Kiongozi Muadhamu Aonana na Washiriki wa Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu
18/05/2016
Participants in the International Quranic Competition met with the LeaderAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo ameonana na washiriki wa Mashindano ya 33 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yaliyomalizika Jumanne Mei 17 mjini Tehran na kusema kuwa, kumwamini Mwenyezi Mungu na kumkufuru taghuti ni katika misingi mikuu na ya kweli ya kuwezesha kuwa imara na kuwa na nguvu ulimwengu wa Kiislamu na huku akisisitiza kwamba, Marekani ndiye "taghuti mkuu" na "shetani mkubwa" amesema kwamba: Jukumu kubwa zaidi la maulamaa, wasomi na watu wenye vipaji (katika ulimwengu wa Kiislamu) ni kuamsha watu na kubainisha mambo kijihadi katika kukabiliana na hila na makri za mataghuti na kwamba umma wa Kiislamu nao unapaswa kuwa macho na usikubali kutekwa na ahadi za kuzuzua na za uongo za madola ya kibeberu na wala usitishwe na makeke na vishindo vya madola hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewashukuru walioendesha na kusimamia mashindano hayo ya kimataifa na kusema kuwa, Qur'ani ni mhimili mkuu wa umoja wa umma wa Kiislamu. Ameongeza kuwa: Katika wakati huu ambapo siasa za madola ya kibeberu zimejikita kwenye kuzusha hitilafu na mizozo kati ya Waislamu, umma wa Kiislamu una wajibu wa kushikamana vilivyo na neema hiyo kubwa ya Mwenyezi Mungu na kuitumia vizuri katika njia ya kuleta umoja na mshikamano baina ya Waislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, moja ya baraka za mahafali na vikao vya kusoma Qur'ani ni kuyafanya matabaka mbali mbali ya watu hususan ya vijana kuwa na ukuruba na mapenzi makubwa na Qur'ani na kuongeza kuwa: Umma wa Kiislamu, leo hii unahitajia zaidi mafundisho, miongozo na utambuzi wa Qur'ani Tukufu, kuliko wakati mwingine wowote, kwani mtindo wa maisha ya Waislamu leo hii yako mbali sana na mtindo wa maisha unaotakiwa na Qur'ani Tukufu.
Aidha ameashiria njama na makri kubwa zinazofanya na madola ya kitaghuti kwa lengo la kutoa pigo kwa Uislamu na kwa umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Maadui wanajua vyema kwamba, kama Waislamu watakuwa na nguvu, na iwapo sauti yao itakuwa kubwa na ya wazi, basi maadui hao hawataweza tena kuyadhulumu mataifa mengine na suala la Palestina nalo ambalo maana yake ni kughusubiwa nchi ya Kiislamu, halitasahauliwa tena.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, siri ya kuweza kuzishinda njama na makri hizo za maadui ni kushikamana na Qur'ani na kuwa na misingi mikuu ya kuufanya umma wa Kiislamu uwe na nguvu na kuongeza kwamba: Nguvu za kweli za Waislamu zimo katika imani na istiqama na kusimama kidete na vile vile kumkufuru taghuti.
Ayatullah Udhma Khamenei ameelezea kusikitishwa kwake na namna baadhi ya nchi za Kiislamu zinavyoshikamana na taghuti badala ya kushikamana na Mwenyezi Mungu na kusisitiza kwamba: Nchi ambazo katika eneo hili ni waendeshaji wa siasa za Marekani, kwa hakika zinausaliti umma wa Kiislamu na zinaanda uwanja wa kujipenyeza Marekani katika safu za Waislamu.
Amesema, imani, istiqama na kusimama kidete taifa la Iran na kutotetereka katika kukabiliana na siasa za Marekani za kupenda kujikumbizia kila kitu upande wake, ndiyo sababu kuu ya uimara na nguvu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesisitiza kwamba: Sababu inayoyafanya madola ya kibeberu yaliogope taifa la Iran na jambo linaloyafanya madola hayo kufanya njama za kila aina dhidi ya taifa hili, ni kuwa kwake imara na kushikamana vilivyo na msingi wa Uislamu na ni wazi kuwa adui anauogopa Uislamu wenye nguvu na Uislamu wa kishujaa.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, misimamo na miamala ya nia safi na yenye uaminifu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo sababu kuu inayoifanya Iran kuwa na taathira nzuri katika nyoyo za Waislamu na hiyo ni sababu nyingine ya nguvu na kuwa imara mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesisitiza kuwa: Hadi hivi sasa ahadi zilizotolewa na madhaghuti zimeshindwa kulidaganya taifa la Iran na wala makeke na vishindo vyao havijaweza kulitia woga taifa hili.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, moja ya mahitaji muhimu na ya dharura kabisa katika ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa ni kuwa macho na kutokubali kudanganywa na hila na makri za madola ya kibeberu kupitia ahadi zao za kihadaa na vile vile kutoogopeshwa na vishindo na makeke ya madola hayo ya kiistikbari. Ameongeza kuwa: Jukumu kubwa zaidi la Waislamu wote leo hii hususan maulamaa, wasomi na watu wenye muono mpana katika nchi za Kiislamu, ni kuendesha mapambano kwa ajili ya kuwaamsha Waislamu na kubainisha kijihadi mambo ya uhakika yanayohusiana na ulimwengu wa Kiislamu.
Aidha amelitaja suala la kuzuka magenge ya kigaidi na kitakfiri katika eneo la Mashariki ya Kati na kuanzishwa vita na mizozo kati ya Waislamu kwa niaba ya maadui, kuwa ni matokeo ya upotofu na kukosa mwamko na muono wa mbali baadhi ya Waislamu na kuongeza kuwa: Inabidi mahafali za Qur'ani Tukufu zitumike vizuri sana katika kuwaamsha watu na kwa wale watu ambao wanashiriki katika mahafali kama hizo kutoka nchi mbali mbali duniani, wanapaswa warejee makwao wakiwa na ujumbe wa kuwaongoza na kuwaamsha watu wao kuhusu uhakika wa mambo katika ulimengu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, msaada na nusra ya Mwenyezi Mungu inategemea harakati ya mataifa ya Kiislamu na harakati hiyo inapatikana kupitia ubainishaji wa kijihadi wa mambo. Amesema: Hapana shaka hata kidogo kuwa, kambi ya ukafiri hatimaye itashindwa tu na kambi ya Kiislamu ya mapambano na jihadi.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammadi, mwakilishi wa Fakihi Mtawala (Waliyyul Faqih) na Mkuu wa Taasisi ya Wakfu na Mambo ya Kheri alitoa hotuba fupi na kusema kuwa, kaulimbiu ya Mashindano ya 33 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya mjini Tehran ilikuwa ni: "Kitabu Kimoja, Umma Mmoja" na kuongeza kuwa: Katika mashindano ya mwaka huu, washiriki 130 katika fani za hifdhi na qiraa kutoka nchi 70 walishiriki kwenye mashindano hayo ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu.
Vile vile amewakumbuka kwa kheri mashahidi ya maafa ya Mina hususan mashahidi wa fani za Qur'ani Tukufu na kusema kuwa: Kushiriki wasomaji wa Qur'ani wenye nyoyo safi kutoka nchi tofauti tena kwa mara ya kwanza, kuenziwa familia za mashahidi wa Qur'ani na mashahidi wa kulinda Haram, kuwasilishwa makala na uchunguzi mbali mbali wa Qur'ani na kufanyika maonyesho na mahafali ya Qur'ani ni miongoni mwa kazi zilizofanyika wakati wa Mashindano ya 33 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yaliyomalizika siku ya Jumanne, Mei 17, 2016, mjini Tehran.L