Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Waziri Mkuu wa India
23/05/2016
Indian Prime Minister met with Ayatollah KhameneiAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo jioni, (Jumatatu) ameonana na Waziri Mkuu wa India, Bw. Narendra Modi na huku akigusia uhusiano wa muda mrefu, wa kihistoria na mawasiliano ya kiutamaduni na kiuchumi baina ya watu wa Iran na watu wa India amesema kuwa, nchi hizi mbili zina fursa nyingi sana za kustawisha ushirikiano wao katika nyuga nyingi tofauti. Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha jitihada zozote za kupanua wigo wa ushirikiano kati yake na India ambayo ni moja ya nchi yenye nguvu za uchumi zinazodhihiri hivi sasa na inazidi kupiga hatua za kimaendeleo. Amesema, Tehran inalipa uzito wa hali ya juu suala la kutekelezwa kikamilifu maafikiano yote ya pande mbili bila ya kuathiriwa na siasa za dola lolote lile.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia mustakbali mzuri wa uchumi wa India na vile vile akiba kubwa ya mafuta ya gesi ya Iran ambapo mambo hayo yanapokusanywa pamoja yanaifanya Iran kuwanchi tajiri zaidi yenye maliasili hizo na kumwambia Waziri Mkuu wa India kwamba: Kama ulivyoashiria wewe, mbali na mafuta na gesi, eneo la Chabahar ni moja ya nukta muhimu za mawasiliano baina ya Mashariki na Magharibi na baina ya Kaskazini na Kusini mwa dunia na linaweza kuwa eneo zuri la ushirikiano mkubwa, wa muda mrefu na wenye faida nyingi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia siasa sahihi za serikali ya India za kutojiingiza katika muungano wowote ule wa Magharibi na wa Marekani katika kile kinachodaiwa kuwa ni vita dhidi ya ugaidi na kusema kuwa: Mapambano ya kweli na ya uhakika dhidi ya ugaidi, yanaweza kuwa uwanja mwingine wa ushirikiano baina ya Iran na India kwani baadhi ya nchi za Magharibi hazilipi uzito suala la kupambana na ugaidi bali hata zinahusika katika kuundika na kuzuka magenge ya kigaidi nchini Afghanistan na vile vile makundi ya kigaidi katika nchi za Iraq na Syria.
Aidha amesisitiza kuwa, suala la kupambana na ugaidi ambao kwa bahati mbaya unafanyika kwa jina la Uislamu, inabidi waachiwe Waislamu na nchi za Kiislamu na kuongeza kwamba: Tab'an katika vita hivyo inabidi zishirikishwe zile nchi za Kiislamu ambazo si vibaraka wa siasa za Marekani na Magharibi kwani nchi hizo zinazofuata siasa za Marekani na Magharibi, hazina nia ya kweli ya kupambana na magaidi.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalipa uzito wa hali ya juu suala la kupambana na ugaidi na inatumia suhula na uwezo wake wote katika kupambana nao.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia namna baadhi ya magenge na makundi ya kigaidi yanavyotumia vibaya matatizo na udhaifu uliopo katika jamii ya Waislamu kwenye baadhi ya nchi kwa ajili ya kuwashawishi watu kujiunga na magenge hayo na kusisitiza kuwa: Tawala za nchi hizo zinapaswa kuwapokonya magaidi visingizio kama hivyo.
Amesema, ugaidi ni maradhi hatari sana ya kuambukiza na kusisitiza kwamba: Kama ambavyo uko uwezekano wa kuyazidi nguvu maradhi ya kuambukiza, ni vivyo hivyo, upo uwezekano pia wa kupambana na kuushinda nguvu ugaidi.
Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Waziri Mkuu wa India ameashiria safari ya Ayatullah Udhma Khamenei nchini India mwaka 1359 (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia sawa na 1980 Milaadia) na kusema kuwa, ziara hiyo ya Kiongozi Muadhamu nchini India iliandaa uwanja wa kuimarishwa vizuri uhusiano wa nchi hizi mbili. Amesema, katika ziara yake ya hivi sasa ya nchini Iran, kumefikiwa makubaliano mazuri na kumechukuliwa maamuzi makuaa ambayo tuna yakini kuwa, kwa nia ya kweli ya pande mbili, yataweza kuzaa matunda mazuri.
Bw. Narendra Modi ameyaunga mkono matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na hatari ya ugaidi na ulazima wa kupambana nao vikali na kuongeza kuwa: Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa baadhi ya nchi zinaugawa ugaidi kati ya ugaidi mzuri na ugaidi mbaya na hazichukui hatua za maana katika kupambana nao ghairi ya kutamka kwa maneno tu.
Waziri Mkuu wa India amesisitiza kuwa, Uislamu ni dini ya mapenzi na mahaba na haina uhusiano wowote na ugaidi na kuongeza kuwa: Siku kadhaa zilizopita, India ilitoa pendekezo la kufanyika mkutano wa kimataifa wa kupambana na ugaidi kwa kushirikishwa vilivyo nchi za Kiislamu lakini pendekezo hilo lilipingwa na baadhi ya nchi za Magharibi.
Ameongeza kuwa: Inabidi nchi ambazo zina nia ya kweli ya kupambana na ugaidi zishirikiane na zifanye kazi kwa pamoja na kwa karibu katika suala hilo.