Kiongozi Muadhamu Aonana na Vyuo Vikuu vya Kidini vya Mkoa wa Tehran
14/05/2016
Seminary Teachers and Students from Tehran Province met with Ayatollah KhameneiAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumamosi) ameonana na majimui ya wakuu, walimu na wanafunzi wa Hawza (vyuo vikuu vya kidini) za mkoa wa Tehran na kutaja majukumu matatu makuu ya watu wa dini ambayo ni kuongoza watu kifikra na kidini, kuongoza watu kisiasa na kuwafanya kuwa na busuri na muono wa mbali sana na tatu kutoa miongozo na kushiriki vilivyo katika nyuga za kutoa huduma kwenye jamii. Amesisitiza kuwa: Wanafunzi wa kidini wanapaswa kujiidilisha kupata ustahiki wa kuwa kweli wanafunzi wa kidini na kuwa na elimu na mwamko unaotakiwa katika dunia tofauti ya leo hii ili kwa njia hiyo waweze kujiweka katika mazingira ya kutekeleza vilivyo majukumu yao katika jamii.
Ayatullah Udhma Khamenei amewausia wanafunzi wa kidini kujua thamani ya matukufu na majukumu ya wanafunzi wa kidini na kuongeza kuwa: Kama watu wote watakuwa na utaalamu unaohitajika katika jamii tena kwa sura bora kabisa lakini jamii ikashindwa kuwa ya kidini, taifa la jamii hiyo litakuwa limepata khasara duniani na Akhera na litakuwa na matatizo makubwa. Amesema jukumu hilo adhimu, yaani kuibadilisha jamii kuwa jamii ya kidini, ni la maulamaa, wanachuoni na wanafunzi wa dini.
Amesema, kuwaongoza watu katika dini kuna maana ya kubainisha fikra sahihi za Uislamu na huku akiashiria taathira kubwa za mawasiliano ya kompyuta na Intaneti katika kuongezeka shubha na masuala yenye utata wa kidini na kuweko njama nyingi za baadhi ya wanasiasa za kupandikiza fikra potofu na ghalati katika fikra za vijana amesisitiza kuwa: Medani hiyo ndiyo medani ya vita vya kweli na kwamba wanachuoni na wanafunzi wa kidini wanapaswa kujizatiti kwa silaha madhubuti na kuingia katika uwanja wa mapambano kwa nia ya kupata ushindi katika medani hiyo ya kukabiliana na shubha na fikra ghalati na potofu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja "Uislamu wa fikra mgando, wa kitaasubu na usio na welewa sahihi kuhusiana na mambo ya hakika ya kimaanawi na Uislamu usioona mbali" ni mfano wa wazi wa fikra potofu na kuongeza kuwa: Katika ncha ya pili ya Uislamu huo, kuna Uislamu wa kuokota na Uislamu wa Kimarekani ambao umesimama kukabiliana na Uislamu wa kweli.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuuelewa Uislamu sahihi uliosimama juu ya msingi wa Kitabu na Sunna kwa kutumia hekima, maarifa na fikra ya Kiislamu kuwa ni jukumu kuu la watu wa dini na kuongeza kwamba: Njia ya Mitume na Manabii ni ndiyo hiyo hiyo ya kueneza fikra asili na kwamba wanavyuoni wa kidini ni waendelezaji wa njia hiyo ya ufanisi yaani kuwaongoza watu kwenye misingi na mafundisho sahihi ya dini.
Amesema, kuwaongoza watu kivitendo ni mkamilishaji wa kuwaongoza kifikra na kusisitiza kuwa: Watu wa dini wana jukumu la kutumia mbinu nzuri kabisa za kuwaongoza watu kivitendo kwenye ibada, kwenye matendo mazuri katika maisha na kwenye masuala yanayosisitizwa na dini ikiwa ni pamoja na ukweli, uaminifu, taqwa, kuancha maasi, kuamrishana mema na kukataza mabaya na kuwa na mtindo sahihi wa maisha.
Vile vile amesema ni jambo muhimu sana kuzidi kutilia nguvu na kuimarisha imani sahihi za kidini walizorithi watu kutoka kwa wazee wao na kuongeza kuwa: Inabidi kuwe kunatolewa hoja na ushahidi sahihi wa kuzilinda na kuzitia nguvu itikadi sahihi za kurithi ambazo yumkini baadhi yake zikawa zimeshatoweka baada ya kupita muda, kama ambavyo ni wajibu kuziongoza itikadi hizo katika njia zake sahihi.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuwaongoza watu katika masuala ya kisiasa kuwa ni jukumu jingine muhimu la maulamaa na wanavyuoni wa kidini na kuongeza kuwa: Sababu inayonifanya nisisitizie mara kwa mara udharura wa kuweko mapinduzi katika hawza (vyuo vikuu vya kidini) ni kwamba harakati sahihi na ya kimapinduzi haiwezi kuendelea nchini na katika jamii bila ya kushiriki vilivyo watu wa dini katika jambo hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia matukio yaliyowahi kutokea nchini Iran katika miaka ya huko nyuma kama vile kadhia ya tumbaku, kipindi cha kupigania utawala wa sheria nchini pamoja na harakati ya kuyafanya mafuta ya Iran yawe mali ya taifa na kuongeza kuwa: Harakati za kupigania utawala wa sheria na ile ya kuyafanya mafuta yawe mali ya taifa hazikuweza kufikia matunda yake ya mwisho kutokana na kujitoa wanachuoni wa kidini katika harakati hizo, lakini kipaji na ustadi wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) kilikuwa ni hicho kwamba hakuruhusu adui awatoe watu wa dini katika harakati adhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu kwani kama wanachuoni na watu wa dini wangelijitoa basi si tu Mapinduzi ya Kiislamu yasingeliweza kupata ushindi, lakini pia Jamhuri ya Kiislamu nayo isingeliweza kuendelea na harakati yake.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Tangu awali kabisa ya Mapinduzi ya Kiislamu hadi leo hii Wamarekani wamekuwa wakifanya njama za kuwatoa wanavyuoni na watu wa dini katika harakati ya umma ya taifa la Iran ili wakishafanya hivyo, wawatoe wananchi wa Iran katika medani ya mapambano na hatimaye kuyafanya Mapinduzi ya Kiislamu yashindwe kabisa. Hata hivyo hadi hivi sasa wameshindwa kufanikisha njama zao hizo na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu hawataweza kufanya hivyo pia katika siku za usoni.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Katika zilizala ya mwamko wa Kiislamu pia, ni dini ndiyo iliyowavuta wananchi katika medani ya mapambano (kwenye nchi za Kiarabu), lakini kwa vile taasisi za kidini za nchi hizo hazikuwa na umoja; mapambano hayo hayakuendelea na mwamko huo haukufikia kwenye matunda yaliyokusudiwa. Lakini katika Jamhuri ya Kiislamu, matunda ya kuendelea kuwepo imara maulamaa na wanavyuoni katika medani ni kuzidi kuwepo imara wananchi katika nyuga mbali mbali, jambo ambalo limeipa nguvu ya kuendelea, harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Baada ya kubainisha uongozaji wa kidini na uongozaji wa kisiasa, Ayatullah Udhma Khamenei ameanza kuzungumzia jukumu la tatu muhimu la wanavyuoni na watu wa dini ambalo ni kushiriki kwao vilivyo katika kuwaongoza watu kifikra na kuwaongoza watu kivitendo katika medani ya huduma za kijamii.
Ameongeza kuwa: Kushiriki wanafunzi wa kidini katika kutoa huduma kwa watu, kujenga mashule na madrasa, kujenga mahospitali, kuwasaidia watu katika matukio mbali mbali na kwenye nyuga nyinginezo nyingi, huwatia hamu watu wengine kujitokeza kwa wingi kwenye masuala hayo na hivyo watu wa dini kuwa chimbuko la kutolewa huduma zinazotakiwa katika jamii.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewausia wanafunzi wa dini kujibidiisha katika kusoma vizuri na kuzilea nafsi katika maadili bora na kuongeza kuwa: Elekezeni hima zenu katika kutekeleza vilivyo majukumu yenu kama watu wa dini majukumu ambayo hakuna utaalamu wowote mwingine unaoweza kuchukua nafasi yake hiyo. Tab'an jambo hilo halipaswi kufanywa kwa nia ya kutafuta cheo, ukubwa na umaarufu, bali wakati wote inabidi lifanyike kwa lengo moja tu la kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu pamoja na kumridhisha Imam wa Zama (Imam Mahdi AS Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake).
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia matakwa ya baadhi ya wahadhiri na wanafunzi wa Hawza za Tehran na kusema kuwa: Miongoni mwa majukumu makuu ya wakuu wa Hawza ni kuwa macho na kutoruhusu Hawza hizo kutoka katika mtindo na muundo wake wa wanafunzi wa kidini na kuingia katika mfumo wa wanafunzi wa vyuo vikuu. Pia wahakikishe kunatolewa masomo ya Akhlaq katika Hawza sambamba na kuzidi kuwavuta wanafunzi kujiunga na vyuo hivyo vikuu vya kidini na kuvifanya vya kieneo. Amesema, inabidi masuala hayo yachukuliwe maamuzi baada ya kufanyika utafiti wa kina na unahotajika.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria historia ndefu na yenye umuhimu mkubwa wa Hawza na chuo kikuu cha kidini cha Tehran na maulamaa na wanafunzi wakubwa wakubwa wa kidini katika Hawza hiyo na kuongeza kwamba: Hawza ya Tehran hivi sasa ina utambulisho wake maalumu na inabidi kujua thamani ya utambulisho huo ili fikihi, ulumi za kiakili, tafsir na hadith ziweze kunawiri kwenye chuo hicho kikuu cha kidini.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Sadeghi Rashad, Mkuu wa Baraza la Hawza za Kielimu za Mkoa wa Tehran amegusia historia ndefu ya chuo hicho kikuu cha kidini cha Tehran na nafasi yake muhimu katika mabadiliko ya kisiasa na kijamii na kuongeza kuwa: Hawza hiyo ina madrasa 133, vituo sita vya utafiti na wanafunzi 15 elfu na wahadhiri na walimu 1600 wanaofanya kazi katika kona zote za mkoa wa Tehran.
Hujjatul Islam Walmuslimin Rashad amebainisha kuwa Hawza za mkoa wa Tehran zimetoa mashahidi 360 katika njia ya Mapinduzi ya Kiislamu na baadaye ametaja baadhi ya harakati na mafanikio ya Hawza hizo na kuongeza kuwa: Tab'an moja ya wasiwasi uliopo leo katika Hawza ni kuzidi kuondoka utambulisho wa asili wa Hawza na kuelekea upande wa mtindo wa vyuo vikuu.
Aidha Mahujjatul Islam Walmuslimin mabwana Sedighi, Hosseini, Panahi, Rouhani, Tahsili, Rostami, Biranvand, Rafei, Panahiyan na mabibi Rasti na Mir Momeni, walipata fursa ya kutoa mitazamo tofauti kuhusu maudhui mbali mbali zinazohusiana na hawza na vyuo vikuu vya kidini.
Baadhi ya nukta muhimu zilizotolewa na wahadhiri na wanafunzi wa kidini katika hotuba zao kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni pamoja na:
- Ulazima wa kuzingatia umaanawi katika vyuo vikuu vya kidini na kutiliwa hima akhlaki, kuarifishwa vigezo vilivyofanikiwa na kuvitangazwa kama mtindo wao wa maisha.
- Kusisitiziwa umuhimu wa kushikamana na vazi la uanafunzi wa kidini, kuwa na moyo na mori wa kufanya kazi kimapinduzi, kulipa umuhimu mkubwa suala la dini na kutambua vyema mambo yanayohitajika katika kila zama.
- Umuhimu wa kushirikiana hawza na vyuo vikuu katika masomo ya fikra huru.
- Kuimarisha mawasiliano ya moja kwa moja baina ya wanafunzi wa kidini na wanahuoni wa kidini kwa upande mmoja na wananchi na watu wa kawaida kwa upande wa pili.
- Kuarifisha mpango mkuu unaojulikana kwa jina la "Bunyan Marsus" kwa lengo la kutia nguvu na kuufanya wa kisasa uwezo na utayari wa kila namna wa kielimu, kimaadili na kijamii wa wanafunzi wa kidini.
- Matatizo ya kimaisha ya wanafunzi wa kidini na pendekezo la kutiwa nguvu na kuimarishwa hawza za maeneo tofauti yasiyo maeneo makuu kwa shabaha ya kupunguza idadi ya wanafunzi wa kidini wanaohama maeneo yao kwa ajili ya kutafuta elimu.

- Udharura wa kufanyika mabadiliko katika mfumo wa masomo kwenye hawza kwa lengo la kuongeza faida za kielimu na kuzuia kupotea hamu ya kusoma wanafunzi wa kidini.
- Kushiriki vilivyo wanafunzi wa kidini wa kike katika kutafuta elimu na kufanya tablighi ya mafundisho ya dini na pendekezo la kuanzisha kituo maalumu cha wanawake wafanya jihadi wa Kiislamu kwa shabaha ya kukabiliana na madhara ya kijamii na kifamilia.
- Wajibu wa vyuo vikuu vya kidini wa kutoa majibu ya kina, ya hekima na ya busara kwa shubha zinazojitokeza katika masuala yanayohitajika katika jamii na kutumia vyema uwezo na misingi madhubuti ya utoaji fatwa sahihi, makini na za kimsingi.
- Udharura wa kuanzishwa kituo cha utaalamu wa kufanya tablighi na mafunzo ya umahiri na ustadi wa kutoa khutba za kuwakinaisha hadhirina.
Mwishoni mwa mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amewasalisha hadhirina sala za Adhuhuru na Laasiri.