Miongozo ya Kiongozi Muadhamu Alipoonana na Wawakilishi wa Dini za Wachache katika Majilis
26/01/2015
Ifuatayo hapa chini ni matini kamili ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran, Ayatullah Udhma khamenei aliyoitoa mbele ya wawakilishi wa jamii za wachache wa nchni Iran katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran aliokutana nao Jumatatu ya Januari 26, 2015 na kuonesha ni kiasi gani haki za watu wa jamii za wachache zinavyolindwa na kuheshimiwa nchini Iran. 
 
Bismillahir Rahmanir Rahim.
Sisi tumefundishwa na dini tukufu ya Kiislamu kwamba tunapaswa kuamiliana kwa insafu na kwa uadilifu na wafuasi wa dini nyinginezo. Hiyo ni amri na ni hukumu ya Uislamu kwetu sisi. Amma kitu ambacho kinaonekana duniani leo ni kwamba madola makubwa na tawala zinazodai kupigania insafu na uadilifu, hazifanyi insafu na uadilifu wa aina yoyote ile ila katika wigo finyu unaolinda manufaa ya siasa zao za kidhulma. Leo hii mnaona namna wanavyofanyiwa Waislamu huko barani Ulaya na Marekani. Mjadala hapa si kwamba kwa nini Waislamu wananyimwa uhuru wao wanaopaswa kuwa nao katika aghlabu ya nchi hizo (za Magharibi) bali mjadala hapa ni kwamba kwa nini Waislamu hao hawana hata usalama wa roho zao!? Kwa kweli huo ndio uhakika wa mambo. Hata hii filamu ya "(Mmarekani) mdunguaji" (Filamu ya Kimarekani iliyoanza kuoneshwa mwezi Januari 2015. Filamu hiyo imetegemea kitabu chenye jina la American Sniper kilichoandikwa na askari mdunguaji wa Marekani Christopher Scott "Chris" Kyle na imetengenezwa na Clint Eastwood. Inahusiana na tukio la kweli la maisha ya mwandishi wa kitabu hicho Chris Kyle ambaye alikuwa ni askari wa jeshi la majini la Marekani na ambaye pole pole alibadilika kuwa muuaji mkubwa katika jeshi la Marekani na akavunja rekodi ya kuua watu wengi zaidi vitani na humo anatajwa kwa jina la Mmarekani Mdunguaji (American Sniper), yaani askari anayepiga risasi watu kwa kuwadungua kwa risasi kutokea mbali kiasi cha kupata umaarufu huo. Yaani alipata umaarufu wa askari mdunguaji na Shaitan al Ramadi yaani shetani wa Ramadi Iraq! Baada ya kuonyeshwa mara chache tu, filamu hiyo imepata umaarufu mkubwa na imeteuliwa mara kadhaa kuingia katika orodha ya filamu zilizopigania kupewa zawadi ya Oscar). Hivi sasa kumezuka kelele kuhusu kitabu hicho na shirika la Hollywood (shirika la kutengeneza filamu la Marekani) nalo limekitengenezea filamu kitabu hicho ili kumshawishi kijana wa Kikristo au asiye Muislamu awanyanyase Waislamu kwa kadiri yua uwezo wake na asipoteze fursa hiyo kila anapoipata. Kimsingi filamu hiyo inahamasisha unyanyasaji dhidi ya Waislamu kwa mujibu wa habari tulizopewa, kwani sisi filamu yenyewe hatujaiona. Mbinu ya namna hiyo haikubaliwi kabisa na inapingwa vikali na Uislamu. Uislamu unahimiza mno insafu na uadilifu. Amirul Muumini (Imam Ali Alayhis Salaam) amenukuliwa akisema kuhusiana na shambulio la mji wa al Anbar (hadithi iliyonukuliwa kwenye Nahjul Balagha, khutba ya 27 ikiwa na tofauti kidogo) kwamba amesema: Nimesikia ya kwamba watu hao walioshambulia katika mji huo wameingia kwenye nyumba ya mwanamke Muislamu na mwanamke aliye kwenye dhima - asiye Muislamu yaani Myahudi au Mkristo ambaye yuko chini ya himaya ya dola ya Kiislamu) na kuwanyanyasa, kuwaudhi na kuwadhulumu. Baadaye Imam Ali AS akasema: Kama Muislamu atakufa kwa uchungu wa jambo hilo, halaumiki! Angalieni! Huyo ndiye Amirul Muumini (Imam Ali AS). Anasema kama Muislamu atakayeona maudhi, idhlali na dhulma inayofanywa na jeshi la adui ya kuingia katika nyumba ya mtu asiye Muislamu na kumdhulumu na kumdhalilisha, kama ataona hivyo na akafa kwa uchungu wa jambo hilo, basi Muislamu huyo halaumiki. Huo ndio mtazamo wa Uislamu. Ni matumaini yetu kuwa Inshaallah mambo yatafanyika hivyo na tutaendelea kutenda hivyo.
Aidha sisi hapa nchini Iran tuna kumbukumbu nzuri sana. Mimi mara nyingi nimekwenda kuzitembelea familia za mashahidi wa Kiarmania na Kiashuri (Wakristo na Mayahudi wa nchini Iran) - mwaka huu pia kwa bahati njema nimeshakwenda kuzitembelea familia kadhaa za mashahidi wa Kiarmania - kila ninapotembelea familia hizo huwa naona ni jinsi gani zilivyo na uchungu na nchi yao (ya Iran), yaani wana uchungu wa ndani ya nyoyo zao kuhusu nchi yao. Ninakumbuka pia wakati wa vita (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) kwamba, Wakristo hawa wa Kiarmania walikuja Ahwaz, nakumbuka niliona katika uwanja wa ndege kundi la watu limekusanyika, nikajiuliza hawa ni akina nani? Nikasema, hawa ni Wakristo wa Kiarmania nao wamekuja vitani kuja kusaidia kazi za kiufundi. Ikumbukwe kuwa Wakristo wa Kiarmenia (wa Iran) ni mahiri sana katika masuala ya kiufundi, injini, mashine na vitu kama hivyo. Walikuja kushirikiana na wananchi wenzao kulinda nchi yao. Marhum Chamran alistafidi nao vizuri sana. Walijitolea mali zao, walitumikia nchi yao, walifanya kazi muhimu na baadhi yao waliuawa shahidi.
Mmoja wa [watu wa] familia hizo za Wakristo wa Kiarmenia ambaye wiki hii iliyopita nilikwenda kuwatembelea nyumbani kwo, mwanawe alikuwa katika huduma za lazima jeshini (ambazo kila kijana wa kiume wa Kiirani lazima azitekeleze); aliniambia kwamba muda wa kuhudumu jeshini mwanawe huyo ulikuwa umeisha, akawa na huzuni sana kwani vita vilikuwa bado vinaendelea [akawa anasema] muda wangu wa kuhudumu jeshini umeshaisha sijui hata nifanye nini. Kisha [mzee wa mtoto huyo] akaendelea kuhadithia akisema, kwa bahati nzuri lilitoka tangazo la kwamba wale watu ambao walikuwa wamehudumu jeshini kwa miezi kadhaa - miezi mitatu au muda fulani kwa mfano - wanatakiwa waende tena kwenye medani ya vita. Anasema kijana wao huyo alifurahi sana kusikia wameitwa tena kuhudumu jeshini; bila ya kucherewa aliondoka na kurejea kwenye medani ya vita na akauawa shahidi, mwili wake ukarejeshwa nyumbani. Naam namna hivi mtu anaona hisia za dhati za wananchi wenzetu wasio Waislamu (na uchungu walio nao kuhusu nchi yao). Kwa hakika wamefanya juhudi kubwa (za kutumikia nchi yao). Namuomba Mwenyezi Mungu ajaalie mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nao uweze kutekeleza wajibu na majukumu yake ipasavyo katika nyuga hizo. Na wananchi wenzetu wasio Waislamu nao wanapaswa kuendelea kuwa na uchungu wa dhati wa nchi yao kwa maana halisi ya neno.
Muamala huu mzuri wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wasio Waislamu inabidi muuakisi na muutangaze pia nje ya nchi. Yaani wafanyeni watu ulimwenguni na watu wa ulimwengu wa Kikristo waelewe na wafahamu kwamba katika nchi ya Kiislamu kuna kuvumiliana na kuishi kwa salama baina ya watu wa dini mbali mbali kwa namna ambayo hali haiwezi kufananishwa hata kidogo na hali ilivyo katika ulimwengu huo (wa Kikristo wa Magharibi). Hebu jiulizeni, mumesikia mara ngapi katika nchi kama vile Ujerumani, vijana wenye fikra za Kinazi - ambao sasa hata wanajifakharisha kwa kuwa na fikra za Kinazi na kujipachika jina la Wanazi mambo leo - wanavyowashambulia Waislamu, wanavyoshambulia misikiti ya Waislamu, wanawapiga na kuwaua Waislamu na hawafuatiliwi kisheria na wala kuchukuliwa hatua zinazotakiwa. Au yule binti wa kike wa Kiarabu kwa mfano ambaye tuseme amevaa kilemba au niqabu, utaona wanampiga kutokana na kuvaa kwake Hijabu bali hata wanamuua na humuoni mtu yeyote hata akishughulishwa na jambo hilo au kuwafuatilia kisheria (wauaji na wanyanyasaji hao). Baadhi ya wakati utasikia wamepandishwa kizimbani na kuhukumiwa, mtu asidhani kuwa hilo suala wanalipa uzito, hapana, uhakika wa mambo ni kuwa hata kuwafuatilia kisheria huwa hawawafuatilii inavyotakiwa. Inasikitisha kuona kuwa hali ni hiyo hiyo katika maeneo mengine; hali ni hiyo hiyo huko Marekani na katika nchi na maeneo mengine. Amma cha kusikitisha zaidi ni kuona kuwa wanadai wanatetea haki za binadamu (na watu wanawaamini)! Sasa wachukue mambo hayo wayapime na hali ilivyo kwa watu wasio Waislamu nchini Iran. Wataona kuwa kitu kama hicho hakijawahi kutokea nchini Iran. Yaani haijawahi kutokezea hata mara moja Muislamu nchini Iran kumnyanyasa na kumshambulia asiye Muislamu katika kipindi chote hiki cha utawala wa Jamhuri ya Kiislamu. Hata yule kijana wa Kiislamu mwenye imani thabiti ya dini yake na ambaye hataki kuona dini yake ya Kiislamu ikichezewa hata kidogo, kamwe humuoni akiruhusu nafsi yake kwenda kumshambulia au kumnyanyasa asiye Muislamu au kufanya vitu vingine kama hivyo. Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atupe taufiki sisi na nyinyi ya kuweza Inshaallah kutekeleza ipasavyo majukumu yetu.