Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Wasimamiaji na Waendeshaji wa Uchaguzi
06/05/2013

Ifuatayo hapa chini ni matini kamili ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa tarehe 06/05/2013 mbele ya wasimamiaji na waendeshaji wa Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mabaraza ya Miji na Vijiji.

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu

Ninakukaribisheni makaka na madada wote azizi; watunzaji wa amana kubwa na yenye thamani ya kitaifa na Kiislamu. Kila mtu ambaye yuko katika sehemu fulani ya majimui hii kubwa, mnapaswa kutambua kwamba, muna kazi muhimu, ya kimsingi, yenye taathira na yenye thamani na Inshallah mutabakia namna hii na mtafanya kazi zenu kwa njia bora kabisa; iwe ni waheshimiwa katika Baraza la Kulinda Katiba na majimui ya usimiaji ambao unafungamana na baraza hili, au iwe ni waheshimiwa katika Wizara ya Mambo ya Ndani na majimui ya wananchi na serikali ambayo inafungamana na majimui hii, iwe ni maafisa wa kulinda anga ya usalama (usalama wa uchaguzi) na kuhakikisha kwamba, uchaguzi unafanyika katika mazingira salama; kama kikosi cha polisi na wengine wanaohusika katika haya.
Kabla ya kuanza mazungumzo yangu mafupi katika uwanja huu, ni lazima niashirie tukio chungu lilitokea katika masiku haya; ambapo lenyewe lilikuwa ni tukio chungu na nyuma ya pazia lilikuwa na mikono ya watu wengi; nalo ni kubomolewa na kufukuliwa kaburi la Sahaba Mtukufu Hujr bin Adi (Radhi za Mwenyezi Mungu na salamu Zake ziwe juu yake) na kuvunjiwa heshima mwili wa mtukufu huyu.
Kwa hakika tukio hili ni chungu katika engo kadhaa: tukio lenyewe la kuvunjiwa heshima Sahaba ambaye ni mmoja wa masahaba wakubwa wa Mtume SAW na mfuasi wa Amir al Muminina Ali bin Abi Talib (Alayihs Swalaatu Wassalaam) na shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu na kufukua kaburi lake tukufu baada ya miaka 1400, na kisha kuutokea mwili wake mtukufu na kuuvunjia heshima ni jambo linalosikitisha na kutia uchungu na ghamu kubwa moyoni. Kando ya hilo jambo linalozidisha uchungu wa tukio hili, ni kuwepo katika Umma wa Kiislamu watu wenye fikra chafu, mgando na zilizodumaa na kubakia nyuma ambao wanakutambua kuwaenzi watu adhimu na shakhsia muhimu na wakubwa wa zama za awali za Uislamu kuwa ni shirki na ukafiri; kwa hakika kuwepo kwa fikra kama hizi za hurafa na potofu ni msiba kwa Uislamu na Waislamu. Watu hawa ndio wale ambao mababu zao walivunja makaburi ya Maimamu katika kizazi cha Mtume Muhammad (SAW) katika eneo la Baqii mjini Madina huko Saudi Arabia na kama si kusimama imara Waislamu kote duniani, basi bila shaka hata kaburi tukufu la Mtume wa Allah pia wangelivunja.
Tazameni ni fikra batili kiasi gani ya watu wenye fikra mbaya na chafu kama hizi ambao wanakutambua kwenda kwenye haram za watu adhimu na mawalii wa Mungu kwa ajili ya kufanya ziara, kuwaombea rehma za Mwenyezi Mungu na kujiombea wao wenyewe kuwa ni shirki wana fikra batili na nyoyo chafu. Inasikitisha kuona kuwa, watu hawa wanataka kuhalilisha vitendo vyao hivyo vichafu na kuonyesha kuwa ni katika majukumu ya kidini! Wakati hawa walipobomoa makaburi ya Baqii, tambueni kwamba, kila kona ya ulimwengu wa kiislamu ililalamikia kitendo hicho. Nimesema kuwa, kuanzia mashariki wa ulimwengu wa Kiislamu - kuanzia India - mpaka magharibi mwa ulimwengu wa Kiislamu watu walijitokeza na kulalamikia hilo. Watu hawa wamekuwa wakifanya vitendo hivi khabithi na vichafu na kuviona kuwa ni miongoni mwa ibada! ni fikra gani hizi ambazo hazikutambui kutii, kuwaabudu na kunyenyekea mbele ya matwaghuti hai kuwa ni shirki na wakati huo huo zinakutambua kuwaenzi watu adhimu (na shakhsia muhimu kama masahaba na mawalii wa Mwenyezi Mungu) kuwa ni shirki? Kwa hakika (watu wanapaswa kutambua kwamba) shirki ni ile inayofanywa na watu vibaraka na nyenzo za siasa na mashirika ya kijasusi na Marekani na Uingereza na wanaowatia simanzi Waislamu kwa vitendo vyao. Hili lenyewe ni msiba. Tapo ovu linalowakufurisha Waislamu na linalopewa misaada ya kifedha na isiyo ya kifedha na suhula nyingine ni moja ya misiba mikubwa na halisi kwa Uislamu. Alhamdulilahi, Mashia kila walipo duniani - iwe ni hapa (nchini Iran), Iraq, iwe ni Pakistan au katika nukta yoyote ile miongoni mwa nukta ambazo katika siku za hivi karibuni Mashia walionesha radiamali yao kuhusiana na kadhia hii - kwa hakika walionyesha kuwa wamekomaa mno kifikra.
Kwa hakika maadui wanataka kutumia mambo kama haya kwa ajili ya kuchochea moto wa fitna na mizozo kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni; lakini jamii kubwa ya Mashia na familia kubwa ya wafuasi wa Ahlul Bayt AS hawadaiki na michezo kama hii. Aidha ndugu zetu Masuni nao wamelaani vikali kitendo hiki kichafu katika kila kona ya nchi; na wao kwa hakika wameonesha kupevuka mno kifikra. Kwa hakika hii sio miongoni mwa kadhia ambazo baada ya kupita siku mbili, tatu, tano, wiki moja na wimbi la kelele kadhaa duniani kisha iachwe.
Kwa hakika radiamali na msimamo wa Waislamu kuhusu tukio hilo chungu na hatua yao ya kulaani jambo hilo inabidi iendelee vivi hivi; kwani kama watu wakubwa kielimu, wanafikra na shakhsia wa kisiasa katika umma wa Kiislamu watashindwa kutekeleza vilivyo majukumu yao, basi fitna hii haitaishia hapa; bali itakuwa ni balaa ambayo itaikumba jamii ya Kiislamu na moto wake utaongezeka siku baada ya siku. Hivyo ni lazima kuizuia fitina hii iwe ni kwa njia za kisiasa, au kupitia njia za fatuwa za kidini, au kupitia njia ya kuandikwa makala na wasomi, waandishi, wanafikra na wenye vipaji vya kifikra na kisiasa duniani.
Ni lazima kufahamu kwamba, katika hili kuna mikono ya siri ya maadui; kwa hakika hiki sio kitu ambacho mtu anaweza kukipuuza. Watu ambao wanalia na kuweka vikao vya maombolezo wanapoona athari za kale zinaharibiwa, na hata kusimama na kupigia makele kwa nguvu zao zote kitendo hicho, mbona wamenyamazia kimya kuvunjiwa heshima kote huku Sahaba huyo wa Bwana Mtume Muhammad SAW? Iwe ni asasi za kimataifa, shakhsia wa kimataifa au wanasiasa ambao wanaunga mkono nyoyo hizi pofu, wote wamenyamzia kimya kadhia ya kuvunjiwa heshima Sahaba Hujr bin Adi na kaburi lake kufukuliwa; kwa hakika hili ni jambo linaloonyesha kwamba, wanahusika pia katika hili; kadhia hii imeonyesha mikono ya watu wanaohusika katika hili.
Kwa hakika wanapaswa kutambua kwamba:
Hakika Mola wako Mlezi yupo kwenye mavizio anawavizia. (Al-Fajr 89:14). Aidha Mwenyezi Mungu anasema katika Kitabu Kitukufu cha Qur'ani kwamba: Hakika wao wanapanga mpango, Na Mimi napanga mpango (at-Tariq 86:15-16). Kwa hakika wao wanapanga mipango na Allah anapanga mipango na bila shaka mipango ya Allah ndio itakayoshinda. Mwenyezi Mungu anayaona yote haya na bila ya shaka yoyote mbinu ya Mwenyezi Mungu ya kubatilisha vitimbi vyote hivyo vya adui ni kubwa sana kwani Mwenyezi Mungu ni mbora wa kubatilisha vitimbi vya maaduni na Inshaallah atakwamisha njama zote za maadui wenye nia ya kukwamisha maendeleo ya umma wa Kiislamu na ataikwamisha harakati hii ambayo inataka kuweka mawe na vizingiti katika njia ya umoja wa umma wa Kiislamu na maendeleo pamoja na ustawi wa umma wa Kiislamu.
Suala la uchaguzi katika kipindi chote hiki cha miaka 34 limekuwa jambo muhimu na lenye kuainisha mambo kwa nchi hii na limekuwa ni kuhuisha na kufufua majimui ya harakati ya nchi yetu. Katika kipindi chote cha miaka hii, hiki kipindi cha miaka thelathini na ushei ambapo kumefanyika chaguzi hapa nchini na wananchi kuelekea katika masanduku ya kupigia kura, kila mara balaa fulani ilisukumwa na kuzuiwa iliyokuwa ikiiandama nchi hii na kila mara wananchi wa taifa hili wameweza kupulizia nguvu mpya, roho na moyo mpya katika mwili wa nchi, taifa na mapinduzi; mara hii pia 9hali itakuwa namna hiyo) ambapo uchaguzi huu ni muhimu kuliko chaguzi zilizopita; sasa ni kwa upande mmoja - kama nilivyoashiria - ni kwamba, uchaguzi wa Rais, uchaguzi wa mabaraza ya miji na katika baadhi ya maeneo kumekusanyika chaguzi kadhaa nyingine kama chaguzi ndogo na kadhalika.
Uchaguzi wa Rais ni muhimu sana, uchaguzi wa mabaraza ya miji nao una umuhimu wa aina yake. Linalopaswa kuzingatiwa hapa ni kwamba, umuhimu wa uchaguzi wa rais usiwafanye maafisa, wananchi na wenye vipawa kutoupa umuhimu uchaguzi wa mabaraza ya miji na vijiji. Hii kwamba, sisi kuanzia katika ngazi ya vijiji, miji na katika ngazi ya nchi, kazi na maamuzi tunayakabidhi kwa wananchi, ni tukio muhimu sana. Kwa hakika mambo haya ni dhihirisho la kushirikishwa kivitendo na daima wananchi 9kupewa nafasi na uwanja wa kushiriki) katika maamuzi ya nchi yao.
Nafasi na umuhimu wa Rais unaeleweka. Katiba ya nchi na sheria za hapa nchini, zimekabidhi kwa Rais na serikali yake majukumu, juhudi, suhula, bajeti na njia zote hizi za kuelekea katika malengo matukufu; hivyo basi uchaguzi wa Rais una umuhimu maradufu. Kufanyika uchaguzi hapa nchini ni miongoni mwa fakhari za Jamhuri ya Kiislamu. Siku ambayo katika nchi hii kulizungumziwa suala la uchaguzi, kuanzia mwanzoni mwa mapambano ya Mashrutiyyat (ya kupigania kuwepo utawala wa kikatiba nchini) hadi zama za Jamhuri ya Kiislamu - kabla ya maneno haya kuwa na maana - kwa hakika hakukuwahi kufanyika uchaguzi wa nchi nzima wenye hamasa kwa maana halisi ya neno uchaguzi.
Hata katika kipindi cha Harakati ya kitaifa pia, licha ya kuwa ulikuwa ni uchaguzi wa kweli, lakini haukuwa katika kiwango na hadhi ya taifa la Iran, yaani wananchi wao wenyewe waje kutoka pembe mbalimbali, kutoka vijiji vya mbali na kuja katika masanduku ya kupigia kura, wajitambue, wajifahamu na wapige kura wao wenyewe; jambo hili limetokea tu katika kipindi cha Jamhuri ya Kiislamu na Imam Khomeini (quddisa sirruh) ndiye mbunifu, mpangaji na mhandisi wa "Jengo kubwa la kushirikishwa wananchi ndani ya Jamhuri ya Kiislamu".
Kuanzia mwanzo kabisa, Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) alisisitiza kwamba, lazima kufanyike kura ya maoni haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kuainisha mfumo utakaotawala katika Jamhuri ya Kiislamu. Katika mapinduzi mbalimbali yanayotokea katika pembe mbalimbali duniani, jambo kama hili hufanyika baada ya miaka mitatu, minne, mitano na wakati mwingine zaidi; lakini katika Jamhuri ya Kiislamu, kura ya maoni ya kuainisha mfumo utakaotawala hapa nchini baada ya mapinduzi ilifanyika chini ya siku 50 baada ya ushindi wa mapinduzi na wakajitokeza watu wengi katika masanduku ya kupigia kura na kupiga kura zao.
Hii kwamba, wamepigia kura nini, ni jambo la pili; lakini kadhia ya kwanza ni kwamba, wananchi walijitokeza kwa ujudi wao wote kwa ajili ya kuchukua maamuzi na kwa ajili ya kuainisha mstari na mfumo wanaotaka utawale katika nchi yao. Hili lilikuwa jiwe la msingi lililowekwa na Alhamdulilahi hali hiyo ikaendelea. Mwanzoni mwa mapinduzi ambapo Katiba ya ilikuwa bado haijaandaliwa na ilikuwa ni lazima Baraza la Wataalamu liundwe, haikupita miezi mingi, Imam Khomeini (RA) akaliita Baraza na Mapinduzi mjini Qum. Tukaenda. Imam alizungumza kwa ukali mno akisema: Kwa nini hamchukui hatua za kuunda Baraza ili liweze kutayatisha Katiba?
Imam alikuwa akiona kwamba, mambo yanachelewa. Kwa hakika hii sifa na tabia ya Jamhuri ya Kiislamu ambayo Alhamdulillah hadi hivi sasa tabia hiyo nzuri na yenye mvuto mkubwa imelindwa na kubakia. Kuna watu wengi walikuwa wakitaka uchaguzi usiwe na mahudhurio makubwa, uakhirishwe na kusogezwa mbele, mahudhurio ya wananchi yasiwe makubwa na uchaguzi huo usiwe na hamasa - walikuwa na malengo kwa ajili ya kufanya hivi - lakini hakuweza; hadi leo hawajaweza, na baada ya hapa Inshallah kwa tawfiki na uwezo wa Mwenyezi Mungu hawataweza kufanikiwa katika malengo yao. Kwa nini watu hao wanataka kupunguza shauku ya wananchi ya kushiriki katika uchaguzi na hivyo kupunguza umuhimu wa uchaguzi huu?
Kwa sababu maadui wanafahamu kwamba, nguzo na nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu inaegemea kura za wananchi na mahudhurio yao katika medani ya uchaguzi na medani nyingine mbalimbali. Katika Jamhuri ya Kiislamu ya Kiislamu kama wananchi hawatakuwepo katika medani, Jamhuri ya Kiislamu si lolote sio chochote. Jamhuri ya Kiislamu sio viongozi kadhaa wanne mfano wa mja dhaifu kama mimi; hapana, Jamhuri ya kiislamu maana yake ni mahudhurio ya wananchi wote na taifa la Iran katika harakati jumla na ya pamoja kuelekea upande wa malengo matukufu na matumaini makubwa na ya kivitendo; hii ndio maana ya Jamhuri ya Kiislamu.
Nguvu za Jamhuri ya Kiislamu zinategemea nyoyo, upole, hekima, fikra, tabasuri, muono wa mbali na uwepo wa wananchi katika medani na lau kama nguzo hiyo muhimu isingelikuwepo, basi madola ya kibeberu na khabithi duniani, yasingeliuacha hai mfumo huu ambao kaulimbiu yake kuu ni Jamhuri ya Kiislamu. Bila shaka mnaona jinsi wanavyoamiliana na nchi ambazo ndani yake kuna harakati za Kiislamu; mnaona wanazishinikiza na mnaona jinsi wanavyozitwisha nchi hizo matakwa yao na kuzilazimisha mambo yao. Katika Jamhuri ya Kiislamu (ya Iran) mambo hayo hayajafanyika; maadui hawajaweza kufanya hayo. Maadui wanataka kuitwisha Jamhuri ya Kiislamu matakwa yao, waifanye Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni yenye kutii amri zao; kwa hakika hilo litawezekana tu pale, Jamhuri ya Kiislamu itakapokuwa dhaifu na isiyo na nguvu.
Mahudhurio ya wananchi katika medani mbalimbali yanaifanya Jamhuri ya Kiislamu izidi kupata nguvu; maadui hawataki nguvu hii iwepo; hivyo basi ndio maana wamekuwa wakifanya propaganda za kiuadui katika chaguzi zetu zote katika kipindi cha miaka yote hii. Propaganda za maadui zimekuwa zikifanyika kabla hata ya kufanyika uchaguzi hapa nchini; yaani kabla hata ya maafisa na viongozi wetu na hata vyombo vya habari na magazeti yetu kuanza kuzungumzia suala la uchaguzi, maadui huwa tayari wameshaanza kupanga mipango na mikakati yao; mara hii pia hali iko namna hii pia.
Sisi tuna taarifa kwamba, mara hii pia vyombo rasmi na vyenye kutambulika vya adui - ambapo kila mara vilipoweza vilifanya jambo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu - kwa muda sasa vimekuwa vikipanga mikakati, mipango na ratiba ili kuzifanya nyoyo za wananchi (wananchi wa Iran) zisiwe na hamu wala shauku na uchaguzi (shauku ya kushiriki katika uchaguzi); wameshaanza kufanya hivyo, tab'an, mipango yao ni mikubwa na mipana mno; wanataka kuwafanya wananchi wasijitokeze katika masanduku ya kupigia kura; wanataka wananchi wasiwe na hisa na wasishiriki katika kuiongoza nchi; wananchi wananchi wasiwe na mahudhurio katika medani; na ndio maana wanafanya njama ili kufikia lengo lao hilo.
Kwa hakika kama wananchi hawatajitokeza katika medani, basi kwa urahisi kabisa maadui wanaweza kuongeza hujuma zao mara kadhaa. Kwa hakika mahudhurio ya wananchi ndio yanayoipa kinga mfumo wa Kiislamu na nchi yetu azizi. Ni mahudhurio ya wananchi katika medani ambayo ndio yanaimarisha nguvu na uwezo wetu wa ndani: yanatupa maendeleo na ustawi, yanatuongezea muono wa mbali na kuimarisha masuala ya usimamizi na uongozi wetu wa nchi - kama ambavyo maendeleo hayo yamepatikana katika kipindi cha miaka yote hii - haya yote ni kutokana na mahudhurio ya wananchi, kutokana na hamu na shauku ya wananchi; maadui wanataka hamu na shauku hii isiwepo na ndio maana wanafanya njama za kuhakikisha kwamba, uchaguzi unapooza na kutokuwa na shauku na hamasa.
Napenda kusema kuwa, kile ambacho mtu anakifahamu kutokana na fadhila za Mwenyezi Mungu, anachokijua kutokana na hima ya wananchi hawa azizi na Inshallah kwa tawfiki na idhini ya Mwenyezi Mungu, huu uchaguzi ulioko mbele yetu, utakuwa uchaguzi bora kabisa na wenye hamasa na shauku kubwa kabisa miongoni mwa chaguzi zetu (zilizowahi kufanyika) hapa nchini Iran. Tab'an, adui anafanya njama ili kubatilisha na kuvuruga juhudi na hima ya wananchi - kama alivyofanya katika uchaguzi wa mwaka 88 Hijria Shamsia sawa na 2009 Miladia, - hii nayo ilikuwa miongoni mwa kazi za maadui; waliwashawishi na kuwachochea watu wafanye mambo kinyume na sheria, walikuwa na matarajio (malengo fulani) na wakasimama kukabiliana na mfumo kutokana na matarajio yao; hata hivyo, Alhamdulilahi kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu hawakufanikiwa.
Njia bora na ya kimsingi ya kuepusha matatizo ya uchaguzi ni kushikamana kikamilifu na sheria na kuiheshimu; hili ni jambo ambalo napenda kuwaeleza. Wananchi wote popote walipo; katika miji, vijijini, katika miji mikubwa na kila mahala, wanapaswa kufuatilia hili kwamba, kila mtu anayezungumza maneno yake basi yanapaswa kwenda sambamba na sheria; kila mtu mwenye matarajio, basi matarajio yake yanapaswa kuwa katika fremu ya sheria na kwa mujibu wa kanuni za nchi. Wale ambao katika mwaka huo (2009) walilisababishia taifa hili hasara ile na kuibebesha nchi mzigo wa gharama, laiti wangekuwa wamesalimu amri mbele ya sheria, hali ile isingetokea. Sheria imeainisha kwamba, kama mtu ana malalamiko aje na kutoa malalamiko yake kulingana na sheria na katika kalibu ya sheria. Mwaka ule hili lilielezwa; hata sisi tukalikata na kulitafadhalisha baraza heshimiwa la kulinda Katiba, liongeze muda ili kura zihesabiwe tena; tukasema kuwa, kila mwenye akili na busara atakapotaka sanduku lolote lile kura zake zihesabiwe upya, ombi lake likubaliwe na hilo lifanyike; vizuri, hawakukubaliana na hili! Waliyoyafanya hayakuwa ya kimantiki wala ya kiakili; wakaisababishia nchi gharama.
Vizuri, bila shaka nchi yetu inaweza kuyashinda mambo kama haya. Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni imara na madhubuti. Huu uharibifu, usumbufu na maudhi haya ni mambo ambayo hayawezi kuudondosha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Katika kipindi cha miaka yote hii, Jamhuri ya Kiislamu imekumbana na aina kwa aina ya siasa na wanasiasa; lakini pamoja na kuweko upinzani wote Jamhuri ya Kiislamu imeweza kuvuka vizingiti vyote hivyo na kusonga mbele; baada ya hapa pia hali itakuwa namna hii. Jamhuri ya Kiislamu haiwezi kudondoka chini kwa maneno kama haya, isipokuwa walilisababishia taifa hili gharama na hasara. Njia ya kutoisababishia nchi gharama na hasara ni kuheshimu sheria. Hizi ni nasaha zangu kwenu nyinyi waheshimiwa maafisa na wasimamiaji wa uchaguzi: Ifanyeni sheria kuwa ndio kigezo chenu. Katika kisomo cha Qur'ani Tukufu, imesomwa aya moja hapa inayozungumzia suala la kurejesha amana kwa wenyewe. Mwenyezi Mungu anasema: "Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe". (An-Nisaai 4:58).
Kurejesha amani kwa wenyewe maana yake ni kufanya mambo katika njia ya sheria; katika hatua ya kuainisha na kuchambua sifa za wagombea - iwe ni kuhusiana na mgombea wa kiti cha urais, kuhusiana na uchaguzi wa Mabaraza ya Miji na Vijiji na kuhusiana na mambo mengine ambayo yako mbele yetu - na vile vile katika hatua ya kusoma na kuchambua kura na vile vile katika hatua ya kuhifadhi kura na masanduku. Ni lazima mstari na njia ya sheria iheshimiwe na suala la kutunza amana lifanyike kwa kiwango cha juu kabisa; Alhamdulilahi mpaka leo hali imekuwa namna hii.
Ni jambo la kawaida kwamba, katika kila uchaguzi kuna watu hushindwa kufikia malengo yao - mimi sitaki kuwapa jina la walioshindwa katika uchaguzi; haipasi kutumia maneno ya mshindi na mshindwa na mfano wa istilahi kama hizo za Kimagharibi na za kimaada; kama tunaingia uwanjani kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya kutekeleza jukumu na taklifu, hakuna suala la mshindi na mshindwa - vizuri, bila shaka hawa wana malalamiko.
Hata mtu anapokwenda mbele ya hakimu, huwa namna hii. Kuna suala la kutoa hukumu katika mahakama; mtu wa upande wa pili ambaye amefanikiwa kufikia lengo lake hufurahi na upande wa pili hukosa raha; upande wa mtu ambaye ameshindwa katika kesi, hapaswi kuituhumu mahakama kwamba, imefanya mambo kinyume na haki; hapana, mahakama ni chombo kinachofanya mambo yake kwa mujibu wa sheria; lakini yeye kwa kuwa ameshindwa katika kesi hiyo husononeka. Sote tunapaswa kuvumilia na kustahmili kile ambacho kimejitkeza kwa mujibu wa sheria na kanuni; hili ni jambo ambalo watu wote tunapaswa kujifunza; hii ni subira ya kimapinduzi na huku ni kuvumilia kimapinduzi. Tuna matarajio kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu ataziongoza nyoyo katika kile ambacho ni bora kwa ajili ya nchi hii.
Usimamiaji na utekelezaji wa masuala ya nchi ni kazi kubwa; na ni kazi muhimu sana. Neno moja huwa na taathira, hatua moja ndogo au kubwa itakayofanywa na viongozi wa juu serikali - Rais wa nchi na mawaziri - huwa na taathira kubwa; serikali iko namna hii. Huduma zao kwa ajili ya nchi huwa na taathira kubwa; Mwenyezi Mungu aepushie mbali, kama itatokea kwamba, wafanye uzembe fulani, basi hatua hiyo huwa na taathira nyingi hasi. Haya ni mambo ambayo yanatufanya mimi na nyinyi ambao tunataka kuchagua tuwe makini zaidi.
Tupime suala la mtu kuwa na uwezo, maandalizi na mfungamano wake (na mapinduzi) na tuainishe chaguo letu kwa mujibu wa haya. Kama mimi na nyinyi ambao tunataka kupiga kura tutaingia uwanjani tukiwa na nia ya dhati na ya kweli na yenye ikhlasi na tukataka kuchukua uamuzi kwa ajili ya mustakbali wa nchi, Inshallah Mwenyezi Mungu Mtukufu atatupa muongozo ndani ya nyoyo zetu. Mwenyezi Mungu Mtukufu, Inshallah anaziongoza nyoyo kwa sharti kwamba, wananchi wawe katika mstari wa kutekeleza jukumu lao. Imesemwa mara chungu nzima kwamba, uchaguzi ni haki ya wananchi na vile vile ni jukumu na wadhifa wa wananchi; tunapaswa kutumia vizuri haki hiyo na wakati huo huo, kutekeleza jukumu letu kwa njia bora na inayostahiki. Uchaguzi huu una hali kama hii.
Watu ambao wanataka kutazama ustahiki na sifa za watu na kuchukua uamuzi kwa mujibu wa sifa na ustahiki wanapaswa kutazama mambo yote. Rais wa nchi anapaswa kuwa mchapa kazi, mtu wa watu, anapaswa kuwa imara, anapaswa kuwa mtu wa kuheshimu thamani, mudiri, mtu wa tadbiri na mipango na vile vile anapaswa kuwa mwenye kufungamana na sheria na kanuni - mtekelezaji wa sheria - anapaswa kuwa ni mtu mwenye kuhisi machungu ya wananchi na anapaswa kuyaona matabaka mbalimbali ya wananchi; haya ni mambo ambayo yana nafasi kwa mtu ambaye tunataka kumkabidhi ufunguo wa uendeshaji nchi. Sisi wananchi ndio wenye kuchukua maamuzi katika hili. Asitokee mtu na kusema, kura yangu moja tu ina taathira gani.
Mamilioni ya watu idadi yao hufikia kuanzia mtu mmoja. Watu wote wanapaswa kuhisi kwamba, wana jukumu na masuuliya na Inshallah waingine uwanjani. Kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu, hali itakuwa namna hii, Inshallah. Hapana shaka kuwa, usalama wa nchi, kinga ya nchi na maendeleo ya nchi huongezeka kwa kuweko mahudhurio ya kila upande na ya akthari ya wananchi na nchi hii kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu itaweza tena kupiga hatua nyingine moja mbele kuelekea upande wa malengo aali ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusonga mbele.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu ataziongoze nyoyo zetu sote, aziongoze nyoyo za maafisa wa serikali, wasimamizi wa uchaguzi na wananchi kwa ujumla na azifanye zifanye kile ambacho kinamridhisha Yeye na ambacho kina manufaa na maslahi na nchi hii.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullah Wabakaatuh.