Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Rais wa Korea Kusini
02/05/2016
South Korean President meets with Leader of Revolution Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo jioni (Jumatatu) ameonana na Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini na huku akiashiria mtazamo chanya wa Jamhuri ya Kiislamu katika suala zima la kupanua wigo wa ushirikiano baina yake na nchi za bara la Asia amelitaja suala la kuwepo mawasiliano yasiyokatika na ya kudumu baina ya Iran na Korea Kusini kuwa ni jambo lenye manufaa sana kwa nchi zote mbili. Amesisitiza kuwa, maafikiano na mikataba inayowekwa baina ya nchi mbili inapaswa iwe kwa namna ambayo haitaweza kuathiriwa na mambo ya pembeni na vikwazo kwani si jambo jema na si katika hadhi ya Korea Kusini na Iran kuona kuwa uhusiano wao unaathiriwa na misimamo ya nchi kama Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuweko mabadilishano ya uzoefu katika nyuga tofauti za kielimu, kiteknolojia, kisiasa, kijamii na kiusalama ni kwa manufaa ya nchi zote hizi mbili na kuongeza kuwa: Sisi katika siasa zetu za kigeni tunapendelea zaidi kuwa na ushirikiano na nchi za Asia kwani tuna mambo mengi ya pamoja ya kiutamaduni na kihistoria baina yetu na ni kwa sababu hiyo ndio maana tunaamini kuwa, kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kufikiwa maelewano, mwafaka na ushirikiano baina ya nchi za bara hilo ikiwemo Korea Kusini ambayo ni moja ya nchi zilizoendelea barani Asia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia matatizo muhimu ya kiusalama yaliyopo katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kiujumla na kusisitiza kwamba: Kama hivi sasa hakutakuwa na mapambano ya kweli dhidi ya hatari ya ugaidi na usalama, basi kukabiliana na hatari hiyo katika siku za usoni litakuwa ni jambo zito zaidi na hakuna nchi yoyote itakayobakia salama mbele ya hatari ya ugaidi.
Vile vile ameashiria namna Wamarekani wanavyougawanya ugaidi makundi mawili kati ya ugaidi mzuri na ugaidi mbaya na kusema kuwa: Wamarekani wanajinadi kuwa wanapambana na ugaidi lakini kivitendo hawapambani kwa dhati na ugaidi wakati ambapo ugaidi wa namna yoyote ile ni hatari kwa usalama wa mataifa yote duniani na sababu yake ni kuwa iwapo usalama na amani haitkuwepo, maendeleo yanayotakiwa nayo hayawezi kupatikana.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amezungumzia ushirikiano na maafikiano baina ya nchi mbili za Iran na Korea Kusini na kugusia pia mambo yanayopasa kupewa kipaumbele katika ushirikiano wa pande hizo mbili na kusema: Kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo ushirikiano wenye faida kubwa baina ya Iran na Korea Kusini lakini vipaumbele vyetu katika ushirikiano huo havimalizikii tu katika masuala ya biashara bali inabidi kutiwe saini mikataba inayohitajiwa na Iran katika miundombinu na uchumi kwa ujumla.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema pia kuwa, kuathiriwa maelewano na mikataba ya pande mbili na mambo ya pembeni ni moja ya mambo ya kimsingi yanayopasa kuwekewa mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa hayatokei katika ushirikiano wa nchi mbili na kusisitiza kuwa: Si sahihi kuruhusu uhusiano wa Iran na Korea Kusini uathiriwe na misimamo na ushawishi wa Marekani, bali inabidi uhusiano wa nchi hizi mbili uwe wa kuendelea, wa kudumu, usiotetereka, wa kiudugu na wa kupendana kikweli kweli.
Vile vile amegusia historia takriban ndefu - lakini yenye panda shuka na misukosuko mingi - ya uhusiano wa Iran na Korea Kusini na kusisitiza kuwa: Kwa bahati nzuri serikali iliyoko madarakani huko Korea Kusini hivi sasa ni serikali inayopenda maelewano na kwa upande wake, Iran ina nafasi kubwa na nyingi pamoja na nguvu kazi mahiri ya vijana wenye nguvu, wenye vipaji na wasomi, suala ambalo linatoa fursa ya kuwepo ushirikiano wa kudumu, mpana na usioyumba baina ya nchi mbili.
Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini amesema kuwa ziara yake ya kutembelea Tehran ni fursa yenye thamani kubwa kwa ajili ya kustawisha uhusiano wa pande mbili na kuongeza kiwango cha kuaminiana. Ameongeza kuwa: Sisi hata katika kipindi cha kuwekewa vikwazo Iran tulijitahidi kuendelea kuwepo nchini Iran kadiri tulivyoweza.
Rais wa Korea Kusini amesema, Iran ni nchi yenye fursa nyingi yenye nguvu kazi muhimu, madhubuti na yenye taathira kama ambavyo pia Iran ni nchi iliyopo kwenye eneo la kijiografia lenye umuhimu wa kipekee. Amesema: Ni matumaini yetu kuwa uhusiano wa nchi hizi mbili hususan katika sekta ya uchumi ya ustawi utaimarika zaidi.
Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini amegusia pia mitazamo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu ustawi wa kiuchumi wa nchini Iran na vile vile sisitizo lake la mara kwa mara la kutiliwa mkazo ustawi wa kielimu, kiuchumi na kiviwanda kwa kutegemea nguvu na suhula za ndani ya nchi na kusema: Nina yakini kwamba sisitizo lako juu ya ustawi na juu ya kuboreshwa uchumi wa Iran litailetea nchi hii mustakbali mzuri sana, na sisi pia tuko tayari kuongeza ushirikiano wetu katika nyuga tofauti kama vile mazingira, sayansi na teknolojia pamoja na masuala ya kiuchumi.