la kuwavuta na kuwaingiza watu wa dini na taqwa kwenye tapo lao chafu na lenye sumu. Maulamaa wa dini na shakhsia wenye kushika dini wanapaswa wajihadhari mno na kuwa makini.
Nukta ya pili ni ya ulazima wa kupanga malengo ya muda mrefu kwa ajili ya Mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiislamu; ambayo ni nukta aali na ya juu inayopasa kutoa muelekeo wa mwamko kwa mataifa na kuyafikisha kwenye nukta hiyo. Ni kwa kuitambua nukta hii ndipo itawezekana kuandaa ramani ya njia na kuainisha ndani yake malengo ya muda wa kati na wa karibu. Lengo hili kuu na la ghaya haliwezi kuwa kitu kingine ghairi ya "kuasisi Ustaarabu unaong'ara wa Kiislamu". Umma wa Kiislamu pamoja na uwezo wake wote ulionao katika kalibu wa wananchi wa mataifa na nchi za Kiislamu unapaswa kufikia kwenye nafasi ya ustaarabu inayotakiwa na Qur'ani. Vipimo vikuu na vya wote vya kufikia kwenye ustaarabu huu ni kufaidika wanadamu na fursa na neema zote za kimaada na kimaanawi ambazo Mwenyezi Mungu amevijaalie katika ulimwengu wa maumbile na ndani ya nafsi za wanadamu wenyewe kwa ajili ya kudhamini saada na utukukaji wao. Dhihirisho la nje la ustaarabu huo linaweza kushuhudiwa katika utawala unaotokana na wananchi, katika sheria zinazotokana na Qur'ani, katika ijtihadi na kuyapatia majibu mahitaji mapya yanayojitokeza ya mwanadamu, katika kujiepusha na fikra mgando na mitazamo finyu na vilevile bid'a na ughushi, katika kuleta ustawi na utajiri kwa jamii, katika kusimamia uadilifu, katika kujivua na uchumi unaotokana na upendeleo kwa watu maalumu, riba na ulimbikizaji mali, katika kueneza akhlaqi za kiutu, katika kutetea wanaodhulumiwa duniani na katika kufanya juhudi za uchapaji kazi na ubunifu. Kuwa na mtazamo wa ijtihadi na wa kielimu katika nyuga mbalimbali, kuanzia kwenye Sayansi Jamii mpaka kwenye mfumo rasmi wa elimu na malezi, kuanzia kwenye uchumi na mfumo wa benki mpaka kwenye uzalishaji wa kiufundi na kiteknolojia, na kuanzia kwenye mfumo wa vyombo vya habari vya kisasa mpaka kwenye sanaa na sinema pamoja na uhusiano wa kimataifa na mengineyo, yote hayo ni mambo ya lazima kwa ajili ya kujenga ustaarabu huo. Tajiriba imeonyesha kuwa haya yote ni mambo yanayowezekana na yaliyoko ndani ya uwezo wa jamii zetu. Haifai kuliangalia suala hili kwa mtazamo wa pupa au kwa jicho baya la kutokuwa na matumaini. Kuuangalia uwezo tulionao kwa jicho baya ni kukufuru neema za Mwenyezi Mungu; ni kughafilika na auni ya Mwenyezi Mungu na msaada wa kanuni za uumbaji na ni kuteleza na kutumbukia kwenye hilaki ya: الظّانّين باللَّه ظنّ السّوء "Wanaomdhania Mwenyezi Mungu dhana mbaya" (Al - Fat - h: 48:6). Sisi tunao uwezo wa kuuvunja uzio wa ukiritimba wa kielimu, kiuchumi na kisiasa wa madola ya kibeberu na kuufanya Umma wa Kiislamu kuwa kiranja wa kurejesha haki za mengi ya mataifa duniani ambayo hivi sasa yanatezwa nguvu na Waistikbari wachache.
Ustaarabu wa Kiislamu wenye vipimo vya imani, elimu, akhlaqi na jitihada endelevu unao uwezo wa kuutunukia Umma wa Kiislamu na wanadamu wote fikra za maendeleo na akhlaqi aali, na kuwa kitovu cha kujikomboa na mtazamo wa kimaada na wa kidhalimu wa ulimwengu na wa kukanyaga na kudunisha akhlaqi ambayo ndiyo misingi mikuu ya ustaarabu wa sasa wa Magharibi.
Suala la tatu ni kwamba katika harakati za Mwamko wa Kiislamu inapasa izingatiwe kila mara tajiriba chungu na ya kutisha ya kuiiga kibubusa Magharibi katika siasa, maadili, tabia na mitindo ya maisha. Nchi za Kiislamu zimesibiwa na madhara angamizi yakiwemo ya kuwa na utegemezi na kudhalilishwa kisiasa, ukata na ufakiri wa kiuchumi, kuporomoka maadili na akhlaqi na kubaki nyuma kielimu kunakoaibisha kutokana na kuiga na kufuata kwa muda wa zaidi ya karne moja utamaduni na siasa za madola ya Kiistikbari; na haya yalijiri hali ya kuwa Umma wa Kiislamu ulikuwa na historia na rekodi ya kujivunia katika masuala yote hayo.
Maneno haya yasichukuliwe kuwa na maana ya kuwa na uadui na Magharibi. Sisi hatuna uadui na kundi lolote la watu kwa sababu ya tofauti za kijiografia. Sisi tumejifunza kwa Ali (alayhis salam) ambaye amesema kuhusu wanadamu kwamba: امّا اخ لك فى الدّين او نظير لك فى الخلق "Ima ni ndugu yako katika dini au kiumbe aliye sawa na wewe". Malalamiko yetu sisi ni dhidi ya dhulma na Uistikbari, udhibiti na uchokozi, na ufisadi na upotofu wa kiakhlaqi na wa matendo ulioingizwa ndani ya mataifa yetu na madola ya Kikoloni na Kiistikbari. Hivi sasa tunashuhudia uburuzaji, uingiliaji na ubabe wa Marekani na baadhi ya wafuasi wake katika eneo unaofanywa katika nchi ambazo pepo za mwamko zimebadilika kuwa tufani ya mapambano na mapinduzi. Ahadi na waadi wao usije ukaathiri katika maamuzi na hatua zinazochukuiliwa na wenye vipawa vya kisiasa na katika harakati adhimu ya wananchi. Inapasa hapa tupate funzo pia kutokana na tajiriba za huko nyuma. Wale ambao kwa muda wa miaka kadha wa kadha nyoyo zao zilitiwa matumaini na ahadi za Marekani, na kumtii dhalimu kukawa ndio msingi wa dira na siasa zao, hawakuweza kutatua mushkili wowote wa mataifa yao au kuondoa dhulma yoyote dhidi yao na dhidi ya wengine. Kwa kusalimu amri mbele ya Marekani hawakuweza kuzuia kubomolewa hata nyumba moja ya Palestina katika ardhi ambayo ni milki ya Wapalestina. Wanasiasa na wenye vipawa wanaokubali kutekwa na vishawishi au kutiwa hofu na vitisho vya kambi ya Uistikbari na kuipoteza fursa adhimu ya Mwamko wa Kiislamu wanapaswa walihofu onyo hili la kutisha la Mwenyezi Mungu aliposema: أ لم تر الى الّذين بدّلوا نعمت اللَّه كفرا و احلّوا قومهم دار البوار. جهنّم يصلونها و بئس القرار "Je! Hukuwaona wale waliobadilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa kukufuru; na wakawafikisha watu wao katika nyumba ya maangamizo" (Ibrahim: 14:28).
Nukta ya nne ni kwamba leo moja ya vitu hatari zaidi vinavyotishia harakati ya Mwamko wa Kiislamu ni kuzusha hitilafu, na kuzigeuza harakati hizi kuwa mizozo ya umwagaji damu wa kimatapo, kimadhehebu, kikaumu na kitaifa. Njama hii inafuatiliwa hivi sasa kwa hima na uzito mkubwa na mashirika ya ujasusi ya Magharibi na Uzayuni, na kwa msaada wa dola za mafuta na wanasiasa waliojiuza, kuanzia Mashariki mwa Asia hadi Kaskazini mwa Afrika na hasa katika eneo la nchi za Kiarabu; na zile fedha ambazo zingeweza kutumiwa kwa ajili ya kuwaneemesha viumbe wa Mwenyezi Mungu, zinatumika kuzusha vitisho, ukufurishaji, mauaji ya kigaidi, utegaji mabomu, kumwaga damu ya Waislamu na kukoleza moto wa uadui utakaodumu kwa muda mrefu. Wale wanaohisi kwamba nguvu za mshikamano wa Kiislamu zinawazuia wao kufikia malengo yao maovu, njia rahisi zaidi kwao wao ya kufikia makusudio yao ya kishetani ni kuchochea hitilafu ndani ya Umma wa Kiislamu; na wamezifanya hitilafu za mitazamo katika fiqhi, Ilmul-kalam, historia na hadithi - ambalo ni jambo la kawaida na lisiloepukika - kuwa kisingizio cha ukufurishaji, umwagaji damu na kuzusha fitna na ufisadi.
Mtazamo wenye umakini kwenye uwanja wa mapigano ya ndani unaonyesha wazi kuwepo mkono wa adui nyuma ya maafa haya. Mkono huu wa kihaini, bila ya shaka yoyote unautumia kwa faida yake ujinga, taasubi na uoni finyu wa mambo ndani ya jamii zetu na kumimina petroli ndani ya moto unaowaka. Jukumu la warekebishaji na wenye vipawa vya kidini na vya kisiasa katika kadhia hii ni zito mno.
Hivi sasa Libya kwa namna moja, Misri na Tunisia kwa namna nyengine, Syria kwa namna hii, Pakistan kwa namna ile na Iraq na Lebanon pia kwa namna moja au nyingine ima zimekumbwa au zinakabaliwa na hatari ya kukumbwa na moto huu hatari. Inapasa kuchukua hadhari kubwa na kutafuta dawa. Ni kuwa na uoni mdogo wa kufikiri kama tutayahusisha yote haya na vyanzo na sababu za kiitikadi na kikaumu. Propaganda za Magharibi na vyombo vibaraka na mamluki vya habari vya eneo ni kujaribu kuonyesha kuwa vita angamizi nchini Syria vinatokana na mzozo baina ya Shia na Suni, na kwa njia hiyo kuwaandalia mazingira ya amani Wazayuni na maadui wa muqawama katika nchi za Syria na Lebanon. Haya yanafanyika ilhali pande mbili katika mzozo wa Syria si Masuni na Mashia, bali ni waungaji mkono wa muqawama dhidi ya Uzayuni na wale wanaopinga. Si serikali ya Syria ya Kishia wala si wapinzani wake wa kisekula wanaoipinga na walio dhidi ya Uislamu ni kundi la Kisuni. Ustadi pekee wa waendeshaji mchezo huu wenye maafa makubwa ni kwamba wameweza kuzitumia hisia za kimadhehebu za watu wenye uoni mdogo wa kufikiri katika kuwasha moto huu angamizi. Kwa kuutupia jicho mchezo wenyewe na waendeshaji wake katika ngazi tofauti kila mtu mwenye insafu atabainikiwa wazi na hakika ya mambo.
Hili wimbi la propaganda zinazoenezwa kuhusiana na Bahrain pia ni uwongo na hila ya kuwapumbaza watu kwa namna nyengine. Nchini Bahrain kuna wananchi walio wengi wanaodhulumiwa ambao kwa miaka na miaka wananyimwa haki ya kupiga kura pamoja na haki nyengine za msingi za wananchi, hivyo wamesimama kudai haki zao hizo. Kwa kuwa wananchi hao walio wengi wanaodhulumiwa ni Mashia, na kwa kuwa utawala wa kijabari na wa kisekula unajidai kuonyesha mielekeo ya Kisuni itakuwa sawa kweli kuufanya mzozo huu kuwa ni baina ya Shia na Suni? Wakoloni wa Ulaya, wa Kimarekani na washirka wao katika eneo, wao bila ya shaka wanataka ionekane hivyo, lakini je huu ndio ukweli halisi?
Haya ni mambo yanayowataka maulamaa wa dini na warekebishaji wa jamii wenye insafu wayataamali, wayazingatie kwa makini na kujihisi kuwa na jukumu, na ni jambo la wajibu kwa wote kufahamu malengo ya maadui ya kukuza hitilafu za kimadhehebu, za kikaumu na za kichama.
Nukta ya tano ni kwamba ili kuelewa kama harakati za Mwamko wa Kiislamu zinafuata mkondo sahihi inapasa kuchunguza misimamo ya harakati hizo kuhusiana na suala la Palestina. Tangu miaka 60 nyuma hadi hivi sasa hakuna jeraha kubwa zaidi ulilopata moyo wa Umma wa Kiislamu kama kughusubiwa nchi ya Palestina. Maafa ya Palestina, tokea siku yake ya kwanza hadi sasa ni mchanganyiko wa mauaji, ugaidi, uharibifu, kughusubiwa na kuvamiwa matukufu ya Kiislamu. Wajibu wa kusimama imara na kupambana na adui huyu mpenda vita na ghasibu ni suala lililoafikiwa na madhehebu zote za Kiislamu na kukubaliwa kwa kauli moja na harakati zote sahihi na za kweli za kitaifa. Harakati yoyote katika nchi za Kiislamu itakayoghafilika na wajibu huu wa kidini na kitaifa kwa kuridhia matakwa ya uburuzaji ya Marekani au kwa kisingizio cha kutetea hoja zisizo na mantiki isitarajie kuwa itaangaliwa kwa jicho la kuwa mwaminifu kwa Uislamu au kuwa mkweli katika madai yake ya uzalendo wa kuipenda nchi. Hapa ni mahala pa kutathminiwa. Kila asiyeikubali sha'ar ya ukombozi wa Quds Tukufu na kuliokoa taifa la Palestina na ardhi ya Palestina, au akaliweka pembeni na kuipa kisogo kambi ya muqawama, yeye ni mtu wa kutuhumiwa. Umma wa Kiislamu unapaswa kila mahala na kila wakati uzingatie vipimo na vigezo hivi vya wazi na vya msingi.
Wageni wapenzi! Kina kaka na akina dada!
Msighafilike katu na vitimbi vya adui. Kugahfilika kwetu kunatoa fursa kwa maadui zetu. Somo la Ali (alayhis salam) kwetu sisi ni hili: من نام لم ينم عنه Mwenye kulala bila ya hofu ya adui, adui hatoipoteza fursa hiyo dhidi yake. Tajiriba yetu katika Jamhuri ya Kiislamu katika suala hili pia ni yenye kutoa ibra. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran madola ya Kiistikbari ya Magharibi pamoja na Marekani ambayo kwa muda mrefu kabla ya hapo yalikuwa yamewadhibiti mikononi mwao mataghuti wa Kiirani na yakawa ndiyo yanayopanga na kuamua mustakabali wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni wa nchi yetu, lakini yakawa yameipuuza nguvu kubwa ya imani ya Kiislamu iliyokuwemo ndani ya jamii na kutokuwa na habari ya uwezo wa uhamasishaji na uongozaji wa Uislamu na Qur'ani, ghafla yalibaini mghafala uliowapata, na hapo vyombo vyao vya utawala, mashirika yao ya kiintelijinsia na vituo vyao vya kamandi vikaanza kushughulika ili kutafuta njia ya kufidia pigo kubwa la kushindwa yaliyopata.
Katika muda huu wa miaka thelathini na ushei tumejionea anuai za njama na hila. Kitu kilichoviza na kuzima hila zao ni mambo mawili makuu ya msingi: Kushikamana barabara na misingi ya Kiislamu na kujitokeza uwanjani wananchi. Mambo mawili haya ndio ufunguo wa ushindi na faraja. Jambo la kwanza linathibiti kutokana na imani ya kweli kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu, na jambo la pili linathibiti kwa baraka za jitihada zinazofanywa kwa moyo wa dhati na ubainishaji mambo kwa moyo wa ukweli. Taifa linalokuwa na imani juu ya ukweli na mapenzi ya viongozi wake hujitokeza uwanjani kwa moyo wake wote; na kila pale wananchi wanapojitokeza na kubaki uwanjani kwa azma thabiti, hakuna nguvu yoyote itakayokuwa na uwezo wa kulishinda taifa hilo. Hii ni tajiriba ya mafanikio kwa wananchi wa mataifa yote waliofanikisha kutokea Mwamko wa Kiislamu kutokana na kujitokeza kwao uwanjani.
Ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akupeni auni, msaada, uongofu na rehma zake nyinyi na mataifa yote ya Kiislamu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh .