Kiongozi Muadhamu Aonana na Mkuu na Wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu
26/05/2016
The head and the members of the Assembley of Experts met with the Leader of the Revolution Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Alkhamisi) ameonana na mkuu na wajumbe waliochaguliwa na wananchi wa Baraza la Tano na Wanavyuoni Wataalamu linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema kuwa, kwa hakika baraza hilo ni kitu adhimu; na huku akibainisha utambulisho na njia ya kimapinduzi ya baraza hilo amesisitiza kuwa: Njia pekee ya kuendelea kuwepo na kupiga hatua za kimaendeleo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kufanikishwa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu, ni "nchi kuwa na nguvu za kweli" pamoja na kuweko "Jihadi Kubwa" yaani kutomfuata adui.
Ameitumia fursa hiyo kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa taufiki wananchi wa Iran ya kuchagua watu wazuri na kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi na pamoja na taufiki kuzinduliwa baraza hilo lenye heshima na uzito mkubwa na kusema kuwa: Baraza la Wanavyuoni Wataalamu ni atia ya Mwenyezi Mungu na hata tukiweka pembeni majukumu yake yaliyoainishwa na katiba, baraza hilo binafsi yake ni kitu adhimu na chenye taathira kubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, kukusanyika pamoja majimui ya maulamaa na wanafikra wa kidini na kielimu kwa kuchaguliwa na wananchi, lenyewe jambo hilo lina umuhimu mkubwa na kuongeza kuwa: Majmui hiyo adhimu na tukufu ina uwezo mkubwa wa kubadilishana mawazo na nadharia, kufanya mambo kwa mashauriano na uratibu mzuri na kufanya kazi zenye taathira kubwa.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia uhusiano uliopo baina ya maulamaa na watu wenye heshima na nafasi muhimu katika jamii yaani wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu kwa upande mmoja na matabaka mbali mbali ya wananchi katika kona zote za Iran kwa upande wa pili pamoja na nguvu za ushawishi wa maulamaa hao kwa watu na kuongeza kuwa: Majimui hiyo haipaswi kusubiri kufika wakati wa kutekeleza majukumu yake yaliyoainishwa na katiba ndipo ifanye kazi, bali inatakiwa kuwa katika harakati muda wote.
Vile vile ameyataja masuala kama ya kuwa na fikra moja katika mambo tofauti, kujikita na kuzingatia masuala yaliyokusudiwa, kutangaza misimamamo na matakwa yake na kuunda aina fulani ya mjadala na matakwa ya umma kwamba ni miongoni mwa majukumu makubwa ya Baraza la Wanavyuoni Wataalamu. Ameongeza kuwa: Iwapo lengo hilo litafikiwa, mihimili mingine tofauti pamoja na viongozi na watekelezaji wa sheria nchini nao bila ya shaka yoyote watafanya juhudi za kufanikisha ipasavyo matakwa hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, njia na malengo ya Baraza la Wanavyuoni Wataalamu inabidi iwe njia na malengo yale yale ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: "Utawala wa Kiislamu," "uhuru," "kujitawala," "uadilifu wa kijamii," "ustawi wa jamii," "kung'oa mizizi ya umaskini na ujinga," "kusimama imara kukabiliana na wimbi la vishawishi vya ufisadi wa kimaadili, kiuchumi, kijamii na kisiasa" lililoenea katika nchi za Magharibi na "kusimama imara kukabiliana na ubeberu wa kambi ya kiistikbari," ni miongoni mwa malengo makuu ya Mapinduzi ya Kiislamu na ya taifa la Iran.
Amesema, ubeberu ndiyo dhati na maumbile ya uistikbari na kuongeza kuwa: Kambi ya kiistikbari dhati yake ni kupenda kupanua wigo wa ubeberu wake kwa mataifa ya dunia na kama nchi na taifa lolote halitosimama imara kukabiliana na ubeberu huo, bila ya shaka yoyote litaingia kwenye mtego wa kuwa mateka wa uistikbari.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, bila ya shaka yoyote Uislamu ndiye mpambanaji wa kweli na ndiyo dini itakayong'oa mizizi yote ya dhulma na uistikbari na kuongeza kwamba: Tab'an Uislamu ambao una uwezo wa kupambana na mabeberu wa dunia na kusimama imara kukabiliana na kambi ya kiistikbari ni ule Uislamu ambao umekuwa imara kwa kuunda mfumo madhubuti wa utawala na wenye zana na nguvu za kijeshi, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni pamoja na nguvu za vyombo vya habari.
Vile vile amesema, kuyalinda Mapinduzi ni kazi ngumu zake kuliko hata kufanya Mapinduzi hayo na huku akitoa ufafanuzi kuhusiana na namna ya kukabiliana kwa njia sahihi na kambi ya madhalimu wa dunia amesema: Maadui wa taifa la Iran, awali walikuja na ajenda ya kufanya mashambulizi makali dhidi ya taifa hili; waliitumbukiza Iran kwenye vita vya miaka minane, wakaanzisha uasi wa kila namna mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamundani ya Iran, wakayaunga mkono magenge ya kigaidi, wakashambulia maeneo ya mafuta ya Iran na wakatungua ndege ya abiria ya Iran; na hiyo ni mifano tu ya mashambulio yao hayo lakini kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na kwa kujiweka chini ya kivuli cha haiba ya mja mcha Mungu aliyokuwa nayo Imam Khomeini (quddisa sirruh) pamoja na subira na muqawama wa wananchi wa Iran, maadui walishindwa katika njama zao zote hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, mashambulizi laini ni hatua nyingine ya hujuma zisizosita za mabeberu wa dunia dhidi ya taifa la Iran na kukumbusha kuwa: Vikwazo vya mtawalia vya kiuchumi, mashambulizi ya kila sekunde ya kisiasa, propaganda za kupotosha na kuchochea watu na kumshambulia kila anayefuata fikra za Mapinduzi ya Kiislamu katika nchi nyingine, ni mbinu nyingine zinazotumiwa na maadui katika hatua ya pili ya hujuma zao, lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na kwa kusimama imara taifa na viongozi wa Iran, maadui wameshindwa kufikia malengo yao katika njama zao hizo za kiuadui.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja hatua ya tatu ya hujuma za maadui kuwa ni kujipenyeza na amesema, hiyo ndiyo mbinu hatari zaidi na ni muondelezo wa vile vile vita laini dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesisitiza kuwa, ubeberu unatumia mbinu ya kujipenyeza ili kufanikisha malengo yake kadhaa ambayo ni pamoja na kuziathiri taasisi za uchukuaji na utengenezaji maamuzi za Iran, kubadilisha imani na itikadi za wananchi wa Iran na pia kuvuruga mahesabu na misimamo ya viongozi wa Iran.
Amesema, maadui wanatekeleza njama zao hizo kupitia kushambulia misingi na nguzo kuu za Mapinduzi ya Kiislamu kama vile Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, Baraza la Kulinda Katiba, vijana walioshikamana barabara na dini na wanavyuoni wanamapinduzi. Amesisitiza kuwa: Lengo kuu la maadui katika awamu hii ya vita vyao laini ni kuandaa uwanja wa kuubana mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuufanya ushindwe kutumia vizuri taasisi zake muhimu zinazoufanya mfumo huo uwe na nguvu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kama lengo hilo litafikiwa na Jamhuri ya Kiislamu ikashindwa kutumia vyombo vyake vinavyoipa nguvu, haitakuwa kazi nzito kuumaliza na kuungamiza mfumo huo utawala wa Kiislamu au kuleta mabadiliko makubwa katika harakati yake na ni kwa sababu hiyo ndio maana tunasisitiza mno kuwa, kutomfuata adui na kusimama imara kukabiliana na matakwa yake ni "Jihadi Kubwa."
Baada ya kubainisha njia zinazopaswa kupitia harakati ya kimapinduzi ya Baraza la Wanavyuoni Wataalamu, Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Ubunifu unaoheshimu misingi ya dini na kwa kutumia watu wenye elimu na wenye uwezo na nguvu za kutoa fatwa na uwezo wa kutibu majeraha yanayoingizwa na adui kwa njia mbali mbali kama vile kuzusha mifarakano ya kimadhehebu na kitaifa, hitilafu za kimirengo na kuzusha kambi mbili bandia ndani ya Iran, ni miongoni mwa majukumu muhimu ya Baraza la Wanavyuoni Wataalamu.
Aidha amewaambia wagombea waliochaguliwa na wananchi kuwa wajumbe katika Baraza la Tano la Wanavyuoni Wataalamu kwamba haijuzu kukwama sehemu yoyote; bali zingatieni vizuri asili ya mabadiliko na maendeleo kwa ajili ya kufanikisha malengo ya Uislamu na ya Mapinduzi na upeni uzito wa hali ya juu ufuatiliaji wa karibu wa jambo hilo.
Sehemu ya mwisho ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imehusiana na ufafanuzi kuhusu majukumu jumla ya viongozi nchini Iran katika kipindi na muda huu uliopo hivi sasa.
Amesema, kuhakikisha kwamba Iran inakuwa na nguvu za kweli ndiyo njia pekee ya kuweza kubakia, kupiga hatua na kufanikishwa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na ya taifa na kuongeza kwamba: Taasisi na viongozi wote nchini wana majukumu mazito katika njia hiyo na kila mmoja ana wajibu wa kutekeleza vizuri majukumu yake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kuwa na nguvu Iran kutaifanya nchi hii iweze kupata inalotaka hata kutoka kwa madola makuu ya kibeberu duniani na kuongeza kuwa: Kama hali haitakuwa hivyo, basi hata tawala dhaifu na hakiri zitataka kulifanyia jeuri na zitapata uthubutu wa kujaribu kulichezea taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi kuhusu mfano mmoja wa kupata Iran ilichokitaka kutoka kwa adui chini ya kivuli cha nguvu za taifa kwa kusema: Marafiki zetu azizi wanasema kuwa, katika mazungumzo ya nyuklia tumefanikiwa kupata tulichokitaka na kwamba pande zilizokuwa zinafanya mazungumzo nasi zimelazimika kutambua rasmi haki ya Iran ya kuwa na teknolojia ya nyuklia; tab'an jambo hilo limewezekana baada ya kubainika wazi nguvu za Iran. Yaani taifa la Iran lilionesha nguvu zake za kielimu na uwezo wake katika uga huo kupitia kujizalishia asilimia 20 ya urani iliyorutubishwa kwani kila mtu anajua kwamba, kuwa na uwezo wa kurutubisha urani kwa asilimia 20 ndiyo hatua ngumu zaidi katika mchakato mzima wa urutubishaji urani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, uwezo wa Iran wa kuzalisha mashinepewa 19 elfu za kizazi cha kwanza, uwezo wake wa kutumia maelfu ya mashinepewa (kwa wakati mmoja kwa ajili ya kurutubisha urani), uwezo wake wa kuzalishaji kizazi cha pili, cha tatu na cha nne cha mashinepewa hizo na kuweza kujijengea kiwanda cha kuzalisha maji mazito (ya nyuklia) ni mifano mingine ya uwezo wa kinyuklia wa Iran. Amesema, kuna wakati adui alikuwa hayuko tayari kusikia kuna hata mashinepewa moja tu nchini Iran, lakini alipokumbana na nguvu na uwezo huo mkubwa wa nyuklia wa Iran, amelazimika kusalimu amri na kukubali. Kwa kweli haya yote hayakupatikana kwa hiari ya Wamarekani, bali tumeyachukua kutokana na nguvu na uwezo wetu wa nyuklia.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Inshaallah kwa kubainika matunda ya uchumi wa kimuqawama na nguvu za kiuchumi za Iran, adui ataelewa kuwa vikwazo vyake dhidi yetu havina maana.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, miongoni mwa uwezo wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu ni kutaka maelezo ya kina na kufuatilia ufanikishaji wa vielelezo vya ndani ya nchi vya uwezo wa taifa kutoka kwa viongozi na kwa taasisi mbali mbali na kuongeza kuwa: Majimui ya maulamaa hao wakubwa inaweza kuwa na taathira nzuri katika njia hiyo.
Aidha Ayatullah Udhma Khamenei amesema, taqwa, ushujaa, busuri na kuwa na muono wa mbali, kuchukua misimamo ya wazi na kwa wakati unaotakiwa, kutoogopeshwa na lawama za watu na kuwa na welewa sahihi na wa kina kuhusu kambi ya adui na mbinu zake ni miongoni mwa vielelezo vikuu vya kuwa mwanamapinduzi.
Amesisitiza kuwa: Kuna baadhi ya wakati adui anafanya mambo ambayo kidhahiri yanaonekana ni mazuri lakini kumbe ana malengo yake maalumu nyuma ya pazia na kuna baadhi ya wakati wanaweza kutokezea watu ndani ya Iran wakaipokea vizuri hatua hiyo ya adui, lakini lau kama tungelikuwa tumejiwekea misingi mizuri tangu zamani ya kutambua malengo hasa ya adui, kamwe hatuwezi kudanganywa na hatua zake kama hizo.
Nasaha nyingine za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu waliochaguliwa na wananchi, zilikuwa ni kujiamini na kuhakikisha roho zao hazikati tamaa.
Amewaambia wajumbe hao kwa kusisitiza kwamba: Tahadharini na woga na kukata tamaa ndani ya nyoyo zenu, kwani kama hilo litatokea, mtashindwa pia katika medani ya utekelezaji wa kivitendo vya maamuzi yenu.
Aidha mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakaribisha wajumbe wapya wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu hususan wanavyuoni vijana wenye ijtihadi na wenye harakati nyingi na vile vile amewakumbuka kwa wema wajumbe wa huko nyuma wa baraza hilo waliotangulia mbele ya Haki hususan Marhum Ayatullah Vaez Tabasi, na kuwaombea maghufira mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Jannati, Mkuu wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu amemshukuru Kiongozi Muadhamu kwa ujumbe wake wenye kutoa ilhamu alioutoa kwa mnasaba wa kuzinduliwa duru ya tano ya baraza hilo na kusema kuwa anga ya vikao vya baraza hilo ilijaa utulivu na nidhamu na vile vile amegusia nafasi muhimu sana ya Baraza la Wanavyuoni Wataalamu katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema kuwa, baraza hilo lina heshima kubwa mbele ya wananchi.
Mkuu wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu aidha amesema: Tuna wajibu wa kutekeleza vilivyo majukumu yetu katika nafasi zozote tunazokuwepo na ni kwa njia hiyo ndipo tutaweza kupata radhi za Mwenyezi Mungu na imani ya watu. Vile vile ametoa ahadi kwa kusema: Tutafuatilia msimamo wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kila nukta na kipengee.
Naye Ayatullah Hashemi Shahroudi, Naibu wa Pili wa Mkuu wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu amepata fursa ya kuzungumza na kwa upande wake ametoa ripoti fupi na huku akigusia mambo mazuri yaliyojadiliwa katika kikao kilichomalizika jana (Jumatano) cha baraza hilo amesema: Ulazima wa kuwa mwanamapinduzi na kutenda kiuanamapinduzi, sisitizo la kushiriki taasisi zote nchini katika kutekeleza vilivyo miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na udharura wa watu wote hususan viongozi nchini Iran kujiepusha kikamilifu kutamka maneno ambayo yanaweza kupandikiza katika jamii; fikra ya kuweko kambi mbili nchini ni miongoni mwa mambo muhimu yaliyojadiliwa na wajumbe wa baraza hilo katika kikao hicho.
Ayatullah Hashemi Shahroudi ameongeza kuwa: Wajumbe wa Baraza la Wanachuoni Wataalamu wameelezea wasiwasi na daghadagha yao kubwa kuhusiana na matatizo yaliyopo nchini kama vile mapungufu ya kiutamaduni, matatizo ya kimaisha na kiuchumi, suala la kazi na ajira kwa vijana, uzorotaji wa kiuchumi, magendo ya bidhaa, kutofanikishwa siasa za uchumi wa kimuqawama, kutotekelezwa kivitendo fikra ya Benki ya Kiislamu, kuzuka fikra potofu na misimamo mikali, madhara yatokanayo na Intaneti na mawasiliano ya kompyuta pamoja na matatizo mbali mbali yaliyoko katika mikoa ya mipakani; na wametaka hatua za lazima zichukuliwe kukabiliana vilivyo na matatizo hayo.