Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wafanyakazi
27/04/2016
Laborers meet with Ayatollah KhameneiAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumatano) ameonana na maelfu ya wafanyakazi wa sekta mbali mbali katika wakati huu wa kukaribia Mei Mosi, Siku ya Wafanyakazi Duniani. Ameitumia fursa hiyo kuishukuru jamii ya wafanyakazi nchini Iran kwa uaminifu wao na kutotetereka kwao katika kuyalinda na kuyatumikia vilivyo Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusisitizia wajibu wa kutatuliwa matatizo ya jamii ya wafanyakazi, kuimarishwa na kutiwa nguvu uzalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi, udharura wa kukabiliana vilivyo na magendo ya bidhaa na kuzuia kuingizwa nchini bidhaa ambazo mfano wake zinazalishwa pia nchini. Vile vile ameashiria namna Marekani inavyoendelea na uadui wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: Wamarekani si watu wa kuaminika hata kidogo. Hivi sasa wanang'ang'ania kuendelea kuiwekea vikwazo Iran kwa kila namna ili kwa njia hiyo wazidi kueneza chuki dhidi ya Iran na hatimaye wakwamishe njia ya mataifa mengine ya kushirikiana na Tehran sambamba na kuifanya Iran isiweze kuwa na miamala ya kiuchumi na nchi nyingine.
Aidha amegusia duru ya pili ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) wa siku ya Ijumaa wiki hii na kuwataka watu wote waliotimiza masharti ya kupiga kura washiriki kwenye duru hiyo ya pili ya uchaguzi huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameishukuru jamii ya wafanyakazi kwa jitihada zake kubwa katika kuijenga nchi na kusema kuwa, kila mtu ambaye ni mfanyakazi katika jamii, iwe ni kiongozi, au waziri, au mhadhiri wa Chuo Kikuu, au wanachuo, au wanafunzi wa vyuo vya kidini au wakurugenzi, bali kila mtu anayefanya kazi katika sekta yoyote ile, kwa hakika huwa anafanya kazi yenye thamani.
Ayatullah Udhma Khamenei amesititiza pia kuwa, kwa mtazamo wa Uislamu, kutopenda kufanya kazi, uvivu na kupoteza bure wakati bila ya kufanya kazi ya maana ni kinyume na mambo ya thamani aliyoumbwa nayo mwanadamu na kuongeza kuwa: Inabidi watu wote wanaofanya kazi katika sekta tofauti, wazingatie kuwa mbali na kutekeleza wajibu wa kuboresha utendaji kazi wao, pia waipe haki yake kamili kazi wanayoifanya na wahakikishe kuwa wanaitekeleza kwa njia bora kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kila mtu ambaye amekubali kubeba jukumu la kufanya kazi fulani nchini, anapaswa wakati na uwezo wake wote auelekeze kwenye kutekeleza kwa njia sahihi jukumu alilolichukua.
Vile vile amegusia uaminifu na kutotetereka jamii ya wafanyakazi katika kuyalinda na kuyatumikia vilivyo Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu katika kipindi chote hiki cha miaka 37 iliyopita na kusisitiza kuwa: Pamoja na kuweko matatizo ya kimaisha, lakini wafanyakazi nchini wameendelea kuwa waaminifu bila ya kuathiriwa na propaganda mbaya dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kamwe hawajawahi hawakusimama kuupinga mfumo wa Kiislamu bali muda wote wameiunga mkono na kuilinda Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameishukuru kwa dhati jamii ya wafanyakazi nchini Iran kutokana na uaminifu na muono wao wa mbali kuhusiana na masuala ya Mapinduzi ya Kiislamu na ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuashiria majukumu ya wafanyakazi na asasi za kiuchumi pamoja na majukumu ya viongozi katika kutekeleza siasa za uchumi wa kimuqawama na kuongeza kuwa: Ujumbe mkuu wa kaulimbiu ya "Uchumi wa Kimuqawama, Hatua na Vitendo" ni kwamba viongozi nchini wanapaswa kuweka mikakati maalumu ya kutekeleza vizuri na kivitendo kila kipengee cha siasa kuu za uchumi huo.
Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia pia nafasi ya jamii ya wafanyakazi nchini Iran katika utekelezaji wa siasa za uchumi wa kimuqawama na kusisitiza kuwa: Jukumu kubwa zaidi la wafanyakazi katika suala hilo ni kufanya kazi zao kwa ubora mkubwa na kwa umakini wa hali ya juu.
Vile vile amesisitizia udharura wa kupandishwa ubora wa kazi na kusema: Miongoni mwa masuala muhimu ambayo yanasaidia sana katika kupandisha ubora wa kazi za wafanyakazi ni kulipa uzito wa hali ya juu suala la kuzalisha maarifa na utaalamu na kuongeza uwezo wa kufanya kazi kiufundi na kiutalaamu wafanyakazi wa sekta tofauti ambapo Serikali ina jukumu kubwa zaidi katika kufanikisha jambo hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja jambo jengine muhimu lenye taathira kubwa katika kupandisha juu ubora wa kazi kuwa ni kudhaminiwa usalama wa kazi kwa wafanyakazi kazi na kuongeza kwamba, kudhaminiwa usalama wa kazi za wafanyakazi ni jukumu la viongozi pamoja na waajiri.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kufungwa karakana na maeneo ya uzalishaji bidhaa kuwa ni katika mambo yenye madhara makubwa na kusisitiza kuwa: Baadhi ya wakati inapofungwa karakana au aneo fulani la uzalishaji bidhaa kutokana na matatizo kama vile ya ukosefu wa fedha na suhula au kuchakaa vifaa vya kiwanda hicho na mfano wa mambo kama hayo, wakati huo mwajiri huwa hana kosa hivyo viongozi wanaohusika katika sekta na viwanda na biashara, mabenki, viongozi katika sekta ya ufundi na teknolojia na mashirika ya elimu za kimsingi, kila mmoja wao anapaswa kutekeleza vizuri jukumu lake kuepusha kutokea jambo kama hilo.
Ameongeza kuwa: Tab'an katika baadhi ya wakati kiwanda kinaweza kufungwa kutokana na baadhi ya waajiri kutumia vibaya nafasi zao kama vile kutumia usahilishaji wanaofanyiwa pamoja na mikopo katika masuala ya ujenzi badala ya uzalishaji bidhaa; na hilo linapotokea inabidi vyombo vya sheria, serikali na asasi za usalama zifuatilie ipasavyo na kwa uzito wa hali ya juu suala hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Hakuna mtu anayepinga uzalishaji wa utajiri lakini uzalishaji huo wa utajiri haupaswi kufanywa kwa mdhara ya kuiangamiza jamii ya wafanyakazi na watu maskini na wa matabaka ya chini.
Vile vile amelitaja suala la kueneza tabia ya kutumia bidhaa zinazozalishwa na wafanyakazi wa Iran, kudhaminiwa usalama na amani katika mazingira ya kazi na kuongezwa kiwango cha mishahara katika gharama za uzalishaji bidhaa kuwa ni katika mambo mengine yenye taathira katika kupandisha ubora wa utendaji kazi wafanyakazi. Amesisitiza kuwa: Inawezekana pia kustafidi na njia sahihi na vile vile uzoefu wa nchi nyingine kuhusu masuala yote hayo na kuweka mipangilio mizuri ya kuyatekeleza mambo hayo ili sambamba na kupandisha juu mori na ubora wa utendaji kazi wafanyakazi; waajiri nao wasipate hasara katika kazi na rasilimali zao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kubainisha pia haki za waajiri kwa kusema: Mwajiri na mwajiriwa katika mantiki ya dini tukufu ya Kiislamu ni watu wawili wanaokamilishana, si watu wanaokinzana.
Ayatullah Udhma Khamenei amewashukuru pia waajiri ambao wanaamua kutumia mitaji yao katika ujasiriamali na kwenye medani ya uzalishaji bidhaa badala ya kubakisha mitaji yao katika hesabu za benki licha ya kwamba katika hesabu hizo za benki huwa hakuna mashaka na wasiwasi unaokuweko kwenye medani za uzalishaji bidhaa na kuongeza kuwa: Ushirikiano wa kidugu na wa kushibana baina ya wafanyakazi na waajiri, kufanya juhudi za kurahisishia njia uwekezaji katika sekta tofauti na kuandaa uwanja wa kusafirisha nje bidhaa na kulinda haki za wasafirishaji bidhaa kwenda nchi nyingine ni miongoni mwa haki za waajiri ambazo ni wajibu zilindwe.
Aidha amewataka viongozi nchini wahakikishe kuwa wanasimamia vizuri usalama na ubora wa bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi kwani kama bidhaa zisizo salama na zisizo na ubora zitasafirishwa nje ya nchi, jambo hilo litapelekea kuharibika jina la Iran na kutoa pigo kwa sekta ya usafirishaji nje bidhaa za humu nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia mno suala la kuthaminiwa na kupewa umuhimu mkubwa bidhaa za ndani ya nchi na kuongeza kuwa: Suala la uzalishaji wa bidhaa za ndani inabidi lihesabiwe kuwa ni jambo takatifu ambalo kuliunga mkono na kulisaidia jambo hilo ni jukumu kubwa la kila mtu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amelitaja suala la kuingiza nchini bidhaa ambazo kama hizo zinazalishwa pia ndani ya nchi kuwa ni marufuku kikamilifu na kuongeza kwamba: Inabidi kuyapongeza sana yale maduka makubwa ambayo yanahakikisha kuwa hayauzi bidhaa yoyote ila zinazozalishwa ndani ya nchi na kwa hakika inabidi kuwapa heko watu hao wenye ghera na uchungu na nchi yao.
Ameongeza kuwa: Tab'an kuna na baadhi ya maduka ambayo mara nyingi ni yale makubwa na baadhi ya wakati hata yenye mfungamano na serikali huwa yanauza bidhaa za nje tu. Jambo hili ni aibu, na kimsingi maduka hayo yanawakosesha kazi wafanyakazi wa Kiirani na kustawisha hali ya wafanyakazi wa nchi nyingine.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa tabia ya kununua bidhaa za nje na kuona fakhari kuwa na bidhaa zenye nembo ya nje ya nchi akisema kuwa: Sisi tuna miamala na nje ya nchi na hilo si tatizo, lakini katika nyuga ambazo tuna bidhaa tunazozalisha ndani ya nchi, inabidi tupinge vikali kutumia bidhaa za kigeni na tulihesabu kuwa ni kinyume na haki kuuza na kutumia bidhaa za nje ambazo mfano wake zinazalishwa pia humu nchini.
Ameongeza kuwa: Tab'an sisi hatuungi mkono misimamo ya kuchupa mipaka katika uwanja huo, bali tunachosisitiza sisi ni kuwa, inabidi jambo hilo lifanyike kwa hekima na tadibiri nzuri.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mfano wa wazi wa kuingiza bidhaa za namna hiyo kwa kugusia uingizaji wa magari ya Kimarekani ndani ya Iran na kusema: Hata Wamarekani wenyewe hawapendi kununua magari hayo kutokana na gharama zake kubwa na nzito sana, sasa licha ya hali kuwa hivyo, sisi tukurupuke na kuingiza magari ya namna hiyo humu nchini na kuvisaidia viwanda vilivyofilisika vya Marekani vinavyozalisha magari ya namna hiyo!? Hili kwa hakika ni jambo la kushangaza sana.
Ameongeza kuwa: Viongozi na maafisa husika nchini wanapaswa kusimama imara kukabiliana na mashikizo ya siri wanayowekewa ili kukubali mambo kama hayo, na kamwe wasiruhusu masuala kama haya yaendelee.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amelaumu kutumiwa mabilioni ya fedha kuingiza bidhaa zisizo na ulazima wowote humu nchini kama ambavyo amegusia pia tatizo kubwa la magendo ya bidhaa za nje na kuziingiza nchini kinyume cha sheria akisema kuwa: Tumekuwa tukiwakumbusha viongozi wa serikali tofauti zinazoingia madarakani humu nchini kuhusu udharura wa kukabiliana vilivyo na tatizo hilo, na viongozi wa serikali hizo wamekuwa wakisema kuwa, kama tutapandisha kodi na kuifanya kubwa dhidi ya bidhaa hizo, magendo ya bidhaa za namna hiyo nayo yataongezeka, lakini kwa mtazamo wetu hoja hiyo haikubaliki.
Amesema, magendo ya bidhaa ni balaa na sumu kwa sekta ya uzalishaji wa ndani na huku akilaumu vikali kutochukuliwa hatua kali katika kukabiliana na jambo hilo amesisitiza kuwa: Inabidi watu wenye nguvu zaidi wapewe kazi hiyo; na serikali inapaswa kukabiliana kwa nguvu zake zote na magendo yanayofanywa kitaasisi, sambamba na kutia nguvu asasi zinazoshughulikia suala hilo.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei ameongeza kuwa: Tab'an lengo letu hasa katika kupambana na magendo ya bidhaa si kukabiliana na wafanya magendo wadogo wadogo ambao hufanya magendo ya bidhaa ndogo ndogo hapa na pale nchini, bali lengo letu hasa ni kukabiliana na wafanya magendo wakubwa ambao wanaingiza nchini makumi na mamia ya makontena ya bidhaa za magendo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria suala jengine moja muhimu sana katika uzalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi akisema: Baadhi ya wakati bidhaa fulani inaweza kuzalishwa ndani ya nchi, lakini ikakwamishwa na yule mtu anayeiingiza nchini bidhaa hiyo kutokana nje ambaye anapata faida kubwa zaidi kwa bidhaa zake hizo kulikoni bidhaa za ndani, na wakati anapoingiza bidhaa hizo kutoka nje anatumia mbinu na ujanja wa kila namna kama vile kutoa rushwa kubwa, vitisho na hata kufanya vitendo vya jinai alimradi tu ahakikishe anaikwamisha sekta ya uzalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi.
Amesisitiza kuwa: Suala hili ni muhimu sana kulishuhughlikia ipasavyo na linahusiana pia na masuala ya usalama hivyo haipasi kulidharau na kutolipa uzito unaotakiwa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea kubainisha mambo yanayoweza kukwamisha uzalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi kwa kuwalaumu watu ambao wanadai kuwa teknolojia ya uzalishaji wa bidhaa za ndani ni ya zamani ili kwa njia hiyo warahisishe njia ya kumiminwa bidhaa za kigeni nchini.
Amesema: Baadhi ya watu wanaotetea kuingizwa bidhaa za nje nchini kila wanapoishiwa na hoja wanakimbilia kusema kuwa, teknolojia inayotumiwa nje ya nchi imepiga hatua kubwa zaidi na teknolojia inayotumiwa ndani ya nchi ni ya zamani; sawa; lakini kama ni hivyo kwa nini vipaji na akili kubwa za ubunifu za Wairani hazitumiwi kutatua tatizo hilo?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuliza swali akisema: Je, akili na kipaji cha Muirani ambaye anaweza kutengeneza kombora lenye uwezo wa kupiga nukta ya shabaha kwa tofauti ya chini mita kumi tu tena baada ya kombora hilo kuvuka masafa ya kilomita elfu mbili, hawezi kutatua tatizo la teknolojia inayohitajika ndani ya nchi na kupelekea kuzalishwa bidhaa kwa teknolojia ya kisasa? Sasa kama kweli kuna tatizo kama hilo, kwa nini hawatumiwi vijana wenye uwezo mkubwa kama huo kutatua matatizo hayo?
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Baadhi ya maendeleo ya nchi ni ya siri na hayawezi kutangazwa hadharani, vinginevyo kama maendeleo hayo yangelifichuliwa basi watu wangelistaajabishwa na vipaji vikubwa vya vijana wa nchi hii.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa majumuisho ya hotuba yake hadi kufikia hapo kwa kusema: Mimi nina matumaini na mtazamo mzuri kuhusu jamii ya wafanyakazi, waajiri na viongozi serikalini, lakini uhakika wa mambo ni kuwa kuna baadhi ya sehemu mambo hayaendi vizuri na kuna baadhi ya mambo ambayo hayaruhusu juhudi zinazofanyika kuzaa matunda yanayotakiwa, hivyo viongozi wanapaswa kufanya jitihada za kugundua tatizo liko wapi na kulitatua ili kwa njia hiyo waweze kuongeza kasi ya harakati ya maendeleo ya nchi yetu.
Vile vile amesisitiza kuwa: Kuweza Iran kufikia vile vile vya juu vya ustaarabu wa Kiislamu si maneno matupu bali ni jambo la uhakika linalohitajia suhula, uwezo na kujipamba kwa sifaa maalumu za kutufikisha huko; suala ambalo kama litazingatiwa na kupewa uzito unaotakiwa, bila ya shaka yoyote litaandaa uwanja wa kufanikishwa lengo hilo kwa njia bora kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tab'an tujue kuwa, adui anayeongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni naye ataendelea kuweka vizuizi na kukwamisha mambo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Baadhi ya wakati Wamarekani wananung'unika kutokea mbali wakisema kuwa kwa nini Wairani wanatuangalia kwa jicho baya?! Tab'an jambo hilo halikuja vivi hivi, bali lina sababu zake; tunaona miamala yao na hatuwezi kuyafumbia mambo hayo yanayotufanya tuwe na mtazamo mbaya kuhusiana na Wamarekani.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, moja ya mfano wa wazi kabisa unaondaa mazingira ya kuwa mtazamo mbaya kuhusiana na Marekani ni suala la miamala yetu ya kibenki ambayo inafanyika kwa usumbufu mkubwa na kwa kuzorota sana kutokana na vizuizi vinavyowekwa na Wamarekani katika miamala hiyo ya kibenki. Ameongeza kuwa: Hivi sasa viongozi wa serikali nchini nao wanalizungumzia suala hilo la ukwamishaji unaofanywa na Wamarekani katika miamala hiyo ya kibenki, lakini cha kujiuliza ni kuwa, kwa nini mabenki makubwa duniani yanashindwa kufanya miamala na Iran?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi zaidi akisema: Sababu inayoyafanya mabenki ya dunia yakatae kushirikiana na Iran ni siasa za kueneza chuki dhidi ya Iran ambazo zimetungwa na zinaendelea kuendeshwa na Wamarekani dhidi ya Iran.
Amesisitiza kuwa: Nimekuwa nikisema mara chungu nzima kuwa Wamarekani si watu wa kuaminika, hivi sasa sababu ya maneno yangu hayo inazidi kuonekana waziwazi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia kuwa, utawaona wanaandika juu ya karatasi na kusema kwa maneno kuwa, benki za nje ziko huru kufanya miamala ya kibenki na Iran lakini wanapokuja katika vitendo wanafanya tofauti kabisa na maneno yao na wanaendesha propaganda za kueneza chuki dhidi ya Iran. Amesema: Wamarekani wanadai kuwa Iran ni nchi inayounga mkono ugaidi na hivyo imejiwekea mazingira ya kuwekewa vikwazo kutokana na kuunga mkono ugaidi.
Amesisitiza kuwa: Cha kujiuliza hapa ni kwamba, maneno hayo ya Wamarekani yanapeleka ujumbe gani kwa benki za nje zenye nia ya kuwa na miamala ya kibenki na Iran? Ujumbe unaopelekwa huko na Wamarekani ni kuziambia benki hizo kuwa msiwe na miamala na Iran na matokeo yake ni kuyaona mabenki na wewekezaji wa nje wakiogopa kushirikiana na Tehran na kuwekeza kuwekeza humu nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kusema kuwa: Tab'an kuhusu maudhui ya ugaidi, Wamarekani ni wabaya zaidi kuliko magaidi wote na kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo ni kuwa hadi leo hii Wamarekani wanawasaidia magaidi maarufu na wanaojulikana wazi duniani.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia mbinu nyingine inayotumika kueneza chuki dhidi ya Iran na namna serikali ya Marekani inavyoweka vizuizi mbali mbali vya kuzikwamisha nchi nyingine kushirikiana kibenki na kiuwekezaji na Iran na kusema kuwa: Wamarekani wanadai kuwa sababu zinazopelekea nchi nyingine zishindwe kufanya kazi na Tehran ni hali ya ndani ya Iran wakati ambapo hivi sasa hakuna nchi yoyote katika eneo hili yenye usalama na utulivu mkubwa zaidi kama Iran na tukiangalia hali ya ndani ya Iran tutaona kuwa usalama wake ni mkubwa mno kuliko nchi kama Marekani ambayo kila siku watu kadhaa wanauawa bali Iran ina usalama zaidi kuliko hata nchi za Ulaya. Kwa kweli hali ya ndani ya Iran ni nzuri sana tofauti kabisa na wanavyoota maadui wa taifa hili la Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia namna viongozi wa Marekani wanavyolikariri mara kwa mara suala la kulindwa na kuhifanyiwa muundo na mfumo wa vikwazo dhidi ya Iran na kusema kuwa, hiyo ni mbinu nyingine ya wazi inayotumika kueneza chuki dhidi ya Iran kwa ajili ya kuwazuia wawekezaji wa kigeni wasiwekeze nchini na kukumbusha kuwa: Sisi tunakabiliwa na adui wa namna hii, hivyo tunapoamua kufanya jambo lolote lile tutambue mapema kuwa tuna adui wa namna hii.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha miaka 37 iliyopita - licha ya kuweko uadui wa kila namna wa Marekani - na kusisitiza kuwa: Hata kama uadui huo utaendelea kuwepo kwa miaka mia moja mengine, maadui hao wataendelea kuumia wenyewe tu nyoyoni na kamwe hawatoweza kuzuia maendeleo hayo ya Iran.
Ameongeza kuwa: Marekani ni adui; ni sawa tu tutalisema jambo hilo hadharani au hatutalisema hadharani, na ni sawa tutautangaza uhakika huo au hatutaungaza, vyovyote tutakavyofanya, uadui huo wa Wamarekani hautaisha.
Ayatullah Udhma Khamenei amewataka viongozi wote wa Mihimili Mitatu Mikuu wa dola (Serikali, Bunge na Mahakama) pamoja na viongozi wa taasisi na asasi za Mapinduzi ya Kiislamu na matabaka mbali mbali ya wananchi, wote amewataka wajue thamani ya nchi kuwa na uwezo na nguvu katika kila sekta na kuongeza kuwa: Sisi kama ilivyokuwa kwa Amirul Muminin Ali Alayhis Salaam, ni watu tuliodhulumiwa, lakini vile vile tuna nguvu, na kama tutatumia uwezo na nguvu zetu kwa njia bora zaidi, kibinadamu zaidi na Kiislamu zaidi, basi bila ya shaka yoyote tutafanikiwa kuvuka vizuizi vyote vinavyojitokeza mbele yetu.
Vile vile amesisitiza kuwa: Njia yetu si nyepesi, lakini pia si njia iliyojaa mawe, hivyo kama tutategemea uwezo na nguvu zetu, bila ya shaka yoyote tutaweza kupata mafanikio na maendeleo makubwa zaidi.
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia duru ya pili ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) wa siku ya Ijumaa ya Aprili 29, 2016, katika baadhi ya miji ya Iran na kusema kuwa: Umuhimu wa duru ya pili ya uchaguzi huo ni sawa kabisa na umuhimu wa duru ya kwanza ya uchaguzi huo na watu wote waliotimiza masharti ya kupiga kuwa wanapaswa kushiriki kwenye zoezi hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kushiriki katika uchaguzi ni jambo muhimu mno kwani kama hatutoshiriki kwenye uchaguzi, tutashindwa kufikisha hamu, hisia na utambulisho tunaoutaka kupitia masanduku ya kura.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Waziri wa Ushirika, Kazi na Ustawi wa Jamii wa Iran ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) na kugusia pia matatizo ya wafanyakazi na watu wanaostaafu na kusema kuwa: Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na kutokana na kutegemea kaulimbiu ya kupendana na kushirikiana baina ya wafanyakazi na waajiri, tumefanikiwa kupunguza ufa uliokuwepo baina ya mfumuko wa bei na mishahara ya wafanyakazi.
Aidha Bw. Ali Rabei amezungumzia udharura wa kustawishwa na kutiwa nguvu asasi ndogo ndogo na za kati kati za kiuchumi kwa lengo la kuweka msingi wa kutia nguvu mkakati wa kupambana na umaskini kupitia kuzalisha nafasi nyingi za kazi kadiri inavyowezekana na kuongeza kuwa: Kuzitia nguvu bima, kuwaingiza ndani ya mfumo wa bima wananchi milioni 10 wasio na bima ya afya, kupambana na umaskini na ufisadi, kustawisha hali ya watoto wanaolazimika kufanya kazi, kupanua wigo wa asasi za ushirika, kupanua wigo wa matibabu katika maeneo yenye maendeleo duni, kuongeza uwezo wa kikazi wa wafanyakazi kupitia kuwaimarisha kiufundi na kimaarifa, kutunga muswada wa kuwaunga mkono na kuwasaidia watu vilema na kuwaandalia nafasi za kazi pamoja na makazi mazuri, kuanza kutekelezwa mradi wa bima za mama wa nyumbani wanaosimamia familia, kukabiliana na madhara ya kijamii pamoja na kulipa uzito wa hali ya juu suala la kulindwa heshima na shakhsia ya wafanyakazi, ni katika ratiba na kazi muhimu zinazofanywa na Wizara ya Ushirika, Kazi na Ustawi wa Jamii ya Iran.