Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Katibu Mkuu wa Jihadul Islami ya Palestina
01/05/2016
Leader meets with Ramadan Abdullah, the head of the Palestinian Islamic Jihad movementAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo jioni ameonana na Bw. Ramadhan Abdullah, Katibu Mkuu wa Jihadul Islami ya Palestina na ujumbe alioandamana nao, na metoa ufafanuzi kuhusu hali iliyopo hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na kusema kuwa, hali na matukio ya hivi sasa katika eneo hili yanaonesha kuweko njama za kambi ya Magharibi inayoongozwa na Marekani za kutaka kulidhibiti eneo hili kupitia vita vikubwa na vya pande zote dhidi ya kambi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Vita vikubwa na vvya pande zote vinavyoendelea hivi sasa katika eneo hili ni muendelezo wa vita ambavyo vilianza miaka 37 iliyopita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwamba katika mapambano hayo, kadhia ya Palestina imeendelea kuwa suala kuu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama ilivyokuwa tangu mwanzoni kabisa; hadi leo hii inalihesabu suala la kuiunga mkono Palestina kuwa ni jukumu lake, na katika siku za usoni pia itaendelea kufanya hivyo hivyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu kadhia ya Palestina tangu mwanzo haukuwa msimamo wa kupita na kamwe hautakuwa wa kupita. Ameongeza kuwa, hata kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaani katika kipindi cha mapambano, kadhia ya kuiunga mkono Palestina na ulazima wa kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel ilibainishwa wazi na tena mara kadhaa katika misimamo ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) na baada ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu pia, suala la kuwaunga mkono wananchi wa Palestina lilikuwa katika mambo ya awali kabisa tuliyoyafanya. Hivyo suala la kulinda na kutetea malengo matukufu ya Palestina ni jambo ambalo limo katika dhati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Mapinduzi ya Kiislamu yalifikia ushindi katika wakati ambao Wamarekani walikuwa na nguvu kubwa kabisa katika eneo hili na mambo yote katika dhahiri yake yalionekana kuwa yanaenda kwa maslahi ya Marekani, lakini Mapinduzi ya Kiislamu yalipuliza uhai na roho mpya ndani ya mwili wa jamiii ya Kiislamu na kubadilisha kabisa hali ya eneo hili.
Aidha amegusia mashinikizo mbali mbali na makubwa; ya kisiasa, kipropaganda, kiuchumi na hata ya kijeshi yenye lengo la kuyapigisha magoti Mapinduzi ya Kiislamu au kuufanya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ulegeze kamba katika misimamo yake na kusisitiza kuwa: Jambo ambalo linatendeka hivi sasa katika eneo hili, kwa hakika ni muemdelezo wa vita vya Marekani dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, lengo kuu la vita vikubwa vinavyoendeshwa hivi sasa na kambi ya Magharibi inayoongozwa na Marekani dhidi ya kambi ya Kiislamu, ni kutaka kulidhibiti eneo hili kwa kutumia vita. Amesema: Inabidi matukio yanayojiri katika eneo hili yaangaliwe na yachunguzwe na kutathminiwa kwa mtazamo huo na kwamba kadhia ya Syria, Iraq, Lebanon na Hizbullah ni sehemu ya vita hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, kwa kuzingatia hali ilivyo hivi sasa, suala la kuilinda na kuinga mkono Palestina linapaswa kuhesabiwa kuwa ni nembo ya kuulinda Uislamu na kuongeza kuwa: Kambi ya kiistikbari imefanya njama kubwa za kujaribu kuonesha kuwa vita vilivyopo hivi sasa katika en0eo hili ni vita vya Waislamu wenyewe kwa wenyewe, Waislamu wa Kishia na Kisuni.
Vile vile amegusia kuwa, huko nchini Syria, serikali iliyoko madarakani si ya Kishia na kuongeza kuwa: Pamoja na hayo lakini, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaiunga mkono serikai ya nchi hiyo kwani watu waliosimama kukabiliana na Syria kwa hakika ni wapinzani wa dhati na asili ya dini tukufu ya Kiislamu na wanatumikia malengo ya Marekani na utawala wa Kizayuni.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuchochea chuki na mizozo kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni kuwa ni katika njama za kibeberu na kikoloni za Marekani na kusisitiza kuwa: Jambo muhimu zaidi hivi sasa kulingana na hali ilivyo katika eneo hili ni kuwa na welewa sahihi kuhusu kambi mbili kuu zilizomo kwenye vita hivyo vikubwa na kutambua vyema na kwa njia sahihi nafasi yake mtu na upande gani anapaswa kuwa; kwani iwapo ukubwa na upana wa mpaka unaozitenganisha kambi hizo mbili hautatambuliwa vyema, basi kuna hatari ya mtu kusimama dhidi ya kambi ya Kiislamu bila ya yeye mwenyewe kutaka.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayaangalia kwa upana mkubwa masuala ya aneo hili na ni kwa kuwa na mtazamo huo ndio maana inaihesabu Marekani kuwa ndiye adui mkuu, na utawala wa Kizayuni wa Israel unafuatia nyuma ya Marekani katika uadui huo. Ameongeza kuwa: Iran daima inalihesabu suala la kuilinda na kuitetea kadhia ya Palestina kuwa ni katika majukumu yake na kwamba itaendelea kuiunga mkono na kuitetea Palestina.
Aidha ameashiria vikwazo vikubwa na visivyo na kifani vya miaka ya hivi karibuni vya Marekani na vya wale wanaolifuata kibubusa dola hilo la kiistikbari na kusema kuwa: Lengo na shabaha kuu ya vikwazo hivyo ni kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itoke katika njia yake hiyo, lakini pamoja na hivyo wameshindwa kufikia malengo yao hayo na katika siku za usoni pia hawataweza kufanikisha shabaha zao hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kwa mujibu wa ahadi za Mwenyezi Mungu ambazo tuna yakini nazo, sisi ndio tutakaokuwa washindi katika vita hivi vikubwa na hadi hivi sasa pia sisi ndio tuliopata ushindi kwenye vita hivyo kwani lengo kuu la maadui lilikuwa ni kuiangamiza Jamhuri ya Kiislamu, lakini si tu kwamba mfumo huu wa Kiislamu upo hadi hivi sasa, bali pia unazidi kupiga hatua na kuimarika siku hadi siku katika nyuga tofauti.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile ameashiria matamshi ya Katibu Mkuu wa Jihadul Islami ya Palestina kuhusiana na baadhi ya njama zinazofanywa kupitia kuongeza vikwazo dhidi ya Hizbullah na kusema kuwa: Hizbullah ya Lebanon ina nguvu kubwa na si rahisi kutetereshwa na vitendo kama hivyo na hivi sasa woga na hofu ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa Hizbullah ni kubwa zaidi kuliko huko nyuma.
Aidha amesisitiza kuwa sunna ya Mwenyezi Mungu ya kushinda kambi ya haki lazima itatimia na kuongezwa kuwa: Ushindi huo ni jambo la lazima kupatikana, ingawa kutakuwa na panda shuka na kutetereka na misukosuko, lakini ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwasaidia na kuwanusuru wanaoinusuru dini Yake ni kitu ambacho hakiwezi kwenda kinyume, lazima kitatimia.
Mwanzoni mwa mazungumzo hayo, Bw. Ramadhan Abdullah, Katibu Mkuu wa Jihadul Islami ya Paletina sambamba na kushukuru uungaji mkono wa kila namna na misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu kadhia ya Palestina, ametoa ripoti fupi kuhusu hali na matukio ya karibuni kabisa ya Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kusema kuwa: Pamoja na kuendelea kuzingirwa kila upande na kuishi katika mazingira magumu sana, lakini wananchi wa Ghaza bado wamesimama imara bila ya kutetereka, na huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan pia, licha ya kuweko ukandamizaji mkubwa na wa pande zote wa utawala wa Kizayuni, lakini pamoja na hayo moto wa Intifadha umewaka katika eneo hilo kwa hima na nia ya kweli ya kizazi kipya cha vijana wa Palestina.
Vile vile amesisitiza juu ya namna vikosi vya muqawama vya Palestina vinavyojiimarisha na kujiweka tayari wakati wote kiasi kwamba sasa hivi vina nguvu isiyotasawirika na kugusia matukio ya eneo la Mashariki ya Kati na kusema: Wamarekani na nchi zinazowafuata kibubusa wanaendelea na njama zao za kupotosha na kujaribu kuonyesha sura isiyo sahihi kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuusahaulisha utawala wa Kizayuni wa Israel, na pia wanafanya njama za kuleta migawanyiko katika eneo hili kupitia kuzusha vita baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni na ni kwa sababu hiyo ndio maana mashinikizo dhidi ya Hizbullah yameongezeka, lakini Jihadul Islami ya Palestina inatambua vyema mambo yanayoendelea katika eneo hili na ndio maana inahimiza sana kuungwa mkono Hizbullah na muqawama mbele ya njama hizo za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.