Miongozo ya Kiongozi Muadhamu baada ya Kupanda Mche wa Mti katika Wiki ya Maliasili
08/03/2016

Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo (Jumanne) ameshiriki katika Wiki ya Maliasili nchini Iran kwa kupanda mche wa mti na baada ya kupanda mti huo amesisitizia udharura wa kujua thamani ya miti na mimea. Matini kamili ya matamshi yake ni kama ifuatavyo:


Bismillahir Rahmanir Rahim.

Siku ya kupanda mti ni siku ya baraka kwa nchi yetu kwani mimea na miti ni baraka katika maisha ya mwanadamu. Lakini inabidi pia tuchukue tahadhari. Kwa mfano hivi sasa mimi hapa nimepanda mche mmoja na pengine kuna miche mingine itapandwa kwa maelfu, lakini wakati huo huo tunapoona misitu yetu inavamiwa, mabustani yetu ya kale yanavamiwa, hili kusema kweli ni kinyume na maslahi ya nchi yetu. Huwa ninasikia baadhi ya wakati kwamba misitu kama hiyo ya kale na yenye muundo asili wa Kiirani ilikuwepo katika misitu yetu lakini pole pole imeanza kupungua, Mtu anaingia wasiwasi kwamba kuna siku misitu hiyo ya asili ya Kiirani itapotea kabisa, hivyo inabidi misitu ilindwe vizuri, wasiruhusiwe watu kuivamia.
Naam, ni jambo zuri wananchi kuwa na tabia ya kupenda kupanda miti, lakini pia wananchi pamoja na viongozi wanapaswa kujenga tabia pia ya kulinda na kuhifadhi maeneo kijani hususan misitu, hususan maeneo ya malisho ya wanyama. Haya ni miongoni mwa majukumu yetu. Tab'an watu wengi wanaume na wanawake wanalizungumzia sana suala hili, lakini kuzungumza kwa maneno tu hakutoshi, inabidi hatua za kivitendo zichukuliwe, na badala ya kuzungumza sana, vitendo vifanyike kwa wingi.
Ni matumaini yangu Inshaallah Mwenyezi Mungu atakupeni nyote taufiki.