Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Rais wa Afghanistan
23/05/2016
Photos: Indian Prime Minister met with Ayatollah KhameneiAyatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo jioni (Jumatatu) ameonana na Rais Mohammad Ashraf Ghani wa Afghanistan na huku akiashiria mambo mengi ya pamoja ya kiitikadi, kiutamaduni na kihistoria baina ya watu wa Iran na watu wa Afghanistan na namna nchi hizi mbili zilivyo na mipaka mirefu ya pamoja amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikilipa umuhimu mkubwa suala la maslahi na usalama wa Afghanistan na inaendelea kufanya hivyo hadi leo hii na itaendelea na msimamo wake huo katika mustakbali kwani inaamini kuwa, maendeleo ya nchi hiyo katika nyuga zote ni sawa na maendeleo yake yenyewe.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, watu wa Afghanistan ni watu mashujaa, wenye ghera na werevu na kuongeza kuwa: Afghanistan ina neema mbili kuu za utajiri wa maliasili na utajiri wa watu ambapo kama neema na utajiri huo utatumiwa vizuri unaweza kuiletea maendeleo mazuri nchi hiyo.
Aidha amegusia mapokezi mazuri ya watu wa Iran kwa ndugu zao wa Afghanistan katika miaka ya vita nchini mwao na hata baada ya miaka hiyo ya vita na kukumbusha kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tofauti na zinavyofanya baadhi yza nchi kama vile Marekani na Uingereza, daima imekuwa ikiwaangalia watu wa Afghanistan kwa jicho la heshima, udugu na wageni wake wapenzi na haitosita kutoa msaada wowote wa kiufundi, kiuhandisi na ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kuiwezesha Afghanistan kustafidi vizuri na maliasili zake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesisitizia ulazima wa kutatuliwa haraka iwezekanavyo suala la maji na mito iliyoko katika mpaka wa nchi hizi mbili na kuongeza kuwa: Mambo kama hayo hayapaswi kuleta manung'uniko na utesi katika uhusiano wa nchi mbili kama Iran na Afghanistan ambazo zina mpaka, utamaduni na mahitaji ya pamoja na yanayofanana.
Katika mazungumzo hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Mohammad Ashraf Ghani wa Afghanistan ameelezea kufurahishwa kwake na ziara yake ya mjini Tehran na maafikiano yaliyofikiwa kuhusu uhusiana wa kupitisha bidhaa kati yake na India kupitia bandari ya Chabahar ya nchini Iran na kusema kuwa: Sisi daima tutaendelea kuwashukuru watu wa Iran kwa kutupokea vizuri na amemwambia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba: Tunakushukuru sana kwa mtazamo wako chanya na mzuri kuhusiana na Afghanistan na ni matumaini yetu kuwa mazungumzo ya Tehran yataandaa uwanja wa kustawishwa uhusiano wa nchi hizi mbili kadiri inavyowezekana.
Bw. Ashraf Ghani vile vile amesema: Katika kipindi cha wiki chache zijazo, kutafanyika kikao cha wataalamu kuhusiana na namna nchi hizi mbili zinavyoweza kutumia kwa pamoja mito iliyoko katika mpaka wao wa pamoja na ni matumaini yetu kuwa suala hilo litafanyika kwa sura nzuri na inayofaa kabisa.