Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Walimu
02/05/2016
Leader of Revolution meets with EducatorsAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumatatu) ameonana na maelfu ya walimu wa kona zote za Iran na sambamba na kuishukuru jamii ya walimu nchini kwa jitihada na kazi nzito zenye usumbufu mwingi wanazozifanya, amelitaja suala la kulea kizazi cha baadaye chenye utambulisho wa kupigania uhuru, kuwa na heshima, kushikamana na dini na chenye shakhsia za hali ya juu na zenye uwezo wa kufanya mambo makubwa, kuwa ndilo jukumu kuu na lenye hatari nyingi la Wizara ya Elimu na Malezi ya Jamhuri ya Kiislamu na Iran na kusisitiza kuwa: Kama jamii itajengekwa kwa sifa kama hizo bila ya shaka yoyote masuala kama uchumi wa kimuqawama usiotegemea mafuta, kuwa na utamaduni huru, kuwa na kigezo bora cha matumizi na kuwa na moyo wa muqawama na wa kusimama kidete mbele ya madola yanayopenda kujikumbizia kila kitu upande wake, yatapata maana yake halisi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kazi ya ualimu ni kazi nzito na kuongeza kwamba: Kazi inayofanywa kwa ikhlasi na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hubakia milele na huleta wokovu. Ameongeza kuwa, mazingira ya kuwawezesha walimu kufanya kazi zao kwa ikhlasi yako wazi kabisa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja harakati na athari za shahid Ayatullah Mutahhari kuwa ni mfano wa kazi mzuri inayong'ara iliyofanywa kwa ikhlasi na kupata baraka na kuongeza kuwa: Matunda ya ikhlasi ya alimu na mwanachuo huyo mkubwa aliyekuwa anajua vyema kutumia wakati na mahitaji ya wakati huo, ni kubakia hai kazi na athari zake kubwa kiasi kwamba licha ya kupita makumi ya miaka tangu kuuawa kwake shahidi, hadi leo hii watu wa kutoa fikra na nadharia wanaendelea kustafidi na kufaidika vizuri sana na kazi na athari zake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwa kusema: Tab'an ikhlasi na kukinai jamii ya walimu hakupaswi kuwafanya viongozi kughafilika na masuala ya kimaada na kimaisha ya jamii hiyo inayofanya jitihada kubwa za kutekeleza vizuri majukumu yake na kama ambavyo tumesema mara nyingi, hapa tunasema tena kwamba, bajeti na gharama zozote zinazotumika kwa ajili ya Wizara ya Elimu na Malezi kwa hakika huwa ni uwezekezaji wenye faida kubwa.
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza kujadili suala kuu na la kimsingi akisema: Suala la kimsingi ni kwamba, Wizara ya Elimu na Malezi inapaswa kukiandaa na kukilea kizazi kijacho kwa sifa gani maalumu na nchi inahitajia kizazi cha namna gani hasa cha kuiwezesha kuendelea na njia yake hii muhimu?
Kabla ya kuanza kuzungumzia sifa maalumu zinazohitajika kwa ajili ya kulea kizazi kama hiyo, Ayatullah Udhma Khamenei amegusia nukta moja nyingine akisema: Tunapaswa kutambua vyema kuwa katika jitihada za kulea kizazi kijacho, hatuwezi kufanya jambo hilo muhimu katika anga na medani isiyo na upinzani, bali tunakabiliwa na mpinzani anayejulikana kwa jina la mfumo wa kibeberu wa kimataifa.
Aidha amekumbusha kuwa: Yumkini baadhi ya watu wakastaajabishwa na matamshi haya na kujiuliza, kuna uhusiano gani baina ya Wizara ya Elimu na Malezi na mfumo wa kibeberu wa kimataifa? Hata hivyo uhakika wa mambo ni kuwa, mfumo wa kibeberu duniani umeweka ratiba maalumu za kuwapotosha vijana hususan vijana wa Iran (nasi hatupaswi kughafilika hata kidogo na jambo hilo).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinmduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Marekani, mabepari wa Kizayuni na baadhi ya tawala za kiistikbari ndilo dhihirisho la mfumo wa kibeberu wa kimataifa na kusisitiza kuwa: Mfumo huo wa kibeberu unataka kizazi kijacho cha nchi zote duniani kiwe kizazi ambacho fikra, utamaduni, mitazamo na misimamo yao kuhusiana na masuala ya dunia ni ile ile inayotakiwa na madola ya kibeberu na hatimaye watu wenye vipaji, wanasiasa na watu wenye taathira katika jamii hizo wawe wanafikiri na kuchukua maamuzi kwa namna ile ile inayotakiwa na mabeberu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria historia ndefu ya mpango huo wa kiutamaduni wa wakoloni na kusema: Wanafikra wa Magharibi kwa mara chungu nzima wamekuwa wakisema kuwa, badala ya kutumia mbinu ya kikoloni ya karne ya 19 ya kuzivamia na kuzikalia moja kwa moja nchi nyingine, mbinu bora zaidi na yenye gharama ndogo zaidi, ni kupandikiza fikra na utamaduni wa madola ya kikoloni katika nyoyo na akili za vijana wa nchi nyinginezo na kulea watu wenye vipaji na vipawa ambao watakuwa mithili ya maafisa wa kijeshi wa kuulinda mfumo wa kibeberu katika jamii hizo.
Vile vile amesema, baadhi ya tawala za nchi za eneo la Mashariki ya Kati ni mfano wa wazi wa matunda ya mpango huo wa muda mrefu wa mabeberu na kuongeza kuwa: Tawala hizo hivi sasa zinafanya kazi ile ile inayotakiwa na Marekani na hata zinakubali kubeba gharama za kazi yote zinayoifanyia Marekani tena bila ya kupata faida yoyote bali faida pekee zinayopata tawala hizo ni kukubali Wamarekani kuzilinda na kuzuia zisianguke.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, mpinzani wetu ana mipango ya namna hiyo kwa ajili ya kizazi cha baadaye cha nchi yetu. Aidha ametilia mkazo ulazima wa kueneza fikra, utamaduni na lugha ya asili na ya kienyeji na kusema: Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa katika baadhi ya nyakati, badala ya kuenezwa na kutiwa nguvu lugha ya Kifarsi, kunaenezwa lugha ya Kiingereza na sasa hivi hali imefikia hadi ambayo lugha ya Kiingereza inafundishwa hadi katika chekechekea.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Suala hili halina maana ya kupinga kufundishwa kabisa lugha za kigeni bali mjadala mkuu unaopasa kuzingatiwa hapa ni hatari ya kuenea utamaduni wa kigeni nchini na kati ya watoto wadogo, mabarobaro na vijana wetu.
Amesisitiza kuwa baadhi ya nchi zina ratiba maalumu za kukabiliana na uenezaji wa lugha na tamaduni za kigeni na kusema: Inasikitisha kuona kuwa katika nchi yetu, hatuna ratiba yoyote ya kukabiliana na jambo hilo na medani tumeiwacha wazi kwa ajili ya kuenea utamaduni wa kigeni.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, baadhi ya nchi za Magharibi zinaweka vizuizi na vikwazo vingi vya kuzuia kuenea lugha ya Kifarsi katika nchi hizo na kuongeza kuwa: Wakati ambapo nchi hizo za Magharibi haziruhusu kuenea lugha ya Kifarsi nchini kwao, sisi huku kwetu tunaruhusu kuenea lugha na utamaduni wao! Je, jambo hilo linaingia akilini kweli?
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbusha pia kuwa: Maneno haya hayana maana ya kuacha kabisa kufundisha lugha ya Kiingereza mashuleni, lakini maudhui kuu hapa ni kwamba tunapaswa tuelewe ni mpinzani wa aina gani tunayekabiliana naye na tutambue mpinzani huyo ni kiasi gani ameweka mipango makini ya kukiathiri kizazi kijacho cha nchi yetu.
Baada ya hapo ameanza kubainisha vielelezo na sifa maalumu zinazohitajika kwa ajili ya kulea kizazi kinachohitajiwa na Iran katika siku za usoni na kusema: Kielelezo muhimu zaidi ambacho inabidi kizingatiwe katika kulea wanafunzi wadogo ni kuwajengea utambulisho unaopenda uhuru, heshima na kushikamana na dini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Ni lazima mabarobaro na vijana nchini walelewe kwa namna ambayo watakuwa huru katika kufuatilia masuala ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni, na wasikubali kivyovyote vile kuwa tegemezi katika masuala hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa nchi imepata madhara katika suala hilo na kuongeza kuwa: Kupenda kutumia istilahi za kigeni ni moja ya mifano ya madhara hayo ambayo yamebakia nchini Iran tangu katika kipindi cha utawala wa kitaghuti nchini.
Aidha ametaja moja ya mambo makuu ya lazima kwa ajili ya kufanikisha uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete kwamba ni vijana nchini Iran kuwa na utambulisho wa kupenda kuwa huru na kuongeza kuwa: Iwapo roho na moyo wa kuwa huru na moyo wa muqawama na wa kusimama kidete hautakuwepo, hata kama viongozi nchini wataitisha mamia ya vikao vya kujadili njia za kufanikisha uchumi wa kimuqawa, watashindwa kufikia matunda kamili na sahihi yanayotakiwa na uchumi huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kwamba: Kuwa na uchumi wa kimuqawama usiotegemea mafuta na kuwa na utamaduni huru kutaweza kupata maana yake halisi pale tu utambulisho wa kupenda kuwa huru utakapokita mizizi katika jamii.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuhuisha vielelezo bora kabisa na maana halisi ya kufanya kazi kitaasisi kati ya wanafunzi kuwa ni jukumu jingine zito walilo nalo walimu na Wizara ya Elimu na Malezi ya Iran na kuongeza kuwa: Imani, kutafakari, ushirikiano na jamii kufanya kazi kwa pamoja pamoja na kufanyia marekebisho kigezo cha matumizi ni miongoni mwa vielelezo bora ambavyo inabidi vistawishwe kati ya vijana wa kizazi kijacho cha wananchi wa Iran.
Aidha amegusia matatizo yaliyopo nchini katika suala zima na kigezo cha matumizi na ametoa mifano kadhaa kuhusiana na suala hilo akisema: Kupenda kutumia bidhaa za nje na kuingiza nchini bidhaa za anasa kwa njia ya magendo zenye thamani ya makumi na mamia ya mabilioni ya fedha ni mfano wa wazi wa kuweko kigezo kibaya na ghalati cha matumizi nchini na inabidi jambo hilo lirekebishwe ambapo moja na miundombinu mikuu ya kufanyia marekebisho jambo hilo ni kujenga utamaduni wa kutopenda kutumia bidhaa za namna hiyo ndani ya kizazi cha vijana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kumvumilia na kumstahamilia mpinzani kuwa ni kielelezo kingine bora wanachopaswa kujengwa nacho vijana wa kizazi kijacho nchini na amesema: Bado utamaduni wa kumstahamilia mpinzani haujajengeka katika jamii, kwani mtu akianza kukosoa kidogo tu "anapigwa ngumi kifuani" na hii inaonesha wazi namna watu wasivyoweza kuvumiliana.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la adabu na kuwa na heshima na vile vile kujipamba kwa mafundisho ya dini na kutopenda ukubwa na anasa kuwa ni kielelezo kingine kinachohitajika katika kuwalea wanafunzi wadogo na kusisitiza kuwa: Kujengwa na kuwekewa misingi mizuri vielelezo hivyo ndani ya kizazi cha baadaye na kujenga utamaduni wa kuheshimu na kutekeleza kivitendo vielelezo hivyo ni miongoni mwa majukumu makubwa ya walimu na Wizara ya Elimu na Malezi nchini Iran.
Vile vile amesema, Wizara ya Elimu na Malezi haiwezi peke yake kufanikisha jukumu hili takatifu na kugusia majukumu ya asasi na taasisi nyingine tofauti kwa kusema: Taasisi za malezi pamoja na asasi zote zinazojishughulisha na elimu na malezi ni miongoni mwa taasisi zenye taathira kwenye suala hilo na zina jukumu zito la kufanikisha jambo hilo na ni lazima zifanye jitihada kubwa, zenye malengo na shabaha maalumu pamoja na jitihada za busara na salama katika upande wa kiitikadi, kisiasa na kimaadili kwa nia ya kufanikisha jambo hilo na kwamba kuzembea kwa namna yoyote ile kutakuwa na madhara, bali ni pigo kwa Wizara ya Elimu na Malezi nchini na kwa kizazi kijacho.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB kuwa ni chombo kingine chenye jukumu la kujenga na kuweka misingi ya vielelezo bora kwa ajili ya kizazi kijacho na kujenga utamaduni wa kupewa umuhimu suala hilo katika jamii na huku akikosoa utendaji wa shirika hilo la utangazaji la taifa amesema: Mwaka jana nilibainisha pia ulazima wa Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuwa na mipangilio ya kina na sahihi kwa ajili ya kizazi cha vijana, lakini cha kusikitisha ni kuwa mambo hayo hayakufanyiwa kazi.
Ameongeza kuwa: Shirika la IRIB linapaswa kutumia wanafikra na wataalamu wenye miono mipana na ya mbali kwa ajili ya kuandaa ratiba maalumu kwa ajili ya Wizara ya Elimu na Malezi nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia barua moja aliyopewa na mwanafunzi mmoja wiki iliyopita wakati alipoonana naye na malalamiko ya mwanafunzi huyo kuhusu kutokuweko vipindi vinavyofaa na vyenye taathira kwa vijana wa shule za sekondari katika Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB na kusisitiza kwa kusema: Inabidi shirika hilo la utangazaji la taifa litumie mbinu za kisanii na kiutaalamu kuandaa vipindi vizuri vya kuwavutia na kuwakinaisha kifikra, kiroho, kidini na kielimu vijana nchini na kwamba vipindi vya sasa hivi vya baadhi ya kanali za shirika hilo haviendani kabisa na mambo yanayohitajiwa katika suala hilo.
Vile vile amesema, Wizara ya Mawasiliano nayo ni chombo kingine chenye jukumu katika malezi ya kizazi kizuri cha baadaye na huku akiashiria upana wa anga ya Intaneti na kasi kubwa inayoongezeka kila siku ya kutumia anga hiyo kwa ajili ya mawasiliano ya kila sekunde baina ya vijana na kukumbusha kuwa: Hakuna mtu anayepinga kutumiwa anga ya Intaneti bali suala muhimu na la kimsingi hapa ni kuelewa kuwa, katika anga hiyo kuna hatari nyingi na inabidi kuandaliwe uwanja wa kutumiwa kwa njia sahihi anga hiyo na sio kuachwa watu watumie wanavyotaka Intaneti bila ya kuweko udhibiti wa aina yoyote ile.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameelezea masikitiko yake kuhusiana na Wizara ya Mawasiliano na Baraza Kuu la Kusimamia Matumizi ya Intaneti na kusema kuwa: Hakuna mtu anayetaka matumizi ya Intaneti yapigwe marufuku au Intaneti ifungwe, kwani jambo hilo haliingii akili, lakini kwa nini wakati nchi nyingine zinafanya juhudi kubwa za kulinda na kuhifadhi utamaduni wao na kuweka mipaka na sheria maalumu za kudhibiti matumizi ya Intaneti, sisi tukae vivi hivi bila ya kuchukua hatua za maana za kulidhibiti jambo hilo?
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, kazi nyingine ya lazima kwa ajili ya Wizara ya Elimu na Malezi ni kupuliza roho ya furaha na uchangamfu na ujana kwa walimu na hapo hapo amesisitizia udharura wa kuundwa upya mfumo wa elimu nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mfumo wa hivi sasa wa elimu nchini umeshachakaa, umeshakonga na umeshazeeka na kusisitiza kuwa: Mfumo wa masomo uliopo leo nchini chimbuko lake ni mfumo wa elimu wa Ulaya na umebakia vile vile hadi leo hii bila ya kubadilishwa licha ya kwamba umeshazeeka, hivyo kuna ulazima wa kuundwa upya mfumo wa elimu nchini.
Amesema kuwa, kuunda upya mfumo wa elimu nchini kwa kutumia mbinu za jadi na kwa kukopi na kunukuu mfumo wa Magharibi ni jambo lisilofaa kabisa na kuongeza kusema kuwa: Tab'an kutumia uzoefu wa huko nyuma na uzoefu wa watu wengine ni jambo zuri, lakini wana fikra na wana nadharia wanapaswa kuandaa muswada maalumu wa kuleta mapinduzi katika Wizara ya Elimu na Malezi na kutunga mfumo mpya wa elimu nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesema, vituo vya kiufundi na kiutaalamu navyo vina jukumu kubwa katika kuongeza maarifa kwa vijana na kuwafanya kuwa na manufaa katika jamii na kwamba hilo ni katika vitu vinavyopasa kupewa kipaumbele na Wizara ya Elimu na Malezi nchini na kuongeza kuwa: Ripoti zinaonesha kuwa, kuna aina 12 elfu za kazi katika jamii. Lakini cha kujiuliza hapa ni kuwa, je, wanafunzi wote, licha ya kuwa na vipaji tofauti na vya kila namna, wanapaswa kufuata njia moja na kuwa na aina moja ya masomo?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kuna wajibu wa kuvigundua vipaji vya wanafunzi na kuvilea kwa njia sahihi ili vipaji hivyo vije viwe chimbuko la ubunifu katika maeneo mbali mbali ya kazi na ya utaalamu na ufundi.
Suala jengine lililokosolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Wizara ya Elimu na Malezi nchini ni kutumia baadhi ya majina na nembo zilizokuwa zinatumiwa katika kipindi cha utawala wa kitaghuti (wa Shah) nchini kama vile "pishahangan."
Ameongeza kuwa: Kwa vile katika Wizara ya Elimu na Malezi kuna majina na taasisi kama vile Basiji ya Wanafunzi na Umoja wa Jumuiya za Kiislamu za Wanafunzi, wizara hiyo haipaswi kutumia majina ya huko nyuma ambayo yalikuwa na maana zake maalumu na yaliwekwa kwa malengo mahsusi (na badala yake inapaswa kutumia majina ya hivi sasa yenye maana pana na nzuri).
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia suala la shule za serikali na zisizo za serikali na kusema: Wizara ya Elimu na Malezi katika Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina sura ya mtawala wa masuala yote ya kielimu na malezi, lakini hili halina maana ya kwamba majukumu na kazi zote zinaondolewa kwa serikali, bali serikali inapaswa kuwa na mchango mkubwa katika Wizara ya Elimu na Malezi na ni kwa msingi huo ndio maana kuendelea kuzigeuza shule za serikali kuwa za kulipia tena baadhi yake zikiwa zinatoza ada kubwa za masomo, hatuwezi kusema kuwa ni jambo sahihi kikamilifu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Inabidi kiwango na ubora wa shule za serikali kipandishwe juu na kuzifanya familia za wanafunzi zipende kupeleka watoto wao kwenye shule hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia usalama wa kifikra na kikazi wa Waziri wa Elimu na Malezi na huku akitilia mkazi ulazima wa kutumiwa fursa hiyo kwa ajili ya kutekeleza majukumu mazito katika wizara hiyo amesisitiza kuwa: Chuo Kikuu cha walimu ni moja ya vituo muhimu mno ambacho inabidi kistawishwe kiukubwa na kiubora na kuwekezwe kwa ajili ya kufanikisha jambo hilo, kadiri inavyowezekana.
Baada ya hapo ametoa majumuisho ya hotuba yake kwa kusisitizia umuhimu wa kuijenga na kuitia nguvu nchi pamoja na kuipa kipaumbele nafasi muhimu na ya juu ya walimu katika jambo hilo na kusema kuwa, kitu muhimu na cha msingi cha kufanikisha jambo hilo ni elimu. Ameongeza kuwa: Nguvu haziishii tu katika kuwa na silaha za kisasa, bali elimu, imani, kuwa na shaksia ya kitaifa, kusimama kidete na kuwa na utambulisho wa kimapinduzi ni mambo mengine muhimu ya kuifanya nchi kuwa na nguvu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema: Wakati adui anapokuoneni mna nguvu kama hizo, huwa hana njia nyingine ila kurudi nyuma lakini kama tutafanya muhali na iwapo tutashindwa kuonesha misingi na mambo yetu yenye nguvu au kama tutaogopa, basi bila ya shaka yoyote adui atazidi kuwa na jeuri dhidi yetu.
Vile vile ameashiria muswada unaojadiliwa na Baraza la Congress la Marekani kuhusiana na mazoezi ya kijeshi ya baharini ya Iran na kusema kuwa: Leo hii maadui wanatamka maneno ya kijeuri yanayopindukia ukubwa wa midomo yao na eti wanasema, Iran haipaswi kufanya mazoezi ya kijeshi katika Ghuba ya Uajemi, wakati (hata wenyewe hao maadui wanajua kuwa) hayo ni matamshi ghalati kupita kiasi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, taifa kubwa la Iran linao uwezo wa kupambana na kujibu ubeberu wote huo na kusisitiza kuwa: Ghuba ya Uajemi ni nyumbani kwa taifa la Iran na fukwe za Ghuba ya Uajemi na fukwe pana za Bahari ya Oman ni mali ya taifa lenye nguvu la Iran, hivyo sisi ni lazima tuwepo kwenye eneo hili kwa nguvu zetu zote na ni lazima tufanye mazoezi ya kuonesha nguvu zetu za kijeshi na kwamba ni Wamarekani ndio ambao wanapaswa wajiulize kwa nini wanatoka huko walikotoka na kuja kufanya mazoezi ya kijeshi katika eneo letu hili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Namna hivi ndivyo inavyobidi kukabiliana na madola ya kibeberu yanayopenda kujikumbizia kila kitu upande wao.
Amesema, kuzidi kudumu na kuwa imara siku hadi siku Jamhuri ya Kiislamu ni ushahidi wa kushindwa njama za maadui na kuongeza kuwa: Qur'ani imetufunza kwamba tunapaswa kujiandaa kwa namna ambayo muda wote adui atakuwa na woga na hofu juu yetu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Waziri wa Elimu na Malezi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyouawa shahidi mwanafikra mkubwa wa zama hizi, shahid Mutahhari pamoja na mashahidi Rajai na Bahonar na vile vile ametoa mkono wa kheri na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya Wiki ya Mwalimu nchini Iran na kusisitiza kuwa: Wizara ya Elimu na Malezi inafanya juhudi za kuweka misingi mizuri ya kufanikisha utekelezaji wa siasa za uchumi wa kimuqawama kupitia kujenga utamaduni maalumu kuhusu suala hilo.
Bw. Ali Asghar Fani, Waziri wa Elimu na Malezi wa Iran amebainisha kuwa, mipango ya kiistratijia ya Wizara ya elimu na Malezi katika kipindi chote cha mpango wa sita wa elimu nchini itasimama juu ya msingi wa kutekeleza hati ya mabadiliko ya kimsingi na kuongeza kuwa: Kuandaa muongozo na ramani ya njia kwa ajili ya kutekeleza hati wa mabadiliko katika Wizara ya Elimu na Malezi, kubuni na kuandaa fani na masomo mapya, kustawisha na kupandisha juu heshima ya walimu, kutunga na kuandaa mpango wa kiistratijia wa vyuo vikuu vya walimu na kutia nguvu nafasi ya kushiriki wananchi sambamba na kustawisha malezi ya wanafunzi na kuwafanya wajenge tabia ya kufanya utafiti ni miongoni mwa kazi muhimu za Wizara ya Elimu na Malezi ya Iran katika mwaka uliopita.